Alhamisi, 5 Agosti 2021

Fanya ile taa iwake Daima!


Mambo ya walawi 24:2-4Waagize wana wa Israeli kwamba wakuletee mafuta ya zeituni safi ya kupondwa kwa ajili ya ile nuru, ili hiyo taa iwake daima. Hapo nje ya pazia la ushahidi, ndani ya hema ya kukutania, Haruni ataitengeza tangu jioni hata asubuhi mbele za BWANA daima; ni amri ya milele katika vizazi vyenu.  Atazitengeza hizo taa katika kile kinara kilicho safi mbele za BWANA daima.”

Kutoka 27:20-21Nawe waamuru wana wa Israeli wakuletee mafuta ya zeituni safi ya kupondwa kwa ajili ya nuru, ili kufanya ile taa kuwaka daima. Ndani ya ile hema ya kukutania, nje ya hilo pazia, lililo mbele ya huo ushuhuda, Haruni na wanawe wataitengeza tangu jioni hata asubuhi mbele ya BWANA; itakuwa ni amri ya milele katika vizazi vyao vyote kwa ajili ya wana wa Israeli.”

 


Utangulizi:

Moja ya fanicha muhimu sana ambazo ziliwekwa katika Hema ya kukutania na baadaye katika hekalu lililokuwako Yerusalem, ni pamoja na taa ya dhahabu yenye vinara saba,taa hii ilitengenezwa wakati wa Torati kwa maelekezo ya Mungu mwenyewe kwa mtumishi wake Musa huko jangwani, Taa hii ambayo ilipaswa kuwaka kwa kutumia mafuta ya zeituni ilipaswa kuwaka daima, Waebrania wanaiita taa hii yenye vinara saba Menorah, Ni moja ya alama muhimu sana kwa watu wote wanaoamini maandiko lakini ni ya muhimu zaidi kwa wayahudi na wakristo, Taa hii imekuwa ni alama muhimu ya Kiyahudi na ndio nembo ya taifa la Israel kwa sasa.

Hema ya kukutania pamoja na hekalu lililokuwako Yerusalem ilikuwa ni ishara ya mpango wa Mungu kukaa katikati ya wanadamu na kushirikiana nao, Hema ile ya kukutania pamoja na Hekalu lilikuwa limegawanyika katika maeneo makuu matatu:-

1.       Ua wa nje ambao ulikuwa umetengenezwa kwa Mapazia maalumu na kulikuwa na Madhababu ya shaba kwa sadaka za kuteketezwa na Bakuli la shaba la kutawadhia, ua wa nje ulikuwa ni maalumu kwa watu kufika na kufanya ibada na kutoa kafara za wanyama kwa mujibu wa maelekezo ya Torati. Nuru iliyoangaza mahali hapa ilikuwa nuru ya asili ya mwanga wa jua tu.

 

2.       Mahali patakatifu, kutoka uwa wa nje mtu angeingia ndani ambapo pamefunikwa na mapazia maalumu, mahali hapa waliingia makuhani tu, hapa palikuwa na Meza ya mikate ya wonyesho, Madhabahu ya dhahabu ya kufukizia uvumba na taa ya dhahabu yenye vinara saba, ni makuhani tu walioruhusiwa kuingia hapa tena wakiwa wamejitakasa kwa maelekezo maalumu, Nuru iliyotakiwa kuangaza mahali hapa ilikuwa ni ile taa yenye vinara saba.

 

 

3.       Patakatifu pa patakatifu, hapa ni chumba cha ndani zaidi, ni eneo ambalo lilikuwa limetengana na patakatifu, palitengwa na pazia maalumu, ndani yake kulikuwa na lile sanduku la agano lililotengenezwa kwa dhahabu na Makerubi waliofunikia kiti cha rehema kwa mbawa zao Nuru iliyoangaza mahali hapa ilikuwa ni nguzo ya wingu la utukufu wa Mungu mwenyewe

Ile taa

Kwa mujibu wa maelekezo ya Mungu kupitia mtumishi wake Musa, waliagizwa watu watengeneze mafuta ya mzeituni na kisha wayapeleke hekaluni kwaajili ya taa hii ya dhahabu yenye vinara saba na kwamba wahakikishe kuwa taa hii inawaka daima, ingawa ni kuhani tu aliyepaswa kuingia hemani, na kuhakikisha kuwa taa inawaka lakini kumbuka watu walishiriki kwa kuchangia mafuta kwa msingi huo kila mtu alishiriki. Walawi 24:1-4 “Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia, Waagize wana wa Israeli kwamba wakuletee mafuta ya zeituni safi ya kupondwa kwa ajili ya ile nuru, ili hiyo taa iwake daima. Hapo nje ya pazia la ushahidi, ndani ya hema ya kukutania, Haruni ataitengeza tangu jioni hata asubuhi mbele za BWANA daima; ni amri ya milele katika vizazi vyenu.  Atazitengeza hizo taa katika kile kinara kilicho safi mbele za BWANA daima.”

Umuhimu mkubwa sana wa ile taa yenye vinara saba ni kutoa huduma, yenye kusababisha makuhani waweze kufanya wajibu wao wa kufanya mamombi kwaajili ya watu na kuwapatanisha na Mungu, kumbuka eneo hili lilikuwa limefunikwa kwa mapazia mazito ya ngozi, na kwa sababu hiyo kwa vyovyote vile mahali hapo palikuwa pana giza, kwa hiyo ingekuwa ni vigumu kwa viongozi wa kiroho kuendelea kuutafuta usio wa Bwana kwaajili ya watu wake kama taa hii muhimu yenye vinara sana haingelikuwepo, kwa hiyo taa hii ilikuwa muhimu kwaajili ya kuwawezesha makuhani kufanya wajibu wao, na taa ingeweza kuwaangazia waone madhabahu ua dhahabu ya kufukizia uvumba ba maombi, na pia waweze kuiona meza ya mikate ya wonyesho na kuwawezesha hivyo makuhani kuwa na ushirika na Mungu na kuwaiombea watu wa Mungu kwa niaba yao!

Maana ya ile taa yenye vinara saba!

Ni muhimu kufahamu kuwa taa hii ya dhahabu yenye vinara saba imekuwa ikileta utata sana miongoni mwa wana theolojia kutokana na kuwa na mitazamo mbalimbali hasa inayosababishwa na uwepo wa vinara sana, kwa hiyo imeleta changamoto kwa wayahudi na wakristo katika kufikiri namna halisi ya kutafasiri taa hii, yako majibu na mitazamo mbalimbali kuhusiana na taa hii

·         Wengine hufikiri kuwa taa hii inazungumzia siku sita za uumbaji wa Mungu na siku ya saba ya mapumziko ya kisabato kwa taa ile ya kati kati ya saba

 

·         Wengine hufikiri kuwa labda taa hii inawakilisha wazo la Hekima na uahamu wote unaokusudiwa na Mungu kama utakavyokuwa juu ya masihi  Isaya 11:2-3 “Na roho ya Bwana atakaa juu yake, roho ya hekima na ufahamu, roho ya shauri na uweza, roho ya maarifa na ya kumcha Bwana;  na furaha yake itakuwa katika kumcha Bwana; wala hatahukumu kwa kuyafuata ayaonayo kwa macho yake, wala hataonya kwa kuyafuata ayasikiayo kwa masikio yake;”

 

·         Wengine hufikiria kuwa taa yenye vinara saba kwa wayahudi inahusishwa na kusheherekea sikukuu ya Hanukkah ambayo maana yake ni sikukuu ya Nuru kwa hivyo moja kwa moja wanachukua maana ya neno Menorah jina la ile taa ambalo maana yake kuangaza kwa hiyo ni kama taa hii ina ujumbe wa amka uangaze.

 

 

·         Wengine huzungumzia kuwa taa yenye vinara saba huwakilisha uwepo wa kuhani mkuu Yesu Kristo ambaye ndie asili ya nguvu ya kanisa hasa kutokana na maono ya kitabu cha ufunuo katika Ufunuo 1;12-13 “Nikageuka niione ile sauti iliyosema nami. Na nilipogeuka, niliona vinara vya taa saba vya dhahabu; na katikati ya vile vinara nikaona mtu mfano wa Mwanadamu, amevaa vazi lililofika miguuni, na kufungwa mshipi wa dhahabu matitini”.

 

·         Na wengine kutokana na asili hii ya kitabu cha ufunuo wannamuona Yesu ambaye ndie mmiliki wa kanisa katika nyakati zote hivyo wanahusisha na Historia ya Kanisa tangu ufunuo mpaka kurudi tena kwa Yesu kwa hiyo wao huzungumzia nyakati saba za kanisa ona yaani Makanisa yale saba katika kitabu cha ufunuo pia huwakilisha nyakati saba za kihistoria katika kanisa tangu wakati wa kanisal  la kwanza  siku ya pentekoste hata wakati wa kuja kwa Bwana, haya pia yanaweza kuwa makanisa au madhehebu ambayo yana mapungufu mbalimbali na baraka mbalimbali sambamba na hali ya yale makanisa saba, makanisa hayo pia yanawakilisha Roho za kinabii Ufunuo 19;10.

 

o   Apostolic Church 33-100 Kanisa la wakati wa Mitume kanisa lenye shughuli.

o   Persecuted Church 100-113 kanisa la Karne ya kwanza lililoteseka

o   Imperial Church 313- 476 Kanisa la kpindi cha lililopata ushindi na kanisa lililokosea

o   Medieval Church 476-1453 kanisa lililopoa kipindi cha giza kanisa lenye tatizo

o   Reformed Church 1453-1648 kanisa la kimapinduzi kanisa lililotazama nyuma

o   Morden church 1648-1970 kanisa la leo kanisa la kiinjilisti

o   Morden charismatic church 1970 mpaka leo. Kanisa lenye mafanikio

 

§  Fanya ile taa iwake Daima!

 

Tumeona kuwa kuna dhana tofauti tofauti kuhusiana na mafundisho yaliyoko katika taa yenye vinara saba vyovyote vile watu wanavyofikiri Mungu Roho Mtakatifu alinirudisha mimi kujiuliza kwanini Mungu akazie kuwa taa ile iwake fanya taa iwake daima hii maana yake ni kuwa kama taa ile ingezimika makuhani wasingeliweza kuona, wasingeliweza kufanya majukumu yao ya kila siku, wasingeliweza kupatanisha watu na Mungu kwani sehemu ya huduma ya upatanisho ingekuwa iko giza, Taanyenye vinara saba ninatufundishan kuhakikisha kuwa uhusiano wetu na Mungu unadumu kila siku na kuwa tunakuwa karibu naye kila siku, tyunapodumisha uhusiano wetu na Mungu tunapewa nafasi ya kuona na kufikiri na kutambua mambo kama Mungu anavyoona, kuna matokeo makubwa sana kwa kanisa kuhakikisha kuwa tunadumisha uhusiano na Mungu, kuhakikisha kuwa taa inawaka daima ni sawa na kuhakikisha kuwa hatuvunji uhusiano wetu na Mungu, sio makuhani tu watru wote wanapaswa kushiriki katika kuhakikisha kuwa wote kwa pamoja na kanisa kwa pamoja na Israel kwa pamoja wanadumisha uhusiano wao na Mungu, kukua kwetu kiroho na kuona Mungu akijishughuklisha na maisha yetu kutakuwa dhahiri endapo imani yetu na upendo wetu utaendelea kuwa pamoja na Yesu daima, Mungu hana mpango wa kutuacha yeye ameahidi kuwa atakuwa pamoja nasi ni sisi ndio twenye wajibu wa kubaki ndani yake lakini yeye ameahidi kuwa hatatuacha wala hatatutupa nje kamwe ona

Yoahana 6:37 “Wote anipao Baba watakuja kwangu; wala ye yote ajaye kwangu sitamtupa nje kamwe”.

Isaya 41:10 “usiogope, kwa maana mimi ni pamoja nawe; usifadhaike, kwa maana mimi ni Mungu wako; nitakutia nguvu, naam, nitakusaidia, naam, nitakushika kwa mkono wa kuume wa haki yangu.”

Mika 7:8 “Usifurahi juu yangu, Ee adui yangu; niangukapo, nitasimama tena; nikaapo gizani, Bwana atakuwa nuru kwangu.”           

Torati 31:6-8 “Iweni hodari na moyo wa ushujaa, msiogope wala msiwahofu; kwa maana Bwana, Mungu wako, yeye ndiye anayekwenda pamoja nawe, hatakupungukia wala kukuacha. Musa akamwita Yoshua, akamwambia machoni pa Israeli wote, Uwe hodari na moyo wa ushujaa, maana utakwenda pamoja na watu hawa hata nchi Bwana aliyowaapia baba zao, ya kwamba atawapa; nawe utawarithisha. Naye Bwana, yeye ndiye atakayekutangulia, atakuwa pamoja nawe, hatakupungukia wala kukuacha; usiogope wala usifadhaike.

Usalama wetu uko ndani ya kudumisha mahusiano yetu na Mungu, taa ile ilitakiwa kuwaka daima ili makuhani waendelee kutoa huduma za kiungu kwa watu, tunapodumisha uhusiano wetu na Mungu ndipo tunapokuwa salama na ndipo tunapoweza kusema kwa ujasirimkuwa Bwana ni Nuru yangu na wokovu wangu nimuogope nani

 

Zaburi 27:1-3 “   Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu, Nimwogope nani? Bwana ni ngome ya uzima wangu, Nimhofu nani? Watenda mabaya waliponikaribia, Wanile nyama yangu, Watesi wangu na adui zangu, Walijikwaa wakaanguka. Jeshi lijapojipanga kupigana nami, Moyo wangu hautaogopa. Vita vijaponitokea, Hata hapo nitatumaini.”

 

Mtu wa Mungu kama unataka kufanikiwa usiharibu wala usiruhusu uhusiano wako na Mungu ukavunjika unao wajibu wa kuleta mafuta na kuhakikisha kuwa taa ile haizimiki, fanya ile taa iwake daima Mungu alimuita Samuel na kusema naye wakati ambapo taa ile haijazimika 1Samuel 3:1-3 “Basi, mtoto Samweli akamtumikia Bwana mbele ya Eli. Na neno la Bwana lilikuwa adimu siku zile; hapakuwa na mafunuo dhahiri. Ikawa wakati huo, Eli alipokuwa amelala mahali pake (tena macho yake yalikuwa yameanza kupofuka, hata asiweze kuona), na taa ya Mungu ilikuwa haijazimika bado, na Samweli alikuwa amelala katika hekalu la Bwana, palipokuwa na sanduku la Mungu;   uhusiano wetu na Mungu, kujibiwa maombi, kuisikia sauti ya mungu, kukuia kwetu kiroho, kupata ufunuo mpya, maelekezo maono, nuru, kujua siri za Mungu, kuwa na karama na vipawa, ujuzi na taarifa za kiungu kutakuwa hai katika maisha yetu kama taa ya Mungu haijazimika ile taa tukiiacha ikazima tumekwisha ! twende kwa nani Bwana wewe unayo maneno ya uzima wa milele!

 

Na Rev. Innocent Samuel Kamote

 

Mkuu wa wajenzi mwenye hekima !

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni