Alhamisi, 19 Agosti 2021

Huyu mjane masikini ametia zaidi kuliko wote!

Marko 12:41-44Naye akaketi kulielekea sanduku la hazina, akatazama jinsi mkutano watiavyo mapesa katika sanduku. Matajiri wengi wakatia mengi. Akaja mwanamke mmoja, mjane, maskini, akatia senti mbili, kiasi cha nusu pesa. Akawaita wanafunzi wake, akawaambia, Amin, nawaambia, Huyu mjane maskini ametia zaidi kuliko wote wanaotia katika sanduku la hazina; maana hao wote walitia baadhi ya mali iliyowazidi; bali huyu katika umaskini wake ametia vyote alivyokuwa navyo, ndiyo riziki yake yote pia.”



Utangulizi:

Mara nyingi sana tumewahi kusikia neno kutoa ni moyo, katika semi zetu mbalimbali za Kiswahili, lakini je hivi tumewahi kujiuliza kwa undani maana ya msemo huo na sababu zake? Bila shaka msemo huu una uhusiano mkubwa sana na Mafundisho ya Bwana wetu Yesu Kristo kuhusu Kutoa, hususani kulikotokana na mama mjane kabisa aliyefika Hekaluni na kutoa sadaka katika hazina ya nyumba ya Mungu. Yesu alimsifika kuwa ndiye mtu aliyetoa zaidi kuliko wote katika ibada ile aliyoikusudia!

Kila mmoja wetu anapokuwa amejiandaa kwenda kuabudu na kumtolea Mungu anapaswa kuliweka somo hili moyoni mwake! Kwa sababu Mungu haangalii tu nini tunatoa lakini anaangalia ni kwa sababu gani tunaoa, Mungu hutazama moyo! Hebu tuone tena andiko la Msingi ili tuweze kujifunza kitu kutoka kwa mama huyu! Marko 12:41-44Naye akaketi kulielekea sanduku la hazina, akatazama jinsi mkutano watiavyo mapesa katika sanduku. Matajiri wengi wakatia mengi. Akaja mwanamke mmoja, mjane, maskini, akatia senti mbili, kiasi cha nusu pesa. Akawaita wanafunzi wake, akawaambia, Amin, nawaambia, Huyu mjane maskini ametia zaidi kuliko wote wanaotia katika sanduku la hazina;  maana hao wote walitia baadhi ya mali iliyowazidi; bali huyu katika umaskini wake ametia vyote alivyokuwa navyo, ndiyo riziki yake yote pia.” Tutajifunza somo hili Huyu Mjane masikini ametia zaidi kuliko wote kwa kuzingatia mambo ya msingi yafuatayo:-


·         Maana ya neno masikini:-

·         Huyu Mjane masikini ametia zaidi kuliko wote!

·         Utoaji wa sadaka kama mjane:-

 


Maana ya neno Masikini:-

Neno masikini lililotumika katika andiko hilo kwa lugha ya kiyunani linasomeka kama “PTOCHOS” ambalo linaweza kujumuisha maneno ya tafasiri ya kiingereza kama “Crouching,  and Cringing” sawa kabisa na watu wanaoombaomba na kuchakura majalalani, wakenya wana neno zuri linalokaribiana na hilo la “CHOKORAA” yaani masikini wa kutupwa au ombaomba, ni mtu asiye na kitu kabisa mtu anayeishi maisha ya kuomba omba, kwa maana nyingine wakati sisi wengine tunajidhania kuwa masikini kwa kujilinfanisha na wengine na kuona labda wametuzidi kitu Fulani na ndipo tunapoweza kujifikiri kuwa sisi ni masikini, huyu anayetajwa hapa alikuwa masikini kabisa asiye na lolote! Wala hata mtu wa kujilinganisha naye! Mwanamke huyu hakuwa na kitu lakini sio tu hakuwa na kitu pia tunaambiwa alikuwa mjane, amefiwa na mume wake! Ni Mtu wa namna hii asiye na kitu kabisa ndio Yesu anasema ametoa zaidi kuliko wote jambo hili lina maana gani na linatufundisha nini:-

Huyu Mjane masikini ametia zaidi kuliko wote!

Yesu anajua mioyo yetu na anayajua maisha yetu, lakini pia wakati wa matoleo katika ulimwengu war oho Yesu huketi kuelekea sanduku la hazina, maana yake anafuatilia mwenedno wa utoaji wetu kwake, anajua namna na jinsi na hisia zetu wakati wa kutoa  unaweza kuona wazi tabia yake hapa Marko 12:41 “Naye akaketi kulielekea sanduku la hazina, akatazama jinsi mkutano watiavyo mapesa katika sanduku. Matajiri wengi wakatia mengi.” Unaona imani yangu inaniambia kuwa tukio la Yesu kufuatilia utoaji wetu sio tu kuwa lilikuwa katika siku hii HAPANA kila inapofanyika ibada ni wazi kuwa Yesu yupo pamoja nasi katika ulimwengu wa kiroho na anafuatilia kila jambo linalotendeka na namna tunavyofanya katika ibada na uchunguiz wa mioyo yetu Neno la Mungu linasema hivi Mathayo 18:20 “Kwa kuwa walipo wawili watatu wamekusanyika kwa jina langu, nami nipo papo hapo katikati yao.” Unaona kumbe tunapokusanyika wakati wowote tuwe wawili ama zaidi kwaajili ya kumuabudu yeye mwenyewe anakuwepo katikati yetu na saa ya kutoa maana yake ni kuwa anakuwepo pamoja nasi na kufuatilia kila kitu, bila shaka sasa utakuwa umekubaliana nami. Kwa msingi huo Yesu aliwashuhudia wengi wakitoa na alifanya ufuatiliaji na anafanyi hizi hata sasa, na katika ufuatiliaji huu Yesu alibaini kwamba mwanamke Yule mjane na tena masikini wa kutupwa ALITOA KATIKA KILA KITU ALICHOKUWA NACHO ona Marko 12:44 “maana hao wote walitia baadhi ya mali iliyowazidi; bali huyu katika umaskini wake ametia vyote alivyokuwa navyo, ndiyo riziki yake yote pia.” Kumbuka kuwa neno la Mungu halimaanishi kuwa tutoe kila kitu tulichonacho, wala halimaanishi kuwa tusijiwekee akiba hapana Lakini utoaji wa mjane huyu masikini ulimshangaza zaidi Yesu kwa sababu ilikuwa ndio chakula chake yaani hana nyingine zaidi ya ile, lakini kwanini alitoa Mwanamke huyu alitoa kwa sababu aliamini kwamba Mungu atamtunza tu, hata kama ametioa kila alichikuwa nacho mungu atafanya njia kwa namna nyingine, aliamini kuwa kumpa Mungu hakutamfanya apungukiwe na kitu  Wafilipi 4:19 “Na Mungu wangu atawajazeni kila mnachokihitaji kwa kadiri ya utajiri wake, katika utukufu, ndani ya Kristo Yesu.” Hii ndio kanuni ya Mungu, tunapotoa huwa hatupungukiwi, Mungu hujaziliza kwa namna nyingine mimi na mke wangu huwa tunatabia ya kupunguza nguo zetu na kuzigawa kwa watu wengine, wakati mwingine huwa tunagawa nguo zote ambazo hazitutoshi au hata ambazo huwa hatuzivai mara nyingi tu, huwa tunahakikisha tunapunguza ili zibaki chache tu tunazotumia kwa maisha ya kila sku hapa na pale lakini baada ya miezi kadhaa unashangaa tena Nguo zimekuwa nyingi tena, Mungu wetu ni mchungaji mwema na hukakikisha kuwa kondoo zake hawapungukiwi na kitu Zaburi 23:1 “Bwana ndiye mchungaji wangu, Sitapungukiwa na kitu.” Awaye yote anayefanya kitu kwaajili ya Mungu na kwa imani katika Mungu hawezi kupungukiwa na kitu, mjane Yule alitoa kwa imani hii aliamini kuwa Mungu hatamuacha ateseke na njaa hata kidogo ona Zaburi 37:25 “Nalikuwa kijana nami sasa ni mzee, Lakini sijamwona mwenye haki ameachwa Wala mzao wake akiomba chakula.” Mjane huyu aliamini hivyo na liishi hayo katika maisha yake hakuwaza kujilimbikizia alimuamini Mungu kwa asilimia mia moja na alipoukunjua moyo wake katika hili Yesu alimuona na kumtumia kama somo kuu katika maisha ya wanafunzi wake, je ni kitu hani tunaweza kujifunza kutoka katika utoaji wa mjane huyu:-

Utoaji wa sadaka kama mjane:-

Kwa kuwa Bwana Yesu alimfanya mwanamke huyu kuwa kielelezo, ni wazi kuwa kuna maswala ya Muhimy ya kujifuza kutokana na utoaji wa mjane huyu masikini, liko jambo la kujifunza kutoka kwake

a.       Alijitoa yeye mwenyewe kwanza!

 

Utoaji wa mwanamke huyu mjane haukuwa rahisi, na hauwezi kuwa rahisi kama mtoaji huyu angekuwa na ubinafsi, ni wazi kuwa mtoaji huyu alitoa akiwa hana hata chembe ya ubinafsi nah ii maana yake yeye mwenyewe alikuwa tayari amejitoa amejidhabihu kwa Mungu Warumi 12:1 “Basi, ndugu zangu, nawasihi, kwa huruma zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza Mungu, ndiyo ibada yenu yenye maana.” Ni ukweli ulio wazi katika maandiko kuwa kabla hatujamtolea Mungu au hata kumpa mwanadamu sisi ndio sadaka ya kwanza, mwanamke huyu alikuwa ameuua umimi kabisa ukilinganisha na upendo wake kwa Mungu, yeye alikuwa anampenda Mungu kwa dhati, moyo wake na mauisha yake alikuwa ameyatoa kwa Bwana, mtu hawezi kufanya ibada ghali namna hii kama hajajichukia yeye mwenyewe kwanza Luka 9:23-24 “Akawaambia wote, Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake kila siku, anifuate. Kwa kuwa mtu atakaye kuiponya nafsi yake ataiangamiza, na mtu atakayeiangamiza nafsi yake kwa ajili yangu ndiye atakayeisalimisha.” Unaona huyu mwanamke alitoa kwa kujikana, ni muhimu kufahamu kuwa ibada ni kafara na hakuna kafara isiyogharimu, hatupaswi kumpa Mungu vitu visivyogharimu nafsi zetu, ibada yenye maana zaidi inahusisha kujitoa kwaajili ya Mungu na wengine! Nyakati za kanisa la kwanza katika makanisa yaliyokuwepo Macedonia yaani Ugiriki Bila shaka Kanisa la wafilipi walielewa aina hii ya utoaji katika mapenzi ya Mungu na hivyo japo walikuwa hawana kitu, walitoa tena sio kwa kulazimishwa kwa hiyari, kwa furaha, kwa uwezo na hata zaidi ya uwezo lakini wakitanguliwa na kujitoa kwanza nafsi zao 2Wakoritho 8:1-5 “Tena ndugu zetu, twawaarifu habari ya neema ya Mungu, waliyopewa makanisa ya Makedonia; maana walipokuwa wakijaribiwa kwa dhiki nyingi, wingi wa furaha yao na umaskini wao uliokuwa mwingi uliwaongezea utajiri wa ukarimu wao. Maana nawashuhudia kwamba, kwa uwezo wao, na zaidi ya uwezo wao, kwa hiari yao wenyewe walitoa vitu vyao; wakituomba sana pamoja na kutusihi kwa habari ya neema hii, na shirika hili la kuwahudumia watakatifu. Tena walitenda hivi si kama tulivyotumaini tu, bali kwanza walijitoa nafsi zao kwa Bwana; na kwetu pia, kwa mapenzi ya Mungu.” Unaona huu ndio utoaji ambao Yesu aliukusudia wanafunzi wake waelewe, kanisa la leo linapoteza Baraka kwa sababu kwanza wao wenyewe hawajajitoa kwa Mungu na kwa sababu hiyo wanaona taabu kutoa kwa Mungu, wakiwa hawana imani na wamejaa woga kuwa kesho itakuwaje na matokeo yake tuna wakristo wachoyo hata kuliko waislamu na wapagani!, unapooona makanisani kila siku watumishi wa Mungu wanafundisha juu ya kutoa ujue watu hawajitambui na wala somo kuhusu utoaji halijaeleweka kwao!

 

b.      Mjane alitaka kuyatenda mapenzi ya Mungu

 

Mjane Yule hakuenda ibadani kutoa kama maonyesho, alikuwa ameelewa neno la Mungu linataka nini na alikuwa kazini akiyatekeleza mapenzi ya Mungu, akitoa hakuketi chi ni na kufikiri kuhusu ujane wake , wala hakufikiri kuwa Mungu amemtenza mabaya kwa kumuacha katika umasikini wa kutupwa na akiwa hana mtu wa kumsaidia, huenda alikuwa akimshukuru Mungu hata kwa kile alichokipata, na hakusema moyoni ngoja nipate zaidi nitatoa hapana alitaka kuabudu kweli kweli sio kwa mdomo kwa vitendo Mathayo 7:21 “Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni.” Mwanamke huyu mjane na masikini alikuwa kazini, hakuwa kwenye maonyesho, hapiti kutoa sadaka aonekane kuwa kaja ibada, haoiti mkunyesha nguo nzuri wala hapito kuionyesha amekuja ibada hapana yuko kazini kwelikweli ilikuwa saa ya kutoa na alikuwa anakwenda kutoa akijua kwa nini anatoa na tena sio kwa kulazimishwa bali kwa hiyari na uelewa ulio wazi na kwa nia na alikusudia hivyo tangu anatoka nyumbani  2Wakoritho 9:7-8 “Kila mtu na atende kama alivyokusudia moyoni mwake, si kwa huzuni, wala si kwa lazima; maana Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo wa ukunjufu. Na Mungu aweza kuwajaza kila neema kwa wingi, ili ninyi, mkiwa na riziki za kila namna siku zote, mpate kuzidi sana katika kila tendo jema;” unaiona mwanamke huyu alitoa kwa ukunjufu wa moyo, na Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo na kama sadaka inakukwaza na kukufanya ujisikie huzuni sadaka hiyo haifai, tunapotioa Mungu huangalia nia yetu 2Wakoritho 8:12 “Maana, kama nia ipo, hukubaliwa kwa kadiri ya alivyo navyo mtu, si kwa kadiri ya asivyo navyo.” Haya ndiyo yaliyiompa maksi mjane Yule.

 

c.       Alitoa licha ya umasikini wake!

Pamoja na umasikini mku bwa aliokuwa nao mwanamke Yule mjane, hii haikumfanya aka chini na kujifikiri kuwa kuwa yeye bado sana ! unajua wako watu makanisani ukifika wakati wa sadaka na changizo nyingine za kikanisa wao huwa wanakuwa wapole na wanakaa kimya hawanyooshi mkono kujitoa wanajifikiri wao ni masikini, wanadhani kuwa wako watu maalumu watakaomtolea Mungu lakini wao bado sana nisikilize katika moyo wa Mungu wewe bado sana na tena utaendelea kuwa masikini kwa sababu unajua kutokutoa kwako kwa sababu ya hali yako kunageuka kuwa dua mbaya kwamba ni kama unamwambia Mungu  mimi sitoi kwa sababu hujanipa, unapochangamka na kutoa kama mjane huyu maana yeke ni kuwa unamshawishi Mungu kuona na kukuamini kuwa huyu nikimpa vingi kwa kuwa amekuwa mwaminifu katika madogo atakuwa mwaminifu katika makubwa pia Luka 16:10-12 “Aliye mwaminifu katika lililo dogo sana, huwa mwaminifu katika lililo kubwa pia; na aliye dhalimu katika lililo dogo, huwa dhalimu katika lililo kubwa pia. Basi, kama ninyi hamkuwa waaminifu katika mali ya udhalimu, ni nani atakayewapa amana mali ya kweli? Na kama hamkuwa waaminifu katika mali ya mtu mwingine, ni nani atakayewapa iliyo yenu wenyewe? unaona mwanamke huyu mjane na masikini kweli kweli alikuwa mwaminifu katika umasikini wake na kwa sababu hiyo alitoa katika hali hiyo hiyo ya umasikini wake wakati wengine walitoa vilivyowazidi, walitoa wasivyovihitaji, hawakuwa wamejikana katika kutioa kwao, Mwanamke huyu mjane alitoa kwa sababu alimpenda Bwana, alikuwa hana ubinafsi, wala hakutaka kujilimbikizia, hakuwa na muda wa kupiga hesabu, alikuwa akifuarahia ikiwezekana labda hata zawadi ya uhai aliyopewa na Mungu, kutokuugua, kupata nafasi ya kuabudu akiutzama wema wa Mungu kuliko yaliyomkuta huu ndio utoaji usio na ubinafsi


Hitimisho!

Mtu awaye yote anayetaka kupokea kutoka kwa Mungu anapaswa kuelewa kwanini tunatoa, na lazima ieleweke wazi kuwa Mungu huwabariki wale wanaotoa kwa Moyo, utoaji wa kikristo ni hiyari na sio lazima, ni furaha na sio huzuni, ni moyo na sio utajiri, Nyakati za Kanisa la kwanza watu walitoa hata mali zao na kuwagaia wengine na kuifadhili kazi ya Mungu iweze kwenda mbele Barnaba alikuwa mmoja wao ona  Matendo ya Mitume 4:36-37. “Na Yusufu, aliyeitwa na mitume Barnaba, (maana yake, Mwana wa faraja), Mlawi, asili yake ni mtu wa Kipro,alikuwa na shamba akaliuza, akaileta fedha, akaiweka miguuni pa mitume.” Wakristo wanapaswa kujifunza kutoa na wazazi wanapaswa kuwafundisha watoto wao umuhimu wa kutoa tangu wakiwa wadogo, tusisubiri mpaka tumekomaa au kuzeeka tukiwa na tabia ngumu ya choyo Mungu anataka tuwe na tabia hii tangu mwanzo, iwe ni tabia ya maisha yetu na sidhani kama ni sahihi kusubiri wakati tumechoka au umestaafu Muhubiri 12:1 “Mkumbuke Muumba wako siku za ujana wako, Kabla hazijaja siku zilizo mbaya, Wala haijakaribia miaka utakaposema, Mimi sina furaha katika hiyo.” Kuwafundisha watu wakishakuwa watu wazima ni kuchelewa sana kuwafanya watu hawa kuja kuelewa mapenzi ya Mungu na yanakuwa mmzigo kwao Maombolezo 3:27 “Ni vema mwanadamu aichukue nira Wakati wa ujana wake.” Ni wachache sana wanaweza kuelewa na kujaribu kulitendea kazi somo kama hili lenye kuhusisha kujitoa nasfi lakini wakati wote tukumbuke kutoa kwa moyo pasipo manung’uniko na kuhakikisha kuwa tunatoa kwa sababu nia yetu ni njema na kwa furaha katika kuhakikisha kuwa injili inakwenda mbele na wale wanaoishi kwa injili wanapata mkate wao wa kila siku, kwa kuyajua haya utakuwa umeyatimiza hivyo mapenzi ya Mungu, Muongezewe neema

Na. Rev. Innocent Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni