Jumatatu, 23 Agosti 2021

Kwa kuwa yuko kuumeni kwangu, sitaondoshwa !


Zaburi 16:1-9 “Mungu, unihifadhi mimi, Kwa maana nakukimbilia Wewe.  Nimemwambia Bwana, Ndiwe Bwana wangu; Sina wema ila utokao kwako. Watakatifu waliopo duniani ndio Walio bora, Hao ndio niliopendezwa nao. Huzuni zao zitaongezeka Wambadilio Mungu kwa mwingine; Sitazimimina sadaka zao za damu, Wala kuyataja majina yao midomoni mwangu. Bwana ndiye fungu la posho langu, Na la kikombe changu; Wewe unaishika kura yangu. Kamba zangu zimeniangukia mahali pema, Naam, nimepata urithi mzuri.Nitamhimidi Bwana aliyenipa shauri, Naam, mtima wangu umenifundisha usiku. Nimemweka Bwana mbele yangu daima, Kwa kuwa yuko kuumeni kwangu, sitaondoshwa. Kwa hiyo moyo wangu unafurahi, Nao utukufu wangu unashangilia, Naam, mwili wangu nao utakaa kwa kutumaini.


Utangulizi:

Daudi alikuwa mtu wa mapambano alipokuwa Duniani, alipambana vita vingi sana kwaajili yake, watu wake na kwaajili ya ufalme wa Mungu, kwa msingi huo katika kuabudu kwake kwa njia ya zaburi mara nyingi sana analugha tamu zinazoweza kujenga imani na ujasiri katika maisha yetu, na kutufanya tusiogope lolote linalotukabili katika maisha yetu, Lakini sio hivyo tu, kuna kujengeka kwa uhusiano wetu wa karibu na Mungu unapofuatilia zaburi za Daudi ambaye anaonyesha mara kadhaa sababu za ushindi wake na siri ya ushindi wake kuwa ulitokana na namna na jinsi alivyojenga uhusiano wake wa karibu na Mungu. Katika zaburi hii tunasoma :-

Zaburi 16:1-9 “Mungu, unihifadhi mimi, Kwa maana nakukimbilia Wewe. Nimemwambia Bwana, Ndiwe Bwana wangu; Sina wema ila utokao kwako. Watakatifu waliopo duniani ndio Walio bora, Hao ndio niliopendezwa nao. Huzuni zao zitaongezeka Wambadilio Mungu kwa mwingine; Sitazimimina sadaka zao za damu, Wala kuyataja majina yao midomoni mwangu. Bwana ndiye fungu la posho langu, Na la kikombe changu; Wewe unaishika kura yangu. Kamba zangu zimeniangukia mahali pema, Naam, nimepata urithi mzuri.Nitamhimidi Bwana aliyenipa shauri, Naam, mtima wangu umenifundisha usiku. Nimemweka Bwana mbele yangu daima, Kwa kuwa yuko kuumeni kwangu, sitaondoshwa. Kwa hiyo moyo wangu unafurahi, Nao utukufu wangu unashangilia, Naam, mwili wangu nao utakaa kwa kutumaini.Kuna maswala kadhaa ya kujifunza ambayo Daudi anayataja lakini mazuri zaidi au yale ambayo nimevutiwa nayo leo ni ule mstari wa nane unaosema Nimemweka Bwana mbele yangu daima, Kwa kuwa yuko kuumeni kwangu, sitaondoshwa. Katika mstari huu kuna mambo mawili ya msingi ya kujifunza na ambayo yalikuwa siri kubwa sana ya ujasiri na ushindi wa Daudi katika maisha yake yote. Mambi hayo tukiwa nayo nasi vilevile kama Daudi tutakuwa na ushindi mkubwa sana katika maisha yetu, tutajifunza somo hili Kwa kuwa yuko kuumeni kwangu, sitaondoshwa. Kwa kuzingatioa vipengele vitatu viofuatavyo:-

 

1.       Kumuweka Bwana mbele Daima.

2.       Kwa kuwa yuko kuumeni kwangu.

3.       Sitaondoshwa.

 

Kumweka Bwana mbele Daima

Lugha inayotumika hapo Kumuweka Bwana mbele Daima ina maana ya kumpa Mungu kipaumbele au kumtegemea Mungu na kutambua uwepo wake kwenye kila jambo, kwamba Mungu yuko pamoja naye iwe usiku au mchana, kumfikiri yeye wakati wote, kumtafakari na kumkiri mbele ya watu, ni kuutambua uwepo wake kila mahali na kila wakati na katika hali zote, kumhisi kuwa yuko pamoja naye, kutambua tu mara zote kuwa macho yake yako pamoja naye, ni kufikiri wazi kuwa wakati wote niko katika uwepo wa Mungu na wakati wote yeye ananiangalia  kutokana na umuhimu ya jambo hili ganao jipya pia limeuridia mstari wetu wa msingi katika namna nyingine ;- Matendo 2:25 “Maana Daudi ataja habari zake, Nalimwona Bwana mbele yangu siku zote, Kwa kuwa yuko upande wa mkono wangu wa kuume, nisitikisike.” Mwandishi wa zaburi hii haoni kitu kingine kwanza haoni msaada mwingine kokote, yeye msaada wake na kipaumbele chake ni Mungu kwanza, wakati wote na siku zote anamtanguliza Mungu, ni sawa na kusema au kutii amri ya Mungu inayotaka tusiwe na miungu mingine ila yeye peke yake ona Kutoka 20:3 “Usiwe na miungu mingine ila mimi.” Siri ya ushindi katika maisha ya Daudi ni kuwa kabla ya kufikiri kutafuta msaada kwa mwingine yeye msaada wake ni Mungu aliyeziumba Mbingu na nchi Mungu aliye hai, wakati watu wengine katika vita wanategemea wingi wa majeshi yao, wanategemea akili zao, wanategemea silaha zao nzito, mbinu na mikakati ya ajabu ya kibinadamu mwandishi wa zaburi yeye anataja jina la Bwana Zaburi 20:7-8 “Hawa wanataja magari na hawa farasi, Bali sisi tutalitaja jina la Bwana, Mungu wetu. Wao wameinama na kuanguka, Bali sisi tumeinuka na kusimama.” Siri ya ushindi wetu ni kumuweka Mungu mbele, zinapokuja changamoto za aina yoyote Mungu anataka kwanza ufikiri kuhusu yeye, uone yeye kuwa ndio msaada umtegemee yeye na kumwangalia yeye lakini ukitegemea mengine wewe uko chini ya laana Yeremia 17:5-8 “Bwana asema hivi, Amelaaniwa mtu yule amtegemeaye mwanadamu, Amfanyaye mwanadamu kuwa kinga yake Na moyoni mwake amemwacha Bwana. Maana atakuwa kama fukara nyikani, Hataona yatakapotokea mema; Bali atakaa jangwani palipo ukame, Katika nchi ya chumvi isiyokaliwa na watu. Amebarikiwa mtu yule anayemtegemea Bwana, Ambaye Bwana ni tumaini lake. Maana atakuwa kama mti uliopandwa kando ya maji, Uenezao mizizi yake karibu na mto; Hautaona hofu wakati wa hari ujapo, Bali jani lake litakuwa bichi; Wala hautahangaika mwaka wa uchache wa mvua, Wala hautaacha kuzaa matunda.” kwa msingi huo maandiko yanatutaka tumuweke Mungu mbele na kumfanya yeye kuwa  wa kwanza katika kila jambo, agano jipya linasema tafuteni kwanza ufalme wa Mungu na haki yake na mengine yote mtazidishiwa, asili ya ushindi wetuni kumuweka Mungu mbele! Na ndio ilikuwa siri kuu ya Daudi.

Kwa kuwa yuko kuumeni kwangu!

Nyakati za utawala wa kifalme zamani mtu kukuweka mkono wake wa kuume ilikuwa na maana ya Heshima au ukuu, ni nafasi ya kuheshimika na ya juu kabisa kukaa upande wa kuume wa mfalme au katika meza moja naye, na kula chakula pamoja naye 2Samuel 9:1-8 “Kisha Daudi akasema, Je! Amesalia mtu mmoja katika nyumba ya Sauli, nipate kumtendea mema kwa ajili ya Yonathani? Palikuwa na mtumishi mmoja wa nyumba ya Sauli, jina lake Siba, basi wakamwita aende kwa Daudi; na mfalme akamwuliza, Wewe ndiwe Siba? Naye akasema Mimi, mtumwa wako ndiye. Mfalme akasema, Je! Hakuna hata sasa mtu ye yote wa nyumba ya Sauli, nipate kumtendea mema ya Mungu? Siba akamwambia mfalme, Yonathani anaye mwana hata sasa, aliye na kilema cha mguu. Mfalme akamwambia, Yuko wapi? Siba akamwambia mfalme, Tazama, yumo katika nyumba ya Makiri, mwana wa Amieli, katika Lo-debari. Basi mfalme Daudi akatuma watu, akamwondoa katika nyumba ya Makiri, mwana wa Amieli, katika Lo-debari. Basi Mefiboshethi, mwana wa Yonathani, mwana wa Sauli akaenda kwa Daudi, akaanguka kifudifudi, akasujudu. Daudi akasema, Mefiboshethi! Naye akaitika, Mimi hapa, mtumwa wako! Daudi akamwambia, Usiogope, maana bila shaka nitakutendea mema; kwa ajili ya Yonathani, baba yako, nami nitakurudishia mashamba yote ya Sauli, baba yako; nawe utakula chakula mezani pangu daima. Akasujudu, akasema, Mimi mtumwa wako ni nini, hata ukamwangalia mbwa mfu kama mimi?  lakini vilevile kijeshi mtu aliyekaa mkono wa kuume maana yake alihesabika kama mlinzi, mtu aliye karibu sana, aliye tayari kuokoa au kulinda au kuzuia uzipatwe na madhara ni askari mwenzako mjamaa, kwa kiingereza  your colleague au  COMRADE Zaburi 109:30-31 “Nitamshukuru Bwana kwa kinywa changu, Naam, nitamsifu katikati ya mkutano. Maana atasimama mkono wa kuume wa mhitaji Amwokoe na wanaoihukumu nafsi yake” ona pia Zaburi 110:5 “Bwana yu mkono wako wa kuume; Ataseta wafalme, Siku ya ghadhabu yake.” Kwa msingi huo ili tuweze kuona maisha ya ushindi katika kila eneo la maisha yetu lazima tuwe na hisia kuwa tuna mpiganaji aliye karibu mkono wetu wa kuume kutulinda na kutusaidia, ni rafiki wa karibu wa mtazamo mmoja sawa na sisi yeye atatoa msaada  kwa hiyo Mwandishi wa zaburi alikuwa anamwangalia Mungu kuwa yuko mkono wake wa kuume na kwa vyovyote vile hatasinzia atahakikisha anatutetea katika kila jambo linalotukabili atatulinda na mabaya yote Zaburi 121:1-8 “Nitayainua macho yangu niitazame milima, Msaada wangu utatoka wapi? Msaada wangu u katika Bwana, Aliyezifanya mbingu na nchi. Asiuache mguu wako usogezwe; Asisinzie akulindaye; Naam, hatasinzia wala hatalala usingizi, Yeye aliye mlinzi wa Israeli. Bwana ndiye mlinzi wako; Bwana ni uvuli mkono wako wa kuume. Jua halitakupiga mchana, Wala mwezi wakati wa usiku. Bwana atakulinda na mabaya yote, Atakulinda nafsi yako. Bwana atakulinda utokapo na uingiapo, Tangu sasa na hata milele.”

Sitaondoshwa!

Daudi anaonyesha sasa hiyimisho kwamba ikiwa umemuweka Mungu mbele daima na ukamuweka mkono wako wa kuume kinachofuata sasa ni kuwa hutaiondoshwa, maana yake ni kuwa hakuna cha kukutikisha, hakuna cha kukusumbua, unakuwa na ujasiri ulio wazi, utasimama milelel, utaimarika. utakuwa salama, hutaogopa, utalindwa dhidi ya maadui, watatawanyika wanaokutafura nafsi yako, wataanguka na kurudishwa nyuma utadumu Zaburi 10:6 “Asema moyoni mwake, Sitaondoshwa, Kizazi baada ya kizazi sitakuwamo taabuni. Hakuna kutetemeshwa utasimama imara Zaburi 46:5 Mungu yu katikati yake hautatetemeshwa; Mungu atausaidia asubuhi na mapema.” Wakati wote mtu anayemtegemea Mungu hatatikiswa na lolote, hata kama yatatokea magumu kiasi gani, fitina kiasi gani, majungu kiasi gani, vitisho kiasi gani, uzushi kiasi gani, vita kiasi gani, masengenyo kiasi gani, njaa, kiasi gani aibu kiasi gani, mitego kiasi gani, chuki kiasi gani, panga panghua kiasi gani, nia ovu kiasi gani, kuchafuliwa kiasi gani, mashambulizi ya kiwango chochote kile, Hakuna kitakachozeza kukuondosha, Mungu akiwa pamoja nawe na akiwa ndio Comrade wako anayeketi mkono wako wa kuume, uko pamoja naye umempa heshima yake nataka nikuambie ya kuwa hatakuazha kamwe , hatasinzia atahakikisha kuwa unasimama, sasa inategemea wewe umemuweka Mungu wapi, maisha yako yatakuwa na mashaka sana kama Mungu sio kipaumbele chako, utayumbishwa hukona huko kwa sababu umeweka tegemeo lako kwa wanadamu, umewafanya wanadamu kuwa kinga yako, Muweke Mungu mbele, tengeneza uhusiano wako na yeye, mfanye bwana kuwa rafiki yako, muweke mkono wako wa kuume na hutatikiswa

 

Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni