Wimbo uliobora 2:15 “Tukamatie mbweha, Wale
mbweha wadogo, Waiharibuo mizabibu, Maana mizabibu yetu yachanua.”
Utangulizi:
Kitabu cha wimbo uliobora ni
mojawapo ya kitabu katika vitabu vijulikanavyo kama vitabu vya mashairi, vitabu
vingine ni pamoja na Ayubu, Zaburi, Mithali, Muhubiri na kitabu hiki cha wimbo
ulio bora, Katika vitabu hivi kuna mafunzo mengi sana ya hekima kuhusu maisha,
na kwa kuwa ni vitabu vya mashairi wakati mwingine unaweza kukutana na lugha au
misemo yenye kushangaza lakini yenye mafunzo muhimu sana kwa jamii!, kitabu cha
wimbo ulio bora hata hivyo mashairi yake ni mashairi ya kimapenzi na ni mtu na
mpenzi wake waliokuwa wakiimbiana na kujibizana, katikati ya mahaba yao
wakaambiana maneno haya Wimbo Ulio Bora
2:15 “Tukamatie mbweha, Wale mbweha wadogo,
Waiharibuo mizabibu, Maana mizabibu yetu yachanua.” Kimsingi lugha
hii ni lugha ya kimashairi na inatufunza mamswala ya msingi katika Nyanja
nyingi za maisha katika maeneo mbalimbali, Wafasiri wengi wa maandiko na
wanatheolojia wanakiri kuwa mahusiano haya ya kimapenzi yalikuwa ni kati ya
kijana wa kifalme Suleimani na mwanamke Mshulami, hata hivyo kitheolojia wimbo
huu unahusu vilevile mahusiano yaliyoko kati ya Yesu na Kanisa lake.
Tunajifunza somo hili kwa kuzingatia vipengele vifuatavyo:-
1. Mbweha wadogo waiharibuo mizabibu!
2.
Maana
ya mbweha wadogo waiharibuo Mizabibu
Mbweha wadogo
waiharibuo mizabibu!
Nyakati za Biblia katika Isarael
hasa kutokana na geographia ya nchi ya Kanaani au Israel Mbweha walijulikana
kama wanyama wadogo waharibifu, hususani kwa sababu wao walijihusisha na kilimo
ikiwemo kilimo cha mizabibu, Na wanyama hawa walikuwa miongoni mwa wanyama
waharibifu kwa mizabibu hususani pale inapoanza kutoa maua au kuchanua !,
inawezekana kuwa wako wanyama wengi wakubwa zaidi na waharibifu, kama ilivyo Afirka
tembo wanaweza kuingia kwenye mashamba ya watu na wakafanya uharibifu mkubwa
kwa dakika chache, Mashariki ya kati mashamba ya mizabizu yalikuwa
yakizungushiwa wigo wa mawe ili kuyalinda na wanyama waharibifu na hivyo
yalikuwa salama, ona
Marko 12:1-2 “Akaanza kusema nao kwa
mifano; Mtu mmoja alipanda shamba la mizabibu, akazungusha ugo, akachimba shimo
la shinikizo, akajenga mnara, akapangisha wakulima, akasafiri. Hata kwa wakati
wake akatuma mtumwa kwa wale wakulima, ili apokee kwa wakulima katika matunda
ya mizabibu”.
Lakini huenda hata hivyo Mbeha
ndio walikuwa adui wakubwa wa mizabibu na labda zaidi sana wakati yakichanua
maua. Lakini hata hivyo watu wengi waliwadharau mbweha kama wanayama wasi
hatarishi sana, ukilinganisha na wengine, Kimsingi unapoiangali Biblia inaweza
kumaanisha kuwa Mbweha alitumika pia au kuhesabiika miongoni mwa wanyama wanaoweza
kutumika kwa uharibifu na hivyo pamoja
na kujilinda dhidi ya wanyama wengine wakubwa na waharibifu wakulima wa
mizabibu hawakupaswa kabisa kuwadharau mbweha kwani nao wanachangia uharibifu
hata kama watacheza cheza kwenye mashamba ya zabibu na kuangusha maua ambayo
ndio asili ya kupata matunda, Ki biblia Mbweha ni mnyama aliyetumika kuonyesha
hali ya uharibifu mfano Samsoni aliwatumia Mbweha kuchoma mashamba ya ngano ya
wafililisti
Waamuzi 15:3-5 “Samsoni akasema, Safari hii
nitakuwa sina hatia katika habari za hawa Wafilisti, hapo nitakapowadhuru.
Samsoni akaenda akakamata mbweha mia tatu; kisha akatwaa vienge vya moto
akawafunga mbweha mkia kwa mkia, akatia kienge kati ya kila mikia miwili.
Alipokwisha kuviwasha moto vile vienge, akawaachia mbweha kati ya ngano ya
Wafilisti, akayateketeza matita, na ngano, hata na mashamba ya mizeituni.”
Pia mbweha walitumika kama ishara
ya dharau kubwa sana, kama kitu kilikuwa cha uongo, au chenye viwango vya chini
sana au mtu mwoga kupita kawaida au chenya kuzuia mapenzi ya Mungu
kilichodharaulika mno kama manabii wa uongo, au ujenzi ulio chini ya kiwango,
au mtu mwoga kuliko kawaida manabii na watu wa nyakati za biblia walilitumia
neno mbweha kwa kitu kilicho dharaulika mfano ona
Nehemia 4:1-5 “Lakini ikawa, Sanbalati
aliposikia ya kwamba tulikuwa tukiujenga ukuta, akaghadhibika, akaingiwa na
uchungu sana, akawadhihaki Wayahudi. Akanena mbele ya nduguze na mbele ya jeshi
la Samaria, akisema, Wayahudi hawa wanyonge wanafanyaje? Je! Watajifanyizia
boma? Watatoa dhabihu? Au watamaliza katika siku moja? Je! Watayafufua mawe
katika chungu hizi za kifusi, nayo yameteketezwa kwa moto? Basi Tobia, Mwamoni,
alikuwa karibu naye, akasema, Hata hiki wanachokijenga, angepanda mbweha,
angeubomoa ukuta wao wa mawe. Sikia, Ee Mungu wetu; maana tunadharauliwa;
ukawarudishie mashutumu yao juu ya vichwa vyao, ukawatoe watekwe katika nchi ya
uhamisho; wala usiusitiri uovu wao, wala isifutwe dhambi yao, mbele zako; kwa
maana wamekukasirisha mbele ya hao wanaojenga.”
Ezekiel 13:1-4 “Kisha neno la BWANA
likanijia, kusema, Mwanadamu, tabiri juu ya manabii wa Israeli wanaotabiri,
uwaambie wanaotabiri kwa mioyo yao wenyewe, Lisikieni neno la BWANA; Bwana
MUNGU asema hivi; Ole wao manabii wajinga, wanaoifuata roho yao wenyewe, wala
hawakuona neno lo lote!Ee Israeli, manabii wako wamekuwa kama mbweha, mahali
palipo ukiwa.”
Luka 13:31-33 “Saa ile ile Mafarisayo kadha
wa kadha walimwendea, wakamwambia, Toka hapa, uende mahali pengine, kwa sababu
Herode anataka kukuua. Akawaambia, Nendeni, mkamwambie yule mbweha, Tazama, leo
na kesho natoa pepo na kuponya wagonjwa, siku ya tatu nakamilika. Pamoja na
hayo imenipasa kushika njia yangu leo na kesho na kesho kutwa; kwa kuwa
haimkini nabii aangamie nje ya Yerusalemu.”
Kwa hiyo suleimani na mpenzi wake
walipokuwa wakiimbiana wimbo wa mapenzi na kuona kuwa penzi lao limechanua
waliimbina na kupeana tahadhari kuwa watajilinda na maadui wakubwa wa mapenzi
yao lakini fvilevile wasidharau maadui wadogo ambao nao wanaweza kuathiri pezni
lao lisiweze kuzaa marunda, Maadui wakubwa wa mapenzi walifanannishwa na
wanyama wakubwa huko Misri maadui wakubwa wa mapenzi walifananishwa na mamba,
na Israel maadui wadogowadogo wa mapenzi walifananishwa na mbwea, kwa hiyo
katika wimbo wao wa kimapenzi Suleimani hakutaka hata vitu vidogovidogo
vinavyodhauliwa na watu, wengi kwao
visiharibu mapenzi yao kwa gharama yoyote wala viziwe tishio la mapenzi
yao, ili mahusiano yaweze kuwa imara
kuna vitu vidogo vidogo vingi ambavyo havipaswi kupuuziwa, kwani vikipuuzwa
navyo vinaweza kufifisha upendo, na vinaweza kuwa hatari sana hivyo wapendanao
lazima wahakikishe kuwa wanajilinda dhidi ya maadui wakubwa na wale
wadogowadogo ili kutunza mahusiano mema katika upendo wao, Upendo haulindwi na kumnunulia mtu nguo
pekee, au kumnunulia chakula, au kumtunza, au kumzalisha, au kumpa fedha ya
saloon, au kumuachia fedha mezani, au kufanya kazi kwa bidii ili uitunze
familia yako, au kushughulika sana katika tendo la ndoa au kumpa mumeo au mkeo
kila siku, kuna vitu vidogovidogo sana ambavyo vinaweza kumfanya mwenzi wako
ajisikie yuko peponi, leo hii watu wanagombana sana, hawasameheani, kila mmoja
na simu yake, hakuna kupokeana, hakuna mazungumzo na vitu vingi ambavyo ni vya
muhimu katika kujenga uhusiano hata hivyo kumbuka sitaki kuzungumzia mapenzi
katika somo langu hili mimi nazungumzia maswala ya rohoni
Maana ya mbweha wadogo waiharibuo Mizabibu
Ni muhimu kufahamu kama
tulivyosema awali kuwa Mbweha sio wanyama wakubwa sana wanaoweza kusababisha
uharibifu mkubwa kama tembo au dubu na kadhalika, mbweha wana urefu wa inchi
kama 20 na uzito kama wa kilo nane hivi, lakini tatizo lao kubwa ni kuwa wana
uwezo wa kuharibu maua lakini pia kutafuna na kusababisha mzabibu kukauka na
ukakosa matunda na ndio maana nyakati za Biblia licha ya kuwadharau mbweha
lakini pia walikuwa na kampeni ya kuwakamata na kuwaua kabisa kutokana na uwezo
wao mkubwa wa kusababisha uharibifu
Wimbo Ulio Bora 2:15 “Tukamatie mbweha,
Wale mbweha wadogo, Waiharibuo mizabibu, Maana mizabibu yetu yachanua.”
Jambo kubwa analolizungumza
Suleimani hapa ni kuwa mapenzi yake na Mshulami ndio yanaanza kuchanua hivyo
anatoa tahadhari kwa maswala ambayo kimsingi ynaweza kuleta uharibifu mkubwa
katika mahusiano yawe ya kimapenzi yawe
na watu au na Mungu, watu wengi sana wanaompokea Yesu wanaweza kuwashinda
maadui wakubwa wanaoonekana kwa nje wanaweza kuwa sio waizi, wanaweza kuwa sio
wazinzi, wanaweza kuwa sio walevi, wanaweza kuwa hawaviti sigara, wanaweza kuwa
sio wasengenyaji, wala sio wafitini, wala sio wachonganishi, wanaweza kuwa sio
wenye tamaa ya fedha lakini kuna vitu ambavyo watu wengi wanavidharau, Maswala
ambayo yanaharibu maisha yetu, na kuharibu ndoa zetu, yanayoharibu ushuhuda
wetu, au yanayotutia gizani, yanayoharbu mahisiano wakati mwingine sio yale
yanayoonekana kwa macho wakati mwingine ni yale yaliyoko mioyoni mwetu
1.
Ubinafsi
- wanadamu wengi sana wanasumbuliwa
na ubinafsi, wanataka kujitukuza wenyewe, wanataka wao wenyewe ndio wabaki juu,
wajitumikie wenyewe wajifurahishe wenyewe na wawe juu yaw engine tu Biblia inaonyesha kuwa ni watu wachache sana
ambao huangalia mambo ya wengine lakini wengi sana huangalia maslahi yao
2Timotheo 3:2-4 “Maana
watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe, wenye kupenda fedha, wenye kujisifu,
wenye kiburi, wenye kutukana, wasiotii wazazi wao, wasio na shukrani, wasio
safi, wasiowapenda wa kwao, wasiotaka kufanya suluhu, wasingiziaji,
wasiojizuia, wakali, wasiopenda mema, wasaliti, wakaidi, wenye kujivuna,
wapendao anasa kuliko kumpenda Mungu;”
Kujipenda
mwenyewe ni moja ya dhambi ambayo inaweza kuonekana kuwa ni ndogo lakini
inaweza kusababisha madhara makubwa sana katika ndoa, familia na hata taifa au
kanisa ni rahisi kufikiri kuwa ubinafsi sio tatizo lakini ni tatizo kubwa sana
ambalo kwa hili wengi watakosa nafasi ya kuingia mbinguni hii ni ile hali ya
mimi kwanza, mtu anaweza kuwa sio mzinzi, wala mlevi wala mwizo lakini akawa ni
mbinafsi kuliko kawaida mchoyo anataka afanikiwe yeye tu
Luka 18:18-25 “Tena,
mtu mkubwa mmoja alimwuliza, akisema, Mwalimu mwema, nifanye nini ili nipate
kuurithi uzima wa milele? Yesu akamwambia, Mbona unaniita mwema? Hakuna aliye
mwema ila mmoja, naye ndiye Mungu. Wazijua amri; Usizini, Usiue, Usiibe,
Usishuhudie uongo, Waheshimu baba yako na mama yako. Akasema, Hayo yote
nimeyashika tangu utoto wangu. Yesu aliposikia hayo alimwambia, Umepungukiwa na
neno moja bado; viuze ulivyo navyo vyote, ukawagawanyie maskini, nawe utakuwa
na hazina mbinguni; kisha, njoo unifuate. Lakini aliposikia hayo alihuzunika
sana, maana alikuwa na mali nyingi. Yesu alipoona vile alisema, Kwa shida gani
wenye mali watauingia ufalme wa Mungu! Kwa maana ni vyepesi ngamia kupita
katika tundu la sindano kuliko tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu.”
Tatizo kubwa la
huyu tajiri ilikuwa iko dhambi ya choyo na umimi na ubinafsi ambayo yeye
aliiona kama sio tatizo kubwa kwa sababu ameshika mari zote lakini kumbe
alikuwa na mbweha anayeharibu mzabibu wake ambayo ni choyo na umimi na ubinafsi
mkubwa kujikana nafsi sio jambo jepesi
Mathayo 16:24-26 “Wakati
huo Yesu aliwaambia wanafunzi wake, Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane
mwenyewe, ajitwike msalaba wake, anifuate. Kwa kuwa mtu atakaye kuiokoa nafsi
yake, ataipoteza; na mtu atakayepoteza nafsi yake kwa ajili yangu, ataiona.
Kwani atafaidiwa nini mtu akiupata ulimwengu wote, na kupata hasara ya nafsi
yake? Au mtu atatoa nini badala ya nafsi yake? ”
Ubinafsi
umeharibu maisha ya watu wengi duniani umeharibu mahusiano ya watu, umeharibu
ndoa, umeharibu na kusababisha vita, mafarakano na migawanyiko mikubwa katika
jamii, imeleta misiba mikubwa na hata vifo kwa sababu ya ubinafsi tu japo
linaonekana ni jambo dogo
2.
Uchungu:
Watu wengi sana
wanadhani ni haki wao kuwa na uchungu na hawaoni kuwa kuwa na uchungu ni dhambi
inaonekana ndogo lakini ina madhara makubwa, kwa sababu ya uchungu na hofu mtu
anajikuta akakosoa tu kila kitu au anakosoa mtu, linaweza lisiwe tatizo kubwa
lakini biblia imaonya kwamba ni shina ambalo likiwemo ndani ya mtu linaweza
kuleta madhara makubwa kwa jamii
Waebrania 12:14-15 “Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao
hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao; mkiangalia sana mtu asiipungukie
neema ya Mungu; shina la uchungu lisije likachipuka na kuwasumbua, na watu
wengi wakatiwa unajisi kwa hilo.”
3.
Kutokusamehe:
Kusamehe ni
swala la kutangaza msamaha kwa mtu mwingine, bila kujali amakukosea nini katika
maandiko kibiblia msamaha wa Mungu unahusiana na dhambi zetu lakini ili
tusamehewe na Mungu sharti lake ni kuwa lazima tuwasamehe wengine kutokuwasamehe wengine kunakuweka katika
magereza ngumu ya kukufanya nawe usisamehewe na Mungu
Mathayo 18:21-35 “Kisha
Petro akamwendea akamwambia, Bwana, ndugu yangu anikose mara ngapi nami
nimsamehe? Hata mara saba? Yesu akamwambia, Sikuambii hata mara saba, bali hata
saba mara sabini. Kwa sababu hii ufalme wa mbinguni umefanana na mfalme mmoja
aliyetaka kufanya hesabu na watumwa wake.Alipoanza kuifanya, aliletewa mtu
mmoja awiwaye talanta elfu kumi. Naye alipokosa cha kulipa, bwana wake akaamuru
auzwe, yeye na mkewe na watoto wake, na vitu vyote alivyo navyo, ikalipwe ile
deni. Basi yule mtumwa akaanguka, akamsujudia akisema, Bwana, nivumilie, nami
nitakulipa yote pia. Bwana wa mtumwa yule akamhurumia, akamfungua, akamsamehe
ile deni. Mtumwa yule akatoka, akamwona mmoja wa wajoli wake, aliyemwia dinari
mia akamkamata,akamshika koo,akisema Nilipe uwiwacho. Basi mjoli wake akaanguka
miguuni pake, akamsihi, akisema, Nivumilie, nami nitakulipa yote pia. Lakini
hakutaka, akaenda, akamtupa kifungoni, hata atakapoilipa ile deni. Basi wajoli
wake walipoyaona yaliyotendeka, walisikitika sana, wakaenda wakamweleza bwana
wao yote yaliyotendeka. Ndipo bwana wake akamwita, akamwambia, Ewe mtumwa
mwovu, nalikusamehe wewe deni ile yote, uliponisihi; nawe, je! Haikukupasa
kumrehemu mjoli wako, kama mimi nilivyokurehemu wewe? Bwana wake akaghadhibika,
akampeleka kwa watesaji, hata atakapoilipa deni ile yote. Ndivyo na Baba yangu
wa mbinguni atakavyowatenda ninyi, msiposamehe kwa mioyo yenu kila mtu ndugu
yake.”
Sio rahisi
kusamehe lakini inahitajika neema ya Mungu, kuachia makosa ya aina mbalimbali
ambayo tumetendewa na wenzetu watu wengi sana wanafikiri kuwa wa haki ya
kutokusamehe wakidhani kuwa kununa kwao na kukasirika kwao ni halali kwa Mungu,
lakini ni ukweli ulio wazi kuwa mtu asiposamehe anaharibu kabisa maombi mfano
katika sala ya Bwana
Mathayo 6: 12. “Utusamehe
deni zetu, kama sisi nasi tuwasamehevyo wadeni wetu.” Watu wengi
kwaajili ya kutokusamehe wamepoteza kwa Mungu na wanadamu.
4.
Hasira
Hasira ni mojawapo
ya udhaifu ambao watu wengi wanafikiri ni sifa kuwa nazo kumbe ni moja ya tabia
mbaya sana, Mtu anayeweza kujizuia asikasirike ni mtu mwenye nguvu sana kuliko
anayekasirika hovyo maandiko yanatuagiza kuwa tusiache jua likachwa kabla
hatujaondoa hasira vifuani mwetu andiko
hili halitii moyo kuwa na hasira lakini linatia moyo kuhakikisha kuwa tunafanya
mapatano na wale tuliowakosea kwa sababu ya hasira zetu kabla jua halijachwa na
kama tutashindwa kufanya hayo mapema tunampa shetani nafasi ya kupanda mbegu ya
uchungu ambayo itakuwa na kuathiri wenguine
Waefeso 4:26-27 “Mwe
na hasira, ila msitende dhambi; jua lisichwe na uchungu wenu bado haujawatoka;
wala msimpe Ibilisi nafasi.”
Maandiko
yanataka tuweke mbali na kuzifisha kabisa dhambi mbalimbali kubwa na nyinginezo
tunazozidharau ikiwepo hasira na ghadhabu
Wakolosai 3:5-8 “Basi,
vifisheni viungo vyenu vilivyo katika nchi, uasherati, uchafu, tamaa mbaya,
mawazo mabaya, na kutamani, ndiyo ibada ya sanamu; kwa ajili ya mambo hayo huja
ghadhabu ya Mungu. Katika hayo ninyi nanyi mlitembea zamani, mlipoishi katika
hayo. Lakini sasa yawekeni mbali nanyi haya yote, hasira, na ghadhabu, na uovu,
na matukano, na matusi vinywani mwenu”
Ni hasira iliyomfanya Musa na Haruni kukataliwa na Mungu kuingia katika inchi ya mkanaani
Hesabu 20:12 “Bwana akamwambia Musa na Haruni, Kwa kuwa hamkuniamini mimi, ili kunistahi mbele ya macho ya wana wa Israeli, basi kwa sababu hiyo, hamtawaingiza kusanyiko hili katika ile nchi niliyowapa.”Hasira za Musa zikamfanya azungumze na kutenda mambo yasiyopasa ona
Zaburi 106:32-33. “Wakamghadhibisha penye maji ya Meriba, Hasara ikampata
Musa kwa ajili yao, Kwa sababu waliiasi roho yake, Akasema yasiyofaa kwa midomo
yake.”Kutokana
na kujaa ghadhabu Nabii Musa alimkosea Mungu na kupata hasara kwa kuzungumza na
kutenda yasiyofaa watu wengi sana wamepata hasara kwa sababu ya hasira
zilizowapelekea kutenda na kunena yasiyofaa hao ni mbweha wadogo wanaoharibu
mizabibu
5.
Wivu.
Ni hali ya
kutokujisikia vizuri kwa sababu ya mafanikio ya mtu mwingine, ubora wake,
mafanikio yake na kibali chake au bahati yake wako watu wanaumia sana wanapoona
wengine wamefanikiwa, wameolewa wao hawajaolewa, wamefanikiwa wao bado,
wamefaulu wao wamefeli, wanakibali wao hawana, wanakubaliwa na Mungu wao hawana
kitu na wanajisikia vibaya kiasi cha kukasirika kukosoa na hata kubeza ana
wakati mwingine hata kuua kwa sababu ya wivu wenye uchungu ona
Mwanzo 4:3-5 “Ikawa
hatimaye Kaini akaleta mazao ya ardhi, sadaka kwa BWANA. Habili naye akaleta
wazao wa kwanza wa wanyama wake na sehemu zilizonona za wanyama. BWANA
akamtakabali Habili na sadaka yake; bali Kaini hakumtakabali, wala sadaka yake.
Kaini akaghadhibika sana, uso wake ukakunjamana.”
Hali kama hii
ilimtokea pia kaka mkubwa katika Mfano ule wa mwana mpotevu pale alipoona ndugu
yake aliyepotea na akarudi japo alichukua mali za baba yake kama sehemu ya
urithi unaomuangukia akaenda kuzitapanya na makahaba aliporejea baba yake
alimpokea kwa furaha lakini kaka mkubwa aliposikia alisusa na kulaumu maamuzi
ya baba yake
Luka 15:11-32 “Akasema,
Mtu mmoja alikuwa na wana wawili; yule mdogo akamwambia babaye, Baba, nipe
sehemu ya mali inayoniangukia. Akawagawia vitu vyake. Hata baada ya siku si
nyingi, yule mdogo akakusanya vyote, akasafiri kwenda nchi ya mbali; akatapanya
mali zake huko kwa maisha ya uasherati. Alipokuwa amekwisha tumia vyote, njaa
kuu iliingia nchi ile, yeye naye akaanza kuhitaji. Akaenda akashikamana na mwenyeji
mmoja wa nchi ile; naye alimpeleka shambani kwake kulisha nguruwe.Akawa
akitamani kujishibisha kwa maganda waliyokula nguruwe, wala hapana mtu aliyempa
kitu. Alipozingatia moyoni mwake, alisema, Ni watumishi wangapi wa baba yangu
wanaokula chakula na kusaza, na mimi hapa ninakufa kwa njaa. Nitaondoka,
nitakwenda kwa baba yangu na kumwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele
yako;sistahili kuitwa mwana wako tena; nifanye kama mmoja wa watumishi wako.
Akaondoka, akaenda kwa babaye. Alipokuwa angali mbali, baba yake alimwona,
akamwonea huruma, akaenda mbio akamwangukia shingoni, akambusu sana. Yule mwana
akamwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako; sistahili kuitwa mwana
wako tena. Lakini baba aliwaambia watumwa wake, Lileteni upesi vazi lililo
bora, mkamvike; mtieni na pete kidoleni, na viatu miguuni;mleteni ndama yule
aliyenona mkamchinje; nasi tule na kufurahi; kwa kuwa huyu mwanangu alikuwa
amekufa, naye amefufuka; alikuwa amepotea, naye ameonekana. Wakaanza
kushangilia. Basi, yule mwanawe mkubwa alikuwako shamba na alipokuwa akija na
kuikaribia nyumba, alisikia sauti ya nyimbo na machezo. Akaita mtumishi mmoja,
akamwuliza, Mambo haya, maana yake nini? Akamwambia, Ndugu yako amekuja, na
baba yako amemchinja ndama aliyenona, kwa sababu amempata tena, yu mzima.
Akakasirika, akakataa kuingia ndani. Basi babaye alitoka nje, akamsihi.
Akamjibu baba yake, akasema, Tazama, mimi nimekutumikia miaka mingapi hii, wala
sijakosa amri yako wakati wo wote, lakini hujanipa mimi mwana-mbuzi, nifanye furaha
na rafiki zangu; lakini, alipokuja huyu
mwana wako aliyekula vitu vyako pamoja na makahaba, umemchinjia yeye ndama
aliyenona. Akamwambia, Mwanangu, wewe u pamoja nami sikuzote, na vyote nilivyo
navyo ni vyako. Tena, kufanya furaha na shangwe ilipasa, kwa kuwa huyu ndugu
yako alikuwa amekufa, naye amefufuka; alikuwa amepotea, naye ameonekana.”
Wako watu wana
wivu wa ajabu sana kwa sababu wanachukizwa na neema ya Mungu iliyojuu yako hata
wanaposikia umekosea wanatamani kama Mungu angekuua au kukutupilia mbali
jehanamu ya moto, hawataki kabisa kuona Mungu amekurehemu na anaendelea
kukubariki hii ni tabia mbaya sana na hawa ni mbweha waharibuo mzabimu, Bwana
ampe neema kila mmoja kuwa mbali na wivu wenye uchungu katika jina la Yesu.
6.
Unafiki.
Watu wengi sana ni wanafiki, unafiki ni tabia ya kuigiza pretending Mungu hapandezwi na unafiki, kujipendekeza na kutaka sifa ili hali moyo wako uko mbali naye au na mapenzi yake
Mathayo 15:7-9 “ Enyi wanafiki, ni vema alivyotabiri Isaya kwa habari zenu, akisema, Watu hawa huniheshimu kwa midomo; Ila mioyo yao iko mbali nami. Nao waniabudu bure, Wakifundisha mafundisho Yaliyo maagizo ya wanadamu.”
Unafiki ni dhambi inayooenakana kuwa ni ya kawaida sana kwa watu wengi wanaodai kuwa wanamcha Mungu, bila kujua kuwa Mungu anachukizwa na jambo hili na Mungu alimuadhibu vikali Anania na mkewe kwa sababu ya dhambi ya unafiki
Matendo ya mitume 5:1-10 “Lakini mtu mmoja jina lake Anania, pamoja na Safira
mkewe, aliuza mali,akazuia kwa siri sehemu ya thamani yake, mkewe naye akijua
haya, akaleta fungu moja akaliweka miguuni pa mitume. Petro akasema, Anania,
kwa nini Shetani amekujaza moyo wako kumwambia uongo Roho Mtakatifu, na kuzuia
kwa siri sehemu ya thamani ya kiwanja?Kilipokuwa kwako, hakikuwa mali yako? Na
kilipokuwa kimekwisha kuuzwa, thamani yake haikuwa katika uwezo wako? Ilikuwaje
hata ukaweka neno hili moyoni mwako? Hukumwambia uongo mwanadamu, bali Mungu.
Anania aliposikia maneno haya akaanguka, akafa. Hofu nyingi ikawapata watu wote
walioyasikia haya. Vijana wakaondoka, wakamtia katika sanda, wakamchukua nje,
wakamzika. Hata muda wa saa tatu baadaye mkewe akaingia, naye hana habari ya
hayo yaliyotokea. Petro akamjibu, Niambie, Mlikiuza kiwanja kwa thamani hiyo?
Akasema, Ndiyo, kwa thamani hiyo. Petro akamwambia, Imekuwaje hata mkapatana
kumjaribu Roho wa Bwana? Angalia, miguu yao waliomzika mumeo ipo mlangoni, nao
watakuchukua nje wewe nawe.Mara akaanguka miguuni pake akafa; wale vijana
wakaingia wakamkuta amekufa, wakamchukua nje, wakamzika pamoja na mumewe.”
Kwa hiyo utaweza
kuona dhambi zile tunazazidharau na kuzifikiri kuwa ni ndogo zina athari kubwa
sana katika kuharibu uhusiano wetu na Mungu na hivyo nazo Mungu anataka
tuzishughulikie
7.
Choyo:
Maandiko yanatahadharisha sana kuhusu choyo, watu wengi sana ni wachoyo, na watu wengi sana wanapenda kujimilikisha vitu vingi wakifikiri kuwa kwa kuwa na vitu watakuwa na uzima Yesu aktika mafundisho yake alionya kuhusu choyo anasema katika Luka 12:15 “Akawaambia, Angalieni, jilindeni na choyo, maana uzima wa mtu haumo katika wingi wa vitu vyake alivyo navyo.” Wako watu wana masanduku na nguo zimejaa kwenye begi zao masanduku mengine yamejaa mpaka zipu zimeachia au wanashundilia kwa miguu wakati wa kuyafunga lakini hawagawi Yesu akikolezea mungu mafundisho yake alionya kuwa sisi ni wapitaji tu katika ulimwengu huu na hivyio kujilimbikizia au mpango wa kujilimbikizia hautatufikisha kokote
Luka 12:16-20 “Akawaambia mithali, akisema, Shamba la mtu mmoja tajiri lilikuwa limezaa sana;akaanza kuwaza moyoni mwake, akisema, Nifanyeje? Maana sina pa kuyaweka akiba mavuno yangu. Akasema, Nitafanya hivi; nitazivunja ghala zangu, nijenge nyingine kubwa zaidi, na humo nitaweka nafaka yangu yote na vitu vyangu. Kisha, nitajiambia, Ee nafsi yangu, una vitu vyema vingi ulivyojiwekea akiba kwa miaka mingi; pumzika basi, ule, unywe, ufurahi. Lakini Mungu akamwambia, Mpumbavu wewe, usiku huu wa leo wanataka roho yako! Na vitu ulivyojiwekea tayari vitakuwa vya nani?”
choyo ni moja ya mbweha wadogo na waharibifu, kuna choyo za aina nyingi, moja ya choyo maarufu sana katika mapenzi na inayokera na kuharibu mahusiano ni pamoja na kunyimana tendo la ndoa aina hii ya choyo imeharibu mapenzi sana na watu wengi wameachana kwa sababu wako wanaotumia fursa ya tendo la ndoa kuwekea mgomo na kuesa nafsi za wengine aina hii ya choyo imekemewa vikali katika maandiko
1Wakoritho 7:1-5 “Basi kwa habari ya mambo
yale mliyoandika, ni heri mwanamume asimguse mwanamke. Lakini kwa sababu ya
zinaa kila mwanamume na awe na mke wake mwenyewe, na kila mwanamke na awe na
mume wake mwenyewe. Mume na ampe mkewe haki yake, na vivyo hivyo mke na ampe
mumewe haki yake. Mke hana amri juu ya mwili wake, bali mumewe; vivyo hivyo
mume hana amri juu ya mwili wake, bali mkewe. Msinyimane isipokuwa mmepatana
kwa muda, ili mpate faragha kwa kusali; mkajiane tena, Shetani asije
akawajaribu kwa kutokuwa na kiasi kwenu.” Neno la
Mungu linatahadharisha pia kuhusiana na jambo hili na ain azote za choyo
Bwana na ampe neema kila mmoja wetu kujilinda na choyo za aina mbalimbali ili
tuwe na mahusiano imara kwa Mungu na wanadamu
Athari za kutokukamata mbweha wadogo:-
-
Kunatokea kumzimisha Roho Mtakatifu Wathesalonike 5:19 “Msimzimishe
Roho;”
-
Tunashindwa kuzaa matunda ya Roho Wagalatia 5:19-23 “Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu,
ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka,
uzushi, husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo, katika hayo
nawaambia mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo
ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu. Lakini tunda la Roho ni upendo,
furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi; juu ya
mambo kama hayo hakuna sheria.”
-
Tunapoteza furaha Zaburi 51:11-12 “Usinitenge na uso wako, Wala roho yako mtakatifu
usiniondolee. Unirudishie furaha ya wokovu wako; Unitegemeze kwa roho ya wepesi.”
-
tunapoteza amani Wafilipi 4:7 “Na amani ya Mungu, ipitayo
akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.”
-
inaharibu uhusiano na Mungu 1Yohana 1:3 “hilo tuliloliona na kulisikia,
twawahubiri na ninyi; ili nanyi pia mpate kushirikiana nasi: na ushirika wetu
ni pamoja na Baba, na pamoja na Mwana wake Yesu Kristo.”
-
Tunapoteza ujasiri katika maombi Warumi 8:26 “Kadhalika Roho naye hutusaidia udhaifu
wetu, kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo, lakini Roho mwenyewe hutuombea
kwa kuugua kusikoweza kutamkwa.”
-
tunakuwa waoga 1Yohana 2:28 “Na sasa, watoto wadogo, kaeni ndani yake, ili kusudi,
atakapofunuliwa, mwe na ujasiri, wala msiaibike mbele zake katika kuja kwake.”
Dhambi hizo tunazofikiri kuwa sio
tatizo katika maisha yetu zinatuletea athari na kuharibu hali yetu ya kiroho na
wakati mwingine kuturudisha nyuma na kuharibu uhusiano wetu na Yesu, hatuna
budi kuhakikisha tunashughulikia maswala ya ndani tunayofafikiri kuwa ni madogo
madogo na kumbe yanaharibu sana uhusiano wetu na Mungu, ukiyajua hayo heri wewe
ukiyatenda.
Na mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!
Rev. Innocent Samuel Kamote
Mungu akubariki sana mchj kwa somo lililojaa baraka tele"Tukamatie mbweha,wale mbweha wadogo...."Ameni
JibuFutaAsante sana Mtumishi wa Mungu ubarikiwe sana sana
JibuFuta