1Nyakati 13:9-12 “Hata walipofika penye uga
wa Nakoni, Uza akaunyosha mkono wake alishike sanduku; kwa maana wale ng'ombe
walikunguwaa. Ndipo hasira ya Bwana ikawaka juu ya Uza, naye akampiga, kwa
sababu alilinyoshea sanduku mkono wake, hata akafa pale pale mbele za Mungu.
Naye Daudi akaona uchungu, kwa kuwa Bwana amemfurikia Uza; akapaita mahali pale
Peres-uza hata leo. Naye Daudi akamwogopa Mungu siku ile, akasema, NITAJILETEAJE
SANDUKU LA MUNGU KWANGU? ”
Utangulizi:
Moja ya mazingira ya
kusikitisha sana katika Historia ya maandiko ni Pamoja na historia ya kufa kwa
kuhani aliyeitwa Uza kifo chake kimeelezewa kwa kina katika 1Nyakati 13:1-14, Kifo cha kuhani huyu
kilikuwa ni matokeo ya uamuzi wa Daudi kulileta Sanduku la Agano la Mungu
kutoka mji ulioitwa Kiriath Yearimu kuja Yerusalem mwendao wa miles kama kumi
hivi (10). Sanduku lililetwa likiwa limebebwa kwenye mkokoteni uliokuwa
ukikokotwa na ngombe!
Walipokuwa wakisafiri
kuja Yerusalem ng’ombe wale walikunguwaa yaani walijikwaa na ikawa kama
wanataka kuangusha Sanduku la agano, ndipo Uza aliyekuwa karibu na sanduku la
agano la Mungu akanyoosha mkono wake kujaribu kulizuia ili lisianguke, Hasira
za Mungu zikawaka na Bwana akampiga Uza kwa sababu ile na akafa mbele za Bwana
pale pale, Jambo hili lilikuwa la kusikitisha sana na kila mmoja aliogopa Daudi
naye aliogopa akajawa na uchungu sana akaliacha sanduku la Agano katika nyumba
ya Obedi- Edom na akaanza kuwaza nitaliletaje Sanduku la Mungu kwangu! Ama linanijiaje
Sanduku la Bwana Mungu wangu!
2Samuel 6:6-11 “Hata walipofika kwa uga ya
Nakoni, Uza akalinyoshea mkono sanduku la Mungu, akalikamata kwa maana wale
ng'ombe walikunguwaa. Ndipo hasira ya Bwana ikawaka juu ya Uza; naye Mungu
akampiga huko kwa kosa lake; hata akafa pale pale penye sanduku la Mungu. Daudi
akaona uchungu kwa kuwa Bwana amemfurikia Uza; akapaita mahali pale Peres-uza
hata leo. Naye Daudi akamwogopa Bwana siku ile; akasema, LITANIJIAJE SANDUKU LA
BWANA? Basi Daudi hakutaka kulileta sanduku la Bwana kwake mjini mwa Daudi; ila
Daudi akalihamisha nyumbani kwa Obed-edomu, Mgiti. Sanduku la Bwana akalitia
katika nyumba ya Obed-edomu, Mgiti, muda wa miezi mitatu; naye Bwana
akambarikia Obed-edomu, na nyumba yake yote.”
Wanatheolojia wengi
sana hujiuliza sasa ni lipi kosa la Uza? Je Mungu hakuwa mwema kwa kumuua Uza
lipi lilikuwa jema kuliacha sanduku la agano lianguke? Au kuzuia lisianguke?
Kwanini Uza alikuwa akifanya jambo jema na Mungu akamkasirikia na kumuua?
Kwanini, bila shaka kuna mambo ya msingi ya kujifunza katika tukio hili, tutajifunza
somo hili kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-
·
Ufahamu kuhusu
Sanduku la Agano
·
Litanijiaje
Sanduku la Bwana Mungu wangu!
·
Mambo ya
kujifunza katika tukio hili.
Ufahamu kuhusu Sanduku la Agano.
Sanduku la agano,
ambalo pia huitwa Sanduku la ushuhuda au sanduku la Mungu, kilikuwa ni moja ya
chombo muhimu sana na kitakatifu mno kwa wana wa Israel, Miongoni mwa Thamani
zlizokuwa zikikaa katika hema la kukutania au hekaluni Chombo hiki kilijengwa
wa mti wa mshita (Acacia) na kufunikwa
kawa dhahabu kutokana na maelekezo ya
Mungu kwa Musa, Ndani yake kulihifadhiwa mbao mbili za mawe zenye amri kumi
zilizoandikwa na Mungu, mwenyewe na ile fimbo ya Haruni iliyochipuka pamoja na
kopo la dhahabu lenye mana iliyohifadhiwa, Chombo hiki juu kilikuwa na Makerubi
wawili walioinamisha mbawa zao na kufunika kiti cha Rehema cha Mungu, na ni
kutoka Hapo ndio mahali Mungu alikuwaakizungumza na Musa ona:-
Kutoka 25:10-22 “Nao na wafanye sanduku la
mti wa mshita; urefu wake na uwe dhiraa mbili na nusu, na upana wake dhiraa
moja na nusu, na kwenda juu kwake dhiraa moja na nusu. Nawe ulifunike kwa
dhahabu safi, ulifunike ndani na nje, nawe tia na ukingo wa dhahabu kulizunguka
pande zote. Nawe subu vikuku vinne vya dhahabu kwa ajili yake, na kuvitia
katika miguu yake minne; vikuku viwili upande mmoja, na vikuku viwili upande
wake wa pili. Nawe fanya miti mirefu ya mshita na kuifunika dhahabu. Nawe tia
hiyo miti katika vile vikuku vilivyo katika pande mbili za sanduku ili
kulichukua hilo sanduku. Hiyo miti itakaa katika vile vikuku vya sanduku;
haitaondolewa. Kisha tia ndani ya sanduku huo ushuhuda nitakaokupa. Nawe fanya
kiti cha rehema cha dhahabu safi; urefu wake utakuwa dhiraa mbili na nusu, na
upana wake dhiraa moja na nusu. Nawe fanya makerubi mawili ya dhahabu; uyafanye
ya kazi ya kufua, katika hiyo miisho ya kiti cha rehema, huku na huku. Weka
kerubi moja mwisho mmoja, na kerubi la pili mwisho wa pili; fanya hayo makerubi
ya kitu kimoja na kiti cha rehema, mwisho huku na mwisho huku. Na hayo makerubi
yatainua mabawa yao juu, na kukifunika hicho kiti cha rehema kwa mabawa yao, na
nyuso zao zitaelekeana hili na hili; nyuso za hayo makerubi zitaelekea kiti cha
rehema. Weka kiti cha rehema juu ya hilo sanduku, kisha utie huo ushuhuda
nitakaokupa ndani ya sanduku. Nami nitaonana nawe hapo, na kuzungumza nawe pale
nilipo juu ya kiti cha rehema, katikati ya hayo makerubi mawili yaliyo juu ya
sanduku la ushuhuda, katika mambo yote nitakayokuagiza kwa ajili ya wana wa
Israeli.”
Kimsingi kuna mambo
mengi sana tunaweza kujifunza kutoka katika chombo hiki kitakatifu na cha
thamani mno,mbao mbili za mawe zilizoandikwa Amri kumi zinatufundisha wazi kuwa
Mungu ni Mungu wa Utaratibu, Fimbo ya haruni iliyochipuka inatufundisha kuwa
Mungu anaheshimu itifaki uongozi aliouchagua, Kopo la dhahabu na ile mana
iliyohifadhiwa inatufundhisha kuwa Mungu anashughulika na mahitaji yetu kila
siku, kwa ujumla kuna mambo mengi ya kujifunza kutoka katika chombo hiki lakini
kwa leo itoshe tu kusema maana kuu hasa ya chombo hiki ilikuwa ni uwakilishi
unaoonekana wa uwepo wa Mungu asiyeonekana, Chombo kiliwakilisha “UWEPO WA MUNGU” chombo hiki kilikuwa na
uwezo mkubwa sana wa kusababisha Baraka na madhara, Baraka kama kitapewa
heshima inayostahili na madhara endapo ukiukwaji wa Heshima yake utafanyika!
2Samuel 6:10-12 “Basi Daudi hakutaka
kulileta sanduku la Bwana kwake mjini mwa Daudi; ila Daudi akalihamisha
nyumbani kwa Obed-edomu, Mgiti. Sanduku la Bwana akalitia katika nyumba ya
Obed-edomu, Mgiti, muda wa miezi mitatu; naye Bwana akambarikia Obed-edomu, na
nyumba yake yote. Kisha mfalme Daudi akaambiwa ya kwamba, Bwana ameibarikia
nyumba ya Obed-edomu, na vitu vyote alivyo navyo kwa ajili ya sanduku la Mungu.
Daudi akaenda, akalileta sanduku la Mungu, toka nyumba ya Obed-edomu mpaka mji
wa Daudi, kwa shangwe.”
Kutokana na tukio la
kifo cha kuhani Uza watu waliingiwa na Hofu na Daudi pia alimuogopa Mungu siku
ile lakini aliingiwa na uchungu sio wa kuchukizwa na Mungu lakini kujutia na
kujiuliza imekuwaje Mungu akafanya vile! Hili lilimpa kujiuliza swali kubwa
kuwa litanijiaje Sanduku la Bwana Mungu wangu!
Litanijiaje Sanduku la Bwana Mungu wangu!
Swala kubwa hapa ni
namnagani sanduku la Mungu litafika Yerusalem, kwani walipokuwa katika kulileta
Ndio kuhani Uza akauawa na Mungu kwa kulinyooshea mkono Sanduku, na Daudi
aliogopa sasa kulileta na alipoliacha kwa Obed-
Edom mtu huyu ndani ya miezi mitatu tu alibarikiwa sana kwa nini hasa
sanduku la agano lilishindwa kufika Yerusalem katika wakati uliokusudiwa na
kusababisha madhara njiani?
Tukio linatukumbusha
umuhimu wa kufuata maagizio ya Mungu na kufanya sawasawa na Mapenzi yake, Mungu
alikuwa ametoa maagizo yaliyokuwa wazi namna na jinsi sanduku la agano
linavyopaswa kubebwa katika Torati
Kutoka 25:14-15 “Nawe tia hiyo miti katika
vile vikuku vilivyo katika pande mbili za sanduku ili kulichukua hilo sanduku.
Hiyo miti itakaa katika vile vikuku vya sanduku; haitaondolewa.”
Katika maelekezo ya
ujenzi wake sanduku lilipaswa kuwa na vikuku ambavyo vingechomekwa miti ya
dhahabu kwa kusudi la kuichomeka na kulibeba sanduku la agano mabegani mwa
makuhani maalumu walioteuliwa kufanya kazi hiyo wengi wakiwa ni walawi na hususani kabila la walawi wa wakohathi
Hesabu 7:9 “Lakini hakuwapa wana wa
Kohathi; maana, utumishi wa vile vitu vitakatifu ulikuwa ni wao; nao
wakavichukua mabegani mwao.”
Daudi pamoja na kuhani
Uza walisahahu kufuata maelekezo ya Mungu, na Mungu akamshughulikia Uza mara
moja kwa kifo, jambo hili lilimfanya Daudi kumuogopa sana Mungu, Mungu yuko
Sirius/Makini na maagizo yake, yeye alitaka Sanduku la agano liheshimiwe kwa
kiwango kikubwa sana chochote ambacho Mungu amakitangaza kuwa ni kitakatifu
hakipaswi kuchukuliwa kimzaha mzaha, Ulimwengu wa kiroho uwe wa giza au wa nuru
unazingatia sana masharti wakati wote kama ukivunja mashari au miiko au
kutokufuata maelekezo huwezi kutoboa! Ona madhara;-
1Samuel 6:19 “ Basi Bwana aliwapiga baadhi ya watu wa Beth-shemeshi, kwa
sababu wamechungulia ndani ya hilo sanduku la Bwana, wapata watu sabini, na
watu hamsini elfu; nao watu wakalalamika, kwa kuwa Bwana amewapiga watu kwa
uuaji mkuu.”
Daudi alikuwa
amejifunza kuwa ubebwaji wa sanduku la Mungu mwanzoni haukuwa umefuata
maelekezo yake na sasa Daudi akawa amejifunza kupitia uchungu alioupata kwa
kifo cha Uza ilikuwa ni lazima sanduku la Agano libebe Mabegani tena na
makuhani kama Bwana alivyoagiza, wao walibeba kama wafilisti wasiomjua Mungu
walivyolirudisha Sanduku la Agano
1Nyakati 15:2 “Ndipo Daudi akasema, Haimpasi mtu awaye yote kulichukua
sanduku la Mungu, isipokuwa Walawi peke yao; kwa kuwa hao ndio aliowachagua
Bwana, ili walichukue sanduku la Mungu, na kumtumikia daima. 15 Na wana wa
Walawi wakalichukua sanduku la Mungu mabegani mwao kwa miti yake, kama vile
Musa alivyoamuru, sawasawa na neno la Bwana.”
Walipofuata maelekezo
ya Mungu kwa uaminifu ndipo walipokuwa na uwezo wa kulibeba sabduku la Bwana
bila kusababisha madhara na safari yao
ikawa salama tofauti na mwenendo wao wa Mwanzo, watu wengi sana hawafanikiwi
kwa sababu hawafuati maelekezo, huwezi kubeba uwepo wa Mungu kama Mungu
hajakuchagua uubebe, Kama hujali kuhusu maelekezo na kufuata utaratibu hakuna
mafanikio mahali popote ambapo watu hawafuati utaratibu Mungu ni Mungu wa
utaratibu, Sanduku la agano litakujiaje ni kwa kufuata maelekezo, mafanikio
katika maisha, kujibiwa maombi na kufurahia Baraka na uwepo wa Mungu vitatujia
katika maisha yetu endapo tutakuwa makini kufuata maelekezo na kuyatii na
kuacha kutumaini hekima yetu na ujuzi wetu wa kibinadamu.
Mambo ya kujifunza katika tukio hili.
Mungu ni mwema nani mwenye
upendo mwingi sana na rehema zake ni kubwa kwa wanadamu lakini linapokuja swala
la kutokufuata Maelekezo yake Mungu anachukizwa sana na yuko tayari hata
kuahirisha mpango wake kwa mtu asiyefuata maelekezo, Endapo mtu anataka
kufanikiwa katika njia za Mungu basi ni vema akafuata maelekezo.
·
UTII: 1Samuel
15:22-23 “Naye Samweli akasema, je! Bwana huzipenda
sadaka za kuteketezwa na dhabihu Sawasawa na kuitii sauti ya Bwana? Angalia,
kutii ni bora kuliko dhabihu, Na kusikia kuliko mafuta ya beberu. Kwani kuasi
ni kama dhambi ya uchawi, Na ukaidi ni kama ukafiri na vinyago; Kwa kuwa
umelikataa neno la Bwana, Yeye naye amekukataa wewe usiwe mfalme.”
Lazima wakati wote watu wajifunze, kukubali kujifunza sio
dhambi, Yesu alikubali kujifunza Kabla ya kuwa Mwalimu mzuri na kiongozi mzuri
alichukua Muda kukaa na walimu na aliuliza maswali na hivyo tunamuona yeye
baadaye anakuja kuwa kiongozi na mwalimu mwema na bora zaidi Duniani
1Wakoritho 8:2 “Mtu akidhani ya kuwa anajua neno, hajui neno lo lote
bado, kama impasavyo kujua.”
Daudi mwanzoni alikuwa hajui na alipokubali kujifunza
akafanikiwa wako watu wanaona noma kujifunza wanafikiri kuwa watakuwa duni sana
wakijifunza na kuuliza wanataka waonekane kuwa wanajua, Mungu hamfurahii mtu awayeyote
anayekataa maarifa
Hosea 4:6 “Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa; kwa kuwa
wewe umeyakataa maarifa, mimi nami nitakukataa wewe, usiwe kuhani kwangu mimi;
kwa kuwa umeisahau sheria ya Mungu wako, mimi nami nitawasahau watoto wako.”
·
KUMTEGEMEA
MUNGU SIO AKILI: Mungu hapandezwi na
mtu anayezitegemea akili zake mwenyewe, kutegemea akili zako mwenyewe ni
kiburi, Kanuni ya Mungu inatutaka kuyatafuta mapenzi yake na kuyafuata
tunapoanza kujifanya tuna akili na tunazitumainia akili zetu na hekima zetu
basi madhara yake ni pamoja na kuharibikiwa Lazima tumtegemee Mungu katika njia
zetu zote
Mitahli 3:5-8 “Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote, Wala usizitegemee
akili zako mwenyewe; Katika njia zako zote mkiri yeye, Naye atayanyosha mapito
yako.Usiwe mwenye hekima machoni pako; Mche Bwana, ukajiepushe na uovu. Itakuwa
afya mwilini pako, Na mafuta mifupani mwako.”
Maandiko yanatuonya sana tuache kujiamini kupita kawaida na
kufikiri kuwa yale tunayoyaona sisi ni sahihi wakati wote kumbe wakati mwingine
yako kinyume na mapenzi ya Mungu, kujifikiri kuwa sisis ni smart mno tuko
vizuri kichwani kunatupelekea kuumbuka kwa sababu tunaweza kudhani njie yetu ni
sahihi kumbe njia ile ni njia ya mauti
Mithali 14:12 “Iko njia ionekanayo kuwa sawa machoni pa mtu, Lakini
mwisho wake ni njia za mauti.”
Ilionekana ni sahihi kwa Uza kulinyooshea mkono Sanduku la
agano ndio kwani ng’ombe walikuwa wamejikwaa na Sanduku lingeanguka isingekuwa
vema machoni pa Uza ilikuwa ni sahihi lakini kumbe tukio hilo lingeleta mauti,
Jambo linaweza kuonekana sahihi machoni pako lakini likawa sio sahihi machoni
pa Mungu, kama mtu anataka kuufurahia uwepo wa Mungu, amani yake na uvumilivu
wake hatuna budi klujifunza kutoka katika neno la Mungu na kulitendea kazi
katika maisha yetu.
Na. Rev. Innocent
Samuel Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye
Hekima!
Ubarikiwe sana mtumishi wa Mungu aliye hai
JibuFuta