Jumapili, 8 Mei 2022

Mfalme juu ya Punda


Mathayo 21:1-5Hata walipokaribia Yerusalemu, na kufika Bethfage, katika mlima wa Mizeituni, ndipo Yesu alipotuma wanafunzi wawili akiwaambia, Enendeni mpaka kijiji kile kinachowakabili, na mara mtaona punda amefungwa, na mwana-punda pamoja naye; wafungueni mniletee. Na kama mtu akiwaambia neno, semeni, Bwana anawahitaji; na mara huyo atawapeleka. Haya yote yamekuwa, ili litimie neno lililonenwa na nabii, akisema, Mwambieni binti Sayuni Tazama, mfalme wako anakuja kwako, Mpole, naye amepanda punda, Na mwana-punda, mtoto wa punda.”


Utangulizi:

Ni muhimu kufahamu kwamba tukio la Yesu Kristo kupokelewa kwa shangwe jijini Yerusalem, lilikuwa ni tukio la kipekee sana lililofanywa na watu, sawa kabisa na namna watu wanavyompokea mfalme, tukio hili halikuwa tukio la bahati mbaya kwani vilevile lilikuwa ni sehemu ya kutimizwa kwa maandiko ya kinabii kuhusu kuja kwa mfalme wa kipekee ambaye angejibu mahitaji yote ya wanadamu Nabii Zekaria alilitabiri tukio hili miaka 400 kabla ya kuzaliwa kwa Yesu ona;-

Zecharia 9:9Furahi sana, Ee binti Sayuni; Piga kelele, Ee binti Yerusalemu; Tazama, mfalme wako anakuja kwako; Ni mwenye haki, naye ana wokovu; Ni mnyenyekevu, amepanda punda, Naam, mwana-punda, mtoto wa punda.”

Swali moja kubwa ambalo wanafunzi wengi wa maandiko hupenda kujiuliza ni kwamba, iko wazi kuwa Yesu alipokelewa Yerusalem kwa shangwe kubwa sana watu walimfurahia kwa matawi ya mitende na hata kutandaza nguo zao njiani, lilikuwa ni tukio la kipekee sana ambalo hakuna mfalme amewahi kufanyiwa,Mungu roho Mtakatifu aliinua mioyo ya watu na wakasangilia kwa nguvu sana kuingia kwa Maishi pale Sayuni, lakini swali kubwa kwanini mfalme huyu awe amepanda punda?  Hili ndio swali kubwa na la Muhimu kwa kila mmoja wetu kujiuliza na kutafuta majibu.

Wafalme huja na Majibu ya mahitaji ya watu!

Moja ya Kazi kubwa sana ya wafalme wa zamani na labda huenda hata sasa ilikuwa ni pamoja na kutawala mfalme alipaswa kuwa na majibu ya aina yoyote dhidi ya mahitaji ya watu wake, wafalme walitakiwa kutatua changamoto zilizowakabili watu hata kuamua kesi za aina mbalimbali mfano;- 

1Wafalme 3:16-28 “Ndipo wanawake wawili, makahaba, walimwendea mfalme, wakasimama mbele yake. Na mwanamke mmoja akasema, Ee bwana wangu, mimi na mwanamke huyu tunakaa katika nyumba moja; nami nalizaa nilipokuwa pamoja naye nyumbani. Kisha, siku ya tatu baada ya kuzaa kwangu, ikawa mwanamke huyu naye akazaa; na sisi tulikuwa pamoja; hapakuwa na mtu mwingine pamoja nasi nyumbani, isipokuwa sisi wawili tu. Na mtoto wa mwanamke huyu akafa usiku, maana alimlalia. Akaondoka kati ya usiku, akamwondoa mtoto wangu ubavuni pangu, mimi mjakazi wako nilipokuwa usingizini, akamweka kifuani pake, na mtoto wake mwenyewe, aliyekuwa amekufa, akamweka kifuani pangu. Nilipoondoka asubuhi nimnyonyeshe mtoto wangu, kumbe? Amekufa. Hata asubuhi nilipomtazama sana, kumbe! Siye mtoto wangu niliyemzaa. Ndipo yule mwanamke wa pili akasema, Sivyo hivyo; bali mtoto wangu ndiye aliye hai, na mtoto wako ndiye aliyekufa. Na mwenzake akasema, Sivyo hivyo; bali mtoto wako ndiye aliyekufa, na mtoto wangu ndiye aliye hai. Ndivyo walivyosema mbele ya mfalme.  Ndipo mfalme akasema, Huyu anasema, Mtoto wangu yu hai, na mtoto wako amekufa. Na huyu anasema, Sivyo hivyo; bali mtoto aliyekufa ni wako, na mtoto aliye hai ni wangu. Mfalme akasema, Nileteeni upanga. Wakaleta upanga mbele ya mfalme. Mfalme akasema, Mkate mtoto aliye hai vipande viwili, kampe huyu nusu, na huyu nusu. Ndipo mwanamke yule, ambaye mtoto aliye hai ni wake, akamwambia mfalme kwa maana moyoni mwake alimwonea mtoto wake huruma, akasema, Ee bwana wangu, mpe huyu mtoto aliye hai, wala usimwue kamwe. Lakini yule mwingine akasema, Asiwe wangu wala wako; na akatwe. Ndipo mfalme akajibu, akasema, Mpe huyu wa kwanza mtoto aliye hai, maana yeye ndiye mama yake. Na Israeli wote wakapata habari za hukumu ile aliyoihukumu mfalme wakamwogopa mfalme; maana waliona ya kuwa hekima ya Mungu ilikuwa ndani yake, ili afanye hukumu.”

Wafalme walitakiwa kujibu hoja zozote ngumu za watu wao waliowatembelea kuhitaji msaada katika maeneo mbalimbali ya maisha yao 1Wafalme 10:1 “Na malkia wa Sheba aliposikia habari za Sulemani juu ya jina la Bwana, alikuja ili amjaribu kwa maswali ya fumbo.” Biblia ya kiingereza inatumia maneno “she came to test her with HARD questions       Hata hivyo Mfalme Suleimani pia aliweza kutoa majibu ya maswali yote aliyouliza malikia wa Sheba. Hata hivyo maandiko pia yanatueleza kuwa kuna wakati ambapo wafalme walikosa majibu na uwezo wa kutatua changamoto kadhaa na hivyo walilia, na kufunga na kuvaa magunia au kurarua mavazi yao. Angalia kwa mfano:-

2Wafalme 6:25-30 “Njaa ikawa kuu huko Samaria; na tazama, wakauhusuru, hata kichwa cha punda kikapata kuuzwa kwa vipande themanini vya fedha, na kibaba cha mavi ya njiwa kwa vipande vitano vya fedha. Ikawa mfalme wa Israeli alipokuwa akipita ukutani, mwanamke mmoja akamwita akisema, Unisaidie, bwana wangu, mfalme. Akasema, Bwana asipokusaidia, nikusaidieje mimi? Ya sakafuni, au ya shinikizoni? Mfalme akamwambia, Una nini? Akajibu, Mwanamke huyu aliniambia, Mtoe mtoto wako, tumle leo, na mtoto wangu tutamla kesho. Basi, tukamtokosa mtoto wangu, tukamla; nikamwambia siku ya pili, Mtoe mtoto wako, tumle; naye amemficha mtoto wake. Ikawa, mfalme alipoyasikia maneno ya huyo mwanamke, aliyararua mavazi yake; (naye alikuwa akipita juu ya ukuta;) na watu wakaona, na tazama, alikuwa amevaa magunia ndani mwilini mwake.”

Unaona kwa msingi huo Mfalme alikuwa na kazi ngumu ya kutatua changamoto za maisha ya watu,  ukiacha swala la kutatua changamoto ya maisha ya watu, mfalme pia alitakiwa kuwa mtu wa vita na mwenye uwezo wa kutwatetea watu wake dhidi ya adui zao kwa kupigana kwa silaha na kwa uwezo wa kujihami, wafalme walipaswa kuwa watu wa vita, Heshima ya mfalme ilikuwa kupitia uwezo wake wa kuamua mambo na kuwapigania watu wakena kuwashindia dhidi ya adui zao, mfano

 1Samuel 17:1- 11. Wakati huo Wafilisti walikusanya majeshi yao kwa vita, nao wakakusanyika huko Soko, ulio mji wa Yuda, wakatua kati ya Soko na Azeka, katika Efes-damimu. Naye Sauli na watu wa Israeli wakakusanyika, wakatua katika bonde la Ela, nao wakapanga vita juu ya hao Wafilisti. Wafilisti wakasimama juu ya mlima upande huu, na Waisraeli wakasimama juu ya mlima upande huu, napo palikuwa na hilo bonde katikati. Ndipo akatoka shujaa katika kambi ya Wafilisti, aliyeitwa Goliathi, wa Gathi, ambaye urefu wake ulikuwa mikono sita na shibiri moja. Alikuwa na chapeo ya shaba kichwani, tena amevaa darii ya shaba; na uzani wake ile darii ya shaba ulikuwa shekeli elfu tano za shaba. Tena amevaa mabamba ya shaba miguuni mwake, naye alikuwa na mkuki wa shaba kati ya mabega; yake. Na mti wa fumo lake ulikuwa kama mti wa mfumaji; na kichwa cha mkuki wake kilikuwa shekeli mia sita za chuma uzito wake; na mtu aliyemchukulia ngao yake akamtangulia. Naye akasimama, akawapigia kelele majeshi ya Israeli akawaambia, Mbona mmetoka kupanga vita? Je! Mimi si Mfilisti, na ninyi si watumishi wa Sauli? Jichagulieni mtu, akanishukie mimi. Kama akiweza kupigana nami na kuniua, sisi tutakuwa watumwa wenu; nami nikimshinda yeye na kumwua, ninyi mtakuwa watumwa wetu, na kututumikia. Yule Mfilisti akasema, Nayatukana leo majeshi ya Israeli; nipeni mtu tupigane. Basi Sauli na Israeli wote waliposikia maneno hayo ya Mfilisti, wakafadhaika na kuogopa sana.”

Mfalme juu ya Punda !

Sasa moja ya tukio la kushangaza ni kuwa pamoja na kuwa wafalme walikuwa ni watu waliotakiwa kujibu hoja na mahitaji ya watu ya aimna mbalimbali na kuwashindia watu vita dhidi ya adui zao, ni muhimu kufahamu kuwa wafalme walipotaka kuonyesha nguvu zao na ukuu wao wakati wote walitumia farasi katika kusafiri kwao, Farasi ilikuwa ni alama ya vita na ufahari na utajiri, kwa hiyo kila mfalme aliyekuwa anataka kuonyesha ufahari wake alitumia farasi, farasi ni mnyama anayeonyesha uhodari, wakati punda ni mnyama anayeonyesha huduma,  kama watu walikuwa wakijivuna walijivunia magari yao ya farasi kwani hayo ndio yalikuwa yakidhihirisha nguvu na uwezo wao

Zaburi 20:1-9 “Bwana akujibu siku ya dhiki, Jina la Mungu wa Yakobo likuinue. Akupelekee msaada toka patakatifu pake, Na kukutegemeza toka Sayuni. Azikumbuke sadaka zako zote, Na kuzitakabali dhabihu zako. Akujalie kwa kadiri ya haja ya moyo wako, Na kuyatimiza mashauri yako yote. Na tuushangilie wokovu wako, Kwa jina la Mungu wetu tuzitweke bendera zetu. Bwana akutimizie matakwa yako yote. Sasa najua kuwa Bwana amwokoa masihi wake;Atamjibu kutoka mbingu zake takatifu.Hawa wanataja magari na hawa farasi, Bali sisi tutalitaja jina la Bwana, Mungu wetu. Wao wameinama na kuanguka, Bali sisi tumeinuka na kusimama. Bwana, umwokoe mfalme, Utuitikie siku tuitayo.”

Watu wanachohitaji ni kuokolewa kutoka katika changamoto zinazowakabili, haijalishi mfalme anakuja namna gani, anaweza akaja na magari ya farasi lakini akawa hana majibu ya kutosheleza mioyo ya watu wake Zekaria alitabiri kuwa anakuja mfalme mnyenyekevu, mpole hana majivuno wala majigambo wala hana nia ya kutafuta kiki au ufahari yeye anakuja na wokovu anakuja na kifurushi kitakachotuletea amani ni mfalme wa tofauti mwenye uwezo wa kutatua changamoto za watu kwa kiwango kikubwa sana yeye anatabiriwa kuwa angekuja akiwa amepanda punda na mwana punda mtoto wa punda, hii ilikuwa ni ishara madhubuti ya kumtambua mfalme huyo mwenye nguvu zote lakini mnyenyekevu!

 Zakaria 9:9-10 “Furahi sana, Ee binti Sayuni; Piga kelele, Ee binti Yerusalemu; Tazama, mfalme wako anakuja kwako; Ni mwenye haki, naye ana wokovu; Ni mnyenyekevu, amepanda punda, Naam, mwana-punda, mtoto wa punda. Na gari la vita nitaliondoa liwe mbali na Efraimu, na farasi awe mbali na Yerusalemu, na upinde wa vita utaondolewa mbali; naye atawahubiri mataifa yote habari za amani; na mamlaka yake yatakuwa toka bahari hata bahari, na toka Mto hata miisho ya dunia.”

Maandiko yanaonyesha kuwa mfalme huyu

o   Atakomesha vita

o   Silaha za vita kama upinde utaondolewa mbali

o   Hatakuja na majeshi

Yeye atatangaza amani kwa mataifa yote na ufalme wake utakuwa ni wa dunia nzima, Luka 2:14 “Atukuzwe Mungu juu mbinguni, Na duniani iwe amani kwa watu aliowaridhia.” Mfalme atakayeingia Yerusalem, yaani katika mlima wa Sayuni akiwa juu ya Punda, ni simple but powerful ni mnenyekevu na mpole lakini ana majibu yote yeye atatoa suluhu ya mahitaji yetu yote na hivyo tunachopaswa kusema ni Hosana mwana wa Daudi, mfalme mwenye majibu ya wokovu wako haji na vifaru, haji na ufahari wowote anakuja na mwana punda, humble but very powerful, huyu ndiye mfalme aliyetabiriwa na Zekaria na Mathayo anatudhihirishia kuwa Yesu ndiye mfalme huyu ambaye amekuja kulitimiza andiko, ana hekima kuliko suleimani na ana nguvu kuliko Daudi, yeye atatupigania na hakuna kinachoweza kusimama mbele yake yeye ndiye mtetezi wa adui zetu na mkombozi wetu dhidi ya unyonge si mwingine ni Yesu !

Rev. Innocent Kamote

Mkuu wa wajenzi Mwenye Hekima!

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni