Mwanzo 26:12-22 “Isaka akapanda mbegu
katika nchi ile, akapata mwaka ule vipimo mia kwa kimoja, BWANA akambariki. Na
mtu huyu akawa mkuu, akazidi kusitawi, hata akawa mkuu sana. Akawa na mali ya
kondoo, na mali ya ng'ombe, na watumwa wengi. Hao Wafilisti wakamhusudu. Na
vile visima vyote walivyochimba watumwa wa baba yake, siku za Ibrahimu babaye,
Wafilisti walikuwa wamevifukia, wakavijaza kifusi. Abimeleki akamwambia Isaka,
Utoke kwetu, maana wewe una nguvu sana kuliko sisi. Basi Isaka akatoka huko
akapiga kambi katika bonde la Gerari, akakaa huko. Isaka akarudi akavichimbua vile visima vya
maji walivyovichimba siku za Ibrahimu babaye; maana wale Wafilisti walikuwa
wamevifukia baada ya kufa kwake Ibrahimu; naye akaviita majina kufuata majina
alivyoviita babaye. Watumwa wa Isaka wakachimba katika lile bonde, wakapata
kisima cha maji yanayobubujika. Wachungaji wa Gerari wakagombana na wachungaji
wa Isaka wakisema, Maji haya ni yetu. Ndipo akakiita jina la kile kisima Eseki,
kwa sababu waligombana naye. Wakachimba kisima kingine, wakagombania na hicho
tena. Akakiita jina lake Sitna. Akaondoka huko akachimba kisima kingine, wala
hicho hawakukigombania. Akakiita jina lake Rehobothi, akasema, Kwa kuwa sasa
BWANA ametufanyia nafasi, nasi tutazidi katika nchi.”
Utangulizi:
Ni muhimu kufahamu kuwa katika
ulimwengu tulionao ni watu wachache sana tena wenye ukomavu wa kifikra
wanaoweza kustahimili pale mtu mwingine anapobarikiwa, na wako wengi wenye
kushangaza katika upande wa pili ambao hawawezi kuvumilia pale Mungu
anapokubariki, Baraka za Mungu kwetu zina tabia ya kuvutia umati mkubwa sana wa
watu, lakini pia zinauwezo wa kuvutia maadui kwa upande mwingine, kwa msingi
huo kila mmoja anapokuwa amebarikiwa na mbaraka wa Mungu na mbaraka huo
ukamtajirisha ni lazima aelewe kuwa atakuwa na maadui na hawa ni wale ambao
hawawezi kuvumilia Baraka zako na hivyo wakati mwingine tunaweza kujikuta
tunavuna Baraka lakini tunapata na changamoto za Baraka hizo, kimsingi Mungu katika
mapenzi yake kamili alikusudia kuwa Baraka zake zisilete huzuni iwayo yote ona Mithali 10:22 “Baraka
ya Bwana hutajirisha, Wala hachanganyi huzuni nayo.” Lakini kwa sababu tuko duniani wakati
mwingine Baraka hizo zitaambatana na huzuni au udhia kutokana na watu
wanaotuzunguka kushindwa kustahimili kishindo cha Baraka za Mungu kwetu, ni
muhimu kufahamu kuwa watu wanaweza kushindwa kustahimili Baraka za Mungu kwetu
katika mazingira yafuatayo-
1. Wakati mwingine Mungu anapotutakabali.
Watu wengine
wanaweza kushindwa kuvumilia Baraka zetu tunapotakabaliwa na Mungu,
kutakabaliwa na Mungu katika lugha ya kiingereza ni “When God looked us with favor” ni tukio la kukubalika kiibada Mungu
kukubali au kusikiliza maombi yetu na dua zetu, wengine wanachukizwa kwa nini
huyu amesikilizwa na Mungu, kwanini huyu ameolewa mie bado, kwanini huyu
amejenga mie bado, kwa nini huyu ana mashamba mimi bado, kwa nini huyu ana
watoto mimi bado wako watu wanashindwa kuvumilia wanapoona Mungu amekutakabali,
wanaweza kuona wivu, wanaweza kukukasirikia na wanaweza hata kukuua.
Mwanzo 4:1-8 “Adamu
akamjua Hawa mkewe; naye akapata mimba, akamzaa Kaini, akasema, Nimepata mtoto
mwanamume kwa BWANA. Akaongeza akamzaa
ndugu yake, Habili. Habili alikuwa mchunga kondoo, na Kaini alikuwa mkulima
ardhi. Ikawa hatimaye Kaini akaleta mazao ya ardhi, sadaka kwa BWANA. Habili
naye akaleta wazao wa kwanza wa wanyama wake na sehemu zilizonona za wanyama.
BWANA akamtakabali Habili na sadaka yake; bali Kaini hakumtakabali, wala sadaka
yake. Kaini akaghadhibika sana, uso wake ukakunjamana. BWANA akamwambia Kaini,
Kwa nini una ghadhabu? Na kwa nini uso wako umekunjamana? Kama ukitenda vyema,
hutapata kibali? Usipotenda vyema dhambi iko, inakuotea mlangoni, nayo
inakutamani wewe, walakini yapasa uishinde. Kaini akamwambia Habili nduguye,
[Twende uwandani] Ikawa walipokuwapo uwandani, Kaini akamwinukia Habili
nduguye,akamwua.”
Habili alipoteza
maisha kwa sababu ya kutakabaliwa na Mungu, kaini alijawa na wivu wenye uchungu
na kumkusudia nduguye mabaya, unaweza kukusudiwa mabaya, unaweza kupigwa vita
kwa sababu una huduma nzuri, unaweza kupigwa vita kwa sababu unahubiri vizuri,
kwa sababu unaimba vizuri, kwa sababu una sura nzuri, kwa sababu uko vizuri
katika kila eneo kwa nini inafanyika hivyo ni kwa sababu wako watu hawawezi
kuvumilia Baraka zako!
2.
Wakati
mwingine tunapopata kibali kuliko wao.
Watu wengine
wanaweza kushindwa kuvumilia Baraka zako kwa sababu tu unakibali, unakubalika
kuliko wao, kwa sababu ya wao kujiona duni “inferiority
complex” kutokana na kukubalika kwako wataanza kukuchukia na kukuonea wivu
na hata kukupiga vita kwanini kwa sababu hawawezi kuvumilia Baraka zako ona
Mwanzo 37:3-5 “Basi
Israeli akampenda Yusufu kuliko wanawe wote, maana ni mwana wa uzee wake,
akamfanyia kanzu ndefu. Ndugu zake wakaona ya kuwa baba yao anampenda kuliko
ndugu zake wote, wakamchukia, wala hawakuweza kusema naye kwa amani. Yusufu
akaota ndoto, akawapa ndugu zake habari, nao wakazidi kumchukia;”
Ndugu zake
Yusufu walipoona kuwa Yusufu anapendwa zaidikuliko wao, na baba yake
amemnunulia nguo nzuri anapiga pamba kali kuliko wao, wanabadilishana mawazo na mzee Yakobo, Yusufu
anatoa taarifa kwa baba yake kuhusu kila kitu nyumbani jamaa wakahisi
anapendelewa walishindwa kuvumilia Baraka hii ya kibali na wakazidi kumchukia
sana, wako watu wanaweza kuchukizwa
nawe kwa wazi au mioyoni mwao na wakawa wanaumia tu kwa sababu wewe unapendwa,
kwa sababu wewe una kibali, una kibali kazini, unakibali kwa bosi, una kibali
kikubwa na ni Mungu amesababisha kibali hicho na wanaokuzunguka wakashindwa
kuvumilia Baraka zako na wanaanza kuchukizwa nawe na kukuonea wivu kwa sababu
hawawezi kuvumilia Baraka zako!
3.
Wakati
mwingine tunapopewa sifa zaidi kuliko wao
Watu wengine
wanaweza kushindwa kuvumilia Baraka zako kwa sababu tu umesifiwa kuliko wao
unaupiga mwingi katika jamii kuwazidi, unaposifiwa zaidi au sana kuliko wao, wao
wanaaza kujiona duni na kupoteza kujiamini na hivyo wanaweza kukuonea wivu na
kujenga uadui na kuanza kukupiga vita tangu waliposikia sifa zako kwanini
watafanya hivyo kwa sababu hawawezi kuvumilia Baraka zako!
1Samuel 18:6-9 “Hata
ikawa, walipokuwa wakienda, hapo Daudi aliporudi baada ya kumwua yule Mfilisti,
wanawake wakatoka katika miji yote ya Israeli, kwa kuimba na kucheza, ili
kumlaki mfalme Sauli; wakatoka na matari, na shangwe, na vinanda. Nao wale
wanawake wakaitikiana wakicheza, wakasema, Sauli amewaua elfu zake, Na Daudi
makumi elfu yake. Basi Sauli akaghadhibika sana, na maneno haya yakamchukiza;
akasema, Wamempa Daudi makumi elfu, na mimi wamenipa elfu tu; kuna nini tena
awezayo kupata, isipokuwa ni ufalme? Sauli akamwonea Daudi wivu tangu siku ile”
Unaona ni Daudi
ambaye kwa nia njema alikuja kumpiga Goliath ambaye alikuwa ni adui wa taifa
zima alisumbua ati kwa hiyo shujaa wa wafilisti alipigwa na Daudi ambaye ndani
yake kulikuwa na upako wa kiungu ambao ulimwezesha kuwatetea wana wa Israel na
jina la Mungu likatukuzwa watu walipomsifu tayari Sauli alimuonea wivu na
kuanza uadui na Daudi, wako watu wanaweza kuanzisha uadui na wewe na
wakakuchukia na kukupiga vita lakini sababu kubwa ni kuwa hawawezi kuvumilia
Baraka zako!, angalia kuwa Sauli akimuwa mfalme na Daudi alikuwa mchunga kondoo
tu, dunia ni yenye kushangaza kwa sababu wakati mwingine mtu mkubwa na mwenye
nguvu kuliko wewe anakupiga vita wewe uliye mdogo kwa nini kwa sababu hawawezi
kuvumilia Baraka zako!
4.
Wakati
Mwingine tunapopandishwa Cheo.
Wako watu ambao
wanaweza kushindwa kuvumilia Baraka zako kwa sababu eti wewe umekuwa mkubwa
kuliko wao kwa sababu wewe una cheo kikubwa kuliko wao, unajua watu wanadhani
cheo ni kuukata au kuuchinja au kuula, lakini Mungu huwa anatupa majukumu ili
tuwatumikie watu hivyo kutokana na Baraka za kiungu Mungu anaweza kusababisha
uinuliwe juu sana na ukawa na sifa njema lakini jambo la kushangaza ni kuwa
wako watu hawataweza kustahimili kuinuliwa kwako na kwa sababu hiyo wataanza
kupanga mikakati ya kibinadamu kabisa ili wakumalize kwa sababu hawawezi
kuvumilia Baraka zako!
Daniel 6:1-5 “Ilimpendeza
Dario kuweka juu ya ufalme maliwali mia na ishirini, wawe juu ya ufalme wote;
na juu yao akaweka wakubwa watatu, na Danieli alikuwa mmoja wao; ili maliwali
hawa watoe hesabu kwao, mfalme asipate hasara. Basi Danieli huyo alipata sifa
kuliko wakubwa na maliwali, kwa kuwa roho bora ilikuwa ndani yake; naye mfalme
akaazimu kumweka juu ya ufalme wote. Basi mawaziri na maamiri wakatafuta sana
kupata sababu za kumshitaki Danieli kwa habari za mambo ya ufalme; lakini
hawakuweza kuona sababu wala kosa; kwa maana alikuwa mwaminifu, wala
halikuonekana kosa wala hatia ndani yake. Ndipo wale watu wakasema, Hatutapata
sababu ya kumshitaki Danieli huyo, tusipoipata katika mambo ya sheria ya Mungu
wake.”
Unaona watu
wanapata taabu sana kwa sababu una cheo na unaupiga mwingi katika mamlaka uliyo
nayo kwa hiyo zinatafutwa sababu ili wakukamate, uweze kutiwa hatiani, Daniel
alianza kutafutia namna hii iko kila mahali, iwe ni makazini, au makanisani, na
kwenye taasisi mbalimbali kuna watu ni waroho wa Madaraka wanatafuta kila
linalowezekana wakuangushe tu na hawajisikii vizuri wewe ukitamalaki! Kwa nini kwa sababu hawawezi kuvumilia Baraka zako!
5.
Wakati
mwingine kwa sababu unajenga.
Wako watu
wengine kwa sababu wewe uko kwenye ujenzi unajenga basi wivu unawainuka na
wanatamani kupingana na kile unachikifanya, wakati nakumbuka nilipokuwa najenga
nyumba yangu, wachwi walikuja na kufanya uchawi wao wa kusotea huu ni uchawi wa
kuhakikisha kuwa nyumba inadumaa na haiwezi kujengeka kama unaishia kwenye
linta inakuwa ni kwenye linta tu, lakini mimi nilimtegemea Mungu hata baada ya
wachawi kusotea na kuacha kinyesi kwenye nyumba ile, nilimuomba Mungu na ujenzi
ukaenda kwa kasi sana na nikafanikiwa na ndipo wachawi walipokuja waziwazi na
kugombana na mimi kwa hasira kali sana kwa nini kwa sababu hawawezi kuvumilia
Baraka zangu, Nehemia alipokuwa anaujenga ukuta wa Yerusalem maadui wa wayahudi
walitoa maneno ya kufuru kwa sababu Nehemia na wayahudi walikuwa kwenye ujenzi
ona
Nehemia 4:1-8 “Lakini
ikawa, Sanbalati aliposikia ya kwamba tulikuwa tukiujenga ukuta, akaghadhibika,
akaingiwa na uchungu sana, akawadhihaki Wayahudi. Akanena mbele ya nduguze na
mbele ya jeshi la Samaria, akisema, Wayahudi hawa wanyonge wanafanyaje? Je!
Watajifanyizia boma? Watatoa dhabihu? Au watamaliza katika siku moja? Je!
Watayafufua mawe katika chungu hizi za kifusi, nayo yameteketezwa kwa moto?
Basi Tobia, Mwamoni, alikuwa karibu naye, akasema, Hata hiki wanachokijenga,
angepanda mbweha, angeubomoa ukuta wao wa mawe. Sikia, Ee Mungu wetu; maana
tunadharauliwa; ukawarudishie mashutumu yao juu ya vichwa vyao, ukawatoe
watekwe katika nchi ya uhamisho; wala usiusitiri uovu wao, wala isifutwe dhambi
yao, mbele zako; kwa maana wamekukasirisha mbele ya hao wanaojenga. Basi
tukaujenga ukuta; nao ukuta wote ukaungamanishwa kiasi cha nusu ya kimo chake;
maana watu walikuwa na moyo wa kufanya kazi. Lakini ikawa, Sanbalati, na Tobia,
na Waarabu, na Waamoni, na Waashdodi, waliposikia ya kuwa kazi ya kuzitengeneza
kuta za Yerusalemu inaendelea, na ya kuwa mahali palipobomoka panaanza kuzibwa,
basi wakaghadhibika mno; wakafanya shauri wote pamoja kuja kupigana na
Yerusalemu, na kufanya machafuko humo.”
Unaona kuna watu
wanaweza kutoa maneno ya kejeli kwako, au hata kughadhibika na kufanya
machafuko lakini ukiangalia sababu kubwa ni kua hawawezi kuvumilia Baraka zako,
wala usishangae, wala usifadhaike they can’t handle your blessing wakati mwingine utajenga nyumba watasema ni
nyumba basin i kakibanda tu ili mradi wakukatishe tama usiogope ni kwa sababu
hawawezi kuvumilia Baraka zako!
6.
Wakati
mwingine ili wakunyamazishe
Kuna watu wakati
mwingine hawafurahii kuona ukivuma au ukisifiwa au jina lako likiwa na nguvu,
au ukishangiliwa hivyo kutokana na wivu wanatamani wakunyamazishe, wanapoona
unafanya vizuri unakubalika na una nafasi kubwa sana sifa zako zinaenea kila
mahali utashangaa wanakunyamazisha au wanataka hata na watu wanaokusifia
wanyamaze ona
Luka 19:37-40 “Hata
alipokuwa amekaribia matelemko ya mlima wa Mizeituni, kundi zima la wanafunzi
wake walianza kufurahi na kumsifu Mungu kwa sauti kuu, kwa ajili ya matendo
yote ya uwezo waliyoyaona, wakasema, Ndiye mbarikiwa Mfalme ajaye kwa jina la
Bwana; amani mbinguni, na utukufu huko juu. Baadhi ya Mafarisayo waliokuwa
katika mkutano wakamwambia, Mwalimu, uwakanye wanafunzi wako. Akajibu, akasema,
Nawaambia ninyi, wakinyamaza hawa, mawe yatapiga kelele.”
Unaona wakati
mwingine unaweza kujikuta unanyamazishwa ziko namna nyingi watu watataka
wakunyamazishe kwa sababu sifa zako zinaenea na kukua kwa kasi na wanajisikia
vibaya hawawezi kustahimili, kwa nini hii ni kwa sababu hawawezi kuvumilia
Baraka zako.!
7.
Wanataka
uwasujudie
Kuna watu
wengine huwa wakipata cheo tayari wanageuka kuwa miungu watu na wanataka
uwatetemekee na kuwasujudia na ikiwa hutetemeki wala kuwasujudia wanachukia
sana na hiyo inaweza kuwa sababu ya kuanzisha mapambanao na wewe, na hata
kukuangamiza ona
Esta 5:9-13 “Basi
Hamani alitoka siku ile kwa furaha na ukunjufu wa moyo; lakini Hamani
alipomwona Mordekai mlangoni pa mfalme, ya kwamba hasimami wala kutetemeka
mbele yake, alijaa ghadhabu juu ya Mordekai. Walakini Hamani akajizuia, akaenda
zake nyumbani kwake; akatuma kuwaita rafiki zake na Zereshi mkewe. Naye Hamani
akawasimulia habari za fahari ya mali zake, na wingi wa watoto wake, nayo mambo
yote pia ambayo mfalme amemfanikisha katika hayo, na jinsi alivyompandisha juu
ya maakida na watumishi wa mfalme. Zaidi ya hayo Hamani akasema, Naye malkia
Esta hakumkaribisha mtu ye yote pamoja na mfalme katika karamu aliyoiandaa, ila
mimi peke yangu; hata na kesho pia nimealikwa naye pamoja na mfalme. Bali haya
yote yanifaa nini, pindi nimwonapo yule Mordekai, Myahudi, ameketi mlangoni pa
mfalme? ”
unaona ni
kwanini Hamani pamoja na fahari yake aliyokuwa nayo alikuwa hajisikii raha ?
kwa sababu alikuwa anataka asujudiwe, wako watu wanataka watetemekewe,
wababaikiwe kwa sababu tu eti wana madaraka makubwa wa kutetemekewa ni Mungu tu
yeye ndiye mwenye destiny Hatima ya maisha yetu, na sio mwanadamu
Esta 3:1-6 “Baada
ya hayo mfalme Ahasuero alimwongezea cheo Hamani bin Hamedatha, Mwagagi,
akampandisha, akamwekea kiti chake juu ya maakida wote waliokuwapo pamoja naye.
Nao watumishi wote wa mfalme, walioketi mlangoni pa mfalme, wakainama na
kumsujudia Hamani, maana ndivyo alivyoamuru mfalme kwa habari zake. Bali
Mordekai hakuinama, wala kumsujudia. Basi watumishi wa mfalme walioketi
mlangoni pa mfalme wakamwambia Mordekai, Mbona wewe waihalifu amri ya mfalme? Ikawa,
waliposema naye kila siku asiwasikilize, wakamwarifu Hamani, ili kuona kama
mambo yake Mordekai yatasimama; maana alikuwa amewaambia ya kuwa yeye ni
Myahudi. Hata Hamani alipoona ya kwamba Mordekai hainami wala kumsujudia,
alighadhibika sana. Akaona si shani kumtia mikono Mordekai peke yake; maana
wamemjulisha kabila yake Mordekai; kwa hiyo Hamani alitaka kuwaangamiza
Wayahudi wote waliokuwa wakikaa katika ufalme wote mzima wa Ahasuero, yaani,
watu wake Mordekai.”
Umeona wako watu
wanadhani wewe huwaheshimu kwa sababu huwasujudii sie wengine ni wayahudi tunaheshimu
kila mtu lakini hatuabudu watu, tunamwabudu Mungu peke yake kama maandiko
yalivyotuelekeza Luka 4:8 “Yesu akajibu akamwambia, Imeandikwa, Msujudie Bwana Mungu
wako, umwabudu yeye peke yake” wakati
mwingine visa na mikasa huinuka kwa sababu watu wanataka kuabudiwa, mtu unamuheshimu
laki ni anataka kuvuka mipaka ya kiheshima na kwenda mbali zaidi, Mordekai
aliyekuwa myahudi alikuwa amejifunza kuwa mwanadamu wa kawaida muheshimu lakini
wakumuinamia na kumtetemekea ni Mungu peke
yake anayestahili kuabudiwa na kusujudiwa wengine wakiona hufanyi hivyo
hawawezi kuvumilia kwa sababu hauabudu mwanadamu.!
8.
Wakati
mwingine kwa sababu unatumiwa na Mungu kuliko wao
Kuna watu wakati
mwingine hawafurahii kuona namna Mungu anavyokutumia katika karama na vipawa
mbalimbali kuliko wao na kwa sababu hiyo watajisikia wivu moyoni na wakati
mwingine watazusha maneno ya uwongo kwa kusudi la kukuchafulia huduma yako,
wanaweza kusema unafanya mioujiza kwa kutumia nguvu za giza, wanaweza kusema
wewe ni freemason, wanaweza kusema wewe ni mchawi, anaweza kusema wewe ni imani
potofu, hutumii jina la Yesu na kadhalika hiii yota inafanyika kwa sababu
hawawezi kuvumilia Baraka na upako ambao Mungu ameweka ndani yako ona
Mathayo 12:22-24 “Wakati
ule akaletewa mtu mwenye pepo, kipofu, naye ni bubu; akamponya, hata yule bubu
akanena na kuona. Makutano wote wakashangaa, wakasema, Huyu siye mwana wa
Daudi? Lakini Mafarisayo waliposikia, walisema, Huyu hatoi pepo, ila kwa
Beelzebuli mkuu wa pepo”
Unaona Mafarisayo
hawakufurahia Yesu kukubalika kutokana na ishara na miujiza aliyokuwa
akiifanya, sisis nasi Yesu alituambia kuwa Mwanafunzi hawezi kumpita Mwalimu
wake maana yake yale majaribu ambayo Mwalimu aliyapitia sisi nasi tutayapitia
na kuzidi, tumetumwa kama Kondoo katikati ya mbwa mwitu, lazima adui wa Baraka
za kiungu ndani yetu watajitokeza na kuleta kila aina ya upinzani katika jambo
lolote ambalo kwalo Mungu ameweka mkono wake usiogope jambo kubwa na la msingi
la kukumbuika ni kuwa hawawezi kuvumilia Baraka zako!
Tumeona katika Mstari wetu wa
Msingi kuhusu baba yetu wa Imani nabii Isaka ya kuwa Mungu alimbariki upeo,
ilikuwa kuna njaa katika nchi ya kanaani na ilikuwa ni kawaida kuwa kukiwa na
njaa kama ilivyokuwa wakati wa Ibrahimu baba yake, wao walikimbilia Misri kwa
sababu ya chakula, hata hivyo Mungu alimuonya Isaka kuwa asishuke kwenda Misri,
na Mungu akaweka Baraka zake, Isaka na baba yake Ibrahimu walikuwa ni wataalamu
wa kuchimba visima, walifahamu namna na jinsi ya kuchimba maji, na huenda pia Isaka
alikuwa na ujuzi wa kumwagilia, njaa ilipokuwa kali yeye alipanda mbegu na bila
shaka alimwagilia hivyo Mungu alimbariki na akampa kuvuna mara mia lakini sio
hivyo tu mali yake iliongezeka na umaarufu wake ukawa mkubwa mno, hivyo akastawi
na kuwa mtu mkubwa sana, wafilisti walianza kuona wivu, kila kisima
alichokichimba wao walikigombea na kukifukia au kudai kuwa ni cha kwao, Biblia
imeweka wazi kuwa wafilisti WAKAMHUSUDU
yaani maana yake waluiona wivu tena wivu wenye uchungu, Isaka alikuwa mpenda
amani hivyo aliwaachia na kuchimba kingine lakini walifanya fitina hii ama ile
na mwisho wakaona haya Isaka akachimba na kingine na wakapata Maji na wakakiita
kisima kile REHOBOTHI maana yake
sasa Bwana ametufanyia nafasi, Isaka aliteseka kwa sababu ya Baraka zake, yako
mateso mengine unayapitia na changamoto nyingine unazipitia sio kwa sababu
umemkosea Mungu bali kwa sababu Mkono wa Mungu uko juu yako na wanaokuzunguka
hawawezi kustahimili wala kuvumilia aina ya upako ulio nao, aina ya huduma
uliyo nayo aina ya Baraka ulizoanazo, aina ya uimbaji unaoimba, aina ya mavazi
unayovaa, aina ya uzuri ulio nao na kila aina ya Baraka kwa kawaida ina tabia
ya kuvutia watu na maadui kwa nini ulipobarikiwa wengine walikukimbia ni kwa
sababu hawawezi kuvumilia Baraka zako!, wako ambao hawatavumilia wewe kuzaa,
hawatavumilia wewe kuolewa, hawatavumilia we kuwa na mtoto, hatawatavumilia
wewe kufanikiwa au kua na ustawi wa aina yoyote ilekatika jamii kwa nini kwa
sababu wako watu watakupoenda na kukusoegelea lakini wako wengine hawataweza
kuvumilia Baraka zako! Bwana Mungu wa Baba zangu Ibrahim, Isaka na Yakobo na
akufanyie nafasi, ili ufurahie Baraka zako bila usumbufu kutoka kwa maadui
katika jina la Yesu nakuombea amen!
Na Rev. Innocent Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!
Barikiwa sana mtu wa Mungu aliye hai nimejifunza mengi kupitia ujumbe huu na mimi pia nitawafundisha wengine ujumbe huu. Ameeni
JibuFuta