Jumapili, 19 Juni 2022

Waandaa meza mbele yangu, Machoni pa watesi wangu !

Zaburi 23:1-6Bwana ndiye mchungaji wangu, Sitapungukiwa na kitu. Katika malisho ya majani mabichi hunilaza, Kando ya maji ya utulivu huniongoza. Hunihuisha nafsi yangu; na kuniongoza Katika njia za haki kwa ajili ya jina lake. Naam, nijapopita kati ya bonde la uvuli wa mauti, Sitaogopa mabaya; Kwa maana Wewe upo pamoja nami, Gongo lako na fimbo yako vyanifariji. Waandaa meza mbele yangu, Machoni pa watesi wangu. Umenipaka mafuta kichwani pangu, Na kikombe changu kinafurika.  Hakika wema na fadhili zitanifuata Siku zote za maisha yangu; Nami nitakaa nyumbani mwa Bwana milele.”



Utangulizi:

Moja ya zaburi maarufu zaidi duniani labda kuliko zaburi zote ni zaburi ya 23, Zaburi hii imetumiwa sana na Wayahudi na Wakristo katika ibada na maombi lakini vilevile kwaajili ya kujenga imani, Kiini kikuu cha zaburi hii ni yale maneno Bwana ndiye Mchungaji wangu maneno haya yanazigusa jamii nyingi sana Duniani, Hata huko Mesopotamia, Inasemekana kuwa Mfalme Hammurabi katika mojawapo ya hutuba yake muhimu sana aliyowahi kuitoa alihitimisha kwa kusema “Mimi ndiye Mchungaji ninayehakikisha usalama na mafanikio ya watu wangu, utawala wangu utakuwa wa haki, wenye nguvu hawatawaonea wanyonge, na hata yatima na wajane watatendewa kwa haki” maneno ya kiongozi huyu wa zamani sana yalikuwa maarufu na huenda yakawa yalichangia mtunzi wa Zaburi hii kuyachanganua kwa kina katika uimbaji wake kwa kusudi la kutambua uhusiano wake na Mungu.

Zaburi hii ina mistari michache sana lakini yenye kubeba maana pana sana na hatuwezi kwa somo moja kama hivi kugusia kila neno linalozungumziwa na zaburi hii, Hata hivyo leo Mwalimu mkuu Roho Mtakatifu anatupeleka kuutazama mstari wa tano (5) katika zaburi hii ya (23) ili tuweze kujifunza kile ambacho Mungu amekikusudia kwetu .

Katika Zaburi 23:5 Daudi anasema “WAANDAA MEZA MBELE YANGU, MACHONI PA WATESI WANGU maneno haya peke yake yanaashiria uhusiano mkubwa sana na wa karibu ulioko kati yake na Mungu, lakini sio hivyo tu mstari huu unafunua heshima kubwa sana ya kifalme ambayo mwandishi anapewa na Mungu, kwani kumbuka kuwa anayeandaa meza hapa sio Daudi bali Mungu anamuandalia Daudi meza hivyo kimsingi mahali hapa pana maana pana na kubwa sana ambayo inaweza kumfaa kila mmoja wetu leo!

Ni muhimu kufahamu kuwa katika taratibu za kifalme, unapomualika mtu ambaye unamuheshimu sana katika utawala wako basi mgeni huyo rasmi labda ni rais au mfalme wa taifa lingine kama alikuja aidha kwa mazungumzo au kwa mualiko wa serikali yako au ziara ya kuimarisha uhusiano basi inapofika jioni kiongozi huyo mualikwa huandaliwa chakula maalumu ambacho huitwa dhifa ya kitaifa kwa kusudi la kusalimiana, kubadilishana mawazo, kufarijiana, kutiana moyo kujenga mahusiano, kufurahi na kisha kula pamoja, na unapokuwa umemualika kiongozi huyo mfalme au Rais aliyemualika mfalme mwingine anapaswa vilevile kuhakikisha kuwa anatoa na huduma zote ikiwemo ulinzi mkali na hata kama ana ulinzi wake, Kwa msingi hata kama ana maadui katika taifa lake au mataifa yanayomzunguka hawawezi kumgusa akiwemo katika himaya yako na itakuwa ni aibu kubwa sana kushindwa kuimarisha ulinzi wa mgeni wako huyu wa heshima endapo atauawa mbele yako, Dhifa hii kwa kawaida huonyesha kuwa umempa heshima ya juu sana mgeni wako! Na haya ni maswala muhimu katika mambo ya kidiplomasia.

Mwaka 1969 Mwenyekiti wa chama cha ukombozi wa Msumbiji Edward Mondlane aliuawa makao makuu ya chama cha FRELIMO yaliyokuwa jijini Dar es salaam baada ya kuletewa kikapu cha zawadi ya kitabu alichokuwa akikifungua kwenye nyumba ya rafiki yake wa kimarekani aliyeitwa Betty King, bomu lililipuka na kumuaa na mpaka leo haujajulikana aliuawa na nani ingawa inahisiwa ni wapinzani wa ukomonisti, hii inatufundisha kuwa mtu anaweza kuuawa hata mahali anakodhania kuwa ni salama!

Mungu aliwahi kuwapa heshima ya kidiplomasia na kuwaandalia meza wazee 74 wanaoheshimika sana katika Israel akiwemo Musa na haruni ingawa maandiko hayaelezei kwa kina ilikuwaje kuwaje ona lakini waliandaliwa meza mbinguni

Kutoka 24:9-11 “Ndipo akakwea juu, Musa, na Haruni, na Nadabu, na Abihu, na watu sabini miongoni mwa wazee wa Israeli; wakamwona Mungu wa Israeli; chini ya miguu yake palikuwa na kama sakafu iliyofanyizwa kwa yakuti samawi, kama zile mbingu zenyewe kwa usafi wake. Naye hakuweka mkono wake juu ya hao wakuu wa wana wa Israeli; nao wakamwona Mungu, wakala na kunywa.”

Hii ilikuwa ni neema kubwa na heshima ya juu zaidi kuwahi kutokea!, Daudi anaonyesha kuwa alikuwa ana uhusiano na Mungu wa karibu mno na anadhihirisha wazi kuwa neema ya Mungu ilikuwa juu yake kiasi cha kualikwa katika uwepo wa Mungu na kuandaliwa meza, huku Mungu akimlinda dhidi ya adui zake  na kumhakikishia usalama, huku akiendelea kuonyesha wema wake kwake, Daudi alikuwa mtu wa vita kwa hiyo alikuwa na maadui wengi sana, lakini kwa heshima hii aliyopewa na Mungu, hakuna adui anaweza kumgusa watamuona tu maana ameketi kwenye meza ya mwenye nguvu na hakuna mtu wa kumgusa kwa gharama yoyote.

Jambo hili pia vilevile licha ya kumhusu Daudi, lakini pia linaihusu Israel yote, nchi ya mkanaani haikuwa ya Israel kwa asili, lakini ilikuwa ni Mungu aliyemuahidi Ibrahimu kuwa atawapa, kwa msingi huo basi Israel wamealikwa katika nchi ya Mkanaani, Mwenyeji wao ni Mungu, Israel kule kaskazini inapakana na nchi ya Lebanon, na Syria, magharibi inapakana na Jordan na kusini iko Misri na eneo la wafilisti pale Palestina (Ukanda wa Gaza) kwa kawaida  wote tunafahamu namna na jinsi Israel inavyostawi na jinsi inavyokuwa na nguvu kubwa sana ya kijeshi, huku tukifahamu kuwa inazungukwa na adui pande zote na ambao wangetamani ifutwe mara moja, lakini wako salama kwa sababu wameandaliwa meza machoni pa watesi wao mwenyeji aliyewaalika ni Mungu.

Jambo hili vilevile linaweza likalihusu kanisa kwani kanisa limepewa kazi ngumu ya kuipeleka injili lakini kwa mfano wa kondoo na mbwa mwitu, aliyetualika kuihubiri injili alisema atakuwa pamoja nasi hata ukamilifu wa dahari. Haijalishi kuwa ni changamoto za aina gani tunapitia yeye mwenyewe anajua kuwa ametutuma kama kondoo katikati ya mbwa mwitu!.

Mathayo 10:16-20 “Angalieni, mimi nawatuma kama kondoo kati ya mbwa-mwitu; basi iweni na busara kama nyoka, na kuwa watu wapole kama hua. Jihadharini na wanadamu; kwa maana watawapeleka mabarazani, na katika masinagogi yao watawapiga; nanyi mtachukuliwa mbele ya maliwali na wafalme kwa ajili yangu, kuwa ushuhuda kwao na kwa mataifa. Lakini hapo watakapowapeleka, msifikiri-fikiri jinsi mtakavyosema; maana mtapewa saa ile mtakayosema. Kwa kuwa si ninyi msemao, bali ni Roho wa Baba yenu asemaye ndani yenu.”

Hata hivyo pamoja na hatari zote zinazoweza kumzunguka mtu mmoja mmoja au Israel au kanisa au wewe kumbuka Zaburi hii ya 23 ina maana panasana katika maisha yako yenyewe inaaanza kwa kusema Bwana ndiye Mchungaji wangu, sitapungukiwa na kitu, Na katika kuandaliwa meza kumbuka kuwa ni Mungu mwenyewe ndiye aliyekualika na ni yeye ndiye aliyekuheshimisha kwa hiyo zaburi hii inataka tuwe na ujasiri uliopitiliza na kutokuogopa!.

Zaburi hii inamtia nguvu kila mmoja kujua ya kuwa Mungu yuko pamoja nasi, na kuwa hatutapungukiwa na kitu, na kuwa lazima tuwe na ujuzi kuwa Mungu yuko pamoja nasi na kuwa hatatupungukia wala hatatuacha, haijalishi tunapitia maswala gani magumu au laini hata yawe mazingira yenye kutishia amani yetu na usalama wetu, Mungu atajishughulisha na kutupatia mahitaji yetu huku akituhakikishia usalama wetu.

Wafilipi 4:19 “Na Mungu wangu atawajazeni kila mnachokihitaji kwa kadiri ya utajiri wake, katika utukufu, ndani ya Kristo Yesu.”

Mungu anapotuandalia meza kazi yetu ni kusubiri tu, hatupaswi kuwa na wasiwasi kama ilivyo kwa wageni wengine unatulia tu mwenyeji wako anajua unachohitaji na anaweza kukuuliza akuletee kinywaji gani, unapokuwa unaandaliwa meza haupambani ukae wapi, haupambani ule nini,   haupambanii usalama wako ni yeye aliyekualika anajua unayoyahitaji kwa msingi huo unapaswa kuwa na utulivu, huwezi kujiandalia mwenyewe  ni aibu umealikwa sebuleni kwa mtu kisha unaanza kufungua friji, unaingia jikoni, unaulizia matunda na kadhalika  Hapana haipaswi kuwa hivyo kwani yeye anayeandaa meza ataleta kila tunachiokihitaji, Israel walipokuwa wanaalikwa katika inchi ya kanaani mwenyeji wao aliwapa maji, aliwapa na mana wakala na aliwapa kware walipolilia.

Kutoka 16:14-16 “Na ulipoinuka ule umande uliokuwa juu ya nchi, kumbe! Juu ya uso wa bara kitu kidogo kilichoviringana, kidogo kama sakitu juu ya nchi. Wana wa Israeli walipokiona, wakaambiana, Nini hiki? Maana hawakujua ni kitu gani. Musa akawaambia, Ndio mkate ambao BWANA amewapa ninyi, mle. Neno hili ndilo aliloagiza BWANA, Okoteni ninyi kitu hicho kila mtu kama ulaji wake ulivyo; kichwa pishi, kama hesabu ya watu wenu ilivyo; ndivyo mtakavyotwaa, kila mtu kwa ajili ya hao walioko hemani mwake.”

Daudi kwa zaburi hii alikuwa anamuamini Mungu ana ujasiri katika Mungu anamjua Mungu kuwa hawezi kumuangusha yeye atatupa mahitaji yetu kwa kadiri ya neema ya uhitaji wetu maandiko yanaema katika  Waebrania 4:16 “Basi na tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji.”

Mungu ndiye mwenyeji amemkaribisha mgeni kwenye dhifa maana yake ni nini kila kitu kimekwisha kuandaliwa kwaajili yake, ni yeye ndiye aliyetupa mwaliko sisi sio wazamiaji, hivyo tunamtegemea yeye kwa mahitaji yetu yote ya kimwili na kiroho na muhimu zaidi atatulinda Mungu sio tu atatupatia kila tunachikihitaji katika ulimwengu huu lakini kama Mungu atakuwa pamoja nasi milele

2Petro 1:3 “Kwa kuwa uweza wake wa Uungu umetukirimia vitu vyote vipasavyo uzima na utauwa, kwa kumjua yeye aliyetuita kwa utukufu wake na wema wake mwenyewe.”

Kwa msingi huo Zaburi ya 23:5 inapandisha chati ya mwamini ambaye amealikwa katika karamu ya mwana kondoo na katika uwepo wa Mungu uhakika wa wema na fadhili za Mungu kutufuata siku zote za maisha yetu na kukaa katika uwepo wake milele

 

Rev. Innocent Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni