Jumanne, 14 Juni 2022

Kaburi liko wazi!

Luka 24:1-3 “Hata siku ya kwanza ya juma, ilipoanza kupambazuka, walikwenda kaburini, wakiyaleta manukato waliyoweka tayari. Wakalikuta lile jiwe limevingirishwa mbali na kaburi, Wakaingia, wasiuone mwili wa Bwana Yesu.”


Utangulizi: 

Moja ya mambo ambayo wanadamu wengi sana huyaogopa duniani ni pamoja na Kaburi, au eneo la makaburini, sehemu nyingi sana duniani na katika jamii nyingi duniani kumekuwepo na hofu ya aina Fulani ambapo watu huogopa sana kaburi au makaburini, lakini sio hivyo tu hata pamoja na kuweko kwa hofu ya kifo, bado watu wengi wanahofia tukio la kuzikwa wakifikiri ni moja ya tukio gumu, au wakidhani kuwa wanaweza kuzikwa wakiwa na fahamu zao, au wakifikiri itakuwaje kama itatangazwa kuwa nimekufa kwa bahati mbaya kisha nikashituka nikiwa kaburini hofu ya aina hii imekuwepo kwa miaka mingi, katika lugha ya kiyunani (Greek) hofu hii ya kisaikolojia kwa kiyunani inaitwa TAPHOPHOBIA  neno hilo ni neno la kiyunani lenye muunganiko wa maneno makuu mawili TAPHO – ambalo maana yake ni Kaburi (Grave) na PHOBIA – Maana yake hofu, kwa hiyo neno TAPHOPHOBIA maana yake ni hofu ya kaburi, kwa hiyo kimsingi watu wengi sana wanaogopa kifo lakini hata hivyo ni ukweli uliowazi kuwa watu wengi wanaogopa zaidi kaburi, kwa hiyo kuna hofu ya kifo na kuna hofu ya kaburi, au hofu ya kufikia mwisho!, sasa basi ni muhimu kufahamu kuwa kufufuka kwa Yesu, sio tu kunatusaidia kutokuogopa kifo lakini vilevile kunatusaidia kutokuogopa nguvu za kaburi au kuzimu! Tutajifunza somo hili kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-

·        
  
Kuzikwa kwa Yesu Kristo.

·         Umuhimu wa kaburi lililo wazi.

·         Kaburi liko wazi.

Kuzikwa kwa Yesu Kristo.! 

Mara kadhaa tumezungumzia sana kuhusu Mateso ya Bwana wetu Yesu, na huenda wahubiri wengi hawajawahi kuzungumzia kuhusu kuzikwa kwa Yesu Kristo, lakini ni muhimu sana kuuthibitishia ulimwengu kuwa Kristo alizikwa, kuzikwa kwa Yesu Kristo ni moja ya jambo, Muhimu sana katika injili kwa sababu Manabii waliliona  na kulitabiria pia kama walivyotabiria mambo mengine. 

Isaya 53:8-9 “Kwa kuonewa na kuhukumiwa aliondolewa; Na maisha yake ni nani atakayeisimulia? Maana amekatiliwa mbali na nchi ya walio hai; Alipigwa kwa sababu ya makosa ya watu wangu. Wakamfanyia kaburi pamoja na wabaya; Na pamoja na matajiri katika kufa kwake; Ingawa hakutenda jeuri, Wala hapakuwa na hila kinywani mwake.” 

Unaweza kuona Isaya nabii aliyeishi miaka 700 kabla ya Kristo, alitabiri kuhusu kuzikwa yaani kufanyiwa kaburi kwa Yesu Kristo, Hili ni jambo la msingi sana kama sehemu ya injili unapozungumzia mateso ya Kristo na hata kufufuka kwake basi tukio la kuzikwa ni la muhimu na ni sehemu ya injili ambayo hata Paulo Mtume alikabidhiwa ona 

1Wakorintho 15:1-4 “Basi, ndugu zangu, nawaarifu ile injili niliyowahubiri; ambayo ndiyo mliyoipokea, na katika hiyo mnasimama, na kwa hiyo mnaokolewa; ikiwa mnayashika sana maneno niliyowahubiri isipokuwa mliamini bure. Kwa maana naliwatolea ninyi hapo mwanzo yale niliyoyapokea mimi mwenyewe, ya kuwa Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu, kama yanenavyo maandiko; na ya kuwa alizikwa; na ya kuwa alifufuka siku ya tatu, kama yanenavyo maandiko;” 

Unaweza kuona kumbe unabii na injili vyote vinakazia swala zima la kuwa Yesu alizikwa, mtu akifa hilo ni jambo lingine na akizikwa hilo ni jambo lingine, Neno kuzikwa katika kiingereza linatumika neno “Burial” au “Interment” au “inhumation” ambalo maana yake ni hatua ya mwisho kabisa ya kuwepo duniani kwa kuuweka mwili wa Mwanadamu chini au kuuchoma (Cremation) au kuufungia na kuhitimisha huzuni au huruma kwa kumuweka mtu au mwili wake na kuufunika kabisa, kwa hiyo licha ya kufa ukizikwa maana yake umetoweka kabisa, kibinadamu imethibitika na kukubalika kuwa huwezi kuweko tena, Hivyo Yesu alizikwa maana yake ilithibitishwa kuwa hawezi kuweko tena kabisa duniani, lakini na pamoja na tendo hilo, serikali ya kirumi iliweka walinzi ili kuhakikisha kuwa pale alipozikwa hakuna kitu kinaweza kubatilika. Kimsingi jamii inapomzika mtu maana yake imekubali kuwa asiweko tena kabisa duniani! Sasa Yesu alizikwa lakini sio kuzikwa tu na ulinzi uliwekwa kuhakikisha kuwa amezikika. 

Mathayo 27:62-66 “Hata siku ya pili, ndiyo iliyo baada ya Maandalio, wakuu wa makuhani, na Mafarisayo wakamkusanyikia Pilato, wakasema, Bwana, tumekumbuka kwamba yule mjanja alisema, alipokuwa akali hai, Baada ya siku tatu nitafufuka. Basi amuru kwamba kaburi lilindwe salama hata siku ya tatu; wasije wanafunzi wake wakamwiba, na kuwaambia watu, Amefufuka katika wafu; na udanganyifu wa mwisho utapita ule wa kwanza. Pilato akawaambia, Mna askari; nendeni mkalilinde salama kadiri mjuavyo. Wakaenda, wakalilinda kaburi salama, kwa kulitia lile jiwe muhuri, pamoja na wale askari walinzi.” 

Asee sio tu kuwa mtu amekufa hapa lakini AMEZIKWA na hata maziko yake yanawekewa ulinzi kwa siku tatu, kuhakikisha kuwa hafufuki mtu, ndio maana katika nguvu ya injili hatuwezi kamwe kupuuzia swala la kuzikwa “ALITESWA, AKAFA AKAZIKWA…”  Wako watu katika maisha yako sio tu unapokuwa umesitawi inawapa shida sana, na watatamani uharibikiwe, upotee na ikiwezekana historia yako ifutike na usambaratike kabisa wanaweza hata kulinda hata taarifa zako zisisambae watakuchafua ikiwezekana usisimame milele hawa wanataka kukufuta “inhumation” “Cremation” kuhakikisha kuwa hauko tena hata tuta lako la kaburi lisiweko, ni kama kwa kaburi la Colonel Muammar Gadafi, au Osama Bin Laden wameuawa na makaburi yao yamefutika hawako kabisa, waliochukizwa nao hawakutaka hata wazikwe katika hali ya kawaida, wawe wamefutika hivyo ndivyo adui za Kristo Yesu walivyotaka iwe, kwa hiyo kuzikwa, kutoweka kusahaulika ni sehemu ya injili unaposema Yesu aliteswa, akafa usiseme tu akafufuka siku ya tatu kumbuka alizikwa! 

Umuhimu wa Kaburi lililo wazi. 

Kufufuka kwa Yesu Kristo ndio moja ya muujiza Mkubwa sana katika ukristo, kama Yesu hangelifufuka imani yetu ingekuwa ni imani potofu na ya hovyo kabisa kuliko zote, nisikilize ni kufufuka kwa Yesu Kristo pekee kunakotuthibitishia uwezo wa Mungu kwamba hatuwezi kukata tamaa katika jambo lolote lile, Kaburi lililo wazi ni ushahidi ulio wazi wa kutimizwa kwa unabii wa Mfalme Daudi ya Kwamba Mungu hatamuacha Mtakatifu wake aone uharibifu

Zaburi 16:10 “Maana hutakuachia kuzimu nafsi yangu, Wala hutamtoa mtakatifu wako aone uharibifu.”

Kaburi lililo wazi ni ishara iliyowazi ya ushindi unaobainisha kuwa Mungu anauwezo wa kufufua hata pale mtu anapofikia hatua ya kuzikwa, Yesu yuko hai nani wazi kuwa nguvu ileile iliyomfufua Yesu Kristo ina uwezo wa kufufua lolote katika maisha yetu ambalo linaonekana kama linataka kufa na hata kama limekufa machoni pa watu, Bado ana uwezo wa kulifufua.

Warumi 8:11 “Lakini, ikiwa Roho yake yeye aliyemfufua Yesu katika wafu anakaa ndani yenu, yeye aliyemfufua Kristo Yesu katika wafu ataihuisha na miili yenu iliyo katika hali ya kufa, kwa Roho wake anayekaa ndani yenu” 

Nyakati za zamani sana alama ya wakristo ilikuwa sio msalaba ilikuwa ni kaburi lililowazi, kaburi lililo wazi ni ishara ya kuwa Yesu amefufuka na kuwa Mauti haimuwezi, ni ishara kwetu kuwa hakuna mtu anaweza kuifuta historia ya kuwepo kwa masihi, ni ushahidi kwetu kuwa Mungu wetu yu hai na ana nguvu, ni ishara kwetu kuwa hata kama watu watakukusudia ufutike hawataweza kukufuta wewe juu ya uso wa dunia, Kaburi lilowazi ni ushahidi kuwa yuko mwenye mamlaka mmoja tu mwenye ufunguo ambao akifunga hakuna afunguaye wala akifungua hakuna awezae kufunga mwenye mamlaka ya kufisha na kuhuuisha ni Yesu pekee! 

Ufunuo 1:17-18 “Nami nilipomwona, nalianguka miguuni pake kama mtu aliyekufa. Akaweka mkono wake wa kuume juu yangu, akisema, Usiogope, Mimi ni wa kwanza na wa mwisho, na aliye hai; nami nalikuwa nimekufa, na tazama, ni hai hata milele na milele. Nami ninazo funguo za mauti, na za kuzimu.” 
     

Kaburi liko wazi!

Msikilizaji wangu mpendwa nimepewa mamlaka ya kukutangazia ya kuwa kaburi liko wazi, tutaweza kupitia kila aina ya changamoto tuwapo duniani, kila aina ya mawimbi na mateso na matukano na dharau za watu, watu wanaweza kupanga mikakati ya kishetani katika kuhakikisha kuwa tunapotea na kutoweka na kuwa historia yetu inafagiliwa na kufutiliwa mbali na tunazikwa na kaburi zetu zinawekewa muhuri kuhakikisha ya kuwa hatuchomoki lakini nataka nikutangazie kuwa kaburi liko wazi, hakuna mahali ambako mkono wa Mungu hauwezi kufika na kukuchomoa, alimezwa Yona na nyangumi na nyangumi akamtapika, alimezwa Yesu na Kaburi na kaburi likamtapika, aliwekwa Danieli katika tundu la simba na makanwa ya simba yakazuibwa, walitupwa Daniel, Shadrak na Abednego na katika tanuri ya moto yaani kaburi la moto ili wafanyiwe “Cremation” lakini mauti ilishindikana nakutangazia kwa jina la Yesu Kristo hakuna mauti katika kazi yako, hakuna mauti katika masomo yako, hakuna mauti katika ndoa yako, hakuna mauti katika biashara yako, hakuna mauti katika sifa zako, hakuna mauti katika familia yako hakuna mauti kokote kule itakayokuweza! Ndio maana kaburi liko wazi, kaburi lililo wazi ndio kiini cha injili inayotuthibitishia kuwa Yesu yu hai, mtetezi wetu yu hai hajafa naye atasimama juu ya nchi apate kututetea, kila mauti inayokusudiwa, katika kila sehemu ya maisha yako naitangazia kuwa Kaburi liko wazi, mwambie shetani kaburi liko wazi, mwambie adui yako kaburi liko wazi, kaburi lililo wazi ni ishara ya kuwa kuna maitumaini kila wakati na kuwa Mungu hatatuacha tuone uharibifu wa namna yoyote! Na badala yake tutawaona adui zetu wakitoweka kwa haraka.!

 

Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni