Jumatatu, 18 Julai 2022

Mwana wa Muungwana na mwana wa mjakazi


Wagalatia 4:28-31 “Basi, ndugu zangu, kama Isaka sisi tu watoto wa ahadi. Lakini kama vile siku zile yule aliyezaliwa kwa mwili alivyomwudhi yule aliyezaliwa kwa Roho, ndivyo ilivyo na sasa. Lakini lasemaje andiko? Mfukuze mjakazi na mwanawe, kwa maana mwana wa mjakazi hatarithi kabisa pamoja na mwana wa mwungwana. Ndiposa, ndugu zangu, sisi si watoto wa mjakazi, bali tu watoto wa huyo aliye mwungwana.”


Utangulizi:

Ni muhimu kuelewa kuwa Paulo Mtume alikuwa anakamilisha Mafundisho yake kwa Kanisa lililokuwako Galatia ambao walikuwa wamekumbana na kadhia ya  Mateso pamoja na Mafundisho mabaya ya Jamii ya wayahudi waliokuwa waanaamini katika sheria ya Musa na hata baada ya Injili kuhubiriwa wao waliwataka wakristo waendelee kuwa chini ya sheria ya Musa badala ya kuutumia uhuru wao waliokuwa nao katika kristo, Katika kuhitimisha mafundisho yake anaonyesha kuwa kuna wana wa Muungwana na wana wa Mjakazi.  Na anajaribu kuonyesha tofauti zao watoto hao kwamba Mwana wa Mjakazi alizaliwa kwa mapenzi ya Mwili na yule wa  Muungwana alizaliwa kwa kusubiri Ahadi ya Mungu, sawa tu na tukio la kuzaliwa kwa Ishmael na baadaye Isaka, Ishmael Alizaliwa kwa mapenzi ya mwili wakati Isaka alizaliwa kutokana na ahadi ya Mungu ona

 Mwanzo 16:1-4 “Basi Sarai mkewe Abramu hakumzalia mwana, naye alikuwa na mjakazi, Mmisri, jina lake Hajiri. Sarai akamwambia Abramu, Basi sasa, BWANA amenifunga tumbo nisizae, umwingilie mjakazi wangu labda nitapata uzao kwa yeye. Abramu akaisikiliza sauti ya Sarai. Sarai mkewe Abramu akamtwaa Hajiri Mmisri mjakazi wake, baada ya kukaa Abramu katika nchi ya Kanaani miaka kumi, akampa Abramu mumewe, awe mkewe. Basi akamwingilia Hajiri, naye akapata mimba. Naye alipoona ya kwamba amepata mimba, bibi yake alikuwa duni machoni pake.”     Kwa hiyo tunaweza kuona mtoto wa Kwanza wa Abraham anazaliwa kutokana na jitihada za kibinadamu yaani kwa mapenzi ya mwili na kwa mwanamke aliyekuwa mtumwa (Kijakazi)  Na mtoto wa pili alizaliwa kwa uvumilivu na subira kwa kusubiri ahadi ya Mungu na kupitia mwanamke aliyekuwa mtawala (Huru) Mwanzo 21:1-4 “BWANA akamjia Sara kama alivyonena, na BWANA akamfanyia kama alivyosema. Sara akapata mimba akamzalia Ibrahimu mwana wa kiume katika uzee wake, kwa muhula alioambiwa na Mungu. Ibrahimu akamwita jina lake Isaka, yule mwana aliyezaliwa, ambaye Sara alimzalia. Ibrahimu akamtahiri Isaka mwanawe, alipokuwa mwenye siku nane, kama Mungu alivyomwamuru.

Hawa wote ni watoto wa Ibrahimu, mmoja alizaliwa kutokana na mawazo na mipango ya kibinadamu na mwingine alizaliwa kwa kusubiria ahadi ya Mungu, Paulo anajaribu kuunganisha swala hili na hali halisi waliyokuwa wanaipitia Makanisa ya Galatia, taabu kubwa waliyokuwa wanaipitia ni Mateso pamoja na Mafundisho potofu ya wayahudi yanayowataka waishike sheria ya Musa huku wakiwa wamemuamini Yesu Kristo ambaye tayari alikuwa amekwisha kuwaokoa na laana ya torati, Kitendo cha aalimu hawa wa kiyahudii kulisumbua kanisa alikifananisha na Ishamael kumdhihaki Isaka, Ishmael akiwa ni mtoto wa mjakazi na Isaka akiwa ni mtoto wa Muungwana, dhihaka hii haikuweza kuvumilika kiasi ambacho Sara alitoa wazo la mjakazi na mtoto wake kufukuzwa kabisa kwani wangemuharibu kabisa Isaka kutokana na ushawishi wao wa kifisadi

Mwanzo 21:8-12 “Mtoto akakua, akaachishwa kunyonya; Ibrahimu akafanya karamu kuu siku ile Isaka alipoachishwa kunyonya. Sara akamwona yule mwana wa Hajiri Mmisri, ambaye alimzalia Ibrahimu, anafanya dhihaka. Kwa hiyo akamwambia Ibrahimu, Mfukuze mjakazi huyu na mwanawe, maana mwana wa mjakazi hatarithi pamoja na mwanangu, Isaka. Na neno hilo lilikuwa baya sana machoni pa Ibrahimu, kwa ajili ya mwanawe. Mungu akamwambia Ibrahimu, Neno hili lisiwe baya machoni pako, kwa ajili ya huyo mwana, na huyo mjakazi wako. Kila akuambialo Sara, sikiza sauti yake, kwa maana katika Isaka uzao wako utaitwa.”

Unaweza kuwa na swali moyoni ambalo hata mimi nilikuwa nalo, kwamba ni aina gani ya dhihaka ilikuwa inafanyika tena siku ya sherehe hata kumuuzi Sara na kuamuru kuwa mtoto huyo afukuzwe pamoja na mama yake?  Kwa mujibu wa Marabi wa kiyahudi ni kuwa kijana huyu alikuwa na miaka kama 14 hivi na tayari alikuwa ameshaonyesha kutokuishi sawa na njia ya baba yake, na kwamba kulikuweko na dalili nyingi za kukiuka sheria za Mungu ambazo hata Abrahamu alikuwa anazishika, Sara alikuwa amebaini hilo kwa uwazi kuliko Abrahamu, Sara aliona kuwa kuna hatari mtoto wa ahadi akasawishika kufuata njia za kaka yake ambaye kwa siri wayahudi wanaeleza kuwa alikuwa akionekana anaabudu miungu ya mama yake na kushindana na kijana mdogo wa Ibrahimu. Neno dhihaka kwa waebrania linasomeka kama TSACHAQ  kufanya dhihaka katika mambo muhimu na ya msingi, neno hili pia huumika kumaanisha watu wasiomcha Mungu au wenye kupuuzia njia za Mungu. Unaweza kuliona katika zaburi na maandiko mengine ya kiyahudi;-

Zaburi 1:1-2 “Heri mtu yule asiyekwenda Katika shauri la wasio haki; Wala hakusimama katika njia ya wakosaji; Wala hakuketi barazani pa wenye mizaha. Bali sheria ya Bwana ndiyo impendezayo, Na sheria yake huitafakari mchana na usiku.”

Wakati Abraham na watu wake wanafanya karamu ya kumshukuru Mungu Ishamel yeye alikuwa anadhihaki kwa msingi huo kama tungekuwepo kwenye tafrija ile tungebaini kuwa watu wako makini katika kumshukuru Mungu kwa matendo makuu aliyomfanyia Sara na Abraham na kundi la Hajiri  na mwanaye wanapuuzia na kucheka au kuona kinachofanyika ni upuuzi tu na hawajali kile Mungu alichokifanya wala hawaoni kuwa ni jambo kubwa.  Sara aliona hilo na kubaini kuwa kijana huyu na mama yake hawana budi kutimuliwa kwani hawangeweza kuishi pamoja, wala kurithi pamoja na Isaka Mwanzo 21:10 “Kwa hiyo akamwambia Ibrahimu, Mfukuze mjakazi huyu na mwanawe, maana mwana wa mjakazi hatarithi pamoja na mwanangu, Isaka.”

Paulo anautumia mfano huo sasa kulifundisha kanisa kuhusu mateso yanayofanywa na wale wanaolitesa kanisa kwa Mateso na mafundisho yasiyo sahihi ambayo yanalitesa Kanisa Kama Ishamel alivyokuwa akimdhihaki Isaka waalimu wa uongo walikuwa wakilitesa kanisa kwa kufundisha kuwa watu wanaweza kukubaliwa na Mungu kwa sababu ya bidii ya mwilini, wakati kuzaliwa kwa Isaka kulitokana na Mungu kuitimiza ahadi yake na sio juhudi za kibinadamu, Jamii kubwa ya wayahudi hata pamoja na kuiamini injili waligeuka kubwa mwiba mkubwa wa mateso katika kanisa na mafundisho yasiyo sahihi  aidha wakati wote walihakikisha kuwa wanapingana na injili na kuwaudhi wahubiri wa injili ona

Matendo 13:48-51 “Mataifa waliposikia hayo wakafurahi, wakalitukuza neno la Bwana, nao waliokuwa wamekusudiwa uzima wa milele wakaamini. Neno la Bwana likaenea katika nchi ile yote. Lakini Wayahudi wakawafitinisha wanawake watauwa wenye cheo na wakuu wa mji, wakawataharakisha watu wawaudhi Paulo na Barnaba; wakawatoa katika mipaka yao. Nao wakawakung'utia mavumbi ya miguu yao, wakaenda Ikonio.”

Matendo 17:5-9 “Na Wayahudi wakaona wivu, wakajitwalia watu kadha wa kadha katika watu ovyo wasio na sifa njema, nao wakakutanisha mkutano, wakafanya ghasia mjini, wakawaendea watu wa nyumba ya Yasoni, wakataka kuwapeleka mbele ya watu wa mji; na walipowakosa, wakamkokota Yasoni na baadhi ya ndugu mbele ya wakubwa wa mji, wakipiga kelele, wakisema, Watu hawa walioupindua ulimwengu wamefika huku nako, na Yasoni amewakaribisha; na hawa wote wanatenda mambo yaliyo kinyume cha amri za Kaisari, wakisema na kwamba yupo mfalme mwingine, aitwaye Yesu. Wakafadhaisha ule mkutano na wakubwa wa mji walipoyasikia hayo. Nao walipokwisha kumtoza dhamana Yasoni na wenziwe wakawaacha waende zao.”

Matendo 17: 13 “Lakini Wayahudi wa Thesalonike walipopata habari ya kwamba neno la Mungu linahubiriwa na Paulo hata katika Beroya, wakaenda huko nako wakawachafua na kuwafadhaisha makutano.”

Unaweza kuona kuwa kanisa sio tu lilikuwa linapitia mateso ya kawaida na upinzani dhidi ya injili lakini pia lilipingwa kwa mafundisho yasiyo sahihi Na kanisa la Galatia lilikuwa ni moja ya kanisa lililoathiriwa na mafundishi hayo

Wagalatia 3:1-9 “Enyi Wagalatia msio na akili, ni nani aliyewaloga, ninyi ambao Yesu Kristo aliwekwa wazi mbele ya macho yenu ya kuwa amesulibiwa? Nataka kujifunza neno hili moja kwenu. Je! Mlipokea Roho kwa matendo ya sheria, au kwa kusikia kunakotokana na imani? Je! Mmekuwa wajinga namna hii? Baada ya kuanza katika Roho, mnataka kukamilishwa sasa katika mwili? Mmepatikana na mateso makubwa namna hii bure? Ikiwa ni bure kweli. Basi, yeye awapaye Roho na kufanya miujiza kati yenu, je! Afanya hayo kwa matendo ya sheria, au kwa kusikia kunakotokana na imani? Kama vile Ibrahimu alivyomwamini Mungu akahesabiwa haki. Fahamuni basi, ya kuwa wale walio wa imani, hao ndio wana wa Ibrahimu. Na andiko, kwa vile lilivyoona tangu zamani kwamba Mungu atawahesabia haki Mataifa kwa imani, lilimhubiri Ibrahimu habari njema zamani, kusema, Katika wewe Mataifa yote watabarikiwa. Basi hao walio wa imani hubarikiwa pamoja na Ibrahimu aliyekuwa mwenye imani

Wakristo ni watoto wa Mungu kwa njia  imani na ahadi inayotenda kazi kupitia uwezo wa Roho Mtakatifu, na kwamba tunapokea wokovu kwa neema na si kwa juhudi wala kwa matendo ili awaye yote asijisifu:-

Waefeso 2:4-9 “Lakini Mungu, kwa kuwa ni mwingi wa rehema, kwa mapenzi yake makuu aliyotupenda; hata wakati ule tulipokuwa wafu kwa sababu ya makosa yetu; alituhuisha pamoja na Kristo; yaani, tumeokolewa kwa neema. Akatufufua pamoja naye, akatuketisha pamoja naye katika ulimwengu wa roho, katika Kristo Yesu; ili katika zamani zinazokuja audhihirishe wingi wa neema yake upitao kiasi kwa wema wake kwetu sisi katika Kristo Yesu. Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu; wala si kwa matendo, mtu awaye yote asije akajisifu.”

Katika imani ye Kikristo tunapata kila tunachokipata kwa neema na sio kwa matendo au bidii za kibinadamu hii iko katika kaisha ya kawaida na katika maisha ya wito wa kumtumikia Mungu hakuna juhudi wala matakwa ya kibinadamu bali ya Mungu

Warumi 9:14-15 “Maana amwambia Musa, Nitamrehemu yeye nimrehemuye, nitamhurumia yeye nimhurumiaye. Basi, kama ni hivyo, si katika uwezo wa yule atakaye, wala wa yule apigaye mbio; bali wa yule arehemuye, yaani, Mungu.”

Hata Mungu anapoita watu katika utumishi huu anawaita watu kwa neema yake na sio kwa kujipendekeza au kwa kujidhani ya kuwa ninafaa, wako watu wanaweza kujidhania kuwa wanafaa kuwa watumishi wa Mungu na wengine hawafai, au mtu akajikinai akifikiri yeye ni zaidi ya mwingine jambo la namna hii pia liko kinyume na ile dhana ya kiungu, Mungunhuchagua vile tunavyovidhania kuwa havifai, kumbuka lililotyukuka kwa mwanadamu ni chukizo kwa Mungu!

1Wakoritho 1:26-29 “Maana, ndugu zangu, angalieni mwito wenu, ya kwamba si wengi wenye hekima ya mwilini, si wengi wenye nguvu, si wengi wenye cheo walioitwa; bali Mungu aliyachagua mambo mapumbavu ya dunia awaaibishe wenye hekima; tena Mungu alivichagua vitu dhaifu vya dunia ili aviaibishe vyenye nguvu; tena Mungu alivichagua vitu vinyonge vya dunia na vilivyodharauliwa, naam, vitu ambavyo haviko, ili avibatilishe vile vilivyoko; mwenye mwili awaye yote asije akajisifu mbele za Mungu.”  

Tunawezaje kujua kuwa hawa ni wana wa Muungwana na hawa ni wana wa kijakazi? Maandiko yanaeleza wazi kuwa wana wa muungwana walizaliwa kwa ahadi na wana wa kijakazi walizaliwa kwa mapenzi ya mwili na hivyo tunaweza kuwatambua kwa matendo yao, wale waliokuwa wakiliudhi kanisa na kulitesa ndio wana wa kijakazi na wale waliowapole na waungwana Paulo ana sema

Wagalatia 4:29 “Lakini kama vile siku zile yule aliyezaliwa kwa mwili alivyomwudhi yule aliyezaliwa kwa Roho, ndivyo ilivyo na sasa

Wana wa kijakzi ni wale waliozaliwa kwa mwili na wana wa muungwana ni wale waliozaliwa kwa ahadi na uweza wa Roho Mtakatifu na matunda yao unaweza unaweza kuwatambua

Wagalatia 5:19-21 “Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo, katika hayo nawaambia mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu.”

Wagalatia 5:22-24 “Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria. Na hao walio wa Kristo Yesu wameusulibisha mwili pamoja na mawazo yake mabaya na tamaa zake

-          Wana wa mjakazi hawashindwi kuua  mtu, mioyo yao imejawa na chuki na uchungu ni wakatili na hawana huruma ona Mwanzo 4:1-11 “Adamu akamjua Hawa mkewe; naye akapata mimba, akamzaa Kaini, akasema, Nimepata mtoto mwanamume kwa BWANA. Akaongeza akamzaa ndugu yake, Habili. Habili alikuwa mchunga kondoo, na Kaini alikuwa mkulima ardhi.     Ikawa hatimaye Kaini akaleta mazao ya ardhi, sadaka kwa BWANA. Habili naye akaleta wazao wa kwanza wa wanyama wake na sehemu zilizonona za wanyama. BWANA akamtakabali Habili na sadaka yake; bali Kaini hakumtakabali, wala sadaka yake. Kaini akaghadhibika sana, uso wake ukakunjamana. BWANA akamwambia Kaini, Kwa nini una ghadhabu? Na kwa nini uso wako umekunjamana? Kama ukitenda vyema, hutapata kibali? Usipotenda vyema dhambi iko, inakuotea mlangoni, nayo inakutamani wewe, walakini yapasa uishinde. Kaini akamwambia Habili nduguye, [Twende uwandani]Ikawa walipokuwapo uwandani, Kaini akamwinukia Habili nduguye,akamwua. BWANA akamwambia Kaini, Yuko wapi Habili ndugu yako? Akasema, Sijui, mimi ni mlinzi wa ndugu yangu? Akasema, Umefanya nini? Sauti ya damu ya ndugu yako inanililia kutoka katika ardhi. Basi sasa, umelaaniwa wewe katika ardhi, iliyofumbua kinywa chake ipokee damu ya ndugu yako kwa mkono wako; utakapoilima ardhi haitakupa mazao yake; utakuwa mtoro na mtu asiye na kikao duniani.”

 

-          Hawaishi kuwa na Makundi wala Mafarakano  1Wakoritho 3:1-9 “Lakini, ndugu zangu, mimi sikuweza kusema nanyi kama na watu wenye tabia ya rohoni, bali kama na watu wenye tabia ya mwilini, kama na watoto wachanga katika Kristo. Naliwanywesha maziwa sikuwalisha chakula; kwa kuwa mlikuwa hamjakiweza. Naam, hata sasa hamkiwezi,kwa maana hata sasa ninyi ni watu wa tabia ya mwilini. Maana, ikiwa kwenu kuna husuda na fitina, je! Si watu wa tabia ya mwilini ninyi; tena mnaenenda kwa jinsi ya kibinadamu? Maana hapo mtu mmoja asemapo, Mimi ni wa Paulo; na mwingine, Mimi ni wa Apolo, je! Ninyi si wanadamu?Basi Apolo ni nani? Na Paulo ni nani? Ni wahudumu ambao kwao mliamini; na kila mtu kama Bwana alivyompa. Mimi nilipanda, Apolo akatia maji; bali mwenye kukuza ni Mungu. Hivyo, apandaye si kitu, wala atiaye maji, bali Mungu akuzaye. Basi yeye apandaye, na yeye atiaye maji ni wamoja, lakini kila mtu atapata thawabu yake mwenyewe sawasawa na taabu yake mwenyewe.Maana sisi tu wafanya kazi pamoja na Mungu; ninyi ni shamba la Mungu, ni jengo la Mungu.

 

-          Wanaweza kupelekana hata mahakamani  wala kudhulumiana 1Wakorintho 6:1-10 “ Je! Mtu wa kwenu akiwa ana daawa juu ya mwenzake athubutu kushitaki mbele ya wasio haki, wala si mbele ya watakatifu?Au hamjui ya kwamba watakatifu watauhukumu ulimwengu? Na ikiwa ulimwengu utahukumiwa na ninyi, je! Hamstahili kukata hukumu zilizo ndogo? Hamjui ya kuwa mtawahukumu malaika, basi si zaidi sana mambo ya maisha haya? Basi, mkiwa na mahali panapohukumiwa mambo ya maisha haya, mwawaweka kuwa waamuzi hao waliohesabiwa kuwa si kitu; katika kanisa? Nasema hayo nipate kuwatahayarisha. Je! Ndivyo, kwamba kwenu hakuna hata mtu mmoja mwenye hekima, awezaye kukata maneno ya ndugu zake? Bali mwashitakiana, ndugu kwa ndugu, tena mbele yao wasioamini. Basi imekuwa upungufu kwenu kabisa kwamba mnashitakiana ninyi kwa ninyi. Maana si afadhali kudhulumiwa? Maana si afadhali kunyang'anywa mali zenu? Bali kinyume cha hayo ninyi wenyewe mwadhulumu watu na kunyang'anya mali zao; naam, hata za ndugu zenu. Au hamjui ya kuwa wadhalimu hawataurithi ufalme wa Mungu? Msidanganyike; waasherati hawataurithi ufalme wa Mungu, wala waabudu sanamu, wala wazinzi, wala wafiraji, wala walawiti, wala wevi, wala watamanio, wala walevi, wala watukanaji, wala wanyang'anyi.”

Unapoangalia kwa kina na upana na urefu, watu wenye matendo haya ya mwilini wanaweza kuwapo hata makanisani katika siku za leo,  na wanaweza kuwa na muda mrefu sana katika wokovu au hata kufikia ngazi Fulani ya kiroho lakini maandiko yanasema mtawatambua kwa matunda yao, kuwajua wana wa muungwa na wana wa kijakazi kwa mujibu wa maandiko ni rahisi sana kila mmoja anapaswa kujihoji na kujichunguza kama ni mwana wa Muuungwana au ni mwana wa kijakazi na kama ni wa kijakazi au kuna tabia ya kijakazi hatuna budi kutubu na kubadilika , tuongeweze neema

 

Na Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa Wajenzi mwenye Hekima!



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni