Alhamisi, 21 Julai 2022

Waachie watu wangu waende!


Kutoka 3:7-10 “BWANA akasema, Hakika nimeyaona mateso ya watu wangu walioko Misri, nami nimekisikia kilio chao kwa sababu ya wasimamizi wao; maana nayajua maumivu yao; nami nimeshuka ili niwaokoe na mikono ya Wamisri, niwapandishe kutoka nchi ile, hata nchi njema, kisha pana; nchi ijaayo maziwa na asali; hata mahali pa Mkanaani, na Mhiti, na Mwamori, na Mperizi, na Mhivi, na Myebusi. Basi, tazama, kilio cha wana wa Israeli kimenifikilia; tena nimeyaona hayo mateso ambayo Wamisri wanawatesa. Haya, basi, nitakutuma sasa kwa Farao, ili upate kuwatoa watu wangu, hao wana wa Israeli, katika Misri.”



Utangulizi:

Tuwapo Duniani tunapitia changamoto za aina mbalimbali, ikiwa ni pamoja na mikandamizo ya aina mbalimbali kutoka kwa Shetani ambaye ndiye adui mkubwa wa maisha ya wanadamu, Mungu hafurahii uonevu au udhalimu wa aina yoyote ule unaowapata wanadamu, Wana wa Israel kwa Muda mrefu sana walikuwa wakionewa na wamisri na wakikandamizwa ili waendelee kuwa watumwa katika nchi ya Misri, hawakuweza kutoka, na adui hakutaka kuwaachia kwa haraka mpaka Mungu alipoamua kuingilia kati.

Mungu alimtuma Musa kwa mfalme wa Misri yaani Farao ili amuamuru mfalme huyu awaachie wana wa Israel waende zao kwa kusudi alilolikusudia Mungu mwenyewe yaani wakamtumikie Mungu na kutimiza kusudi lake, Ujumbe mkubwa aliopewa Musa ulikuwa ni kumwambia Farao Mungu wa ewaebrania ameamuru uwaachie watu wake waende, WAACHE WATU WANGU WAENDE hii ilikuwa ni Amri na sio ombi ujumbe huu umerudiwa tena na tena kwa farao waachie watu wangu waende ona katika maandiko yafuatayo:-

Kutoka 5:1  Hata baadaye, Musa na Haruni wakaenda wakamwambia Farao, wakasema, BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi, WAPE WATU WANGU RUHUSA WAENDE, ili kunifanyia sikukuu jangwani.”

Unaona sifurahiswi kwa namna fulani na lugha inayotumika katika Kiswahili kwa sababu yenyewe iko katika mfumo wa kiungwana nani kama  ombi WAPE WATU WANGU RUHUSA WAENDE kimsingi Mungu hakuwa anaomba ruhusa Mungu alikuwa anaamuru ni amri kwa Farao WAACHIE WATU WANGU WAENDE, Lugha ya kiingereza katika maeneo yote yanayozungumzia WAPE WATU WANGU RUHUSA WAENDE  inatumia AMRI lugha inayotumika kiingereza ni neno LET MY PEOPLE GO sawa na kuamuru Waachie watu wangu waende ni aina hii ya lugha ndio inayojirudia rudia kila mahali kwenye kitabu cha kutoka  na maeneo mengine na unaweza kuona ;-

Kutoka 8:1 “BWANA akamwambia Musa, Ingia kwa Farao, ukamwambie, BWANA asema hivi, Wape watu wangu ruhusa, ili wapate kunitumikia.”

Kutoka 8:20 “BWANA akamwambia Musa, Inuka asubuhi na mapema usimame mbele ya Farao; angalia! Atoka aende majini; kamwambie, BWANA asema, Wape watu wangu ruhusa waende zao, ili wanitumikie mimi.”

Kutoka 9:1 “Ndipo BWANA akamwambia Musa, Ingia wewe kwa Farao, umwambie, BWANA, Mungu wa Waebrania, yuasema, Wape ruhusa watu wangu ili waende wanitumikie.”

Kutoka 9:16-17 “lakini, nilikusimamisha wewe kwa sababu hii hii, ili nikuonyeshe uweza wangu, tena kwamba jina langu litangazwe katika dunia yote. Nawe, je! Hata sasa wajitukuza juu ya watu wangu, usiwape ruhusa waende zao”?          

Unaona ni kwanini Mungu amerudia mara kwa mara kwa msisitizo waache watu wangu waende? Mungu hafurahii udhalimu, ukandamizaji na mateso ambayo kwaasili watu wake wanayapitia Mungu aliamua kuingilia katika hali ya wana wa Israel kwa kuwa walikuwa wanaonewa na wamisri na wamisri ndio walikuwa wenye nguvu zaidi kuliko Israel, Mungu hakubaliani na uonevu wa aina yoyote ile:-

Uonevu ni nini hasa!

1.       Ni kukandamizwa na kuwekwa chini ya mamlaka ya mtu mwingine mwenye nguvu zaidi yako bila matakwa yako mwenyewe

2.       Ni kuonewa au kuteswa na nguvu Fulani iliyojuu zaidi ya uwezo wako wa kawaida, bila uhuru kamili

3.       Uonevu hauko katika eneo moja tu, unaweza kuweko katika mwili, katika akili, katika nafsi, katika ndoa, katika fedha katika Elimu,Biashara, haki na kadhalika  na pia uko uonevu wa kiroho au tunaweza kusema kuwa asili yauonevu wa aina yoyote unaouona ni kutokea rohoni au katika ulimwengu wa kiroho;

Hatuna budi kugundua na kubaini ni maeneo gani ya uonevu shetani anatuonelea ili tuweze kuliitia jina la Mungu atuokoe, kumbuka Israel waliteseka mpaka pale walipolia na kutafuta msaada wa Mungu ndipo Mungu aliposhuka ili awaokoe ona Zaburi 118:5 “Katika shida yangu nalimwita BWANA; BWANA akanijibu akaniweka panapo nafasi.” Unaona kila shida unayoipitia kama mwanadamu hakikisha ya kuwa unamuita Bwana yaani Mungu naye atakuweka panapo nafasi yaani atakujibu na kutatua tatizo ulilonalo usinyamaze ukafikiri ya kuwa Mungu amekusahau, HAPANA Mungu anakutaka uwajibike na kufanya sehemu yako kwa kukataa hali unayoipitia.

Zaburi 42:9 “Nitamwambia Mungu, mwamba wangu, Kwa nini umenisahau? Kwa nini ninakwenda nikihuzunika, adui wakinionea?

Mwandishi wa zaburi aliamua kuomba Mungu Mwamba wake aliona kama amesahaulika adui alikuwa akimuonea na hakuwa na furaha alikumbuka kumwambia Mungu, ni lazima tumlilie Mungu atutoe katika hali zozote za mikandamizo tunazozipitia duniani kumbuka kuwa ni ahadi ya Mungu kutuweka huru kutoka kwa wale wanaotuonea, Mungu ameahidi kwamba utakuwa mbali na kunewa ona  

Isaya 54:14. “Utathibitika katika haki; utakuwa mbali na kuonewa, kwa maana hutaogopa; na mbali na hofu, kwa maana haitakukaribia.”

Wakati wowote uonevu sio jambo zuri, maandiko yanasema uonevu humfanya mtu awe kama kichaa, Moja ya sababu ya kuja kwa Yesu Kristo duniani kama Mwokozi ni pamoja na kufanya kazi ya kuwafungua walioonewa ona Matendo 10:38 “habari za Yesu wa Nazareti, jinsi Mungu alivyomtia mafuta kwa Roho Mtakatifu na nguvu naye akazunguka huko na huko, akitenda kazi njema na kuponya wote walioonewa na Ibilisi; kwa maana Mungu alikuwa pamoja naye.” Adui yetu mkuu adui wa wanadamu wote na anayetuonea ni shetani yeye hutuonea katika mazingira mbalimbali na wakati mwingine anawatumia watu kuleta uonevu, shetani na mapepo na maajenti wake wanaweza kumuonea mwanadamu katika maeneo zaidi ya kumi na tano:-

·         Unaweza kuonewa Mwili

·         Unaweza kuonewa kwa asili

·         Unaweza kuonewa kiakili

·         Unaweza kuonewa Kiroho

·         Unaweza kuonewa katika Ndoa yako

·         Unaweza kuonewa kiuchumi

·         Unaweza kuonewa Kazini

·         Unaweza kuonewa katika ndoto

·         Unaweza  kuonewa kwa maneno

·         Unaweza kuonewa kihisia/Kisaikolojia/kijinsia.

·         Unaweza kuonewa kichawi

·         Unaweza kuonewa kwa ukoo mzima mnateswa ukoo wenu wote au familia yenu yote

·         Unaweza kuonewa kwa nguvu na uonevu wa kukandamizwa

·         Unaweza kuonewa katika haki zako makahamani

·         Unaweza kuonewa bila sababu

·         Unaweza kuonewa kwa sababu

·         Unaweza kuonewa kihuduma

Maandiko yanaonyesha kuwa kila aina ya uonevu hutoka kwa shetani Yohana 10:10Mwivi haji ila aibe na kuchinja na kuharibu; mimi nalikuja ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele.” Ni kwa sababu ya kuonewa kwa namna mbalimbali Mungu alimpaka Yesu Mafuta ili aweze kuwakomboa wanadamu, na Mungu vilevile huwapaka watumishi wake mafuta ili kuzivunja nira za uonevu ona Luka 4:18-19 “Roho wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa, Na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa.” Unaona Lugha inayotumika hapo kusetwa maana yake ni kuonewa huduma ya kimasihi ilitolewa na Mungu kwa wanadamu kwa kusudi la kuwaweka watu huru kutoka katika uonevu wa kila namna, kama Musa ambaye alikuwa na ujumbe waache watu wangu waende, Yesu ana ujumbe ulio bora zaidi katika ufalme wa ibilisi kumuamuru kwa jina lake kukuacha uwe huru kutoka katika aina yako ya mgandamizo uliyo nayo!

Tunawezaje basi kutoka katika migandamizo ya shetani.

1.       Kubali zawadi ya wokovu:

Ni ukweli ulio wazi kuwa wokovu ni msamaha wa dhambi, nani ukweli ulio wazi kuwa Mungu anatuhurumia na mgandamizo mkubwa na wa kwanza alionao mwanadamu ni kuwa katika maisha ya dhambi, dhambi yenyewe ikukutawala inakugeuza kuwa mtumwa inakukandamiza, wanadamu wengi wanakandamizwa na dhambi hivyo ni watumwa wa dhambi hawawezi kuimudu na hawawezi kuishinda ona Yohana 8:34 “Yesu akawajibu, Amin, amin, nawaambia, Kila atendaye dhambi ni mtumwa wa dhambi.” Matatizo mengi ya wanadamu yamesababishwa na dhambi, mtu anayedumu katika dhambi naye ni mtumwa wa dhambi, dhambi ni mlango mkubwa wa mashambulizi mengi ya adui katika maisha yetu na uharibifu wa kila namna,  wakati mwingine utaweza kuona mtu aliposamehewa dhambi hapo hapo alipata na uponyaji wa mwili na akili na roho ona Zaburi 103:3 “Akusamehe maovu yako yote, Akuponya magonjwa yako yote,” unaona Mungu anaposamehe dhambi katika kifurushi kimoja hikihiki cha msamaha anatoa na uponyaji kwa hivyo kimaandiko ni dhahiri kwamba dhambi ikiondoka kwetu ni rahisi sana kuwa huru katika maeneo mengine Yohana 5:14 “Baada ya hayo Yesu akamkuta ndani ya hekalu, akamwambia, Angalia, umekuwa mzima; usitende dhambi tena, lisije likakupata jambo lililo baya zaidi.” Unaona yako mateso mengine ambayo yana uhusiano wa moja kwa moja na dhambi japo sio yote hivyo Mungu anapotusamehe dhambi basi moja kwa moja anatuweka huru vile vile na kutupa uzima wa maeneo mengine, unapokuwa kwenye dhambi unapoteza haki zako nyingi ikiwa ni pamoja na ulinzi wa Mungu na hivyo adui anakuwa na mamlaka ya kukuonea lakini wokovu unapokuja kwetu tunapewa haki yetu

 

Warumi 6:16-20 “Hamjui ya kuwa kwake yeye ambaye mnajitoa nafsi zenu kuwa watumwa wake katika kumtii, mmekuwa watumwa wake yule mnayemtii, kwamba ni utumishi wa dhambi uletao mauti, au kwamba ni utumishi wa utii uletao haki. Lakini Mungu na ashukuriwe, kwa maana mlikuwa watumwa wa dhambi, lakini mliitii kwa mioyo yenu ile namna ya elimu ambayo mliwekwa chini yake; na mlipokwisha kuwekwa huru mbali na dhambi, mkawa watumwa wa haki. Nasema kwa jinsi ya kibinadamu kwa sababu ya udhaifu wa miili yenu. Kwa kuwa kama mlivyovitoa viungo vyenu vitumiwe na uchafu na uasi mpate kuasi, vivyo hivyo sasa vitoeni viungo vyenu vitumiwe na haki mpate kutakaswa. Kwa maana mlipokuwa watumwa wa dhambi, mlikuwa huru mbali na haki.”

 

Uko uhusiano mkubwa sana wa mafanikio yetu ya kiroho yaani wokovu na afya yetu Yakobo 5:13-15 “Mtu wa kwenu amepatikana na mabaya? Na aombe. Ana moyo wa kuchangamka? Na aimbe zaburi. Mtu wa kwenu amekuwa hawezi? Na awaite wazee wa kanisa; nao wamwombee, na kumpaka mafuta kwa jina la Bwana. Na kule kuomba kwa imani kutamwokoa mgonjwa yule, na Bwana atamwinua; hata ikiwa amefanya dhambi, atasamehewa.”


3Yohana 1:2 “Mpenzi naomba ufanikiwe katika mambo yote na kuwa na afya yako kama vile roho yako ifanikiwavyo

 

Unaona kwa hiyo kuipokea zawadi ya wokovu ni kwa Muhimu na msingi wa kufunguliwa kwetu kutoka katika migandamizo ya namna mbalimbali wokovu una uhusiano mkubwa na kusamehewa dhambi Luka 1:77 “Uwajulishe watu wake wokovu, Katika kusamehewa dhambi zao.”  Na Mafanikio yetu katika mambo yote asili yake ni mafanikio ya roho zetu, Ni kwaajili ya ukombozi wa Mwanadamu Mungu alimtuma Yesu duniani ili kila anayemwamini awe na uzima wa milele kwa hivyo tunapata uzima huu na uzima wa milele, Yesu alitolewa pale msalabani na kuteswa na kuuawa ili sisi tuweze kupona katika maeneo yote kama asemavyo nabii Isaya mahali Fulani hivi:-

 

Isaya 53:3-5 “Alidharauliwa na kukataliwa na watu; Mtu wa huzuni nyingi, ajuaye sikitiko; Na kama mtu ambaye watu humficha nyuso zao, Alidharauliwa wala hatukumhesabu kuwa kitu. Hakika ameyachukua masikitiko yetu, Amejitwika huzuni zetu; Lakini tulimdhania ya kuwa amepigwa, Amepigwa na Mungu, na kuteswa. Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, Alichubuliwa kwa maovu yetu; Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona.”

 

Kumbe ni ukweli ulio wazi kuwa tukimwamini Bwana Yesu kazi yake aliyoifanya pale msalabani na kuikubali kama zawadi tutaokolewa, Na ndani ya wokovu tutapata raha nyingi sana nafsini mwetu wokovu huwa na ukombozi mkubwa na wa aina nyingi. Yesu alikuwa ameahidi tujitie nira yake ili tusilemewe na mizigo yaani utumwa wa namna mbalimbali Mathayo 11:28-29 “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu;”    

 

2.       Uwe na ufahamu wa neno la Mungu.

 

Ufunuo 12:10-11 “Nikasikia sauti kuu mbinguni, ikisema, Sasa kumekuwa wokovu, na nguvu, na ufalme wa Mungu wetu, na mamlaka ya Kristo wake; kwa maana ametupwa chini mshitaki wa ndugu zetu, yeye awashitakiye mbele za Mungu wetu, mchana na usiku. Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo, na kwa neno la ushuhuda wao; ambao hawakupenda maisha yao hata kufa.”

 

Neno la ushuhuda maana yake ni neno la Mungu, neno la Mungu lina nguvu na mamlaka kubwa sana kuliko tunavyodhani lenyewe linafananishwa na nyundo ivunjayo mawe vipande vipande ona Yeremia 23:28-29 “Nabii aliye na ndoto, na aseme ndoto yake; na yeye aliye na neno langu, na aseme neno langu kwa uaminifu. Makapi ni kitu gani kuliko ngano? Asema Bwana. Je! Neno langu si kama moto? Asema Bwana; na kama nyundo ivunjayo mawe vipande vipande?

 

Unaona iwapo unataka ushindi katika maisha yako huna budi kujaa neno, Neno linafananishwa na moto au nyundo ivunjayo mawe vipande vipande, hivyo tukiujaza ufahamu wetu kwa neno la Mungu kila aina ya utumwa itavunjika haijalishi ni utumwa  wa zamani kiasi gani, au ni wenye nguvu kiasi gani wala haijalishi ni nani ametuweka kwenye utumwa huo, au utumwa huo unatokea wapi?, kinga kubwa na ya kipekee na silaha ya kumshambulia adui na kupata ushindi ni neno la Mungu.

 

Waebrania 4:12-13 “Maana Neno la Mungu li hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili, tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta yaliyomo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo. Wala hakuna kiumbe kisichokuwa wazi mbele zake, lakini vitu vyote vi utupu na kufunuliwa machoni pake yeye aliye na mambo yetu.”       

 

Kamwe tusilidharau neno la Mungu wala kulichukulia kama kitu cha kawaida neno la uzima linga nguvu ya kubadili kila kitu katika maisha yetu neno la Mungu linapotamkwa huwa haliendi bure ni lazima litatimiza mapenzi ya Mungu ona

 

Isaya 55:9-11 “Kwa maana kama vile mbingu zilivyo juu sana kuliko nchi, kadhalika njia zangu zi juu sana kuliko njia zenu, na mawazo yangu kuliko mawazo yenu. Maana kama vile mvua ishukavyo, na theluji, kutoka mbinguni, wala hairudi huko; bali huinywesha ardhi, na kuizalisha na kuichipuza, ikampa mtu apandaye mbegu, na mtu alaye chakula; ndivyo litakavyokuwa neno langu, litokalo katika kinywa changu; halitanirudia bure, bali litatimiza mapenzi yangu, nalo litafanikiwa katika mambo yale niliyolituma.”

 

Neno la Mungu ni roho tena ni uzima Yohana 6:63 “Roho ndiyo itiayo uzima, mwili haufai kitu; maneno hayo niliyowaambia ni roho, tena ni uzima.”               

 

Muda usingeweza kutosha kupitia maeneo kadhaa wa kadhaa yanayotufundisha kuhusu neno la Mungu ni ukweli ulio wazi kuwa Yesu alipopandishwa katika mlima wa majaribu alikutana na shetani na kwa kutumia neno la Mungu aliweza kupata ushindi mkubwa hakuweza kujitia chini ya ushawishi na majaribu ya yule Muovu, tunaweza kushinda hali zozote zile endapo tutakuwa na tabia ya kutafuta neno la Mungu linazungumza nini kutokana na hali yetu na ile hali tunayokumbana nayo na tukajiweka huru!

 

3.       Omba kwaajili ya ukombozi.

 

Mwanadamu anapokuwa anakandamizwa na ibilisi katika maeneo mbalimbali, kumbuka kuwa huwezi kujitoa mwenyewe katika maeneo hayo, ni lazima umuombe Mungu aje akupe msaada wa ukombozi, akukomboe kutoka katika hali unayoipitia, Neno ukombozi limetajwa mara 147 katika maandiko, Yesu ni mwokozi maana yake vilevile ni Mkombozi,  watu waliokuwa wanatazamia kuzaliwa kwa Masihi vilevile wanaitwa watu waliokuwa wakiutazamia ukombozi

 

Luka 2:36-38 “Palikuwa na nabii mke, jina lake Ana, binti Fanueli, wa kabila ya Asheri, na umri wake ulikuwa miaka mingi, alikuwa amekaa na mume miaka saba baada ya uanawali wake. Naye ni mjane wa miaka themanini na minne; haondoki katika hekalu, ila huabudu usiku na mchana kwa kufunga na kuomba.Huyu alitokea saa ile ile akamshukuru Mungu, na wote waliokuwa wakiutarajia ukombozi katika Yerusalemu akawatolea habari zake.”

 

Yesu kwa kuwa ni Mkombozi ni vema tunapopita taabuni ni muhimu kuliitia jina lake kwaajili ya ukombozi, kwanini kwa sababu maandiko yanaonyesha ya kuwa ndani yake yeye tunao ukombozi, Waefeso 1:6-7 “Na usifiwe utukufu wa neema yake, ambayo ametuneemesha katika huyo Mpendwa. Katika yeye huyo, kwa damu yake, tunao ukombozi wetu, masamaha ya dhambi, sawasawa na wingi wa neema yake.” Kwa hiyo tunakubaliana kuwa kuna ukombozi na huu hufanywa na Yesu Kristo kwa neema yake, Yeye alijitoa mwenyewe ili atukomboe sisi

 

Tito 2:13-14 “tukilitazamia tumaini lenye baraka na mafunuo ya utukufu wa Kristo Yesu, Mungu mkuu na Mwokozi wetu; ambaye alijitoa nafsi yake kwa ajili yetu, ili atukomboe na maasi yote, na kujisafishia watu wawe milki yake mwenyewe, wale walio na juhudi katika matendo mema.”

 

1Wakorintho 1:30-31 “Bali kwa yeye ninyi mmepata kuwa katika Kristo Yesu, aliyefanywa kwetu hekima itokayo kwa Mungu, na haki, na utakatifu, na ukombozi; kusudi, kama ilivyoandikwa, Yeye aonaye fahari na aone fahari juu ya Bwana.”

 

Yesu kama mkombozi wetu yu aweza kutukomboa nafsi zetu miili yatu na roho zetu, Mungu alimkomboa Daudi katika shida zake zote na hakusahau jambo hili katika maisha yake yote, kumbe tunaweza kupitia shida na mateso ya aina mbalimbali lakini Mungu anaweza kutukomboa na shida zote ona 1Wafalme 1:30 “Naye mfalme akaapa, akasema, Bwana aishivyo, aliyenikomboa roho yangu katika shida zoteKristo Yesu anaweza kutukomboa na shida zetu zote maana yake kila eneo ambalo kwalo adui anakusudia kutukandamiza au anatukandamiza tayari tunaye mkombozi,  tunaweza kukombolewa, familia zetu, maisha yetu, ndoa zetu, uchumi wetu,  na hata kama tunadhani kuwa tuna laana ya aina yoyote laana hizo zinaweza kukombolewa kupitia Jina la Yesu, Lakini vilevile kwa imani katika kazi yake aliyoifanya pale Msalabani

 

Wagalatia 3:13-14 “Kristo alitukomboa katika laana ya torati, kwa kuwa alifanywa laana kwa ajili yetu; maana imeandikwa, Amelaaniwa kila mtu aangikwaye juu ya mti; ili kwamba baraka ya Ibrahimu iwafikilie Mataifa katika Yesu Kristo, tupate kupokea ahadi ya Roho kwa njia ya imani.”

 

Ni wajibu wetu kama waamini kuutarajia ukombozi Zaburi 130:7-8 “Ee Israeli, umtarajie Bwana; Maana kwa Bwana kuna fadhili, Na kwake kuna ukombozi mwingi.Yeye atamkomboa Israeli na maovu yake yote.”  Mungu ameahidi kuwa tumtarajie yeye, kumtarajia maana yake kumsubiria, kumgojea katika njia ya Maombi, na kumtazamia, tunapaswa kuiamini ahadi hii ya Mungu na kumuomba ukombozi katika maeneo mbalimbali tunayokandamizwa, Yeye ana uwezo wa kutukomboa katika taabu zote, tunapomlilia yeye hutuponya na taabu zetu zote na kutukomboa  Zaburi 107:1-6. “Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema, Kwa maana fadhili zake ni za milele. Na waseme hivi waliokombolewa na Bwana, Wale aliowakomboa na mkono wa mtesi. Akawakusanya kutoka nchi zote, Mashariki na magharibi, kaskazini na kusini. Walitanga-tanga jangwani katika njia ya nyika; Hawakuona mji wa kukaa. Waliona njaa, waliona na kiu, Nafsi yao ilikuwa ikizimia ndani yao. Wakamlilia Bwana katika dhiki zao, Akawaponya na shida zao.”

 

Tukimlilia Mungu na kumuomba yeye atatuma ukombozi katika maisha yetu Zaburi 111:9 “Amewapelekea watu wake ukombozi, Ameamuru agano lake liwe la milele, Jina lake ni takatifu la kuogopwa.”

 

Hatuna budi kumuomba Mungu na kumlilia ili atukomboe na kutuachia kila mmoja asiwe chini ya uonevu na kukandamizwa na ibilisi, Mungu na amuweke huru kila mmoja na familia yake na ndugu zake na jamaa zake, Mungu atupe kuwa mbali na uonevu, Mungu na atuthibitishe katika haki!, hatuna budi kumuomba Mungu atukomboe na roho zote chafu za uharibifu, kiburi, migawanyiko, woga, uzushi, mikandamizo, rushwa, uchafu, ufisadi, tamaa, mashaka, kutokusamehe, upotoshaji, uvivu, uchawi, utapeli, uasi, hasira, ulevi, Mauti, maluweluwe, uchungu, zinaa na uasherati, ulafi, choyo, ubinafsi,  na mambo yanayofanana na hayo!.

 

4.       Tumia silaha ya kusifu:

 

Moja ya silaha Muhimu ya ukombozi wetu kutoka kwa Mungu kwa mujibu wa maandiko ni pamoja na kumsifu Mungu, Yesu aliwafundisha wanafunzi wake kuanza maombi kwa Msingi wa kumsifia Mungu kumuheshimu na kumtukuza yaani kumsifu Luka 11:1-2 “Ikawa alipokuwa mahali fulani akiomba, alipokwisha, mmoja katika wanafunzi wake alimwambia, Bwana, tufundishe sisi kusali, kama vile Yohana alivyowafundisha wanafunzi wake. Akawaambia, Msalipo, semeni, Baba [yetu uliye mbinguni], Jina lako litakaswe, Ufalme wako uje, [Mapenzi yako yatimizwe, hapa duniani kama huko mbinguni.] Kusifu ni mlango au ufunguo wa kuingilia katika nyua yaani katika ukumbi wa Mungu kwaajili ya kupokea huduma na majibu ya mahitaji yetu Zaburi 100:1-5 “Mfanyieni Bwana shangwe, dunia yote; Mtumikieni Bwana kwa furaha; Njoni mbele zake kwa kuimba; Jueni kwamba Bwana ndiye Mungu; Ndiye aliyetuumba na sisi tu watu wake; Tu watu wake, na kondoo wa malisho yake. Ingieni malangoni mwake kwa kushukuru; Nyuani mwake kwa kusifu; Mshukuruni, lihimidini jina lake; Kwa kuwa Bwana ndiye mwema; Rehema zake ni za milele; Na uaminifu wake vizazi na vizazi.” Kwa hiyo tunapoenda mbele za Mungu kwa ibada ya aina yoyote ile ikiwa ni pamoja na maombi ni muhimu kuanza na kusifu kwa sababu sifa kwa Mungu inafungua mambo mengi na kumfanya Bwana atujali, na kutusikiliza, Zaburi 29:1-2 “Mpeni Bwana, enyi wana wa Mungu, Mpeni Bwana utukufu na nguvu; Mpeni Bwana utukufu wa jina lake; Mwabuduni Bwana kwa uzuri wa utakatifu.” Kwa nini maandiko yaaagiza kuanza ibada au maombi kwa kumsifu Mungu? Ziko sababu kadhaa wa kadhaaa:-

 

1.       Kusifu kunaandaa mioyo yetu kumwangalia Mungu huku tukiwa tunatambua sifa zake, tunapoaishwa kupelekwa kwenye uwepo wake na kutusaidia kuelewa ukuu wake pale tunapomuendea  lakini sio hivyo tu sifa zina tabia ya kuufanya uwepo wa Mungu kushuka na kutuhudumia 2Nyakati 5:13 “tena Walawi waimbaji, wote pia, yaani Asafu, na Hemani, na Yeduthuni, na wana wao, na ndugu zao, hali wamevaa kitani safi, wenye matoazi na vinanda na vinubi, wamesimama upande wa mashariki wa madhabahu, na pamoja nao makuhani mia na ishirini wakipiga panda;) hata ikawa, wenye panda na waimbaji walipokuwa kama mmoja, wakisikizisha sauti moja ya kumsifu na kumshukuru Bwana nao wakipaza sauti pamoja na panda na matoazi na vinanda, wakimsifu Bwana, wakisema, Kwa kuwa ni mwema; kwa maana fadhili zake ni za milele; ndipo nyumba ikajawa na wingu, naam, nyumba ya Bwana,hata makuhani hawakuweza kusimama ili kufanya huduma yao, kwa sababu ya lile wingu; kwa kuwa nyumba ya Mungu imejaa utukufu wa Bwana.” Kumbuka ya kuwa Mungu anakaa katikati ya sifa Zaburi 22:3 -5 “Na Wewe U Mtakatifu, Uketiye juu ya sifa za Israeli.Baba zetu walikutumaini Wewe, Walitumaini, na Wewe ukawaokoa.Walikulilia Wewe wakaokoka, Walikutumaini wasiaibike.”

2.       Kusifu kunaharibu vifungo vya adui Kila kitu ambacho kinakandamiza maisha ya mwanadamu na kututishia katika uonevu wa aina yoyote ile kimwili na hata kiroho vinaweza kutiishwa na kuharibiwa kupitia Maombi Matendo 16:23-26 “Na walipokwisha kuwapiga mapigo mengi, wakawatupa gerezani, wakamwamuru mlinzi wa gereza awalinde sana. Naye akiisha kupata amri hii akawatupa katika chumba cha ndani, akawafunga miguu kwa mkatale. Lakini panapo usiku wa manane Paulo na Sila walikuwa wakimwomba Mungu na kumwimbia nyimbo za kumsifu, na wafungwa wengine walikuwa wakiwasikiliza. Ghafula pakawa tetemeko kuu la nchi, hata misingi ya gereza ikatikisika, na mara hiyo milango ikafunguka, vifungo vya wote vikalegezwa.”

3.       Kusifu na kuabudu kunamfanya adui achanganyikiwe na kupoteana, Hakuna silaha ya ajabu kama kumsifu Mungu na kumuabudu, silaha hii ni ya kipekee inapotumika katika tishio la kivita au uonevu Bila kujali kuwa jeshi lililojipanga ni kubwa kwa kiwango gani kumsifu Mungu kutatuletea ushindi wa kushangaza sana angalia 2Nyakati 20:1-4 “Ikawa baadaye, wana wa Moabu, na wana wa Amoni, na pamoja nao baadhi ya Wameuni, wakaja juu ya Yehoshafati vitani.Wakaja watu waliomwambia Yehoshafati, wakisema, Wanakuja jamii kubwa juu yako watokao Shamu toka ng'ambo ya bahari; na tazama, wako katika Hasason-tamari (ndio En-gedi).Yehoshafati akaogopa, akauelekeza uso wake amtafute Bwana; akatangaza mbiu ya watu kufunga katika Yuda yote.Yuda wakakusanyika pamoja ili wamtafute Bwana; hata kutoka miji yote ya Yuda wakaja kumtafuta Bwana.” Wakati majeshi ya wana wa Moabu na wana wa Amoni na Wameuni walipokuwa wameungana kinyume na mfalme Yeshoshafati, unaweza kuona pamoja na silaha yote ya kufunga na kumuomba Mungu safari hii maelekezo ya Mungu namna ya kupigana na kupata ushindi ilikuwa ni kupanga waimbaji ili wamsifu Mungu ona 2Nyakati 20:14-26 “Ndipo Yahazieli mwana wa Zekaria, mwana wa Benaya, mwana wa Yeieli, mwana wa Matania, Mlawi, wa wana wa Asafu, akajiliwa na roho ya Bwana, katikati ya kusanyiko; akasema, Sikieni, Yuda wote, nanyi mkaao Yerusalemu, na wewe mfalme Yehoshafati; Bwana awaambia hivi, Msiogope, wala msifadhaike kwa ajili ya jeshi kubwa hili; kwani vita si yenu bali ni ya Mungu. Kesho shukeni juu yao; tazameni, wanakwea kwa kupandia Sisi; nanyi mtawapata penye mwisho wa bonde, mbele ya jangwa la Yerueli. Hamtahitaji kupigana vita, jipangeni, simameni, mkauone wokovu wa Bwana ulio pamoja nanyi, enyi Yuda na Yerusalemu; msiogope, wala msifadhaike; kesho tokeni juu yao; kwa kuwa Bwana yu pamoja nanyi. Yehoshafati akainama kichwa, kifulifuli; wakaanguka mbele za Bwana Yuda wote na wakaao Yerusalemu, wakimsujudia Bwana. Na Walawi, wa wana wa Wakohathi na wa wana wa Wakorahi, wakasimama ili wamsifu Bwana, Mungu wa Israeli, kwa sauti kuu sana. Wakaamka asubuhi na mapema, wakaenda nje katika jangwa la Tekoa; nao walipokuwa wakitoka, Yehoshafati akasimama, akasema, Nisikieni, enyi Yuda nanyi wenyeji wa Yerusalemu; mwaminini Bwana, Mungu wenu, ndivyo mtakavyothibitika; waaminini manabii wake, ndivyo mtakavyofanikiwa. Naye alipokwisha kufanya shauri na watu, akawaweka wale watakaomwimbia Bwana, na kumsifu katika uzuri wa utakatifu, wakitoka mbele ya jeshi, na kusema, Mshukuruni Bwana; kwa maana fadhili zake ni za milele. Nao walipoanza kuimba na kusifu, Bwana akaweka waviziao juu ya wana wa Amoni, na Moabu, na wa mlima Seiri, waliokuja juu ya Yuda; nao wakapigwa. Kwani wana wa Amoni na wa Moabu waliwaondokea wenyeji wa mlima Seiri kuwaulia mbali na kuwaharibu; nao walipokwisha kuwakomesha hao wakaao Seiri, wakajitia kuharibu kila mtu mwenziwe. Hata Yuda walipofika mnara wa kulindia wa jangwani, wakalitazama hilo jeshi; nao, angalia, walikuwa maiti walioanguka nchi, wala hapana aliyeokoka. Nao Yehoshafati na watu wake walipokuja kuchukua nyara zao, wakaona kati yao wingi wa mali, na mavazi, na johari za thamani, walivyojivulia, zaidi kuliko wawezavyo kuchukua; wakawa siku tatu katika kuteka nyara, maana zilikuwa nyingi sana.Hata siku ya nne wakakusanyika katika bonde la Baraka; maana ndipo walipombarikia Bwana; kwa hiyo jina lake mahali pale pakaitwa Bonde la Baraka hata leo.”

Unaona kumbe hatupaswi kuwa na hofu iko njia nyepesi sana na silaha nzito ya kutukomboa nayo ni kumsifu Mungu, hii ni silaha kuu ya kiroho hatupaswi kwa namna yoyote kudhani au kufikiri kuwa wakati wa kumsifu Mungu ni wakati wa mzaha hapana ni wakati ambapo Mungu yuko kazini hivyo hatuna budi kumaanisha linapokuja swala la kumsifu Mungu Zaburi 8:2 “Vinywani mwa watoto wachanga na wanyonyao Umeiweka misingi ya nguvu; Kwa sababu yao wanaoshindana nawe; Uwakomeshe adui na mijilipiza kisasi.”  Watu wanapomsifu Mungu hata kama ni watoto kunakuwa na misingi ya nguvu na kukomesha adui na kujilipizia kisasi wote wanaoshindana nasi watatupwa nje kama tutagundua siri iliyoko katika sifa, kusifu kunatoa nguvu na kibali cha kuwafanyika hukumu dhidi ya adui zetu na wafalme wao Zaburi 149:5-9 “Watauwa na waushangilie utukufu, Waimbe kwa sauti kuu vitandani mwao. Sifa kuu za Mungu na ziwe vinywani mwao, Na upanga mkali kuwili mikononi mwao. Ili kufanya kisasi juu ya mataifa, Na adhabu juu ya kabila za watu. Wawafunge wafalme wao kwa minyororo, Na wakuu wao kwa pingu za chuma. Kuwafanyia hukumu iliyoandikwa; Hiyo ndiyo heshima ya watauwa wake wote. Haleluya.”               

 

Unaona kwa msingi huo hatuna budi wakati wote kukumbuka ya kuwa kumsifu Mungu ni silaha yenye nguvu kubwa na ya ajabu sana inayoweza kusukuma nyuma majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho na mwili pia, kumsifu Mungu na kumtukuza hutufanya na kuyanoa mawazo yetu ili yaweze kumuelekea Mungu na kutambua ukuu wake na uweza wake kila siku kama ikiwezekana tuwe na Muda wa kumtukuza Mungu na kumsifu Biblia imeeleza hata vitandani mwetu, unapopita katika wakati Mgumu acha kuogopa mwamini Mungu na hakikisha kuwa unamuelekea yeye na wakati mwingine jaribu tu kumsifu na utaweza kuona Mungu atakuweka huru! Hakuna Jeshi la aina yoyote litakaloweza kushindana nawe kama wewe ni mtu uliyejaa sifa kwa Mungu, Kumsifu Mungu namna hii ndio siri ya ushindi wa Daudi katika maisha yake yote yeye alikuwa mtu aliyejaa zaburi za sifa na hivyo hakuwahi kushindwa vita ya aina yoyote!

 

Zaburi 27:1-6 “Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu, Nimwogope nani? Bwana ni ngome ya uzima wangu, Nimhofu nani? Watenda mabaya waliponikaribia, Wanile nyama yangu, Watesi wangu na adui zangu, Walijikwaa wakaanguka. Jeshi lijapojipanga kupigana nami, Moyo wangu hautaogopa. Vita vijaponitokea, Hata hapo nitatumaini. Neno Moja nimelitaka kwa Bwana, Nalo ndilo nitakalolitafuta, Nikae nyumbani mwa Bwana Siku zote za maisha yangu, Niutazame uzuri wa Bwana, Na kutafakari hekaluni mwake. Mradi atanisitiri bandani mwake siku ya mabaya, Atanisitiri katika sitara ya hema yake, Na kuniinua juu ya mwamba. Na sasa kichwa changu kitainuka Juu ya adui zangu wanaonizunguka. Nami nitatoa dhabihu za shangwe hemani mwake; Nitaimba, naam, nitamhimidi Bwana.”

 

5.       Omba upako wa Roho Mtakatifu.

 

Roho Mtakatifu ni moja ya mwanachama muhimu katika utatu wa Mungu anajihusisha sana na maeneo mengi ya ukombozi wetu, yeye ni chanzo cha ushuhuda na ufunuo, anatuongoza katika maamuzi ya kiulinzi kimwili na kiroho ili tusiiingie hatarini,  yeye ni mfariji pia na hivyo anauwezo wa kutusaidia na kutupa tumaini, Katika nyakati za agano la kale popote pale ambapo palitokea uonevu na ukahitajika msaada wa kiungu basi Roho wa Mungu alikuja kwa nguvu juu ya mmoja wapo ya waamuzi au mfalme na mfalme huyo akawaweka watu huru,  uhuru huu ulitokana na upako wa Roho Mtakatifu, tunaambiwa kuwa Upako unavunja nira  ona Isaya 10:27Tena itakuwa katika siku hiyo mzigo wake utaondoka begani mwako, na nira yake shingoni mwako, nayo nira itaharibiwa, kwa sababu ya kutiwa mafuta.” Maandiko yanaonyesha kuwa Upako yaani mafuta ya Roho Mtakatifu huwa yanafanya kazi ya kuondoa uonevu, Ni kazi ya Roho Mtakatifu kuwatia mafuta watumishi wake ili wafanye kazi ya kuwatoa watu kutoka katika uonevu wa namna mbalimbali ona Luka 4:18-19 “Roho wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa, Na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa.” Unaona mafuta yaliyokuwa juu ya Yesu kutokana na Roho Mtakatifu yalifanya kazi mbalimbali ya kuwafungua watu walioonewa na kukandamizwa na shetani, sio hivyo tu lakini na kuwaponya na kuwaweka huru, tunaweza kusoma pia katika Matendo 10:38 “habari za Yesu wa Nazareti, jinsi Mungu alivyomtia mafuta kwa Roho Mtakatifu na nguvu naye akazunguka huko na huko, akitenda kazi njema na kuponya wote walioonewa na Ibilisi; kwa maana Mungu alikuwa pamoja naye.”

 

Nyakati za agano la kale hususani kipindi cha waamuzi na wafalme Mungu Roho Mtakatifu aliwawezesha wakati wote kufanya matendo ya ukombozi baada ya yeye kuja juu ya watumishi wake na kuwatia nguvu iliyowawezesha kuwasaidia ndugu zao wasikandamizwe au waliokuwa wanakandamizwa na maadui na kuwakimbiza adui zao ona maeneo mblimbali:-

 

Waamuzi 3:9-11 “Kisha wana wa Israeli walipomlingana Bwana, Bwana akawainulia wana wa Israeli mwokozi, aliyewaokoa, yaani, Othnieli mwana wa Kenazi, ndugu mdogo wa Kalebu. Roho ya Bwana ikamjilia juu yake, naye akawa mwamuzi wa Israeli; akatoka kwenenda vitani, naye Bwana akamtia huyo Kushan-rishathaimu, mfalme wa Mesopotamia, mkononi mwake; na mkono wake ukamshinda Kushan-rishathaimu. Nayo nchi ikawa na amani muda wa miaka arobaini. Kisha Othnieli, mwana wa Kenazi, akafa.”

 

Waamuzi 13:24-25 “Basi yule mwanamke akamzaa mtoto mwanamume akamwita jina lake Samsoni, mtoto huyu akakua, Bwana akambarikia. Roho ya Bwana ikaanza kumtaharakisha katika Mahane-dani, katikati ya Sora na Eshtaoli.”

 

Waamuzi 14:19 “Roho ya Bwana ikamjilia juu yake kwa nguvu, naye akatelemkia Ashkeloni, akapiga watu waume thelathini katika watu hao, na kuzitwaa nyara zao, na kuwapa hao waliokitambua kitendawili mavao hayo. Hasira zake zikamwaka, naye akakwea kwenda nyumbani kwa baba yake.”     

 

Waamuzi 11:28-29. “Lakini mfalme wa wana wa Amoni hakuyasikiza hayo maneno ya Yeftha aliompelekea. Ndipo roho ya Bwana ikamjilia juu yake Yeftha, naye akapita katika Gileadi na Manase, akapita na katika Mispa ya Gileadi, na kutoka hapo Mispa ya Gileadi akapita kuwaendea wana wa Amoni.”

 

Unaona popote pale waaamuzi walipowasaidia watu ili kuwaletea ukombozi utaweza kuona Roho Mtakatifu alikuja juu yao kwanza, Ni Roho huyu huyu Mtakatifu aliyeyainua maisha ya waamuzi ili kuwatetea watu wake dhidi ya migandamizo ya aina mbalimbali anaweza kwa uhalisia kutuwezesha na sisi kuondoka katika migandamizo ya aina mbalimbali, ni mfariji, ni kiongozi kwa awaye yote anayemtegemea atakuonyesha yakupasayo kufanya na kukupa mbinu unazozihitaji,  kila mtu anahitaji, kuwa na maono, hekima, ujasiri na kukabiliana na changamoto za aina mbalimbali unapotaka kulitumikia shauri la Bwana au kutimiza kusudi lake duniani, utakuwa kwenye nafasi nzuri ya kutimiza hilo kama utamruhusu Roho Mtakatifu akutie nguvu, unapojaribu kuongoza bila Roho Mtakatifu utaanguka lakini ili uweze kufanikiwa tunamuhitaji Roho wa Mungu. Matendo 11:22-24 “Habari hizo za watu hao zikafika masikioni mwa kanisa lililokuwako katika Yerusalemu; wakamtuma Barnaba, aende hata Antiokia. Naye, alipokwisha kufika na kuiona neema ya Mungu akafurahi, akawasihi wote waambatane na Bwana kwa kusudi la moyo. Maana alikuwa mtu mwema amejaa Roho Mtakatifu na imani; watu wengi wakaongezeka upande wa Bwana.”

 

6.       Mkemee shetani na majeshi yake yote.

 

Katika maombi yetu ni muhimu kukumbuka kuwa na maombi ya kufanya vita dhidi ya ibilisi, kumshughulikia shetani na majeshi yake na maajenti wake wote ni wajibu pekee tuliopewa na Mungu sio ombi ni amri ona, Mfumo wa kishetani uko katika protokali za kijeshi, hivyo Ndivyo Mungu alivyowaumba, Mungu anaitwa Bwana wa Majeshi, Yeye ndio Amiri Jeshi mkuu ana serikali na ana dola Mbinguni, Malaika waliumbwa kama vyombo vya Dola, hii ikiwa ni pamoja na Malaika walioasi baadaye yaani majeshi ya Pepo wabaya katika ulimwengu war oho, kwa msingi huo wao husikiliza amri na mari haitolewi kama ombi inatolewa kwa mamlaka kwa kuamuru kupitia mairi Jeshi mkuu wa Majeshi ya Bwana yaani Kristo ona Waefeso 6:10-13 “Hatimaye, mzidi kuwa hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake.Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani. Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho.Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama.”

 

Kwa msingi huo unaweza kugundua kuwa shetani na serikali zake wako katika mfumo wa kijeshi na ndio maana Yesu aliamuru tumshughulikie alitupa amri sio ombi la kumshughulikia shetani angalia mfumo wa lugha inayotumika  katika     

 

Luka 10:17-19 “Ndipo wale sabini waliporudi kwa furaha, wakisema, Bwana, hata pepo wanatutii kwa jina lako. Akawaambia, Nilimwona Shetani, akianguka kutoka mbinguni kama umeme. Tazama, nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na nge, na nguvu zote za yule adui, wala hakuna kitu kitakachowadhuru.”

 

Maandiko wakati wote yanaonyesha lugha ya kupinga na kukemea linapokuja swala la maombi yetu dhidi ya kushughulikia kazi za shetani, wakati wote maombi ya kimapambano dhidi ya ibilisi ni kukemea ni kupigana vita ona maagizo ya kimaandiko:-

 

2Wakoritho 10:3-5 “Maana ingawa tunaenenda katika mwili, hatufanyi vita kwa jinsi ya mwili; (maana silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome;) tukiangusha mawazo na kila kitu kilichoinuka, kijiinuacho juu ya elimu ya Mungu; na tukiteka nyara kila fikira ipate kumtii Kristo; tena tukiwa tayari kupatiliza maasi yote, kutii kwenu kutakapotimia

 

1Petro 5: 8-9 “Mwe na kiasi na kukesha; kwa kuwa mshitaki wenu Ibilisi, kama simba angurumaye, huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze. Nanyi mpingeni huyo, mkiwa thabiti katika imani, mkijua ya kuwa mateso yale yale yanatimizwa kwa ndugu zenu walioko duniani.”

 

Yakobo 4:7-8 “Basi mtiini Mungu. Mpingeni Shetani, naye atawakimbia. Mkaribieni Mungu, naye atawakaribia ninyi. Itakaseni mikono yenu, enyi wenye dhambi, na kuisafisha mioyo yenu, enyi wenye nia mbili. 

 

Zekaria 3:2 “Bwana akamwambia Shetani, Bwana na akukemee Ewe Shetani; naam, Bwana, aliyechagua Yerusalemu, na akukemee; je! Hiki si kinga kilichotolewa motoni?

 

Yuda 1:9 “Lakini Mikaeli, malaika mkuu, aliposhindana na Ibilisi, na kuhojiana naye kwa ajili ya mwili wa Musa, hakuthubutu kumshitaki kwa kumlaumu, bali alisema, Bwana na akukemee.”

 

Kwa kuwa shetani anataka kuwakandamiza watu wetu, sisi wenyewe,familia zetu na hata taifa letu linapokuja swala la kumtaka aachie huwa ni amri kali, achiaa, toka, nakuamuru, bwana na akukemee na kadhalika hakuna lugha laini wakati wa kumkemea shetani, ni kumuamuru aachie haraka na taaachialia

 

7.       Vunja madhabahu za uovu

 

Ni muhimu kufahamu kuwa mawasiliano yote ya kiroho kati ya Mungu na wanadamu au miungu na wanadamu hufanyika kupitia madhabahu, kwa msingi huo Mungu aliwaagiza wana wa Israel watakapoingia katika inchi ya kanaani moja ya jambo muhimu wanalopaswa kulifanya ni kuzivunja madhabahu zao agizo hili la kuharibu madhabau za uovu limerudiwa tena na tena katika maandiko ona Kutoka 34:12-13 “Ujihadhari nafsi yako, usije ukafanya agano na wenyeji wa nchi ile unayoiendea, lisiwe mtego katikati yako. Bali utabomoa madhabahu zao, na kuvunja-vunja nguzo zao, na kuyakata-kata maashera yaoUnaona unaweza kuona tena Kumbukumbu la torati 7:1-7 “Bwana, Mungu wako, atakapokutia katika nchi uendayo kuimiliki, atakapoyang'oa mataifa mengi watoke mbele yako, Mhiti, na Mgirgashi, na Mwamori, na Mkanaani, na Mperizi, na Mhivi, na Myebusi, mataifa saba makubwa yenye nguvu kukupita wewe; wakati Bwana, Mungu wako, atakapowatoa mbele yako, nawe utawapiga; wakati huo ndipo uwaondoe kabisa; usifanye agano nao, wala kuwahurumia; wala usioane nao;binti yako usimpe mwanawe mume, wala usimtwalie mwanao mume binti yake.Kwa kuwa atamkengeusha mwanao mume asinifuate, ili wapate kuabudu miungu mingine; ndipo itakapowaka hasira ya Bwana juu yenu, naye atakuangamiza upesi. Lakini watendeni hivi; zivunjeni madhabahu zao zibomosheni nguzo zao, yakateni maashera yao, ziteketezeni kwa moto sanamu zao za kuchonga. Kwa maana wewe u taifa takatifu kwa Bwana, Mungu wako; Bwana Mungu wako, amekuchagua kuwa watu wake hasa, zaidi ya mataifa yote walioko juu ya uso wa nchi.”

Kwa nini Mungu aliamuru Madhabau za mataifa yasiyomcha Mungu yaharibiwe? Hii ni kwa sababu madhabahu ndio ni eneo la kutolea sadaka kwa miungu au kwa shetani ndio eneo la mwasiliano kati ya miungu na wanadamu, kwa hiyo madhabahu ndizo zinaziotumika kufanya mawasiliano ya kipepo na kufanya uchawi, kutengeneza hirizi, kupokea maelekezo ya kipepo, kufanya uaguzi, kufanya utambuzi kwa ramli  na mawasiliano yote kati ya miungu na wanadamu hufanyika kupitia madhabahu, ni madhabahu ndio zinazotumika kuwafunga watu na kuwaweka katika mahusiano ya kipepo na kusababisha mikandamizo, watu wanapotaka kukutana na ulimwengu wa kiroho basi pale wanapokutania kwa ibada ndio maagano ya kipepo yanapofanyika au mahusiano na mapepo ndipo yanapofanyika na ndipo maisha ya watu wengi yanapoharibiwa

 

2Wafalme 3:26-27 “Naye mfalme wa Moabu alipoona ya kwamba ameshindwa vitani, alitwaa pamoja naye watu mia saba wenye kufuta panga ili wapenye hata kwa mfalme wa Edomu; wala hawakudiriki. Ndipo akamtwaa mwanawe wa kwanza, yeye ambaye angetawala mahali pake, akamtoa awe sadaka ya kuteketezwa juu ya ukuta. Kukawa hasira kuu juu ya Israeli; basi wakatoka kwake, wakarudi kwenda nchi yao wenyewe.”               

 

Balaamu alipokodiwa kuja kuwalaani Israel utaweza kuona jambo la kwanza kulifanya ni kutengeneza madhabahu unaweza kuona Hesabu 23:1-5 “Balaamu akamwambia Balaki, Nijengee hapa madhabahu saba, ukaniandalie hapa ng'ombe waume saba, na kondoo waume saba.Balaki akafanya kama Balaamu alivyonena. Balaki na Balaamu wakatoa sadaka, ng'ombe mume mmoja na kondoo mume mmoja juu ya kila madhabahu. Balaamu akamwambia Balaki, Simama karibu na sadaka yako, nami nitakwenda, labda Bwana atakuja kuonana nami; na lo lote atakalonionyesha nitakuambia. Akaenda hata mahali peupe juu ya kilima. Mungu akakutana na Balaamu; naye Balaamu akamwambia, Nimetengeneza madhabahu saba, nami nimetoa sadaka ng'ombe mume mmoja na kondoo mume mmoja juu ya kila madhabahu. Bwana akatia neno katika kinywa chake Balaamu, akasema, Umrudie Balaki; ukaseme maneno haya.”

 

Kabla ya Mungu kumtumia Gideoni kama Mwamuzi wa Israel kwa uwezo wake Gideoni alipoisikia msauti ya Mungu aliye hai aliamua kuivinja kwanza Madhabahu ya baba yake ona Waamuzi 6:24-32 “Ndipo Gideoni akamjengea Bwana madhabahu hapo, akaiita jina lake, Yehova-Shalomu; hata hivi leo iko huko katika Ofra ya Waabiezeri. Ikawa usiku uo huo Bwana akamwambia, Mtwae ng'ombe wa baba yako, yaani ng'ombe wa pili, wa miaka saba, ukaiangushe madhabahu ya Baali, aliyo nayo baba yako, ukaikate Ashera ile iliyo karibu nayo; ukamjengee Bwana, Mungu wako, madhabahu juu ya ngome hii, kwa taratibu zake; ukamtwae yule ng'ombe wa pili na kumtoa awe sadaka ya kuteketezwa, kwa kuni za ile Ashera uliyoikata. Ndipo Gideoni akatwaa watu kumi miongoni mwa watumishi wake, akafanya kama Bwana alivyomwambia; lakini ikawa kwa sababu aliwaogopa watu wa nyumba ya baba yake, na watu wa mji, hakuweza kuyatenda hayo wakati wa mchana, basi aliyatenda usiku. Hata watu wa mji walipoondoka asubuhi na mapema, tazama, madhabahu ya Baali imebomolewa, na ile Ashera iliyokuwa karibu nayo imekatwa, na yule ng'ombe wa pili ametolewa sadaka juu ya ile madhabahu iliyojengwa. Wakaambiana, Ni nani aliyetenda jambo hili? Hata walipotafuta habari na kuuliza, wakasema, Gideoni, mwana wa Yoashi, ndiye aliyetenda jambo hili. Ndipo watu wa mji wakamwambia Yoashi Mlete mwanao, afe; kwa sababu ameibomoa madhabahu ya Baali na kwa sababu ameikata ile Ashera iliyokuwa karibu nayo. Yoashi akawaambia watu wote waliokuwa wakishindana naye, Je! Mtamtetea Baali? Au mtamwokoa ninyi? Yeye atakayemtetea na auawe hivi asubuhi; kama yeye ni Mungu, na ajitetee nafsi yake, kwa sababu mtu mmoja ameibomoa madhabahu yake. Basi akamwita Yerubaali siku hiyo, akisema, Baali na atete naye kwa ajili ya nafsi yake, kwa sababu ameibomoa madhabahu yake.”        

 

Unaona kwa sababu hiyo ni lazima tunapotaka ukombozi kutoka katika maeneo mbalimbali ya maisha yetu hatuna budi kuharibu kila njia za mawasiliano ya kishetani kwani hizo ndio madhabahu zenyewe, haribu, hirizi, pembe au vyungu, vimbo au vifaa vyote vya kiroho ambavyo umepewa na waganga au ambavyo vimezindikwa nyumbani kwenu, kumbuka kuwa Madhabahu ndio njia ya mawasiliano, na ikiwa madhabahu hiyo sio ya kiungu, basi itapingana na sheria za kiungu, za Mungu aliye hai, madhabahu ya miungu migeni itazuia neema ya Mungu wetu kwetu, itaweka mipaka ya utendaji wa kiungu kwetu, itafungua milango ya roho chafu, itasababisha matatizo yasiyoweza kupata ufumbuzi, itachelewesha sana upatikananaji wa Baraka zako, itasababisha matatizo yasiyoisha, inaweza kushababisha talaka, umasikini, kurudi nyuma, utasa, vifo, aibu  na mambo ya ajabu ajabu, madhabahu zina uwezo wa kusababisha laana au Baraka, Madhabahu ni ukumbusho kwa wale walioziinua, ili uweze kupata upenyo katika maisha yako ni lazima uziharibu madhabahu zisizo rasmi na makuhani wake, Madhabahu hugeuka na kuwa njia (Malango) ya kuvutia viumbe wa kiroho kufanya utembeleo aidha awe Mungu au miungu yaani mapepo

 

Mathayo 16:18 . “Nami nakuambia, Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu; wala milango ya kuzimu haitalishinda.”

 

Mwanzo 28:11-19 “Akafika mahali fulani akakaa huko usiku kucha, maana jua lilikuwa limekuchwa; akatwaa jiwe moja la mahali pale akaliweka chini ya kichwa chake, akalala usingizi pale pale.Akaota ndoto; na tazama, ngazi imesimamishwa juu ya nchi, na ncha yake yafika mbinguni. Tena, tazama, malaika wa Mungu wanapanda, na kushuka juu yake. Na tazama, BWANA amesimama juu yake, akasema, Mimi ni BWANA, Mungu wa Ibrahimu baba yako, na Mungu wa Isaka; nchi hii uilalayo nitakupa wewe na uzao wako. Na uzao wako utakuwa kama mavumbi ya nchi, nawe utaenea upande wa magharibi, na mashariki, na kaskazini, na kusini; na katika wewe, na katika uzao wako, jamaa zote za dunia watabarikiwa. Na tazama, mimi nipo pamoja nawe, nitakulinda kila uendako, nami nitakuleta tena mpaka nchi hii, kwa maana sitakuacha, hata nitakapokufanyia hayo niliyokuambia. Yakobo akaamka katika usingizi wake, akasema, Kweli BWANA yupo mahali hapa, wala mimi sikujua. Naye akaogopa akasema, Mahali hapa panatisha kama nini! Bila shaka, hapa ni nyumba ya Mungu, napo ndipo lango la mbinguni. Yakobo akaondoka asubuhi na mapema, akalitwaa lile jiwe aliloliweka chini ya kichwa chake, akalisimamisha kama nguzo, na kumimina mafuta juu yake. Akaita jina la mahali pale Betheli; lakini jina la mji ule hapo kwanza uliitwa Luzu.”

 

Unaona kwa msingi huo hatuna budi kuhakikisha kuwa tunaharibu kila aina ya madhabahu ambayo iko kinyume na Mungu wetu ili kuzuia sisi kuwa chini ya utumwa wa miungu mingine kama haya yakifanyika vema basi Ibilisi atatii na kukuacha uende, waachie watu wangu waende, Wakati wote unapotaka Mungu awe pamoja nawe na kukukomboa unapotaka mpenyo katika maisha yako na unapotaka Mungu atembee nawe ni lazima kuhakikisha kuwa njia zote za mawasiliano na miungu migeni zinahabiwa na kutupwa mbali ili Mungu atembee katikati yako na familia yako haribu miungu migeni iondoe katika nyumba yako ichome moto ifukie baki na Mungu akiye hai na uwepo wa Mungu utakuwa pamoja nawe na hakuna wa kukuonea utaogopwa kila utakakopita

 

Waefeso 19:19 “Na watu wengi katika wale waliotumia mambo ya uganga wakakusanya vitabu vyao, wakavichoma moto mbele ya watu wote; wakafanya hesabu ya thamani yake, wakaona ya kwamba yapata fedha hamsini elfu.”  

 

Mwanzo 35:1-5 “Mungu akamwambia Yakobo, Ondoka, panda uende Betheli, ukakae huko; ukamfanyie Mungu madhabahu huko; yeye aliyekutokea ulipomkimbia Esau, ndugu yako. Yakobo akawaambia watu wa nyumbani mwake, na wote waliokuwa pamoja naye, Ondoeni miungu migeni iliyoko kwenu, mjisafishe mkabadili nguo zenu.Tuondoke, tupande kwenda Betheli, nami nitamfanyia Mungu madhabahu huko; yeye aliyenisikia siku ya shida yangu, akawa pamoja nami katika njia yote niliyoiendea. Nao wakampa Yakobo miungu migeni yote iliyokuwa mikononi mwao, na pete zilizokuwa masikioni mwao, naye Yakobo akazificha chini ya mwaloni ulioko Shekemu. Wakashika njia, hofu ya Mungu ikaishika miji iliyowazunguka, wala hawakuwafuata wana wa Yakobo.”

 

Imani yangu ni kuwa somo hili ukilifanyia kazi na kuweka yote niliyokufundisha kivitendo utashangaa kwa miujiza ya ajabu na mpenyo wa ajabu utakaoambatana na maisha yako kuanzia leo namuomba Mungu kwamba uongezewe neema unapoadhimisha siri za ukombozi wako kupitia somo hili katika jina la Yesu Kristo  wa Nazareth Mwana wa Mungu aliye hai amen.

 

Na Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni