Alhamisi, 15 Septemba 2022

Kuhani mkuu kwa Mfano wa Melkizedek


Zaburi 110:1-4 “Neno la Bwana kwa Bwana wangu, Uketi mkono wangu wa kuume, Hata niwafanyapo adui zako Kuwa chini ya miguu yako.  Bwana atainyosha toka Sayuni Fimbo ya nguvu zako. Uwe na enzi kati ya adui zako; Watu wako wanajitoa kwa hiari, Siku ya uwezo wako; Kwa uzuri wa utakatifu, Tokea tumbo la asubuhi, Unao umande wa ujana wako. Bwana ameapa, Wala hataghairi, Ndiwe kuhani hata milele, Kwa mfano wa Melkizedeki.”



Utangulizi

Maandiko yanamuonyesha Yesu Kristo kama ni Nabii mkubwa na aliyebora zaidi kuliko Musa, lakini pia ni Kuhani mkuu aliye bora zaidi kwa mfano wa Melkizedeki unaweza kuona poia katika Waebrania 6:20 “alimoingia Yesu kwa ajili yetu, mtangulizi wetu, amekuwa kuhani mkuu hata milele kwa mfano wa Melkizedeki.” Tunapojifunza somo hili kuhani mkuu kwa mfano wa Melkizedeki tutazingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-

·         Tofauti ya nabii na kuhani

·         Wajibu wa kikuhani.

·         Kuhani mkuu kwa mfano wa Melkizedeki

Tofauti ya Nabii na kuhani

Neno la Mungu linatufundisha tofauti kubwa iliyoko kati ya nabii na kuhani, kwa kawaida hawa wote ni watumishi wa Mungu, na huwa wanaitwa ama kuteuliwa na Mungu mwenyewe ona Kumbukumbu 18:18 “Mimi nitawaondokeshea nabii miongoni mwa ndugu zao mfano wako wewe, nami nitatia maneno yangu kinywani mwake, naye atawaambia yote nitakayomwamuru.” Unaona ni Mungu ndiye anayeinua nabii na kuweka neno lake ndani yao ili aseme kwa niaba yake na kuwafundisha watu wa Mungu njia zake nan i Mungu mwenyewe anayechagua kuhani ona Waebrania 5:1-4 “Maana kila kuhani mkuu aliyetwaliwa katika wanadamu amewekwa kwa ajili ya wanadamu katika mambo yamhusuyo Mungu, ili atoe matoleo na dhabihu kwa ajili ya dhambi; awezaye kuwachukulia kwa upole wao wasiojua na wenye kupotea, kwa kuwa yeye mwenyewe yu katika hali ya udhaifu; na kwa sababu hiyo imempasa, kama kwa ajili ya watu, vivyo hivyo kwa ajili ya nafsi yake mwenyewe, kutoa dhabihu kwa ajili ya dhambi. Na hapana mtu ajitwaliaye mwenyewe heshima hii, ila yeye aitwaye na Mungu, kama vile Haruni.” Unaweza kuona hawa wote huteuliwa au kuitwa na Mungu, Nabii yeye huchaguliwa na Mungu ili awe msemaji kwa niaba ya Mungu Neno nabii katika Lugha ya kiibrania huwakilishwa kwa maneno makuu matatu ambayo ni NABI, ROEH, na HOZEH

Nabi – Maana yake ni Msemaji, au mtangazaji Hawa ni wasemaji au wanenaji wanaosukumwa na Roho wa Mungu kuyasema mapenzi ya Mungu kwa msukumo na wivu mkali wa kiungu, lakini pia ni walimu wa neno la Mungu kwa ufupi ni wasemaji kwa niaba ya Mungu, ni wasemaji wa Mapenzi ya Mungu

Roeh – Maana yake ni waonaji, au wafunuaji wao hitwa na Mungu na kuwawezesha kuona mambo yaliyofichika na kuyasema au kuonya au kutangaza au kufundisha mapenzi ya Mungu baada ya kufunuliwa na Mungu, mwisho wa siku nao ni wasemaji kwa niaba ya Mungu

Hozeh – Ni msahuri au mwenye hekima ambao kazi yao ni kufikiri na kutoa ushauri kwa niaba ya Mungu kwa watu wake ni wenye uwezo wa kutambua kama ujumbe ni wa kiungu au la walitumika sana kuwashauri wafalme ili watende sawasawa na mapenzi ya Mungu

Katika kiyunani Prophet ni mtu anayezungumza jambo kwa niaba ya mwingine kwa hivyo wao husema au kutafasiri jambo kwa niaba ya Mungu, ili watu wa Mungu wajue mapenzi ya Mungu katika maisha yao hivyo kwa vyovyote vile manabii ni walimu wa neno la Mungu, ni walimu kwa niaba ya Mungu ni wajumbe kwa niaba ya Mungu, Mungu anapotaka kuyafunua mapenzi yake kwa wanadamu.

Kuhani kwa upande mwingine ni mwanaume anayechaguliwa na Mungu kuwawakilisha wanadamu kwa Mungu, wao ni wasemaji wa wanadamu kwa Mungu, wana wana kibali maalumu cha kumfikia Mungu, na kuzungumza au kutenda kwa niaba ya wanadamu kwa Mungu , hata hivyo hii haiachi ukweli kuwa nao ni walimu wa nenola Mungu kwa watu wa Mungu, lakini mafundisho yao ni tofauti nay ale ya manabii, wakati manabii wanakazia uadilifu, hali safi ya kiroho na wajibu wetu kwa Mungu, Makuhani wao hushughulika na njia sahihi za kumuendea Mungu.

Wajibu wa kikuhani.

Huduma ya kikuhani kwa kawaida kihistoria ilianzishwa na Mungu kwa wana wa Israel baada ya kutoka katika inchi ya Misri, baada ya maelekezo ya Mungu kwa Musa katika mlima wa Sinai, Kutoka 28:1 “Nawe umlete Haruni ndugu yako karibu nami, na wanawe pamoja naye, miongoni mwa wana wa Israeli, ili anitumikie katika kazi ya ukuhani. Haruni, na Nadabu, na Abihu, na Eleazari, na Ithamari, wana wa Haruni.” Makuhani hawa walichaguliwa kutoka miongoni mwa wanadamu ili waweze kuwawakilisha wanadamu kwa Mungu kwa hiyo sifa zao zilikuwa

1.       Walichaguliwa kutoka miongoni mwa wanadamu ili kuwawakilisha wanadamu

2.       Walichaguliwa na Mungu mwenyewe

3.       Walifanya kazi ya Mungu kwa niaba ya wanadamu, kwa mambo yote ya wanadamu ya kidini ili kumfikia Mungu

4.       Walikuwa na kazi ya kutoa sadaka za kuteketezwa kwaajili ya watu kwa Mungu

5.       Walikuwa na wajibu wa kuwaombea watu kwa Mungu

6.       Walikuwa na wajibu wa kuwabariki watu wa Mungu

Kwa msingi huo katika maandiko iko wazi kabisa kuwa wajibu wa kikuhani ulikuwa ni kutoa sadaka zakuteketezwa, kuwaombea watu, na kuwabariki watu kwa jina la Mungu, hata hivyo kazi zote hizi zilizokuwa zikifanywa na makuhani bado zilikuwa zinaashiria kuwa siku moja atakuja kuhani mkuu aliye bora zaidi huyu ndiye ametabiriwa kuwa kuhani mkuu kwa mfano wa Melkizedeki “Zaburi 110:1-4 “Neno la Bwana kwa Bwana wangu, Uketi mkono wangu wa kuume, Hata niwafanyapo adui zako Kuwa chini ya miguu yako.  Bwana atainyosha toka Sayuni Fimbo ya nguvu zako. Uwe na enzi kati ya adui zako; Watu wako wanajitoa kwa hiari, Siku ya uwezo wako; Kwa uzuri wa utakatifu, Tokea tumbo la asubuhi, Unao umande wa ujana wako. Bwana ameapa, Wala hataghairi, Ndiwe kuhani hata milele, Kwa mfano wa Melkizedeki.” Huyu atakuwa ni masihi ambaye hangetoka katika ukoo wa kikuhani bali katika kabila nyingine ya Yuda na ukoo wa Daudi ukuhani wake huyu utakuwa wa milele kuhani huyu vilevile ataketi katika kiti cha enzi cha Daudi milele na milele, kuhani huyu atakuwa ni mfalme na wakati huo huo kuhani kama ilivyokuwa kwa Melkizedeki, Kuhani huyu atakuwa bora zaidi ya wale wa agano la kale kutoka kabila ya walawi, Huyu ni Yesu Kristo ambaye anafanya kazi zilezile zilizokuwa zikifanywa na makuhani katika agano lililo bora zaidi Warumi 8:33-34 “Ni nani atakayewashitaki wateule wa Mungu? Mungu ndiye mwenye kuwahesabia haki. Ni nani atakayewahukumia adhabu? Kristo Yesu ndiye aliyekufa; naam, na zaidi ya hayo, amefufuka katika wafu, naye yuko mkono wa kuume wa Mungu; tena ndiye anayetuombea.” Waebrania 7:24-25 “bali yeye, kwa kuwa akaa milele, anao ukuhani wake usioondoka. Naye, kwa sababu hii, aweza kuwaokoa kabisa wao wamjiao Mungu kwa yeye; maana yu hai sikuzote ili awaombee.”  Kwa msingi huo tunaona kwamba Mungu ametupa kuhani aliyebora zaidi kutoka nje ya kabila la walawi, ambaye ni kuhani na mfalme sawa na ilivyokuwa kwa Melkizedeki

Kuhani mkuu kwa mfano wa Melkizedeki

Yesu kuwa kuhani mkuu kwa mfano wa Melkizedeki ina faida gani kwetu?  Kama wakristo? Yako mambo kadhaa ya muhimu na msingi yenye faida kwetu kwa kristo Yesu kuwa kuhani mkuu kwaajili yetu.

1.       Tunaweza kupatanishwa na Mungu

 

Kwa sababu ya kazi aliyoifanya Yesu Kristo pale msalabani kama Kuhani mkuu ametupatanisha na Mungu 2Wakoritho 5:18-20 “Lakini vyote pia vyatokana na Mungu, aliyetupatanisha sisi na nafsi yake kwa Kristo, naye alitupa huduma ya upatanisho; yaani, Mungu alikuwa ndani ya Kristo, akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake, asiwahesabie makosa yao; naye ametia ndani yetu neno la upatanisho. Basi tu wajumbe kwa ajili ya Kristo, kana kwamba Mungu anasihi kwa vinywa vyetu; twawaomba ninyi kwa ajili ya Kristo mpatanishwe na Mungu.”

 

Wakolosai 1:19-20 “Kwa kuwa katika yeye ilipendeza utimilifu wote ukae; na kwa yeye kuvipatanisha vitu vyote na nafsi yake akiisha kufanya amani kwa damu ya msalaba wake; kwa yeye, ikiwa ni vitu vilivyo juu ya nchi, au vilivyo mbinguni.”

 

Dhambi ilisababisha uadui kati yetu na Mungu, sote tulikuwa tumefarakanishwa na Mungu lakini kupitia Kuhani mkuu kwa mfano wa Melkizedeki Neema ya Mungu imekuwa juu yetu na uadui uliokuweko kati yetu umevunjwa wote tunajua kuwa maovu huwa yanatufarikisha kwa Mungu

 

Isaya 59:1-2 “Tazama, mkono wa Bwana haukupunguka, hata usiweze kuokoa wala sikio lake si zito, hata lisiweze kusikia; lakini maovu yenu yamewafarikisha ninyi na Mungu wenu, na dhambi zenu zimeuficha uso wake msiuone, hata hataki kusikia.”

 

Lakini kupitia Mwokozi wetu Yesu Kristo hakuna uadui tena kati yetu na Mungu Warumi 5:8:-11 “Bali Mungu aonyesha pendo lake yeye mwenyewe kwetu sisi, kwa kuwa Kristo alikufa kwa ajili yetu, tulipokuwa tungali wenye dhambi. Basi zaidi sana tukiisha kuhesabiwa haki katika damu yake, tutaokolewa na ghadhabu kwa yeye. Kwa maana ikiwa tulipokuwa adui tulipatanishwa na Mungu kwa mauti ya Mwana wake; zaidi sana baada ya kupatanishwa tutaokolewa katika uzima wake. Wala si hivyo tu, ila pia twajifurahisha katika Mungu kwa Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kwa yeye sasa tumeupokea huo upatanisho.”            

 

2.       Tunaweza kumfikia Mungu kwa Maombi tukiwa na ujasiri

 

Sasa tunaweza kumuomba Mungu kwa ujasiri kwa sababu ya kazi kubwa ya ukuhani aliyoifanya Bwana wetu Yesu, Mwanzoni ilikuwa ngumu kumfikia Mungu na kumuomba bila kuhani mkuu kutuombea kwanza kwa kutoa sadaka ya dhambi zake na zetu ndio tupate kibali cha kumfikia Mungu na ujasiri wa mioyo yetu, Lakini kupitia ubora wa sadaka aliyoitoa kuhani huyu mkuu kwa mfano wa Melikizedeki sasa tunaweza kabisa kumuendea Mungu kwa ujasiri na kumuomba moja kwa moja ikifahamika ya kuwa tunaye mwombezi na mpatanishi mbinguni Warumi 8:33-34 “Ni nani atakayewashitaki wateule wa Mungu? Mungu ndiye mwenye kuwahesabia haki. Ni nani atakayewahukumia adhabu? Kristo Yesu ndiye aliyekufa; naam, na zaidi ya hayo, amefufuka katika wafu, naye yuko mkono wa kuume wa Mungu; tena ndiye anayetuombea.” Waebrania 7:24-25 “bali yeye, kwa kuwa akaa milele, anao ukuhani wake usioondoka. Naye, kwa sababu hii, aweza kuwaokoa kabisa wao wamjiao Mungu kwa yeye; maana yu hai sikuzote ili awaombee.” Tunaoujasiri ya kuwa Mungu anasikia maombi yetu na kuwa atatujibu sawa na mapenzi yake kwanini kwa sababu mwanzoni ilikuwa ngumu Yohana 9:31 “Twajua ya kuwa Mungu hawasikii wenye dhambi; bali mtu akiwa ni mcha Mungu, na kuyafanya mapenzi yake, humsikia huyo.”

 

3.       Tunapata amani nafsini mwetu

 

Jambo lingine bora zuri na la amani ni kuwa tunapata amani katika dhamiri zetu hii pia ni kutokana na kazi kubwa aliyoifanya Bwana wetu Yesu Kristo pale Msalabani, Waebrania 4:14-16 “Basi, iwapo tunaye kuhani mkuu aliyeingia katika mbingu, Yesu, Mwana wa Mungu, na tuyashike sana maungamo yetu. Kwa kuwa hamna kuhani mkuu asiyeweza kuchukuana nasi katika mambo yetu ya udhaifu; bali yeye alijaribiwa sawasawa na sisi katika mambo yote, bila kufanya dhambi.  Basi na tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji.”

4.       Sisi sasa ni makuhani pia.

 

Moja ya faida kubwa tunayoipata katika ukuhani wa Yesu Kristo, ni pamoja na sisi kuwa tunaushiriki huo ukuhani hivyo kila aaminiye ni kuhani 1Petro 2:9-10 “       Bali ninyi ni mzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa milki ya Mungu, mpate kuzitangaza fadhili zake yeye aliyewaita mtoke gizani mkaingie katika nuru yake ya ajabu; ninyi mliokuwa kwanza si taifa, bali sasa ni taifa la Mungu; mliokuwa hamkupata rehema, bali sasa mmepata rehema.”

 

Ufunuo 1:4-6  Yohana, kwa yale makanisa saba yaliyoko Asia; Neema na iwe kwenu na amani, zitokazo kwake yeye aliyeko na aliyekuwako na atakayekuja; na zitokazo kwa roho saba walioko mbele ya kiti chake cha enzi; tena zitokazo kwa Yesu Kristo, shahidi aliye mwaminifu, mzaliwa wa kwanza wa waliokufa, na mkuu wa wafalme wa dunia. Yeye atupendaye na kutuosha dhambi zetu katika damu yake, na kutufanya kuwa ufalme, na makuhani kwa Mungu, naye ni Baba yake; utukufu na ukuu una Yeye hata milele na milele. Amina.”

 

Raha ya aina yake kuwa na kuhani mkuu wa kipekee mwenye Baraka zetu zote za kimwili na kiroho!

 

Rev. Innocent Kamote.

 

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!

Maoni 1 :