Alhamisi, 15 Septemba 2022

Jiwe la Kukwaza Katika Sayuni !


1Petro 2:6-8 “Kwa kuwa imeandikwa katika maandiko Tazama, naweka katika Sayuni jiwe kuu la pembeni, teule, lenye heshima, Na kila amwaminiye hatatahayarika.  Basi, heshima hii ni kwenu ninyi mnaoamini. Bali kwao wasioamini, Jiwe walilolikataa waashi, Limekuwa jiwe kuu la pembeni. Tena, Jiwe la kujikwaza mguu, na mwamba wa kuangusha, Kwa maana hujikwaza kwa neno lile,wasiliamini,nao waliwekwa kusudi wapate hayo.”


Utangulizi:

Ni muhimu kufahamu kuwa ni kwanini mtume Petro anamtaja Yesu Kristo kama jiwe la kukwaza? (Stumbling block) Hili linaweza kuwa jambo lenye kushangaza sana, kwa sababu kwa lugha rahisi hauwezi kudhani kuwa Mungu angeweza kukusudia Kristo Yesu awe jiwe la Kukwaza pia, Katika hali ya kawaida tunapomuelezea Yesu Kristo kama jiwe la Pembeni na lenye heshima inaweza kueleweka vema zaidi, lakini hata hivyo kama tutaelewa kile kinacho maanishwa katika maandiko tunaweza kutoka tukiwa na amani ya kutosha sana kumuhusu Yesu Kristo na sisi tuliomuamini. Tutajifunza somo hili kwa kuzinagatia vipengele vifuatavyo vikuu viwili vifuatavyo:-

·         Maana ya jiwe la kukwaza.

·         Jiwe la kukwaza katika Sayuni. 

Maana ya jiwe la kukwaza.

Kibiblia neno jiwe la kukwaza au kukwaza maana yake ni kukosesha kwa hila kwa kiingereza ni Stumbling Block yaani ukwazo, au makwazo ambalo kwa kiibrania husomeka kama neno Miksol na kwa kiyunani ni Skandalon ambalo maana yake ni kukosesha au kutegea mtu ili aanguke na kupata madhara au jambo lolote linaloweza kufanyika na kumfanya mtu afanye dhambi au apatikane na madhara na kuhukumiwa sawa na kumuwekea mtu mtego ili aingie hatiani 

Zaburi 140:4-5 “Ee Bwana, unilinde na mikono ya mtu asiye haki; Unihifadhi na mtu wa jeuri; Waliowaza kuzipotosha hatua zangu. Wenye kiburi wamenifichia mtego na kamba; Wametandika wavu kando ya njia; Wameniwekea matanzi.”

Jambo hili kimaandiko sio jambo jema na Katika lugha ya kinabii kukosesha mtu au kumkwaza mtu kulihesabika kuwa ni tukio baya, hasa linapofanyika kwa mtu asiye na hatia, Mungu aliwaagiza makuhani kutokuweka kwazo kwa mtu asiye na ufahamu au asiyeona (kipofu) kwani kufanya hivyo lilionekana kuwa jambo baya na la kikatili sana  

Walawi 19: 14 “Usimlaani kiziwi, wala usitie kwazo mbele ya kipofu, bali umche Mungu wako; Mimi ndimi BWANA.”

Kimsingi maandiko haya yalikuwa na maana ya kutokusababisha makwazo kwa watu wanaohitaji kuelekezwa au kufahamishwa, kwa hiyo kimsingi maonyo haya yanawahusu walimu wa neno la Mungu kwamba wasitumie ufahamu wao kuwapotosha watu kwa hila kwa kufanya hivyo kungeleta hukumu iliyokubwa sana au ya kutisha ona

 Mathayo 18:6 “bali atakayemkosesha mmojawapo wa wadogo hawa waniaminio, yamfaa afungiwe shingoni jiwe kubwa la kusagia, na kutoswa katika kilindi cha bahari.

Unaweza kuona maandiko yanatangaza hukumu kubwa sana kwa mtu atakayekosesha wengine au kwa lugha nyingine anayesababisha makwazo au kwa lugha nyingine kufundisha watu uongo au kumtia mwenye haki hatiani

Yakobo 3:1-2 “Ndugu zangu, msiwe waalimu wengi, mkijua ya kuwa mtapata hukumu kubwa zaidi. Maana twajikwaa sisi sote pia katika mambo mengi. Mtu asiyejikwaa katika kunena, huyo ni mtu mkamilifu, awezaye kuuzuia na mwili wake wote kama kwa lijamu.”  

Kwa msingi huo unaweza kupata picha ya wazi kuwa kukosesha au kukwaza kamwe kibiblia halikuweza kuhesabiwa kuwa  la jambo zuri bali ni tukio baya na lililoambatana na maonyo makali dhidi ya wale wote wanaosababisha makwazo ya aina yoyote ile :-

Luka 17:1-2 “Akawaambia wanafunzi wake, Makwazo hayana budi kuja, lakini ole wake mtu yule ambaye yaja kwa sababu yake! Ingemfaa zaidi mtu huyo jiwe la kusagia lifungwe shingoni mwake, akatupwe baharini, kuliko kumkosesha mmojawapo wa wadogo hawa.  

Sasa ni katika namna ya kushangaza sana unaweza kustaajabu kuona kuwa ujio wa Masihi Bwana wetu Yesu Kristo unatajwa vilevile kuambatana na Heshima kwa wale watakaomwamini lakini vilevile na kukwaza  kwa wale watakaomkataa au kutokumuelewa na kutokumuamini hii maana yake ni nini hilo sasa linatuleta kutafakari kipengele kinachofuata kama ifuatavyo:-         

Jiwe la kukwaza katika sayuni

Ni muhimu kufahamu kuwa kuja kwa Yesu Kristo duniani, kulitabiriwa na manabii na kuwekwa wazi kuwa Yesu angekuja kwa makusudi makuu mawili, yaani kuokoa wengi  na kuwapa heshima kubwa lakini vilevile kukwaza wengi hasa wale wasiomuamini au wasiomuelewa na kumkubali na kusababisha hukumu kubwa sana kwao, 

Yohana 3:16 -18 “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. Maana Mungu hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye. Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa Mungu.”

Kwa msingi huo ujio wa Yesu Kristo una maswala makubwa mawili ya msingi kwa wanaomuamini na kwa wasiomuamini, wanaomuamini hawatatahayarika lakini kwa wale wasiomuamini watapata hukumu watakutana na mambo magumu sana sawa na alivyotabiri nabii isaya ona.  

Isaya 28:16 “kwa ajili ya hayo Bwana, MUNGU, asema hivi, Tazama, naweka jiwe katika Sayuni, liwe msingi, jiwe lililojaribiwa, jiwe la pembeni lenye thamani, msingi ulio imara; yeye aaminiye hatafanya haraka.”

Swala hili lilielezwa mapema katika maandiko lakini vilevile nabii mwingine alimuelezea Mariamu mama yake Yesu waziwazi mara baada ya kuzaliwa na walipokuwa wamempeleka kijana Yesu Hekaluni kwa kubarikiwa ona katika

Luka 2: 25-34 “Na tazama, pale Yerusalemu palikuwa na mtu, jina lake Simeoni, naye ni mtu mwenye haki, mcha Mungu, akiitarajia faraja ya Israeli; na Roho Mtakatifu alikuwa juu yake. Naye alikuwa ameonywa na Roho Mtakatifu ya kwamba hataona mauti kabla ya kumwona Kristo wa Bwana. Basi akaja hekaluni ameongozwa na Roho; na wale wazazi walipomleta mtoto Yesu ndani, ili wamfanyie kama ilivyokuwa desturi ya sheria, yeye mwenyewe alimpokea mikononi mwake, akamshukuru Mungu, akisema, Sasa, Bwana, wamruhusu mtumishi wako, Kwa amani, kama ulivyosema; Kwa kuwa macho yangu yameuona wokovu wako, Uliouweka tayari machoni pa watu wote; Nuru ya kuwa mwangaza wa Mataifa, Na kuwa utukufu wa watu wako Israeli.  Na babaye na mamaye walikuwa wakiyastaajabia hayo yaliyonenwa juu yake. Simeoni akawabariki, akamwambia Mariamu mama yake, Tazama, huyu amewekwa kwa kuanguka na kuinuka wengi walio katika Israeli, na kuwa ishara itakayonenewa.”

Kuna maneno kadhaa ambayo watafasiri wa biblia ya Kiswahili waliyachanganya au kuyanukuu vibaya hasa katika mstari wa 34 hapo ambao katika biblia ya Kiswahili Union Version unasomeka hivi Simeoni akawabariki, akamwambia Mariamu mama yake, Tazama, huyu amewekwa kwa kuanguka na kuinuka wengi walio katika Israeli, na kuwa ishara itakayonenewa.” Mstari huo katika biblia ya  kiingereza  ya NIV yaani New International version unasomeka hiviThen Simeon blessed them and said to Mary, his mother: This child is destined to cause the Falling and rising of many in Israel, and to be a sign that will be spoken againstkwa hiyo kwa tafasiri yangu mimi kifungu hiki kilitakiwa kusomeka Simeoni akawabarikia na kumwambia Mariam, mama yake, Mtoto huyu hatima yake itasababisha kuanguka (Kujikwaa) na kuinuka (kuokolewa) kwa wengi katika Israel  na kuwa Ishara itakayonenwa kinyume  unaona Kwa msingi huo Petro anamuelezea Yesu katika pande hizo mbili ya kuwa ni jiwe zuri sana la thamani na heshima kwa wale walimuamini lakini vilevile ni jiwe la kukwaza kwa wale waliomkataa na wasiomuelewa, au waliompuuzia, Wakati wote Yesu alipokuwa duniani na kufanya kazi yake  makundi mawili yalitokea wale waliomuamini na wale wasiomuamini na wale wasiomuamini Kristo wamepata hasara kubwa sana Yohana 6:54-62 Petro anatoa ushauri kwa waamini waendelee kumfuata Yesu kwa sababu yeye ni jiwe lililo hai, ni jiwe teule, ni jiwe lenye heshima na kwa kufanya hivyo hakuna mtu atakayetahayari au atakayeaibika kwa kumtegemea Yesu. 

1Petro 2:4-9 “Mmwendee yeye, jiwe lililo hai, lililokataliwa na wanadamu, bali kwa Mungu ni teule, lenye heshima. Ninyi nanyi, kama mawe yaliyo hai, mmejengwa mwe nyumba ya Roho, ukuhani mtakatifu, mtoe dhabihu za roho, zinazokubaliwa na Mungu, kwa njia ya Yesu Kristo. Kwa kuwa imeandikwa katika maandiko Tazama, naweka katika Sayuni jiwe kuu la pembeni, teule, lenye heshima, Na kila amwaminiye hatatahayarika. Basi, heshima hii ni kwenu ninyi mnaoamini. Bali kwao wasioamini, Jiwe walilolikataa waashi, Limekuwa jiwe kuu la pembeni.Tena, Jiwe la kujikwaza mguu, na mwamba wa kuangusha, Kwa maana hujikwaza kwa neno lile,wasiliamini,nao waliwekwa kusudi wapate hayo. Bali ninyi ni mzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa milki ya Mungu, mpate kuzitangaza fadhili zake yeye aliyewaita mtoke gizani mkaingie katika nuru yake ya ajabu;    
    

Petro anakazia katika ujumbe wake sawa na neno la Mungu kwa vinywa vya manabii ya kuwa tumchague Yesu, yeye ni jiwe lenye heshima ni teule limendaliwa na Mungu baba kwaajili ya ukombozi wetu na kwamba ni fahari kumuamini Yesu na kumkubali na kuwa yeye hatatukataa na kuwa hatutatahayari, yesu hatamuangusha mtu awaye yote anayemtumaini na kumwendea yeye wakati wowote hata tuwapo majaribuni, hatatuangusha kwa hiyo ukimuamini Yesu na kumtegemea katika maisha yako kutoboa katika jambo lolote kuko nje nje lakini ukimpuuzia Yesu aibu na makwazo na hukumu zinakungoja ona katika maandiko:- 

Warumi 9:33 “kama ilivyoandikwa, Tazama, naweka katika Sayuni jiwe likwazalo, na mwamba uangushao; Na kila amwaminiye hatatahayarika.”  

Kumwamini Yesu kunalipa na kuliwapa faida kubwa wale waliomsadiki, lakini wale wanaojifanya wana hekima na akili na wanaomtambua Yesu kama mtu wa kawaida watajikwaa, watu hawajikwai kwa Yesu tu wanajikwaa hata kwa neno lake na kukataa ujumbe wake hata leo, Yesu hatambuliki kwa historia ya kibinadamu tu na hekima ya kibinadamu tu huwezi kumtambua Yesu kwa hisia tu, au kwa ujuzi wako binafsi, wako watu waliojikwaa kwa sababu walimuona Yesu kuwa ni wa kawaida tu wakitimia akili zao na hekima ya kibinadamu watu wengi wataingia dhambini na hatimaye kuingia mtoni kwa sababu ya kutumia fahamu zao katika maswala ya kiungu, wako watu wenye dharau kubwa sana kuhusu Mungu, na mambo ya Mungu huonekana kama ya kipumbavu kwao, na wengine hulichukulia neno la Mungu kwa mazoea tu  jambo hili litawagharimu gharama kubwa sana kwa sababu watajikwaa na ukijikwaa hukumu itakupasa 

Marko 6:1-3 “Akatoka huko, akafika mpaka nchi ya kwao; wanafunzi wake wakamfuata. Na ilipokuwa sabato, alianza kufundisha katika sinagogi; wengi waliposikia wakashangaa, wakisema, Huyu ameyapata wapi haya? Na, Ni hekima gani hii aliyopewa huyu? Na, Ni nini miujiza hii mikubwa inayotendeka kwa mikono yake? Huyu si yule seremala, mwana wa Mariamu, na ndugu yao Yakobo, na Yose, na Yuda, na Simoni? Na maumbu yake hawapo hapa petu? Wakajikwaa kwake.” 

Hatuwezi kumtambua Yesu kwa akili za kawaida na ujuzi wa kawaida Yesu alikuja ili wanyenyeevu watu waliovunjika moyo waweze kumkubali na watu wenye kiburi waweze kukataliwa Yesu ataendelea kuwa jiwe la kukwaza kwa watu wote wanaojidhani kuwa wana hekima ya mwilini na watu wote wenye kiburi na wale wanaojihesabia haki na ndio maana Yesu alipokuja duniani Mafarisayo ambao  walifikiriwa kuwa ndio wenye Haki waliumbuliwa na kujulikana kama wanafiki, wale waliokuwa wakiitumainia haki yao wenyewe waliumbuka na kujiona kuwa sio kitu kila mtu anayejitumainia na kujiamini mwenyewe Yesu kama jiwe la kukwaza litawasaga tikitiki, watu wasio na akili huitegemea akili yao wenyewe, lakini Yesu ameifanya hekima ya dunia hii kuwa ni upuuzi na kuifanya kuwa si kitu ni kupitia kumwamini Yesu tu tunaweza kuokolewa na kuhesabiwa haki kutoka kwa Mungu, kila anayemuami Yeye hatatahayari wala hatakwazika lakini kila anayejitumainia atakwazika na kukengeuka na kuingia katika hukumu ya Mungu. Mungu hawezi kueleweka kwa hekima ya kibinadamu, wengi waliokosa Baraka za Mungu ni wale waliopuuzia neno la Mungu na kuona kama Yesu hana maana lakini wale wanaomkubali wanazijua nguvu zake na uwezo wake 

1Wakoritho 1:18-19 “Kwa sababu neno la msalaba kwao wanaopotea ni upuzi, bali kwetu sisi tunaookolewa ni nguvu ya Mungu. Kwa kuwa imeandikwa, Nitaiharibu hekima yao wenye hekima, Na akili zao wenye akili nitazikataa.”   
              

Rev. Innocent Samuel Kamote.

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni