Jumatano, 16 Novemba 2022

Akikulazimisha maili moja nenda naye mbili !


Mathayo 5:39-41Lakini mimi nawaambia, Msishindane na mtu mwovu; lakini mtu akupigaye shavu la kuume, mgeuzie na la pili. Na mtu atakaye kukushitaki na kuitwaa kanzu yako, mwachie na joho pia. Na mtu atakayekulazimisha mwendo wa maili moja, nenda naye mbili.”


Utangulizi:

Mathayo 5:38-42 ni  mojawapo ya sehemu muhimu sana katika hotuba ya Yesu Kristo ya Mlimani ambapo Yesu anafundisha namna ya kuonyesha muitikio wakati mtu anapokudhalilisha au kukutesa, wakati kanuni za msingi wa agano la kale zilikuwa zinakazia usawa na malipo ya jino kwa jino au jicho kwa jicho zikimaanisha kwamba mtu akikufanyia kosa Fulani alipaswa kulipizwa sawasawa na ukubwa wa kosa hilo, yaani kimahakama mtu apewe adhabu inayolingana na makosa yake, Lakini Kristo anakuja na mtazamo tofauti mno wakati mtu anapotendewa mambo yasiyo ya haki, Yesu anawataka wakristo kuonyesha uvumilivu mkubwa sana bila kulipiza kisasi, badala yake kuwapenda maadui na  hata kuwatendea mema yaliyopitiliza!

Akikulazimisha maili moja nenda naye mbili !

Nyakati za Biblia wakati wa Yesu Kristo, Israel pamoja na mataifa mengine yalikuwa chini ya utawala wa kikoloni wa warumi, Wakoloni wa kirumi hata hivyo kuna wakati hawakuweza kuwatendea haki raia wa kawaida na hasa raia wa kiyahudi, waliwaburuza barabarani na pia kuwalazimisha kubeba mizigo mizito kama watumwa  hali hii ilipelekea wakati mwingine kuamsha gahadhabu na kuchochea watu kutaka kujilipizia kisasi, kitamaduni ilikuwa inawasukuma sana wayahudi kutaka kujilipizia kisasi na kujitangazia uhuru na utawala

Baadhi ya wale waliokuwa wakimfuata Yesu, kwa kuwa walitambua kuwa ndiye Masihi walikuwa na fikra kuwa ataushimamisha ufalme wa Mungu kwa kuuondoa utawala wa Warumi hata hivyo amri ya Yesu Kristo na fundisho lake lilikuwa kinyume na matarajio yao na liliwashangaza sana  yeye aliwafundisha kuwa wakubaliane na mateso yale hata ikiwezekana zaidi ya kile walichokuwa wakifanyiwa, Yesu alisisitiza kuwa wakilazimishwa maili moja na waende nao mbili.

Kimsingi Yesu hakuwa anafundisha wanafunzi wake kuwa dhaifu kama wengi wanavyoweza kudhani, badala yake Yesu alikuwa anamaanisha kuwa hakuna mtu dhaifu duniani, Yesu alikuwa anatufundisha kuwa watu Hodari na wavumilivu kiasi cha kuweza kuvumilia watu waovu na kuwapa maadui zaidi ya kile wanachokitarajia, Kristo hakutaka wakristo washindwe na ubaya badala yake alikuwa akitutaka tuushinde uovu kwa wema

Warumi 12:19-21 “Wapenzi, msijilipize kisasi, bali ipisheni ghadhabu ya Mungu; maana imeandikwa, Kisasi ni juu yangu mimi; mimi nitalipa, anena Bwana. Lakini, Adui yako akiwa na njaa, mlishe; akiwa na kiu, mnyweshe; maana ufanyapo hivyo, utampalia makaa ya moto kichwani pake. Usishindwe na ubaya, bali uushinde ubaya kwa wema.”  

Yesu anawataka wafuasi wake watoe zaidi ya kile ambacho ulimwengu unaweza kutoa, Yesu hataki tuwe dhaifu lakini anataka tuwe wavumilivu kwa wanadamu ambao ni wadhaifu sana, wakristo wanapaswa kuwa hodari na wenye nguvu kiasi cha kuzalisha mambo bora wakati wengine wakizalisha uovu, hatuwezi kuwa sawa na wana wa ibilisi, sisi ji lazima mtuwe wakamilifu kama baba yetu wa Mbinguni alivyo mkamilifu,  Ubaya wa watu waovu kamwe haupaswi kuwa sababu ya kuvunjika moyo kwa wakristo na badala yake lazima sisi tuzalishe jamno lililobora ili kuonyesha kuwa wao ni wapuuzi.

Maandiko yanamsifia mtu anayejitawala kuwa bora kuliko shujaa, mtu anayeweza kujizuia nafi yake asikasirike ni mwema sana kuliko hata mtu mwenye uwezo wa kuteka mji, Wakristo waliokomaa kiroho hawasukumwi kamwe na misukumo ya kihisia bali wanakuwa wenye nguvu ndani kwa kuonyesha kuwa wanaweza kujizuia hata pale mtu anapotaka wakasirike

Mithali 16:32 “Asiye mwepesi wa hasira ni mwema kuliko shujaa; Na mtu aitawalaye roho yake kuliko mtu atekaye mji.”

Mtu mwenye ukomavu wa hali ya juu ni yule ambaye anaweza kuwasamehe adui zake na kuwapenda, Daudi ni moja ya Mfano wa watu waliokuwa wanaweza kuushinda ubaya kwa wema hakuwahi kufurahia hata kufa kwa adui zake kabisa   

2Wafalme 19:4-6 “Mfalme akajifunika uso; na mfalme akalia kwa sauti kuu, Mwanangu Absalomu, Absalomu, mwanangu, mwanangu! Basi Yoabu akaingia nyumbani kwa mfalme, akasema, Wewe leo umefedhehesha nyuso za watumishi wako wote, waliokuokoa leo roho yako, na roho za wanao, na za binti zako, na roho za wakezo, na roho za masuria wako; kwa kuwa unawapenda wakuchukiao, na unawachukia wakupendao. Maana umetangaza leo ya kuwa wakuu na watumishi wako si kitu kwako; maana leo nimetambua hivi; kama Absalomu angaliishi, na sisi sote tungalikufa leo, ingalikuwa vyema machoni pako.”

Luka 6:27-30 “Lakini nawaambia ninyi mnaosikia, Wapendeni adui zenu, watendeeni mema wale ambao wawachukia ninyi, wabarikieni wale ambao wawalaani ninyi, waombeeni wale ambao wawaonea ninyi. Akupigaye shavu moja, mgeuzie la pili, naye akunyang'anyaye joho yako, usimzuilie na kanzu. Mpe kila akuombaye, na akunyang'anyaye vitu vyako, usitake akurudishie.”

Mitume wa Bwana adiha walisisitiza pia fundisho hili la bwana na kuwataka wakristo kutokuwa watu wa kulipa baya kwa baya, wala laumu kwa laumu na wanatakiwa kubariki hata watu wanaowafanyia  maovu kwa kufanya hivi inaashirikia ukomavu mkubwa na unaonyesha kuwa sisi kweli tumekuwa wanafunzi wa Yesu kweli kweli jambo hili linapaleka habari njema kwa maadui wa Ukristo na kuwafanya wamkubali Kristo!

1Petro 3:9 “Neno la mwisho ni hili; mwe na nia moja, wenye kuhurumiana, wenye kupendana kama ndugu, wasikitikivu, wanyenyekevu; watu wasiolipa baya kwa baya, au laumu kwa laumu; bali wenye kubariki; kwa sababu hayo ndiyo mliyoitiwa ili mrithi baraka.”

Hitimisho:

Aina hii ya muiikio ndio utakaosababisha watu wauone uzuri wa Mungu hata katika maisha ya wale wanaowashutumu, kuwaonea na kuwatesa, aidha hii itamfanya mtu muovu akome kuutumia uovu wake kukomoa wakristo, kwa hiyo mateso na nia ovu za watu wabaya hazitakuja zishinde nguvu ya Mungu na uwepo wa utendaji nwa Kristo katika maisha yetu siku zote za maisha yetu. Nabii Elisha aliwahi kuitumia njia hii na washamu wakaacha kuwafuatia Israel kwa muda mrefu ona

2 Wafalme 6:19-23 “Elisha akawaambia, Njia hii siyo, na mji huu sio, nifuateni mimi, nami nitawapeleka kwa mtu yule mnayemtafuta. Akawapeleka Samaria. Hata walipokwisha kuingia Samaria, Elisha akasema, Bwana wafumbue macho watu hawa, wapate kuona. Bwana akawafumbua macho wakaona; kumbe! Walikuwa katikati ya Samaria. Naye mfalme wa Israeli alipowaona, akamwambia Elisha, Ee baba yangu, niwapige? Niwapige? Akamjibu, Usiwapige; je! Ungetaka kuwapiga watu ambao umewatwaa mateka kwa upanga wako na uta wako? Weka chakula na maji mbele yao, wapate kula na kunywa, na kwenda kwa bwana wao. Basi akawaandalia chakula tele; nao walipokwisha kula na kunywa, akawaacha, wakaenda zao kwa bwana wao. Na vikosi vya Shamu havikuja tena katika nchi ya Israeli.

Na Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni