Luka 16: 9 - 12 “Nami nawaambia, Jifanyieni rafiki kwa mali ya udhalimu,
ili itakapokosekana wawakaribishe katika makao ya milele. Aliye mwaminifu
katika lililo dogo sana, huwa mwaminifu katika lililo kubwa pia; na aliye
dhalimu katika lililo dogo, huwa dhalimu katika lililo kubwa pia. Basi, kama
ninyi hamkuwa waaminifu katika mali ya udhalimu, ni nani atakayewapa amana mali
ya kweli? Na kama hamkuwa waaminifu katika mali ya mtu mwingine, ni nani
atakayewapa iliyo yenu wenyewe? Hakuna mtumishi awezaye kutumikia mabwana wawili; kwa
maana, ama atamchukia huyu na kumpenda huyu, ama atashikamana na huyu na
kumdharau huyu. Hamwezi kumtumikia Mungu na mali. ”
Utangulizi:
Mojawapo ya kifungu kigumu katika
tafasiri za mafundisho ya Yesu ni pamoja na maneno haya ambayo Yesu aliyasema
kama sehemu ya Hitimisho ya mfano tajiri na wakili wake, katika Luka 16:1-8 ambako kimsingi Yesu Kristo
alikuwa anatufundisha wazi namna ya kutumia fedha na mali tulizopewa na Mungu
na ujuzi ya kuwa hatuna tunachomiliki duniani, na kuwa tunwajibika namna tunavyotumia
mali na fedha na kwamba tutatoa hesabu ya kila alichotupa Mungu. Baada ya
fundisho hilo Muhimu ndipo sa Yesu alianza kuweka mikazo ya maneno haya
tunayojifunza leo JIFANYIENI RAFIKI KWA
MALI YA UDHALIMU! Kimsingi Yesu alikuwa anafundisha namna ya kujipatia
utajiri wa kweli. Yesu qanawataka wanafunzi wake kutumia fedha na mali za
ulimwengu huu walizonazo kujipatia thawabu za kudumu katika ufalme wa Mungu.
Tutajifunza somo hili kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-
Ø Tafasiri
ya Mali, fedha, Utajiri na udhalimu wakati wa Yesu Mst9-11
Ø Jifanyieni
rafiki kwa mali ya Udhalimu Msta 9-12
Ø Jinsi
ya kumtumikia Mungu na Mali Mst 13
Tafasiri ya Mali, fedha, Utajiri na udhalimu wakati wa Yesu (Mst9)
Luka 16:9-11 “Nami nawaambia, Jifanyieni
rafiki kwa mali ya udhalimu, ili itakapokosekana wawakaribishe katika makao ya
milele. Aliye mwaminifu katika lililo
dogo sana, huwa mwaminifu katika lililo kubwa pia; na aliye dhalimu katika
lililo dogo, huwa dhalimu katika lililo kubwa pia. Basi, kama ninyi hamkuwa waaminifu katika
mali ya udhalimu, ni nani atakayewapa amana mali ya kweli?”
Ni muhimu kufahamu kuwa wakati wa
Yesu Kristo katika mwili Duniani falsafa kuhusu Mali utajiri na fedha ilikuwa
na mitazamo mikubwa mwiwili, hasa katika jamii ya mafarisayo na watu wa
ulimwengu wa wakati ule Katika mtazamo wa kwanza wa Mafarisayo hasa katika
lugha ya KIARAMU, kuwa na Mali, fedha
na utajiri kulihusishwa moja kwa moja na dhuluma (UDHALIMU). Kwa kiyunani ni “ADIKOS”- Wicked, treacherous, unjust au
unrighteousness, Matajiri walikuwa
wanafikiriwa kuwa ni watu dhalimu na kuwa walivyonavyo wamevipata kwa kudhulumu
au kwa njia zisizofaa kwa hiyo walivipata kwa kufanya dhambi, kwa njia za uovu,
kudhulumu watu kwa hila, au isivyo
sawasawa na pia walivitumia kwa anasa na ubinafsi mkubwa ona
Yakobo 5:1-6 “Haya basi, enyi matajiri!
Lieni, mkapige yowe kwa sababu ya mashaka yenu yanayowajia. Mali zenu zimeoza,
na mavazi yenu yameliwa na nondo. Dhahabu yenu na fedha yenu zimeingia kutu, na
kutu yake itawashuhudia, nayo itakula miili yenu kama moto. Mmejiwekea akiba
katika siku za mwisho. Angalieni, ujira wa wakulima waliovuna mashamba yenu,
ninyi mliouzuia kwa hila, unapiga kelele, na vilio vyao waliovuna vimeingia
masikioni mwa Bwana wa majeshi. Mmefanya anasa katika dunia, na kujifurahisha
kwa tamaa; mmejilisha mioyo yenu kama siku ya machinjo. Mmehukumu mwenye haki
mkamwua; wala hashindani nanyi.”
Kwa hiyo fedha na mali na utajiri
ulifikiriwa na kuhusishwa na choyo na dhambi katika mtazamo wa kwanza, lakini
vilevile katika mtazamo mwingine au falsafa ya pili fedha ilifikiriwa kuwa ni
Baraka kutoka kwa Mungu kama mmiliki alikuwa amezipata kwa haki huku akiwa
anamcha Mungu,
Marko 10:17-23 “Hata alipokuwa akitoka
kwenda njiani, mtu mmoja akaja mbio, akampigia magoti, akamwuliza, Mwalimu
mwema, nifanye nini nipate kuurithi uzima wa milele? Yesu akamwambia, Kwa nini
kuniita mwema? Hakuna aliye mwema ila mmoja, ndiye Mungu. Wazijua amri, Usiue,
Usizini, Usiibe, Usishuhudie uongo, Usidanganye, Waheshimu baba yako na mama
yako. Akamwambia, Mwalimu, haya yote nimeyashika tangu utoto wangu. Yesu
akamkazia macho, akampenda, akamwambia, Umepungukiwa na neno moja. Enenda,
ukauze ulivyo navyo vyote, uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni;
kisha njoo unifuate. Walakini yeye akakunja uso kwa neno hilo, akaenda zake kwa
huzuni; kwa sababu alikuwa na mali nyingi. Yesu akatazama kotekote, akawaambia wanafunzi
wake, Jinsi itakavyokuwa shida wenye mali kuingia katika ufalme wa Mungu! ”
Hata hivyo Matajiri wote wale
waliofikiriwa ni wadhuluma na wale wa haki wote walikuwa na matatizo wote
walikuwa wanakabiliwa na choyo na ubinafsi, na hivyo Yesu yeye alizuiona fedha
mali na utajiri wa dunia hii kama havitatumika kwa usahihi madamu ni mali za
duniani zote aliziita mali za udhalimu, kwa nini kwa sababu haziwezi kuwapa
wanadamu manufaa ya kudumu katika ulimwengu wa ufalme wa Mungu.
Jifanyieni rafiki kwa mali ya Udhalimu Msta 9-12
Kama tulivyojifunza hapo awali ya
kuwa Yesu aliona matumizi yote ya fedha kwa watu wa dunia hii bila kujali mali
zao wamezipataje mali zao zingeliweza kuwapa manufaa ya kudumu kama watakosa
akili na ufahamu wa kutosa katika kuzitumia, akiendelea kukazia mfano wa wakili
dhalimu alioutoa katika Luka 16:1-8 Kwamba pamoja na kuwa wakili yule alikuwa
afukuzwe kazi, alikumbuka kuwa kuna maisha baaya ya kufukuzwa kazi na hivyo
alikumbuka kujiandalia marafiki kwa mali yake ya udhalimu ilia je kunufaika
baadaye, aidha matajiri wa dunia hii vilevile wakati ule waliweza kutumia
fedha kujipatia marafiki na hata kujiongezea umaarufu duniani na ilikuwa rahisi
kukubalika kwa sababu ya uwezo mkubwa wa kifedha waliokua nao
Mfano hata leo kama utahitaji
kugombea ubunge na vyeo vinginevyo vya kikampeni, utaweza kuona kwamba ni
lazima uwe na fedha za kutosha kuweza kuongeza ushawishi kujipatia nafasi
uitakayo wazo hili hili alilokuwa nalowakili dhalimu kuhusu kesho yake
lingeweza vilevile kutumiwa na wanafunzi wa Yesu kuwa na ujuzi na hekima na
akili ya kujitengenezea maisha ya baadaye kwa kuwekeza katika Mungu, tunaweza
kutumia fedha mali na utajiri kwa makusudi
mema, tunaweza kuzitumia mali fedha na
utajiri wao (Kwa Mtazamo wa Kiaramu Mali ya Udhalimu) kwa lengo zuri la
kuujenga ufalme wa Mungu, badala ya kutumia fedha na mali na utajiri wetu
kujifurahisha, kwa choyo na ubinafsi, tunaweza kuitumia kujijengea jina kwa
kuwekeza kwa Mungu na kuwatendea mema wengine jambo litakalotufanya tuwe
matajiri katika kazi njema kwa msingi huo
Agizo hili la Kristo linaweza
kutafasiriwa sambamba na,
1Timotheo 6:17-18 “Walio matajiri wa
ulimwengu wa sasa uwaagize wasijivune, wala wasiutumainie utajiri usio yakini,
bali wamtumaini Mungu atupaye vitu vyote kwa wingi ili tuvitumie kwa furaha.
Watende mema, wawe matajiri kwa kutenda mema, wawe tayari kutoa mali zao, washirikiane
na wengine kwa moyo;”
kwa hiyo kama hatutakuwa
waaminifu kuitumia mali, fedha na utajiri huu wa duniani (Wa Kidhalimu) kwa
Mungu wetu, Mungu naye hatatatutumia au kutuamini katika mambo Halisi ya kweli
ya ufalme wa Mbinguni, huko tutakuwa na hazina isiyoharibika, Kimsingi Yesu hakuwa anamaanisha kuwa na
fedha ni jambo baya wala hakuwa anatia moyo kuwa watu wajitafutie fedha kwa nia
mbaya au kwa njia zisizofaa, lakini kama waili yule muovu alikuwa na uwezo wa
kufikiri kuhusu maswala yajayo kwanini matajiri wa kawaida wawe wachoyo na kushindwa kuutumia utajiri wao ambao
kimsingi utawanufaisha tu hapa duniani kisha wasahau kujiwekeza katika ufalme
wa Mbinguni. Aidha tunaweza kuzitumia fedha zetu sio kwaajili ya kutafuta
umaarufu lakini kuwasaidia wengine wenye uhitaji jambo ambalo pia linatupa
thawabu Mbinguni, Mungu anapotumilikisha fedha mali na utajiri maana yake
ametuamini kuwa tunaweza kutunza kwaajili ya wote na sio kwaajili yetu, hivuo
kila Mkristo anapaswa kuwa mwaminifu katika kutumia rasilimali ambazo Mungu
ametupa kwa faida ya ufalme wake!
“Luka 6:11 Basi, kama ninyi hamkuwa
waaminifu katika mali ya udhalimu (mali fedha na
utajiri wa Duniani), ni nani atakayewapa amana mali ya kweli (ya ufalme
wa Mungu, na umilele)”?
Jinsi ya kumtumikia Mungu na Mali Mst 13
Kimsingi Bwana wetu Yesu Kristo
anauona mlango ni mdogo sana kwa wenye utajiri kuingia katika ufalme wa Mungu
kwa sababu ya ubinafsi na choyo, Wakristo ni lazima waende mbele zaidi na
kujifunza kumpa Mungu kipaumbele kikubwa zaidi na jamii, Mungu anapokuwa ametubarikia wingi wa mali,
fedha na utajiri vilevile anataka tuvutumie kwa utkufu wake na kumuabudu yeye
Kutoka 10:8-11 “Musa na Haruni wakaletwa
tena kwa Farao; naye akawaambia, Nendeni, mkamtumikie BWANA, Mungu wenu; lakini
ni kina nani watakaokwenda? Musa akamjibu, Tutakwenda na vijana wetu na wazee
wetu, na wana wetu, na binti zetu, tutakwenda na kondoo zetu na ng'ombe zetu;
kwa kuwa inatupasa kumfanyia BWANA sikukuu. Lakini akawaambia, Ehe, BWANA na
awe pamoja nanyi, kama nitakavyowapa ruhusa kwenda zenu pamoja na watoto wenu;
angalieni, kwa kuwa pana uovu huko mbele yenu. Sivyo; endeni ninyi mlio watu
wazima, mkamtumikie BWANA; kwa kuwa ndilo jambo mtakalo. Nao walifukuzwa usoni
pa Farao.”
Mungu anapotuita Kumuabudu yeye
na kumfanyia ibada hatuiti nusu nusu
anakuwa ametuita sisi na kila
tulichonacho, kama sisis ni watumishi wake basi kila tunachomiliki ni kwaajili
ya utumishi ulioko mbele yetu, sisis ni mawakili tu ambao tumeaminiwa na Mungu, na tunawezaje kuonyesha imani yetu kwa Mungu
ni pamoja na kumuabudu Mungu na kila tunachokitaka! Tunaweza kuonyesha imani
yetu kwa Kristo kwa kumtumikia pamoja na mali zetu, katika kila jambo lazima
tumpe Mungu kipaumbele na kuonyesha ya kuwa ni yeye anayetawala na wala sio
mali zinazotutawala, kutawaliwa na fedha kuliko kutawaliwa na Mungu ni kosa la
kiufundi katika maswala ya kiroho, lazima Bwana awe juu ya kila kitu na kila
kitu kitiishwe chini yake
Luka 16:13 “Hakuna mtumishi awezaye
kutumikia mabwana wawili; kwa maana, ama atamchukia huyu na kumpenda huyu, ama
atashikamana na huyu na kumdharau huyu. Hamwezi kumtumikia Mungu na mali”
1Timotheo 6:10 “Maana shina moja la mabaya
ya kila namna ni kupenda fedha; ambayo wengine hali wakiitamani hiyo wamefarakana
na Imani, na kujichoma kwa maumivu mengi.”
Unaona kila mmoja wetu anapaswa
kujiuliza kuwa je ni
1. Mungu
anayemiliki kila kitu katika maisha yake?
2. Je
una moyo wa ukarimu au kuna hali ya choyo katika maisha yako?
3. Je
unatenga fungu la kumtolea Mungu katika maisha yako?
4. Je
unahofu ya kuwa utapungukiwa?
Mafarisayo ambao kwa kweli
walikuwa wamekwisha zama katika mtego wa kupenda fedha walijikwaa kwa
mafundisho ya Kirsto na kumpuuzia kwa sababu choyo kilikuwa ikmetawala nia zao
na mioyo yao ili hali wakati huo huo wakijikinai kuwa ni watumishi wa Haki. ona
Luka 16:14 -15 “Basi Mafarisayo, ambao
wenyewe ni wapenda fedha, waliyasikia hayo yote, wakamdhihaki. Akawaambia,
Ninyi ndinyi mnaojidai haki mbele ya wanadamu, lakini Mungu awajua mioyo yenu;
kwa kuwa lililotukuka kwa wanadamu huwa chukizo mbele za Mungu.”
Na Rev. Innocent Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!
Asante kwa mafundisho, barikiwa sana
JibuFuta