Jumapili, 17 Septemba 2023

Uhusiano wa uzuri na ulimwengu wa roho


1Wafalme 1:1 – 4  Mfalme Daudi alikuwa mzee, mkongwe katika siku zake, nao wakamfunika nguo, lakini asipate moto. Kwa hiyo watumishi wake wakamwambia, Bwana wangu mfalme na atafutiwe kijana mwanamwali; naye asimame mbele ya mfalme, amtunze; alale kifuani mwako, ili bwana wangu mfalme apate moto. Basi wakatafuta kijana mzuri mipakani mwote mwa Israeli, wakamwona Abishagi, Mshunami, wakamleta kwa mfalme. NAYE KIJANA HUYO ALIKUWA MZURI SANA; akamtunza mfalme, akamtumikia; walakini mfalme hakumjua.”





 

Utangulizi.

Ni muhimu kwetu kuwa na ufahamu ya kwamba uko uhusiano mkubwa sana wa uzuri na ulimwengu wa roho, kuwa mzuri pekee bila kuwa na hamu ya kumpenda Mungu,  au kuwa na tabia ya kumcha Mungu kunauweka uzuri wako katika hatari kubwa sana ya kushambuliwa kiroho na ulimwengu wa kiroho wa shetani na kukuweka katika matumizi ya haribiko kubwa la mwili wako na roho yako, yaani uzuri wa mwili wako bila tabia ya kumcha Mungu ni msiba mkubwa sana, Wakati kuna fahari kubwa sana mtu anapokuwa mzuri kimwili, kimaadili na kiroho, jambo hilo huleta Baraka kubwa sana! Maandiko yanatuonyesha wazi kuwa Mungu aliwatumia watu wazuri kimwili na kiroho kuwa Baraka kubwa sana kwa ulimwengu hata leo mfano:-

Kutoka 2:1-2 “Mtu mmoja wa nyumba ya Lawi akaondoka akaoa binti mmoja wa Lawi. Yule mwanamke akachukua mimba akazaa mwana, na alipoona ya kuwa ni mtoto mzuri akamficha miezi mitatu.”

1Samuel 16:11-13 “Kisha Samweli akamwambia Yese, Watoto wako wote wapo hapa? Naye akasema, Amesalia mdogo wao, na tazama, anawachunga kondoo. Basi Samweli akamwambia Yese, Tuma watu, wamlete; kwa sababu hatutaketi hata atakapokuja huku. Basi akatuma mtu, naye akamleta kwao. Naye alikuwa mwekundu, mwenye macho mazuri, na umbo lake lilikuwa la kupendeza. Bwana akasema, Ondoka, umtie mafuta; maana huyu ndiye. Ndipo Samweli akaitwaa pembe yenye mafuta, akamtia mafuta kati ya ndugu zake; na roho ya Bwana ikamjilia Daudi kwa nguvu tangu siku ile. Basi Samweli akaondoka, akaenda zake Rama.”        

Esta 2:7 “Naye alikuwa amemlea Hadasa, yaani, Esta, binti wa mjomba wake, kwa kuwa hana baba wala mama. Naye msichana huyu alikuwa wa umbo mzuri na uso mwema; nao walipokufa baba yake na mama yake, yule Mordekai alimtwaa kuwa binti yake yeye.”

Maneno yanayotumika kuelezea uzuri wa sura, umbo, mvuto na maumbile yenye kukubalika na kuvutia katika maandiko ya kiebrania ni pamoja na:-

-          Tob - kuelezea uzuri wa sura na umbo  neno hili limetumika mara 361

-          Yapheh – kuelezea mvuto na mwenye kupendeza limetumika mara 21

-          Mareh –uzuri wa kimaumbile na muonekano hili limetumika mara 35

Maneno yote hayo yalitumika kuelezea muonekano wa nje wa kibinadamu, na ambao pia Mungu aliutumia kwa faida zake au kwaajili ya utukufu wake, maneno hayo yalitumika kumuelezea mwanaume na mwanamke aliyekuwa mzuri kwa muonekano lakini vilevile ambao Mungu aliwatumia katika kazi zake kwa utukufu wake.

Katika vifungu kadhaa vichache hapo juu tumeona maandiko yakitueleza habari za Musa, Daudi na Esta hawa walikuwa wazuri sana kama maandiko yanavyosema lakini vile vile tunaona Mungu akiwatumia vijana hawa wazuri Katika kazi zake kwaajili ya utukufu wake, ni wazi hapa utaona kuwa kuna uhusiano wa uzuri na ulimwengu wa roho, lakini vilevile shetani hutumia watu wazuri, vijana kwa wasichana wazuri katika kutimiza mpango wake wa kuharibu dunia kwa hila. Hivyo katika somo kama hili tunataka kujifunza umuhimu wa kuutumia uzuri kwaajili ya utukufu wa Mungu, Mungu hakukupa uzuri ili uutumie vibaya bali amekupa uzuri kwaajili ya utukufu wake! Tutajifunza somo hili kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-

Ø  Uhusiano wa uzuri na matumizi ya Mungu

Ø  Uhusiano wa uzuri na matumizi ya shetani

Ø  Matumizi ya sahihi ya uzuri katika ulimwengu wa mwili na roho.

Uhusiano wa uzuri na Matumizi ya Mungu.

Kama tulivyoona katika utangulizi wa somo hili ya kwamba Mungu aliumba kila kitu na kila kitu alikifanya kizuri kwaajili ya utukufu wake, tunaona pia Mungu akiwatumia watu mbalimbali katika kuyatimiza mapenzi yake lakini wakati huo huo tunaambiwa kuwa watu hao ambao Mungu aliwatumiwa maandiko yanatuambia kuwa walikuwa wazuri:-

-          Sara ambaye ni mama wa Imani mama aliyemzaa Isaka, mke wa Ibrahimu maandiko yanatueleza ya kuwa alikuwa mzuri sana ona Mwanzo 12:11-14 “Ikawa alipokuwa karibu kuingia Misri, akamwambia Sarai mkewe, Tazama, najua ya kuwa u mwanamke mzuri wa uso; basi itakuwa, Wamisri watakapokuona watasema, Huyu ni mkewe; kisha wataniua mimi na wewe watakuacha hai. Tafadhali useme, wewe u ndugu yangu, iwe heri kwangu kwa ajili yako, na nafsi yangu iishi kwa ajili yako. Basi ikawa Abramu alipofika Misri, Wamisri wakamwona huyo mwanamke ya kwamba yeye ni mzuri sana.”

 

Lakini pamoja na kuwa Sara alikuwa mwanamke Mzuri sana katika muonekanao wa mwili bado mwanamke huyu alikuwa ni Mwanamke wa Imani, alimcha Mungu na alikuwa na tabia njema sana, alimuheshimu mumewe na alikuwa na upendo dhidi ya mumewe kiasi cha kupitiliza, Sara hakuutumia uzuri wake kwa kiburi na Mungu alimtumia kama mwanamke aliyeleta Baraka kupitia Isaka ambaye ni mwana wa ahadi kwao na kwetu pia maandiko yanamsifia Sara kuwa alikuwa na roho ya upole, na utulivu na alimuheshimu sana mumewe na kuwa mfano wa kuigwa katika jamii kama mama wa Imani. Ona

 

1Petro 3:1-6 “Kadhalika ninyi wake, watiini waume zenu; kusudi, ikiwa wako wasioliamini Neno, wavutwe kwa mwenendo wa wake zao, pasipo lile Neno; wakiutazama mwenendo wenu safi, na wa hofu.  Kujipamba kwenu, kusiwe kujipamba kwa nje, yaani, kusuka nywele; na kujitia dhahabu, na kuvalia mavazi; bali kuwe utu wa moyoni usioonekana, katika mapambo yasiyoharibika; yaani, roho ya upole na utulivu, iliyo ya thamani kuu mbele za Mungu. Maana hivyo ndivyo walivyojipamba wanawake watakatifu wa zamani, waliomtumaini Mungu, na kuwatii waume zao. Kama vile Sara alivyomtii Ibrahimu, akamwita Bwana; nanyi ni watoto wake, mfanyapo mema, wala hamkutishwa kwa hofu yo yote.”

 

Unaona Sara alikuwa mzuri wa Uso lakini hakuwa na kiburi, Petro anamtumia kama mfano au kielelezo kwa wanawake wote kuwa kama yeye alikuwa mpole, mwenye utulivu, akimtii Mungu pamoja na mumewe  na Mungu alimtumia kama Baraka kwa ulimwengu mzima kama tulivyoona

 

-          Rebeka - anatajwa katika maandiko kama mwanamke aliyekuwa mzuri wa uso, lakini vilevile ni mwanamke aliyemcha Mungu, alikuwa na tabia nzuri pamoja na ukarimu uliokithiri kwa wanadamu mpaka kwa wanyama, Mungu alimpa neema ya kuolewa na kijana wa Ibrahimu yaani Isaka na baadaye alifanikiwa kuzaa mapacha Esau na Yakobo ambao wamekuwa Baraka kubwa sana kwa ulimwengu na wamekuwa kielelezo cha mafundisho mengi mema ya kifamilia, kiroho na kiuchumi hii ni kwa sababu Rebeka alikuwa mzuri wa uso na mzuri wa tabia na mcha Mungu ona

 

Mwanzo 24:10-26 “Kisha huyo mtumishi akatwaa ngamia kumi katika ngamia za bwana wake akaenda zake, maana mali zote za bwana wake zilikuwa mkononi mwake, akaondoka, akaja mpaka Mesopotamia, mpaka mji wa Nahori. Akawapigisha magoti ngamia nje ya mji karibu na kisima cha maji wakati wa jioni, wakati ambapo wanawake wanakwenda kuteka maji. Naye akasema, Ee BWANA, Mungu wa bwana wangu Ibrahimu, nakuomba mambo yangu uyajalie yawe heri leo, ukamfadhili bwana wangu Ibrahimu. Tazama! Nimesimama karibu na kisima cha maji, na binti za watu wa mjini wanatoka kuteka maji, basi na iwe hivi; yule msichana nitakayemwambia, Tua mtungi wako, nakuomba, ninywe; naye akasema, Unywe, nami nitawanywesha na ngamia zako pia; basi huyu na awe ndiye uliyemchagulia mtumishi wako Isaka; na kwa hayo nitajua ya kuwa umemfadhili bwana wangu. Ikawa, kabla hajaisha kunena, tazama, Rebeka anatokea, binti wa Bethueli mwana wa Milka, mkewe Nahori, ndugu wa Ibrahimu, naye ana mtungi begani pake. Naye yule msichana alikuwa mzuri sana uso wake, bikira, wala mwanamume hajamjua bado; akashuka kisimani, akajaza mtungi wake, akapanda. Ndipo yule mtumishi akapiga mbio kwenda kumlaki, akasema, Tafadhali unipe maji kidogo katika mtungi wako ninywe. Naye akasema, Unywe, bwana wangu, akafanya haraka, akatua mtungi wake mkononi mwake, akamnywesha. Hata alipokwisha kumnywesha akasema, Na ngamia zako nitawatekea, hata watakapokwisha kunywa. Akafanya haraka, akamwaga maji ya mtungi wake katika birika, akapiga mbio kisimani ateke, akawatekea ngamia zake wote. Basi yule mtu akamkazia macho, akanyamaza, ili ajue kwamba BWANA ameifanikisha safari yake ama sivyo. Ikawa, ngamia walipokwisha kunywa, yule mtu akatwaa pete ya dhahabu, uzani wake ulikuwa nusu shekeli, na vikuku viwili kwa mikono yake, uzani wake ulikuwa shekeli kumi za dhahabu, akasema, U binti wa nani wewe? Tafadhali uniambie. Je! Iko nafasi katika nyumba ya baba yako tupate mahali pa kukaa kwa muda? Akasema, Mimi ni binti wa Bethueli mwana wa Milka, aliyemzalia Nahori. Tena akamwambia, Kwetu kuna majani na malisho ya kutosha, na mahali pa kukaa wageni. Yule mtu akainama akamsujudu BWANA.”

 

Unaweza kuona Rebeka alikuwa mzuri sana lakini pamoja na uzuri aliokuwa nao alikuwa na tabia njema na alikuwa amejawa na ukarimu, baadaye pia tunamuona Rebeka akipokea muujiza wa kuwa na mapacha tumboni baada yakuombewa na Isaka na sio hivyo tu pia alitaka kujua mapenzi ya Mungu juu ya watoto wake, na hivyo kuhusika katika unabii mkubwa wa kujua mapenzi ya Mungu kwa watoto wake waliokuwa tumboni, Mwanamke mzuri, tabia nzuri na alimuweka Mungu mbele.

 

-          Yusufu - Mwana wa Israel au Yakobo, alikuwa ni kijana ambaye maandiko yanamtaja kuwa alikuwa mzuri, lakini licha ya kuwa mzuri wa uso pia alikuwa na tabia nzuri, aliwavutia watu akiwemo baba yake, lakini vilevile alimpendeza Mungu alimcha Mungu wa Mbinguni, Mungu alisema naye kuhusu kusudui la kuweko kwake duniani, alimtumia Kule Misri kuhifadhi watu wa dunia ya wakati ule, aliweza kutabiri kurudi kwa wana wa Israel katika inchi ya kanaani kwa kuamuru wabebe mifupa yake baadaye, alitembea na Mungu alikuwa na hofu ya Mungu ona

 

Mwanzo 39:2-9 “BWANA akawa pamoja na Yusufu, naye akasitawi; naye alikuwa katika nyumba ya bwana wake, yule Mmisri. Bwana wake akaona ya kwamba BWANA yu pamoja naye, na ya kuwa BWANA anafanikisha mambo yote mkononi mwake. Yusufu akaona neema machoni pake, akamtumikia. Naye akamweka awe msimamizi juu ya nyumba yake, na yote yaliyomo akayaweka mkononi mwake. Ikawa tokea wakati alipomweka awe msimamizi juu ya nyumba yake, na vyote vilivyomo, BWANA akabariki nyumba ya yule Mmisri kwa ajili ya Yusufu. Mbaraka wa BWANA ukawa juu ya vyote alivyokuwa navyo katika nyumba, na katika shamba. Akayaacha yote aliyokuwa nayo mkononi mwa Yusufu; wala hakujua habari za kitu cho chote chake, ila hicho chakula alichokula tu. Ikawa baada ya mambo hayo, mke wa bwana wake akamtamani Yusufu, akamwambia, Lala nami. Lakini akakataa, akamwambia mke wa bwana wake, Tazama, bwana wangu hajui kitu kilichowekwa kwangu nyumbani, na vyote alivyo navyo amevitia mkononi mwangu. Hakuna mkuu katika nyumba hii kuliko mimi, wala hakunizuilia kitu cho chote ila wewe, kwa kuwa wewe u mkewe. Nifanyeje ubaya huu mkubwa nikamkose Mungu?

 

Yusufu alikuwa kijana mzuri na wa kuvutia sana, mke wa Potifa alimpenda sana na kuvutiwa naye kiasi cha kutaka kumbaka Lakini Yusufu hakukubali, sio kwa sababu alikuwa mjinga hapana alikuwa anamjali Mungu, alimcha Mungu aliogopa kuharibu uhusuano wake na Mungu na hivyo aliutunza na ndio maana unaona Mungu alikuwa pamoja naye.

 

-          Mfalme Sauli – Mfalme wa kwanza wa Israel ambaye Mungu alimuelekeza nabii Samuel amtie mafuta ili awe mfalme wa Israel maandiko yanaeleza kuwa kijana huyu alikuwa mzuri sana  na katika Israel nzima hakukuwa na kijana Mzuri kama yeye ona 

 

1Samuel 9:1-2 “Basi, kulikuwa na mtu mmoja wa Benyamini, jina lake akiitwa Kishi, mwana wa Abieli, mwana wa Serori, mwana wa Bekorathi, mwana wa Afia, mwana wa Mbenyamini, mtu shujaa, mwenye nguvu. Naye alikuwa na mwana, aliyeitwa jina lake Sauli, kijana, tena mzuri; wala katika wana wa Israeli hakuwako mtu mzuri kuliko yeye; tangu mabega yake kwenda juu alikuwa mrefu kuliko watu wote.”

 

Hili ni jambo la kushangaza sana katika maandiko kwani inaonekana wazi kabisa kuwa uzuri ulikuwa unaambatana na mambo mengi sana kuanzia muoneako, akili na ushujaa, ujuzi hekima na werevu, n ahata urefu wake,  ilikuwa wazi kabisa kuwa Mungu alikuwa na anatumia watu wazuri mpaka sasa, kwa hiyo uko uhusiano mkubwa kati ya utumishi wa Mungu na uzuri.

 

-          Abigail - maandiko yanamtaja mwanamke huyu kuwa alikuwa mzuri sana lakini utaweza kuona pia alikuwa na akili sana bahati mbaya tu mara ya kwanza aliolewa na mwanaume mpumbavu mpaka pale Daudi alipomuoa baadaye baada ya kufa kwa mumewe mpumbavu aliyeitwa Nabali ona kisa chao kinatumika kutufundisha kuhusu Torati na Injili kama waume na Abigaili kama mke au kanisa Mume wa kwanza ni Torati na Mume wa Pili ni injili kwa mwanamke yule yule tunaambiwa mwanamke huyo alikuwa mzuri na mwenye akili nyingi sana ona

 

1Samuel 25:2-3 “Na huko Maoni kulikuwa na mtu mmoja, ambaye alikuwa na mali yake katika Karmeli; naye yule mtu alikuwa mkuu sana, mwenye kondoo elfu tatu na mbuzi elfu; naye alikuwa akiwakata manyoya kondoo zake huko Karmeli. Na jina la mtu huyo aliitwa Nabali; na jina la mkewe aliitwa Abigaili, na huyo mwanamke alikuwa mwenye akili njema, mzuri wa uso; bali yule mwanamume alikuwa hana adabu, tena mwovu katika matendo yake; naye alikuwa wa mbari ya Kalebu.”

 

Unaona mwanamke alikuwa mwenye akili njema na pia alikuwa mzuri wa uso, hapa utaweza kugundua jinsi ambavyo uzuri wa kimaumbile ulivyokuwa unakamilishwa na uzuri wa tabia na mwenendo na akili, na roho njema nay a ukarimu kwa hiyo tunaweza kupata piacha iliyo wazi kuwa Mungu alikusudia watu wazuri wa uso wawe vilevile na tabia nzuri na kili ili zitumike kwa utukufu wa Mungu!

 

-          Vijana wa kiibrania Daniel, Hanania na Mishael (Daniel Shadrak na Meshaki na Abednego)

Daniel 1:3-6 “Mfalme akamwambia Ashpenazi, mkuu wa matowashi wake, awalete baadhi ya wana wa Israeli, wa uzao wa kifalme, na wa uzao wa kiungwana;  vijana wasio na mawaa, wazuri wa uso, wajuzi wa hekima, werevu kwa sababu ya maarifa yao, wenye kufahamu elimu, watakaoweza kusimama katika jumba la mfalme; tena alimwambia awafundishe elimu ya Wakaldayo, na lugha yao. Huyo mfalme akawaagizia posho ya chakula cha mfalme, na ya divai aliyokunywa, akaagiza walishwe hivyo muda wa miaka mitatu; ili kwamba hatimaye wasimame mbele ya mfalme. Basi katika hao walikuwapo baadhi ya wana wa Yuda, Danieli, na Hanania, na Mishaeli, na Azaria.”

 

Muda usingeweza kutosha kupitia vijana na mabinti wazuri ambao Mungu aliwatumia katika maandiko lakini ni wazi kuwa utakubaliana nami kuwa Mungu anapenda na kutumia watu wazuri, wenye maadili mema kwaajili ya utukufu wake unaona! Tumewaona vijana waliochukuliwa mateka utumwani Daniel na wenzake maalumu kabisa walichaguliwa vijana wazuri, waungwana , wasio na mawaa wenye hekima akili na werevu na wenye maarifa hawa walichaguliwa na mfalme Nebukadreza ili wamtumikia lakini wote tunajua uhodari wao vile vile wa Imani katika Mungu wa kweli, lakini walikuwa wazuri ni katika hali kama hiyo pia uzuri hutumiwa na ibilisi pia kwa faida zake kama tunavyojifunza katika kipengele kifuatacho:-

 

Uhusiano wa uzuri na matumizi ya shetani

Kama jinsi ambavyo tumeona jinsi ambavyo Mungu aliwatumia vijana wa kike na kiume walio wazuri kuwa watumishi wake naye akitukuzwa kupitia imani zao na matendo yao, hali kadhalika shetani huutumia uzuri kwa kusudi la kuwatumia watu wazuri wa muonekano na sura kwaajili ya kazi zake huku yeye mwenyewe akiwa ni kielelezo cha Matumizi mabaya ya uzuri ona:- 

Ezekiel 28:13-17 “Ulikuwa ndani ya Adeni, bustani ya Mungu; kila jiwe la thamani lilikuwa kifuniko chako, akiki, na yakuti manjano, na almasi, na zabarajadi, na shohamu, na yaspi, na yakuti samawi, na zumaridi, na baharamani, na dhahabu; kazi ya matari yako na filimbi zako ilikuwa ndani yako; katika siku ya kuumbwa kwako zilitengenezwa tayari. Wewe ulikuwa kerubi mwenye kutiwa mafuta afunikaye; nami nalikuweka hata ukawa juu ya mlima mtakatifu wa Mungu, umetembea huko na huko kati ya mawe ya moto. Ulikuwa mkamilifu katika njia zako tangu siku ile ulipoumbwa, hata uovu ulipoonekana ndani yako. Kwa wingi wa uchuuzi wako watu walikujaza udhalimu ndani yako, nawe umetenda dhambi; kwa sababu hiyo nimekutoa kwa nguvu katika mlima wa Mungu, kama kitu kilicho najisi; nami nimekuangamiza, Ewe kerubi ufunikaye, utoke katika mawe hayo ya moto. Moyo wako uliinuka kwa sababu ya uzuri wako; umeiharibu hekima yako kwa sababu ya mwangaza wako; nimekutupa chini, nimekulaza mbele ya wafalme, wapate kukutazama.”              

Yeye mwenyewe Shetani (LUSIFA) maandiko yanatueleza wazi kuwa alikuwa ni malaika mzuri sana  mwenye utukufu mwingi yeye aliyekaa katika uwepo wa Mungu, lakini inaelezwa kuwa MOYO WAKE ULIINUKA KWA SABABU YA UZURI WAKE,  kwa hiyo zawadi ya uzuri wakati mwingine imewaletea wengi majivuno na kuuwafanya wautumie uzuri kutekeleza matakwa ya kishetani  matokeo yake wanakuwa ni wazuri wa sura na muonekano lakini wakiwa hawana uadilifu unaokusudiwa na Mungu, kinyume na makusudi ya Mungu ya kuumba watu wazuri ili awatumie shetani amekuwa akiwatumia wanaume wazuri na wanawake wazuri kwaajili ya tabia mbaya

-          Uzuri umetumiwa kwa kusudi la umalaya Mithali 6:24-26 “Yakulinde na mwanamke mwovu, asikupate, Na kukuponya na ubembelezi wa mgeni. Usiutamani uzuri wake moyoni mwako; Wala usikubali akunase kwa kope za macho yake. Maana kwa malaya mtu hutiwa katika hali ya kuhitaji kipande cha mkate; Na kahaba humwinda mtu anase nafsi yake iliyo ya thamani

 

-          Uzuri unatumiwa na ibilisi kwa makusudi ya ubakaji wakati mwingine  2Samuel 13:1-2. “Ikawa baada ya hayo, Absalomu, mwana wa Daudi, alikuwa na umbu mzuri, jina lake akiitwa Tamari, naye Amnoni, mwana wa Daudi, akampenda. Akasononeka Amnoni, hata akaugua, kwa ajili ya umbu lake Tamari, maana huyu msichana alikuwa mwanamwali, Amnoni akaona ni vigumu kumtendea neno lo lote.”

 

Unaona tunaelezwa kuwa Absalom mwana wa Daudi alikuwa na dada mzuri kiasi ambacho kaka yake Ammnoni alimpenda sana mpaka akaugua yaani aliumwa kwaajili ya ndugu yake ambaye alikuwa mzuri, uzuri wa Tamari ulimpoza kiasi ambacho kaka yake hakuweza kuvumilia wala kusubiri michakato ya kuomba kwa mfalme ili amuoe na badala yake akambaka na kufanya upumbavu ona

 

2Samuel 13:6-14 “Basi Amnoni akalala, akajifanya mgonjwa; na mfalme alipokuja kumtazama, Amnoni akamwambia mfalme Mwache ndugu yangu, Tamari, aje, nakusihi, aniandalie mikate miwili machoni pangu, nipate kula mkononi mwake. Basi Daudi akatuma mjumbe aende nyumbani kwa Tamari, akasema, Nenda sasa nyumbani kwa Amnoni, ndugu yako, ukamwandalie chakula. Akaenda Tamari nyumbani kwa nduguye Amnoni; naye alikuwa amelala. Akachukua unga, akaukanda, akaiandaa mikate machoni pake, akaioka mikate. Akalitwaa kaango, akaisongeza mbele yake; lakini alikataa kula. Naye Amnoni akasema, Toeni watu wote kwangu. Wakatoka kila mtu kwake. Amnoni akamwambia Tamari, Kilete chakula chumbani, nipate kula mkononi mwako. Basi Tamari akaitwaa mikate aliyoifanyiza, akamletea Amnoni nduguye mle chumbani. Naye alipokwisha kuileta karibu naye, ili ale, Amnoni akamkamata, akamwambia, Njoo ulale nami, ndugu yangu. Naye akamjibu, La, sivyo, ndugu yangu, usinitenze nguvu; kwani haifai kutendeka hivi katika Israeli; usitende upumbavu huu. Nami nichukue wapi aibu yangu? Wewe nawe utakuwa kama mmoja wa wapumbavu wa Israeli. Basi, sasa, nakusihi, useme na mfalme; kwa maana hatakukataza kunioa. Walakini yeye hakukubali kusikiliza sauti yake; naye akiwa na nguvu kuliko yeye, akamtenza nguvu, akalala naye.”

 

Tunajifunza hapa kuwa wakati mwingine uzuri wa watu umewaponza, shetani amatumia tamaa za watu kuwashambulia watu wazuri, kama Tamari ambaye alibakwa kwa sababu ya uzuri wake, unaweza kushambuliwa na shetani kwa sababu ya uzuri, sio lazima kwa kubwakwa tu, unaweza kuteswa na mapepo kwa sababu tu wameona u mzuri, unaweza kutupiwa majini na watu kwa sababu tu wameona u mzuri, unaweza kufanyiwa ulaghai wa kila aina kwa sababu tu watu wameona u mzuri, uzuri unaweza kumfanya adui akushambulie, uzuri unaweza kumfanya mtu akakushawishi, uzuri unaweza kufanya hata mumeo akauawa, au hata kama umeolewa bado watu wakaingilia ndoa yako na kukuchukulia ukipendacho kwa sababu ya uzuri, uzuri wako ndio jaribu lako, uzuri wako unaweza kukaribisha changamoto nyingi

 

Uzuri unaweza kuiponza ndoa yako na nyumba yako ona 2Samuel 11:2-4 “Ikawa wakati wa jioni, Daudi akaondoka kitandani, akatembea juu ya dari ya jumba la mfalme; na alipokuwa juu ya dari aliona mwanamke anaoga; naye huyo mwanamke alikuwa mzuri sana, wa kupendeza macho. Naye Daudi akapeleka, akauliza habari za yule mwanamke. Mtu mmoja akasema, Je! Huyu siye Bath-sheba, binti Eliamu, mkewe Uria, Mhiti? Basi Daudi akapeleka wajumbe, akamtwaa; naye akaingia kwake; naye akalala naye; (maana yule mwanamke amekwisha kutakasika unajisi wake); kisha akarudi nyumbani kwake.”

 

Unaiona tunaambiwa kuwa Bathsheba binti Eliamu huyu ndiye mama yake Mfalme Sulemani alikuwa mzuri sana wa kupendeza macho, na Daudi alipomuaona alimtamani na kuagiza aletewe na kuingia kwake, kumbuka kuwa alikuwa mke wa mtu, lakini mtu mwingine mwenye fedha, mamlaka na utawala anaingiwa na tamaa na kuona kuwa mwanamke huyu anafaa kuwa wake na sio hivyo tu alienda mbali na kufanya njama za kumuua mumewe ili amuoe yeye mwanamke yul, uzuri wa mwanamke huyu unamleta katika majonzi na sababu kubwa sana ya maangamizi na dhambi katiika familia ya Daudi, Kwa nini kwa sababu shetani alimpa moyo wa kutokuvumilia alipoona uzuri wa mwanamke huyu, tunajifunza kuwa uzuri wako utawavutia watu wa kila aina wenye tabia mbaya, wenye tamaa, wenye mamlaka na mali ili umuone mumeo au mkeo kuwa mtu duni na wao wakuchukue kwajili ya fahari ya miili yao, wako watu ambao watakuona kama hicho ulicho nacho haustahili kuwa nacho, na ulicho nacho ni chao pia, watataka waonje uzuri wa mumeo watataka waonje uzuri wa mkeo.     

 

-          Uzuri unaweza kutumiwa na shetani kukufanya uwe na kiburi na kukosa adabu  2Samuel 14:25 -27 “Basi katika Israeli wote hapakuwa na mtu hata mmoja mwenye kusifiwa kwa uzuri wake kama huyo Absalomu; tangu nyayo za miguu yake hata utosi wa kichwa chake hapakuwa na ila kwake.  Naye aliponyoa kichwa, (basi mwisho wa kila mwaka hunyoa; na kwa sababu nywele zilikuwa nzito kwake, kwa hiyo akanyoa;) hupima nywele za kichwa chake shekeli mia mbili kwa uzani wa mfalme. Kisha wakazaliwa kwake Absalomu wana watatu na binti mmoja, ambaye jina lake aliitwa Tamari; naye alikuwa mwanamke mzuri wa uso.”

 

Tunasoma hapo katika maandiko ya kwamba Absalom mwana wa Daudi alikuwa gumzo katika Israel kijana alikuwa mzurii, kijana alisifiwa Israel yote kwa sababu ya uzuri wake alikuwa mzuri kutoka utosini mpaka kwenye unyao wa miguu yake  na inaelezwa kuwa hakuwa hata na doa lolote, alikuwa ananyoa mara moja kwa mwaka hivyo alikuwa na nyele nzito, nzuri ndefu zinazoangukia mgongoni au mabegani  n ahata alipofanikiwa kuna na binti binti yake naye alikuwa mzuri uzito wa nywele zake ziliponyolewa ilikuwa ni shekel mia mbili kwa vipimo vya wakati ule shekeli moja kwa sasa ni sawa na  kilogram 0.0114 kwa hiyo 0.0114 x 200 = 2.28 hii ni sawa na kusema Nyele za Absalom ziliponyolewa zilipatikana kilo mbili na gram 28  kwa kweli alikuwa ni kijana mzuri mno mzuri sana na ilikuwa halali aweze kuwa gumzo katika Israel na alipendwa na kukubalika na watu, hata hivyo tunasima mwisho mbaya wa kijana huyu, uzuri wake ulimpa kiburi, akili yake ilijaa hila shetani alimuharibu alimpingua baba yake na nyele zake ambazo zilikuwa ni moja ya fahari yake kubwa sana zilikuwa sababu ya kifo chake licha ya kulala na wake za baba yake na kumuasi na kupigana naye vita  tunasoma hivi

 

2Samuel 18:6 -16 “Hivyo watu wakatoka waende nyikani ili kupigana na Israeli; na vita vikatokea ndani ya msitu wa Efraimu.Watu wa Israeli wakapigwa huko mbele ya watumishi wa Daudi, kukawa na maangamizo makuu huko siku ile, ya watu ishirini elfu. Kwa maana vita vilienea huko juu ya uso wote wa nchi; na siku ile huo msitu ukala watu wengi kuliko wale walioliwa na upanga. Na kwa bahati Absalomu akakutana na watumishi wa Daudi. Naye Absalomu alikuwa amepanda nyumbu wake, na yule nyumbu akapita chini ya matawi manene ya mwaloni mkubwa, hata kichwa chake kikakwama katika mwaloni huo, akanyakuliwa juu kati ya mbingu na nchi; na yule nyumbu aliyekuwa chini yake akaenda mbele. Basi mtu mmoja akaona hayo, akaenda akamwambia Yoabu, akasema, Tazama, mimi nalimwona Absalomu ametundikwa katika mwaloni. Naye Yoabu akamwambia mtu yule aliyempasha habari, Je! Wewe umeona haya; Mbona, basi, hukumpiga hata nchi papo hapo? Nami ningalikupa fedha kumi na mshipi. Yule mtu akamwambia Yoabu, Kama ningalipata fedha elfu mkononi mwangu, hata hivyo singalinyosha mkono wangu juu ya mwana wa mfalme; kwa maana mfalme masikioni mwetu alikuagiza wewe, na Abishai na Itai, akisema, Angalieni sana mtu awaye yote asimguse yule kijana, Absalomu. Na tena, kama ningaliitendea roho yake kwa hila; (wala hapana neno lo lote liwezalo kufichwa mbele ya mfalme); ndipo wewe mwenyewe ungalijitenga. Ndipo Yoabu akasema, Siwezi kungoja na kusema nawe hivi. Akachukua vyemba vitatu mkononi mwake, akamchoma Absalomu moyoni, alipokuwa akali hai katikati ya ule mwaloni. Kisha vijana kumi, waliomchukulia Yoabu silaha zake wakamzunguka, wakampiga Absalomu, na kumwua. Kisha Yoabu akapiga tarumbeta, wakarudi watu toka kuwafuatia Israeli; kwani Yoabu akawazuia watu.”

 

Ni jambo la kusikitisha sana ya kuwa nyele zake zilezile Absalom ambazo zilikuwa moja ya sababu kubwa ya uzuri wake ndizo zilinasa kichwa chake juu ya mti wa mwaloni na hivyo kuuawa kwa kuchomwa moyoni na kushambuliwa kwa silaha na ukawa mwisho wake ni somo kwetu kuwa wakati mwingine sifa ile ile njema na uzuri ule ule tulio nao unaweza kugeuka au kutumiwa na adui kuwa maangamizi yetu  

 

Kumbuka pia kuwa ni uzuri wake Vashti uliosababisha akapoteza umalikia na kuonyesha dharau kwa mumewe ambaye alitaka kuonyesha fahari kwa wenzako ya kuwa ana mwanamke mzuri na matatat sana ona

 

Esta 1:10-21 “Hata siku ya saba, mfalme alipofurahiwa moyo wake kwa divai, aliwaamuru Mehumani, Biztha, Harbona, Bigtha, Abagtha, Zethari, na Karkasi, wale wasimamizi-wa-nyumba saba waliohudumu mbele za mfalme Ahasuero, wamlete Vashti, malkia, mbele ya mfalme, amevaa taji ya kifalme; ili kuwaonyesha watu na maakida uzuri wake, maana alikuwa mzuri wa uso. Bali Vashti, malkia, alikataa kuja kwa amri ya mfalme kwa mkono wa wasimamizi-wa-nyumba; kwa hiyo mfalme akaghadhibika sana, na hasira yake ikawaka ndani yake. Basi mfalme akawaambia wenye hekima, walio na elimu ya nyakati; maana ndivyo ilivyokuwa desturi ya mfalme kwa wote waliojua sheria na hukumu; na karibu naye wameketi Karshena, Shethari, Admatha, Tarshishi, Meresi, Marsena, na Memukani, wale maakida saba wa Uajemi na Umedi, waliouona uso wa mfalme, na kuketi wa kwanza katika ufalme; akawauliza, Tumfanyieje Vashti, malkia, kwa sheria, kwa sababu hakufanya kama vile alivyoamriwa na mfalme Ahasuero kwa mkono wa wasimamizi-wa-nyumba? Basi Memukani akajibu mbele ya mfalme na maakida, Huyu Vashti, malkia, hakumkosa mfalme tu peke yake, ila na maakida wote, na watu wote pia walioko katika majimbo yote ya mfalme Ahasuero. Kwa maana tendo hilo la malkia litajulikana na wanawake wote, hata waume zao watadharauliwa machoni pao, itakaponenwa ya kuwa mfalme Ahasuero aliamuru Vashti, malkia, aletwe mbele yake, bali hakuja. Hata na leo hivi mabibi wastahiki wa Uajemi na Umedi waliokwisha kuzisikia habari za tendo lake malkia watawaambia vivi hivi maakida wote wa mfalme. Hivyo kutatokea dharau nyingi na ghadhabu tele. Basi mfalme akiona vema, na itoke kwake amri ya kifalme, nayo iandikwe katika sheria za Waajemi na Wamedi isitanguke, ya kwamba Vashti asifike tena mbele ya mfalme Ahasuero; na umalkia wake mfalme ampe mwingine aliye mwema kuliko yeye. Basi mbiu ya mfalme atakayoipiga itakapotangazwa katika ufalme wake wote, nao ni mkubwa, wake wote watawaheshimu waume zao, wakubwa kwa wadogo. Basi neno hili likawapendeza mfalme na maakida; naye mfalme akafanya sawasawa na neno lake Memukani.”

 

Muda usingeweza kutosha kuona namna shetani alivyotumia uzuri kuharibu maisha ya watu tofauti na namna Mungu alivyokusudia, watu wengi tunawasoma kuwa walipata hasara katika maisha yao na machungu katika maisha yao kwa sababu shetani alitumiz uzuri wao kama sababu ya kuharibikiwa kwao, leo hii wanawake kwa wanaume wazuri wasio na ila wala madoa ndio wanaotumiwa katika kupiga picha za ngono, na kurekodi mikanda ya ngono, wanatumiwa kutangaza bidhaa mbalimbali, wanatumiwa katika kutangazaa pombe, sigara na wanatumiwa kama wanengua viuno katika miziki ya dansi, maarufu kama (video queens)  na katika anasa nyingi, wanatumiwa kama vivutia na sehemu ya viburudisho katika jamii sehemu za starehe mbalimbali, wanatumiwa katika madaa, na makasino wanatumika katika maeneo mbalimbali ya kuharibu aina binadamu kwa sababu tu ya uzuri

 

Katika andiko letu la Msingi tunasoma habari za Mwanamke aliyeitwa Abishagi nib inti aliyekuwa mzuri sana mzuri mno, washauri wa mfalme walumuona Daudi kuwa amezeeka na hivyo walitaka kumtia moyo mfalme ili achangamke na kupewa joto, na ndipo alipotafutwa binti huyu aliyekuwa kijana mzuri ili amuhudumie mfalme mzee ambaye kimsingi hakuweza kumgusa lakini alimtumia kwaajili ya kujiburudisha tu, asingeliweza kuzaa naye wala kulala naye lakini binti wa watu alitwaliwa na kutumiwa hovyo tu kwa sababu ya uzuri Abishagi alitumika kama nesi wa mfalme tu na muhudumu wa mfalme tu wa kumpa joto ashukuriwe Mungu kuwa baadaye aliolewa na Mfalme Suleimani lakini ni jambo la kusikitisha kuona uzuri wake ulikuwa kama unapotezewa muda na kutafuta namna ya kubebeshwa ujane, nyakati za leo tunaweza kuona matukio ya namna hii ambapo wazee wanatafuta kujifariji kwa wanawake vijana tena wazuri, hatuwezi kuhukumu lolote lakini tunaweza kukiri kuweko kwa matumizi mabaya ya uzuri na kupotezewa muda na kuachwa ujane kwa sababu ya uzuri

 

1Wafalme 1:1 – 4 “Mfalme Daudi alikuwa mzee, mkongwe katika siku zake, nao wakamfunika nguo, lakini asipate moto. Kwa hiyo watumishi wake wakamwambia, Bwana wangu mfalme na atafutiwe kijana mwanamwali; naye asimame mbele ya mfalme, amtunze; alale kifuani mwako, ili bwana wangu mfalme apate moto. Basi wakatafuta kijana mzuri mipakani mwote mwa Israeli, wakamwona Abishagi, Mshunami, wakamleta kwa mfalme. NAYE KIJANA HUYO ALIKUWA MZURI SANA; akamtunza mfalme, akamtumikia; walakini mfalme hakumjua.”

 

Matumizi  sahihi ya uzuri katika ulimwengu wa mwili na roho.

Ni muhimu kwanza kuelewa kuwa uzuri ni karama ni zawadi anayoitoa Mungu, kama apendavyo yeye mwenyewe tunasoma katika maandiko jinsi Mungu alivyombariki Ayubu baada ya majaribu moja ya zawadi aliyompa ni pamoja na mabinti watatu ambao tunaambiwa walikuwa ni wazuri sana mabinti hao wa Ayubu waliitwa YEMIMA, KESIA NA KEREN  ona Ayubu 42:12-15 “Basi hivyo Bwana akaubarikia huo mwisho wa Ayubu zaidi ya mwanzo wake; naye alikuwa na kondoo kumi na nne elfu, na ngamia elfu sita, na jozi za ng'ombe elfu, na punda wake elfu. Tena alikuwa na wana waume saba, na binti watatu. Akamwita huyo wa kwanza jina lake Yemima; na wa pili akamwita jina lake Kesia; na wa tatu akamwita jina lake Keren-hapuhu. Katika nchi hiyo yote hawakuwapo wanawake waliokuwa wazuri kama hao wana wa Ayubu; na baba yao akawapa urithi kati ya ndugu zao wana waume.” Kwa msingi huo utaweza kukubaliana name kuwa uzuri ni zawadi ambayo Mungu huitoa katika familia kadhaa kama apendavyo Mungu yeye mwenyewe hata hivyo, zawadi au karama ya uzuri ni vema ikatumika vizuri kwaajili yake             

Ni ukweli ulio wazi kuwa uzuri wa mwili bila kujali uadilifu na tabia za kiroho uzuri huo unakuwa ni ubatili mtupu, inaonekana wazi kuwa uzuri wa mwili haujitoshelezi ukibaki pake yake bila uzuri wa kiroho mwili wetu ni hekalu la Roho Mtakatifu na hivyo Mungu amekusudia atukuzwe katika miili yetu ona

1Wakorintho 6:19-20 “Au hamjui ya kuwa mwili wenu ni hekalu la Roho Mtakatifu aliye ndani yenu, mliyepewa na Mungu? Wala ninyi si mali yenu wenyewe; maana mlinunuliwa kwa thamani. Sasa basi, mtukuzeni Mungu katika miili yenu.”

Unaona maandiko yanataka Mungu atukuzwe katika miili yetu kama Mungu ametuumba vizuri na kisha tukashindwa kuutumia uzuri wetu kwa uzuri wa kiroho tutasababisha majaribu makuwa kwa watu na kumuudhi Mungu, tutasababisha majaribu kwa watu na kwetu wenyewe na kumpa shetani nafasi ya kukufuru katika miili yetu, uzuri wa mwili bila uzuri wa kiroho ni sawa na kuwa na ugonjwa unaoambukiza, utasababisha kuenea kwa uharibifu kwa wengine na kwako mwenyewe, uzuri wa mwili bila uzuri wa rohoni ni hatari sana, wote tunakumbuka jinsi Hekalu la Yerusalem lilivyokuwa zuri, hata wanafunzi wa Yesu walikuwa wakimuonyesha Yesu kuwa hekalu lile ni zuri mno, Lakini Yesu aliwaambia haltasalia jiwe juu ya jiwe ambalo halitabomoshwa kwa sababu uziri wa nyumba ile ungekuwa bora kama watu wake wangesimamisha ibada lakini watu walipikuwa waasi na kumsukumia mbali masihi aliyetumwa kwao mbele za Mungu nyumba ile ilionekana kuwa haina maana tena  ona

Mathayo 24:1-2 “Yesu akaenda zake, akatoka hekaluni; wanafunzi wake wakamwendea ili kumwonyesha majengo ya hekalu. Naye akajibu akawaambia, Hamyaoni haya yote? Amin, nawaambieni, Halitasalia hapa jiwe juu ya jiwe ambalo halitabomoshwa.”

Mungu alipokupa uzuri ilikuwa ni dalili iliyo wazi ya kuweka uzuri wake ndani yako, kwa hiyo uko uwezekano mkubwa sana kuwa katika kila mwanadamu aliyeumbwa vizuri ilikuwa Mungu ajifunue kupitia uzuri wake kwaajili ya utukufu wake na ndio maana tunatangulia kuuona uzuri wa kiwmili lakini yamkini Mungu alikusudia pia baadaye kufunua uzuri wa kiroho ndani yake, lakini shetani anapowahi na kuanza kuleta uharibifu ndipo tunapoweza kufikiri kuwa vizuri vizuri viliumbwa kwaajili ya shetani tu hapana Mungu aliumba vitu vizuri kwaajili ya utukufu wake, Hakuna jambo linatia moyo kama kuona wadada wazuri, wakaka wazuri, wamama wazuri, wababa wazuri alafu wakati huo huo wanamcha Mungu kupita kawaida na wana msimamo ya kiroho, wa akili na huku wakiwa mstari wa mbele katika kazi za ukombozi, kama alivyokuwa Musa, Esta, Mariamu, Daniel na wenzake, Daudi, na kadhalika watu ambao walikuwa wazuri sana  kwaajili ya utukufu wa Mungu na wakamtumikia Mungu, shukurani tunayoweza kumrudishia Mungu kwa kutuumba vizuri ni pamoja na kumcha yeye, Lusifa aliumbwa vizuri sana lakini badala yake akawa na kiburi, na kuutumia uzuri wake vibaya Mungu aliahidi ya kuwa atamfukuzilia mbali kwa sababu moyo wake uliinuka kwa sababu ya uzuri, badala ya kuutumia uzuri kwa utukufu wa Mungu, kilichompata Lusifa kinaweza kumpata yeyote ambaye ni mzuri, Mungu anatoa wito kwa wazuri wote leo kugeuka na kuyatoa maisha yao kwa Yesu, msifikiri kuwa uzuri wenu ni kwaajili ya duania hii hapana ni kwaajili ya utukufu wa  Mungu, kila mmoja autumie uzuri kwa kwaajili ya kuonyesha namna anavyoweza kumuadhimisha Mungu balada ya kuwa na kiburi na majivuno kama shetani, aidha nitoe wito kwa wakristo mambibi na mabwana kutokuutumia uzuri wao vibaya wako watu wengine huutumia uzir wao kama ukarimu wa kukubali kila kitu, kwa kuwa ni wazuri basi wanataka kuonjesha uzuri wao kwa kila mtu au kuutumia uzuri wako kwa kiburi na majivuno na kujiinua, bwana ampe neema kila mmoja wetu kuimarisha uzuri wake alionao mwilini kwa kumcha Mungu na kutembea katika uwepo wa Mungu!

Ezekiel 28:13-19 “Ulikuwa ndani ya Adeni, bustani ya Mungu; kila jiwe la thamani lilikuwa kifuniko chako, akiki, na yakuti manjano, na almasi, na zabarajadi, na shohamu, na yaspi, na yakuti samawi, na zumaridi, na baharamani, na dhahabu; kazi ya matari yako na filimbi zako ilikuwa ndani yako; katika siku ya kuumbwa kwako zilitengenezwa tayari. Wewe ulikuwa kerubi mwenye kutiwa mafuta afunikaye; nami nalikuweka hata ukawa juu ya mlima mtakatifu wa Mungu, umetembea huko na huko kati ya mawe ya moto. Ulikuwa mkamilifu katika njia zako tangu siku ile ulipoumbwa, hata uovu ulipoonekana ndani yako.  Kwa wingi wa uchuuzi wako watu walikujaza udhalimu ndani yako, nawe umetenda dhambi; kwa sababu hiyo nimekutoa kwa nguvu katika mlima wa Mungu, kama kitu kilicho najisi; nami nimekuangamiza, Ewe kerubi ufunikaye, utoke katika mawe hayo ya moto. Moyo wako uliinuka kwa sababu ya uzuri wako; umeiharibu hekima yako kwa sababu ya mwangaza wako; nimekutupa chini, nimekulaza mbele ya wafalme, wapate kukutazama. Kwa wingi wa maovu yako, katika uovu wa uchuuzi wako, umepatia unajisi patakatifu pako; basi nimetokeza moto kutoka ndani yako, nao umekuteketeza, nami nimekufanya kuwa majivu juu ya nchi, machoni pa watu wote wakutazamao. Wote wakujuao kati ya kabila za watu watakustaajabia; umekuwa kitu cha kutisha, wala hutakuwapo tena hata milele.”        

 

Na Rev. Innocent Mkombozi Samuel bin Jumaa, bin Athumani Bin Zumbe Salim Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima !

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni