Jumatatu, 25 Septemba 2023

Hata Daudi Mwana wa Yese alirukwa !


1Samuel 16:10-11 “Yese akawapitisha wanawe saba mbele ya Samweli. Samweli akamwambia Yese, Bwana hakuwachagua hawa. Kisha Samweli akamwambia Yese, Watoto wako wote wapo hapa? Naye akasema, Amesalia mdogo wao, na tazama, anawachunga kondoo. Basi Samweli akamwambia Yese, Tuma watu, wamlete; kwa sababu hatutaketi hata atakapokuja huku.”


Utangulizi:

Je wewe umewahi kukataliwa? Umewahi Kurukwa? Umewahi kufanya kazi kwa bidii sana mahali na kwa moyo wako wote lakini hakuna mtu aliyetambua mchango wako, na hatimaye ukawa unapuuziwa tu?  Daudi alikuwa mmojawao! Yeye alikuwa ni kijana wa mwisho kati ya vijana nane wa Mzee Yese, ambaye alikuwa ni Mkulima na mfugaji kutoka kabila la Yuda huko Bethelehemu, lakini kijana huyu aliyekuwa mchunga kondoo alipuuzwa tu, hakujaliwa alirukwa, hakuehesabika kuwa ni kitu! Mungu alipomuagiza Nabii Samuel kwenda kumpaka mafuta mfalme ajaye wa Israel kwa Mzee aitwaye Yese, kila kijana wa Yese alisogezwa mbele ya Samuel katika ibada maalumu ya kumtia mafuta mfalme ajae vijana saba wote waliletwa kwa nini kwa sababu nadhani Karibu wote walikuwa na sifa zinazofaa kwa wao kuwa wafalme na wanadamu walikubali nadhani hata Samuel aliweza kufikiri wazi kuwa mpakwa mafuta angekuwepo pale bila shaka ona !

1Samuel 16:1-3 “Bwana akamwambia Samweli, Hata lini utamlilia Sauli, ikiwa mimi nimemkataa asiwamiliki Israeli? Ijaze pembe yako mafuta, uende, nami nitakupeleka kwa Yese, Mbethlehemi; maana nimejipatia mfalme katika wanawe. Samweli akasema, Nawezaje kwenda? Sauli akipata habari, ataniua. Basi Bwana akasema, Chukua ndama pamoja nawe, ukaseme, Nimekuja ili kumtolea Bwana dhabihu. Ukamwite Yese aje kwenye dhabihu, nami nitakuonyesha utakayotenda; nawe utamtia mafuta yule nitakayemtaja kwako.”

1Samuel 16:4-10 “Samweli akafanya hayo aliyosema Bwana, akaenda Bethlehemu. Wakaja wazee wa mji kumlaki, wakitetemeka, nao wakasema, Je! Umekuja kwa amani? Naye akasema, Naam, kwa amani; nimekuja kumtolea Bwana dhabihu; jitakaseni; njoni pamoja nami kwenye dhabihu. Akawatakasa Yese na wanawe, akawaita kwenye dhabihu. Ikawa walipokuja, alimtazama Eliabu, akasema, Yakini masihi wa BWANA yupo hapa mbele zake. Lakini Bwana akamwambia Samweli, Usimtazame uso wake, wala urefu wa kimo chake; kwa maana mimi nimemkataa. Bwana haangalii kama binadamu aangaliavyo; maana wanadamu huitazama sura ya nje, bali Bwana huutazama moyo. Ndipo Yese akamwita Abinadabu, akampitisha mbele ya Samweli. Naye akasema, Bwana hakumchagua huyu. Ndipo Yese akampitisha Shama. Naye akasema, wala Bwana hakumchagua huyu. Yese akawapitisha wanawe saba mbele ya Samweli. Samweli akamwambia Yese, Bwana hakuwachagua hawa.”

Unaweza kuona kwa vipimo vya kibinadamu wote waloisogezwa ilifikiriwa kuwa wanafaa lakini hata hivyo kwa bahati mbaya Mungu hakuwa amewakusudia hao  Mungu alimuonya Samuel kuwa yeye haaangalii kama wanadamu wanavyoangalia yeye ana mtazamo tofauti na wanadamu kwani yeye anaona tangu moyoni na hazingatii mtazamo wa nje peke yake!

1Samuel 16:7 “Lakini Bwana akamwambia Samweli, Usimtazame uso wake, wala urefu wa kimo chake; kwa maana mimi nimemkataa. Bwana haangalii kama binadamu aangaliavyo; maana wanadamu huitazama sura ya nje, bali Bwana huutazama moyo.”

Unaona aliyekusudiwa alidharauliwa, hakuwa ameonekana kuwa na sifa za kimaongozi, hakuna mtu aliyewajua watoto hawa kwa ukaribu kama  baba na kwa mawazo ya baba mzazi Yese alikuwa anaelewa vizuri sana watoto wenye kufaa kuongoza Israel pengine mapendekezo yake kwa Samuel na hata Kwa Mungu tukinena kiwazimu Yese alikuwa sahihi, yeye ni mzazi hivyo anajua , aliyebaki alikuwa ni mchungaji wa kondoo na kwa nyakati zile wachungaji wa kondoo na mifugo hawakudhaniwa kuwa ni watu safi, walikuwa wachafu ni watu wa porini na ni ngumu kumualika mtu kama huyo kwenye sherehe ya ibada kubwa mbele ya nabii aliyeheshimika sana Samuel hivyo zilikuwepo kila sababu za kumruka au kurukwa kwa kijana yule hii inaweza kumtokea mtu awaye yote miaka ya zamani kufaulu darasa la saba halikuwa jambo rahisi watu wengi sana walirukwa, kwenda kidato cha tano pia halikuwa jambo rahisi kama ilivyo leo na watu wengi walirukwa, wenginehawakwenda hata vyuo vya kawaida walirukwa lakini wengi katika hao Mungu amewatumia kuwa msaada mkubwa kwa taifa letu na makanisani pia, hapa simaanishi kuwa vyeti vya kitaaluma havina maana hapana hata kidogo Mungu alikuwa amemuandaa Daudi kwa namna vyingine hukohuko Porini kuwa kijana jasiri mwenye kuhurumia kondoo ambaye angeweza pia kuwa na huruma kwa kondoo wa Israel Mungu huwaandaa watumishi wake kwa muda mrefu na wa kutosha ili waweze kuja kuwa wenye kufaa kwa utumishi aliowakusudia ilimchukua Mungu miaka 80 kumuandaa Musa, Miaka 30 kumuandaa Yohana kwa huduma ya miezi sita tu Paulo mtume miaka 14 kwaajili ya injili ! Daudi naye alikuwa anaandaliwa kipekee na Mungu na alikuwa amehitimu shule hiyo ambayo hakuwa amemsimulia mtu na sasa Mungu anamuona mtu huyu kuwa anafaa lakini kwa vipimo vya kibinadamu anaonekana kuwa hafai

Wewe ndiye mtu yule !

Kurukwa  na wanadamu sio sababu ya Mungu kutokukutumia, Mungu anamtazamo wake mwingine tofauti sana, Hekima yake ni tofauti sana na Hekima ya kibinadamu, Mungu huchagua vitu vinyonye, vyenye mapungufu, vilivyodarauliwa na au kukataliwa katika hekima ya wanadamu ili avitumie kwa utukufu wake ona

1Wakorintho 1:25-29 “Kwa sababu upumbavu wa Mungu una hekima zaidi ya wanadamu, na udhaifu wa Mungu una nguvu zaidi ya wanadamu. Maana, ndugu zangu, angalieni mwito wenu, ya kwamba si wengi wenye hekima ya mwilini, si wengi wenye nguvu, si wengi wenye cheo walioitwa; bali Mungu aliyachagua mambo mapumbavu ya dunia awaaibishe wenye hekima; tena Mungu alivichagua vitu dhaifu vya dunia ili aviaibishe vyenye nguvu; tena Mungu alivichagua vitu vinyonge vya dunia na vilivyodharauliwa, naam, vitu ambavyo haviko, ili avibatilishe vile vilivyoko; mwenye mwili awaye yote asije akajisifu mbele za Mungu.”

Je wewe umewahi kurukwa? Umewahi kupotezewa? Umewahi kuonekana mbele za watu kuwa hufai hii ilitokea kwa Daudi mwana wa Yese na inawezekana pia ukawa unakubali moyoni mwako kuwa wewe sio mkubwa, wewe sio kama kaka zako, wao wana ujuzi mkubwa wao ni safi wewe ni mchunga mbuzi tu unaweza kujiweka katika daraja lolote la chini unalolitaka na watu pia wanaweza kukuweka katika mzani huo  lakini Mungu anakuita leo na anataka uchangamke kwa sababu wewe ndiye mtu yule wewe ndiye uliyechaguliwa wewe ndiye mtumishi wake  wewe ndiye mtu yule ambaye Mungu ameona moyo wako  na ndiye mtumishi wake aliyekuchagua!

Matendo 13:22-23 “Na alipokwisha kumwondoa huyo, akamwinua Daudi awe mfalme wao ambaye alimshuhudia, akisema, Nimemwona Daudi, mwana wa Yese, mtu anayeupendeza moyo wangu, atakayefanya mapenzi yangu yote. Katika uzao wake mtu huyo Mungu amewaletea Israeli Mwokozi, yaani, Yesu, kama alivyoahidi;”

Unaona Mungu alimuona Daudi tena alipendezwa naye na ni kupitia yeye na katika uzao wake Mungu alimleta Yesu Krito Bwana na Mwokozi wetu  Duniani, Kama Mungu aliweza kumtumia Daudi mchunga kondoo wa kawaida kabisa Mungu hashindwi kukutumia wewe! Iwe unajidharau au iwe umedharaulika au umerukwa!  

Wakati watu wanakutazama kwa jeuri, na kukuona kama hufai katika eneo hili au lile Yeye aliyekuumba anajua wapi unafiti kwa sababu ndiye aliyekuumba anakujua kuliko baba yako mzazi, anakujua kuliko manabii, anajua namna alivyokuandaa anajua uwanja wako wa mafunzo ya vita ulikuwa wapi na hivyo ni yeye ndiye anayependezwa nawe  hata kama wanadamu wanakukataa na kukuona haufai Mungu aliyekuumba anauona moyo wako naye anapendezwa nawe ona :-

Isaya 49:6-10 “naam, asema hivi, Ni neno dogo sana wewe kuwa mtumishi wangu ili kuziinua kabila za Yakobo, na kuwarejeza watu wa Israeli waliohifadhiwa; zaidi ya hayo nitakutoa uwe nuru ya mataifa, upate kuwa wokovu wangu hata miisho ya dunia. Bwana, mkombozi wa Israeli, Mtakatifu wake, amwambia hivi yeye anayedharauliwa na wanadamu; yeye anayechukiwa na taifa hili; yeye aliye mtumishi wao watawalao; Wafalme wataona, watasimama; wakuu nao watasujudu; kwa sababu ya Bwana aliye mwaminifu, Mtakatifu wa Israeli aliyekuchagua Bwana asema hivi, Wakati uliokubalika nimekujibu, na siku ya wokovu nimekusaidia; nami nitakuhifadhi, nitakutoa uwe agano la watu hawa, ili kuiinua nchi hii, na kuwarithisha urithi uliokuwa ukiwa; kuwaambia waliofungwa, Haya, tokeni; na hao walio katika giza, Jionyesheni. Watajilisha katika njia, na juu ya majabali watapata malisho. Hawataona njaa, wala hawataona kiu; hari haitawapiga, wala jua; kwa maana yeye aliyewarehemu atawatangulia, naam, karibu na chemchemi za maji atawaongoza.”

Mungu yuko tayari kumuinua mtumishi wake anayedharauliwa na wanadamu, anayechukiwa na kumfanya kuwa nuru kubwa sana kwa mataifa yote na hivi ndivyo alivyomfanyia Daudi ambaye kweli alidharauliwa lakini sasa ni mwenye sifa kubwa saba duniani, sio yeye tu Hata kristo alikataliwa na kudharauliwa lakini sasa jina la Yesu ni msaada mkubwa kwa watu wote duniani, hiki ndicho Mungu anachiokikusudia kwako wewe unayesioma ujumbe huu na unayepitia changamoto kama hii!         

Leo hii hakuna mtu maarufu sana katika Israel Kama Daudi, Bendera ya Israel ina nyota ya buluu katikati inaitwa nyota ya Daudi amekuwa ni kiongozi maarufu sana hata Yesu aliitwa mwana wa Daudi, alitumiwa na Mungu alikuwa na sifa za kiungu, alimsifu Mungu katika maisha yake, hakufanya jambo bila kumuuliza Mungu, alijaa neno, alikuwa mwenye msamaha, aliwapenda maadui, alipigana vita vingi vya bwana, alipokosea kama wanadamu alitubu, alijinyeneykeza kwa Mungu na Mungu alimtumia katika watu ambao Mungu anajivunia kuwa anapendezwa nao Daudi alikuwa ni mmoja wao, Mungu anakuamini anajua utatenda kwa busara naye atakuinua juu nawe utakuwa juu sana

Isaya 52:13 “Tazama, mtumishi wangu atatenda kwa busara, atatukuzwa, na kuinuliwa juu, naye atakuwa juu sana    

Kama ilivyo kwa Daudi Endelea kuwa hodari, jifunze njia za Mungu, mwamini Mungu jiungamanishe na Mungu katika dua na sala na maombi Na Mungu yule nimwabuduye kwa dhamiri safi atakutokea  na kuifuta aibu yako na kukuweka panapo nafasi na kukuinua juu sana kama yeye mwenyewe alivyokuandaa kwa utukufu wake !

Na Rev. Innocent Kamote

Mkuu wa wajenzi Mwenye Hekima. !



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni