Jumatatu, 2 Oktoba 2023

Mwacheni alaani, Kwa sababu Bwana ndiye aliyemwagiza


2Samuel 16:5-12 “Basi mfalme Daudi alipofika Bahurimu, tazama, kulitoka huko mtu wa jamaa ya nyumba ya Sauli, jina lake akiitwa Shimei, mwana wa Gera; alitoka, akalaani alipokuwa akienda. Tena akamtupia Daudi mawe, na watumishi wote wa mfalme Daudi; na watu wote na mashujaa wote walikuwako mkono wake wa kuume na mkono wake wa kushoto. Na Shimei alipolaani, alisema hivi, Nenda zako! Nenda zako! Ewe mtu wa damu! Ewe mtu usiyefaa!  Bwana amerudisha juu yako damu yote ya nyumba ya Sauli ambaye umetawala badala yake; naye Bwana ametia ufalme katika mkono wa Absalomu mwanao; kisha, angalia, wewe umetwaliwa katika uovu wako mwenyewe, kwa sababu umekuwa mtu wa damu.  Ndipo Abishai mwana wa Seruya, akamwambia mfalme, Mbona mbwa mfu huyu amlaani mfalme bwana wangu? Na nivuke, nakusihi, nikaondoe kichwa chake. Mfalme akasema, Nina nini na ninyi, enyi wana wa Seruya? Kwa sababu yeye analaani, na kwa sababu Bwana amemwambia, Mlaani Daudi, basi, ni nani atakayesema, Mbona umetenda haya?Daudi akamwambia Abishai, na watumishi wake wote, Angalieni, huyu mwanangu, aliyetoka viunoni mwangu, anautafuta uhai wangu; si zaidi Mbenyamini huyu sasa? Mwacheni alaani, kwa sababu Bwana ndiye aliyemwagiza.  Labda Bwana atayaangalia mabaya yaliyonipata, naye Bwana atanilipa mema kwa sababu ya kunilaani kwake leo



Utangulizi:

Absalom Mwana wa Daudi alikuwa ameinuka kinyume na baba yake kwa kusudi la kumpindua na kumuua na kuchukua utawala wake, Hivyo ilimuazimu Daudi na majeshi yake kukimbia kwanza, akiwa njiani anakutana na mtu anaitwa Shimei yeye ni wa jamaa ya familia ya Sauli, Mtu huyu ghafla anaanza kurusha mawe na mavumbi akimlaani Daudi na kumtukana kama mtu aliyechukua madaraka baada ya Sauli, akimshutumu ya kuwa ni Mungu amesababisha machafuko kwa sababu ya Damu ya Sauli na watu wake (Damu ya nyumba ya Sauli), Baadhi ya mashujaa wa Daudi walimkemea na kumuomba Daudi waondoe kichwa cha mbwa mfu huyu, anayemtukana na kumlaani mfalme  jambo hili lilikuwa ni kinyume cha sheria na kinyume cha maagizo ya torati Kutoka 22:28 “Usimtukane Mungu, wala usimlaani mkuu wa watu wako.”

Kumlaani mfalme au kumtukana ni kosa ambalo kwa mujibu wa torati lilikuwa linahalalisha hukumu ya kifo, kama mtu akikubambikizia kesi ya kumtukana mfalme katika Israel pia ilihesabika kuwa umemtukana Mungu unaona?

 1Wafalme 21:8-14.  Basi, akaandika nyaraka kwa jina la Ahabu, akazitia muhuri yake, akazipeleka zile nyaraka kwa wazee, na kwa watu wenye nguvu waliokuwa katika mji wake, waliokaa pamoja na Nabothi. Akaandika katika zile nyaraka, akasema, Pigeni mbiu ya watu kufunga, mkamweke Nabothi juu mbele ya watu,  mkainue watu wawili, watu wasiofaa, ili wamshitaki, na kumshuhudia, kunena, Umemtukana Mungu na mfalme. Kisha mchukueni nje, mkampige kwa mawe, ili afe. Wale wazee wa mji wake, na walio wenye nguvu waliokaa mjini mwake, wakafanya kama Yezebeli alivyowaagiza, kama ilivyoandikwa katika nyaraka alizowapelekea. Wakapiga mbiu ya watu kufunga, wakamweka Nabothi juu mbele ya watu. Na hao watu wawili, watu wasiofaa, wakaingia, wakaketi mbele yake; wale watu wasiofaa wakamshuhudia Nabothi mbele ya watu, wakasema, Nabothi amemtukana Mungu na mfalme. Ndipo wakamchukua nje ya mji, wakampiga kwa mawe hata akafa. Wakampelekea Yezebeli habari, wakasema, Nabothi amepigwa kwa mawe, amekufa.”

Pamoja na kuwa ilikuwa halali kabisa kwa mujibu wa Torati mtu huyo kuuawa na ingekuwa ni makosa kwa mfalme kumuachia kwani naye angekuwa hajaitimiza torati, lakini kwa amri ya kifalme Daudi alimkinga mtu huyo na kuamuru kuwa aachiwe alaani kwa sababu Bwana ndiye aliyeagiza! Daudi hakutaka mtu huyo alipwe apatwe na mabaya wakati ule kwani alikuwa anaamini katika uaminifu wa Mungu, Yeye aliyetoa sheria ana haki ya kuhukumu kwa sheria yake “mwacheni alaani kwa sababu Bwana ndiye aliyemtuma”! Tutajifunza somo hili kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-

·         Puuzia laana zisizo na maana au sababu

·         Kufuata njia ya Mungu

·         Kanuni ya Mungu kuhusu laana na Baraka.

Puuzia laana zisizo na maana au sababu.

Wote tunakubalina ya kuwa tukio kama hili halikuwa tukio rahisi, mara nyingi kama mtu anakulaani au kukutukana wengi wetu tungependa kujibu mapigo mara moja  na wakati huo huo tungeweza kutukana au kulaani mara moja  au tungemuomba Mungu amshughulikie mara moja hili ni jambo la kawaida la kibinadamu hata mimi napenda!

Lakini haikuwa hivyo kwa Daudi, mwana wa Yese yeye alimsamehe mtu huyu, na kuipuuzia laana yake na matukano yake na aliamini katika Mungu ya kuwa Mungu atamlipia na alitazamia kuwa Mungu atamrehemu yeye Daudi na rehema zake zitakuwa juu yake, Daudi aliiona laana ya Shimei na mabaya anayomtakia hayakuwa na mashiko kiasi cha kumfanya Mungu ashawishike kumlaani Daudi kwani laana hiyo haikuwa na maana wala sababu za haki, kwani Daudi hakufanya kosa katika familia ya Sauli iliyokuwa na mashiko ya yeye kulaanika kwa hiyo matusi na laana  za Shimei alizozitoa ilikuwa kama mbayuwayu tu katika kuruka kwake ona Daudi hakuwahi kuinua upanga wake njuu ya Sauli wala familia yake, Ni sauli ndiye aliyekuwa anataka kumuua Daudi lakini Daudi hakufanya hivyo hata kidogo!

Mithali 26:6 “Kama shomoro katika kutanga-tanga kwake, Na kama mbayuwayu katika kuruka kwake; Kadhalika laana isiyo na sababu haimpigi mtu.”

Shomoro na mbayu wayu ni ndege wadogo sana ndege hawa huwa na tabia aidha ya kufukuza wadudu au wakati mwingine kucheza kwa kukimbia hewani na kugeuka geuka unaweza kudhani kuwa wataanguka au kutua lakini huishia kugeuka ama unaweza kudhani wataenda moja kwa moja kumbe wanarudi, ukweli kama huu ndivyo ilivyo laana isiyo na maana au sababu, laana ni sawa na  uchawi ni hukumu, Ni tamko ni shambulizi linaloweza kutolewa na mtu na inaweza kumpata mtu kama ziko sababu za  haki za kufanyika hivyo, Daudi alikuwa na ujuzi huo wazi kuwa hakuna mtu anaweza kumlaani akalaanika yeye alianza harakati yake ya kwanza kabisa kwa kulaaniwa na Goliath ona

1Samuel 17:42-43 “Hata Mfilisti alipotazama huku na huku, akamwona Daudi akamdharau; kwa kuwa ni kijana tu mwekundu, tena ana sura nzuri. Mfilisti akamwambia Daudi, Je! Mimi ni mbwa hata umenijia kwa fimbo? Mfilisti akamlaani Daudi kwa miungu yake.”

Hata pamoja na Goliath kumlaani Daudi kwa miungu yale laana hiyo haikuweza kufanya kazi na kinyume chake akiwa anapigana vita kwa jina la Bwana ni Goliath ndiye aliyeishia kupigwa vibaya yeye na wafilisti wakifuatia  

1Samuel 17:45-50 “Ndipo Daudi akamwambia yule Mfilisti, Wewe unanijia mimi na upanga, na fumo, na mkuki, bali mimi ninakujia wewe kwa jina la Bwana wa majeshi, Mungu wa majeshi ya Israeli uliowatukana. Siku hii ya leo Bwana atakuua mkononi mwangu, nami nitakupiga, na kukuondolea kichwa chako, nami leo nitawapa ndege wa angani na wanyama wa nchi mizoga ya majeshi ya Wafilisti, ili kwamba dunia nzima wajue ya kuwa yuko Mungu katika Israeli. Nao jamii ya watu wote pia wajue ya kwamba Bwana haokoi kwa upanga wala kwa mkuki; maana vita ni vya Bwana, naye atawatia ninyi mikononi mwetu. Ikawa, hapo Mfilisti alipojiinua, akaenda akamkaribia Daudi, ndipo Daudi naye akapiga mbio, akalikimbilia jeshi ili akutane na yule Mfilisti. Daudi akatia mkono wake mfukoni, akatwaa humo jiwe moja, akalitupa kwa kombeo lake, akampiga Mfilisti katika kipaji cha uso; jiwe hilo likamwingilia kipajini, akaanguka chini kifudifudi. Hivyo Daudi akamshinda yule Mfilisti kwa kombeo na jiwe, akampiga Mfilisti, akamwua; walakini Daudi hakuwa na upanga mkononi mwake.”

Hakuna mtu anaweza kukulaani, ni Mungu pekee mwenye uwezo wa kufanya hayo, hakuna mwanadamua anaweza kukutakia mabaya ni Mungu tu, Adui au mtu awaye yote anapokulaani Mungu ana uwezo wa kuigeuza laana hiyo kuwa Baraka ona

Zaburi 109:27-28. “Nao wakajue ya kuwa ndio mkono wako; Wewe, Bwana, umeyafanya hayo. Wao walaani, bali Wewe utabariki, Wameondoka wao wakaaibishwa, Bali mtumishi wako atafurahi.”

Kumbukumbu 28:20 “Bwana atakuletea laana na mashaka, na kukemewa, katika yote utakayotia mkono wako kuyafanya, hata uangamie na kupotea kwa upesi; kwa ule uovu wa matendo yako, uliyoniacha kwayo.”    

Unaona kwa msingi huo hakuna manadamu ana mamlaka ya kulaani kile ambacho Mungu amekibariki, Daudi alikuwa na uhakika kuwa laana ya Shimei na matukano yake yote kinyume na Mfalme Havingeweza kuathiri lolote katika maisha ya Daudi, hata hivyo kisheria Shimei alipaswa kuuawa lakini Daudi alichagua rehema na alichagua kuachia kesi kwa Mungu, msomaji wangu mpendwa usiogope hakuna mtu anaweza kubadili mwenendo wa maisha yako kwa maneno yake yasiyo na maana, wako watu duniani ambao ni wepesi sana kulaani, ukimuudhi kidogo tu anamwaga laana nyingi na wengi wetu tunadhani kuwa laana hizo zimefanya kazi katika maisha yetu n ahata watu wengine wanadani kwa kukubali kuwa ulilaaniwa, nataka nikueleze ukweli wa kibiblia Hakuna laana inaweza kuwa na nguvu juu yako isipokuwa kama tutamuasi Mungu, au kuhusika katika dhuluma au kama kuna mashiko katika hilo

1Petro 3:13-17 “Naye ni nani atakayewadhuru, mkiwa wenye juhudi katika mema? Lakini mjapoteswa kwa sababu ya haki mna heri. Msiogope kutisha kwao, wala msifadhaike; bali mtakaseni Kristo Bwana mioyoni mwenu. Mwe tayari siku zote kumjibu kila mtu awaulizaye habari za tumaini lililo ndani yenu; lakini kwa upole na kwa hofu. Nanyi mwe na dhamiri njema, ili katika neno lile mnalosingiziwa, watahayarishwe wale wautukanao mwenendo wenu mwema katika Kristo. Maana ni afadhali kuteswa kwa kutenda mema, ikiwa ndiyo mapenzi ya Mungu, kuliko kwa kutenda mabaya.”  

Kufuata njia ya Mungu.

Ni muhimu kufahamu kuwa tuwapo hapa duniani wako watu wanaweza kuinuka kama shimei katika maisha yetu na kujiweka katika nafasi ya uadui katika maisha yetu, Hatukuja duniani kutengeneza maadui lakini wako watu kutokana na matukio kadha wa kadha duniani wanaweza kujiweka katika nafasi ya adui wao wenyewe linapokuja swala la namna hii ni muhimu kama ilivyokuwa kwa Daudi kuchagua njia ya Mungu, Shimei alikuwa amemlaani Daudi na kumlaumu kama mtu wa damu, lakini ni ukweli ulio wazi kuwa Sauli aljaribu kumuua Daudi karibu mara saba na Daudi alijaribu kuokoa maisha yake mara kadhaa, akiacha kila kitu kiwe katika mikono ya Mungu yeye aliamini kuwa Mungu ana njia iliyo bora zaidi ya kushughulika na wote wanaojiweka katika njia ya maisha yake kama adui zake na ndio Maana Yesu mwana wa Daudi alifundisha kuwa inatupasa kuwaombea maadui zetu na kuwapenda  Mwalimu alikuwa na maana gani hapa, kwa vyovyote vile alikuwa na maana ya kuwaacha katika mikono ya Mungu, kumuachia Mungu hakimu mwenye haki na mwenye hekima yake kuamua namna njema na nzuri itakayofaa Kwa adui zetu!

Mathayo 5:43-44 “Mmesikia kwamba imenenwa, Umpende jirani yako, na, Umchukie adui yako; lakini mimi nawaambia, Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi,”

Yesu mwenyewe alituachia kielelezo, hata waliokuwa wakimsulubisha aliwaombea rehema kwa Mungu kwa sababu ni Mungu pekee ndiye anayeweza kulaani, na sio kila mtu anaweza kulaanika kwa sababu wako ambao Mungu alikusudia kuwabariki tu uweza huo uko katika mikono ya Mungu hakuna mtu anaweza kukulaani bila Mungu kutoa kibali au wewe mwenyewe kuvunja maagizo kadhaa ya kiungu yanayoweza kuruhusu kanuni ya kuvuna na kupanda ikafanya kazi katika maisha yako, lakini ukweli unabaki wazi kuwa Mungu hana kigeugeu akimbariki mtu amembariki

Hesabu 23:8 “Nimlaanije, yeye ambaye Mungu hakumlaani? Nimshutumuje, yeye ambaye Bwana hakumshutumu?”

Hesabu 23:12 “Naye akajibu, akasema, Je! Hainipasi kuangalia, niseme neno lile Bwana atialo kinywani mwangu?

Daudi alikuwa na ufahamu huu wote kuhusu Neno la Mungu alielewa wazi kuwa hakuna mtu anaweza kumlaani na kuwa kama mtu atafanya hayo anaweza kufanya hayo kwa kibali kutoka kwa Mungu, na ndio maana akawa na ujasiri wa kusema mwacheni alaani Bwana ndiye aliyemuagiza, alijua wazi kuwa kama ni Bwana sawa lakini kama si Bwana hakuna mtu anayeweza kuudhuru kwa sababu zozote zile

Kunaweza kuwako nyakati katika maisha yetu ambapo watu wanaweza kupandisha kichaa na kuanza kutulaani  laana hizo zote zitakuwa ni maneno ya mkosaji tu yatakuwa ni maneno ya kusema mabaya yanaweza kutoka kwa ndugu, jamaa majirani, kazini na hata kanisani, watu wanaweza kukushambulia hadharani au sirini na vyovyote vile lakini tuna njia ambayo tunaweza kuichagua tusiwe kama watu wa ulimwengu huu, ambao wanaweza kujibu tukio kama hilo kwa mtindo wanaotaka wao, au tunaweza kuchagua njia ya Mungu kwa kuiga mfano wa Daudi na Yesu mwana wa Daudi,  na kupuuzia maneno ya kipuuzi na kuonyesha upendo kwa kumuachia Mungu tukijua wazi kuwa hawana madhara yoyote katika maisha yetu!

Kanuni ya Mungu Mtu kuhusu laana na Baraka.

Daudi alikuwa ni mfalme wakati anatukanwa mtu aliyemtukana alikuwa anastahili kufa, Daudi alionyesha kushughulika na kuhitaji Rehema zaidi kwa Mungu kuliko kuruhusu hukumu kwa mtu aliyemtukana, alionyesha uvumilivu, alionyesha unyenyekevu, alitarajia Mungu mwenyewe anaweza kuigeuza laana yake kuwa Baraka kutakiwa mabaya kuwa neema na rehema za Mungu, Mungu atatulipia sio tu huduma tunazofanya bali hata mateso tunayoyapitia  hivyo hatuna budi kumuamini Mungu kuwa atatulipia  2Wathesalonike 1:6 “Kwa kuwa ni haki mbele za Mungu kuwalipa mateso wale wawatesao ninyi Daudi alitambua kuwa ziko kanuni za kiungu mtu anapolaani alijihisi kuwajibika yeye kwa makosa yake  na kukubali mapenzi ya Mungu kuliko kushughulika na wengine, Yeye kama Mwanadamu alikosea sana na Mungu alikuwa amesema upanga hautaondoka nyumbani mwako sasa ulikuwa ni wakati ambapo mtoto wake mwenyewe ameinuka kinyume naye, na kama mtu baki tu anamtukana si shani sana ukilinganisha kuwa hata mwana wake wa kumzaa amefanya mapinduzi:-

-          Kuna wakati ambapo ni vema tukashughulika sana na changamoto zetu, kuliko kutaka kuna wengine wakiadhibiwa, wakati sisi tunapoangukia katika mikono ya Mungu na kunyooshwa, sio vema sana katika wakatio huo huo kutaka Mungu awanyooshe wengine, hatuna budi kutafuta kibali cha kiungu kwaajili ya maisha yetu na kumuhitaji Mungu awe msaada wetu zaidi, atupe rehema, aondoe kiburi, atunyenyekeshe, aondoe ile hali ya kujiona bora kuliko wengine, atupe utambuzi ya kuwa sisi sio wa thamani sana kuliko wengine, Hata hivyo uelewa katika neno la Mungu ulimsaidia sana Daudi kutambua kuwa maneno ya Shimei hayana nguvu kwake Hawezi mtu wa Mungu kulaaniwa na mtu awaye yote bila kibali cha Mungu

 

Hesabu 22:10-12 “Balaamu akamwambia Mungu, Balaki mwana wa Sipori, mfalme wa Moabu, amewatuma kwangu, akisema, Tazama, kuna watu waliotoka Misri, wanaufunika uso wa nchi; basi njoo unilaanie watu hawa; labda nitaweza kupigana nao, na kuwafukuza. Mungu akamwambia Balaamu, Usiende pamoja nao; wala usiwalaani watu hawa, maana wamebarikiwa.”

 

-          Mungu mwenyewe atambariki kila mtu anayetubarikia na atamlaani kila anayetulaani kwa sababu tumekusudiwa kuwa Bwaraka kwa mataifa yote Mwanzo 12:3 “nami nitawabariki wakubarikio, naye akulaaniye nitamlaani; na katika wewe jamaa zote za dunia watabarikiwa.”

 

-          Watu wote wanaopenda kulaani kwa mujibu wa maandiko wanajiweka katika hatari ya kupatwa wao na laana hizo na ndio maana maandiko yanatutaka tupendezwe na kubariki Zaburi 109:17-20 “Naye alipenda kulaani, nako kukampata. Hakupendezwa na kubariki, kukawa mbali naye, Alijivika laana kana kwamba ni vazi lake. Ikamwingilia moyoni kama maji, Na kama mafuta mifupani mwake. Na iwe kwake kama vazi ajivikalo, Na kama mshipi ajifungao daima. Ndiyo malipo ya washitaki wangu toka kwa Bwana, Na ya hao wanaoisingizia nafsi yangu mabaya.”

 

-          Hakuna silaha inayoweza kufanikiwa juu yakow ewe na mimi na hakuna ulimi au laana inayoweza kuinuka juu yetu kwani laana hiyo itahukumiwa Isaya 54:17 “Kila silaha itakayofanyika juu yako haitafanikiwa na kila ulimi utakaoinuka juu yako katika hukumu utauhukumu kuwa mkosa. Huu ndio urithi wa watumishi wa Bwana, na haki yao inayotoka kwangu mimi, asema Bwana.”

 

-          Laana isiyo na mashiko yaani sababu haimpigi mtu “Mithali 26:6 “Kama shomoro katika kutanga-tanga kwake, Na kama mbayuwayu katika kuruka kwake; Kadhalika laana isiyo na sababu haimpigi mtu.”

 

-          Mungu anauwezo wa kutangua laana hata iliyotoka kwa mzazi, Mwanzo 49: 3-4 “Reubeni, u mzaliwa wangu wa kwanza, Nguvu zangu, na malimbuko ya uwezo wangu. Umewapita wengine kwa ukuu na kwa nguvu. Umeruka mpaka kama maji, basi usiwe na ukuu, Kwa sababu ulikipanda kitanda cha baba yako, Ukakitia unajisi; alikipandia kitanda changu.” Maandiko yanaonyesha wazi kuwa Yakobo hakumbariki Reubeni kwa sababu alivuka mpaka alikipanda kitanda cha baba yake ni wazi kuwa kulikuwa na laana iliyojificha na hivyo ukoo huu ungefutika kabisa katika Israel na kuwa dhaifu sana lakini katika jicho la Rohoni baba wa kiroho Musa alitamka Baraka kuwa reubeni asife lakini angalau awe na watu wachache ona  Kumbukumbu 33:6 “Reubeni na aishi, asife; Lakini watu wake na wawe wachache.” Baba wa kimwili alimlaani Reuben na huenda alimfuta katika Hesabu zake lakini baba wa kiroho alibadilisha kauli na kutamka Baraka kuwa Reuben na aishi          

 

-          Usilitumie jina la Mungu kwa kulaani Kutoka 20:7 “Usilitaje bure jina la BWANA, Mungu wako, maana BWANA hatamhesabia kuwa hana hatia mtu alitajaye jina lake bure.” Neno usilitaje bure jina la Bwana Mungu wako katika lugha nyingine linamaanisha pia usilitumie jina lake kulaani No Using the name of God, your God, in curses or silly banter

 

-          Endapo tuliwahi kulaani watu ni vema ukatubu na kufuta laana hizo, kwa sababu kama watu hao walihesabiwa haki na Mungu kuliko wewe yanaweza kukurudia

 

 Yakobo 3:10-11 “Katika kinywa kile kile hutoka baraka na laana. Ndugu zangu, haifai mambo hayo kuwa hivyo. Je! Chemchemi katika jicho moja hutoa maji matamu na maji machungu?

 

Kristo anawatarajia wakristo kuwa watu wenye moyo kama wa Daudi, japo tunafahamu katika mazingira Fulani tunaweza kuzitumia zaburi kama zile zaburi za kulaani, lakini hata hivyo haipaswi kuwa jambo jepesi sana kukimbilia kulaani, na badala yake tunaweza kuonyesha wema wa Mungu kwa wale wanaotupinga ili yamkini ikiwezekana Mungu aweze kulete rehema kwetu pale tunapokuwa na rehema kwa wengine Mathayo 5:7 “Heri wenye rehema; Maana hao watapata rehema.”

 

-          Kataa kurudisha laana kwa anayekulaani – Warumi 12:14 “Wabarikini wanaowaudhi; barikini, wala msilaani.” Na 17-21 “Msimlipe mtu ovu kwa ovu. Angalieni yaliyo mema machoni pa watu wote. Kama yamkini, kwa upande wenu, mkae katika amani na watu wote. Wapenzi, msijilipize kisasi, bali ipisheni ghadhabu ya Mungu; maana imeandikwa, Kisasi ni juu yangu mimi; mimi nitalipa, anena Bwana. Lakini, Adui yako akiwa na njaa, mlishe; akiwa na kiu, mnyweshe; maana ufanyapo hivyo, utampalia makaa ya moto kichwani pake. Usishindwe na ubaya, bali uushinde ubaya kwa wema.”

 

-          Jifunze kubariki – Kubariki ni tabia ya uungu, Mungu alipokuwa anauumba ulimwengu mara kwa mara alikibariki kila alichokiumba, kubariki ni unabii, unatamka maneno mazuri ili yaweze kuwapata na wengine  unatamka kwa Imani, unahakikisha kuwa kile unachokiamuru kama Baraka kinakuwa kwa wengine nawe utabaki kama nabii wa Bwana kwa sababu unachokitamka kizuri kitawapata wengine,

 

Waebrania 11:20-21 “Kwa imani Isaka akawabariki Yakobo na Esau, hata katika habari ya mambo yatakayokuwa baadaye.Kwa imani Yakobo, alipokuwa katika kufa, akambariki kila mmoja wa wana wa Yusufu, akaabudu akiegemea kichwa cha fimbo yake.”     

 

Ukiyajua hayo Heri wewe ukiyatenda!

Na. Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni