Jumapili, 4 Februari 2024

Kuponywa kwa mtu mwenye kibiongo!


Luka 13:10-13 “Siku ya sabato alikuwa akifundisha katika sinagogi mojawapo. Na tazama, palikuwa na mwanamke aliyekuwa na pepo wa udhaifu muda wa miaka kumi na minane, naye amepindana, hawezi kujinyosha kabisa.Yesu alipomwona alimwita, akamwambia, Mama, umefunguliwa katika udhaifu wako.  Akaweka mikono yake juu yake, naye akanyoka mara hiyo, akamtukuza Mungu.”




Utangulizi:

Katika moja ya miujiza kadhaa mikubwa aliyoifanya Bwana Yesu, Moja ya muujiza wa muhimu sana ni pamoja na huu wa kuponywa kwa mtu mwenye kibiongo.(Ugonjwa wa kupindana kwa mgongo) Luka 13:10-13 “Siku ya sabato alikuwa akifundisha katika sinagogi mojawapo. Na tazama, palikuwa na mwanamke aliyekuwa na pepo wa udhaifu muda wa miaka kumi na minane, naye amepindana, hawezi kujinyosha kabisa. Yesu alipomwona alimwita, akamwambia, Mama, umefunguliwa katika udhaifu wako.  Akaweka mikono yake juu yake, naye akanyoka mara hiyo, akamtukuza Mungu.”

Ugonjwa huu wa kibiongo au ugonjwa wa kupindana mgongo ni moja ya ugonjwa mbaya sana sana katika historia ya  magonjwa duniani, na kwa bahati nzuri Yesu Kristo alikuwa haponyi ilimradi tu, utaweza kuona miujiza mingi aliyoifanya Kristo aliifanya kimkakati, aidha kwa watu walioteseka sana na kupoteza matumaini ili awasaidie, au kwa kusudi Mungu atukuzwe na watu wapate kumuamini, na pia kwaajili ya kutufundisha!, Muujiza huu wa kuponywa kwa mtu mwenye kibiongo, una maswala kadhaa ya kutufundisha yanayoonyesha namna Mungu anavyoshughulika na watu wake hasa ambao wanapitia hali ngumu sana, leo tutachukua Muda kuuangalia muujiza huu, kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-  


·         Ufahamu kuhusu ugonjwa wa kupindana mgongo (Kibiongo)

·         Kuponywa kwa mtu mwenye kibiongo

·         Mambo ya kujifunza kupitia muujiza huu


Ufahamu kuhusu ugonjwa wa kupindana mgongo (Kibiongo)

Ugonjwa wa kupinda mgongo (kibiongo) ni mojawapo ya magonjwa mabaya sana duniani, ugonjwa huu kitaalamu unaitwa CAMPTOCORMIA ambapo kwa kawaida wanaopatwa na ugonjwa huu huwa na muonekano wa kupinda usiokuwa wa kawaida anaposimama, na unaweza kuonekana zaidi anapotembea, ni ugonjwa unaotokana na muundo mmbaya unaojitokeza kutokana na kupinda kwa mbele au kwa nyuma kwa uti wa mgongo,  Neno hilo CAMPTOCORMIA  limetokana na neno la Kiyunani KAMPTOS  ambalo maana yake ni BENT FORWARD au BENT BACKWARD  kwa kawaida jina la kawaida kwa kiingereza ni “Bent spine syndrome” kupinda kwa mgongo. Ni ugonjwa mbaya na unapoteza kabisa “shape”  muonekano wa mtu, Ugonjwa huu sio tu kuwa haujulikani sababu zake lakini pia hauna matibabu maalumu zaidi ya kuwaona wataalamu wa mifupa (Physiotherapy) ambao watakuwa wakimpatia mgonjwa matibabu ya kimazoezi tu, ugonjwa huu sio tu unaweza kujitokeza kwa mtu kufutukia kifuani na kudidimia sehemu ya nyuma ya mgongo, au kuwa na umbile kama la upinde mgongoni unaofikia nyuzi 45  na kumfanya mtu huyo kuinama hata asiweze kuiona mbingu au kumchungulia mtu usoni, kwa ujumla ukiacha kuwa mtu mwenye ugonjwa huu hapandezi unapomuona, lakini vilevile unaweza kuhisi maumivu anayoyapata mtu aliyepindana wakati mwingine uti wa mgongo wa mtu mwenye ugonjwa huu unaweza kujichora kama umbo la S na  na wakati mwingine unaweza kusababisha bega moja la mtu huyo likawa juu na lingine chini, au mbavu zake zikaonekana zimeinama upande mmoja, Nguo za kawaida hazimkai vizuri mtu wa jinsi hiyo kwa ujumla ni ugonjwa wa kusikitisha, madaktari wanasema ugonjwa huu unaweza kujitokeza kwa mtu anapoanza kubalehe hasa wanawake na kwa sababu hiyo wanaoshambuliwa sana ni wanawake kwa wingi na wanaume wa uchache, kwa kuwa mpaka sasa hakuna anayejua sababu za ugonjwa huu, Lakini Luka kwa vile alikuwa ni tabibu anaelezea kuwa ugonjwa huu unatokana na UDHAIFU lakini Luka anaelezea wazi kuwa ni udhaifu uliosababishwa na shetani  na tunaelezwa kuwa alikuwa katika hali hiyo kwa miaka 18, Ugonjwa huu unaambatana kwa mbali na hali ya udumavu kwa ujumla wake ni ugonjwa mmbaya sana ona:-  

Luka 13:10-13 “Siku ya sabato alikuwa akifundisha katika sinagogi mojawapo. Na tazama, palikuwa na mwanamke aliyekuwa na pepo wa udhaifu muda wa miaka kumi na minane, naye amepindana, hawezi kujinyosha kabisa. Yesu alipomwona alimwita, akamwambia, Mama, umefunguliwa katika udhaifu wako.  Akaweka mikono yake juu yake, naye akanyoka mara hiyo, akamtukuza Mungu.”

Luka ni tabibu, ni Daktari wa binadamu aliyeokoka hivyo anaelewa wazi kuwa kuna udhaifu wa kawaida na udhaifu unaosababishwa na Shetani, au mapepo, na Luka aliweza kujua udhaifu ule kitabibu hauwezi kuponyeka wala kuutibika lakini kujua kuwa ni Pepo inawezekana ni kutokana na Tabibu mkuu Yesu Mwenyewe kuwafunulia watu kuwa mateso ya mama yule yalitokana na kifungo cha shetani  kumbuika maneno yale “Na huyu mwanamke, aliye wa uzao wa Ibrahimu, ambaye Shetani amemfunga miaka kumi na minane” ona

Luka 13:11-17 “Na tazama, palikuwa na mwanamke aliyekuwa na pepo wa udhaifu muda wa miaka kumi na minane, naye amepindana, hawezi kujinyosha kabisa. Yesu alipomwona alimwita, akamwambia, Mama, umefunguliwa katika udhaifu wako. Akaweka mikono yake juu yake, naye akanyoka mara hiyo, akamtukuza Mungu. Basi mkuu wa sinagogi alikasirika kwa sababu Yesu amemponya mtu siku ya sabato, akajibu, akawaambia mkutano, Kuna siku sita zifaazo kufanya kazi, basi njoni mponywe katika siku hizo, wala si katika siku ya sabato. Lakini Bwana akajibu akasema, Enyi wanafiki, kila mmoja wenu, je! Hamfungui ng'ombe wake au punda wake siku ya sabato katika zizi, aende naye kumnywesha? Na huyu mwanamke, aliye wa uzao wa Ibrahimu, ambaye Shetani amemfunga miaka kumi na minane hii, haikupasa afunguliwe kifungo hiki siku ya sabato? Aliposema haya wakatahayari wote walioshindana naye; mkutano wote wakafurahi kwa sababu ya mambo matukufu yaliyotendwa na yeye.”   

Unaona maelezo ya Luka ya awali yametokana na maelezo ya Yesu mwenyewe Kwamba mwanamke yule alikuwa amefungwa na Shetani kwa miaka 18, tena Yesu anamtaja kuwa mwanamke wa Uzao wa Ibrahimu, hii inaonyesha wazi kuwa kulikuwa na uonevu wa Ibilisi, tena bila kujali kuwa huyu binti ni wa uzao wa Ibrahimu, maana yake nini unaweza kuwa Mkristo na bado ukafungwa katika vifungo na uonevu wa ibilisi, unaweza kuwa wa uzao wa Ibrahimu yaani mtu wa Imani, Binti huyu alikuwa na imani, angalia kuwa alikuwa anahudhuria ibada alifika kwenye Sinagogi, siku ya sabato, lakini alikuwa anaonewa, viongozi wake wa dini hawakuweza kumsaidia, Ashukuriwe Mungu kwamba Mgeni rasmi alikuweko kwenye ibada siku ile, Yesu Kristo mtenda miujiza alikuwepo kwenye singagogi, kuhudhuria ibada pekee hakutoshi, kuwa wa uzao wa Ibrahimu pekee hakutoshi, kuwa na imani ya Ibrahimu pekee hakutoshi, tunamuhitaji Yesu Kristo aliye hai, Tunamtaka Bwana na nguvu zake, yako mambo kibinadamu sio ya kawaida hata kama tunayaona ya kawaida, yako mambo ambayo yako juu ya uwezo wetu ni Yesu pekee ndiye anayeweza kujua sababu ya mambo hayo kumbe mengine ni uonevu wa ibilisi unadhani nani angelijua, yako mambo hata madaktari hawajui ni kwanini, Lakini maandiko yanatukumbusha kuwa Yuko Yesu ambaye maalumu sana anaweza kuyachukua madhaifu yetu na kujitwika na kutupa unafuu bila kujali wataalamu wanasemaje.

Mathayo 8:16-16 “Hata kulipokuwa jioni, wakamletea wengi wenye pepo; akawatoa pepo kwa neno lake, akawaponya wote waliokuwa hawawezi, ili litimie lile neno lililonenwa na nabii Isaya, akisema, Mwenyewe aliutwaa udhaifu wetu, Na kuyachukua magonjwa yetu.” 
            

Haijalishi una udhaifu wa namna gani na umeteseka kwa miaka mingapi, lakini maandiko yanaonyesha kuwa ni kazi yake Yesu kuponya madhaifu na magonjwa yetu, kwa hiyo kila mwanadamu bila kujali historia yake, kabila lake, ana uzuri kiasi gani ana ubaya kiasi gani maandiko yanatukumbusha leo kumwangalia Yesu kwa mambo ambayo madaktari na matabibu wa kawaida wameshindwa, Yeye atakuweka huru na kukufungua kutoka katika udhaifu wako

Kuponywa kwa mtu mwenye kibiongo:

Nadhani baada ya kuelezea ugonjwa aliokuwa nao mwanamke huyu wewe mwenyewe unaweza kupata hisia za mateso yake, kwamba alikuwa anateseka kiasi gani, na chukulia kama mwanamke wa aina hii ni binti yako! Au dada yako au mama yako! Au mkeo? Ungejisikiaje? Mateso haya sio tu yalikuwa ya mwilini lakini vilevile na kisaikolojia huenda alichekwa na watu, na sio hivyo tu hata familia yake huenda ilichekwa, au watu walimkwepa, au sio rahisi kuchumbiwa na kuolewa kulikuwa na ndoto nyingi ambazo zilikufa kutokana na maisha ya mateso aliyokuwa nayo mwanamke huyu, Ashukuriwe Mungu Yesu ni mwenye huruma sana, Mwanamke huyu aliyekuwa amepindana na hawezi kuinuka Biblia inasema Yesu alipomuona alimuita mbele, na akamwambia mama umefunguliwa katika udhaifu wako, na kama haitoshi Yesu akamwekea mikono yake na mara moja mwanamke yule aliponywa na akanyooka mara moja nakuanza kumtukuza Mungu, kulikuwa na namna nyingi tu ambazo Yesu angeweza kufanya angelituma neno, angekemea pepo, lakini Yesu akiwa amejawa na huruma, alimuita kitendo cha kuitwa mbele kilimfanya mwanamke yule ajue wazi kuwa ile ilikuwa ni siku yake,  na kuwa Yesu alionyesha kuwa anamjali, labda alisikia habari za Yesu na matendo yake makuu, aliwaza ni lini na mimi nitakuja kukutana na mtu huyo na aniponye? hakua na matumaini, lakini Hakuna jambo zuri duniani kama kuitwa na mtu mkubwa wa kiwango cha Kristo na sio hivyo tu Yesu alitamka neno na mwisho akaweka mikono yake juu yake, Mwanamke huyu aliponywa kwa heshima kubwa sana sio lazima wakati wote muhubiri akuwekee mikono, lakini Yesu alitaka kumuonyesha upendo wake mtu huyu alitaka kuponya na nafsi yake iliyoumizwa, alitaka kuinyesha kuwa yuko mmoja anayemjali, unaposoma juu juu utaweza kudhani kuwa Labda Yesu alifanya muujiza huu kuonyesha nguvu yake juu ya sabato, au juu ya viongozi wa dini, au kuonyesha nguvu yake juu ya shetani lakini stori hii ni kwajili ya upendo, kwaajili ya mateso, kwaajili ya kumuhurumia mtu mwenye fadhaa kubwa na nzito isiyo na tabibu kumtoa katika kifungo cha ibilisi angalia maneno yale UMEFUNGULIWA KATIKA UDHAIFU WAKO!, You are set Free from your infirmity !  Kusudi letu kubwa au langu kubwa kubwa ni kuonyesha kuwa ibada za maombezi haziko kwaajili ya kuonyesha nguvu za Mungu au nguvu za Muhubiri, au kuonyesha kuwa ninasikiwa na Yesu kwa kiwango gani, ua ninatymiwa na Mungu, au kujitafutia umaarufu, nataka watu wawe huru kwa sababu sifurahii kuona mateso, Huu ndio ulikuwa moyo wa Yesu Kristo, Roho Mtakatifu alikuwa amempaka mafuta na kumtumia kwa kusudia la kuwafungua watu wanaoonewa!

Luka 4:18-19 “Roho wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa, Na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa.”

Matendo 10:38 “habari za Yesu wa Nazareti, jinsi Mungu alivyomtia mafuta kwa Roho Mtakatifu na nguvu naye akazunguka huko na huko, akitenda kazi njema na kuponya wote walioonewa na Ibilisi; kwa maana Mungu alikuwa pamoja naye.”

Nia kubwa ya Yesu Kristo ni kuwasaidia watu, hakufurahi Mwalimu kuona watu wanaoonewa na Ibilisi, watu wa Mungu tumtafute Mungu, tutafute nguvu zake ili watu wanaoonewa kila mahali na hata makanisani mwetu na katika masinagogi, wapate kutoka katika uonevu wa ibilisi, haiwezekani watu wa Mungu wawe wanadhalilika na sisi tupo na Mungu ametuweka kwaajili ya kuwasaidia. Kristo Yesu alisikitishwa sana na viongozi wa dini na sinagogi ambao hata ibada ya uponyaji wa mwanamke huyu kwao ilikuwa kama kwazo ona

Luka 13:14-17 “Basi mkuu wa sinagogi alikasirika kwa sababu Yesu amemponya mtu siku ya sabato, akajibu, akawaambia mkutano, Kuna siku sita zifaazo kufanya kazi, basi njoni mponywe katika siku hizo, wala si katika siku ya sabato. Lakini Bwana akajibu akasema, Enyi wanafiki, kila mmoja wenu, je! Hamfungui ng'ombe wake au punda wake siku ya sabato katika zizi, aende naye kumnywesha? Na huyu mwanamke, aliye wa uzao wa Ibrahimu, ambaye Shetani amemfunga miaka kumi na minane hii, haikupasa afunguliwe kifungo hiki siku ya sabato? Aliposema haya wakatahayari wote walioshindana naye; mkutano wote wakafurahi kwa sababu ya mambo matukufu yaliyotendwa na yeye.”

Unaweza kuona nia ya Yesu hapa wala haikuwa shindano la sabato, Yesu alitaka kuonyesha uchungu aliokuwa nao kwa mwanamke aliyekuwa amefungwa, siku sita za kufanya kazi sio siku za ibada ni siku za watu kujitafutia mahitaji yao, na sabato ndio siku ya ibada watu wanajihudhurisha nyumbani kwa Bwana, nadhani  Yesu anatuonyesha siku ya bwana inavyopaswa kutumika, siku ya ibada yako, Leo hii unaweza kwenda kanisani na sio kibiongo, lakini ukawa tu umevunjika moyo na unakutana na watumishi wa Mungu waliojaa hasira, wanafokea watu, wanashushua watu, unatoka katika ibada ulikuja na majanga yako na badala ya kugangwa unatoka ukiwa umeumizwa moyo, watumishi wa Mungu ni lazima tuchague maneno ya kusema siku za ibada, kama unaona moyo wako hauko vizuri basi afadhali uache kuhudumu, wazee mnaotangaza matangazo, hakikisha kuwa mnazungumza kwa busara msiwaharibie watu ibada, Mwanamke huyu ilikuwa ni siku yake ya furaha na hata watu wa kawaida walifurahi na kumtukuza Mungu anakuja mtu kufunga ibada anabwatuka NABANA PUA HAPA “Kuna siku sita zifaazo kufanya kazi, basi njoni mponywe katika siku hizo, wala si katika siku ya sabato.” MWISHO WA KUBANA PUA. Ashukuriwe Yesu ni kiongozi mzuri wa ibada alihakikisha watu wanatoka ibadani wakimtukuza Mungu! Siku ya ibada ni lazima itumike kwa busara kunganga mioyo ya watu na sio kuwakwaza, kuwainua walioinama na sio kuwainamisha, Yesu alikuwa akionyesha matumizi sahihi ya siku ya Bwana, haipaswi kuwa siku ya kukandamiza watu na tafasiri mbaya za sharia bali ni siku ya kuweka watu huru kutoka katika majanga ya maisha yanayowasibu sikuhadi siku!

Mambo ya kujifunza kupitia muujiza huu

1.       Tunajifunza kwamba Yesu Kristo aliongozwa na upendo katika kila jambo alilolifanya, Yesu hakuwahi kufurahi hata siku moja lolote lile lisimame kinyume na msukumo wake wa upendo, ni kupitia upendo Karama na utumishi wetu kwa Mungu na kwa watu unapaswa kujengwa katika msingi huo. 1Wakorintho 13:1-8 “Nijaposema kwa lugha za wanadamu na za malaika, kama sina upendo, nimekuwa shaba iliayo na upatu uvumao. Tena nijapokuwa na unabii, na kujua siri zote na maarifa yote, nijapokuwa na imani timilifu kiasi cha kuweza kuhamisha milima, kama sina upendo, si kitu mimi.Tena nikitoa mali zangu zote kuwalisha maskini, tena nikijitoa mwili wangu niungue moto, kama sina upendo, hainifaidii kitu. Upendo huvumilia, hufadhili; upendo hauhusudu; upendo hautakabari; haujivuni;haukosi kuwa na adabu; hautafuti mambo yake; hauoni uchungu; hauhesabu mabaya; haufurahii udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli; huvumilia yote; huamini yote; hutumaini yote; hustahimili yote. Upendo haupungui neno wakati wo wote; bali ukiwapo unabii utabatilika; zikiwapo lugha, zitakoma; yakiwapo maarifa, yatabatilika.” 

 

2.       Ugonjwa huu ulikuwa ni mbaya sana na uliambatana na ubaguzi wa hali ya juu watu wa jinsi hii kama walikuwa wanaume tena wa kabila la lawi hawakuruhusiwa kuwa makuhani kwani Torati iliwatenga na ilionekana ni kama watu waliokataliwa na Mungu ona Walawi 21:17-20 “Nena na Haruni, umwambie, Mtu awaye yote wa kizazi chako wewe katika vizazi vyao, aliye na kilema, asikaribie kusongeza chakula cha Mungu wake. Kwa kuwa mtu awaye yote aliye na kilema hatakaribia; mtu kipofu, au kiwete, au mtu aliye na pua iliyoharibika, au aliye na kitu kilichozidi vimpasavyo mwili, au mtu aliyevunjika mguu, au aliyevunjika mkono, au aliye na kijongo, au aliye kibeti, au aliye na kilema cha jichoni, au aliye na upele, au mwenye buba, au aliyevunjika mapumbu;” Yesu alithibitisha kuwa yuko kwaajili ya watu wa namna hii, alikuwa anafunua wazi kuwa hali ile kamwe sio kazi za Mungu bali ni uonevu wa shetani na kuwa Mungu yuko kinyume na aina zote za uonevu, Kristo alichukizwa na aina hii ya uonevu na akamfungua

 

3.       Kiongozi wa Sinagogi mwenye roho mbaya – kutokana na Yesu kutenda mema yeye alikasirika ndivyo maandiko yanavyotuambia, mtazamo wake kuhusu uponyaji na utendaji wa miujiza anaona kama ni kazi inayotakiwa kufanyika siku za kawaida na sio siku ya sabato, haishangazi kuwa na watu wenye ufahamu finyu kuhusu namna na jinsi Mungu anavyofanya kazi, ni hao hao ambao walikuwa wakifungulia punda kunywa maji au kuokoa mnyama asidumbukie shimoni siku ya sabato, lakini wanaona mtu kuponywa siku ya sabato ni ishu, Yesu alikemea tabia hii mbaya, watumishi wa Mungu wanapaswa kuwa na roho nzuri, huruma na upendo na ufahamu mkubwa kuliko hata wanaowaongoza, wakati watu wanafurahia matendo makuu ya Mungu inashangaza kuona mkuu wa sinagogi anakasirika, washirika wa siku hizi wana ufahamu mkubwa sana wa neno la Mungu hivyo viongozi hawana budi kujiongeza, na kuwa makini kwa wanachokiongea na hija wanayoijenga kuhusu utendaji wa Mungu na matendo yake ya huruma kwa watu

 

4.       Shetani anahusika kuwafunga watu ni kazi ya watumishi wa Mungu kuutafuta uso wa Bwana na karama za rohoni kwa kusudi la kuwasaidia watu kwa upendo, aidha katika upendo wake Yesu anaonyesha kuwa anaweza kuponya changamoto yoyote hata kama ni ya Muda mrefu, kumbuka mwanamke yule alionewa na ibilisi kwa miaka 18 lakini alipokutana na Yesu ukawa mwisho wa changamoto zake! Changamoto zako zitafikia mwisho hata bila kujali imechukua muda mrefu kwa kiasi gani!

 

5.       Wako watu ambao katika hali ya kawaida wamenyooka lakini roho zao zimepindana wana kibiongo nao wanahitaji kuhudumiwa roho zao, Kristo Yesu yupo tayari kuwahudumia watu wake leo, yeye hajabadilika yeye ni yeye yule jana leo na hata milele, kama moyo wako na roho yako imeinama huwezi hata kuangalia mbinguni leo kwa mamlaka niliyopewa kama mtumishi wa Mungu nakutangazia uzima katika jina la Yesu Kristo wa Nazareth aliye hai Bwana akutane na wewe katika kila eneo la maisha yako, bwana akuinue kutoka katika kupindana kwako.Bwana akuinue kutoka katika hali ya kuinama kwako kwa namna yoyote ile Katika jina la Yesu!

 

6.       Hakuna ugonjwa usiotibika kwa Yesu!, kama jinsi ambavyo tumejifunza kuhusu ugonjwa wa kibiongo au kupindana kwa mgongo ni ugonjwa mbaya haujulikani Dhahiri sababu zake na pia hauna tiba, Lakini kufumba na kufumbua Yesu alipomuombea mwanamke huyu Mwenye kibiongo alisimama pale pale, hii inatufundisha na kutufunulia kuwa hakuna uogonjwa wwowote ambao unaweza kusimama mbele za Yesu, uwe unaeleweka kitaalamu, au uwe haueleweki, uwe una tiba au hauna tiba, linapokuja swala la Yesu kujihusisha na tatizo lako hakuna linaloshindikana, Yote yawezekana kwa Mungu, Katika jina la Yesu Kristo tatizo lako leo kwa mamlaka niliyopewa kama Mtumishi wake nakutangaza kuwa umefunguliwa kutoka katika udhaifu wako kwa jina la Yesu Kristo mwana wa Mungu aliye hai Ameeeen!

 

Na Rev. Innocent Samuel Bin Hamza Bina Jumaa, Bin bin Athuman Sekivunga Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni