Jumapili, 11 Februari 2024

Yule mjanja alisema siku ya tatu nitafufuka


Mathayo 27:62-66 “Hata siku ya pili, ndiyo iliyo baada ya Maandalio, wakuu wa makuhani, na Mafarisayo wakamkusanyikia Pilato, wakasema, Bwana, tumekumbuka kwamba yule mjanja alisema, alipokuwa akali hai, Baada ya siku tatu nitafufuka. Basi amuru kwamba kaburi lilindwe salama hata siku ya tatu; wasije wanafunzi wake wakamwiba, na kuwaambia watu, Amefufuka katika wafu; na udanganyifu wa mwisho utapita ule wa kwanza. Pilato akawaambia, Mna askari; nendeni mkalilinde salama kadiri mjuavyo. Wakaenda, wakalilinda kaburi salama, kwa kulitia lile jiwe muhuri, pamoja na wale askari walinzi.”




Utangulizi:

Moja ya tukio muhimu sana katika Imani ya Ukristo ni pamoja na tukio la Kusulubiwa, kufa na kufufuka kwa Yesu Kristo, tukio hili halikuwa tukio la bahati mbaya na ndio maana Yesu Kristo katika Hekima yake alilirudia tena na tena mara kwa mara alipokuwa pamoja na wanafunzi wake na hii ni kwa sababu Mateso yake na kifo chake ndio kilele cha juu zaidi cha huduma yake ya ukombozi kwa wanadamu, Na ndio maana tunaona Yesu akizungumza juu ya tukio hili mara kadhaa na kila wakati akijitaja kama Mwana wa Adamu ona :-

-          Mathayo 16:21-23 “Tangu wakati huo Yesu alianza kuwaonya wanafunzi wake ya kwamba imempasa kwenda Yerusalemu, na kupata mateso mengi kwa wazee na wakuu wa makuhani, na waandishi, na kuuawa, na siku ya tatu kufufuka. Petro akamchukua, akaanza kumkemea, akisema, Hasha, Bwana, hayo hayatakupata. Akageuka, akamwambia Petro, Nenda nyuma yangu, Shetani; u kikwazo kwangu; maana huyawazi yaliyo ya Mungu, bali ya wanadamu.”

 

-          Marko 8:31-32 “Akaanza kuwafundisha kwamba imempasa Mwana wa Adamu kupatikana na mateso mengi, na kukataliwa na wazee, na wakuu wa makuhani, na waandishi, na kuuawa, na baada ya siku tatu kufufuka. Naye alikuwa akinena neno hilo waziwazi. Petro akamchukua, akaanza kumkemea.”

 

-          Luka 9:21-22 “Akawaonya, akawakataza wasimwambie mtu neno hilo; akisema, Imempasa Mwana wa Adamu kupata mateso mengi, na kukataliwa na wazee na wakuu wa makuhani na waandishi, na kuuawa na siku ya tatu kufufuka.”

 

-          Mathayo 17:22-23 “Nao walipokuwa wakikaa Galilaya, Yesu akawaambia, Mwana wa Adamu anakwenda kutiwa katika mikono ya watu, nao watamwua, na siku ya tatu atafufuka. Wakasikitika sana.”

 

-          Marko 9:30-32 “Wakatoka huko, wakapita katikati ya Galilaya; naye hakutaka mtu kujua. Kwa sababu alikuwa akiwafundisha wanafunzi wake, akawaambia, Mwana wa Adamu yuaenda kutiwa katika mikono ya watu, nao watamwua; hata akiisha kuuawa, baada ya siku tatu atafufuka. Lakini hawakulifahamu neno lile, wakaogopa kumwuliza.          “

 

-          Luka 9:43-45 “Wote wakashangaa, wakiuona ukuu wa Mungu. Nao walipokuwa wakiyastaajabia mambo yote aliyoyafanya, aliwaambia wanafunzi wake, Yashikeni maneno haya masikioni mwenu, kwa kuwa Mwana wa Adamu anakwenda kutiwa katika mikono ya watu. Lakini hawakulifahamu neno lile, likafichwa kwao wasilitambue; wakaogopa kumwuliza maana yake neno lile.”

 

Unaona Yesu alikuwa na kusudi maalumu la kurejea tena na tena kuhusiana na tukio hili, na anaeleza hivi mbele ya wanafunzi wake ili kwamba wapate kuamini litakapotukia.

Yohana 14: 28-29 “Mlisikia ya kwamba mimi naliwaambia, Naenda zangu, tena naja kwenu. Kama mngalinipenda, mngalifurahi kwa sababu naenda kwa Baba, kwa maana Baba ni mkuu kuliko mimi. Na sasa nimewaambia kabla halijatokea, kusudi litakapotokea mpate kuamini.”   

Kwanini Yesu alirejea tena na tena tukio hili sio tu wanafunzi wake wapate kumuamini lakini pia ijulikane wazi kuwa alikuwa akiyatoa maisha yake yawe fidia ya wengi na kuleta ukombozi wa Mwanadamu, kwa Msingi huo kuna uwezekano mkubwa sana maadui wa Yesu Kristo walikuwa wamesikia Yesu akizungumza wazi wazi kuhusiana na swala hili na hivyo alipokufa walitaka kuhakikisha kuwa wanalidhibiti kaburi la Yesu ili wanafunzi wake wasije wakamuiba na kudai kuwa amefufuka kama alivyosema na hapo ndipo kukawa na mikakati ya kuhakikisha Kaburi la Yesu linawekwa muhuri na kuwekwa walinzi kuhakikisha kuwa halibatiliki neno. Kwa Msingi huo leo tutachukua Muda kutafakari kwa kina somo hili lenye kichwa YULE MJANJA ALISEMA SIKU YA TATU NITAFUFUKA. Tutajifunza somo hili muhimu kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:- 


·         Maana ya maneno yule mjanja.

·         Jinsi Kaburi la Yesu lilivyopewa Ulinzi mkali.

·         Yule Mjanja alisema siku ya tatu nitafufuka.  



Maana ya maneno Yule mjanja.

Tunasoma katika kifungu cha Msingi maneno haya Mathayo 27:62-66 “Hata siku ya pili, ndiyo iliyo baada ya Maandalio, wakuu wa makuhani, na Mafarisayo wakamkusanyikia Pilato, wakasema, Bwana, TUMEKUMBUKA KWAMBA YULE MJANJA ALISEMA, ALIPOKUWA AKALI HAI, BAADA YA SIKU TATU NITAFUFUKA. Basi amuru kwamba kaburi lilindwe salama hata siku ya tatu; wasije wanafunzi wake wakamwiba, na kuwaambia watu, Amefufuka katika wafu; na udanganyifu wa mwisho utapita ule wa kwanza. Pilato akawaambia, Mna askari; nendeni mkalilinde salama kadiri mjuavyo. Wakaenda, wakalilinda kaburi salama, kwa kulitia lile jiwe muhuri, pamoja na wale askari walinzi.”

Tunaona Neno yule Mjanja likitumika hapa, kabla ya kuzungumza mambo mengine nataka tuchukue muda mfupi kuangalia neno hili walilolitumia dhidi ya Yesu Kristo kwa kumuita mjanja neno Mjanja linalotumika hapo katika kiingereza linatumika neno DECEIVER  Na katika kiyunani linatumika neno PLANOS ambayo kwa ujumla yana tafasiri mbaya na chafu, kwa kiingereza  linatumika neno Misleader, Seducer,  na Neno hili limetumika kama mara 4 katika biblia ya kiingereza, Kwa ujumla ni neno baya sana lililotumiwa kwa Yesu Kinyume kabisa na Sifa Halisi alizokuwa nazo, Neno Deceiver  ufafanuzi wake katika kiingereza ni a Liar, Fraud, Cheat, fake, betrayer, crook, Pretender na deluder  Kwa ujumla wanazungumza Kwamba Yesu alikuwa ni Tapeli au mtu anayepotosha watu, kwa uwongo, kutunga, kudanganya, kupika majungu, kusaliti, kuigiza, Mwongo, Haya yalikuwa ni maneno ya viongozi waliokuwa wamejawa na uchungu sana na kutoa neno kali sana kwa Yesu licha ya kuwa wakati huu walikuwa wamemuua kwa hila lakini bado waliendelea kuzungumza mambo mabaya kumuhusu kwa kusudi la kuchafua utu wake na tabia yake Yesu anatajwa katika maandiko kama:- 

Yohana 14:6 “Yesu akamwambia, Mimi ndimi njia, na KWELI, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi.”

Yohana 1:14 “Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na KWELI.”

Yohana 16:13 “Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa KWELI, atawaongoza awatie kwenye KWELI yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake.”

Ufunuo 3:14 “Na kwa malaika wa kanisa lililoko Laodikia andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye Amina, Shahidi aliye MWAMINIFU NA WA KWELI, mwanzo wa kuumba kwa Mungu.”

Muda usingelitosha kuona jinsi maandiko yanavyomtaja Yesu kuwa ni kweli na Mwaminifu, kwa msingi huo wivu na chuki za maadui wa Yesu Kristo, uliwasukuma kushughulika naye wakimuita mjanja kwa kusudi la kumdhalilisha na kumuhakikishia Pilato kuwa Yesu alikuwa Mzushi tu na hakuwa mkweli  wakati Yesu alizaliwa kwa kusudi la kuishuhudia kweli

Yohana 18:37-38 “Yesu akajibu, Ufalme wangu sio wa ulimwengu huu. Kama ufalme wangu ungekuwa wa ulimwengu huu, watumishi wangu wangenipigania, nisije nikatiwa mikononi mwa Wayahudi. Lakini ufalme wangu sio wa hapa. Basi Pilato akamwambia, Wewe u mfalme basi? Yesu akajibu, Wewe wasema, kwa kuwa mimi ni mfalme. Mimi nimezaliwa kwa ajili ya haya, na KWA AJILI YA HAYA MIMI NALIKUJA ULIMWENGUNI, ILI NIISHUHUDIE KWELI. Kila aliye wa hiyo kweli hunisikia sauti yangu.Pilato akamwambia, Kweli ni nini? Naye akiisha kusema neno hilo akawatokea Wayahudi tena, akawaambia, Mimi sioni hatia yo yote kwake.”

Hata hivyo kutokana na ujinga waliokuwa nao na ufahamu waliokuwa nao Pilato aliwataka walilinde kaburi kwa nguvu zote kwa kadiri wawezavyo na kuliwekea kaburi hilo Muhuri ili huyo wanayedai kuwa ni mjanja yeye au wanafunzi wake wasiweze kufanya jambo lolote kinyume na wanavyofikiri au kinyume na alivyosema !

Jinsi Kaburi la Yesu lilivyopewa Ulinzi mkali

Kutokana na madai ya wazee wa Sanhedrin (Mahakama ya juu ya kiyhahudi) kupeleka madai hayo kwa Pilato tunaona amri ikitolewa kufanyika kwa ulinzi maalumu wa Kaburi la Yesu ili isiwe kama alivyosema. 

Mathayo 27:64-66 “Basi amuru kwamba kaburi lilindwe salama hata siku ya tatu; wasije wanafunzi wake wakamwiba, na kuwaambia watu, Amefufuka katika wafu; na udanganyifu wa mwisho utapita ule wa kwanza.PILATO AKAWAAMBIA, MNA ASKARI; NENDENI MKALILINDE SALAMA KADIRI MJUAVYO. Wakaenda, wakalilinda kaburi salama, kwa kulitia lile jiwe muhuri, pamoja na wale askari walinzi.”

Ni jambo la kusikitisha sana na kushangaza kuwa maadui wa Yesu Kristo hawakuridhika kwamba wamefanya fitina na kuhakikisha kuwa Yesu anakufa Msalabani, wakuu hawa wa makuhani na wazee siku ile ya pili ilikuwa ni sabato, lakini jambo la kusikitisha ni kuwa walikuwa tayari kuongeza dhambi juu ya dhambi siku ambayo walipaswa kuishika sabato na wakati wanafunzi wa Yesu na watu wengine wametulia wao walikuwa na mkakati wa kumdhibiti Yesu zaidi, mioyo yao ilikuwa imejawa na uovu na chuki kubwa sana hata pale ambapo Yesu alikuwa amekufa, Dunia ya leo pia imejawa na watu wanaopingana na maswala ya Mungu na kushindana na watumishi wa Mungu wa kweli na hata pale unapoamua kunyamaza kimya bado wako watu watatafuta kukuchafua, kumekuwako na watu waovu, wasiomcha Mungu, wasiotenda haki, waliojawa na wivu na uovu wa kila aina ambao kazi yao kubwa ni kupingana na Mungu na watumishi wake na wengine wakijifanya ni watumishi wa Mungu, ni jambo la kusikitisha kuona Viongozi wa Dini tena siku ya sabato Yesu akiwa kaburini bado wanaendelea kumfuatilia na kushitaki kwa Pilato na Pilato aliamuru Kaburi lilindwe kwa kadiri iwezekanavyo, Ukiona bado watu wanakusema vibaya hata baada ya wewe kuondoka au kufa ujue wewe umeacha historia ya kuigwa aidha kwa wema au kwa ubaya, tunaweza kumkumbuka Hitler kwa sababu ya ukatili wake wa kuua watu wengi, tunaweza pia kumkumbuka Idd Amin kwa ukatili wake lakini vilevile tunaweza kuwakumbuka watu wema kupitia wema wao, lakini ukiona mtu mwema anachafuliwa hata baada ya kifo chake au yeye mwenyewe akiwa hayupo ujue mtu huyo ameacha rekodi (legacy) isiyokuwa ya kawaida na hata ingawa hayupo bado ni tishio,

1.       Kaburi liliwekwa Muhuri – “Seal” – Ni muhimu kufahamu hapa tunapozungumza kuhusu Muhuri hatuzungumzii ule muhuri ambao watu wamezoea, kizazi cha leo kinajua Muhuri ule waliozoea kuiona ikiwepo Ofisini, na wino wake, Muhuri hii inayotajwa katika Biblia ikiwepo kule katika kitabu cha Ufunuo ni aina ya Kamba maalumu au nyororo maalumu inayofungwa na chuma katika kitu kinachomilikiwa na Serikali ikiwa na alama ya marufuku kufunguliwa na mtu mwingine, Muhuri hiyo ni alama ya ulinzi na usalama mfano serikali inapoweka umeme katika nyumba Mita ya umeme  ni mali ya shirika na hivyo hufungwa na Kamba au waya maalumu na kubanwa ili kwamba mtu mwingine asiweze kufungua, hali kadhalika mita ya maji, na ikiwa muhuri itaharibiwa maana yake amri halali ya kiulinzi imehalifiwa, na hatua kali za kisheria zinaweza kuchukuliwa dhidi ya mtu aliyevunja muhuri hiyo, wanaoweza kufungua Muhuri hiyo ni wale tu waliofunga,  kwa kiyunani Muhuri hiyo huitwa SPHRAGIZO. Kwa hiyo unaposikia kuwa Kaburi liliwekwa Muhuri maana yake kuna aidha kuna Kamba maalumu zilihusika kulifunga kabisa kaburi, ili isitokee mtu akasogeza lile jiwe na au lilisilibwa kwa simenti ili kuliunga kaburi hilo kusipatikane upenyo wowote wa kitu kupita,  au alama inayowekwa kuthibitisha kuwa hakuna uharibifu wowote unaoweza kufanyika ni tukio kama hili lilifanywa kwa nabii Daniel kuhakikisha kuwa anabaki katika tundu la Simba ona

 

Daniel 6:15-17“Ndipo watu wale wakakusanyika pamoja mbele ya mfalme, wakamwambia mfalme, Ee mfalme, ujue ya kuwa ni sheria ya Wamedi na Waajemi, lisibadilike neno lo lote lililo marufuku, wala amri yo yote iliyowekwa na mfalme. Basi mfalme akatoa amri, nao wakamleta Danieli, wakamtupa katika tundu la simba. Mfalme akanena, akamwambia Danieli, Mungu wako unayemtumikia daima, yeye atakuponya. Likaletwa jiwe, likawekwa mdomoni mwa lile tundu; naye mfalme akalitia muhuri kwa muhuri yake mwenyewe, na kwa muhuri ya wakuu wake, lisibadilike neno lo lote katika habari za Danieli.”               

 

Muhuri huu ulikuwa ni alama ya kuhakikisha kuwa hakuna mabadiliko yoyote yanayoweza kufanyika kinyume na kile ambacho serikali imekiamua na kuwa hakuna kutoka ndani ya kaburi au pango kwa msaada wa kibinadamu isipokuwa kama mfalme au aliyetoa amri atabatilisha, kwa hiyo kitu kilipowekwa muhuri ilimaanisha lisibatilike neno katika jambo lolote ambalo limeamuriwa labda Mungu aingilie kati.

 

2.       Kaburi liliwekewa ulinzi mkali sana – Utafiti wa kibiblia na kihistoria unakubaliana na ukweli kuwa hakuna askari walikuwa na utii kama askari wa Kirumi, na katika tamaduni za kirumi kama askari waliagizwa kulinda kitu na kitu hicho kikabainika kuwa hakikulindwa ipaswavyo hukumu yake ilikuwa ni kifo tu na kwa sababu hiyo wakati mwingine askari waliweza kuamua kujiua wenyewe kuliko kushughulikiwa na serikali angalia

 

-          Matendo ya Mitume 12:4-19 “Alipokwisha kumkamata, akamweka gerezani akamtia mikononi mwa vikosi vinne vya askari wanne wanne, wamlinde, akitaka baada ya Pasaka kumtoa na kumweka mbele ya watu. Basi Petro akalindwa gerezani, nalo kanisa likamwomba Mungu kwa juhudi kwa ajili yake. Hata wakati Herode alipotaka kumtoa, usiku ule ule Petro alikuwa analala katikati ya askari wawili, amefungwa minyororo miwili; walinzi mbele ya mlango wakailinda gereza. Mara malaika wa Bwana akasimama karibu naye, nuru ikamulika mle chumbani, akampiga Petro ubavuni, akamwamsha, akisema, Ondoka upesi. Minyororo yake ikamwanguka mikononi. Malaika akamwambia, Jifunge, kavae viatu vyako. Akafanya hivyo. Kisha akamwambia, Jivike nguo yako, ukanifuate. Akatoka nje, akamfuata; wala hakujua ya kuwa ni kweli yaliyofanywa na malaika; bali alidhani kwamba anaona maono. Na walipopita lindo la kwanza na la pili, wakaja hata mlango wa chuma wa kuingilia mjini, ukawafungukia wenyewe. Wakatoka nje, wakapita katika njia moja; mara malaika akamwacha. Hata Petro alipopata fahamu akasema, Sasa nimejua yakini ya kuwa Bwana amempeleka malaika wake na kunitoa katika mkono wa Herode na katika kutazamia kote kwa taifa la Wayahudi. Na alipokuwa akifikiri haya akafika nyumbani kwa Mariamu, mamaye Yohana, ambaye jina lake la pili ni Marko; na watu wengi walikuwa wamekutana humo wakiomba. Naye alipobisha kilango cha lango, kijakazi, jina lake Roda, akaja kusikiliza.  Alipoitambua sauti ya Petro, hakukifungua lango, kwa ajili ya furaha, bali alipiga mbio, akaingia ndani akawaambia kwamba Petro anasimama mbele ya lango. Wakamwambia, Una wazimu. Lakini yeye akakaza sana, akasema ya kwamba ndivyo hivyo. Wakanena, Ni malaika wake. Petro akafuliza kugonga, hata walipokwisha kumfungulia wakamwona, wakastaajabu. Naye akawapungia mkono wanyamaze, akawaeleza jinsi Bwana alivyomtoa katika gereza. Akasema, Kampasheni Yakobo na wale ndugu habari hizi. Akaondoka, akaenda mahali pengine. Hata kulipopambauka askari wakaingiwa na fadhaa nyingi, amekuwaje Petro. Na Herode alipomtafuta, asimwone, aliwauliza-uliza wale walinzi, akaamuru wauawe. Kisha akatelemkia kutoka Uyahudi kwenda Kaisaria, akakaa huko.”                

 

-          Matendo ya Mitume 16:25-27 “Lakini panapo usiku wa manane Paulo na Sila walikuwa wakimwomba Mungu na kumwimbia nyimbo za kumsifu, na wafungwa wengine walikuwa wakiwasikiliza. Ghafula pakawa tetemeko kuu la nchi, hata misingi ya gereza ikatikisika, na mara hiyo milango ikafunguka, vifungo vya wote vikalegezwa.Yule mlinzi wa gereza akaamka, naye alipoona ya kuwa milango ya gereza imefunguka, alifuta upanga, akataka kujiua, akidhani ya kuwa wafungwa wamekimbia.”

Kwa msingi huo unaweza kupata picha kuwa licha ya kuwepo kwa Muhuri lakini vile vile kaburi la Yesu lilikuwa na ulinzi mkali sana, kuna uwezekano walikuwepo askari zaidi ya 16 na kwa taratibu za kirumi askari asipotimiza wajibu alitakuwa kuuawa na ndio maana unaona hata mkuu wa gereza aliyekuwa akiwashikilia Paulo na Sila alitaka kujiua yeye mwenyewe kwa sababu ilieleweka wazi kuwa kama ameshindwa kutimiza wajibu katika kulinda kile alichotakiwa kukilinda basi hukumu yake ni kifo, kwa msingi huo tamaduni hii inatuhakikishia kuwa Kaburi la Yesu lililindwa bara bara na ilipaswa kuwa hivyo maana wao waliona Yesu kuwa ni Mjanja, mwongo, tapeli na mzushi kwa hiyo ulinzi wao ulikuwa ni wa kuhakikisha kuwa huyo mjanja hatoki! 

Yule Mjanja alisema siku ya tatu nitafufuka 

Ukweli ni kuwa wazee wale walikuwa wanafanya ujinga, Mungu alikuwa anataka wao wenyewe ndio wawe mashahidi wa Kwanza wa kufufuka kwake Kristo, Kumbuka pamoja na Yesu kurudia rudia kuwa atasulubiwa na kuuawa na siku ya tatu atafufuka jambo hili lilikuwa zito kueleweka kwa wanafunzi wa Yesu, lakini maadui wa Yesu walikuwa wanakumbuka na sasa wanafanya makakati wa kulilinda kaburi kama tulivyoona lilikuwa jambo jema kwao.

Hawakuwa wanajua kuwa wanashughulika na mtu ambaye Kifo hakiwezi kumzuia, walikuwa wakishughulika na Mwenyewe ambaye ni ufufuo na uzima, mwenye mamlaka ya mauti na uzima! Na ambaye makusudi yake hayawezi kuzuiliwa kamwe

Yohana 11:24-25 “Martha akamwambia, Najua ya kuwa atafufuka katika ufufuo siku ya mwisho. Yesu akamwambia, Mimi ndimi huo ufufuo, na uzima. Yeye aniaminiye mimi, ajapokufa, atakuwa anaishi;”

Huwezi kumuwekea mipaka mwanaume mwenye funguo/Mamlaka ya mauti na uzima Ufunuo 1:17-18 “Nami nilipomwona, nalianguka miguuni pake kama mtu aliyekufa. Akaweka mkono wake wa kuume juu yangu, akisema, Usiogope, Mimi ni wa kwanza na wa mwisho, na aliye hai; nami nalikuwa nimekufa, na tazama, ni hai hata milele na milele. Nami ninazo funguo za mauti, na za kuzimu.”

Yesu alifufuka, kufufuka kwake kunatoa ujumbe kuwa hakuna kitu wala mtu anaweza kuzuia kusudi la Mungu katika maisha yako, kama jinsi ambavyo hawakuweza kuzuia kusudi la Mungu kumfufua Yesu Kristo, Mungu ni mwenye nguvu ya kufufua anauwezo wa kuondoa lolote lililokufa na kulirudishia uhai, anauwezo wa kubadilisha huzuni kuwa furaha, anauwezo wa kubadilisha maombolezo kuwa machezo, kama jinsi ambavyo viongozi wa dini na askari na wazushi walishindwa kuzuia Yesu asifufuke nataka nikutangazie kuwa Roho Mtakatifu amenituma nikutangazie kuwa haijalishi wachawi wameweka muhuri ya namna gani, haijalishi kuwa wapiga majungu wamepiga kwa kiasi gani, hauijalishi kuwa wafitini wamefitinisha kwa kiwango gani, hajalishi kuwa umekandamizwa kwa kiasi gani, Mungu atamtuma malaika wake aliyezivunja zile muhuri na kudongolosha lile jiwe linalosimama kama kizuizi katika maisha yako na utatoka tena nasema utatoka tena nasema utainuka, adui zako wanataka kuhakikisha ya kuwa unalala, wanataka kuharibu sifa na wema wako uonekane kuwa wewe ni mjanja mjanja tu, wanatangaza mwisho wako na kudhani ya kuwa wamekudhibiti na kuwa huwezekani kuinuka tena Lakini  Roho Mtakatifu anatangaza mwanzo wako leo katika jina la Yesu Kristo wa Nazareth aliye hai, hakuna jini, hakuna maimuna, hakuna makata wala kinyamkera, hakuna pepo, hakuna mganga, hakuna mchawi, hakuna hirizi, hakuna pembe, hakuna zindiko, hakuna uchawi, hakuna mamlaka, hakuna jeshi, hakuna askari hakuna, hakuna hakuna kizuizi chochote kitakachozuia kusudi la Mungu katika maisha yako, wakati ambapo ujanja ulitumika kama neno la kejeli leo tunaligeuza kuwa sisi tulio ndani ya Yesu ni wajanja kweli kweli, sisi sio wa kawaida, tumewekwa katika ulimwengu wa roho pamoja na Kristo, tumekufa pamoja naye, tumefufuka pamoja naye, tunatawala pamoja naye hivyo ndivyo neno la Mungu linavyotuambia:-  

Waefeso 2:6 “Akatufufua pamoja naye, akatuketisha pamoja naye katika ulimwengu wa roho”, 

Katika Kristo Yesu; kila anayemuamini Yesu yuko juu, ameinuliwa amefufuka pamoja naye sisi sio wa kawaida, hakuna anayeweza kushindana na mapenzi ya Mungu katika maisha yetu, hakuna anayeweza kuhakikisha kuwa tunabaki kaburini, hakuna wa kutuzuia, hakuna wa kutuzibia, hakuna wa kulinda na kumzuia  Mungu mwenye nguvu, Mungu wa baba zetu anayahuisha tena maisha yetu na kutuweka mahali salama Kristo alitoka kwa mkwara kaburi lilitetemeka muhuri zikavunjwa na malaika akalivingirisha jiwe na akalikalia jiwe, walinzi wakawa kama wafu kiwewe kiliwashika, Yesu ni aliye hai katika wafu, wewe na mimi tu hai leo haleluyaaa! Wakati adui zetu wakikesha kuhakikisha hatuamki ni wao ndio watakaokuwa wafu wakati sisi tunafufuka!, Maandiko yanaonyesha kuwa walinzi wa kirumi safari hii hawakuweza kutimiza wajibu wao malaika wa Bwana alilivingirisha jiwe akalikalia, alivunja mihuri yao, alibatilisha matakwa yao Yesu alifufuka na hakuibiwa mwanaume wa wanaume kaburi halikumuweza, Alifufuka kwelikweli!, Nampenda Mungu nampenda Yesu mipango yao huiweka wazi kabisa kwa sababu hakuna anayeweza kuzuia mpango wa Mungu, Mtu mmoja aliniambia usiweke wazi mipango yako wala usimwambie mtu ndoto zako kwa sababu wanadamu ni waovu wanaweza kwenda kuzuia mipango yako au kupigana nayo, sielewi anatumia andiko gani lakini Tabia ya Mungu huweka wazi mipango yake hueleza mapema siku ya tatu nitafufuka na hakuna wa kuzuia, Kama ndoto zangu ni mpango wa Mungu hata nikiweka wazi hakuna wa kuzuia, kama mipango yangu ni mipango ya Bwana hakuna wa kuzuia, mbona walijaribu kumuua mwenye ndoto Yusufu ili kuua ndoto zake na Je ziliztimizwa hazikutimizwa? Hekima ya Mungu sio kama hekima ya wapuuzi wa dunia hii, Mungu akiwa na mpango na jambo lake hata mroge kwa ramba ramba, chaumbeya au tekelo, au uende kwa waganga kule Pemba, au Newala kule Nchedebwa, au Nachingwea, au Lamu, au Kwasemangube, au Kwamsisi huko Handeni, au Sumbawanga kokote unakoweza kwenda huwezi kuzuia makusudi na mpango wa Mungu, Mungu ni mwenye nguvu angalia walipozuia na kulilinda kaburi kwa ulinzi wao wote maandiko yanasema kulitoka tetemeko kubwa la nchi, malaika alishuka akalivingirisha jiwe na kulikalia, wapinzani wakawa kama wafu hivi ndivyo Mungu wentu anavyofanya mambo yake !

Mathayo 28:2-4 “Na tazama, palikuwa na tetemeko kubwa la nchi; kwa sababu malaika wa Bwana alishuka kutoka mbinguni, akaja akalivingirisha lile jiwe akalikalia. Na sura yake ilikuwa kama umeme, na mavazi yake meupe kama theluji. Na kwa kumwogopa, wale walinzi wakatetemeka, wakawa kama wafu.” 
    

Na. Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni