Alhamisi, 29 Februari 2024

Meza ya Bwana na Karamu za Upendo!


1Wakorintho 11:23-32 “Kwa maana mimi nalipokea kwa Bwana niliyowapa nanyi, ya kuwa Bwana Yesu usiku ule aliotolewa alitwaa mkate, naye akiisha kushukuru akaumega, akasema, Huu ndio mwili wangu ulio kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu. Na vivi hivi baada ya kula akakitwaa kikombe, akisema, Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu; fanyeni hivi kila mnywapo, kwa ukumbusho wangu. Maana kila mwulapo mkate huu na kukinywea kikombe hiki, mwaitangaza mauti ya Bwana hata ajapo. Basi kila aulaye mkate huo, au kukinywea kikombe hicho cha Bwana isivyostahili, atakuwa amejipatia hatia ya mwili na damu ya Bwana. Lakini mtu ajihoji mwenyewe, na hivyo aule mkate, na kukinywea kikombe. Maana alaye na kunywa, hula na kunywa hukumu ya nafsi yake, kwa kutokuupambanua ule mwili. Kwa sababu hiyo wako wengi kwenu walio hawawezi na dhaifu, na watu kadha wa kadha wamelala. Lakini kama tungejipambanua nafsi zetu, tusingehukumiwa. Ila tuhukumiwapo, twarudiwa na Bwana, isije ikatupasa adhabu pamoja na dunia.”




Utangulizi:

Ni muhimu kwetu kufahamu, kuwa kushiriki meza ya Bwana ni mojawapo ya agizo muhimu sana katika kanisa, ni agizo la kibiblia, ambalo wanafunzi wa Yesu Kristo wanapaswa kulifanyia kazi, Meza ya Bwana au Chakula cha Bwana ni Agizo lililotolewa na Yesu Kristo mwenyewe katika karamu yake ya Mwishoaliposhiriki chakula cha pasaka na wanafunzi wake kabla kidogo ya kukamatwa na kusulubiwa kisha kuuawa na kuzikwa na kufufuka na baadaye kupaa mbinguni

Mathayo 26:17-28. “Hata siku ya kwanza ya mikate isiyotiwa chachu, wanafunzi wake wakamwendea Yesu, wakamwambia, Ni wapi utakapo tukuandalie uile Pasaka? Akasema, Enendeni mjini kwa mtu fulani, mkamwambie, Mwalimu asema, Majira yangu ni karibu; kwako nitafanya Pasaka pamoja na wanafunzi wangu. Wanafunzi wakafanya kama Yesu alivyowaagiza, wakaiandaa Pasaka. Basi kulipokuwa jioni aliketi chakulani pamoja na wale Thenashara. Nao walipokuwa wakila, alisema, Amin, nawaambia, Mmoja wenu atanisaliti. Wakahuzunika sana, wakaanza kumwuliza mmoja mmoja, Ni mimi, Bwana? Akajibu akasema, Yeye aliyetia mkono wake pamoja nami katika kombe, ndiye atakayenisaliti. Mwana wa Adamu aenda zake, kama alivyoandikiwa; lakini ole wake mtu yule ambaye amsaliti Mwana wa Adamu! Ingekuwa heri kwake mtu yule kama asingalizaliwa. Yuda, yule mwenye kumsaliti, akajibu, akasema, Ni mimi, Rabi? Akamwambia, Wewe umesema. Nao walipokuwa wakila Yesu alitwaa mkate, akabariki, akaumega, akawapa wanafunzi wake, akasema, Twaeni, mle; huu ndio mwili wangu Akakitwaa kikombe, akashukuru, akawapa, akisema, Nyweni nyote katika hiki; kwa maana hii ndiyo damu yangu ya agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi kwa ondoleo la dhambi.”

Kwa msingi huo leo tutachukua Muda kujifunza kwa kina na mapana na marefu kuhusiana na Meza ya bwana na tutajifunza somo hili Meza ya Bwana na Karamu za Upendo! Kwa kuzingatia vipengele tisa vifuatavyo:-

 

·         Meza ya Bwana na karamu za upendo.

·         Chanzo cha meza ya Bwana au  chakula cha Bwana

·         Agizo la kushiriki meza ya Bwana.

·         Sifa za mshiriki wa meza ya Bwana.

·         Vitu vinavyotumiwa na utaratibu wa kushiriki meza ya Bwana.

·         Maana ya kiroho ya meza ya Bwana

·         Faida nyingine za kushiriki meza ya Bwana.

·         Hasara ya kushiriki meza ya Bwana isivyo stahili.

·         Mambo yasiyo ya Kibiblia yanayihusiana na meza ya Bwana!

  

Meza ya Bwana na Karamu za Upendo !

Ni muhimu kufahamu kuwa nyakati za kanisa la kwanza hawakuwa wanashiriki meza ya Bwana peke yake, Lakini walishiriki meza ya Bwana pamoja na kufanya karamu za Upendo, Karamu hizo za upendo kwa kiyunani ziliitwa KOINONIA ambapo watu waliungana pamoja na kushirikiana vyakula, zawadi, ushirika, na changizo au kufurahia maswala mbalimbali, kwa hiyo baada ya kushiriki meza ya Bwana vilevile watu walishirikiana vyakula kwa upendo kila mmoja akimshirikisha mwenziwake kile alichikuja nacho kutoka nyumbani kwa hiyo chakula hiki cha Bwana kilishirikishwa pamoja na karamu za Upendo, unaweza kuona zikitajwa katika maandiko namna hiyo

Yuda 1:12-13 “Watu hawa ni miamba yenye hatari katika karamu zenu za upendo walapo karamu pamoja nanyi, wakijilisha pasipo hofu; ni mawingu yasiyo na maji, yachukuliwayo na upepo; ni miti iliyopukutika, isiyo na matunda, iliyokufa mara mbili, na kung'olewa kabisa; ni mawimbi ya bahari yasiyozuilika, yakitoa aibu yao wenyewe kama povu; ni nyota zipoteazo, ambao weusi wa giza ndio akiba yao waliowekewa milele.”

2Petro 2:13 “Wakipatikana na madhara, ambayo ni ujira wa udhalimu wao, wakidhania kuwa ulevi wakati wa mchana ni anasa; wamekuwa ni mawaa na aibu wakifuata anasa zisizo kiasi katika karamu zao za upendo, wafanyapo karamu pamoja nanyi;”

Hata hivyo pamoja na wazo zuri la kanisa la kwanza kushiriki meza ya Bwana pamoja na karamu za upendo kulijitokeza kasoro mbalimbali, ikiwapo karamu hizi kutumiwa na walimu wa uongo kueneza mafundisho yao, na vilevile watu matajiri na wachoyo kuamua kula vyakula vyao badala ya kushirikiana na wengine, aidha wengine waliamua kula vyakula vyao bila kuwasubiria watu wengine na kwa sababu hiyo utaweza kuona kuwa mitume walitahadharisha kuhusu kuvamiwa kwa karamu hizo za upendo, na walimu wa uongo, vilevile Paulo mtume alikemea vikali tabia zilizokuwa zikijitokeza na ndipo ilipofikia wakati ambapo Meza ya Bwana ambayo ilikuwa ni ibada maalumu haikuweza tena kuwekwa pamoja na Karamu za upendo

1Wakorintho 11: 17-22 “Lakini katika kuagiza haya, siwasifu, ya kwamba mnakusanyika, si kwa faida bali kwa hasara. Kwa maana kwanza mkutanikapo kanisani nasikia kuna faraka kwenu; nami nusu nasadiki; kwa maana lazima kuwapo na uzushi kwenu, ili waliokubaliwa wawe dhahiri kwenu. Basi mkutanikapo pamoja haiwezekani kula chakula cha Bwana; kwa maana kila mmoja hutangulia kutwaa chakula chake katika kule kula; hata huyu ana njaa, na huyu amelewa. Je! Hamna nyumba za kulia na kunywea? Au mnalidharau kanisa la Mungu, na kuwatahayarisha hao wasio na kitu? Niwaambieni? Niwasifu? La! Siwasifu kwa ajili ya hayo.”

Unaona kwa hiyo kutokana na hitilafu zilizokuwa zimejitokeza Meza ya Bwana ilitenganishwa na Karamu za Upendo, na kubaki Meza ya bwana pekee ambayo ndio moja ya agizo muhimu ambalo Yesu aliagiza kanisa kulifanyia kazi. Hii haimaanishi kuwa KOINONIA ni dhambi bali kila kanisa linaweza kujiandalia KOINONIA yake bila kuiathiri meza ya Bwana ambayo ni ibada inayopaswa kuheshimiwa sana!

 

Chanzo cha meza ya Bwana au Chakula cha Bwana!

Nyakati za agano la kale wana wa Israel waliagizwa kula chakula cha Bwana yaani Pasaka. Pasaka ya kwanza ilikuwa siku ile wana wa Israel walipotoka Misri ambapo walikula mikate isiyotiwa chachu: 

Kutoka 12:3-20 “Semeni na mkutano wote wa Israeli, mkawaambie, Siku ya kumi ya mwezi huu kila mtu atatwaa mwana-kondoo, kwa hesabu ya nyumba ya baba zao, mwana-kondoo kwa watu wa nyumba moja; na ikiwa watu wa nyumba ni wachache kwa mwana-kondoo, basi yeye na jirani yake aliye karibu na nyumba yake na watwae mwana-kondoo mmoja, kwa kadiri ya hesabu ya watu; kwa kadiri ya ulaji wa kila mtu, ndivyo mtakavyofanya hesabu yenu kwa yule mwana-kondoo. Mwana-kondoo wenu atakuwa hana ila, mume wa mwaka mmoja; mtamtwaa katika kondoo au katika mbuzi. Nanyi mtamweka hata siku ya kumi na nne ya mwezi ule ule; na kusanyiko lote la mkutano wa Israeli watamchinja jioni. Nao watatwaa baadhi ya damu yake na kuitia katika miimo miwili na katika kizingiti cha juu, katika zile nyumba watakazomla. Watakula nyama yake usiku ule ule, imeokwa motoni, pamoja na mkate usiotiwa chachu; tena pamoja na mboga zenye uchungu. Msiile mbichi, wala ya kutokoswa majini, bali imeokwa motoni; kichwa chake pamoja na miguu yake, na nyama zake za ndani. Wala msisaze kitu chake cho chote hata asubuhi, bali kitu kitakachosalia hata asubuhi mtakichoma kwa moto. Tena mtamla hivi; mtakuwa mmefungwa viuno vyenu, mmevaa viatu vyenu miguuni, na fimbo zenu mikononi mwenu; nanyi mtamla kwa haraka; ni pasaka ya BWANA. Maana nitapita kati ya nchi ya Misri usiku huo, nami nitawapiga wazaliwa wa kwanza wote katika nchi ya Misri, wa mwanadamu na wa mnyama; nami nitafanya hukumu juu ya miungu yote ya Misri; Mimi ndimi BWANA. Na ile damu itakuwa ishara kwenu katika zile nyumba mtakazokuwamo; nami nitakapoiona ile damu, nitapita juu yenu, lisiwapate pigo lo lote likawaharibu, nitakapoipiga nchi ya Misri.  Na siku hii itakuwa ukumbusho kwenu, nanyi mtaifanya iwe sikukuu kwa BWANA; mtaifanya iwe sikukuu katika vizazi vyenu vyote, kwa amri ya milele Mtakula mikate isiyochachwa muda wa siku saba; siku hiyo ya kwanza mtaondoa chachu yote isiwe katika nyumba zenu kabisa; kwa kuwa mtu ye yote atakayekula mkate uliochachwa tangu siku hiyo ya kwanza hata siku ya saba, nafsi hiyo atakatiliwa mbali na Israeli. Siku ya kwanza kutakuwa kwenu na kusanyiko takatifu, na siku ya saba kutakuwa kusanyiko takatifu; haitafanywa kazi yo yote katika siku hizo, isipokuwa kwa hiyo ambayo kila mtu hana budi kula, hiyo tu ifanyike kwenu. Nanyi mtaitunza ile sikukuu ya mikate isiyochachwa; kwa kuwa katika siku iyo hiyo mimi nimeyatoa majeshi yenu katika nchi ya Misri; kwa hiyo mtaitunza siku hiyo katika vizazi vyenu vyote, kwa amri ya milele. Mwezi wa kwanza, siku ya mwezi kumi na nne, wakati wa jioni, mtakula mikate isiyochachwa, hata siku ya mwezi ishirini na moja jioni. Muda wa siku saba isionekane chachu katika nyumba zenu kabisa; kwa kuwa mtu ye yote atakayekula hiyo iliyotiwa chachu, nafsi hiyo atakatiliwa mbali na mkutano wa Israeli, akiwa mwenye kukaa hali ya ugeni, au akiwa mtu aliyezaliwa katika nchi. Msile kitu chochote kilichochachwa; mtakula mikate isiyochachwa katika makao yenu yote.

Kwa msingi huo ukiacha kuwa siku ya Pasaka wana wa Israel walichinja kondoo na kupaka damu yake katika miimo ya milango, ili malaika wa bwana aweze kuruka kuipiga nyumba isiyo na damu, lakini ukiacha mwana kondoo Pasaka aliliwa au kuadhimishwa pamoja na mikate isiyotiwa chachu na ulaji wa mboga chunguchungu, Pasaka iliadhimishwa siku ya 14 katika Mwezi wa Nisani kwa hiyo unaweza kuona kuwa meza ya Bwana au chakula cha Bwana ni agizo la kibiblia hata kabla ya agano jipya

Mambo ya walawi 23:3-6 “Mtafanya kazi siku sita; lakini siku ya saba ni Sabato ya kustarehe kabisa, kusanyiko takatifu; msifanye kazi ya namna yo yote; ni Sabato kwa BWANA katika makao yenu yote. Sikukuu za BWANA ni hizi, ni makusanyiko matakatifu, ambayo mtayapigia mbiu kwa nyakati zake. Mwezi wa kwanza, siku ya kumi na nne ya mwezi wakati wa jioni, ni pasaka ya BWANA. Na siku ya kumi na tano ya mwezi ule ule ni sikukuu kwa BWANA ya mkate usiotiwa chachu; mtaila mikate isiyochachwa muda wa siku saba.”

Pasaka ya Mwisho kabisa kabla ya angano jipya ndio ambayo iliadhimishwa na Bwana Yesu pamoja na wanafunzi wake usiku ule kabla Yesu hajatolewa na kusulubiwa kama Mwana kondoo wa wokovu

Luka 22:7-19 “Ikafika siku ya mikate isiyotiwa chachu, ambayo ilipasa kuchinja pasaka. Akawatuma Petro na Yohana, akisema, Nendeni, mkatuandalie pasaka tupate kuila. Wakamwambia, Wataka tuandae wapi? Akawaambia, Tazama, mtakapoingia mjini mtakutana na mwanamume akichukua mtungi wa maji; mfuateni mkaingie katika nyumba atakayoingia yeye. Na mtamwambia mwenye nyumba, Mwalimu akuambia, Ki wapi chumba cha wageni, nipate kula pasaka humo pamoja na wanafunzi wangu? Naye atawaonyesha chumba kikubwa orofani, kimekwisha andikwa; andaeni humo.Wakaenda, wakaona kama alivyowaambia, wakaiandaa pasaka. Hata saa ilipofika aliketi chakulani, yeye na wale mitume pamoja naye. Akawaambia, Nimetamani sana kuila pasaka hii pamoja nanyi kabla ya kuteswa kwangu; kwa maana nawaambia ya kwamba siili tena hata itakapotimizwa katika ufalme wa Mungu. Akapokea kikombe, akashukuru, akasema, Twaeni hiki, mgawanye ninyi kwa ninyi; Maana nawaambia ya kwamba tangu sasa sinywi mazao ya mzabibu hata ufalme wa Mungu utakapokuja. Akatwaa mkate, akashukuru, akaumega, akawapa, akisema, [Huu ndio mwili wangu unaotolewa kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu. Kikombe nacho vivyo hivyo baada ya kula; akisema, Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu, inayomwagika kwa ajili yenu.]

Ni katika usiku huu Ndio Yesu aliamurukufanya jambo hili kwa ukumbusho wake, kwa hiyo kimsingi katika wakati huu Yesu alikuwa ameanzisha utaratibu mpya wa kuiandaa Pasaka bila mwana kondoo, na hivyo kumbukumbu yake inafanyika kupitia miakate isiyotiwa chahu na juisi ya uzao wa mzabibu nah ii ikawa ndio nnia mpya ya kumuadhimisha Kristo katika agano jipya na kwa kufanya hivyo alibatilisha yote  na kutuanzia njia mpya

Ebra 10:19-20 “Basi, ndugu, kwa kuwa tuna ujasiri wa kupaingia patakatifu kwa damu ya Yesu, njia ile aliyotuanzia iliyo mpya, iliyo hai, ipitayo katika pazia, yaani, mwili wake;”  

Kwa kawaida Pasaka hii iliadhimishwa nyakati za dhabihu ya jioni na ndio maana meza ya Bwana pia huitwa kwa kiingereza LORD SUPPER ambayo maana yake ni evening meal – Yaani chakula cha jioni Marko 14:16-18 “Wanafunzi wakatoka, wakaenda mjini, wakaona kama alivyowaambia, wakaiandaa pasaka. Basi ilipokuwa jioni yuaja pamoja na wale Thenashara. Nao walipokuwa wameketi chakulani, wakila, Yesu alisema, Amin, nawaambia, Mmoja wenu, naye anakula pamoja nami, atanisaliti.”

Hata hivyo hii haimaanishi kuwa ni lazima Meza ya bwana ifanyike jioni, Lakini kama inaweza kufanyika mida hiyo itapendeza Zaidi lakini sio sharia

 

Agizo la kushiriki Meza ya Bwana!

Kwa msingi huo ni Muhimu kufahamu kuwa agizo la kushiriki Meza ya Bwana linamuhusu kila mtu aliyeokoka, Meza ya bwana sio utaratibu wa kidini ni agizo la kibiblia ni amri

Luka 22:19-20 “Akatwaa mkate, akashukuru, akaumega, akawapa, akisema, [Huu ndio mwili wangu unaotolewa kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu. Kikombe nacho vivyo hivyo baada ya kula; akisema, Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu, inayomwagika kwa ajili yenu.]

1Wakorintho 11:23-25 “Kwa maana mimi nalipokea kwa Bwana niliyowapa nanyi, ya kuwa Bwana Yesu usiku ule aliotolewa alitwaa mkate, naye akiisha kushukuru akaumega, akasema, Huu ndio mwili wangu ulio kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu. Na vivi hivi baada ya kula akakitwaa kikombe, akisema, Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu; fanyeni hivi kila mnywapo, kwa ukumbusho wangu.”

Kwa msingi huo unapoiangalia meza ya Bwana unaweza kudhani kuwa ni kitu cha kipuuzi hizi lakini ni Agizo la Kristo kwa kanisa na kwa sababu hiyo hatupaswi kamwe kupuuzia maagizo ya Mungu wala kuchagua luipi la kulifanyia kazi na lipi la kuliacha, kwani kupouuzia baadhi ya maagizo ya Mungu ni kujitafutia laana  

Zaburi 119:6,21 “Ndipo mimi sitaaibika, Nikiyaangalia maagizo yako yote. Umewakemea wenye kiburi, Wamelaaniwa waendao mbali na maagizo yako.”           

Haitupasi kuchagua maagizo  Fulani na mengine kuchukia, inatupasa kutii.  Kutokuifanya  maagizo Fulani ni  kulaaniwa; Hivyo ni  wajibu wetu kushiriki meza ya Bwana kila inapopatiakana nafasi ya kufanya hivyo, kwa kuwa maandiko yameagiza kila mkutanikapo, hii maana yake ni kila inapofanyika ibada na wakati mwingine uongozi wa kanisa unaweza kuamua ni wakati gani wa kufanya hivyo kutokna na Programu za kikanisa, makanisa mengine hufanya kila jumapili au kila wanapokutanika au kila kunapokuwa na ibada, wengine hufanya mara moja kila mwezi na kadhalika kila kanisa linaweza kujipangia utaratibu wake jambo la msingi ni agizo hili la Bwana kufanyiwa kazi kama tu lilivyo agizo la ubatizo kwa kuwa maandiko hayakupanga wakati  

1Wakoritho 11: 24-26. “naye akiisha kushukuru akaumega, akasema, Huu ndio mwili wangu ulio kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu. Na vivi hivi baada ya kula akakitwaa kikombe, akisema, Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu; fanyeni hivi kila mnywapo, kwa ukumbusho wangu. Maana kila mwulapo mkate huu na kukinywea kikombe hiki, mwaitangaza mauti ya Bwana hata ajapo.”

 

Sifa za Mshiriki wa Meza ya Bwana!

Si kila mtu anaweza kuwa na sifa ya kushiriki Meza ya Bwana, Meza ya bwana unaweza kuona kuwa Yesu aliishiriki akiwa na wanafunzi wake wale 12 tu, hii maana yake ni kuwa kuna sifa maalumu za mtu anayepaswa kushiriki meza ya Bwana, kwa sababu Meza ya Bwana inamshirikisha Kristo au inamhitaji mtu mwenye ushirika na Kristo

Mtu anayeshiriki meza ya Bwana kwanza anapaswa kuwa Mwanafunzi wa Yesu, na sio kila mtu au mtu yeyote Luka 22:10-11 “Akawaambia, Tazama, mtakapoingia mjini mtakutana na mwanamume akichukua mtungi wa maji; mfuateni mkaingie katika nyumba atakayoingia yeye.Na mtamwambia mwenye nyumba, Mwalimu akuambia, Ki wapi chumba cha wageni, nipate kula pasaka humo pamoja na wanafunzi wangu?

Kwa Msingi huo tunapata picha kuwa mshiriki wa meza ya Bwana anapaswa kuwa Mwanafunzi wa Yesu, na Mwanafunzi wa Yesu ni lazima awe na sifa zifuatazo:-

a.      Awe ameokolewa yaani kama vile wale walioshiriki kumla Pasaka katika agano la kale walikuwa ni jamii ya wana wa Israel pamoja na jamii ya watu wengine waliookolewa kutoka Misri kwenda katika nchi ya Kanaani, kwa hiyo ni lazima awe aliyetubu dhambi zake kwa kamaanisha kuziacha, na kuishi maisha ya utauwa yaani utakatifu, katika kipindi hiki cha  kushiriki Meza ya Bwana tunakumbuka jinsi tulivyookolewa kutoka katika utumwa wa dhambi

 

Kutoka 12: 39-42 “Nao wakaoka mikate isiyochachwa ya ule unga waliouchukua walipotoka Misri, maana, haukutiwa chachu, kwa sababu walitolewa watoke Misri, wasiweze kukawia, nao walikuwa hawajajifanyia tayari chakula. Basi wana wa Israeli kukaa kwao, maana, muda waliokaa ndani ya Misri, ulikuwa ni miaka mia nne na thelathini.  Ilikuwa mwisho wa miaka hiyo mia nne na thelathini, ilikuwa siku ile ile, ya kwamba majeshi yote ya BWANA yalitoka nchi ya Misri. Ni usiku wa kuangaliwa sana mbele za BWANA kwa sababu ya kuwatoa katika nchi ya Misri; huu ndio usiku wa BWANA, ambao wapasa kuangaliwa sana na wana wa Israeli wote katika vizazi vyao.”

 

Kama  wana wa Israel  walivyotolewa misri kwenda Kanaani pia  ukawa usiku wa kukumbukwa sana katika pasaka ile ya kwanza washiriki, wa Meza ya Bwana wanapaswa kukumbuka kazi kubwa ya ukombozi iliyofanywa na Yesu Kristo pale Msalabani kwaajili ya ulimwengu lakini Zaidi sana wale wamuaminio! ni wakati wa kujichunguza na kuyaangalia maagizo ya Bwana yaani wakati wa kushiriki meza ya Bwana ni wakati wa kuishi maisha ya utakatifu nyaani kuwa mbali na chahu chahu katika maandiko huwakilisha dhambi 

 

Kutoka 13: 3 “Musa akawaambia hao watu, Kumbukeni siku hii, mliyotoka nchi ya Misri, kutoka nyumba ya utumwa; kwa kuwa BWANA aliwatoa mahali hapa kwa nguvu za mkono wake; na usiliwe mkate uliochachwa.”     

 

b.      Awe amebatizwa kwenye maji tele sawa na maandiko na ni kwa jina la Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu. Au mtu ambaye yuko tayari kubatizwa baada ya kuwa ameokolewa, wote tunafahamu kuwa wana wa Israel licha ya kuokolewa kutoka Misri lakini vilevile tunaelezwa kuwa walibatizwa wawe wa Musa ona

 

1Wakorintho 10:1-4 “Kwa maana, ndugu zangu, sipendi mkose kufahamu ya kuwa baba zetu walikuwa wote chini ya wingu; wote wakapita kati ya bahari; wote wakabatizwa wawe wa Musa katika wingu na katika bahari; wote wakala chakula kile kile cha roho; wote wakanywa kinywaji kile kile cha roho; kwa maana waliunywea mwamba wa roho uliowafuata; na mwamba ule ulikuwa ni Kristo.”

 

Unaona Israel waliokula chakula cha kiroho, na kunywa kinywaji kile cha roho walibatizwa wawe wa Musa, tunajifunza hapa vilevile kwa kuwa Meza ya Bwana ni chakula cha kiroho na kinywaji cha kiroho basi wale wanaoshiriki wanapaswa kuwa watu waliotii au watakaotii agizo la Ubatizo

 

Mathayo 28:19-20. “Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.”

 

Yohana 3:22-23 “Baada ya hayo Yesu na wanafunzi wake walikwenda mpaka nchi ya Uyahudi; akashinda huko pamoja nao, akabatiza. Yohana naye alikuwa akibatiza huko Ainoni, karibu na Salimu, kwa sababu huko kulikuwa na maji tele; na watu wakamwendea, wakabatizwa.”

 

Yohana 4:1-2 “Kwa hiyo Bwana, alipofahamu ya kuwa Mafarisayo wamesikia ya kwamba, Yesu anafanya wanafunzi wengi kuliko Yohana, na kuwabatiza, (lakini Yesu mwenyewe hakubatiza, bali wanafunzi wake,)

 

Wakolosai 2:11-12 “Katika yeye mmetahiriwa kwa tohara isiyofanyika kwa mikono, kwa kuuvua mwili wa nyama, kwa tohara ya Kristo.Mkazikwa pamoja naye katika ubatizo; na katika huo mkafufuliwa pamoja naye, kwa kuziamini nguvu za Mungu aliyemfufua katika wafu.”

 

Matendo 2:41-42 “Nao waliolipokea neno lake wakabatizwa; na siku ile wakaongezeka watu wapata elfu tatu. Wakawa wakidumu katika fundisho la mitume, na katika ushirika, na katika kuumega mkate, na katika kusali.”

 

Matendo 8:12 “Lakini walipomwamini Filipo, akizihubiri habari njema za ufalme wa Mungu, na jina lake Yesu Kristo, wakabatizwa, wanaume na wanawake.”

 

Kwa msingi huo unaweza kuona kwamba Mshiriki wa Meza ya Bwana ni mwanafunzi wa Yesu yaani mtu aliyeisikia injili na kuiamini kisha kubatizwa na anapokuwa anakaa katika fundisho basi huyo ana sifa ya kushiriki meza ya Bwana au chakula cha Bwana  

 

c.       Asiwe mtu mwenye kuabudu Sanamu au miungu mingine 1Wakorintho 10:15-21. “Kwa ajili ya hayo, wapenzi wangu, ikimbieni ibada ya sanamu. Nasema kama na watu wenye akili; lifikirini ninyi ninenalo. Kikombe kile cha baraka tukibarikicho, je! Si ushirika wa damu ya Kristo? Mkate ule tuumegao, si ushirika wa mwili wa Kristo? Kwa kuwa mkate ni mmoja, sisi tulio wengi tu mwili mmoja; kwa maana sisi sote twapokea sehemu ya ule mkate mmoja.     Waangalieni hao Waisraeli walivyokuwa kwa jinsi ya mwili; wale wazilao dhabihu, je! Hawana shirika na madhabahu? Basi niseme nini? Ya kwamba kile kilichotolewa sadaka kwa sanamu ni kitu? Au ya kwamba sanamu ni kitu? Sivyo, lakini vitu vile wavitoavyo sadaka wavitoa kwa mashetani, wala si kwa Mungu; nami sipendi ninyi kushirikiana na mashetani. Hamwezi kunywea kikombe cha Bwana na kikombe cha mashetani. Hamwezi kushirikiana katika meza ya Bwana na katika meza ya mashetani.”                                 

       

d.      Awe mume wa mke mmoja au mke wa mume mmoja  yaani mtu asiyeishi katika maisha ya ukahaba au ndoa ambayo haijahalalishwa katika jamii, au ndoa isiyohalali  I Wakoritho 6:15-20 “Je! Hamjui ya kuwa miili yenu ni viungo vya Kristo? Basi nivitwae viungo vya Kristo na kuvifanya viungo vya kahaba? Hasha! Au hamjui ya kuwa yeye aliyeungwa na kahaba ni mwili mmoja naye? Maana asema, Wale wawili watakuwa mwili mmoja. Lakini yeye aliyeungwa na Bwana ni roho moja naye. Ikimbieni zinaa. Kila dhambi aitendayo mwanadamu ni nje ya mwili wake; ila yeye afanyaye zinaa hutenda dhambi juu ya mwili wake mwenyewe. Au hamjui ya kuwa mwili wenu ni hekalu la Roho Mtakatifu aliye ndani yenu, mliyepewa na Mungu? Wala ninyi si mali yenu wenyewe; maana mlinunuliwa kwa thamani. Sasa basi, mtukuzeni Mungu katika miili yenu.”

 

Tunaposhiriki meza ya Bwana maana yake sisi ni washirika wa Yesu Kristo, mtu anapookolewa mwili wake unakuwa kiuongo katika mwili wa Kristo, naye anakuwa ni hekalu la Roho Mtakatifu kwa msingi huo basi uko umuhimu wa mtu huyu kuwa na maisha matakatifu ikiwa ni pamoja na kujitenga na zinaa au ndoa isiyohalali, huwezi kuishi maisha ya kikahaba kisha ukashiriki meza ya Bwana unaweza kupata madhara au huwezi kuwa mshirikina kisha ukashiriki meza ya bwana unaweza kupata madhara badala ya faida zinazokusudiwa, kimsingi maisha nsafi na matakatifu, kuwa mbali na dhambi na ibada ya sanamu, na ushirikina na kuishi kiholela kunakufanya usiwe mshirika wa Kristo na hivyo sio vema kushiriki meza ya Bwana 

 

Vitu vinavyotumiwa na utaratibu wa kushiriki meza ya Bwana.

Vitu vinavyotumiwa katika Meza ya bwana maana yake ni nyenzo zinazotumika katika kuiandaa meza ya Bwana

-          Mkate usiyotiwa chachu:

 

Mikate inayotumika katika maandalizi ya Meza ya bwana inapaswa kuwa ni mikate isiyotumia hamira au Backingpoweder yaani iliyoumuliwa au mikate isiyotiwa chachu

 

Luka 22:7, 19-20 7. “Ikafika siku ya mikate isiyotiwa chachu, ambayo ilipasa kuchinja pasaka.” 19-20 “Akatwaa mkate, akashukuru, akaumega, akawapa, akisema, [Huu ndio mwili wangu unaotolewa kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu. Kikombe nacho vivyo hivyo baada ya kula; akisema, Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu, inayomwagika kwa ajili yenu.] 

 

Mikate hii siyo kama ile tunayoitumia kwa chai. Ingawa ni vema kutumia hiyo majumbani lakini katika meza ya Bwana hairusiwi kwa nini? Sababu ni kuwa chachu ni mfano wa uovu chachu ni mfano wa dhambi na kwa sababu Meza ya Bwana ni alama kivuli inayomwakilisha Bwana wetu Yesu ambaye hakuishi masiha yandhambi hivyo mkate huo unapaswa kuwa ni mkate usiotiwa chachu au kuumuliwa moja ya mifano ya mkate usiochachwa ni chapati, aidha mafundisho ya uongo pia katika agano jipya huitwa chachu, Yesu hakuwa na dhambi wala hakuwa mwongo

 

1Wakorintho 5:6-8 “Kujisifu kwenu si kuzuri. Hamjui kwamba chachu kidogo hulichachusha donge zima? Basi, jisafisheni, mkatoe ile chachu ya kale, mpate kuwa donge jipya, kama vile mlivyo hamkutiwa chachu. Kwa maana Pasaka wetu amekwisha kutolewa kuwa sadaka, yaani, Kristo; basi na tuifanye karamu, si kwa chachu ya kale, wala kwa chachu ya uovu na ubaya, bali kwa yasiyochachika, ndio weupe wa moyo na kweli.”

 

Mathayo 16:11-12 “Imekuwaje hamkufahamu ya kuwa si kwa sababu ya mkate naliwaambia? Ila jilindeni na chachu ya Mafarisayo na Masadukayo. Ndipo walipofahamu ya kuwa hakuwaambia kujilinda na chachu ya mkate, bali na mafundisho ya Mafarisayo na Masadukayo.”

 

Luka 12:1 “Wakati huo, makutano walipokutanika elfu elfu, hata wakakanyagana, alianza kuwaambia wanafunzi wake kwanza, Jilindeni na chachu ya Mafarisayo, ambayo ni unafiki.”

 

Waebrania 4:14-15 “Basi, iwapo tunaye kuhani mkuu aliyeingia katika mbingu, Yesu, Mwana wa Mungu, na tuyashike sana maungamo yetu. Kwa kuwa hamna kuhani mkuu asiyeweza kuchukuana nasi katika mambo yetu ya udhaifu; bali yeye alijaribiwa sawasawa na sisi katika mambo yote, bila kufanya dhambi.”

 

Waebrania 7:26-27 “Maana ilitupasa sisi tuwe na kuhani mkuu wa namna hii aliye mtakatifu, asiyekuwa na uovu, asiyekuwa na waa lo lote, aliyetengwa na wakosaji, aliyekuwa juu kuliko mbingu; ambaye hana haja kila siku, mfano wa wale makuhani wakuu wengine, kwanza kutoa dhabihu kwa ajili ya dhambi zake mwenyewe, kisha kwa ajili ya dhambi za hao watu; maana yeye alifanya hivi mara moja, alipojitoa nafsi yake.”

 

Tunajifunza nini kwamba Meza ya bwana inapaswa kuandaliwa kwa kutumia nyenzo ya mkate usiotiwa chachu, na sio hivyo tu sisis wenyewe ni lazima tuwe mbali na chachu yaani uovu au dhambi ya aina yoyote, wakati tunaandaa mkate usiotiwa chachu waamini wanapaswa kujiandaa kwa toba na kuhakikisha kuwa hawaishi maisha ya dhambi na unafiki na sio hivyo tu ni wakati wa kuhakikisha kuwa wanafunzi wa Yesu wanakaa katika kweli kwani chachu pia huwakilisha mafundisho ya uongo, mkate huo pia unapaswa kuwa mkate ambao unaweza kuvunjwa vunjwa kama vile watu wanavyokata kata keko au wanvyogawana kitu Fulani  kwa kufanya hivi tunaadhimisha na kutangaza mauti ya Bwana ambapo mwili wake ulisulubiwa na kuvunjwa vunjwa na kuharibiwa vibaya  na kutundikwa msalabani

 

Isaya 52: 13-14 “Tazama, mtumishi wangu atatenda kwa busara, atatukuzwa, na kuinuliwa juu, naye atakuwa juu sana. Kama vile wengi walivyokustaajabia, (uso wake ulikuwa umeharibiwa sana zaidi ya mtu ye yote, na umbo lake zaidi ya wanadamu),                   

 

-          Uzao wa mzabibu

Meza ya Bwana ina nyenzo kubwa mbili yaani mkate usiochachwa pamoja na kinywaji chake ambacho kimsingi kinapaswa kuwa mzao wa mzabibu, Marko 14:23-25 “Akatwaa kikombe, akashukuru, akawapa; wakakinywea wote.  Akawaambia, Hii ndiyo damu yangu ya agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi. Amin, nawaambia ninyi, Sitakunywa tena kabisa uzao wa mzabibu, hata siku ile nitakapounywa mpya katika ufalme wa Mungu.”

 

Kinywaji hicho kinachotumika yaani mzao wa Mzabibu ua juisi ya mzabibu ndio huwakilisha Damu ya Yesu

 

Mathayo 26:26-29 “Nao walipokuwa wakila Yesu alitwaa mkate, akabariki, akaumega, akawapa wanafunzi wake, akasema, Twaeni, mle; huu ndio mwili wangu  Akakitwaa kikombe, akashukuru, akawapa, akisema, Nyweni nyote katika hiki; kwa maana hii ndiyo damu yangu ya agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi kwa ondoleo la dhambi. Lakini nawaambieni, Sitakunywa kabisa tangu sasa uzao huu wa mzabibu, hata siku ile nitakapokunywa mpya pamoja nanyi katika ufalme wa Baba yangu.”

 

Luka 22:17-20 “Akapokea kikombe, akashukuru, akasema, Twaeni hiki, mgawanye ninyi kwa ninyi; Maana nawaambia ya kwamba tangu sasa sinywi mazao ya mzabibu hata ufalme wa Mungu utakapokuja. Akatwaa mkate, akashukuru, akaumega, akawapa, akisema, [Huu ndio mwili wangu unaotolewa kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu. Kikombe nacho vivyo hivyo baada ya kula; akisema, Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu, inayomwagika kwa ajili yenu.]

 

Kinywaji hiki kinawakilisha Damu ya Yesu iliyomwagika pale Msalabani ambayo ni takatifu sana, ni kinywaji ambacho   kilitokana na mzao wa mzabibu, Katika misingi ileile ya kuwa Yesu hakuwa na chachu kinywaji hiki vilevile hakipaswi kuwa kinywaji kilichochachwa yaani chenye pombe, “Fermented grape juice” na badala yake inapaswa kuwa ni juisi ya mzabibu isisyochachwa “Unfermented grape juice” kwa hiyo ni lazima iwe juice ya Mzabibu ambayo hajachachwa au isiyo na kilevi na mtu anaweza kuuliza swali kwanini iwe juisi ya mzabibu na sio kitu kingine kama chungwa, mambibo na kadhalika nii ni kwa sababu Yesu anaitwa katika maandiko Mzabibu wa kweli  Yohana 15:1 “Mimi ndimi mzabibu wa kweli, na Baba yangu ndiye mkulima.”

 

Yesu anaitwa Mzabibu wa kweli kwa sababu alizaa matunda ya haki, tofauti na wana wa Israelambao Mungu aliwapanda kama mche mzuri wa mzabibu kutoka Misri na kuwaweka katika nchi ya Mkanaani na badala yake wakazaa zabibu mwitu  Zaburi 80:8 “Ulileta mzabibu kutoka Misri, Ukawafukuza mataifa ukaupanda.”

 

Isaya 5:1-7 “Na nimwimbie mpenzi wangu wimbo wa mpenzi wangu katika habari za shamba lake la mizabibu. Mpenzi wangu alikuwa na shamba la mizabibu, Kilimani penye kuzaa sana; Akafanya handaki kulizunguka pande zote, Akatoa mawe yake, Akapanda ndani yake mzabibu ulio mzuri, Akajenga mnara katikati yake, Akachimba shinikizo ndani yake; Akatumaini ya kuwa utazaa zabibu, Nao ukazaa zabibu-mwitu. Na sasa, enyi wenyeji wa Yerusalemu, nanyi watu wa Yuda, amueni, nawasihi, kati ya mimi na shamba langu la mizabibu. Je! Ni kazi gani iliyoweza kutendeka ndani ya shamba langu la mizabibu nisiyoitenda? Basi, nilipotumaini ya kuwa litazaa zabibu, mbona lilizaa zabibu-mwitu? Haya basi, sasa nitawaambieni nitakalolitenda shamba langu la mizabibu; nitaondoa kitalu chake, nalo litaliwa; nitabomoa ukuta wake, nalo litakanyagwa; nami nitaliharibu; wala halitapogolewa wala kulimwa, bali litamea mbigili na miiba; nami nitayaamuru mawingu yasinyeshe mvua juu yake. Kwa maana shamba la mizabibu la Bwana wa majeshi ndilo nyumba ya Israeli, na watu wa Yuda ni mche wake wa kupendeza; akatumaini kuona hukumu ya haki, na kumbe! Aliona dhuluma; alitumaini kuona haki, na kumbe! Alisikia kilio.”

 

Kwa msingi huo washiriki wa meza ya bwana wanapoandaa juisi ya mzabibu isiyochachwa, wanapaswa vilevile kuiandaa mioyo yao kumzalia Bwana matunda halisi na sio zabibu mwitu.

Maana ya kiroho ya meza ya Bwana!

Meza ya Bwana inatangaza mauti ya Bwana na ushindi wake huku ikitukumbusha kuwa Kristo atakuja tena, na kwa sababu hiyo inafanya kazi ya kutukumbusha ukombozi wetu kupitia kazi nzima iliyofanyika pale msalabani na wajibu wetu wa kuishi maisha yanayompendeza, kimsingi ni kama wana wa Israel wanavyoikumbuka Pasaka wakiadhimisha kuokolewa kwao katika nchi ya Misri na kupelekwa katika inchi ya Kanaani, Meza ya bwana ni kama kambi ya kujikumbusha namna tunapaswa kujitafakari na kuangalia safari yetu kwa kudumisha ushirika na Yesu ili tusije tukawa watu wa kukataliwa

1Wakorintho 10:1-21. “Kwa maana, ndugu zangu, sipendi mkose kufahamu ya kuwa baba zetu walikuwa wote chini ya wingu; wote wakapita kati ya bahari; wote wakabatizwa wawe wa Musa katika wingu na katika bahari; wote wakala chakula kile kile cha roho; wote wakanywa kinywaji kile kile cha roho; kwa maana waliunywea mwamba wa roho uliowafuata; na mwamba ule ulikuwa ni Kristo. Lakini wengi sana katika wao, Mungu hakupendezwa nao; maana waliangamizwa jangwani. Basi mambo hayo yalikuwa mifano kwetu, kusudi sisi tusiwe watu wa kutamani mabaya, kama wale nao walivyotamani. Wala msiwe waabudu sanamu, kama wengine wao walivyokuwa; kama ilivyoandikwa, Watu waliketi kula na kunywa, kisha wakasimama wacheze. Wala msifanye uasherati, kama wengine wao walivyofanya, wakaanguka siku moja watu ishirini na tatu elfu. Wala tusimjaribu Bwana, kama wengine wao walivyomjaribu, wakaharibiwa na nyoka. Wala msinung'unike, kama wengine wao walivyonung'unika, wakaharibiwa na mharabu. Basi mambo hayo yaliwapata wao kwa jinsi ya mifano, yakaandikwa ili kutuonya sisi, tuliofikiliwa na miisho ya zamani. Kwa hiyo anayejidhania kuwa amesimama na aangalie asianguke. Jaribu halikuwapata ninyi, isipokuwa lililo kawaida ya wanadamu; ila Mungu ni mwaminifu; ambaye hatawaacha mjaribiwe kupita mwezavyo; lakini pamoja na lile jaribu atafanya na mlango wa kutokea, ili mweze kustahimili. Kwa ajili ya hayo, wapenzi wangu, ikimbieni ibada ya sanamu. Nasema kama na watu wenye akili; lifikirini ninyi ninenalo. Kikombe kile cha baraka tukibarikicho, je! Si ushirika wa damu ya Kristo? Mkate ule tuumegao, si ushirika wa mwili wa Kristo? Kwa kuwa mkate ni mmoja, sisi tulio wengi tu mwili mmoja; kwa maana sisi sote twapokea sehemu ya ule mkate mmoja. Waangalieni hao Waisraeli walivyokuwa kwa jinsi ya mwili; wale wazilao dhabihu, je! Hawana shirika na madhabahu? Basi niseme nini? Ya kwamba kile kilichotolewa sadaka kwa sanamu ni kitu? Au ya kwamba sanamu ni kitu? Sivyo, lakini vitu vile wavitoavyo sadaka wavitoa kwa mashetani, wala si kwa Mungu; nami sipendi ninyi kushirikiana na mashetani. Hamwezi kunywea kikombe cha Bwana na kikombe cha mashetani. Hamwezi kushirikiana katika meza ya Bwana na katika meza ya mashetani.” 

Wakati wa kushiriki Meza ya bwana ni wakati wa kujitathimini kama wana wa Israel tumeambiwa sio wote waliingia Kanaani, ni wajati wa kujikumbushankuimarisha uhusiano wetu na Bwana wetu Yesu Kristo, hivyo ni wakati wa kujitafakari na kujikagua  na kuweka maazimio mapya ya kurudi na kukaa katika uwepo wa Bwana

Faida Nyingine za kushiriki Meza ya Bwana !

Ni muhimu kufahamu kuwa katika meza ya Bwana kuna faida nyingi sana za kiwmili na kiroho, tunaposhiriki kinywaji kile na mkate ule na kutangaza mauti ya Bwana na kujiandaa kwaajili ya ujio wake mwili wake ulisulubiwa kwaajili yetu na hivyo kuna nguvu kubwa sana ya uponyaji, Meza ya bwana ni tangazo la aina ya mauti aliyiokufa Kristo na alikuwa kwaajili yetu na hivyo tunaposhiriki inakuwa sawa kabisa na kusema kwa kupigwa kwake sisi tumepona

Isaya 53:2-5 “Maana alikua mbele zake kama mche mwororo, Na kama mzizi katika nchi kavu; Yeye hana umbo wala uzuri; Na tumwonapo hana uzuri hata tumtamani. Alidharauliwa na kukataliwa na watu; Mtu wa huzuni nyingi, ajuaye sikitiko; Na kama mtu ambaye watu humficha nyuso zao, Alidharauliwa wala hatukumhesabu kuwa kitu. Hakika ameyachukua masikitiko yetu, Amejitwika huzuni zetu; Lakini tulimdhania ya kuwa amepigwa, Amepigwa na Mungu, na kuteswa. Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, Alichubuliwa kwa maovu yetu; Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona.”

1Petro 2:21-25 “Kwa sababu ndio mlioitiwa; maana Kristo naye aliteswa kwa ajili yenu, akawaachia kielelezo, mfuate nyayo zake. Yeye hakutenda dhambi, wala hila haikuonekana kinywani mwake. Yeye alipotukanwa, hakurudisha matukano; alipoteswa, hakuogofya; bali alijikabidhi kwake yeye ahukumuye kwa haki. Yeye mwenyewe alizichukua dhambi zetu katika mwili wake juu ya mti, tukiwa wafu kwa mambo ya dhambi, tuwe hai kwa mambo ya haki; na kwa kupigwa kwake mliponywa. Kwa maana mlikuwa mnapotea kama kondoo; lakini sasa mmemrudia Mchungaji na Mwangalizi wa roho zenu.”

Waebrania 13:12-13. “Kwa ajili hii Yesu naye, ili awatakase watu kwa damu yake mwenyewe, aliteswa nje ya lango. Basi na tutoke tumwendee nje ya kambi, tukichukua shutumu lake.”   

Damu yake Yesu inatupa utakaso, magonjwa yetu na madhaifu yetu yanaponywa, Roho zetu zimaimarika, ushirika wetu na Kristo unaimarika, tunapata nafasi ya kumuabudu Yesu katika roho na kweli, tunaweka mbali chachu zote, tunaanza upya safari ya kujihakikishia kuwa tunaushirika na Kristo na tunaenda mbinguni, tunaishi maisha ya utakatifu na kufungua mlango wa Baraka, wagonjwa ambao hawajaponywa katika maombezi ya kawaida hupokea uponyaji kupitia meza ya Bwana hivyo kuna faida za kimwili na kiroho.

Hasara ya kushiriki Meza ya Bwana isivyostahili

Tunaposhiriki meza ya Bwana inatupasa kudhamiria kuacha dhambi. Yaani kuwa mbali na chachu, Sasa tunaposhiriki na  uovu au tukiwa na nia ya kutokuachana na dhambi basi tunapata adhabu kali kwani tunakuwa tumeidharau kazi ya Mungu iliyofanyika Msalabani na tunaweza kupata adhabu

  Waebrania 10:28-29 “Mtu aliyeidharau sheria ya Musa hufa pasipo huruma, kwa neno la mashahidi wawili au watatu. Mwaonaje? Haikumpasa adhabu iliyo kubwa zaidi mtu yule aliyemkanyaga Mwana wa Mungu, na kuihesabu damu ya agano aliyotakaswa kwayo kuwa ni kitu ovyo, na kumfanyia jeuri Roho wa neema?            

Hivyo adhabu hiyo huanzia duniani na hata inaweza kutupeleka Jehanamu milele japo lengo la adhabu hii ya Mungu ni ili mwili wako uadhibiwe utubu na uweze kwenda mbinguni.

Pia tumaweza kuugua magonjwa yasiyoponyeka hata kama tunaombewa namna gani hatuna uponyaji. Pia tunaweza kufa kabisa kwa msingi huo inatupasa kujihoji kwanza kabla ya kushiriki. 1Wakoritho 11: 22-32 “kwa maana kila mmoja hutangulia kutwaa chakula chake katika kule kula; hata huyu ana njaa, na huyu amelewa. Je! Hamna nyumba za kulia na kunywea? Au mnalidharau kanisa la Mungu, na kuwatahayarisha hao wasio na kitu? Niwaambieni? Niwasifu? La! Siwasifu kwa ajili ya hayo. Kwa maana mimi nalipokea kwa Bwana niliyowapa nanyi, ya kuwa Bwana Yesu usiku ule aliotolewa alitwaa mkate, naye akiisha kushukuru akaumega, akasema, Huu ndio mwili wangu ulio kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu. Na vivi hivi baada ya kula akakitwaa kikombe, akisema, Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu; fanyeni hivi kila mnywapo, kwa ukumbusho wangu. Maana kila mwulapo mkate huu na kukinywea kikombe hiki, mwaitangaza mauti ya Bwana hata ajapo. Basi kila aulaye mkate huo, au kukinywea kikombe hicho cha Bwana isivyostahili, atakuwa amejipatia hatia ya mwili na damu ya Bwana. Lakini mtu ajihoji mwenyewe, na hivyo aule mkate, na kukinywea kikombe. Maana alaye na kunywa, hula na kunywa hukumu ya nafsi yake, kwa kutokuupambanua ule mwili. Kwa sababu hiyo wako wengi kwenu walio hawawezi na dhaifu, na watu kadha wa kadha wamelala. Lakini kama tungejipambanua nafsi zetu, tusingehukumiwa. Ila tuhukumiwapo, twarudiwa na Bwana, isije ikatupasa adhabu pamoja na dunia.”

Kushiriki mmeza ya Bwana isivyostahili na ukapata adhabu maana yake ni kuwa ugonjwa utakaotokana na adhabu ya kushiriki meza ya bwana isivyostahili hauwezi kupona kwa tabibu awaye yote wala maombezi ya muhubiri yeyote kwanini kwa sababu ni mtu anaadhibiwa na Bwana

Mambo yasiyo ya Kibiblia yanayihusiana na meza ya Bwana!

Madai ya mkate na Juisi ya Mzabibu kugeka kuwa mwili na Damu ya Yesu halisi baada ya kubarikiwa hayo ni mafundisho ya uongo kwani tendo hilo ni ukumbusho tu, hivyo mkate hubakia vile vile na juisi ya mzabibu pia huwa vile vile na havuiwezi kugeuka kuwa Damu au mwili halisi wa Bwana Yesu bali nguvu za Mungu za uponyaji wa mwili nafsi na roho huambatana na meza ya Bwana.

-          Juisi ya mzabibu kunywewa na Mchungaji  tu kwa niaba ya wote  Hii sio kibiblia kwani  watu wote Wanaume kwa wanawake  wanapaswa kushiriki na sio  mmoja kumiminiwa  kombe  lote  mtu mmoja peke yake Kumbuka kuwa viko vifaa maalumu vinavyoweza kutumika kugawanya juice ya mzabibu na kuigawa mikate hiyo iliyobarikiwa kwa kila mshirika mwenye sifa ya kushiriki meza ya Bwana  Mathayo 26:27 “Akakitwaa kikombe, akashukuru, akawapa, akisema, Nyweni nyote katika hiki;” Marko 14:23 “Akatwaa kikombe, akashukuru, akawapa; wakakinywea wote.”

 

-          Kutawadhana kwa maji na kufutana miguu kabla ya kushiriki meza ya Bwana huu pia ni upotovu:  watu hawa hutumia maandiko ya Yohana 13: 2-12 “Kisha akatia maji katika bakuli, akaanza kuwatawadha wanafunzi miguu, na kuifuta kwa kile kitambaa alichojifunga. Hivyo yuaja kwa Simoni Petro. Huyo akamwambia, Bwana! Wewe wanitawadha miguu mimi? Yesu akajibu, akamwambia, Nifanyalo wewe hujui sasa; lakini utalifahamu baadaye. Petro akamwambia, Wewe hutanitawadha miguu kamwe. Yesu akamwambia, Kama nisipokutawadha, huna shirika nami. Simoni Petro akamwambia, Bwana, si miguu yangu tu, hata na mikono yangu na kichwa changu pia. Yesu akamwambia, Yeye aliyekwisha kuoga hana haja ila ya kutawadha miguu, bali yu safi mwili wote; nanyi mmekuwa safi, lakini si nyote. Kwa maana alimjua yeye atakayemsaliti; ndiyo maana alisema, Si nyote mlio safi. Basi alipokwisha kuwatawadha miguu, na kuyatwaa mavazi yake, na kuketi tena, akawaambia, Je! Mmeelewa na hayo niliyowatendea?

 

Hatuna budi kufahamu kuwa Yesu alitumia mifano na mifano ya kinadharia na vitendo katika, kuwafundisha wanafunzi wake kama Mwalimu na hapo alikuwa akifundisha kuhusu kuwa mkubwa katika ufalme wa Mungu anapaswa mtumwa wa watu wote na kufanya kazi ya kitumwa nay a chini Zaidi kama kutawadha miguu, hivyo kama unataka kufundisha somo hilo kiitendo ni vema kufanya siku tofauti na hakuna ulazima wa nkuifanya kwenye meza ya bwana na kufanya ibada kuwa ndefu na zenye kuchosha Yesu alitumia mfano huo wa kutawadha wanafunzi wake miguu kwa sababu walikuwa na mawazo ya ukubwa badala ya utumishi

 

Luka 22:24-27 “Yakatokea mashindano kati yao, kwamba ni nani anayehesabiwa kuwa mkubwa. Akawaambia, Wafalme wa Mataifa huwatawala, na wenye mamlaka juu yao huitwa Wenye fadhili; lakini kwenu ninyi sivyo; bali aliye mkubwa kwenu na awe kama aliye mdogo; na mwenye kuongoza kama yule atumikaye.Maana aliye mkubwa ni yupi? Yeye aketiye chakulani, au yule atumikaye? Siye yule aketiye chakulani? Lakini mimi kati yenu ni kama atumikaye.”     

 

Hapo alikuwa anawafundisha kunyenyekea maana kulikuwa na migongano ya kugombea ukubwa.  Sasa kitendo cha Yesu kuwatawadha miguu kilikuwa ni kitendo kinacho fanywa na mtumwa au mdogo kwa yule aliyemkubwa

 

Mwanzo 24:31-32 “Akasema, Karibu, wewe uliyebarikiwa na BWANA, mbona unasimama nje? Kwa maana nimeiweka nyumba tayari, na nafasi kwa ngamia. Na mtu yule akaingia katika nyumba, akawafungua ngamia; naye akatoa majani na malisho kwa ngamia, na maji ya kuoshea miguu yake, na miguu ya watu waliokuwa pamoja naye.”

 

1Samuel 25:41 “Naye akainuka na kujiinamisha kifulifuli mpaka nchi, akasema, Tazama, mjakazi wako ni mtumwa wa kuwaosha miguu watumishi wa bwana wangu.”

           

kwa msingi huo Yesu  alikuwa  akiwafundisha unyenyekevu na kitendo chake cha kuwaosha miguu wanafunzi wake kilikuwa ni ishara ya kuchukua nafasi ya chini ya utumwa na kujishusha akichukua nafasi ya chini. Wafilipi 2:3-11 “Msitende neno lo lote kwa kushindana wala kwa majivuno; bali kwa unyenyekevu, kila mtu na amhesabu mwenziwe kuwa bora kuliko nafsi yake. Kila mtu asiangalie mambo yake mwenyewe, bali kila mtu aangalie mambo ya wengine. Iweni na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo Yesu; ambaye yeye mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu;tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba. Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina; ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi; na kila ulimi ukiri ya kuwa YESU KRISTO NI BWANA, kwa utukufu wa Mungu Baba.

 

Kwa hiyo kimsingi tukio la kutawadha miguu haikuwa sehemu ya ibada ya meza ya Bwana bali ilikuwa ni fundisho kuhusu nafasi ya juu katika utawala wa Mungu inapatikana kwa kujishusha na kuwa mtumwa wa watu, Hatupaswi kufikiri kuwa kuna ulazima wa kutawadha miguu watu wakati tunapotaka kushiriki meza ya Bwana asomaye na afahamu

Hitimisho:

Utaratibu wa kufuatwa wakati wa kushiriki meza ya Bwana.

Kuhani ataombea mkate kwanza

-          Mkate – Baada ya maombi  ya shukrani  kwa kazi ya ukombozi aliyoifanya Yesu msalabani kufanyika  na  Baraka  kisha watu wanafunzi  humegewa vipande  vipande na kupewa mkononi na kupata nafasi ya kujiombea 

 

-          1Wakorintho 11:24 “naye akiisha kushukuru akaumega, akasema, Huu ndio mwili wangu ulio kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu.”

 

Kuhani ataombea vikombe vya juisi ya mzabibu pia

-           Kikombe Baada ya Maombi yashukrani kwa kazi ya ukombozi aliyoifanya Yesu Msalabani na Baraka watu wanaweza kunywa katika kikombe kimoja au kugawanjwa katika vikombe vidogo vidogo na kila mtu kushiriki kikombe chake.

 

-           1Wakorintho 11:25 “Na vivi hivi baada ya kula akakitwaa kikombe, akisema, Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu; fanyeni hivi kila mnywapo, kwa ukumbusho wangu.”

 

Mratibu wa ibada ya meza ya Bwana anaweza vilevile kutumia maandiko mengineyo yanayohusiana na meza ya Bwana na wakashiriki na watu wake, kama Kanisa halijafundishwa somo kama hili unaweza kuhubiri au kufundisha kwa ufupia kuhusiana na meza ya bwana na kisha mkashiriki, kama wameshajifunza somo kama hili basi ufikapo wakati wa ibada ya meza ya bwana unaweza tu kuendelea kwa kusoma andiko na kubariki vifaa vya kiroho vya meza ya bwana na kisha watu wakashiriki, watu wanaweza kupata nafasi ya kuomba na kuombeana au hata kusalimiana na kutiana moyo kwa dakika chache wakati wa kushirikiana katika meza ya Bwana

Na Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni