Jumapili, 18 Februari 2024

Neema ya Mungu na mwaliko wa maadui!


Mwanzo 26:12-16 “Isaka akapanda mbegu katika nchi ile, akapata mwaka ule vipimo mia kwa kimoja, BWANA akambariki. Na mtu huyu akawa mkuu, akazidi kusitawi, hata akawa mkuu sana. Akawa na mali ya kondoo, na mali ya ng'ombe, na watumwa wengi. Hao Wafilisti wakamhusudu. Na vile visima vyote walivyochimba watumwa wa baba yake, siku za Ibrahimu babaye, Wafilisti walikuwa wamevifukia, wakavijaza kifusi. Abimeleki akamwambia Isaka, Utoke kwetu, maana wewe una nguvu sana kuliko sisi.”


 

 

Naliweka wakfu somo hili kwa heshima ya Hayati Edward Ngoyai Lowassa waziri mkuu wa zamani wa Tanzania kwani somo hili liliandaliwa siku ambayo yeye alikuwa anazikwa.

 

Utangulizi:

Ni Muhimu kufahamu kuwa wakati mwingine vita na mapito tunayoyapitia kutoka kwa watu yanatokana na neema ya Mungu iliyoko juu yetu, Mungu anapokupa kibali na baraka mbalimbali Baraka hizo au neema hiyo hualika maadui!

Wakati Isaka alipokaa Gerari kwa sababu ya njaa iliyotokea mashariki ya kati, kwa agizo la Mungu, Mungu alimbariki sana Isaka, Mazao yake na mifugo yake iliongezeka sana kiasi ambacho wafilisti walijawa na wivu wenye uchungu!

Maandiko yanaeleza wazi kwamba wafilisti wakamhusudu! Neno Kuhusudu linalotumika hapo katika kiebrania linatumika neno Qana  mbalo maana yake ni Jealous au Zealous in a bad sense kiswahili fasaha wivu wenye uchungu  

Yakobo 3:14-16 “Lakini, mkiwa na wivu wenye uchungu na ugomvi mioyoni mwenu, msijisifu, wala msiseme uongo juu ya kweli. Hekima hiyo siyo ile ishukayo kutoka juu, bali ni ya dunia, ya tabia ya kibinadamu, na Shetani. Maana hapo palipo wivu na ugomvi ndipo palipo machafuko, na kila tendo baya.”

Kwaajili ya wivu wenye uchungu, waliharibu visima alivyokuwa anatumia Isaka, Visima hivi vilichimbwa na Ibrahimu baba yake miaka ya uhai wake, na visima hivi vilikuwa ndio chanzo cha mfumo wa umwagiliaji na unyweshaji wa mifugo, na pasipo visima hivyo ni ngumu kuendesha shughuli za kilimo na ufugaji hususani wakati wa ukame, kwa hiyo wafilisti walikusudia kumuharibu Isaka na walikusudia kuharibi kabisa vyanzo vya Baraka zake, na walipoona majaribio yao yanashindikana mwisho wakamwambia atoke kwao, na bila aibu walimweleza sababu kwanini aende

Mwanzo 26:16 “Abimeleki akamwambia Isaka, Utoke kwetu, maana wewe una nguvu sana kuliko sisikwa nini walifanya hivyo Neema ya Mungu ilikuwa juu ya Isaka, alibarikiwa sana Mungu alimpa akili ya kupata utajiri, familia yao walikuwa na ujuzi wa elimu ya umwagiliaji, na ujuzi wa kuchimba visima hata kujua sehemu zenye maji, Jambo hili liliwapelekea Wafilisti kujawa na wivu wenye uchungu kwaajili ya maisha ya Isaka,  Neema ya Mungu inapokuwa juu yako na akaweka mkono wake kukubariki, ukawa na Nguvu, ukawa na bidii ya kazi, ukawa na fedha, ukawa na ndoa nzuri, ukawa na watoto wenye mafanikio, ukawa na afya nzuri ukastawi pande zote, ukawa na ustawi wa mwili nafsi na roho, hata hali yako ya kiroho ikiwa vizuri, Shetani na majeshi yake ya pepo wabaya pamoja na watu wabaya wataanza kukuonea wivu wenye uchungu, watu wataanza kukuchukia pasipo sababu , kwanini kwa sababu ya neema ya Mungu iliyo juu yako inayokuletea Baraka !

Kwa hiyo ni Lazima uelewe kama wewe ni mtu mkubwa ndani, Mungu ameweka mkono wake juu yako, Mungu amekupa kibali, na Baraka zake zikaanza kumiminika juu yako, Adui hatalala usingizi, hataketi na kukuacha ufurahie Baraka za Mungu kwa Amani, ataanza kuchochea shida na taabu. Leo basi tutachukua muda kujifunza somo hili Neema ya Mungu na Mwaliko wa Maadui kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-

 

·         Mifano ya watu waliopata Neema ya Mungu na kusababisha kuwa na Maadui

·         Neema ya Mungu na mwaliko wa maadui

·         Ushauri kutoka kwa Mungu  

 

Mifano ya watu waliopata Neema ya Mungu na kusababisha kuwa na Maadui

Neno la Mungu limejaa mifano ya watu waliopewa neema ya Mungu katika maisha yao na badala ya kupendwa na watu, watu waliwachukia na kuwawashia moto, na kuwategea mitego ya aina mbalimbali kuhakikisha kuwa wanakwama katika kila eneo la Maisha yao na ikiwezekana vyanzo vya Baraka zao kuharibiwa!

1.       Alichukiwa kwa sababu ya ndoto kubwa na maono makubwa aliyokuwa nayo – Yusufu angalia katika Mwanzo 37:2-11 “Hivi ndivyo vizazi vya Yakobo. Yusufu, aliyekuwa mwenye miaka kumi na saba, alikuwa akichunga kondoo pamoja na ndugu zake; naye alikuwa kijana pamoja na wana wa Bilha, na wana wa Zilpa, wake wa baba yake. Yusufu akamletea baba yao habari zao mbaya. Basi Israeli akampenda Yusufu kuliko wanawe wote, maana ni mwana wa uzee wake, akamfanyia kanzu ndefu. Ndugu zake wakaona ya kuwa baba yao anampenda kuliko ndugu zake wote, wakamchukia, wala hawakuweza kusema naye kwa amani. Yusufu akaota ndoto, akawapa ndugu zake habari, nao wakazidi kumchukia; akawaambia, Tafadhalini, sikieni ndoto hii niliyoiota. Tazama, sisi tulikuwa tukifunga miganda shambani, kumbe! Mganda wangu ukaondoka ukasimama, na tazama, miganda yenu ikazunguka ikainama mbele ya mganda wangu. Ndugu zake wakamwambia, Je! Kweli wewe utatumiliki sisi? Nawe utatutawala sisi? Wakazidi kumchukia kwa ajili ya ndoto yake, na kwa maneno yake. Akaota tena ndoto nyingine, akawaambia ndugu zake, akasema, Angalieni, nimeota ndoto nyingine; na tazama, jua na mwezi na nyota kumi na moja zikaniinamia. Akawaambia baba yake na ndugu zake; baba yake akamkemea akamwambia, Ni ndoto gani hii uliyoiota? Je! Mimi na mama yako na ndugu zako tutakuja tukusujudie hata nchi? Ndugu zake wakamhusudu; bali baba yake akalihifadhi neno hili.”

 

Yusufu alipata neema kutoka kwa Mungu, neema hii ilimfanya apate upendeleo kutoka kwa baba yake, lakini nduguze walimchukia sana na Mungu akasema na Yusufu kwa habari ya Maisha yake ya baadaye kwa njia ya Ndoto, Jambo hili lilipelekea nduguze wamchukie zaidi na hata baadaye walikusudia kumuua,  kumbuka hapo Ndoto zilikuwa hazijatimia, lilikuwa ni ujumbe tu kutoka kwa Mungu, watu wenye maono makubwa huchukiwa, Kimsingi kupitia kisa hiki wako watu wanasema usimweleze mtu maono yako eti ufiche, kutokana na kisa hiki, Lakini, Mungu hanaga tabia ya kuficha maono yake, huwa anaweka wazi, serikali huwa haifichi mipango yake huwa inawekwa wazi, vyama huwa havifichi sera zake huwa wanazinadi, kuficha maono ni woga, Mipango ya Mungu ya kumuokoa mwanadamu, kuja kwa masihi iliwekwa wazi zamani sana Mungu mwenyewe aliiweka wazi, kwa hiyo ukiona mpango umewekwa wazi kisha haukutimia ujue huo haukuwa mpango wa Mungu, Mungu huweka wazi mipango yake na hakuna mtu anayeweza kusimama na kuzuia kusudi lake na ndio maana Ndoto ya Yusufu iliwekwa wazi na Ndugu zake walipigana nayo lakini ilikuja kutimia,.

 

Amosi 3:7 “Hakika Bwana MUNGU hatafanya neno lo lote, bila kuwafunulia watumishi wake manabii siri yake.”

 

Siri za Mungu huwekwa wazi kwa watumishi wake hata kabla Hazijatimizwa, sijui wanaofundisha ufiche siri zako wana maana gani, wanaogopa vita? wanaogopa maadui,? wanaogopa wachawi?  Mungu hana cha kuogopa yeye anaweka wazi mambo yake na ndivyo alivyofanya kwa Yusufu, Mungu alitangaza atakachomfanyia Yusufu hata kabla havijafanyika ni Mungu Bora anatangaza Mwisho tangu mwanzo !

 

Isaya 46:9-10 “Kumbukeni mambo ya zamani za kale; maana mimi ni Mungu, wala hapana mwingine; mimi ni Mungu, wala hapana aliye kama mimi; nitangazaye mwisho tangu mwanzo, na tangu zamani za kale mambo yasiyotendeka bado; nikisema, Shauri langu litasimama, nami nitatenda mapenzi yangu yote

 

Mungu haogopi kutangaza mpango wake, na hakuna anayeweza kuzuia mapenzi yake, yanayoweza kuzuiwa ni mapenzi ya wanadamu tu, lakini ya Mungu hayazuiliki, kusudi la Mungu ni lazima lisimame, kwa hiyo uweke wazi usiweke wazi, Neema ya Mungu ikiwa juu yako ndani yako kukiwa kuna kitu cha ziada ndani yako basi ni lazima kitaalika maadui bila kujali kuwa kimesemwa au hakikusema kitaalika maadui tu na hii ni kwa sababu gani ni kwa sababu ya wivu wenye uchungu! Walionao wanadamu kwa uzito wa maono yako.

 

2.       Alichukiwa kwa sababu ya Upako wa kifalme na uwezo mkubwa aliokuwa nao – Daudi  - angalia katika

1Samuel 18: 6-9 “Hata ikawa, walipokuwa wakienda, hapo Daudi aliporudi baada ya kumwua yule Mfilisti, wanawake wakatoka katika miji yote ya Israeli, kwa kuimba na kucheza, ili kumlaki mfalme Sauli; wakatoka na matari, na shangwe, na vinanda. Nao wale wanawake wakaitikiana wakicheza, wakasema, Sauli amewaua elfu zake, Na Daudi makumi elfu yake. Basi Sauli akaghadhibika sana, na maneno haya yakamchukiza; akasema, Wamempa Daudi makumi elfu, na mimi wamenipa elfu tu; kuna nini tena awezayo kupata, isipokuwa ni ufalme? Sauli akamwonea Daudi wivu tangu siku ile.”

 

Daudi alikuwa amepakwa mafuta ya ufalme kichwani pake, lakini Muda wake ulikuwa bado haujawadia, hata hivyo uweza wa kifalme ulitenda kazi ndani yake kwa kiwango kikubwa sana alimpiga mfilisti na kujipatia umaarufu mwingi sana  kwa sababu ya upako na uweza wa Mungu uliokuwa juu yake, Angalia kuwa mfalme aliyekuwepo madarakani alianza kumpiga vita, alitaka kumuua mara kadhaa kwa sababu alijua kuwa bila shaka ndiye atakayekuwa mfalme, Mungu anapoweka ukubwa wowote ndani yako, hata kama wakati wake bado watainuka wenye ukubwa kama wako watakupiga vita, hii ni kwa sababu hawafurahii wewe uwe kama wao, hata unapotenda kwa busara ukiwa chini yao wanaogopa wanadhani ni ile hali yako ya ukubwa inawaelemea, wanaweza kukuwinda, wanaweza kukuwekea sumu, wanaweza kukusudia kukutendea mabaya wanapigwa upofu kwa sababu ya nini Neema ya Mungu ya ukubwa wako inawatesa na kualika uadui, angalia Daudi alikuwa na Adui ambaye ni Mfalme Sauli hivyo Sauli alikusudia kumuua Daudi, Hata hivyo ukubwa wa Daudi usingeweza kuharibiwa kwa sababu Mungu alikusudia lakini wote tunaelewa jinsi Sauli alivyosababisha maisha ya Daudi kuwa magumu sana akikimbia huku na kule katika mapango na majabali na nyika  kujificha na kuhami uhai wake kwaajili ya wivu wenye uchungu wa Sauli.

 

3.       Alichukiwa kwa sababu hawakuweza kushindana na Hekima iliyokuwa juu yake – Stefano angalia katika

 

Matendo 6:8-10 “Na Stefano, akijaa neema na uwezo, alikuwa akifanya maajabu na ishara kubwa katika watu.Lakini baadhi ya watu wa sinagogi lililoitwa sinagogi la Mahuru, na la Wakirene, na la Waiskanderia, na la wale wa Kilikia na Asia, wakaondoka na kujadiliana na Stefano; lakini hawakuweza kushindana na hiyo hekima na huyo Roho aliyesema naye.”

 

Roho Mtakatifu alikuwa amempaka mafuta Stefano, uweza wa Mungu ulikuwa juu yake akitumiwa na Mungu kufanya ishara na miujiza mikubwa, lakini sio hivyo tu kichwani alikuwa yuko vizuri, alikuwa na ujuzi wa maandiko na neno la Mungu lilikuwa limejaa, watu wa masinagogi kama matano hivi  walikuja kujadiliana naye lakini hawakumuweza kwa sababu alikuwa na hekima ya kupita kawaida na Roho wa Mungu alisema naye, tunajifunza hapa sio mali tu, sio cheo tu hata hekima na uwepo wa Mungu unaoubeba unavutia maadui, wanachukizwa na hali yako ya kiroho, wanatamani uchafuke, uonekane ulikuwa mtu mbaya hufai, wewe ni kama kirusi tu, unatengenezewa skendo adui zako wanatamani wapate sababu mbaya za kukuharibia walifanya hivyo kwa Stefano watafanya hivyo na kwako bila kujali kuwa ni walokole wenzako au la angalia walitafuta kumchafua Stefano kwa sababu za kizushi

 

Matendo 6:11 - 14 “Hata wakashawishi watu waliosema, Tumemsikia mtu huyu akinena maneno ya kumtukana Musa na Mungu. Wakawataharakisha watu na wazee na waandishi, wakamwendea, wakamkamata, wakampeleka mbele ya baraza. Wakasimamisha mashahidi wa uongo waliosema, Mtu huyu haachi kusema maneno ya kufuru juu ya mahali hapa patakatifu na juu ya torati; maana tumemsikia akisema kwamba Yesu huyo Mnazareti atapaharibu mahali hapa, na kuzibadili desturi tulizopewa na Musa.”

 

Unaona? Hamkuwahi kuona watu wakichafuliwa, hamkuwahi kuona watu wakizushiwa maneno ya uongo katika jamii? Hamkuwahi kuona wakiitwa mafisadi, kumbe ni kwaajili ya wivu wenye uchungu kutoka kwa maadui, watu wanachukizwa na utajiri ulio nao, wanachukizwa na Neema ya Mungu iliyoko juu yako, wanachukizwa na Mali alizokupa Mungu wanachukizwa na ndoto zako, wanachukizwa na uchungu na uzalendo na msimamo wako wa dhati na uzalendo kwa watu wako lakini pia wanachukizwa na Hekima iliyoko juu yako, akili kubwa uliyo nayo utendaji wako, uwajibikaji wako kazini na kadhalika ndivyo walivyomfanyia Stefano wakampiga kwa mawe na kumuua, wako watu wamedhurika na magonjwa, wamekufa vifo vyenye utata, wameumizwa mioyo si kwa sababu walikuwa na hatia bali kwa sababu ya watu wenye wivu, wivu wenye uchungu.

 

4.       Alichukiwa kwa sababu tu alikuwa mkweli – Mungu anapokupa neema ya kuwa mkweli Neema hiyo pia huwavutia maadui, Yohana mbatizaji alitiwa gerezani na kuuawa kwa sababu Mungu alimpa neema na ujasiri wa kusema kweli!

 

Marko 6:17-28 “Kwa maana Herode mwenyewe alikuwa ametuma watu, akamkamata Yohana, akamfunga gerezani, kwa ajili ya Herodia, mkewe Filipo ndugu yake, kwa kuwa amemwoa; kwa sababu Yohana alimwambia Herode, Si halali kwako kuwa na mke wa nduguyo. Naye yule Herodia akawa akimvizia, akataka kumwua, asipate. Maana Herode alimwogopa Yohana; akimjua kuwa ni mtu wa haki, mtakatifu, akamlinda; na alipokwisha kumsikiliza alifadhaika sana; naye alikuwa akimsikiliza kwa furaha. Hata ilipotokea siku ya kufaa, na Herode, sikukuu ya kuzaliwa kwake, alipowafanyia karamu wakubwa wake, na majemadari, na watu wenye cheo wa Galilaya; ndipo binti yake yule Herodia alipoingia, akacheza, akampendeza Herode na wale walioketi pamoja naye karamuni. Mfalme akamwambia yule kijana, Niombe lo lote utakalo, nitakupa. Akamwapia, Lo lote utakaloniomba nitakupa, hata nusu ya ufalme wangu. Basi akatoka, akamwuliza mamaye, Niombe nini? Naye akasema, Kichwa cha Yohana Mbatizaji. Mara akaingia kwa haraka mbele ya mfalme, akaomba akisema, Nataka unipe sasa hivi katika kombe kichwa cha Yohana Mbatizaji. Mfalme akafanya huzuni sana, lakini kwa ajili ya viapo vyake, na kwa ajili ya hao walioketi karamuni, hakutaka kumkatalia. Mara mfalme akatuma askari, akaamuru kuleta kichwa chake. Basi akaenda, akamkata kichwa mle gerezani, akakileta kichwa chake katika kombe, akampa yule kijana, naye yule kijana akampa mamaye.”

 

Yohana mbatizaji aliuawa kwa sababu alikuwa Msemakweli, kweli iligharimu maisha yake maandiko yanamtaja kuwa alikuwa mtu wa haki, alimkemea mfalme Herode kwa tendo la kuwa na mke wa ndugu yake, akaamua kumtia gerezani, lakini mwanamke alifanya njama ya kuhakikisha anauawa ili uovu wao uendelee, wakose mtu wa kuwakemea, hivi ndivyo dunia inavyotaka, dunia haitaki watu wa kweli, haitaki watu wa haki, haiitaji watu safi, kuwepo kwako kunawahukumu, hawafaidi maisha yao, ya dhambi, hawataki mtu awe  na kidomo domo watataka wakunyamazishe ili nao wapige, aliyekuambia dunia inataka wasema kweli ni nani hii ilimgharimu maisha ya nabii Yahaya au Yohana mbatizaji kama inenavyo injili

 

5.       Alichukiwa kwa sababu  kwa sababu ya husuda aliwazidi katika kila idara – Yesu alikuwa mwema alifanya kazi njema umati mkubwa wa watu ulimfuata walimuimbia hosanna mwana wa Daudi, ndiye mbarikiwa ajaye kwa jina Bwana

 

Mathayo 27:116-20 “Basi palikuwa na mfungwa mashuhuri siku zile, aitwaye Baraba. Basi walipokutanika, Pilato akawaambia, Mnataka niwafungulie yupi? Yule Baraba, au Yesu aitwaye Kristo? Kwa maana alijua ya kuwa wamemtoa kwa husuda. Na alipokuwa ameketi juu ya kiti cha hukumu, mkewe alimpelekea mjumbe, kumwambia, Usiwe na neno na yule mwenye haki; kwa sababu nimeteswa mengi leo katika ndoto kwa ajili yake. Nao wakuu wa makuhani na wazee wakawashawishi makutano ili wamtake Baraba, na kumwangamiza Yesu.”

 

Hivi umewahi kujiuliza kwanini Yesu alichukiwa? Vikao vya siri vikakaliwa na mikakati ya kuhakikisha anashughulikiwa ikafanyika? Sababu kubwa ni kuwa Yesu alikuwa mashuhuri kuliko watu wote, alijizolea sifa zote, kutokana na huduma na utumishi wake kwa kondoo wa Mungu waliotawanyika, alikuwa Mwalimu mwema, alikuwa ni mchungaji mwema, aliponya watu, aliwahurumia, alikuwa na majibu ya shida na matatizo yote ambayo jamii ilikuwa inakutana nayo, alilisha watu wengi, alifufua alifuta misiba ya wengi alafu mshahara wake ni kusulubiwa? Inakuwaje mtu mwema auawe? Inakuwaje watu wachague mtu muovu wamuache Yesu asulubiwe? Maandiko yanasema Pilato alijua kuwa wamemtoa kwa sababu ya husuda yaani wivu wenye uchungu, kila baya unalofanyiwa wakati mwingine ni kwa sababu umewazidi adui zako katika idara zote Neema iliyokuwa juu ya Yesu ilikuwa imewafunika viongozi wa dini, alikuwa akiwaumbua kwa kujawa na unafiki, aliifundisha kweli na kunyosha mstari, aliwakosoa vikali, akiwatendea mema watu na kuwafungua macho, akiruka vikwazo vyao, kwa hiyo walitafuta sababu za kumsulubisha  kwanini kwa sababu Neema ya Mungu iliyokuwa juu yake iliwavutia maadui!, vaa vizuri, kula vizuri, jenga nyumba nzuri, uwe na cheo kizuri utavutia watu wengi sana wawe karibu na wewe lakini wengine ni nyoka ni watu waliojaa wivu wenye uchungu wanaotaka kukuharibia maisha yako, watakuambia twende uwandani kisha huko watakuinukia wakuue  kama Habili kwanini kwa sababu neema ya Mungu iliyoko juu yako inaalika maadui.

Neema ya Mungu na mwaliko wa maadui

Mwanzo 26:12-16 “Isaka akapanda mbegu katika nchi ile, akapata mwaka ule vipimo mia kwa kimoja, BWANA akambariki. Na mtu huyu akawa mkuu, akazidi kusitawi, hata akawa mkuu sana. Akawa na mali ya kondoo, na mali ya ng'ombe, na watumwa wengi. Hao Wafilisti wakamhusudu. Na vile visima vyote walivyochimba watumwa wa baba yake, siku za Ibrahimu babaye, Wafilisti walikuwa wamevifukia, wakavijaza kifusi. Abimeleki akamwambia Isaka, Utoke kwetu, maana wewe una nguvu sana kuliko sisi.”

Tumeona katika utangulizi wa somo letu, namna Isaka alivyochukiwa na wafilisti na sababu kubwa ni kuwa walimuonea wivu, na wakaamua kuziba vyanzo vya Baraka zake yaani vile visima, Wakisahau kuwa chanzo kikuu cha Baraka za Isaka ni neema ya Mungu iliyokuwa juu yake, hata hivyo kama ipoipo tu, Mungu akishakuwa na mpango na mtu hakuna mwanadamu anaweza kuzuia mpango wa Mungu, Ndugu yangu vita yote kubwa uliyo nayo ni kwa sababu wewe u mzuri, unavaa vizuri, una neema ya Mungu juu yako, Mungu amekusudia kukuweka juu na kukubariki, kwa hiyo usifadhaike unapokutana na changamoto mbalimbali jua tu ya kuwa Mungu akiwa na mpango na wewe mipango yote ya wanadamu inafikia ukingoni, na Mungu anakwenda kujitukuza katika maisha yako, Isaka hakushindania visima na badala yake alichimba kingine na kingine na kingine na mwisho wa siku wakaona aibu wakamwacha na Mungu akaweka mkono wake na kuwapatia ahueni au nafasi Rehoboth wakati mwingine tuondoke na kwenda mbali na maadui zetu ili Bwana atupe nafasi ya kupumua maana wanaumwa sana na wivu wanaumwa mno wanadahani wakifukia visima na kudai kuwa ni vyao basi watatoboa lakini ijulikane wazi ya kuwa Mungu ni Mungu na Mungu kwa neema yake ndio chanzo kikuu cha Baraka zetu, Isaka angeweza kupigana vita lakini kwa kuwa alikuwa ni mtu mwema na mpenda Amani aliamua kujiepusha ili kutafuta kwa bidi kuwa na amani na watu wote!

Mwanzo 16:17-22. “Basi Isaka akatoka huko akapiga kambi katika bonde la Gerari, akakaa huko. Isaka akarudi akavichimbua vile visima vya maji walivyovichimba siku za Ibrahimu babaye; maana wale Wafilisti walikuwa wamevifukia baada ya kufa kwake Ibrahimu; naye akaviita majina kufuata majina alivyoviita babaye.Watumwa wa Isaka wakachimba katika lile bonde, wakapata kisima cha maji yanayobubujika.Wachungaji wa Gerari wakagombana na wachungaji wa Isaka wakisema, Maji haya ni yetu. Ndipo akakiita jina la kile kisima Eseki, kwa sababu waligombana naye.Wakachimba kisima kingine, wakagombania na hicho tena. Akakiita jina lake Sitna.Akaondoka huko akachimba kisima kingine, wala hicho hawakukigombania. Akakiita jina lake Rehobothi, akasema, Kwa kuwa sasa BWANA ametufanyia nafasi, nasi tutazidi katika nchi.”

Ushauri kutoka kwa Mungu.

Huu ni ushauri ambao Mungu anautoa kwa watu wenye wivu, kwamba ili Mungu akubariki, wewe endelea kufanya mema, basi, ukifanya vema naye atakubariki, Mungu amekusudia kumbariki kila mmoja  Mungu hana upendeleo hivyo jitahidi usimuonee wivu nduguyo, acha kuwafanyia watu mabaya, usiwauwe kwa ushahidi wa uongo, usiwachafue, usiwakasirikie ni neema ya Mungu iko juu yake huwezi kushindana naye ikiwa mkono wa Bwana uko juu yake, Mungu baba alimshauri Kaini ili asiingie dhambini kuwa afanye vema ! Mpango wa Mungu ni kumbariki kila mtu, lakini Mungu anataka usiwe na uchungu anapombariki mwengine hakikisha ya kuwa unakuwa mbali na kuumwa pale Mungu anapotoa kibali na neema yake kwa nduguyo kwani ni swala la zamu tu usitende dhambi, usifanye hila usikasirike, fanya vema nawe utabarikiwa pia usiwe na roho ya kaini aliyemuua nduguye  

Mwanzo 4:2-11 “Akaongeza akamzaa ndugu yake, Habili. Habili alikuwa mchunga kondoo, na Kaini alikuwa mkulima ardhi. Ikawa hatimaye Kaini akaleta mazao ya ardhi, sadaka kwa BWANA. Habili naye akaleta wazao wa kwanza wa wanyama wake na sehemu zilizonona za wanyama. BWANA akamtakabali Habili na sadaka yake; bali Kaini hakumtakabali, wala sadaka yake. Kaini akaghadhibika sana, uso wake ukakunjamana. BWANA akamwambia Kaini, Kwa nini una ghadhabu? Na kwa nini uso wako umekunjamana? Kama ukitenda vyema, hutapata kibali? Usipotenda vyema dhambi iko, inakuotea mlangoni, nayo inakutamani wewe, walakini yapasa uishinde. Kaini akamwambia Habili nduguye, [Twende uwandani]Ikawa walipokuwapo uwandani, Kaini akamwinukia Habili nduguye,akamwua. BWANA akamwambia Kaini, Yuko wapi Habili ndugu yako? Akasema, Sijui, mimi ni mlinzi wa ndugu yangu? Akasema, Umefanya nini? Sauti ya damu ya ndugu yako inanililia kutoka katika ardhi. Basi sasa, umelaaniwa wewe katika ardhi, iliyofumbua kinywa chake ipokee damu ya ndugu yako kwa mkono wako;”

Na Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!







Hakuna maoni:

Chapisha Maoni