Jumapili, 24 Machi 2024

Hosana, Mwana wa Daudi; (Jumapili ya Mitende)


Mathayo 21:1-11 “Hata walipokaribia Yerusalemu, na kufika Bethfage, katika mlima wa Mizeituni, ndipo Yesu alipotuma wanafunzi wawili akiwaambia, Enendeni mpaka kijiji kile kinachowakabili, na mara mtaona punda amefungwa, na mwana-punda pamoja naye; wafungueni mniletee. Na kama mtu akiwaambia neno, semeni, Bwana anawahitaji; na mara huyo atawapeleka. Haya yote yamekuwa, ili litimie neno lililonenwa na nabii, akisema, Mwambieni binti Sayuni Tazama, mfalme wako anakuja kwako, Mpole, naye amepanda punda, Na mwana-punda, mtoto wa punda. Wale wanafunzi wakaenda zao, wakafanya kama Yesu alivyowaamuru, wakamleta yule punda na mwana-punda, wakaweka nguo zao juu yao, naye akaketi juu yake. Watu wengi katika ule mkutano wakatandaza nguo zao njiani; na wengine wakakata matawi ya miti, wakayatandaza njiani. Na makutano waliotangulia, na wale waliofuata, wakapaza sauti, wakisema, Hosana, Mwana wa Daudi; ndiye mbarikiwa, yeye ajaye kwa jina la Bwana; Hosana juu mbinguni. Hata alipoingia Yerusalemu, mji wote ukataharuki, watu wakisema, Ni nani huyu? Makutano wakasema, Huyu ni yule nabii, Yesu, wa Nazareti ya Galilaya.”           



Utangulizi:

Leo 24/3/2024 ni jumapili ambayo katika makanisa ya Mengi, utaweza kuona watu wakubwa kwa wadogo wakiwa na matawi ya mitende mikononi mwao, wengine wakifanya maandamano kuanzia nje ya kanisa na kuingia nayo ndani, wote wakiadhimisha siku ya kuingia kwa Bwana wetu Yesu Kristo kwa Shangwe katika jiji la Yerusalem, wengine wakiwa wanajua maana yake na wengine hata hawajui lakini wanafuata tu utaratibu wa kidini, inawezekana hawajaambiwa, wala haajafundishwa, lakini sasa wakati wa kutokuambiwa umeisha kila kitu sasa ni wakati wake kuwekwa wazi ili watu waweze kuelewa, haikuwa tu siku ya kuingia Yerusalem kwa shangwe, wala siku ya kusheherekea sikukuu ya mitende, lakini kinabii ilikuwa ni ushindi dhidi ya Ukoloni! wa kiroho  ni siku ya Kusimikwa kwa mfalme mkuu sana mwenye uwezo wa kuwasaidia watu kutoka katika kila aina ya utumwa na ukandamizaji wa kimwili na kiroho uliowachosha kwa muda mrefu angalia:-

Ufunuo 7:9-10 “Baada ya hayo nikaona, na tazama, mkutano mkubwa sana ambao hapana mtu awezaye kuuhesabu, watu wa kila taifa, na kabila, na jamaa, na lugha, wamesimama mbele ya kile kiti cha enzi, na mbele za Mwana-Kondoo, wamevikwa mavazi meupe, wana matawi ya mitende mikononi mwao; wakilia kwa sauti kuu wakisema, Wokovu una Mungu wetu aketiye katika kiti cha enzi, na Mwana-Kondoo.”

Ni neema kubwa sana kuwa Makanisa ya mengi hasa ya kizamani, wametunza tukio hili la Muhimu aidha kwa kujua au kwa kutokujua lakini wanapoadhimisha wanaadhimisha mojawapo ya tukio la msingi sana katika nabii zinazohusiana na Masihi na kazi aliyoifanya Kwa dunia na ile atakayoifanya na kuitimiza baadaye, hata kama unaweza usikate matawi ya mitende, lakini unaweza kufanya ibada ya kusifu na kuabudu ukimuadhimisha Masihi kwa kazi yake njema aliyoifanya pale Msalabani! Au pia unaweza kuitioa wakfu jumapili hii kwa kuhubiri ujumbe kuhusu kuingia Kwa Yesu jijini Yerusalem kwa shangwe, kwa hiyo sio makanisa ya zamani peke yao Lakini hata makanisa ya uamsho wa kipentekoste na Karismatiki wote tunasheherekea siku hii, lakini kila mmoja kwa namna yake!, Kimsingi katika maandiko jumapili ya mitende ina maana pana sana kuliko tunavyoweza kufikiri juu juu:-

·         Ilikuwa siku ya kutimizwa kwa unabii

·         Ishara ya matawi ya mitende

·         Hosana Mwana wa Daudi (Jumapili ya mitende)

 

Ilikuwa siku ya kutimizwa kwa unabii

Tendo la Yesu Kristo kushangiliwa na kuingia Yerusalem kwa Shangwe halikuwa tu tukio la bahati mbaya, lilikuja kutimiza unabii ulionenwa na nabii Zekaria  na bila kuelewa jamii kubwa ya wayahudi waliokuwa wanasogea Yerusalemu majira ya sikukuu, walimshangilia Bwana Yesu kwa nguvu zao zote ilikuwa ni siku ya kilele cha Huduma ya Yesu Kristo kwa watu walichoka kuwa watumwa wa ukoloni wa Kirumi, kimwili na utumwa wa shetani kiroho, wenye shauku na utawala wa Kisayuni uliokuwa unatarajiwa kuletwa na Mwana wa Daudi, mara kadhaa walikuwa wametaka kumfanya awe mfalme lakini yeye mwenyewe alikataa, lakini wakati huu walikuwa wamemkubali na kumsimika kuwa mfalme bila kufanya mapinduzi yoyote, ilikuwa ni siku ngumu kwa maadui wa Kristo, ilikuwa sio siku rahisi kupinga wala kunyamazisha watu wasimtukuze Kristo kwa kuwa jamii yote ilikuwa imemkubali.

Yohana 6:15-22 “Kisha Yesu, hali akitambua ya kuwa walitaka kuja kumshika ili WAMFANYE MFALME, akajitenga, akaenda tena mlimani yeye peke yake. Hata ilipokuwa jioni wanafunzi wake wakatelemka baharini wakapanda chomboni, wakaanza kuivuka bahari kwenda Kapernaumu. Nako kumekwisha kuwa giza, wala Yesu hajawafikia. Na bahari ikaanza kuchafuka kwa kuvuma upepo mkuu.Basi wakavuta makasia kadiri ya maili tatu nne, wakamwona Yesu anakwenda juu ya bahari na kukikaribia chombo; wakaogopa. Naye akawaambia, Ni mimi, msiogope. Basi wakataka kumpokea chomboni; na mara hiyo chombo kikaifikilia nchi waliyokuwa wakiiendea. Siku ya pili yake mkutano waliosimama ng'ambo ya bahari waliona ya kuwa hakuna mashua nyingine huko ila moja, tena ya kuwa Yesu hakuingia katika mashua ile pamoja na wanafunzi wake, bali wanafunzi wake walikwenda peke yao.”
     

Zekaria 9:9 “Furahi sana, Ee binti Sayuni; Piga kelele, Ee binti Yerusalemu; Tazama, MFALME wako anakuja kwako; Ni mwenye haki, naye ana wokovu; Ni mnyenyekevu, amepanda punda, Naam, mwana-punda, mtoto wa punda.”

Kifungu cha kwanza kinaonyesha Yesu akikataa kwa sababu watu walitaka kumfanya kuwa mfalme kwa manufaa yao, walitaka kumfanya mfalme aliyetukuzwa, mwenye nguvu dhidi ya serikali ya kirumi, mwenye kuwalisha mikate, mfalme mwenye kutenda miujiza, mfalme ambaye ukiwa naye huhitaji hata kufanya kazi ngumu, anakulisha mikate, anafanikisha, anabariki kila ulicho nazo kinazidi, samaki wanazidi, mikate inazidi, faida zinazidi, biashara zinafanikiwa, na zaidi ya yote warumi na serikali yao itaondolewa, lakini Yesu ni mfalme lakini kwa wakati ule hakuwa mfalme aliyetukuzwa, alikuwa mfalme mnyenyekevu ambaye kwanza angepigana vita ya rohoni na kuwakomboa na utumwa mmbaya zaidi wa shetani kuliko utumwa wa kikoloni wa warumi, Hivyo hangepanda farasi, angepanda punda kama alivyo tabiri nabii,  Kupanda Punda ilikuwa ni ishara ya ufalme duni, ufalme wa kinyenyekevu, ufalme usiohusu kujikweza, tena sio  ufalme wa kimapinduzi, bali ufalme wa kujishusha, ufalme usiotokana na vita bali wa Amani.

Kwa hiyo kifungu hiki cha pili, unabii wa nabii Zekaria unatimizwa kwa sababu kubwa zaidi aalitabiri siku hii ambayo masihi ndiye mfalme aliyeingia kwa Amani, kwa kutumia Punda, ilikuwa ni sihara ya unyenyekevu na Amani na anatajwa mfalme huyu kuwa anakuja na zawadi ya wokovu, si kwa fahari ya kifalme bali kwa unyenyekevu alikuwa tayari kuukabili Msalaba apate kuwakomboa wanadamu, Huu ni ushindi mkubwa zaidi kuliko aina nyingine yoyote ya ushindi na Hivyo Sayuni ilipaswa kupiga kelele, kwani Kristo huyu atakuja tena si kwa unyenyekevu huu na kukubali kufa msalabani bali kwa nia  ya kusimamisha utawala wake wa miaka 1000 duniani ambapo kila mtu atafurahia na zaidi sana katika utawala wake na siku yake ya kusimikwa rasmi katika kiti cha enzi.

Kwa hiyo siku hii ya matawi ya mitende ilikuwa ni siku ya ushindi na kusimikwa kwa mtawala na mwokozi wa roho zetu zaidi kabla ya ukombozi wa mwili siasa na uchumi utakaofuata katika utawala wake, japo matumaini makubwa ya Israel yalikuwa ni katika ufalme wenye kuonekana, Lakini Mwokozi alikuwa analeta kwanza zawadi ya wokovu wa roho zetu, na msamaha wa dhambi, na kuuvunja utawala wa shetani na kuharibu kiburi cha wanadamu!

Matendo 1:6-8 “Basi walipokutanika, wakamwuliza, wakisema, Je! Bwana, wakati huu ndipo unapowarudishia Israeli ufalme? Akawaambia, Si kazi yenu kujua nyakati wala majira, Baba aliyoyaweka katika mamlaka yake mwenyewe. Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi.”     


Ishara ya matawi ya mitende

Mathayo 21:1-11 “Hata walipokaribia Yerusalemu, na kufika Bethfage, katika mlima wa Mizeituni, ndipo Yesu alipotuma wanafunzi wawili akiwaambia, Enendeni mpaka kijiji kile kinachowakabili, na mara mtaona punda amefungwa, na mwana-punda pamoja naye; wafungueni mniletee. Na kama mtu akiwaambia neno, semeni, Bwana anawahitaji; na mara huyo atawapeleka. Haya yote yamekuwa, ili litimie neno lililonenwa na nabii, akisema, Mwambieni binti Sayuni Tazama, mfalme wako anakuja kwako, Mpole, naye amepanda punda, Na mwana-punda, mtoto wa punda. Wale wanafunzi wakaenda zao, wakafanya kama Yesu alivyowaamuru, wakamleta yule punda na mwana-punda, wakaweka nguo zao juu yao, naye akaketi juu yake. Watu wengi katika ule mkutano wakatandaza nguo zao njiani; na wengine wakakata matawi ya miti, wakayatandaza njiani. Na makutano waliotangulia, na wale waliofuata, wakapaza sauti, wakisema, Hosana, Mwana wa Daudi; ndiye mbarikiwa, yeye ajaye kwa jina la Bwana; Hosana juu mbinguni. Hata alipoingia Yerusalemu, mji wote ukataharuki, watu wakisema, Ni nani huyu? Makutano wakasema, Huyu ni yule nabii, Yesu, wa Nazareti ya Galilaya.”     
       

Katika siku hii ya kutimizwa kwa unabii wa Zekaria, Yesu aliingia Yerusalem kwa shangwe huku kukiwa na matukio makubwa mawili, ukiacha swala la kupanda Punda watu walichukua matawi ya mitende na  kutoa mavazi yao na kuyatandaza njiani, lakini kubwa zaidi kupaza sauti zao wakisema Hosanna mwana wa Daudi.

Kwanini Matawi ya mitende? Ni kweli kijiografia Israel ni moja ya nchi zenye miti jamii ya mitende ambayo inasitawi sana katika inchi zote za mashariki ya kati, kwa hiyo mitende ni moja ya miti iliyokuwako kwa wingi, hata hivyo ni muhimu kujiuliza kwa nini walichukua matawi ya mitende na sio miti Mingine? Mitende hii ilikuwa ni ishara Mtende una maana kubwa ya muhimu kiroho, kwa hivyo watu hawakuchuma tu kwa sababu ni miti iliyokuwepo, kwani iko pia miti ya mizeituni, mizabibu, tini na kadhalika lakini mti huu ulikuwa na maana kubwa ya kiroho Mti huu ulikuwa ni alama ya USHINDI Mti wa mtende ni mti wenye kuvutia sana nyakati za zamani sana Wagiriki walipokuja kutawala nchi ya Israel waliilita nchi hii PHOENICIA wakimaanisha nchi ya mitende, Mti huu ni alama ya ustawi, ushindi na Baraka Mtende unastawi hata janwani, ni mti wa ushindi, unashinda ukame, unaonyesha ukijani bila kujali majira na nyakati na unazaa matunda wala hauchoki, Kwa hiyo mti huu ulikuwa ni ishara ya kushinda na kuvumilia magumu!

Zaburi 92:12-14 “Mwenye haki atasitawi kama mtende, Atakua kama mwerezi wa Lebanoni. Waliopandwa katika nyumba ya Bwana Watasitawi katika nyua za Mungu wetu.Watazaa matunda hadi wakati wa uzee, Watajaa utomvu, watakuwa na ubichi.”

Wayahudi walikuwa na kiu ya ushindi, walikuwa wamechoshwa na utumwa wa Kirumi, na walikuwa wanataka Mwokozi na mpakwa mafuta kutoka ukoo wa Daudi awarudishie ufalme walioamini kuwa ni ufalme wa Mungu, ilikuwa ni machukizo sana kwao kutawaliwa na watu wasiotahiriwa, ilikuwa ni unajisi kuwa hawako huru kutoka katika inchi yao,  ilikuwa ni maumivu kuwa hawana mfalme wao wala manabii wanaoweza kurudisha uhusiano wa kiungu na taifa lao kwa hiyo walimuona Yesu kuwa mtu maarufu na walijua kuwa ni wa ukoo wa Daudi na waliona ndiye anafaa kuwa kiongozi wao wa kiroho na kisiasa kama alivyokuwa Daudi, na walimjua kuwa alikuwa mwana wa Daudi kwa hiyo walikuwa wanataka Yesu awashindie, walikuwa wanatamani kutolewa katika utumwa ule, hivyo mtende ulikuwa ni alama ya Ushindi, kile ambacho Yesu anakwenda kukifanya katika mji ule mkuu ni kuleta ushindi.

Jambo la Pili wimbo waliouimba HOSANNA mwana wa Daudi Ndiye mbarikiwa ajae kwa jina la Bwana, Hosana juu mbinguni, huu ulikuwa ni wimbo ambao umeandaliwa kwaajili ya Masihi, siku ile kila mmoja alikubali na kumtambua Yesu kuwa Ndiye masihi, waliamini pia kuwa amekubalika Duniani na mbinguni na wakaimba Hosana. Neno Hosana ni neno linalotokana na Neno la kiibrania ambalo ni la kumsifu Mfalme na la kutaka mfalme afanye kazi yake ya kuokoa, neno hili linaweza kutamkwa kwa Mungu na kwa masihi wake tu, TAFADHALI TUOKOE  ni kilio cha ukombozi cha kumtaka mfalme aokoe na Mungu aingilie kati kupitia mfalme awaletee watu wake wokovu, Kwa hiyo Hosana mwana wa Daudi, ni Maombi maalumu ya kumsihi TAFADHALI TUOKOE EE MWANA WA DAUDI, WEWE UMEBARIKIWA NA HOSANA JUU MBINGUNI,  Yalikuwa ni maombi ya Kumuomba Mungu aokoe kupitia mpakwa mafuwa wake na kwa kweli Ndicho ambacho Yesu alikuwa anakwenda kukifanya katika juma lile lakini haikuwa kisiasa.  

Hosana Mwana wa Daudi (Jumapili ya mitende)

Kwa hiyo tunapoadhimisha siku ya Jumapili ya Mitende, haijalishi inaadhimishwaje, yako makanisa wanaadamana huku wakiwa na matawi ya mitende wakiimba nyimbo za kumtukuza Mungu, wanaweza kufanya maandamano hayo ndani au nje ya kanisa, Matawi ya mitende yakiwakilisha mti ule uliotumiwa na wayahudi kumtukuza Mungu na kumuadhimisha Kristo alipokuwa akiingia Yerusalem, wengine wakibariki matawi hayo ya mitende na kufanya ibada maalumu jumapili ya mwisho kabla ya jumapili ya pasaka,  na kusoma maandiko yanayohusiana na siku hiyo,  na tamaduni mbali mbali kila kanisa linaweza kufanya ibada ya jumapili ya mitende vile wanavyoo nan a kupendekeza

Hata hivyo siku hii ni siku ya ushindi, tunaanza kuadhimisha na kusheherekea Kuanza kwa ufalme wa Mungu, Yesu aliingia Yerusalemu akiwa amebeba wokovu, alikuwa yuko tayari kuyakabili mateso ya msalaba na kuyatoa maisha yeke kuwa dhabihu kwaajili ya wengi. Siku zote katika huduma ya masihi hakuna mahali palikuwa pa hatari kama Yerusalem, hii ilieleweka wazi hata kwa wanafunzi wake, njama zote na mipango yote ya kumuua mwanaume huyu aliyepata umaarufu mkubwa nchini Israel ilikuwa ikisukwa Yerusalem angalia :-

Yohana 11:7-8, 16 “Kisha, baada ya hayo, akawaambia wanafunzi wake, Twendeni Uyahudi tena. Wale wanafunzi wakamwambia, Rabi, juzijuzi tu Wayahudi walikuwa wakitafuta kukupiga kwa mawe, nawe unakwenda huko tena?, Basi Tomaso, aitwaye Pacha, akawaambia wanafunzi wenziwe, Twendeni na sisi, ili tufe pamoja naye.” 

Hata hivyo Kristo kwa nini anakubali kwenda katika eneo hatarishi la maisha yake? Yesu alikuwa anajua wazi kuwa ndipo mahali anapopaswa kufia na wakati wake ulikuwa umefika na alijua kuwa haimpasi kufia nje ya Yerusalem, kwa hiyo siku hii Yesu aliingia Yerusalem kwa ujasiri mwingi, akikubali kutukuzwa na watu wote ni siku ambayo kama kuhatarisha maisha yake aliyahatarisha zaidi, lakini hakuwa na hofu yeye alikua anajua anachokwenda kukifanya.

Luka 13:31-33 “Saa ile ile Mafarisayo kadha wa kadha walimwendea, wakamwambia, Toka hapa, uende mahali pengine, kwa sababu Herode anataka kukuua. Akawaambia, Nendeni, mkamwambie yule mbweha, Tazama, leo na kesho natoa pepo na kuponya wagonjwa, siku ya tatu nakamilika. Pamoja na hayo imenipasa kushika njia yangu leo na kesho na kesho kutwa; kwa kuwa haimkini nabii aangamie nje ya Yerusalemu.”

Kristo alikuwa amepanga aende Yerusalem licha ya kuwa kulikuwa na vitisho vya kuuawa kwake, siku hii alikaribishwa kwa furaha na kwa matarajio makubwa sana, wayahudi walikuwa wamemkubali kama mfalme, walikuwa wako tayari awaokoe, ilikuwa ni kilele cha huduma yake kubwa ya ukombozi, Japo Israel walifikiri, atawakomboa dhidi ya ukoloni wakiwarumi lakini ilikuwa ni siku ya ukombozi kwa ulimwengu wote, ilikuwa ni siku ya ushindi kwa wote wanaomtazamia kwa wokovu!

Kwa hiyo ni jumapili ya maombi, ni jumapili ya kusifu, ni jumapili ya kumkubali Yesu, ni jumapili ya kukubali utawala wa masihi katika mioyo yetu, ni jumapili ya kumwambia bwana okoa kila eneo la maisha yetu, ni jumapili ya kufutiwa huzuni zetu, ni siku ya kutarajia ushindi na wokovu katika kila Nyanja ya maisha yetu, ni jumapili ya kumuomba Masihi mwana wa Daudi aingilie kati maisha yetu, kwa hiyo tunapoadhimisha leo Jumapili ya mitende, acha kufikiri kuhusu mitende fikiri kuhusu ushindi katika kila eneo la  maisha yako, kama kuna eneo ulishindwa leo ni siku ya kuomba ukombozi katika maisha yako, kama ulikuwa unatawaliwa na unaonewa na kukandamizwa ni siku ya kuwaambia wakoloni wa kipepo kuondoka, ni siku ya kuvunja mikataba na shetani, ni siku ya kumaliza maadui  na kuitangaza Amani, kwa kuwa mfalme anakuja, ni siku ya Amani na furaha ujumbe mkubwa unaobebwa na Mfalme huyu ni Amani, tabia inayobebwa na Mfalme huyu ni unyenyekevu, tunda linalobebwa na mfalme huyu ni upole. Na ni hukumu ya namna gani inayobebwa na Mfalme huyu ni haki.

Zekaria 9:9-10 “Furahi sana, Ee binti Sayuni; Piga kelele, Ee binti Yerusalemu; Tazama, mfalme wako anakuja kwako; Ni mwenye haki, naye ana wokovu; Ni mnyenyekevu, amepanda punda, Naam, mwana-punda, mtoto wa punda. Na gari la vita nitaliondoa liwe mbali na Efraimu, na farasi awe mbali na Yerusalemu, na upinde wa vita utaondolewa mbali; naye atawahubiri mataifa yote habari za amani; na mamlaka yake yatakuwa toka bahari hata bahari, na toka Mto hata miisho ya dunia.”

Ni siku ambayo Yesu hawezi kuzuiliwa na kitu chochote, kila kitu ni lazima kimsifu, na kama kuna mtu atazui siku ile Mawe yangeifanya kazi hiyo, kwa sababu Mbingu nan chi zilikuwa zimekubali, kwamba ni lazima atimize haki na lazima aokoe hakuna upinzani unaweza kufaulu siku Yesu anapotukuzwa na kuinuliwa, siku ile Mfarisayo walitaharuki sana, walipigwa na butwaa mamlaka ya Kristo ilizidi, alikuwa na nguvu kubwa sana alisifiwa na kutukuzwa kila mahali watu wazima kwa watoto, na ni siku ambayo hakuna mtu angeweza kuzuia Yesu asitukuzwe!

Luka 19:37-40 “Hata alipokuwa amekaribia matelemko ya mlima wa Mizeituni, kundi zima la wanafunzi wake walianza kufurahi na kumsifu Mungu kwa sauti kuu, kwa ajili ya matendo yote ya uwezo waliyoyaona, wakasema, Ndiye mbarikiwa Mfalme ajaye kwa jina la Bwana; amani mbinguni, na utukufu huko juu. Baadhi ya Mafarisayo waliokuwa katika mkutano wakamwambia, Mwalimu, uwakanye wanafunzi wako. Akajibu, akasema, Nawaambia ninyi, wakinyamaza hawa, mawe yatapiga kelele.”

 

Na Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa Wajenzi mwenye Hekima      

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni