Ijumaa, 29 Machi 2024

Hata wajapokunguwazwa wote, lakini siyo mimi!


Marko 14:27-31 “Yesu akawaambia, Mtakunguwazwa ninyi nyote kwa ajili yangu usiku huu; kwa kuwa imeandikwa, Nitampiga mchungaji, na kondoo watatawanyika. Lakini baada ya kufufuka kwangu, nitawatangulia kwenda Galilaya. Petro akamwambia, Hata wajapokunguwazwa wote, lakini siyo mimi. Yesu akamwambia, Amin, nakuambia wewe, Leo, usiku huu, kabla ya kuwika jogoo mara mbili, utanikana mara tatu. Naye akazidi sana kusema, Ijaponipasa kufa nawe, hata hivyo sitakukana kamwe. Na wote wakasema vile vile.”   

          



Utangulizi:

Tunakaribia kabisa katika juma muhimu la Pasaka, na jumbe mbalimbali zitakuwa zinahubiriwa katika majira haya na msimu huu kuelekea katika wakati wa Pasaka, mimi nami nimetia mkono wangu nipate kuzungumza lile ambalo Mungu anataka kusema na watu wake katika majira haya ya Pasaka, Katika majira haya ya pasaka nataka tujikumbushe kwamba uko umuhimu wa kujishusha, tunapokumbuka na kuadhimisha pasaka tunakumbuka tu sio ukombozi wa Mwanadamu pekee bali na umuhimu wa kuchukua nafasi ya chini kwa kujinyenyekeza na kuacha kabisa kujiona Bora kuliko wengine

Wafilipi 2:3-8 “Msitende neno lo lote kwa kushindana wala kwa majivuno; bali kwa unyenyekevu, kila mtu na amhesabu mwenziwe kuwa bora kuliko nafsi yake. Kila mtu asiangalie mambo yake mwenyewe, bali kila mtu aangalie mambo ya wengine. Iweni na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo Yesu; ambaye yeye mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu; tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba.”

Unaona tunajifunza kwamba Pasaka ni unyenyekevu, Kitendo cha Yesu Kristo kuubeba Msalaba na kukibali mateso ili hali alikuwa Mungu, katika msimu huu wa Pasaka kinatukumbusha kuwa wakati wote tunapaswa kuufuata mfano wake, na kuacha kujitutumua au kujiweka katika nafasi ambayo sisi wenywewe tunadhani kuwa ni wa muhimu kuliko wengine, kila mmoja amuhesabu mwenzake kuwa ni bora kuliko nafsi yake! Tutajifunza somo hili Hata wajapokunguwazwa wote, lakini siyo mimi! Kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-


·         Maana ya neno Kunguwazwa

·         Hata wajapokunguwazwa wote lakini sio mimi

·         Mambo muhimu ya kujifunza


Maana ya neno Kungunguwazwa

Marko 14:27-31 “Yesu akawaambia, MTAKUNGUWAZWA ninyi nyote kwa ajili yangu usiku huu; kwa kuwa imeandikwa, Nitampiga mchungaji, na kondoo watatawanyika. Lakini baada ya kufufuka kwangu, nitawatangulia kwenda Galilaya. Petro akamwambia, Hata wajapokunguwazwa wote, lakini siyo mimi. Yesu akamwambia, Amin, nakuambia wewe, Leo, usiku huu, kabla ya kuwika jogoo mara mbili, utanikana mara tatu. Naye akazidi sana kusema, Ijaponipasa kufa nawe, hata hivyo sitakukana kamwe. Na wote wakasema vile vile.”

Ni muhimu kufahamu kuwa lugha ya Kiswahili inayotumika mahali hapo kama Kunguwazwa ni lugha ya Kiswahili cha kizamani, Neno Mtakungwaza katika Biblia ya kiingereza ya KJV mstari wa 27 unasomeka hivi And Jesus saith unto them All Ye shall be OFFENDED because of me this night” kwa hiyo neno kukunguwazwa katika kiingereza ni Offended ambalo kwa kiyunani ni SKANDALIZO Ambalo maana yake ni kuingia mtegoni, au kukwazwa au kukoseshwa, au kuchukizwa kama linavyotumiwa na waandishi wengine

Mathayo 26:31-35 “Ndipo Yesu akawaambia, Ninyi nyote MTACHUKIZWA kwa ajili yangu usiku huu kwa kuwa imeandikwa, Nitampiga mchungaji, na kondoo wa kundi watatawanyika. Lakini baada ya kufufuka kwangu, nitawatangulia kwenda Galilaya. Petro akajibu, akamwambia, Wajapochukizwa wote kwa ajili yako, mimi sitachukizwa kamwe. Yesu akamwambia, Amin, nakuambia wewe, usiku huu kabla ya kuwika jogoo, utanikana mara tatu. Petro akamwambia, Ijaponipasa kufa nawe, sitakukana kamwe. Na wanafunzi wote wakasema vivyo hivyo.”

Kukunguwazwa huku au kuchukizwa kuna uhusiano wa kumkana au kumkimbia Yesu, usiku wa kukamatwa kwa Yesu, ulikuwa ni usiku wa kujaribiwa kwa wanafunzi wake, na shetani alikuwa ameruhusiwa ili awapepete kama ngano, kwaaajili ya kuonyesha kuwa bado walikuwa hawako imara kumtetea au hata kuwa pamoja na Yesu wakati ule

Luka 22:31-34 “Akasema, Simoni, Simoni, tazama, Shetani amewataka ninyi apate kuwapepeta kama vile ngano; lakini nimekuombea wewe ili imani yako isitindike; nawe utakapoongoka waimarishe ndugu zako. Akamwambia, Bwana, niwapo pamoja nawe, mimi ni tayari kwenda gerezani au hata kifoni. Akasema, Nakuambia, Petro, jogoo hatawika leo, kabla wewe hujanikana mara tatu ya kuwa hunijui.”

Yesu Kristo alikuwa amejua kuwa usiku ule atakaokamatwa, utakuwa ni usiku wa majaribu makubwa kwa wanafunzi wake, aliwataka waombe kule bustanini ili wasiingie majaribuni, ulikuwa ni usiku wa kutosha, Imani ya kila mwanafunzi na uaminifu wa kila mwanafunzi ungepimwa wakati wa kukamatwa kwa Yesu, wote wangekimbia maana yake wangemkana Yesu kivitendo na kutokukubali kufa naye, Japo walimuahidi, Lakini katika namna ya kushangaza Petro ndiye ambaye aliharibu zaidi siku ile kuliko wanafunzi wote nan die aliyeombewa na Bwana, na alielezwa wazi kuwa yeye angamkana Yesu mara tatu, kwa sababu alijiamini mno kuliko wengine akidhani kuwa wengine ni wadhaifu kuliko yeye   

 Hata wajapokunguwazwa wote lakini sio mimi

Wakati Yesu akiahidi kuwa usiku ule kila mmoja atakungwazwa kwaajili yake kama tusomavyo katika andiko la Msingi Marko 14:27-31 “Yesu akawaambia, MTAKUNGUWAZWA ninyi nyote kwa ajili yangu usiku huu; kwa kuwa imeandikwa, Nitampiga mchungaji, na kondoo watatawanyika. Lakini baada ya kufufuka kwangu, nitawatangulia kwenda Galilaya. Petro akamwambia, Hata wajapokunguwazwa wote, lakini siyo mimi. Yesu akamwambia, Amin, nakuambia wewe, Leo, usiku huu, kabla ya kuwika jogoo mara mbili, utanikana mara tatu. Naye akazidi sana kusema, Ijaponipasa kufa nawe, hata hivyo sitakukana kamwe. Na wote wakasema vile vile.”

Petro yeye alijiamini kupita kawaida, na kutaka kumthibitishia Yesu kuwa yeye hatakunguwazwa, na akamhakikishia Yesu kuwa yuko tayari kufa naye n ahata kwenda gerezani pamoja naye Petro alimwambia Bwana Hata wajapokunguwazwa wote lakini sio mimi, Petro alikuwa na uhakika kuwa hawezi kukomsea Yesu hata siku Moja, wengine wanaweza kumkosea Yesu lakini sio mtu kama yeye, Petro alikuwa na ujasiri mkubwa sana, wote tunajua jnsi Petro alivyikuwa mwanafunzi muhimu katika wanafunzi wa Yesu, yeye anatajwa kuwa ni nguzo za kanisa 

-          Wagalatia 2:9 “tena walipokwisha kuijua ile neema niliyopewa; Yakobo, na Kefa, na Yohana, wenye sifa kuwa ni nguzo, walinipa mimi na Barnaba mkono wa kuume wa shirika; ili sisi tuende kwa Mataifa, na wao waende kwa watu wa tohara;”

 

Nyakati za Kanisa la Kwanza Petro au Kefa alijulikana kuwa ni Nguzo, katika madarasa ya uanafunzi ya Yesu Kristo, Petro Yakobo na Yohana, walikuwa dara sa la juu zaidi kuliko wanafunzi wenguine wote, walishuhudia mambo makubwa sana, na walijua siri ambazo wanafunzi wengine hawakujua

 

-          Mathayo 17:3-9 “Na baada ya siku sita Yesu akawatwaa Petro, na Yakobo, na Yohana nduguye, akawaleta juu ya mlima mrefu faraghani; akageuka sura yake mbele yao; uso wake ukang'aa kama jua, mavazi yake yakawa meupe kama nuru. Na tazama, wakatokewa na Musa na Eliya, wakizungumza naye. Petro akajibu akamwambia Yesu, Bwana, ni vizuri sisi kuwapo hapa; ukitaka, nitafanya hapa vibanda vitatu, kimoja chako wewe, na kimoja cha Musa, na kimoja cha Eliya. Alipokuwa katika kusema, tazama, wingu jeupe likawatia uvuli; na tazama, sauti ikatoka katika lile wingu, ikasema, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye; msikieni yeye. Na wale wanafunzi waliposikia, walianguka kifulifuli, wakaogopa sana. Yesu akaja, akawagusa, akasema, Inukeni, wala msiogope. Wakainua macho yao, wasione mtu ila Yesu peke yake. Na walipokuwa wakishuka mlimani, Yesu aliwaagiza, akasema, Msimwambie mtu ye yote habari ya maono hayo, hata Mwana wa Adamu atakapofufuka katika wafu.”

 

Unaona Petro alikuwa ni miongoni mwa wanafunzi wachache waliokwenda pamoja na Yesu katika mlima mrefu faraghani na kuona maono mazito na walielezwa wasimwambie mtu awaye yote kwa hiyo unaweza kuona uimara wa Petro, unaweza kujua kuwa alimjua Yesu kwa viwango vikubwa na vya juu zaidi alikuwa shahidi wa Yesu Kristo mwenye ujuzi mkubwa na wa juu zaidi hata wa kuelezea Yesu ni nani, Yeye mwenyewe alikiri kuwa ni miongoni mwa watu waliouona utukufu wake

 

-          1Petro 1:16-18 “Maana hatukufuata hadithi zilizotungwa kwa werevu, tulipowajulisha ninyi nguvu zake Bwana wetu Yesu Kristo na kuja kwake; bali tulikuwa tumeuona wenyewe ukuu wake. Maana alipata kwa Mungu Baba heshima na utukufu, hapo alipoletewa sauti iliyotoka katika utukufu mkuu, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye. Na sauti hiyo sisi tuliisikia ikitoka mbinguni tulipokuwa pamoja naye katika mlima ule mtakatifu.”  

 

Petro alikuwa miongoni mwa wanafunzi wa yesu waliowahi kuisikia sauti ya Mungu baba ikisema huyu ndiye Mwanangu mpendwa ninayependezwa naye, na kama haitoshi miongoni mwa wanafunzi wa Yesu aliyeweza kujibu swala la Yesu kwa ufasaha zaidi ya wanafunzi wengine na kusifiwa kuwa alikuwa amefunuliwa na baba wa Mbinguni Petro alikuwa ni wa kwanza

 

-          Mathayo 16:13-17 “Basi Yesu akaenda pande za Kaisaria-Filipi, akawauliza wanafunzi wake akasema, Watu hunena Mwana wa Adamu kuwa ni nani? Wakasema, Wengine hunena u Yohana Mbatizaji, wengine Eliya, wengine Yeremia au mmojawapo wa manabii. Akawaambia, Nanyi mwaninena mimi kuwa ni nani? Simoni Petro akajibu akasema, Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai. Yesu akajibu, akamwambia, Heri wewe Simoni Bar-yona; kwa kuwa mwili na damu havikukufunulia hili, bali Baba yangu aliye mbinguni.”

 

Petro alikuwa ni Mwanafunzi wa kipekee, alimjua Yesu Vizuri na alikuwa tayari kumfuata alifuzu mitihani yote ya Bwana Yesu, alijaribu mambo mengi kuliko wengine ja unajua ya kuwa ni yeye ndiye mwanafunzi pekee aliyejaribu kutembea juu ya maji?

 

-          Mathayo 14:25-30 “Hata wakati wa zamu ya nne ya usiku Yesu akawaendea, akienda kwa miguu juu ya bahari. Wanafunzi walipomwona akienda juu ya bahari, wakafadhaika, wakisema, Ni kivuli; wakapiga yowe kwa hofu. Mara Yesu alinena, akawaambia, Jipeni moyo ni mimi; msiogope. Petro akamjibu, akasema, Bwana, ikiwa ni wewe, niamuru nije kwako juu ya maji. Akasema, Njoo. Petro akashuka chomboni, akaenda kwa miguu juu ya maji, ili kumwendea Yesu. Lakini alipouona upepo, akaogopa; akaanza kuzama, akapiga yowe, akisema, Bwana, niokoe.”

 

Petro alikuwa miongoni mwa wanafunzi wa Yesu ambao, walipata mafunzi mazui nay a kina nay a ndani zaidi hususani wakati Yesu anafufua wafu

 

-          Marko 5:37-43 “Wala hakumruhusu mtu afuatane naye, ila Petro, na Yakobo, na Yohana nduguye Yakobo. Wakafika nyumbani kwa yule mkuu wa sinagogi, akaona ghasia, na watu wakilia, wakifanya maombolezo makuu. Alipokwisha kuingia, akawaambia, Mbona mnafanya ghasia na kulia? Kijana hakufa, bali amelala tu. Wakamcheka sana. Naye alipokwisha kuwatoa nje wote, akamtwaa babaye yule kijana na mamaye, na wale walio pamoja naye, akaingia ndani alimokuwamo yule kijana. Akamshika mkono kijana, akamwambia, Talitha, kumi; tafsiri yake, Msichana, nakuambia, Inuka. Mara akasimama yule kijana, akaenda; maana alikuwa amepata umri wa miaka kumi na miwili. Mara wakashangaa mshangao mkuu. Akawaonya sana, mtu asijue habari ile; akaamuru apewe chakula

 

Hata muda mchache kidogo kabla ya kukamatwa kwa Yesu, Petro, Yakobo na Yohana walichukuliwa hatua moja zaidi na Bwana kwaajili ya kuwataka waombe kwa kukesha pamoja naye

 

Marko 14:33-35 “Akamtwaa Petro na Yakobo na Yohana pamoja naye, akaanza kufadhaika sana na kuhangaika. Akawaambia, Roho yangu ina huzuni nyingi kiasi cha kufa; kaeni hapa mkeshe. Akaendelea mbele kidogo, akaanguka kifudifudi, akiomba ya kuwa, ikiwezekana, saa hiyo imwepuke.”     

 

Unaweza kuona maswala kadhaa kuhusu Petro kwamba alikuwa ni mtu wa namna gani, na alikuwa na nafasi ya namna gani katika moyo wa Yesu, na sasa bwana anaposema wote watakunguzwazwa usiku ule kwaajili yake unaweza kupata picha ya mtu anayezungumzwa kwa kujiamini kuwa HATA WAJAPOKUNGUWAZWA WOTE LAKINI SIO MIMI, yaani Petro alikuwa ana uhakika ambao haukuwa na shaka ndani yake kuwa yeye anaweza kuwa tayari kwenda na Yesu gerezani, yeye anaweza kumtetea Yesu, yuko tayari hata kufa naye, na hata kama wanafunzi wengine wote watamkimbia Yesu na kumkana jambo kama hilo sio rahisi kwake Petro alizungumza kwa kujiamini sana, huku akiwa na ujasiri uliopitiliza, akijiona yeye ana kitu cha ziada na wengine ni wadhaifu, alijitumaini nafsi yake na akili zake, Watu wanaojifikiria kuwa wao ni wajanja na wenye akili na ujuzi kuliko wengine mara nyingi ndio ambao wakati mwingine hawafai kwa lolote  high self-esteem was also linked to a higher frequency of violent and aggressive behaviours , Watu wanaojiamini kupita kawaida wakati mwingine ndio hujiweka katika nafasi kubwa ya kukosea na kuharibu kabisa,  na wakati mwingine inaongoza katika uharibifu muwa wa mahusiano ya kila aina, kujiamini sio kitu kibaya kwani wakati mwingine kinaongoza katika aina Fulani ya mafanikio, lakini katika mazingira mengine kujiamini kupita kawaida kunatuletea udanganyifu wa moyo, unaweza kujikuta unajikweza kupita kawaida, au unaahidi kitu ambacho hauna uwezo nacho au uwezo wa kukitekeleza,  na Yesu alikuwa anamuelewa Petro alipojipambanua kuwa HATA WAJAPOKUNGUWAZWA WOTE LAKINI SIO MIMI Yesu alikuwa anamuona kuwa usiku ule hata kabla ya kuwika jogoo jamaa atamkana Yesu mara tatu

Luka 22:33-34.” Akamwambia, Bwana, niwapo pamoja nawe, mimi ni tayari kwenda gerezani au hata kifoni. Akasema, Nakuambia, Petro, jogoo hatawika leo, kabla wewe hujanikana mara tatu ya kuwa hunijui.”

Mambo muhimu ya kujifunza

Ni makossa makubwa sana kufikiri au kuamini kuwa njia yako ya kufikiri na kutenda iko juu sana kuliko wengine, au kufikiri kuwa wewe ndiye uko sahihi wakati wote, watu wengi wamefunga mlango wa kupokea mawazo yaw engine na kunufaika na ushauri wa watu wengine  kwa sababu wamefikiri kuwa wao ni bora kuliko wengine na wamedhani wengine ni dhaifu, kufikiri hivyo ni kuona maluwe luwe tu kama Petro maluluwe luwe haya yanaweza kukufikirisha kuwa wewe huwezi kukosea na hutakuja kukosea huku ni kujiamini kuliko pitiliza, Petro alikuwa akimthibitishia Yesu kuwa yeye atakuwa pamoja naye kwa gharama yoyote ile, hakuwa amejua kuwa Yesu ni Mungu na kuwa Mungu anamuona,

Wako watu wa namna kama ya Petro ambao wanajiamini kupita kawaida, wanafikiri kuwa wanamjua yesu kwa ukaribu kuliko yeyote, wanamjua Mungu kuliko wengine, wana mafundisho sahihi kuliko wengine , wana dhehebu zuri kuliko wengine, wana uzoefu na Mungu kuliko wengine, wana ni hadari, ni waombaji, ni watoaji, wako mstari wa mbele katika utumishi, wanaomba sana, wanafunza sana, wamefanikiwa sana na pengine hawana dhambi au hawawezi hata kuanguka, wao wamenyooka kuliko wengine, wao wana nidhamu kuliko wengine, wao waaakili kuliko wengine, Mtazamo wa aina hii hauwezi kukubalika na Yesu,  maandiko yanaonya wazi wazi kila ajidhaniae ya kuwa amesimama na aangalie asianguke

-          1Wakorintho 10:11-12 “Basi mambo hayo yaliwapata wao kwa jinsi ya mifano, yakaandikwa ili kutuonya sisi, tuliofikiliwa na miisho ya zamani. Kwa hiyo anayejidhania kuwa amesimama na aangalie asianguke.”

 

Onyo linatolewa kwa kila Mkrito na mafunzo yanaelekezwa kwetu kwamba wakati wote tusijifikiri kuwa sisi ni bora kuliko wengine, Waandishi wa habari nchini Marekani waliwahi kumuuliza Billy Gharamu kwamba ana maoni gani kuhusu anguko la Muhubiri mwenzake aitwaye Jimmy Swaggat Grahamu alijibu kama swaggart ameanguka mimi naweza kuanguka zaidi yake, Usifikiri wale wanao anguka kuwa hawampendi Mungu kama wewe, Mungu hapadezwi kabisa na kiburi, kiburi na majivuno na kujihesabia haki paee ni anguko tosha  ndio maana maandiko yanatuonya kuwahesabu wengine kuwa ni bora kuliko sisi

 

-          Wafilipi 2:3 “Msitende neno lo lote kwa kushindana wala kwa majivuno; bali kwa unyenyekevu, kila mtu na amhesabu mwenziwe kuwa bora kuliko nafsi yake.”

 

Maandiko yanataka wakati wote tujicheki wenyewe kwanza kabla ya kuacha kuwacheki wengine

 

-          Luka 6:41-42 “Basi, mbona wakitazama kibanzi kilicho ndani ya jicho la ndugu yako, na boriti iliyo ndani ya jicho lako mwenyewe huiangalii? Au, utawezaje kumwambia ndugu yako, Ndugu yangu, niache nikitoe kibanzi kilicho ndani ya jicho lako, nawe huiangalii boriti iliyo ndani ya jicho lako mwenyewe? Mnafiki wewe, itoe kwanza ile boriti katika jicho lako mwenyewe, ndipo utakapoona vema kukitoa kile kibanzi kilichomo katika jicho la ndugu yako.”

 

Mungu atasimama hukumuni na kila mtu anayejifikiri kuwa ana haki inayotokana na juhudi zake, kiufupi maandiko yanaonyesha kukataliwa n ahata kukemewa kwa watu wanaojifikiri kuwa wana ubora Fulani kuliko wengine

 

-          Luka 18:9-14 “Akawaambia mfano huu watu waliojikinai ya kuwa wao ni wenye haki, wakiwadharau wengine wote. Watu wawili walipanda kwenda hekaluni kusali, mmoja Farisayo, wa pili mtoza ushuru. Yule Farisayo akasimama akiomba hivi moyoni mwake; Ee Mungu, nakushukuru kwa kuwa mimi si kama watu wengine, wanyang'anyi, wadhalimu, wazinzi, wala kama huyu mtoza ushuru. Mimi nafunga mara mbili kwa juma; hutoa zaka katika mapato yangu yote. Lakini yule mtoza ushuru alisimama mbali, wala hakuthubutu hata kuinua macho yake mbinguni, bali alijipiga-piga kifua akisema, Ee Mungu, uniwie radhi mimi mwenye dhambi. Nawaambia, huyu alishuka kwenda nyumbani kwake amehesabiwa haki kuliko yule; kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa.”

 

-          Isaya 65:5 “watu wasemao, Simama peke yako, usinikaribie mimi, kwa maana mimi ni mtakatifu kuliko wewe; watu hao ni moshi puani mwangu, moto uwakao mchana kutwa.”

 

Wako watu duniani ambao kwa vipimo vyao vya kibinadamu hufikiri kuwa wana haki kuliko wengine kwa sababu ya juhudi zao,  na hivyo wanashindwa kuona asili yao ya dhambi,  na kutokustahili kwao, hawajui kwamba bila msaada wa Mungu hatuwezi lolote, na kuwa wakati wote tunahitaji rehema za Mungu, neema na msaada wake, kwa sababu ya matendo yao ya nje na wema wa kinafiki wa kujionyesha na kukandamiza wengine wakiwashutumu kuwa ni wenye dhambi na wao ni watakatifu, ni dhaifu na waio ni wenye nguvu, hawana msimamo na wao ndio wanaostahili, ni dhana ya aina hii ndio ilitompoza Petro akidhani ya kuwa yeye ni mwenye nguvu na sio dhaifu kama wanafunzi wengine hili ndio tatizo kuwa la watu wengi wa Mungu, kudhani kuwa wao ndio wao.

 

Nabii Eliya aliwahi kujiamini na kujifikiri kua katika Israel Nzima watu wote wameabudu sanamu na kusujudia mabaali alifikiri amebaki yeye peke yake na kwa kiburi chake alijieleza mbele za Mungu kuwa amesalia yeye peke yake, ona  

 

1Wafalme 19:9-10. “Akafika kunako pango, akalala ndani yake. Na tazama, neno la Bwana likamjia, naye akamwambia, Unafanya nini hapa, Eliya? Akasema, Nimeona wivu mwingi kwa ajili ya Bwana Mungu wa majeshi; kwa kuwa wana wa Israeli wameyaacha maagano yako, na kuzivunja madhabahu zako, na kuwaua manabii wako kwa upanga; nami nimesalia, mimi peke yangu; nao wanitafuta roho yangu, waiondoe.”

 

Warumi 11:2-4 “Mungu hakuwasukumia mbali watu wake aliowajua tokea awali. Au hamjui yale yaliyonenwa na maandiko juu ya Eliya? Jinsi anavyowashitaki Waisraeli mbele za Mungu, Bwana, wamewaua manabii wako, wamezibomoa madhabahu zako, nami nimesalia peke yangu, nao wananitafuta roho yangu. Lakini ile jawabu ya Mungu yamwambiaje? Nimejisazia watu elfu saba wasiopiga goti mbele ya Baali.”

 

Mungu alitaka kushughulika na kiburi cha Eliya aliwashitaki watu wa Mungu kana kwamba wote wameasi na wote hakuna aliyesalia ila yeye peke yake, watu wa Mungu hawashitakiwi, Mungu alimjibu kuwa anao wengine elfu saba wala hawajapiga goti lao kwa baaali, unapokuwa na kiburi unajiona uko katika ulimwengu wa pake yako, unauona umashuhuri wako wewe mwenyewe lakini Mungu anaiona mioyo, tuache kujiamini kupitiliza, na badala yake wakati wote tuombe Mungu atupe unyenyekevu, ujumbe mkubwa katika pasaka hii ni kutembea kwa unyenyekevu, Petro alijiamini aliona kuwa yeye hawezi kukosea Lakini Yesu alimwambia hata kabla ya kuwika jogoo utanikana mara tatu!     

Ni Petro tena yule yule aliyehitaji kufundishwa tena kuhusu kuwahubiri mataifa, kitendo chake cha kuwa myahudi alifikiri hana kibali cha kuwahubiri mataifa, akijiamini tena kupita kawaida kwamba Wayahudi ni safi na mataifa ni najisi, na katika moyo wake aliwaita mataifa najisi Ni Mungu tena alimkemea Petro kuwa kilichotakaswa na Mungu usikiite wewe najisi

 

Matendo 11:8-9. “Nikasema, Hasha, Bwana, kwa maana kitu kilicho kichafu au kilicho najisi hakijaingia kabisa kinywani mwangu. Sauti ikanijibu mara ya pili kutoka mbinguni, Alivyovitakasa Mungu, usivinene wewe najisi.”

 

Wakati wote lazima tukumbuke kuwa chochote ambacho Mungu ametujaalia ni kwa neema yake na sio vinginevyo, juhudi zetu na jitihada binafsi hazina kitu cha ziada cha kutusaidia, tutembee kwa unyenyekevu mbele za Mungu na kuacha kiburi na majivuno na kila tunapozungumza tuweke akiba ya maneno kumbuka Mungu huwapinga wajikwezao bali huwapa wanyenyekevu neema alisema Petro

 

1Petro 5:5Vivyo hivyo ninyi vijana, watiini wazee. Naam, ninyi nyote jifungeni unyenyekevu, mpate kuhudumiana; kwa sababu Mungu huwapinga wenye kiburi, lakini huwapa wanyenyekevu neema.”   

 

Yakobo 4:6 “Lakini hutujalia sisi neema iliyozidi; kwa hiyo husema, Mungu huwapinga wajikuzao, bali huwapa neema wanyenyekevu.”

 

“Hata wajapokunguwaa wote lakini sio Mimi alisema petro kwa kujiamini kumbe atamkana Yesu mara tatu tena kwa kuapia”

 

 

Na Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni