Jumapili, 7 Aprili 2024

Mpaka mlima wa Mizeituni!


Luka 22:39-44 “Akatoka akaenda mpaka mlima wa Mizeituni kama ilivyokuwa desturi yake; wanafunzi wake nao wakafuatana naye. Alipofika mahali pale aliwaambia, Ombeni kwamba msiingie majaribuni. Mwenyewe akajitenga nao kama kiasi cha kutupa jiwe, akapiga magoti akaomba, akisema, Ee Baba, ikiwa ni mapenzi yako, uniondolee kikombe hiki; walakini si mapenzi yangu, bali yako yatendeke. Malaika kutoka mbinguni akamtokea akamtia nguvu. Naye kwa vile alivyokuwa katika dhiki, akazidi sana kuomba; hari yake ikawa kama matone ya damu yakidondoka nchini.]



Utangulizi:

Katika msimu huu wa Pasaka bado tunaendelea kujifunza maswala kadhaa muhimu na madogo madogo, ambayo wakati mwingine kwa sababu ya kutazama mfumo mzima wa mateso ya Bwana tunaweza kujikuta ni kama tunayapuuzia, lakini yana umuhimu Mkubwa, leo nataka kuzungumzia kile ambacho kimejitokeza katika Mlima wa Mizeituni sehemu iitwayo Gethsemane na kuhusiana na tukio zima la Yesu Kristo kuwa na huzuni na kuingia katika maombi lakini zaidi sana hari yake kuwa kama matone ya damu.  Mahali hapa muhimu panaitwa Mlima wa Mizeituni, lakini vilevile sehemu muhimu ya mlima huu wa mizeituni pia panajulikana kama Bustani iitwayo Gethsemane.  

Mathayo 26:36-39 “Kisha Yesu akaenda pamoja nao mpaka bustani iitwayo Gethsemane, akawaambia wanafunzi wake, Ketini hapa, hata niende kule nikaombe. Akamchukua Petro na wale wana wawili wa Zebedayo, akaanza kuhuzunika na kusononeka. Ndipo akawaambia, Roho yangu ina huzuni nyingi kiasi cha kufa; kaeni hapa, mkeshe pamoja nami. Akaendelea mbele kidogo, akaanguka kifulifuli, akaomba, akisema, Baba yangu, ikiwezekana, kikombe hiki kiniepuke; walakini si kama nitakavyo mimi, bali kama utakavyo wewe.”

Mahali hapo ndio mahali ambapo kimsingi tunaweza kusema ushindi halisi wa Msalaba ulikoanzia, akiwa hapo kumbuka kuwa msaliti ndio alikuwa amekwenda kuwaleta maadui wa kumkamata Yesu, Hapa ndio mahali ambapo, Pia angekamatwa, hapa ndio mahali ambapo angeweza kukata tamaa, hapa ndio mahali ambapo alihitaji msaada wa Mungu, Malaika na wanadamu, Ndipo mahali ambapo angehitaji maombi kutoka kwa wenzake wa karibu ambao kimsingi walilala, hapa ndipo mahali ambapo wale walioahidi kwenda naye gerezani na hata kuwa tayari kufa naye walimkimbia, Hapa ndio mahali ambapo alizidiwa na msongo wa mawazo, hapa ndipo mahali ambapo shetani alisema naye kuhusu msalaba kama anaweza kuukabili au kukinywea kikombe cha mateso, hapa ndio mahali ambapo mipango ya adui iliyokuwa mibaya ilikuwa inaenda kufanikiwa, Ndipo mahali ambapo alitiwa nguvu na kukubaliana kuukabili Msalaba, Kimsingi ni kama Yesu alikuwa hapa katika chumba cha wangonjwa mahututi, mgonjwa ambaye anapambania uhai wake aishi ama afe na kisha mgonjwa anakubali kifo kwa Amani, kwa hiyo mlima wa mizeituni, Bustani ya Gethsemane ni eneo la maamuzi magumu. Ni eneo ambalo wakati na Muda muafaka wa ukombozi wa mwanadamu unaenda kuanza, ni eneo la mapito ya moyoni. Na ya kihisia, na ya hofu na ya kutisha zaidi kuliko hata msalaba wenyewe. Kila mwanadamu katika maisha yake huwa anapitia katika bustani hii, kwa namna moja ama nyingine, ni mahali ambapo tunapaswa kuruhusu Mapenzi ya Mungu yatimizwe! Tunajifunza somo hili, Mpaka mlima wa Mizeituni kwa kuzingatia vipengele viwili vifuatavyo:-

 

·         Mlima wa Mizeituni, Bustani iitwayo Gethsemane

·         Mpaka mlima wa Mizeituni

 

Mlima wa Mizeituni, Bustani iitwayo Gethsemane

Ni Muhimu kufahamu kuwa Neno la Mungu, limekuja kwetu kwa uweza wa Roho Mtakatifu, na Ni Roho huyu wa Mungu aliyewaongoza waandishi kuweka rekodi hizi kwa kusudi la kutufundisha maswala mbali mbali. Katika injili zote tunaona wakiwa wameelezea kuhusiana na Mahali hapa alipokamatwa Yesu, Pakiwa panajulikana kama mlima wa Mizeituni, au bustani ya Gethsemane lakini pia panaitwa Mahali pale, Kama ilivyo umuhimu wa Golgotha au Kalvari, Mlima wa Mizeituni na hasa hapo Gethsemane pana umuhimu mkubwa sana katika safari ya ukombozi wa mwanadamu.

Mathayo 26:30 “Nao walipokwisha kuimba, wakatoka nje kwenda mlima wa Mizeituni.”

Luka 22:39 “Akatoka akaenda mpaka mlima wa Mizeituni kama ilivyokuwa desturi yake; wanafunzi wake nao wakafuatana naye.”

Marko 14:26 “Nao walipokwisha kuimba walitoka kwenda mlima wa Mizeituni.”

Kwa hiyo tunaona Injili zote zikitaja habari za Mlima wa Mizeituni, Ni mlima maarufu na wa zamani sana una ukubwa wa kama kilomita mbili hivi, mlima huu uko upande wa Mashariki mwa mji wa Yerusalem, Mlima huu una urefu wa mita 78 au futi 250 ni mrefu kuliko mlima wa hekalu, na hivyo ni eneo zuri ambalo unaweza kukaa na kuliangalia hekalu vizuri, Yesu alipenda kuutumia mlima huu kwa maombi, kwa hiyo palikuwa ni mahali ambapo alipendelea kupatembelea mara kwa mara akiwa Yerusalem na alitumia mlima huo kufanya maombi, mlima unaitwa mlima wa mizeituni kwa sababu unafunikwa na miti hiyo ya mizeituni na kulifanya eneo hilo kupendeza kwa ukijani wa Miti hiyo, Mahali hapa Ndipo mahali ambapo Yesu alipatumia kupaa mbinguni angalia

Matendo 1:9-12 “Akiisha kusema hayo, walipokuwa wakitazama, akainuliwa, wingu likampokea kutoka machoni pao. Walipokuwa wakikaza macho mbinguni, yeye alipokuwa akienda zake, tazama, watu wawili wakasimama karibu nao, wenye nguo nyeupe, wakasema, Enyi watu wa Galilaya, mbona mmesimama mkitazama mbinguni? Huyu Yesu aliyechukuliwa kutoka kwenu kwenda juu mbinguni, atakuja jinsi iyo hiyo mlivyomwona akienda zake mbinguni. Kisha wakarudi kwenda Yerusalemu kutoka mlima ulioitwa wa Mizeituni, ulio karibu na Yerusalemu, wapata mwendo wa sabato.”

Na ni katika mlima huu huu Yesu atakaporudi atashukia hapo akitokea mbinguni na kufanya vita na Mpinga Kristo, na kusimamisha utawala wake, kwa hiyo Mlima huu ni mlima wa kihistoria katika ukombozi wa mwanadamu na utawala wa Mungu yaani ufalme wa Mungu.  

Zekaria 14:3-4 “Hapo ndipo atakapotokea Bwana, naye atapigana na mataifa hayo, kama vile alipopigana zamani siku ya vita. Na siku hiyo miguu yake itasimama juu ya mlima wa Mizeituni, unaoelekea Yerusalemu upande wa mashariki, nao mlima wa Mizeituni utapasuka katikati yake, upande wa mashariki na upande wa magharibi; litakuwako huko bonde kubwa sana; na nusu ya mlima ule utaondoka kwenda upande wa kaskazini, na nusu yake itaondoka kwenda upande wa kusini.”

Kwa hiyo mlima wa mizeituni ni mahali, muhimu sana katika unabii na historia nzima ya ukombozi wa mwanadamu na kusimama kwa serikali ya kiungu yaani ufalme wa Mbinguni, kwa msingi huo Yesu hakwenda tu katika mlima wa mizeituni kwa bahati mbaya, katika eneo hili la Mlima wa Mizeituni juu ilikuweko sehemu ambayo ilikuwa na bustani nzuri na sehemu hiyo iliitwa Gethsemane, kwa hiyo utaweza kuona tena waandishi wa Injili wakiitaja sehemu hiyo angalia tena katika neno la Mungu hususani baadi ya vitavu vya injili.

Mathayo 26:36 “Kisha Yesu akaenda pamoja nao mpaka bustani iitwayo Gethsemane, akawaambia wanafunzi wake, Ketini hapa, hata niende kule nikaombe.”

Marko 14:32 “Kisha wakaja mpaka bustani iitwayo Gethsemane; akawaambia wanafunzi wake, Ketini hapa muda niombapo.”      

Kwa hiyo katika mlima huo wa mizeituni vilevile kulikuwako bustani ambayo iliitwa Gethsemane na Luka anapaita mahali pale hii ni kwa sababu mahali hapo palikuwa ni maarufu sana hata leo

Luka 22:40 “Alipofika mahali pale aliwaambia, Ombeni kwamba msiingie majaribuni.”

Kwa Msingi huo ni muhimu kufahamu kuwa eneo hili muhimu katika historia ya ukombozi wa mwanadamu, linaitwa Mlima wa Mizeituni, lakini Pia Bustani ya Gethsemane, lakini Luka anapaita mahali pale, na kuonyesha kuwa Yesu alikuwa na desturi ya kwenda katika eneo hilo mara kadhaa, eneo hili kwa maelezo ya kale na katika injili ya Yohana palikuwa ng’ambo ya kijito Kedroni, ambapo ndipo bustani hii ilipokuwepo na Yesu alipachagua kama mahali pa maombi unaweza kuona

Yohana 18:1 “Alipokwisha kusema hayo, Yesu alitoka pamoja na wanafunzi wake kwenda ng'ambo ya kijito Kedroni, palipokuwapo bustani; akaingia yeye na wanafunzi wake.”

Eneo hili linaloitwa GETHSEMANE ambalo ni jina lenye asili ya Kiaram ambalo maana yake Sehemu ya kukamulia mafuta, (oil Press) kwa hiyo uko uwezekano ya kuwa katika bustani ile ya Mizeituni, kulikuweko na mashine za kukamulia mafuta ya zeituni,  na ndio sababu pakaitwa pia GETHSEMANE, lakini vile vile kwanini Luka anapaita MAHALI PALE, mahali hapo palikuwa na historia maarufu ya watu hasa Mfalme mkuu Daudi kwenda kuabudu, lakini sio hivyo tu Ni eneo ambalo Daudi aliposalitiwa na Mwanae Absalom alikimbia na kuvuka mto huu yeye na watu wake na wakapanda mlima huu wa mizeituni wakiwa wanalia sana, wakiwa hawana viatu na wakiwa wamejifunika nguo zao vichwani  mahali hapa kimsingi palikuwa na sehemu ambapo Mungu alikuwa akiabudiwa, Lakini Mfalme Daudi na watu wake walipanda mahali hapa wakiwa wamekata tamaa, wakiwa wanalia machozi, wakiwa hawajui mbele yao itakuwaje. Unaweza kuona katika andiko hili:-

2Samuel 15:30-32 “Daudi akapanda akishika njia ya kuupandia mlima wa Mizeituni, akilia alipokuwa akipanda; naye alikuwa amejifunika kichwa chake, akaenda hana viatu; na watu wote waliokuwa pamoja naye wakajifunika vichwa vyao, kila mmoja wao, wakapanda juu, wakilia walipopanda Mtu mmoja akamwambia Daudi ya kwamba, Ahithofeli yu katika hao waliopatana na Absalomu; Daudi akasema, Ee Bwana, nakusihi, uligeuze shauri la Ahithofeli liwe ubatili. Ikawa, Daudi alipofika juu, hapo Mungu alipoabudiwa, tazama, Hushai, Mwarki, akaja kumlaki na joho Lake Limeraruliwa, tena ana udongo kichwani mwake.               

Kwa hiyo unaweza kuona Gethsemane katika mlima wa mizeituni. Zaituni zilikamuliwa na zikatoa mafuta, lakini vilevile ulikuwa ni mlima wa kutoa machozi, Daudi na watu wake walipanda mlima huu huku wanalia, na Yesu alipanda mlima huu akiwa Analia, Daudi alipanda mlima huu akiwa amekata tamaa na kupoteza matumaini akiwa amesalitiwa na Mwanae Absalom na Yesu anapanda mlima huu akiwa amekata tamaa na anapoteza tumaini kuukabili Msalaba akiwa amesalitiwa na mmoja ya Mwanafunzi wake Muhimu, huku roho yake ikiwa ina huzuni mno

Mpaka mlima wa Mizeituni

Luka 22:39-44 “Akatoka akaenda mpaka mlima wa Mizeituni kama ilivyokuwa desturi yake; wanafunzi wake nao wakafuatana naye. Alipofika mahali pale aliwaambia, Ombeni kwamba msiingie majaribuni. Mwenyewe akajitenga nao kama kiasi cha kutupa jiwe, akapiga magoti akaomba, akisema, Ee Baba, ikiwa ni mapenzi yako, uniondolee kikombe hiki; walakini si mapenzi yangu, bali yako yatendeke. Malaika kutoka mbinguni akamtokea akamtia nguvu. Naye kwa vile alivyokuwa katika dhiki, akazidi sana kuomba; hari yake ikawa kama matone ya damu yakidondoka nchini.]

Tunaona katika andiko letu la msingi kuwa Yesu akaenda pamoja na wanafunzi wake mpaka mlima wa mizeituni, Mahali hapa Yesu alikuwa ameelemewa na Huzuni, Huzuni kubwa kwa sababu anakabiliwa na kifo na sio kifo cha kawaida ni kifo cha msalaba, hakuna mauti mbaya kama mauti ya msalaba, katika historia za hukumu ya kifo, kila taifa lilikuwa lina namna yake ya kuua

Waingereza mtu alipohukumiwa kifo walitumia kitanzi, wakati warumi walitumia shoka lililotundikwa, na wayahudi walitumia kupiga mawe mpaka kifo, warumi walikuwa na hukumu nyingine ya kifo kwa raia asiyekuwa Mrumi ambayo ilikuwa ni kumtundika msalabani, kifo hiki kilikuwa ni kibaya zaidi kwa sababu ni mauti ya polepole, ilikuwa pia ni mauti ya aibu, kwa sababu watu walisulubiwa wakiwa tupu na kudhalilishwa, wayahudi waliamini kuwa Mungu hawezi kuruhusu mtu mwema kufa msalabani, mtu aliyehukumiwa kifo cha msalabani alihesabika kuwa amelaaniwa,

Wagalatia 3:13-14 “Kristo alitukomboa katika laana ya torati, kwa kuwa alifanywa laana kwa ajili yetu; maana imeandikwa, Amelaaniwa kila mtu aangikwaye juu ya mti; ili kwamba baraka ya Ibrahimu iwafikilie Mataifa katika Yesu Kristo, tupate kupokea ahadi ya Roho kwa njia ya imani.”

Kwa hiyo katika mawazo ya Kristo kama Mwana wa Mariam yaani kibinadamu mauti hii ilikuwa ni ya kuiepuka, angetamani sana kikombe hiki kimuepuka aliomba kwa hisia kali sana na hapa alikuwa amejawa na msongo wa mawazo, na ni katika eneo hilo hilo ambapo zaituni zilikuwa zinakamuliwa Yesu alikamuliwa na msongo wa mawazo, kiasi cha kutoka jasho (Hari) la damu, tukio hili kisayansi linaitwa Agony – ambalo maana yake ni Msongo mkubwa wa mawazo unaoathiri hali halisi ya mwili kiasi cha mishipa ya damu kuzidiwa na kupanuka kwa vinyeleo na kuruhusu jasho na damu kutoka, tukio hili liliweza kuelezewa na Luka pekee kwa vile yeye alikuwa tabibu, Kwa hiyo Yesu alikuwa ameleemewa na huzuni kubwa kwa sababu aina ya mateso ilikuwa mbaya kubebeka, na malaika walikuja kumtia nguvu kuwa anapaswa kubeba, kwa hiyo tunapata picha hii Yesu alipokuwa Gethsemane

-          Ni mahali ambapo mtu anaelemewa na huzuni kubwa na msongo mkubwa wa mawazo

-          Ni mahali ambapo mtu anakuwa amesalitiwa na kuachwa peke yake

-          Ni mahali ambapo unajaribu kuomba msaada watu hata wakuombee na wanalala

-          Ni mahali ambapo mtu unakata tamaa na kupoteza matumaini

-          Ni mahali ambapo unaweza kuchanganyikiwa kwa sababu mipango ya adui ndiyo inayokwenda kufanikiwa

-          Ni mahali ambapo ni kama Mungu anasikia maombi ya adui zako na mipango yao na ya kwako haisikiwi

-          Ni mahali ambapo hakuna faraja kutoka upande wowote

-          Ni mahali ambapo shetani angependa ubaki hapo ili akulize akukamue

-          Ni mahali ambapo manabii walipanda wakiwa wanalia, machozi wamekata tamaa

-          Ni mahali ambapo Imani yako inakamuliwa ili ikiwezekana iishe na urudie hapo

-          Ni mahali ambapo pamejaa mashaka na marafiki wamekuacha peke yako

-          Ni mahali ambapo ni kama uko chumba cha wagonjwa mahututi na unaota ndoto za kugombea uhai au kifo

-          Ni mahali ambapo huwezi kuamua mambo, na mambo yako yanaamuliwa na adui zako

-          Ni mahali ambapo unachokiona mbele yako ni kifo tu maombi hayajibiwi

-          Ni mahali ambapo ni kama maamuzi yamepita na huwezi hata kukata rufaa tena

-          Ni mahali ambapo utatiwa mikononi mwa adui na rafiki zako wote watakukimbia

-          Ni mahali ambapo unakutana na vita ya kiakili, kihisia na kiroho, na ni mahali pa maamuzi magumu!

Mungu katika hekima yake huruhusu nyakati Fulani na sisi katika maisha yetu tupite tupande mpaka mlima wa Mizeituni, tuende mpaka Gethsemane tukakamuliwe huko, tukalizwe huko, akili zetu zizungumze na shetani, huku Mungu akiwa kimyaa, Katika hali ya kawaida wakati wa mapito na mateso huwa hauonekani kuwa ni wakati mzuri, unakuwa ni wakati wa kukamuliwa, unakuwa ni wakati wa taarifa mbaya, unakuwa ni wakati wa kuamua kufanya mapenzi ya Mungu au kuyaacha taarifa njema ni kuwa Yesu hakukata tamaa, Yesu hakuvunjika moyo na malaika wa Bwana walikuja kumtia nguvu na akawa yuko tayari kuyakabili mateso ya Msalaba, Daudi alilia katika mlima huu, lakini alifanikiwa kujipanga na kukabiliana na Absalom na Mungu alimpa ushindi, Mungu alijibu maombi ya Yesu kwa kumtia nguvu aukabili Msalaba lakini alijua ya kuwa siku ya tatu atamfufua na kumpeleka katika maisha yasiyozuilika  Ushindi wa maisha yetu na furaha ya kweli hupatikana, pia kwa kupitia njia ya mateso,  tumepewa sio kumwamini tu bali na kuteswa kwaajili yake

Wafilipi 1:28-29 “wala hamwaogopi adui zenu, katika neno lo lote; kwao hao ni ishara mathubuti ya kupotea, bali kwenu ninyi ni ishara ya wokovu, huo utokao kwa Mungu. Maana mmepewa kwa ajili ya Kristo, si kumwamini tu, ila na kuteswa kwa ajili yake;”                

Mungu atatuacha tupite katika wakati Mgumu, ambao utatuletea ushindi mkubwa sana na hivyo hatupaswi kuogopa tunapopita Gethsemane wakati ambapo umeachwa peke yako na hakuna wa kukushika mkono usiogope Yesu Kristo anaijua njia hiyo na ni yeye aliyesema Twendeni mpaka mlima wa mizeituni mlima huu sio wa mateso pekee bali ni mlima wa ushindi, ni mlima wa mahali ambapo sio Yesu atakamatwa tu, na kugongwa kisigino, lakini ni mahali ambapo Yesu atakanyaga tena na mlima huu utapasuka na watachinjiliwa mbali adui zake ni mlima ambapo ufalme wa Mungu utastawi, kumbuka muda wa kupita hapa sio mrefu ni mfupi sana

1Petro 5:8-11 “Mwe na kiasi na kukesha; kwa kuwa mshitaki wenu Ibilisi, kama simba angurumaye, huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze. Nanyi mpingeni huyo, mkiwa thabiti katika imani, mkijua ya kuwa mateso yale yale yanatimizwa kwa ndugu zenu walioko duniani. Na Mungu wa neema yote, aliyewaita kuingia katika utukufu wake wa milele katika Kristo, mkiisha kuteswa kwa muda kidogo, yeye mwenyewe atawatengeneza, na kuwathibitisha, na kuwatia nguvu. Uweza una yeye hata milele na milele. Amina.”

Baada ya mateso ya kihisia pale Gethsemane Yesu alitiwa nguvu kuukabili Msalaba, alikwenda msalabani na alipitia dhihaka na mateso akiwa ana utulivu mkubwa sana akijua faida ya mateso yale na kufufuka kwake

-          Alikuwa na nguvu ya kuwaombea maadui zake

-          Alikuwa na nguvu ya kuruhusu majambazi waende peponi

-          Alikuwa na nguvu ya kutangaza kuwa kazi ya ukombozi umekamilika

-          Alikuwa na nguvu ya kukabidhi roho yake kwa Amani akijua ya kuwa Baba yake atamfufua

-          Alikuwa na nguvu ya kuruhusu pazia la hekalu kupasuka na watu kuifikia neema ya Mungu

-          Alikuwa na nguvu ya kufufua watu waliokufa zamani na miili yao kuonekana kwa muda

-          Alikuwa na nguvu dhidi ya Mauti akitupa waamini wote tumaini kubwa lenye Baraka

-          Alikuwa na nguvu ya kusamehe dhambi

-          Alikuwa na nguvu ya kututhibitishia na kutuhakikishia wokovu

-          Alikuwa na nguvu ya kubadilisha maisha ya watu na kuleta mabadiliko makubwa katika jamii zote duniani

-          Alikuwa na nguvu ya kutioa faraja na tumaini kiasi cha kumuwezesha kila mtu kuwa tayari kufa kama yeye

-          Alikuwa na nguvu na mamlaka yote mbinguni na duniani

-          Alikuwa anamejithibitishia kuwa atarudi tena na kukanyaga mlima wa mizeituni

-          Alikuwa na nguvu ya kuwafanya adui zake na wote waliokuwa wakimtesa walikiri hakika alikuwa mwema

Ushindi wote huo hapo juu ni kwa sababu Pale Gethsemane Yesu alikubali Mapenzi ya Mungu, kwamba hata tunapopitia katika njia zilizo ngumu sana hatuachi kuomba tunaomba na baba akiwa kimya tunakubali mapenzi yake yatimizwe

Luka 22:41-43. “Mwenyewe akajitenga nao kama kiasi cha kutupa jiwe, akapiga magoti akaomba, akisema, Ee Baba, ikiwa ni mapenzi yako, uniondolee kikombe hiki; walakini si mapenzi yangu, bali yako yatendeke. Malaika kutoka mbinguni akamtokea akamtia nguvu.”  

Ni pale Gethsemane ndipo Yesu alipotengeneza nguvu ya kukabiliana na hali zote zilizokuwa mbele yake kumbuka alisema ombeni kusudi msiingie majaribuni, aliweza kuyashinda majaribu yote na malaika wa Bwana walikuja kumtia nguvu

Ni pale Gethsemane ndipo Yesu alipoonja hisia na mateso yetu ya kibinadamu tunapokuwa taabuni alionyesha uanadamu wake na sisi tunapopita katika majaribu makali anaujua uanadamu wetu, Ni hapa ndipo wanafunzi wa Yesu walipofahamu umuhimu wa maombi, ni hapa ndipo alipowafundisha namna wanavyoweza kukabiliana na ushindi wanapokuwa matatani.

Mathayo 26:41 “Kesheni, mwombe, msije mkaingia majaribuni; roho i radhi, lakini mwili ni dhaifu.”

Ni pale Gethsemane ndipo Yesu alionyesha kuwa kweli yeye ni Mpakwa mafuta kwa sababu alikubali kuukabili msalaba bila vurumai yoyote aliukabili msalaba kwa upole na unyenyekevu mkubwa

Isaya 53:3-7 “Alidharauliwa na kukataliwa na watu; Mtu wa huzuni nyingi, ajuaye sikitiko; Na kama mtu ambaye watu humficha nyuso zao, Alidharauliwa wala hatukumhesabu kuwa kitu. Hakika ameyachukua masikitiko yetu, Amejitwika huzuni zetu; Lakini tulimdhania ya kuwa amepigwa, Amepigwa na Mungu, na kuteswa. Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, Alichubuliwa kwa maovu yetu; Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona. Sisi sote kama kondoo tumepotea; Kila mmoja wetu amegeukia njia yake mwenyewe; Na Bwana ameweka juu yake Maovu yetu sisi sote. Alionewa, lakini alinyenyekea, Wala hakufunua kinywa chake; Kama mwana-kondoo apelekwaye machinjoni, Na kama vile kondoo anyamazavyo Mbele yao wakatao manyoya yake; Naam, hakufunua kinywa chake.”

Ni pale Gethsemane Ndipo Yesu alipoanza harakati za ukombozi wa mwanadamu kwa kukabiliana na matukio yote kuanzia mahakamani, kusulubiwa kufa na kufufuka akiwa sadaka kamili ya upatanisho na msamaha wa dhambi zetu akitupatanisha sisi na Mungu

1Timotheo 2:5-6 “Kwa sababu Mungu ni mmoja, na mpatanishi kati ya Mungu na wanadamu ni mmoja, Mwanadamu Kristo Yesu; ambaye alijitoa mwenyewe kuwa ukombozi kwa ajili ya wote, utakaoshuhudiwa kwa majira yake.”

Ni Gethsemane ndipo Yesu alipoandaa ukamilisho wa eneo muhimu la huduma yake duniani akionyesha kumtii Mungu hata mauti ya msalaba, akiwa tayari kukamilisha mapenzi ya Mungu, huruma zake kubwa kwa wanadamu na wajibu wake mkubwa kama mwokozi wa ulimwengu jambo ambalo limemletea sifa kubwa sana Mbinguni

Wafilipi 2:5-11 “Iweni na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo Yesu; ambaye yeye mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu; tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba. Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina; ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi; na kila ulimi ukiri ya kuwa YESU KRISTO NI BWANA, kwa utukufu wa Mungu Baba.”

Ndugu msomaji wangu, kumbuka wakati wote unapopitia mateso, ni kama uko Gethsemane, ni kama Mwalimu amekuambia upande mlima wa mizeituni, utakuwepo kwa Muda mfupi na ukimtii Mungu katika wakati huo Mungu, atakupeleka katika maisha ya Gethsemane, na kukupeleka katika maisha yasiyoweza kuzuilika, wote sasa tunaweza kuona umuhimu wa mlima wa mizeituni na eneo la Gethsemane, tunajifunza kujitia nguvu katika Bwana, kuwa na ujasiri na utayari wa kukabiliaba na mambo magumu ambayo kwa kawaida Mungu huyafupiza sana lakini hutupa matokeo mazuri sana tunapokuwa tumeyatii mapenzi yake. Mungu akutie nguvu wakati wote unapopanda mlima wa mizeituni na kupita eneo la kukamuliwa, Malaika wa bwana watakutia nguvu utakuwa na moyo wa ujasiri na utashinda na kuwa msaada mkubwa kwa ulimwengu unaokuzunguka Uongezewe neema!

 

Na. Rev. Mkombozi Innocent Samuel bin Jumaa bin Athumani Sekivunga Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni