Jumapili, 31 Machi 2024

Maisha yasiyozuilika!


Ufunuo 1:17-18 “Nami nilipomwona, nalianguka miguuni pake kama mtu aliyekufa. Akaweka mkono wake wa kuume juu yangu, akisema, Usiogope, Mimi ni wa kwanza na wa mwisho, na aliye hai; nami nalikuwa nimekufa, na tazama, ni hai hata milele na milele. Nami ninazo funguo za mauti, na za kuzimu.”     




Utangulizi:

Leo ni sikukuu ya Pasaka, ambapo wakristo nchini wanaungana na wakristo wote duniani kuadhimisha kuteswa, kufa na kufufuka kwa Bwana wetu Yesu Kristo kulikotokea zaidi ya miaka 2000 iliyopita Huko Yerusalem Nchini Israel, Katika wakati huu wa Pasaka Leo ni Muhimu kujikumbusha kuwa Mungu ametupa maisha yasiyozuilika, Kristo Yesu alipofufuka ametufundisha na kutukumbusha  kuwa kuna maisha yasiyozuilika, Yesu anatufundisha kupitia kufufuka kwake kuwa yako maisha yasiyozuilika,  na kuwa uko uwezekano wa kuishi maisha yasiyozuilika, Haya ni maisha ambayo Mungu alikusudia kila mmoja ayaishi katika ulimwengu huu ambao una vikwazo vingi sana, Lakini kama mtu akiwa na Yesu ataweza kuishi maisha yasiyoweza kuziilika!  Maisha yasiyozuilika ni maisha ya kushinda vikwazo:-

1Yohana 5:11-13 “Na huu ndio ushuhuda, ya kwamba Mungu alitupa uzima wa milele; na uzima huu umo katika Mwanawe. Yeye aliye naye Mwana, anao huo uzima; asiye naye Mwana wa Mungu hana huo uzima. Nimewaandikia ninyi mambo hayo, ili mjue ya kuwa mna uzima wa milele, ninyi mnaoliamini Jina la Mwana wa Mungu.”

Unaweza kujiuliza kuwa Mchungaji anataka kuzungumzia nini? Je maisha yasiyozuilika nini Ni uzima wa milele? Ama ni kitu gani na kwa vipi maisha hayo yana uhusiano na Yesu aliyefufuka?  Tutachukua muda kujifunza kwa ufupi na kwa kina ili tuweze kuelewa maisha hayo yasiyozuilika kwa kuzingatia vipengele viwili tu vifuatavyo:- 

·         Maana ya maisha yasiyozuilika

·         Maisha yasiyozuilika

Maana ya Maisha yasiyozuilika! 

Tunapozungumzia kuhusu Maisha yasiyozuilika, tunazungumzia kuwa na maisha yasiyo na mipaka, au maisha yanayoshinda vikwazo, maisha ya uhuru na na yaliyojaa neema ya Mungu inayotusaidia kufikia ndoto zetu huku tukishinda kila aina ya kikwazo kinachowekwa na shetani au wanadamu,  Maisha yanayoweza kuwa na ushindi, bila kujali nguvu kutoka nje inasema nini, Unapoyasoma maandiko yanaonyesha wazi kuwa Mpango wa Mungu kwa mwanadamu tangu mwanzo ilikuwa ni aina hii ya maisha na Yesu aliyefufuka anatukumbusha kupitia hatua yake ya kufufuka kuwa yako maisha yasiyozuilika!, Mapena na mara kadhaa Yesu alikuwa amesema atafufuka  na alisema kuwa atafufuka siku ya tatu na mpango huu Yesu alitaka ueleweke wazi kwa wanafunzi wake na hata kwa adui zake na ndio maana alirudia tena na tena maneno yake hayo ona:-

-          Mathayo 16:21-23 “Tangu wakati huo Yesu alianza kuwaonya wanafunzi wake ya kwamba imempasa kwenda Yerusalemu, na kupata mateso mengi kwa wazee na wakuu wa makuhani, na waandishi, na kuuawa, na siku ya tatu kufufuka. Petro akamchukua, akaanza kumkemea, akisema, Hasha, Bwana, hayo hayatakupata. Akageuka, akamwambia Petro, Nenda nyuma yangu, Shetani; u kikwazo kwangu; maana huyawazi yaliyo ya Mungu, bali ya wanadamu.”

 

-          Marko 8:31-32a “Akaanza kuwafundisha kwamba imempasa Mwana wa Adamu kupatikana na mateso mengi, na kukataliwa na wazee, na wakuu wa makuhani, na waandishi, na kuuawa, na baada ya siku tatu kufufuka. Naye alikuwa akinena neno hilo waziwazi.”

 

-          Luka 9:21-22 “Akawaonya, akawakataza wasimwambie mtu neno hilo; akisema, Imempasa Mwana wa Adamu kupata mateso mengi, na kukataliwa na wazee na wakuu wa makuhani na waandishi, na kuuawa na siku ya tatu kufufuka.”

 

-          Mathayo 17:22-23 “Nao walipokuwa wakikaa Galilaya, Yesu akawaambia, Mwana wa Adamu anakwenda kutiwa katika mikono ya watu, nao watamwua, na siku ya tatu atafufuka. Wakasikitika sana.”

 

-          Marko 9:30-32 “Wakatoka huko, wakapita katikati ya Galilaya; naye hakutaka mtu kujua. Kwa sababu alikuwa akiwafundisha wanafunzi wake, akawaambia, Mwana wa Adamu yuaenda kutiwa katika mikono ya watu, nao watamwua; hata akiisha kuuawa, baada ya siku tatu atafufuka. Lakini hawakulifahamu neno lile, wakaogopa kumwuliza.       

 

-          Luka 9:43-45 “Wote wakashangaa, wakiuona ukuu wa Mungu. Nao walipokuwa wakiyastaajabia mambo yote aliyoyafanya, aliwaambia wanafunzi wake, Yashikeni maneno haya masikioni mwenu, kwa kuwa Mwana wa Adamu anakwenda kutiwa katika mikono ya watu. Lakini hawakulifahamu neno lile, likafichwa kwao wasilitambue; wakaogopa kumwuliza maana yake neno lile.”

Kwa hiyo huu ulikuwa ni mpango wa Mungu, Na Bwana Yesu aliusema mapema kwamba kifo hakiwezi kumzuia, hakuna kitu kinaweza kuzuia mpango wake wa kufufuka kutoka kwa wafu, huu ndio ulikuwa ujumbe mkuu wa Yesu, Lakini katika namna ya kushangaza shetani pamoja na majeshi yake yote walikuwa na mpango wao wa kuzuia ili yamkini ikiwezekana Yesu asifufuke ona 

Mathayo 27:62-66 “Hata siku ya pili, ndiyo iliyo baada ya Maandalio, wakuu wa makuhani, na Mafarisayo wakamkusanyikia Pilato, wakasema, Bwana, tumekumbuka kwamba yule mjanja alisema, alipokuwa akali hai, Baada ya siku tatu nitafufuka. Basi amuru kwamba kaburi lilindwe salama hata siku ya tatu; wasije wanafunzi wake wakamwiba, na kuwaambia watu, Amefufuka katika wafu; na udanganyifu wa mwisho utapita ule wa kwanza. Pilato akawaambia, Mna askari; nendeni mkalilinde salama kadiri mjuavyo. Wakaenda, wakalilinda kaburi salama, kwa kulitia lile jiwe muhuri, pamoja na wale askari walinzi.”

Unaona njama zilipangwa na viongozi wa kidini wakishirikiana na serikali ya kirumi kuhakikisha kaburi la Yesu linalindwa salama, Kulindwa salama maana yake ni kulinda kwa uhakika, kuhakikisha kuwa hakuna linalobatilika, lindeni kwa kukakisha kuwa haibiwi, lindeni kwa kuhakikisha kuwa hafufuki!  Kwa hiyo wayahudi walitaka kuhakikisha Yesu anabaki kaburini na hatoki tena na hachomoki kabisa kutoka katiia mpango wake huo, walimuwekea ulinzi waliweka mipaka, waliweka kizuizi, walitaka kuakikisha kuwa hakubadiliki neno, Hata hivyo hawakujua kuwa Yesu aliishi maisha yasiyozuilika na hakuna kitu ambacho kingeweza kumzuia asitoke kaburini, hata kifo hakiwezi kumzuia na kumfanya abaki kaburini, Kristo alikuwa na maisha yasiyozuilika, na kifo kisingeliweza kumzuia hakuna cha kumzuia Yesu katika mpango wake.

Maisha yasiyozuilika    

Mathayo 28:1-7 “Hata sabato ilipokwisha, ikipambazuka siku ya kwanza ya juma, Mariamu Magdalene, na Mariamu yule wa pili, walikwenda kulitazama kaburi. Na tazama, palikuwa na tetemeko kubwa la nchi; kwa sababu malaika wa Bwana alishuka kutoka mbinguni, akaja akalivingirisha lile jiwe akalikalia. Na sura yake ilikuwa kama umeme, na mavazi yake meupe kama theluji. Na kwa kumwogopa, wale walinzi wakatetemeka, wakawa kama wafu. Malaika akajibu, akawaambia wale wanawake, Msiogope ninyi; kwa maana najua ya kuwa mnamtafuta Yesu aliyesulibiwa. Hayupo hapa; kwani amefufuka kama alivyosema. Njoni, mpatazame mahali alipolazwa. Nanyi nendeni upesi, mkawaambie wanafunzi wake, Amefufuka katika wafu. Tazama, awatangulia kwenda Galilaya; ndiko mtakakomwona. Haya, nimekwisha waambia.” 

Yesu alisema atafufuka, na wapinzani wake walitaka kuhakikisha kuwa Yesu hafufuki, waliweka walinzi katika kaburi lake, waliweka muhuri kuhakikisha kuwa hakuna neno linalobatilika lakini Yesu/Mungu akisema neno lake hakuna mtu anaweza kusimama kinyume na makusudi na mpango wa Mungu, Yesu alikuwa akituonyesha wazi kuwa tunaweza kuishi maisha yasiyozuilika, kila anaemwamini Yesu na kuiamini kazi aliyoifanya pale msalabani, atakuwa na maisha yasiyozuilika, sio kifo tu lakini kila kitu kinachojaribu kusimama kinyume na kile unachokusudia kukifanya, au biashara zako, au ndoa yako, au mafanikio yako, au kazi yako, au vyovyote vile, unapaswa kukumbuka kuwa Yesu anatuonyesha njia kuwa hakuna anayeweza kukuwekea mipaka katika maisha yako, Kristo aliyefufuka ni mfano mzuri wa maisha yasiozuilika, tangu mwanzo Mungu alikusudia kuwa watu wake wawe mashahidi wa kazi zake na wakati wote kazi zake na mpango wake hakuna anayeweza kuzuia 

Isaya 43:12-13 “Nimetangaza habari, nimeokoa, nimeonyesha, na hapakuwa mungu wa kigeni kati yenu; kwa sababu hiyo ninyi ni mashahidi wangu, asema Bwana, nami ni Mungu. Naam, tangu siku ya leo, mimi ndiye; wala hapana awezaye kuokoa katika mkono wangu; mimi nitatenda kazi, naye ni nani awezaye kuizuia?

Kufufuka kwa Yesu Kristo ndio ulikuwa ushindi mkubwa sana dhidi ya shetani maajenti wake na kazi zake zote, na ilikuwa ndio kilele cha utekelezaji wa kazi ya ukombozi wa Mwanadamu, kwa hiyo shetani alikuwa anataka kuzuia na kuiwekea mipaka kazi iliyofanywa na Bwana, wakati wote unapokaribia katika mafanikio yako, au inapokaribia kuwa Mungu anataka kubadilisa kabisa mpango wa maisha yako na kukuinua, Kuzimu inataharuki na itahakikisha inapambana na kuzuia  mpango wa Mungu katika maisha yako, wakati huo shetani anasahau kuwa Yesu amekupa maisha yasiyozuilika, Kila mtu aliyeokolewa yuko upande wa Mungu yuko na Bwana na Mungu ametupa maisha yasiyizuilika, Kama hakuna kitu cha kututenga na Upendo wa Mungu ni wazi vilevile kuwa hakuna kitu kitaweza kutuzuia katika jambo lolote lile zingatia kuwa Yesu aliyefufuka anaza mamlaka za mauti na kuzimu na zaidi ya yote yeye ndiye huo ufufuo na uzima sasa jaribu kuwaza na kifikiri nini kinaweza kuzuia maisha yako ? angalia maandiko:- 

Warumi 8:31-39 “Basi, tuseme nini juu ya hayo? Mungu akiwapo upande wetu, ni nani aliye juu yetu? Yeye asiyemwachilia Mwana wake mwenyewe, bali alimtoa kwa ajili yetu sisi sote, atakosaje kutukirimia na mambo yote pamoja naye? Ni nani atakayewashitaki wateule wa Mungu? Mungu ndiye mwenye kuwahesabia haki. Ni nani atakayewahukumia adhabu? Kristo Yesu ndiye aliyekufa; naam, na zaidi ya hayo, amefufuka katika wafu, naye yuko mkono wa kuume wa Mungu; tena ndiye anayetuombea. Ni nani atakayetutenga na upendo wa Kristo? Je! Ni dhiki au shida, au adha, au njaa, au uchi, au hatari, au upanga? Kama ilivyoandikwa, ya kwamba, Kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa, Tumehesabiwa kuwa kama kondoo wa kuchinjwa. Lakini katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda. Kwa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo, wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho chote hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu.”

Unaona maandiko yanaonyesha ukimuamini Yesu unapewa maisha yasiyozuilika na hakuna cha kutuzuia, hakuna wa kutushitaki, maana wako watu watatafuta mambo ya kukushitaki, walimshitaki Yesu mbona! tena kwa ushahidi wa uongo, watatafuta kukudhihaki, watakufanyia kila kitu kibaya ili yamkini ikiwezekana ukate tamaa, wanaweza kutuhukumu, wanaweza kutupangia aina ya adhabu, wanaweza kutupangia aina ya hukumu, wanaweza kukadiria aina ya maisha yetu, wanaweza kujifanya wana hatima ya maisha yetu kwa vyovyote vile  lakini kumbuka kuwa hawajafa kwaajili yetu,  Yesu ndiye aliyekufa na zaidi ya hayo amefufuka katika wafu, na yuko mkono wa kuume anatuombea, maombi ya Yesu kwaajili yako na yangu hayawezi kukataliwa, yuko mkono wa kuume wa baba kwa sababu hiyo kumbe kufufuka kwake kuna umuhimu mkubwa sana kwa sababu kunatupa maisha yasiyozuilika, kila anayepambana na kusudi la Mungu ndani yako anapaswa kuchukua tahadhari kubwa kwa sababu huenda anataka vita na Mungu, na akipigana na Mungu atajikuta yuko kwenye madhara makubwa kwa sababu tumepewa maisha yasiyozuilika, Wayahudi sio tu walitaka kuzia Yesu asifufuke lakini pia walitaka kuizua kazi yake mtu mmoja mwenye hekima akawaonya wayahudi kuwa waache kupambana na kazi za Yesu, kama walimsindwa Yeye waachie kazi yake ona   

Matendo 5:33-39 “Wao waliposikia wakachomwa mioyo yao; wakafanya shauri kuwaua. Lakini mtu mmoja, Farisayo, jina lake Gamalieli, mwalimu wa torati, mwenye kuheshimiwa na watu wote, akasimama katika baraza, akaamuru mitume wawekwe nje kitambo kidogo, akawaambia, Enyi waume wa Israeli, jihadharini jinsi mtakavyowatenda watu hawa. Kwa sababu kabla ya siku hizi aliondoka Theuda, akijidai ya kuwa yeye ni mtu mkuu, watu wapata mia nne wakashikamana naye; naye aliuawa na wote waliomsadiki wakatawanyika wakawa si kitu.Baada ya mtu huyo aliondoka Yuda Mgalilaya, siku zile za kuandikiwa orodha, akawavuta watu kadha wa kadha nyuma yake, naye pia akapotea na wote waliomsadiki wakatawanyika.Basi sasa nawaambia, Jiepusheni na watu hawa, waacheni; kwa kuwa shauri hili au kazi hii ikiwa imetoka kwa binadamu, itavunjwa, lakini ikiwa imetoka kwa Mungu hamwezi kuivunja; msije mkaonekana kuwa mnapigana na Mungu.”    
          

Pasaka hii ni onyo dhidi ya watu wote wanaokusudia na waliokusudia kushindana na mapenzi ya Mungu, kwa kanisa, kwa watumishi wake, na kwa maisha yako kwamba wajihadhari waache kushughulika na watu wenye maisha yasiyozuilika, mtu aliyeokolewa na kumuamini Bwaa Yesu kuwa bwana na mwokozi wa maisha yake hakuna cha kumzuia hata ukimuua, anapita tu kutoka mautini na kuingia uzimani, 

Yohana 5:24 “Amin, amin, nawaambia, Yeye alisikiaye neno langu na kumwamini yeye aliyenipeleka yuna uzima wa milele; wala haingii hukumuni, bali amepita kutoka mautini kuingia uzimani.”

Hakuna raha kama kuishi maisha yasiyozuilika maana kuna faida nyingi sana, na hatuwezi kuzimaliza zote lakini lakini zote hizi tunapewa kwa sababu Mungu alitaka tuwe na maisha yasiyozuilika  

-          Watashindana nawe na hawatakushinda – Yeremia 1:18-19 “Maana, tazama, nimekufanya leo kuwa mji wenye boma, na nguzo ya chuma, na kuta za shaba, juu ya nchi yote; juu ya wafalme wa Yuda, na juu ya wakuu wake, na juu ya makuhani wake, na juu ya watu wa nchi hii. Nao watapigana nawe; lakini hawatakushinda; maana mimi nipo pamoja nawe, asema Bwana, ili nikuokoe.”

 

-          Kila silaha itakayofanyika juu yako haitafanikiwa – Isaya 54:17 “Kila silaha itakayofanyika juu yako haitafanikiwa na kila ulimi utakaoinuka juu yako katika hukumu utauhukumu kuwa mkosa. Huu ndio urithi wa watumishi wa Bwana, na haki yao inayotoka kwangu mimi, asema Bwana.”

 

-          Hakuna uchawi wala uganga utakuweza – Hesabu 23:23 “Mungu amewaleta kutoka Misri, Naye ana nguvu kama nguvu za nyati. Hakika hapana uchawi juu ya Yakobo, Wala hapana uganga juu ya Israeli. Sasa habari za Yakobo na Israeli zitasemwa, Ni mambo gani aliyoyatenda Mungu!

               

-          Adui atakuja kwa njia moja atatawanyika kwa njia saba - Kumbukumbu 28:7 “Bwana atawafanya adui zako wainukao juu yako kupigwa mbele yako; watakutokea kwa njia moja, lakini watakimbia mbele yako kwa njia saba.”                 

Ndugu yangu unapoadhimisha sikukuu ya pasaka leo, Nakuombea kwa Mungu, na ni maombi yangu kuwa kila mmoja wetu aweze kuishi maisha yasiyozuilika, Yesu Kristo aliyefufuka ana mamlaka ya kuzimu na mauti, hivyo kila amuaminiye maana yake hakuna mtu anakuweza, sio mauti sio kuzimu, wala lolote linaweza kuyafanya maisha yako yakawa na kizuizi, Alipomwambia Yohana asiogope anakuambia na wewe na mimi tusiogope

Ufunuo 1:17-18 “Nami nilipomwona, nalianguka miguuni pake kama mtu aliyekufa. Akaweka mkono wake wa kuume juu yangu, akisema, Usiogope, Mimi ni wa kwanza na wa mwisho, na aliye hai; nami nalikuwa nimekufa, na tazama, ni hai hata milele na milele. Nami ninazo funguo za mauti, na za kuzimu.”     

Pasaka hii Mungu akuondolee vikwazo vya kila aina katika maisha yako na vile utakavyokutana navyo Mungu akupe kuvishinda, Mimi nilikutana na vikwazo vingi na vizuizi vyingi sana katika maisha yangu, huduma na utumishi, lakini hakuna hata kimoja kiliweza kuyazuia maisha yasiyozuilika Bwana anaweza hata kuandaa meza Machoni pa watesi wako na kukupaka mafuta mpaka kikombe chako kikafurika, Ubarikiwe na usihi maisha yasiyozuilika, kukiwa na maji tembea juu ya maji, wakitaka kukukamata pita katikati yao wende zako, wakikutupa katika makanwa ya simba hutatafunwa, wakikutupa katika tanuru la moto hutatekeketa, bahari ikiwa kikwazo bwana atafanya njia, kila iana ya dhiki na mateso na majaribu utayapitia lakini, utatoboa, wakikuzika na kulilinda kaburi ili usifufuke tetemeko na malaika wa bwana atawafanya aduinzako wawe kama wafu nawe utatoka. Kwa nini kwa sababu Yesu ametukirimia Maisha yasiyozuilika, na kwa jina lake kila kikwazo kinachisimama mbele yako kitabomolewa na kusawazishwa katika jina la Yesu. Nakutakia msimu mzuri wa sikukuu ya Pasaka Mungu akutunze!

Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni