Mwanzo 22:13-14 “Ibrahimu akainua macho
yake, akaangalia, na tazama, kondoo mume yuko nyuma yake, amenaswa pembe zake
katika kichaka. Basi Ibrahimu akaenda akamtwaa huyo kondoo, akamtoa awe sadaka
ya kuteketezwa badala ya mwanawe. Ibrahimu akapaita mahali hapo Yehova-yire,
kama watu wasemavyo hata leo, Katika mlima wa BWANA itapatikana.”
Utangulizi:
Ni muhimu kufahamu na
kujikumbusha tena na tena ya kuwa Mungu wetu ni mwaminifu na anajishughulisha
sana na maisha yetu katika namna ya kushangaza sana kiasi ambacho akili zetu
haziwezi kuelewa wakati mwingine, jinsi Mungu alivyo mwema katika maisha yetu,
Lakini ni ukweli ulio wazi kuwa Mungu anajishughulisha sana na mambo yetu, na yeye
hutupatia mahitaji yetu ya kimwili na kiroho, zaidi ya yote ni Mwalimu mzuri
sana wa neno lake kivitendo. Mungu anazo njia elfu nyingi za kututunza watu
wake ambazo wala hatuzijui, Endapo tu tutaamua kujiachilia kwa Mungu kwa Imani
bila shaka, utamuona Mungu kama Yehova Yire katika maisha yako na hutatikisika.
1Petro 5:6-7 “Basi nyenyekeeni chini ya
mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake; huku mkimtwika yeye
fadhaa zenu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana kwa mambo yenu.”
Wengi wetu tuliookolewa wakati
tunapopita majaribuni, huwa tunajawa na mashaka na kuanza kuumiza vichwa kuwa
mambo yatakuwaje na tunashindwa kwa namna Fulani kumpa Mungu nafasi ya
kutuhudumia kwa sababu tu ya mashaka yetu, ukweli ni kuwa tukishindwa kumwachia
Mungu fadhaa zetu na tukajaribu kuzibeba wenyewe tutajikuta tunashindwa na
tunazimia roho na tunaweza kukosa Amani ile ambayo Mungu ameikusudia kwetu
Leo tutachukua muda kujifunza kwa
kina na mapana na marefu na kumwangalia Mungu wetu kama Jehovah Yire katika
somo hili Katika mlima wa Bwana
itapatikana! Tutajifunza somo hili kwa kuzingatia mambo ya msingi
yafuatayo:-
·
Ibrahimu
katika kipimo cha juu kabisa cha Imani
·
Katika
mlima wa Bwana itapatikana
·
Jinsi na
namna bwana atakavyokupatia
Ibrahimu katika kipimo cha juu kabisa cha Imani
Moja ya eneo ambalo
linathibitisha ukuaji wa Imani ya Ibrahimu ni mara baada ya kushinda kipimo
hiki cha juu kabisa cha Imani, Mwanzo
22:1-3 “Ikawa baada ya mambo hayo Mungu alimjaribu
Ibrahimu, akamwambia, Ee Ibrahimu! Naye akasema, Mimi hapa. Akasema, Umchukue
mwanao, mwana wako wa pekee, umpendaye, Isaka, ukaende zako mpaka nchi ya
Moria, ukamtoe sadaka ya kuteketezwa huko juu ya mlima mmojawapo
nitakaokuambia. Ibrahimu akaondoka alfajiri, akatandika punda wake, akachukua
vijana wawili pamoja naye, na Isaka mwanawe, akachanja kuni kwa ajili ya hiyo
sadaka ya kuteketezwa, akaondoka, akaenda mpaka mahali alipoambiwa na Mungu.”
Mungu alikuwa amemjaribu Ibrahimu
kwa kiwango cha juu kabisa, tena katika namna ya kushangaza sana ambayo iko
kinyume na akili za kawaida za kibinadamu, na tabia na upendo wa Mungu, na
zaidi ya yote kama mzazi wa Isaka, lakini katika namna ya kushangaza sana
Ibrahimu alikuwa tayari kumtii Mungu katika kipimo hiki akiwa na imani kali
sana, kimsingi tunaweza kusema kuwa Ibrahimu aliwahi kupimwa na Mungu katika
mazingira makubwa matatu
1.
Kuondoka
katika nchi yake mwenyewe na kwenda asikojua
- hii ilitokea wakati Mungu aliposema na Ibrahimu kwa mara ya kwanza
kabisa kuwa aondoke katika nchi yake na nchi ya baba zake na watu wake aende
katika inchi atakayoonyeeshwa na kimsingi inchi hiyo pia alikuwa hajaijua na
Mungu alikuwa hajamwambia kuwa ni wapi ona
Mwanzo 12:1-4 “BWANA
akamwambia Abramu, Toka wewe katika nchi yako, na jamaa zako, na nyumba ya baba
yako, uende mpaka nchi nitakayokuonyesha; nami nitakufanya wewe kuwa taifa
kubwa, na kukubariki, na kulikuza jina lako; nawe uwe baraka; nami nitawabariki
wakubarikio, naye akulaaniye nitamlaani; na katika wewe jamaa zote za dunia
watabarikiwa. Basi Abramu akaenda, kama BWANA alivyomwamuru; Lutu akaenda
pamoja naye. Naye Abramu alikuwa mtu wa miaka sabini na mitano alipotoka Harani.”
Waebrania 11:8-9 “Kwa
imani Ibrahimu alipoitwa aliitika, atoke aende mahali pale atakapopapata kuwa
urithi; akatoka asijue aendako. Kwa imani alikaa ugenini katika ile nchi ya
ahadi, kama katika nchi isiyo yake, akikaa katika hema pamoja na Isaka na
Yakobo, warithi pamoja naye wa ahadi ile ile.”
Katika kipimo
hiki Ibrahimu alifanikiwa kwani alitii na kuondoka kwenda katika inchi
aliyoahidiwa na Mungu ambayo kimsingi ilikuwa inchi ya mkanaani na Mungu
alimthibitishia kuwa atampa inchi hiyo yeye na uzao wake
Mwanzo 17:1-9. “Abramu
alipokuwa mtu wa miaka tisini na kenda, BWANA akamtokea Abramu, akamwambia,
Mimi ni Mungu Mwenyezi, uende mbele yangu, ukawe mkamilifu. Nami nitafanya
agano langu kati ya mimi na wewe, nami nitakuzidisha sana sana. Abramu
akaanguka kifudifudi. Mungu akamwambia, akasema, Mimi, agano langu nimefanya
nawe, nawe utakuwa baba wa mataifa mengi, wala jina lako hutaitwa tena Abramu,
lakini jina lako litakuwa Ibrahimu, kwani nimekuweka uwe baba wa mataifa mengi.
Nitakufanya uwe na uzao mwingi sana, nami nitakufanya kuwa mataifa, na wafalme
watatoka kwako. Agano langu nitalifanya imara kati ya mimi na wewe, na uzao
wako baada yako, na vizazi vyao, kuwa agano la milele, kwamba nitakuwa Mungu
kwako na kwa uzao wako baada yako. Nami nitakupa wewe na uzao wako baada yako
nchi hii unayoikaa ugeni, nchi yote ya Kanaani, kuwa milki ya milele; nami
nitakuwa Mungu wao. Mungu akamwambia Ibrahimu, Nawe ulishike agano langu, wewe
na uzao wako kwa vizazi vyao baada yako.”
2.
Jaribu
la kuwa na subira - Mungu alimuahidi
Ibrahimu kuwa atampa uzao kupitia Sara mke wake wakati ahadi inatolewa Ibrahimu
alikuwa na miaka 75 bila shaka Sara alikuwa na miaka 65 kwa sababu Ibrahimu na
Sara walikuwa na tofauti ya miaka 10, Jaribu hili la kuwa na subira kwa kweli
liliwashinda, hata na sisi tunashindwa mara nyingi sana katika eneo la kuwa na
subira wapi Mungu alimuahidi Ibrahimu
mtoto ona
Mwanzo 18:10-13 “Akamwambia, Hakika nitakurudia wakati huu
huu mwakani, na tazama, Sara mkeo atapata mwana wa kiume. Sara akasikia
mlangoni pa hema iliyokuwapo nyuma yake. Basi Ibrahimu na Sara walikuwa wazee,
na umri wao mkubwa, na Sara alikuwa amekoma katika desturi ya wanawake. Kwa
hiyo Sara akacheka moyoni mwake, akisema, Niwapo mkongwe, nitapata furaha, na
bwana wangu mzee? BWANA akamwambia Ibrahimu, Mbona Sara amecheka akisema, Mimi
kweli nitazaa mwana, nami ni mzee? ”
Katika mtihani
huu hata hivyo Sara na Ibrahimu walikosa uvumilivu, kutimia kwa ahadi hii ya
Mungu kuligharimu miaka karibu 25 hivi kwa hiyo hapo katikati mambo yalikuwa
tofauti na Sara alikata tamaa na Ibrahimu alikubaliana na kukata tamaa huko na
wakajitafutia mtoto, kwa njia za kibinadamu na kitamaduni.
Mwanzo 16:1-4 “Basi
Sarai mkewe Abramu hakumzalia mwana, naye alikuwa na mjakazi, Mmisri, jina lake
Hajiri. Sarai akamwambia Abramu, Basi sasa, BWANA amenifunga tumbo nisizae,
umwingilie mjakazi wangu labda nitapata uzao kwa yeye. Abramu akaisikiliza
sauti ya Sarai. Sarai mkewe Abramu akamtwaa Hajiri Mmisri mjakazi wake, baada
ya kukaa Abramu katika nchi ya Kanaani miaka kumi, akampa Abramu mumewe, awe
mkewe. Basi akamwingilia Hajiri, naye akapata mimba. Naye alipoona ya kwamba
amepata mimba, bibi yake alikuwa duni machoni pake.”
Pamoja na Sara
na Ibrahimu kushindwa jaribu hili, utaweza kuona kwa kuwa Mungu ndiye aliyekuwa
ameahidi, Mungu ni mwaminifu hata kama watu hawaamini yeye hubaki wa kuaminiwa 2Timotheo 2:12-13 “Kama tukistahimili, tutamiliki pamoja naye; Kama tukimkana yeye, yeye
naye atatukana sisi; Kama sisi hatuamini, yeye hudumu wa kuaminiwa. Kwa maana
hawezi kujikana mwenyewe.”
Mungu yeye
aliitimiza ahadi yake na Sara na Ibrahimu walipata mtoto kama alivyosema Bwana,
muda haukuwa kitu kwa Mungu lakini Muda ulisumbua wanadamu, na unaendelea kuwasumbua wanadamu hata sasa, kwa
kawaida ni ngumu kusubiri, na kusubiri
huwasumbua wanadamu
Mwanzo 21:1-5 “BWANA akamjia Sara kama alivyonena, na
BWANA akamfanyia kama alivyosema. Sara akapata mimba akamzalia Ibrahimu mwana
wa kiume katika uzee wake, kwa muhula alioambiwa na Mungu. Ibrahimu akamwita
jina lake Isaka, yule mwana aliyezaliwa, ambaye Sara alimzalia. Ibrahimu
akamtahiri Isaka mwanawe, alipokuwa mwenye siku nane, kama Mungu alivyomwamuru.
Naye Ibrahimu alikuwa mtu wa miaka mia, alipozaliwa mwana wake Isaka.”
3.
Jaribu
la kumtoa Isaka kama sadaka ya kuteketezwa – jaribu hili ndilo lilikuwa
kipimo cha juu zaidi kwa Ibrahimu, lakini habari njema ni kuwa Ibrahimu sasa
alikuwa amekuwa kiimani, sasa alijua ya kuwa Mungu akisema kitu amesema na
hakuna ubabaishaji kwake, kwa hiyo Mungu aliposema naye kuhusu swala la kumtoa
Isaka Imani ya Ibrahimu ilikuwa kubwa sana kwani licha ya kuwa mtihani huu
ulikuwa mgumu sana kibinadamu lakini kwaajili ya uelewa wake, upendo wake na
imani yake kwa Mungu. Ibrahimu alikuwa amefikia ngazi ya juu zaidi ya Imani ya
kusema kuwa sasa yuko tayari kutii, huenda kushindwa kwake katika kusubiri kwa
jaribu la pili kulikuwa kumemkomaza kuwa hataki tena kumkwaza Mungu kwa agizo
lolote hivyo jamaa alitii ona:-
Mwanzo 22:1-3 “Ikawa
baada ya mambo hayo Mungu alimjaribu Ibrahimu, akamwambia, Ee Ibrahimu! Naye
akasema, Mimi hapa. Akasema, Umchukue mwanao, mwana wako wa pekee, umpendaye,
Isaka, ukaende zako mpaka nchi ya Moria, ukamtoe sadaka ya kuteketezwa huko juu
ya mlima mmojawapo nitakaokuambia. Ibrahimu akaondoka alfajiri, akatandika
punda wake, akachukua vijana wawili pamoja naye, na Isaka mwanawe, akachanja
kuni kwa ajili ya hiyo sadaka ya kuteketezwa, akaondoka, akaenda mpaka mahali
alipoambiwa na Mungu.”
Tukio la utii wa
Ibrahimu mahali hapa lilimpa Ibrahimu kuwa mtu mwenye heshima zaidi miongoni
mwa watu ambao wamewahi kupata kumuamini Mungu, Mungu aliapa kumbariki Abrahamu
kwa sababu alikuwa amekuwa kiimani, kwani alionyesha kuwa anamwamini Mungu sio
tu kwa kutii agizo hilo lakini Abrahamu aliamini ya kuwa huenda hata baada ya
kufanya hivyo Mungu atamfufua mwanae Isaka kutoka kwa wafu.
Waebrania 11:17-19 “Kwa imani Ibrahimu alipojaribiwa, akamtoa Isaka awe dhabihu; na yeye
aliyezipokea hizo ahadi alikuwa akimtoa mwanawe, mzaliwa pekee; naam, yeye
aliyeambiwa, Katika Isaka uzao wako utaitwa, akihesabu ya kuwa Mungu aweza
kumfufua hata kutoka kuzimu; akampata tena toka huko kwa mfano.”
Katika kuamini
na kutii agizo hili au jaribio hili la tatu kuna matukio kadhaa ya kiimani
yaliyoambatana na tukio hili, tukio hili lilileta Baraka kubwa sana kwa
Ibrahimu, lakini pia lilileta Baraka kubwa sana kwa ulimwengu, Ibrahimu kama
nabii, na mwanae Isaka kama nabii kimsingi walitabiri ujio wa Yesu Kristo,
kinabii Ibrahimu akisimama kama Mungu na Isaka akisimama kama mwana wa Mungu
(Yesu Kristo) na mlima ule Moria ukisimama kama Golgotha na kuni zile zikisimama
kama msalaba, ambapo Isaka anabeba kuni zile ambazo angeenda kutolewa dhabihu
juu yake ni picha ya Yesu Kristo akiwa amebeba msalaba wake ambapo alikwenda
kusulubiwa juu ya msalaba ule kwaajili ya ulimwengu mzima, Pamoja na somo hilo
zuri jambo lingine la msingi tunalojifunza hapa ni neno lile Katika mlima wa
Bwana itapatikana nini hiyo hilo linatuleta katika kutafakari kipengele cha
pili.
Katika mlima wa Bwana itapatikana!
Ibrahimu na
Isaka wakiwa njiani kuna maswala ya Msingi ambayo yanatufundisha na kutufunulia
tabia ya Mungu tunayemuabudu kuwa ni Mungu wa namna gani, kwanza inaonekana
wazi kuwa tabia ya Ibrahimu kumuabudu Mungu lilikuwa ni jambo la kawaida na
huenda alikuwa amemfundisha Isaka mara kadhaa namna na jinsi anavyoendesha
ibada zake, kwa hiyo Isaka katika ujana wake alikuwa amekwisha kuelewa jinsi
Mungu anavyopokea dhabihu na namna dhabihu ya kuteketezwa inavyotekelezwa,
Kimsingi kuwa na moto, na kuni na kisu pekee na kuelekea katika eneo la kuabudu
havikuwa na msingi kama hakuna mwana kondoo, Kwa hiyo Isaka katika akili zake
alifikiri kuwa safari hii baba yake atakuwa amesahahu au amepuuzia jambo la
Muhimu katika ibada hiyo ambayo kimsingi ni mwana kondoo na kukaa kimya
kungeweza kuwafanya waende mbali zaidi huku akiwa au wakiwa hawana kondoo wa
sadaka hivyo Isaka akauliza
Mwanzo 22:5-8 “Ibrahimu
akawaambia vijana wake, Kaeni ninyi hapa pamoja na punda, na mimi na kijana
tutakwenda kule, TUKAABUDU, NA KUWARUDIA TENA. Basi Ibrahimu akazitwaa kuni za
hiyo sadaka, akamtwika Isaka mwanawe; akatwaa moto na kisu mkononi mwake,
wakaenda wote wawili pamoja. Isaka akasema na Ibrahimu baba yake, akinena,
Babangu! Naye akasema, Mimi hapa, mwanangu. Akasema, Tazama! Moto upo, na kuni
zipo, lakini yuko wapi mwana-kondoo kwa sadaka ya kuteketezwa? Ibrahimu
akasema, MUNGU ATAJIPATIA MWANA-KONDOO KWA HIYO SADAKA, mwanangu. Basi
wakaendelea wote wawili pamoja.”
Kimsingi maneno
haya ya Ibrahimu yenyewe yalikuwa yamejaa Imani kubwa na unabii mkubwa na wa
ajabu, Ibrahimu alikuwa amewabakiza vijana wakae na punda na kuwapa maelekezo
kuwa yeye na kijana yaani Isaka watakwenda kuabudu na kisha KUWARUDIA TENA, kwa hiyo Ibrahimu alikua na uhakika kuwa atarudi
na Isaka kama anavyokwenda naye, lakini jambo la pili swali la Isaka kwa baba
yake kuwa moto upo, na kuni zipo lakini mwana-kondoo kwa sadaka ya kutekeketezwa
yuko wapi? Ibrahimu anamjibu Isaka kuwa MUNGU
ATAJIPATIA neno hili kwa kiebrania
linasomeka kama “elohiym raah” au Yehoha Yire maana yake kwa kingereza God will Provide au Kiswahili Mungu atajipatia au katika mlima wa bwana itapatikana, kwa hiyo
Isaka anapouliza sadaka iko wapi Ibrahimu anajibu katika mlima wa Bwana
itapatikana neno hili lilikuwa na maana
gani?
Maana kubwa na
ya msingi ni kuwa Mungu mwenyewe ataleta mwana kondoo sahihi kwa sadaka ya
dhambi itakayowakomboa wanadamu wote, Mungu alitimiza yeye mwenyewe kile
ambacho alikuwa amemuagiza Ibrahimu akifanye, kwa hiyo ni kweli Mungu aliwapa
mwana kondoo aliyekuwa amenasa pembe zake katika kichaka cha miiba ikiwa ni
picha ya Kristo aliyevishwa taaji ya miiba wakati anasulubiwa msalabani pale
Golgotha , kauli ya Ibrahim ilitimizwa na Mungu kwa wakati ule kwa kuwapa
kondoo halisi, lakini kinabii kwa Mungu kumtoa mwanakondoo atakayechukua dhambi
za ulimwengu yaani Yesu Kristo
Mwanzo 22:9-14 “Wakafika
mahali pale alipoambiwa na Mungu, Ibrahimu akajenga madhabahu huko, akaziweka
tayari kuni, kisha akamfunga Isaka mwanawe, akamweka juu ya madhabahu, juu ya
zile kuni. Ibrahimu akanyosha mkono wake, akakitwaa kisu ili amchinje mwanawe.
Ndipo malaika wa BWANA akamwita kutoka mbinguni, akasema, Ibrahimu! Ibrahimu!
Naye akasema,Mimi hapa. Akasema, Usimnyoshee kijana mkono wako, wala usimtendee
neno; kwa maana sasa ninajua ya kuwa unamcha Mungu, iwapo hukunizuilia mwanao,
mwanao wa pekee. Ibrahimu akainua macho yake, akaangalia, na tazama, kondoo
mume yuko nyuma yake, amenaswa pembe zake katika kichaka. Basi Ibrahimu akaenda
akamtwaa huyo kondoo, akamtoa awe sadaka ya kuteketezwa badala ya mwanawe.
Ibrahimu akapaita mahali hapo Yehova-yire, kama watu wasemavyo hata leo, Katika
mlima wa BWANA itapatikana.”
Yohana 1:29-32 “Siku
ya pili yake amwona Yesu anakuja kwake, akasema, Tazama, Mwana-kondoo wa Mungu,
aichukuaye dhambi ya ulimwengu! Huyu ndiye niliyenena habari zake ya kwamba,
Yuaja mtu nyuma yangu, ambaye amekuwa mbele yangu; kwa maana alikuwa kabla
yangu. Wala mimi sikumjua; lakini kusudi adhihirishwe kwa Israeli ndiyo maana
mimi nalikuja nikibatiza kwa maji. Tena Yohana akashuhudia akisema, Nimemwona
Roho akishuka kama hua kutoka mbinguni; naye akakaa juu yake.”
Kwa hiyo
kimsingi, Ibrahimu alikuwa ametabiri ya kuwa Mungu atatimiza mahitaji yetu yote
ya ukombozi wa mwanadamu na kutupatia wokovu, Ibrahimu alikuwa ameonyesha wazi
kuwa kutakuwa na ukomo kwa sadaka za kutetekezwa pale Mungu atakapokuja kumtoa
mwana wake wa pekee ambaye ndiye Yesu aliyekufa msalabani na kutuletea wokovu.
Jambo lingine
tunalijifunza kutoka katika neno Yehova
Yire yaani katika mlima wa Bwana itapatikana ni kuwa Mungu anajihusisha na
mahitaji yetu sio ya kiroho tu bali na ya mwilini, Yehova yire maana yake Mungu
atatoa, kila wakati tunapokuwa na upungufu wa aina yoyote katika mahitaji yetu
ya mwilini ni lazima kwetu kujishusha na kumuachia Mungu na kumtazama Mungu kwa
Imani kuwa atajishughulisha na mahitaji yetu, tunapokuwa tumepungukiwa na kitu
Mungu wetu alituahidi ya kuwa hatatupungukia wala hatatuacha, Mungu atatupima
Imani yetu kwa kutupitisha jangwani, atatupima Imani yetu tunapokuwa hatuna
kazi, atatupima Imani yetu tunapokuwa hatuna chakula, hatuna fedha za kulipa
bili ya umeme, au ya maji, au kodi ya
nyumba, au nauli ya dala dala, na wakati mwingine hata sadaka ya kumtolea yeye,
au tunadaiwa kila kona jiachilie katika Mungu mwamini Mungu ya kuwa
atashughulika na mahitaji yako kwa sababu yeye ni Yehova yire na katika mlima
wake itapatikana! Ikiwa tuna mahitaji yoyote ya kimwili na kiroho, tunahitaji
uwepo wake, tunahitaji neema yake au huruma zake yeye yupo na tunapomwangalia
yeye atatupatia hata baada ya kupitia njia ya mateso, hofu na mashaka yakuwa
itajuwaje Yeye atatupa uwepo wake na nguvu zake zitadhihirika na sisi tutakuwa
katika Imani kwa msaada wa Mungu wetu Haleluyaa!
Jinsi na namna Bwana atakavyokupatia
Inawezeakana unakutana na somo
hili ukiwa huelewi kuwa utatoka vipi katika hali unayoipitia, hujui itakuwaje,
huna wa kukutia moyo, kutokana na magumu unayokutana nayo, huna fedha, huna
namna ya kujitibu, kihisia hakuko vema, umejawa na mashaka na wasiwasi,
majaribu yamekuzunguka kila kona, ni kama umepoteza tumaini, unahangaika,
hakuna anayekujali, kuna mambo chungu nzima yanasumbua kichwa chako, hujui
kesho itakuwaje, ada ya watoto shule itakuwa vipi, wazazi wanaokutegemea
utawatunza vipi, ndugu zako uliokuwa unawasaidia, utawasaidiaje, mbingu ni kama
zimekuwa chuma na ardhi ni kama imekuwa shaba, shambani mambo yamekataa, miradi
imegoma, mzunguko wa fedha ni kama hauko, biashara haziendi, unawaza hivi
itapatikana? Ndoa itapatikana? Kazi itapatikana? Uamsho kanisani kwangu
utapatikana? Mtoto atapatikana? Mavazi yatapatikana ?, washirika katika huduma
yangu watapatikana? Sadaka katika wakati huu mgumu itapatikana? Endapo unazungukwa na maswali mengi sana
yanayofanana na hayo somo hili haliko mikononi mwako kwa bahati Mbaya Roho
Mtakatifu alinitaka niliandae somo hili na aliniambia nilimalize mara moja,
nilikuwa na masomo mengine naendelea nayo, lakini niliamuriwa niayaache
nishughulike na hili kwaajili yako wewe unayesoma somo hili Bwana anakuambia
leo katika mlima wa Bwana itapatikana na unaweza kuniuliza swali itapatikanaje?
Kumbuka Ibrahimu hakuwa na mahali aliponukuu ahadi ya Mungu au neno la Mungu ya
kuwa Mungu ni Yehova Yire wala hakuwa na mahali pameandikwa katika mlima wa
bwana itapatikana lakini Isaka alipouliza, Ibrahimu alijibu moja kwa moja kama
vile vile Mungu alivyomfanyia baadaye nasema katika mlima wa bwana itapatikana,
itapatikanaje sisi tunazo ahadi za Mungu nyingi sana zinazoonyesha kuwa Mungu
anashughulika na mahitaji yetu
a.
Anashughulika
na mahitaji yetu ya mwilini – Mungu aliyetuumba anatujua sisi ni viumbe
wake na alipotuumba aliandaa kila kitu kwaajili yetu, anawajibika kutulisha
kama anavyolisha wanyama na ndege wa angani kwa hiyo Mungu wetu hashindwi
kujitokeza katika mahitaji yetu yote na katika chakula
Wafilipi 4:19 “Na
Mungu wangu atawajazeni kila mnachokihitaji kwa kadiri ya utajiri wake, katika
utukufu, ndani ya Kristo Yesu.”
Luka 12:240-26 “Watafakarini
kunguru, ya kwamba hawapandi wala hawavuni; hawana ghala wala uchaga, na Mungu
huwalisha. Bora ninyi mara nyingi kuliko ndege! Na yupi kwenu ambaye
akijisumbua aweza kujiongeza kimo chake hata mkono mmoja? Basi, ikiwa hamwezi
hata neno lililo dogo, kwa nini kujisumbua kwa ajili ya yale mengine? ”
Zaburi 145:14-16 “Bwana
huwategemeza wote waangukao, Huwainua wote walioinama chini.Macho ya watu wote
yakuelekea Wewe, Nawe huwapa chakula chao wakati wake. Waufumbua mkono wako,
Wakishibisha kila kilicho hai matakwa yake.”
Zaburi 37:25 “Nalikuwa
kijana nami sasa ni mzee, Lakini sijamwona mwenye haki ameachwa Wala mzao wake
akiomba chakula.”
b.
Mungu
atakupa pumziko – Yesu/Mungu ameahidi kutupa pumziko, najua unahangaika
sana roho yako inatanga tanga, hata wale waliokutimua wanataka kujua itakuwaje,
wanatamani kujua unaishije, wanataka kuona ukihangaika, wanatamani kuona ukienda
kuwaomba na kuwakopa, au ukihangaika, moyo wako ni kama una hofu hivi lakini
weka tumaini lako kwa Yesu nawe utapata Pumziko.
Mathayo 11:28-29 “Njoni
kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.
Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa
moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu;”
Zaburi 23:1-6 “Bwana
ndiye mchungaji wangu, Sitapungukiwa na kitu. Katika malisho ya majani mabichi
hunilaza, Kando ya maji ya utulivu huniongoza. Hunihuisha nafsi yangu; na
kuniongoza Katika njia za haki kwa ajili ya jina lake.Naam, nijapopita kati ya
bonde la uvuli wa mauti, Sitaogopa mabaya; Kwa maana Wewe upo pamoja nami,
Gongo lako na fimbo yako vyanifariji.Waandaa meza mbele yangu, Machoni pa
watesi wangu. Umenipaka mafuta kichwani pangu, Na kikombe changu kinafurika.
Hakika wema na fadhili zitanifuata Siku zote za maisha yangu; Nami nitakaa
nyumbani mwa Bwana milele.”
c.
Mungu
atakupa muongozo - Ni kazi ya Mungu kutuongoza na kutusafishia njia kwaajili
ya kusudi lake, wakati mwingine unapokuwa na mashaka kuhusu muelekeo unawaza
itapatikana kweli? Kuna muelekeo kweli yuko anayetoa muelekeo na atakuongoza
kwenye maji ya utulivu, kwa nini kwa sababu anatoa muongozo, watu wengine
hawawezi kujua njia yetu kwa sababu wao sio Mungu, wanadamu wakiijua njia yako
wanaweza kuiharibu lakini Mungu ndiye mwenye mwenendo na yeye ndiye njia.
Mithali 3:5-6 “Mtumaini
Bwana kwa moyo wako wote, Wala usizitegemee akili zako mwenyewe; Katika njia
zako zote mkiri yeye, Naye atayanyosha mapito yako.”
Mithali 20:24 “Mwenendo
wa mtu watoka kwa Bwana; Basi, awezaje mtu kuelewa na njia yake? “
Zaburi 37:5-6 “Umkabidhi
Bwana njia yako, Pia umtumaini, naye atafanya. Ataitokeza haki yako kama nuru,
Na hukumu yako kama adhuhuri ”
d.
Mungu
atatuoa neema – Iko neema maalumu ambayo Mungu atatupa kwaajili ya kila
aina ya mapito unayoyapitia, neema ya Mungu itatuisaidia, itatusaidia
kuwasamehe waliotukosea, na kusahau yote, itatusaidia kufurahi katika mazingira
ambayo tulitakiwa tuwe tunalia, itatusaidia kuwapa kipaumbele wenzetu katika
ndoa, itatusaidia kuzitunza familia zetu, neema itarahisisha maisha na kutupa
nguvu ya kusonga mbele katika namna ya kushangaza sana, neema ya Mungu hainunuliwi,
neema ya Mungu haipatikani kwa kujipendekeza, neema ya Mungu inatolewa Bure na
kutufaa wakati wa mahitaji, Yeye mwenyewe anatoa, Mungu mwenyewe atatupa neema
ya kuitusaidia wakati wa mahitaji yetu!
Waebrania 4:15-6. “Kwa
kuwa hamna kuhani mkuu asiyeweza kuchukuana nasi katika mambo yetu ya udhaifu;
bali yeye alijaribiwa sawasawa na sisi katika mambo yote, bila kufanya dhambi.
Basi na tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata
neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji.”
2Wakorintho 9:8 “Na
Mungu aweza kuwajaza kila neema kwa wingi, ili ninyi, mkiwa na riziki za kila
namna siku zote, mpate kuzidi sana katika kila tendo jema;”
Shetani na
maajenti wake na maadui wanaotutakia mabaya hawajui kuwa iko neema na rehema za
kutusaidia wakati wa mahitaji yetu, Mungu hujalia neema hiyo, Paulo alipokuwa
na uhitaji wa kile alichokiita mwiba katika maisha yake Mungu alimjibu kuwa
neema inatosha, maana yake Mungu akitupa neema yake tunawezeshwa kustahimili
yale yanayotusibu kwa Amani bila kukosana na Mungu wetu wala kuwaudhi watu omba
neema ya Mungu siku zote katika maisha yako na utakuwa na Amani kwani neema
yake itakubeba.
e.
Mungu
atatupa njia ya kutokea – Ni Isaka aliyekuwa amefungwa mikono yake, ni
Isaka aliyekuwa katika hatari ya kuchomwa kisu na baba yake, wakati anasumbuka
yuko wapi mwana kondoo, ghafla anashangaa kumbe yeye ndiye anayefanywa kondoo
siku ile? Najua umefanywa kondoo wa kafara mara kadhaa katika maisha yako, watu
waliona wakutoe wewe, ili wapate nafuu, waliona ufukuzwe wewe, waliona
wakusingizie wewe, waliona wakuharibie wewe lakini kama alivyosema Ibrahimu
Katika mlima wa Mungu itapatikana maana yake Mungu atajipatia mwana kondoo, kwa
kila jaribu unalolipitia bwana ataweka na mlango wa kutokea.
Mwanzo 22:9-13 “Wakafika
mahali pale alipoambiwa na Mungu, Ibrahimu akajenga madhabahu huko, akaziweka
tayari kuni, kisha akamfunga Isaka mwanawe, akamweka juu ya madhabahu, juu ya
zile kuni. Ibrahimu akanyosha mkono wake, akakitwaa kisu ili amchinje mwanawe.
Ndipo malaika wa BWANA akamwita kutoka mbinguni, akasema, Ibrahimu! Ibrahimu!
Naye akasema, Mimi hapa. Akasema, Usimnyoshee kijana mkono wako, wala
usimtendee neno; kwa maana sasa ninajua ya kuwa unamcha Mungu, iwapo
hukunizuilia mwanao, mwanao wa pekee. Ibrahimu akainua macho yake, akaangalia,
na tazama, kondoo mume yuko nyuma yake, amenaswa pembe zake katika kichaka.
Basi Ibrahimu akaenda akamtwaa huyo kondoo, akamtoa awe sadaka ya kuteketezwa
badala ya mwanawe.”
1Wakorintho 10:13 “Jaribu halikuwapata ninyi, isipokuwa lililo
kawaida ya wanadamu; ila Mungu ni mwaminifu; ambaye hatawaacha mjaribiwe kupita
mwezavyo; lakini pamoja na lile jaribu atafanya na mlango wa kutokea, ili mweze
kustahimili.”
Mungu atatupatia
njia ya kutoka au kulishinda jaribu linalotukumba, neema ya Mungu ilivyo njema
tuna neno lake, tuna Roho wake tukisimama karibu naye na kuomba msaada wake
nakuhakikishia tutaona njia mbadala.
f.
Mungu
ataleta msaada wakati tunaumizwa au tunakaribia kuumizwa – wakati wote
Mungu wetu hatakubali uonevu, na tunapoumizwa na yeyote yule hata awe mtu wa
Mungu, hiyo haimaanishi kuwa Mungu hatashughulika na sisi, Yeye ni msaada uonekanao
tele wakati wa mateso, wakati maumivu yanapokuwa magumu kubeba kumbuka
tumkimbilie Mungu yeye sio Mungu aliye mbali, wakati Ibrahimu anakaribia
kumuumiza Isaka Mungu alimtuma malaika wake mbingu ziliingilia kati.
Zaburi 46:1-3 “Mungu
kwetu sisi ni kimbilio na nguvu, Msaada utakaoonekana tele wakati wa mateso.Kwa
hiyo hatutaogopa ijapobadilika nchi, Ijapotetemeka milima moyoni mwa bahari.
Maji yake yajapovuma na kuumuka, Ijapopepesuka milima kwa kiburi chake.”
Zaburi 34:17-19 “Walilia,
naye Bwana akasikia, Akawaponya na taabu zao zote. Bwana yu karibu nao
waliovunjika moyo, Na waliopondeka roho huwaokoa. Mateso ya mwenye haki ni
mengi, Lakini Bwana humponya nayo yote.”
Mwanzo 16:6-11. “Naye
Abramu akamwambia Sarai, Tazama, mjakazi wako yu mkononi mwako, mtendee lililo
jema machoni pako. Sarai akamtesa, naye akakimbia kutoka mbele yake. Malaika wa
BWANA akamwona kwenye chemchemi ya maji katika jangwa, chemchemi iliyoko katika
njia ya kuendea Shuri. Akamwambia, Hajiri, wewe mjakazi wa Sarai, unatoka wapi,
nawe unakwenda wapi? Akanena, Nakimbia mimi kutoka mbele ya bibi yangu Sarai.
Malaika wa BWANA akamwambia, Rudi kwa bibi yako, ukanyenyekee chini ya mikono
yake. Malaika wa BWANA akamwambia, Hakika nitauzidisha uzao wako, wala
hautahesabika kwa jinsi utakavyokuwa mwingi. Malaika wa BWANA akamwambia,
Tazama! Wewe una mimba, utazaa mwana wa kiume, nawe utamwita jina lake
Ishmaeli, maana BWANA amesikia kilio cha mateso yako.”
g.
Mungu
atakupa Amani – unaonaje katika jaribu lile la Ibrahimu kama angemuua
mwanae? Hata kama Mungu angemfufua katika wafu, uhusiano wa mtoto na baba yake
ungekuwa mashakani, kila mmoja angepoteza Amani, lakini njia ya Mungu katika
mlima wake ilikuwa ya kupendeza sana walirudi kwa Amani, Mungu hutupoa Amani katika mazingira yoyote
yale, ataitunza mioyo yetu na akili zetu zisiumizwe vibaya, anatuleta katika
Amani, anatoa Amani,
Wafilipi 4:6-7 “Msijisumbue
kwa neno lo lote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na
kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu. Na amani ya Mungu, ipitayo akili
zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.”
Warumi 5:1 “Basi
tukiisha kuhesabiwa haki itokayo katika imani, na mwe na amani kwa Mungu, kwa
njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kwa yeye tumepata kwa njia ya imani
kuifikia neema hii ambayo mnasimama ndani yake; na kufurahi katika tumaini la
utukufu wa Mungu. Wala si hivyo tu, ila na mfurahi katika dhiki pia; mkijua ya
kuwa dhiki, kazi yake ni kuleta saburi; na kazi ya saburi ni uthabiti wa moyo;
na kazi ya uthabiti wa moyo ni tumaini; ”
h.
Mungu
atakuokoa – unaweza kusema mbona nimeshaokoka lakini neno wokovu katika
lugha ya kiyunani wanatumie neno Sōtēria
ambalo lina maana pana zaidi ya kusamehewa dhambi au kuzaliwa mara ya pili,
Soteria ni kuwekwa huru, kuokolewa hatarini, kulindwa na hatari, kwa hiyo
wakati unapitia changamoto na majaribu ya aina mbalimbali kumbuka pia kuwa
Mungu atakuokoa, kama alivyomuokoa Isaka au alivyomfufua Yesu baada ya
kusulubiwa Msalabani akamuokoa na mauti basi Mungu atakuokoa na wewe katika
mapito yako na hatari zako zote na maumivu yako yote.
Zaburi 61:1-3 “Ee
Mungu, ukisikie kilio changu, Uyasikilize maombi yangu. Toka mwisho wa nchi
nitakulilia nikizimia moyo, Uniongoze juu ya mwamba nisioweza kuupanda. Kwa
maana ulikuwa kimbilio langu, Ngome yenye nguvu adui asinipate.”
Zaburi 27:1-3 “Bwana
ni nuru yangu na wokovu wangu, Nimwogope nani? Bwana ni ngome ya uzima wangu,
Nimhofu nani? Watenda mabaya waliponikaribia, Wanile nyama yangu, Watesi wangu
na adui zangu, Walijikwaa wakaanguka. Jeshi lijapojipanga kupigana nami, Moyo
wangu hautaogopa. Vita vijaponitokea, Hata hapo nitatumaini.”
Unaweza kuona Mungu ametuahidi
katika neno lake kukutana na mahitaji yetu yote, wakati tunapopungukiwa
anatukumbusha tu kuwa tumuamini yeye kwani Yeye kama YEHOVA YIRE “God will
provide” maana yake atakutana na mahitaji yetu na katika mlima wake itapatikana,
Mungu atatoa msaada na atatupa njia na namna ya kujikwamua kutoka katika pito
lako, haijalishi unapitia pito la namna gani,
fahamu tu ya kuwa Mungu amekwisha kutupa njia ya kufanya wakati wa
mahitaji yetu ya kimiwli na kiroho, tunaweza kuwa na amani na utulivu tukijua
ya kuwa KATIKA MLIMA WA BWANA
ITAPATIKANA.
Na. Rev. Innocent Samuel Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye hekima!
Nampa sifa Mungu aliyekutumia kutupa chakula hiki,pili,nikupongeze kwa utii wako ktk kufikisha ujumbe huu. Binafsi nimepokea kwa nafasi yangu. Mungu akutunze.
JibuFutaAsante sana kwa mrejesho huu wa maoni yako, Naamini Mungu alikuwa na kusudi kubwa kwa watu wake kupitia somo hili, Neema ya Mungu itufunike sote kwaajili ya utukufu wake katika jina la Yesu, Amen
JibuFutaMungu akubariki kwa fundisho. Asante limenipa hatua.
JibuFuta