Jumapili, 19 Mei 2024

Roho wa Bwana na Nguvu za uonevu!


Matendo 10:38 “habari za Yesu wa Nazareti, jinsi Mungu alivyomtia mafuta kwa Roho Mtakatifu na nguvu naye akazunguka huko na huko, akitenda kazi njema na kuponya wote walioonewa na Ibilisi; kwa maana Mungu alikuwa pamoja naye


Utangulizi:

Leo ni siku ya Pentecost: Pentecost ni siku ambayo wakristo duniani wanaadhimisha na kukumbuka siku ya kushuka maalumu duniani kwa ROHO MTAKATIFU  na kuanza kufanya kazi akiwa na mitume na wanafunzi wengine wa Yesu Kristo, tukio hilo maalumu limeelezwa katika kitabu cha Matendo

Matendo 2:1-4 “Hata ilipotimia siku ya Pentekoste walikuwako wote mahali pamoja. Kukaja ghafula toka mbinguni uvumi kama uvumi wa upepo wa nguvu ukienda kasi, ukaijaza nyumba yote waliyokuwa wameketi. Kukawatokea ndimi zilizogawanyikana, kama ndimi za moto uliowakalia kila mmoja wao. Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia kutamka.”

Sikukuu ya Pentecost iliadhimishwa siku ya 50 baada ya sikukuu ya Pasaka, Na neno hilo Pentecost limetokana na neno la asili ya kigiriki Pentecost ambalo maana yake ni 50, hata hivyo sikukuu ya Pentekoste ambayo huadhimishwa siku 50 baada ya pasaka au jumapili saba baada ya pasaka kwa wayahudi sikukuu hii huitwa SHAVUOT  ambayo kimsingi ilikuwa sikukuu ya mavuno kwa Wayahudi, Hata hivyo katika siku hiyo Mungu aliitumia kumuachilia Roho wake Mtakatifu kuchukua nafasi na kuleta nguvu kwa wanafunzi wa Yesu ili waweze kuwa mashahidi wake na kuihubiri injili ya utukufu wa Mungu duniani kwa gharama yoyote. Siku hii huadhimishwa na njia mbalimbali na kwa hutuba mbalimbali, wengine wakiliita juma la Roho Mtakatifu, na kadhalika, Hata hivyo kwa upande wangu Roho Mtakatifu alinitaka niikumbushe jamii kuwa Roho Mtakatifu vile vile yuko kwaajili ya kushughulika na uonevu wa kila aina duniani kupitia kanisa lake, maana yake ni kuwa Roho Mtakatifu anapokuja juu ya watumishi wake na kuwapaka mafuta ni Dhahiri kuwa anawataka watumishi wake wakashughulikie uonevu na kuwaweka huru watu wake kutoka katika migandamizo ya aina mbalimbali kama vile alivyoshuka juu ya Masihi.          

Luka 4:17-19. “Akapewa chuo cha nabii Isaya, akakifungua chuo, akatafuta mahali palipoandikwa, Roho wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa, Na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa.”

Kwa msingi huo leo tutachukua muda kujifunza somo hili muhimu ROHO WA BWANA NA NGUVU ZA UONEVU! na tutajifunza somo hili muhimu kwa kuzingatia vipengele kadhaa vifuatavyo:-

 

·         Maana ya  neno uonevu

·         Jinsi Mungu anavyochukizwa na uonevu

·         Roho wa Bwana na nguvu za uonevu

 

Maana ya neno uonevu.

Matendo 10:38 “habari za Yesu wa Nazareti, jinsi Mungu alivyomtia mafuta kwa Roho Mtakatifu na nguvu naye akazunguka huko na huko, akitenda kazi njema na KUPONYA WOTE WALIOONEWA na Ibilisi; kwa maana Mungu alikuwa pamoja naye

Ni muhimu kufahamu kuwa katika Biblia ya kiingereza neno na KUPONYA WOTE WALIOONEWA linasomeka  and HEALING ALL THAT WERE OPPRESSED  neno hilo walioonewa ambalo kwa kiingereza oppressed katika maandiko ya kiyunani linasomeka kama  katadunasteuō ambalo kwa tafasiri ya kiingereza ni exericise Dominion against,  kwa Kiswahili kutawala kwa mabavu, au kuonea kwa nguvu, kutawala kikatili, au Dhuluma. Ukatili huo unaweza kuhusisha kuchukua kitu kwa nguvu, kutumikishwa kwa ujira mdogo, kutawaliwa kimabavu, kukandamizwa, kudhulumiwa, kuteswa, kufanyishwa kazi kupita kawaida au zaidi ya muda wa kawaida, kuwekwa katika hali ya kukosa maamuzi yako mwenyewe, kuwekwa chini ya utawala wa taifa jingine, na kadhalika na kwa sababu hiyo mtu anayeonewa anajisikia uonyonge, anaugua au kulia au kuomboleza, au kukata tamaa moyoni, au kulalamika huku mtu huyo au watu hao wakiwa hawana msaada wa kujitoa katika uonevu huo. Isipokuwa kwa msaada token je yake

Kwa hiyo mojawapo ya kazi za Roho Mtakatifu ni pamoja na kuharibu nguvu za uonevu, kwa hiyo Mungu anapotaka kushughulika na uonevu wakati wowote, lazima atamtumia mtu na kumpaka mafuta mtu huyo ili aweze kushughulikia uonevuo huo,  na ndio maana Leo au katika sikukuu ya Pentekoste ya Mwaka huu tunataka kumwangalia Roho Mtakatifu katika picha kukomesha uonevu!

Luka 4:17-19. “Akapewa chuo cha nabii Isaya, akakifungua chuo, akatafuta mahali palipoandikwa, Roho wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, KUWAACHA HURU WALIOSETWA, Na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa.” Unaweza kuona katika kifungu hiki pia kiingereza cha ESV kinasomeka “to set liberty those who are oppressed”

Kwa hiyo bado tunapata picha kuwa kusudi kuu la Roho Mtakatifu kuwapa nguvu watumishi wake kwa kuwapaka mafuta kusudi kubwa ni kukomesha uonevu, Dunia imejawa na uonevu wa kila aina kutoka kwa shetani na maajenti wake, na magonjwa ni sehemu ya uonevu huo, maendeleo ya kisayansi na teknolojia hayatoshi peke yake kumuweka huru mwanadamu kutoka katika uonevu huo, aidha nguvu za kipepo kila wakati zinawasukuma wanadamu kufanya yale wasiyopenda kuyafanya hasa kuyafanya mapenzi ya Mungu,  ili kwa njia hiyo shetani apate kibali cha kuendelea kuwaonea watu na kuwakandamiza, ni makusudi basi Pentekoste hii tukajikumbusha sio tu kule kujazwa na Roho Mtakatifu na nguvu zake na kufurahia kunena kwa lugha lakini wakati huu, tukubali nguvu za Roho Mtakatifu zituelekeze katika matumizi ya kushughulika na nguvu za uonevu, maana yake nini kuelekeza nguvu zetu zote katika kufunguliwa kwa aina binadamu ambao wanaonewa na ibilisi, hii ikienda sambaba na kazi ya kuihubiri injili.

Jinsi Mungu anavyochukizwa na uonevu

Neno la Mungu linatudhihirishia kuwa Mungu anachukizwa sana na uonevu wa kila aina duniani, wakati Israel wanateswa kule Misri na wakawa wanakandamizwa katika utumwa mzito kiasi cha kulia Machozi, Mungu aliguswa na kuamua kushuka ili ashughulike na uonevu uliokuwa unaendelea wamisri wakiwaonea wana wa Israel

Kutoka 3:7-9 “BWANA akasema, Hakika nimeyaona mateso ya watu wangu walioko Misri, nami nimekisikia kilio chao kwa sababu ya wasimamizi wao; maana nayajua maumivu yao; nami nimeshuka ili niwaokoe na mikono ya Wamisri, niwapandishe kutoka nchi ile, hata nchi njema, kisha pana; nchi ijaayo maziwa na asali; hata mahali pa Mkanaani, na Mhiti, na Mwamori, na Mperizi, na Mhivi, na Myebusi. Basi, tazama, kilio cha wana wa Israeli kimenifikilia; tena nimeyaona hayo mateso ambayo Wamisri wanawatesa.”

Kumbukumbu 26:6-9 “Wamisri wakatuonea, wakatutesa, wakatutumikisha utumwa mzito. Tukamlilia Bwana, Mungu wa baba zetu; Bwana akasikia sauti yetu, akaona na taabu yetu, na kazi yetu, na kuonewa kwetu. Bwana akatutoa kutoka Misri kwa mkono wa nguvu, na kwa mkono ulionyoshwa, na kwa utisho mwingi, na kwa ishara, na kwa maajabu; naye ametuingiza mahali hapa, na kutupa nchi hii, nchi ijaayo maziwa na asali.”

Aidha kwa sababu Mungu alichukizwa na uonevu waliotendewa wana wa Israel kule Misri, aliwaonya waache kuonea watu hata wageni akiwakumbusha kuwa na wao walikuwa wageni katika inchi ya Misri, Neno hili sio kwaajili ya Israel pekee leo, lakini linamuhusu kila mmoja wetu kwamba kupitia kitabu hiki cha Musa (Torati) tunawekewa msingi wa kutokuwaonea watu wengine na kutujulisha kuwa Mungu anachukizwa na uonevu na wakati mwingine ataingilia kati kuhakikisha kuwa anawatoa watu wake kutoka katika mateso na uonevu.

Kutoka 22:21-24 “Usimwonee mgeni, wala kumtendea jeuri; kwa kuwa ninyi mlikuwa wageni katika nchi ya Misri. Usimtese mjane ye yote aliyefiwa na mumewe, wala mtoto yatima. Ukiwatesa watu hao katika neno lo lote, nao wakanililia mimi, hakika yangu nitasikia kilio chao, na hasira yangu itawaka moto, nami nitawaua ninyi kwa upanga; na wake wenu watakuwa wajane, na watoto wenu mayatima.”

Kutoka 23:9 “Usimwonee mgeni; maana, ninyi mwajua moyo wa mgeni ulivyo, kwa kuwa ninyi mlikuwa wageni katika nchi ya Misri.”

Waamuzi 10:11-12 “Naye Bwana akawaambia wana wa Israeli, Je! Sikuwaokoa ninyi na hao Wamisri, na Waamori, na wana wa Amoni, na Wafilisti? Hao Wasidoni nao, na Waamaleki, na Wamaoni, waliwaonea, nanyi mlinililia, nami niliwaokoa na mikono yao.”

Tumeona namna na jinsi ambavyo Mungu anachukizwa na uonevu, uonevu katika mazingira mbalimbali na kila eneo, iwe dhuluma, kuonea masikini, kunyanyasa wanyonge, kuwaonea wajane na yatima, na kuwaonea wageni, na kadhalika haya yote Mungu ameayaamrisha katika neno lake kuwa anachukizwa nayo, anachukizwa na ukoloni, anachukizwa na unyonyaji, anachukizwa na biashara ya utumwa, na mtu mwenye nguvu kumuonea mnyonge na hata taifa moja kulionea taifa lingine, Israel walipoonewa na wamisri, waamori, wana wa Amoni na hata wafilisti na mataifa mengine Mungu alichukizwa na kuingilia kati kukomesha uonevu huo, lakini sio hivyo tu Mungu vile vile anachukizwa na uonevu unaofanywa na shetani na mapepo yake, na zaidi sana anachukizwa na uonevu wa magonjwa na kadhalika sasa ni jinsi gani Mungu anajihusisha na kukomesha uonevu?  Neno la Mungu linatuonyesha wazi kuwa kila wakati Mungu alipotaka kukomesha uonevu aliliacha swala hilo Kwa Mungu Roho Mtakatifu, na ndipo unapoweza kuona Roho wa Mungu akitoa nguvu ya kukomesha uonevu. Roho Mtakatifu alishusha nguvu zake na kuchochea wivu kwa watumishi wake na kuwataharakisha ili kuwakomboa watu wake, hii ni ishara ya wazi kuwa Mungu hawezi kuvumilia dhuluma na uonevu.

Yeremiah 21:12 “Ee nyumba ya Daudi, Bwana asema hivi, Hukumuni hukumu ya haki asubuhi, mkawaponye waliotekwa nyara na mkono wake aliyewadhulumu, ghadhabu yangu isije ikatoka kama moto, ikaunguza, asiweze mtu ye yote kuuzima, kwa sababu ya uovu wa matendo yenu.”

Roho wa Bwana  na Nguvu ya uonevu.

Kama jinsi ambavyo tumejifunza tangu mwanzo ya kuwa Mungu anachukizwa na uonevu, na watu wake wanapougua na kulia kwaajili ya uonevu wa aina yoyote Mungu alikuwa tayari kuwainua wasaidizi, au watumishi wake au waamuzi ambao aliwapaka mafuta yaani aliwapa nguvu za Roho wake Mtakatifu kwa kusudi la kuwaokoa na adui zao waliowaonea, Mungu alifanya hivyo kila wakati, na kitabu cha waamuzi ni mojawapo ya mfano mzuri wa utendaji wa Mungu dhidi ya uonevu

Waamuzi 2:18. “Na wakati Bwana alipowainulia waamuzi, ndipo Bwana alikuwa pamoja na mwamuzi huyo, akawaokoa na mikono ya adui zao siku zote za mwamuzi huyo; maana Bwana alighairi kwa ajili ya kuugua kwao kwa sababu ya watu wale waliowaonea na kuwasumbua.

Waamuzi walipoinuliwa na Mungu waliweza kuwaokoa wana wa Israel kutoka katika mikono ya adui zao na kuwasababishia Amani na utulivu, lakini waamuzi hao hawakuenda kwa nguvu zao wenyewe bali wakati wote walipakwa mafuta na Roho Mtakatifu na kupewa nguvu ili kukomesha nguvu ya uonevu, hata kama wakati mwingine uonevu huo ulisababishwa na makossa na dhambi ya Israel wenyewe, lakini kila walipomlilia alinuka kuwasaidia

-          Wakati wa uonevu wa Kushanrishathaimu  mfalme wa Mesopotamia  aliwaonea Israel na kuwakandamiza katika utumwa mzito na Israel wakawa watumwa wake kwa miaka nane mpaka walipolia na kuugua mbele za Mungu, Na Mungu aliwainulia Mwamuzi aliyeitwa Othiniel ambaye hakwenda vitani hivi hivi bali alijiwa na Roho wa Bwana ona:-

 

Waamuzi 3:7-11 “Wana wa Israeli walifanya yaliyo maovu mbele za macho ya Bwana, nao wakamsahau Bwana, Mungu wao, nao wakawatumikia Mabaali na Maashtorethi. Kwa hiyo hasira za Bwana ziliwaka juu ya Israeli, naye akawauza na kuwatia mikononi mwa Kushan-rishathaimu mfalme wa Mesopotamia; na wana wa Israeli wakamtumikia huyo Kushan-rishathaimu muda wa miaka minane. Kisha wana wa Israeli walipomlingana Bwana, Bwana akawainulia wana wa Israeli mwokozi, aliyewaokoa, yaani, Othnieli mwana wa Kenazi, ndugu mdogo wa Kalebu. Roho ya Bwana ikamjilia juu yake, naye akawa mwamuzi wa Israeli; akatoka kwenenda vitani, naye Bwana akamtia huyo Kushan-rishathaimu, mfalme wa Mesopotamia, mkononi mwake; na mkono wake ukamshinda Kushan-rishathaimu. Nayo nchi ikawa na amani muda wa miaka arobaini. Kisha Othnieli, mwana wa Kenazi, akafa.”

 

-          Tunasoma tena namna na jinsi Israel walivyofanya uovu na kutoa nafasi ya kuonewa tena walionewa sana na wamidiani na amaleki, walikuwa hata wakilima wakati wa mavuno chakula kilichukuliwa, mifugo ilichukuliwa hawakuwa na amani kiasi cha kuamua kuishi kwenye mashimo kwa ujumla walifanyiwa mambo mabaya neno la Mungu linasema walitwezwa sana ! yaani walionewa mno au walionewa kupita kiasi

 

Waamuzi 6:1-6 “Kisha wana wa Israeli walifanya yaliyo maovu mbele za macho ya Bwana; Bwana akawatia mikononi mwa Midiani muda wa miaka saba Mkono wa Midiani ulikuwa na nguvu juu ya Israeli; tena kwa sababu ya Midiani wana wa Israeli walijifanyia hayo mashimo yaliyo milimani, na hayo mapango, na hizo ngome. Basi ikawa, hapo Israeli walipokuwa wamepanda mashamba, Wamidiani wakakwea, na Waamaleki, na hao wana wa mashariki; wakakwea juu yao; wakapanga marago juu yao, na kuyaharibu hayo maongeo ya nchi, hata ufikapo Gaza, wala hawakuacha katika Israeli riziki ziwazo zote; kondoo, wala ng'ombe, wala punda. Kwa maana walikwea na ng'ombe zao na hema zao, wakaja mfano wa nzige kwa wingi; wao na ngamia zao pia walikuwa hawana hesabu; nao waliingia katika hiyo nchi ili kuiharibu. Israeli walitwezwa sana kwa sababu ya Wamidiani; nao wana wa Israeli wakamlilia Bwana.”

 

Wamidiani walifanya uonevu juu ya wana wa Israel kiasi cha kusikitisha sana mpaka wana wa Israel walipomlilia Bwana ndipo Bwana alimpomuinua Gideoni na maandiko yanaeleza ya kuwa Gideoni alijiliwa na Roho wa Bwana juu yake ambaye alimsaidia kupanga vita na kuleta ushindi kwa askari wachache.

 

Waamuzi 6:33-34 “Wakati huo Wamidiani na Waamaleki, na hao wana wa mashariki walikutana pamoja; wakavuka na kupanga hema zao katika bonde la Yezreeli. Lakini roho ya Bwana ikaja juu yake Gideoni; naye akapiga tarumbeta; na Abiezeri walikutanika na kumfuata.”

 

-          Wana wa Amoni waliwasumbua sana Israel waliwapiga na kuwatawala kiasi ambacho wazee wa mji waliamua kwenda kumuomba Yeftha ili aje awasaidie dhidi ya uonevu na taabu waliyokumbana nayo wakati huo kutoka kwa wana wa Amoni angalia

 

Waamuzi 11:5-7 “Ikatukia, hapo wana wa Amoni walipopigana na Israeli, wazee wa Gileadi wakaenda kumtwaa huyo Yeftha katika ile nchi ya Tobu; wakamwambia Yeftha, Njoo wewe uwe kichwa chetu, ili tupate kupigana na wana wa Amoni. Yeftha akawaambia wazee wa Gileadi, Je! Ninyi hamkunichukia mimi na kunifukuza nitoke katika nyumba ya baba yangu? Basi kwani kunijilia hivi sasa wakati mlio katika taabu?

 

Yeftha aliwezaje kupambana na wana wa Amoni? Maandiko yanaeleza ya kuwa Roho wa Bwana alikuja juu yake na ni Mungu aliyemwenzesha Yeftha, kushindana na mfalme wa wana wa Amani na kuwashinda

 

Waamuzi 11:29-33 “Ndipo roho ya Bwana ikamjilia juu yake Yeftha, naye akapita katika Gileadi na Manase, akapita na katika Mispa ya Gileadi, na kutoka hapo Mispa ya Gileadi akapita kuwaendea wana wa Amoni.Naye Yeftha akamwekea Bwana nadhiri, akasema, Kwamba wewe utawatia wana wa Amoni mkononi mwangu kweli, ndipo itakuwa ya kwamba, kile kitakachotoka katika milango ya nyumba yangu kunilaki, hapo nitakaporudi na amani kutoka kwa hao wana wa Amoni, kitu hicho kitakuwa ni cha Bwana, nami nitakisongeza kiwe sadaka ya kuteketezwa. Basi Yeftha akavuka kuwaendea wana wa Amoni ili kupigana nao; naye Bwana akawaua mkononi mwake. Akawapiga kutoka Aroeri hata kufikilia Minithi, miji ishirini, na mpaka Abel-keramimu, akawapiga kwa machinjo makuu mno. Basi hivyo wana wa Amoni walishindwa mbele ya wana wa Israeli.”

 

-          Wafilisti wakati wote wa maisha ya Samsoni walikuwa waonevu dhidi ya Israel, lakini Mungu alimuinua Samsoni kama mwamuzi ili kuwakomesha wafilisti ni namna gani uonevu huo ulikomesha ilikuwa kupitia Roho Mtakatifu ambaye alimshughulisha Samsoni kwa nguvu angalia;-

 

Waamuzi 15:14-16 “Alipofika Lehi, Wafilisti wakapiga kelele walipokutana naye; ndipo roho ya Bwana ikamjia kwa nguvu, na zile kamba zilizokuwa juu ya mikono yake zikawa kama kitani iliyoteketezwa kwa moto, na vile vifungo vyake vikaanguka mikononi mwake. Naye akaona mfupa mbichi wa taya ya punda, akautwaa, akapiga watu elfu kwa mfupa huo; Samsoni akasema, Kwa taya ya punda chungu juu ya chungu, Kwa taya ya punda nimepiga watu elfu.”

Hitimisho:

Katika vifungu vyote hapo juu somo kubwa tunalojifunza ni kuwa hakuna mahali unaweza kutatua changamoto za uonevu wa aina yoyote ile bila Roho wa Bwana, Katika juma hili la Pentekoste wengi wa wahubiri watafundisha na kukazia kuhusu ujazo wa Roho Mtakatifu, watafundisha umuhimu wa nguvu za Roho Mtakatifu, wataombea watu wajazwe Roho Mtakatifu, watafundisha umuhimu wa kunena kwa Lugha, watafundisha kuhusu ubatizo wa Roho Mtakatifu, watafundisha kunena kwa lugha kama ishara ya ujazo wa roho Mtakatifu, watafundisha mpaka karama za Roho, Watafundisha namna na jinsi Roho wa Mungu anavyosaidia katika kuomba, kutia nguvu, kutupa ujasiri na kadhalika na kadhalika hayo yote ni sawa na ni ya muhimu lakini Roho Mtakatifu ni kwaajili ya nini, ni kwaajili ya kukomesha uonevu, Roho Mtakatifu alipokuwa juu ya masihi Yaani Bwana Yesu tunaona wakati wote alishughulika na walioonewa,  Hata wafalme walipotawala Mungu aliwapaka mafuta ili wakomeshe uonevu dhidi ya watu wake, kanisa katika wakati huu halina budi kurudi kwenye msingi huu, tunamuhitaji Roho Mtakatifu na nguvu zake ili tuwasaidie ndugu zetu kwa kuwatoa katika uonevu wa aina mbalimbali, uonevu wa dhambi, uonevu wa ibilisi, uonevu wa magonjwa, na ana nyingine zote za uonevu!

 Luka 4:18-19 “Roho wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa, Na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa.”

Matendo 10:38 “habari za Yesu wa Nazareti, jinsi Mungu alivyomtia mafuta kwa Roho Mtakatifu na nguvu naye akazunguka huko na huko, akitenda kazi njema na kuponya wote walioonewa na Ibilisi; kwa maana Mungu alikuwa pamoja naye

Kwa hiyo Roho Mtakatifu na nguvu zake ni kwaajili ya kuwaokoa wote walioonewa na ibilisi, ni nguvu kwaajili ya kufungua watu, ni nguvu za kuwapa watu ufahamu, kuwafanya vipofu kuona, ni nguvu za kuwaacha huru waliotekwa, na waliosetwa yaani waliogandamizwa na nguvu za giza,  ni nguvu za kuutanganza mwaka wa Bwana uliokubaliwa yaani ni wakati wa kuwaweka huru watu kutoka katika vifungo mbalimbali, Mungu wetu kupitia Roho wake Mtakatifu ataachlia karama na vipawa vikubwa na kuwezesha watu kufanya kazi yake kwa uhodari na kwa hekima na maarifa  na kwa kutenda kazi iliyo njema ya kuwasaidia walioonewa

Na. Rev. Innocent Mkombozi Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye hekima!



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni