Jumapili, 28 Julai 2024

Hukumu ya Mungu isiyoepukika!


Warumi 2:1-8 “Kwa hiyo, wewe mtu uwaye yote uhukumuye, huna udhuru; kwa maana katika hayo umhukumuyo mwingine wajihukumu mwenyewe kuwa na hatia; kwa maana wewe uhukumuye unafanya yale yale. Nasi twajua ya kuwa hukumu ya Mungu ni ya kweli juu yao wafanyao hayo. Wewe binadamu, uwahukumuye wale wafanyao hayo na kutenda yayo hayo mwenyewe, je! Wadhani ya kwamba utajiepusha na hukumu ya Mungu? Au waudharau wingi wa wema wake na ustahimili wake na uvumilivu wake, usijue ya kuwa wema wa Mungu wakuvuta upate kutubu? Bali kwa kadiri ya ugumu wako, na kwa moyo wako usio na toba, wajiwekea akiba ya hasira kwa siku ile ya hasira na ufunuo wa hukumu ya haki ya Mungu, atakayemlipa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake; wale ambao kwa saburi katika kutenda mema wanatafuta utukufu na heshima na kutokuharibika, watapewa uzima wa milele; na wale wenye fitina, wasioitii kweli, bali wakubalio dhuluma, watapata hasira na ghadhabu;”




Utangulizi:

Hukumu ya Mungu kwa wanadamu ni jambo lisiloepukika,Tangu mwanzo Mwanadamu na viumbe wengine walipokosea Mungu mara moja alitoa hukumu, alimuhukumu Shetani, alimuhukumu mwanadamu, Alimuhukumu mwanaume na alimuhukumu mwanamke kila mmoja kwa kadiri ya uhusika wake katika kosa lile la bustanini mwa Edeni, kwa hiyo hukumu ya Mungu ni jambo lisiloepukika, ukweli kuhusu hukumu ya Mungu ni jambo lenye kutisha sana kwa wanadamu, hata hivyo leo tutachukua Muda kutafakari kwa undani kuhusu hukumu ya Mungu na umuhimu wake katika mtazamo wa upendo wake na rehema zake na tabia yake ya uungu ambayo itakushangaza!

Warumi 2:12-16 “Kwa kuwa wote waliokosa pasipo sheria watapotea pasipo sheria, na wote waliokosa, wenye sheria, watahukumiwa kwa sheria. Kwa sababu sio wale waisikiao sheria walio wenye haki mbele za Mungu, bali ni wale waitendao sheria watakaohesabiwa haki. Kwa maana watu wa Mataifa wasio na sheria wafanyapo kwa tabia zao yaliyo ndani ya torati, hao wasio na sheria wamekuwa sheria kwa nafsi zao wenyewe. Hao waionyesha kazi ya torati iliyoandikwa mioyoni mwao, dhamiri yao ikiwashuhudia, na mawazo yao, yenyewe kwa yenyewe, yakiwashitaki au kuwatetea; katika siku ile Mungu atakapozihukumu siri za wanadamu, sawasawa na injili yangu, kwa Kristo Yesu.”

Swala zima la hukumu kwa mujibu wa maandiko Mungu hakuwapa wanadamu, na tumekatazwa kuhukumu, bali amepewa Yesu Kristo na Baba yake aliye mbinguni, kwa hiyo hakuna mtu awaye yote mwenye mamlaka ya kuhukumu isipokuwa mwana wa Adamu yaani Yesu Kristo mwenyewe, kuhukumu ni kukaa katika kiti cha Mungu. Fundisho kuhusu hukumu linatawala maandiko yote katika agano la kale na jipya, Utukufu wa Mungu unaonekana na kufunuliwa katika namna anavyohukumu, Mungu anamtaka kila mmoja awajibike na kwa sababu hiyo hakuna mwanadamu wala taifa litakaloweza kuiepuka hukumu ya Mungu na Yesu ndiye Mwamba wa hukumu hiyo:-

Yohana 5:22-30 “Tena Baba hamhukumu mtu ye yote, bali amempa Mwana hukumu yote; ili watu wote wamheshimu Mwana kama vile wanavyomheshimu Baba. Asiyemheshimu Mwana hamheshimu Baba aliyempeleka. Amin, amin, nawaambia, Yeye alisikiaye neno langu na kumwamini yeye aliyenipeleka yuna uzima wa milele; wala haingii hukumuni, bali amepita kutoka mautini kuingia uzimani. Amin, amin, nawaambia, Saa inakuja, na sasa ipo, wafu watakapoisikia sauti ya Mwana wa Mungu, na wale waisikiao watakuwa hai. Maana kama vile Baba alivyo na uzima nafsini mwake, vivyo hivyo alimpa na Mwana kuwa na uzima nafsini mwake. Naye akampa amri ya kufanya hukumu kwa sababu ni Mwana wa Adamu. Msistaajabie maneno hayo; kwa maana saa yaja, ambayo watu wote waliomo makaburini wataisikia sauti yake. Nao watatoka; wale waliofanya mema kwa ufufuo wa uzima, na wale waliotenda mabaya kwa ufufuo wa hukumu.Mimi siwezi kufanya neno mwenyewe; kama nisikiavyo ndivyo nihukumuvyo; na hukumu yangu ni ya haki, kwa sababu siyatafuti mapenzi yangu mimi, bali mapenzi yake aliyenipeleka.”

Kwa nini Masihi amepewa kuhukumu? Kwa sababu uwezo wake wa kuhukumu ni mkubwa sana na uko juu na sio wa kibinadamu, na kwa sababu yeye amepitia uanadamu anatujua vema lakini pia kwa sababu kuhukumu kwake hakutokani na yale yanayoonekana kwa macho, wala yale ayasikiayo kwa masikio yake lakini hukumu yake ni ya haki kama alivyosema mwenyewe na uwezo wake ni mkubwa sana kwa sababu ya Roho wa Mungu na hekima yake kuu

Isaya 11:1-5 “Basi litatoka chipukizi katika shina la Yese, na tawi litakalotoka katika mizizi yake litazaa matunda.Na roho ya Bwana atakaa juu yake, roho ya hekima na ufahamu, roho ya shauri na uweza, roho ya maarifa na ya kumcha Bwana; na furaha yake itakuwa katika kumcha Bwana; wala hatahukumu kwa kuyafuata ayaonayo kwa macho yake, wala hataonya kwa kuyafuata ayasikiayo kwa masikio yake;bali kwa haki atawahukumu maskini, naye atawaonya wanyenyekevu wa dunia kwa adili; naye ataipiga dunia kwa fimbo ya kinywa chake, na kwa pumzi ya midomo yake atawaua wabaya. Na haki itakuwa mshipi wa viuno vyake, na uaminifu mshipi wa kujifungia.”

Kumbukumbu 1:17 “Msitazame nafsi za watu katika hukumu; mwasikize wadogo na wakubwa sawasawa; msiche uso wa mtu awaye yote; kwa kuwa hukumu ni ya Mungu; na lile neno liwashindalo mniletee mimi, nami nitalisikiza.”

Kumbukumbu 32:3-4 “Maana nitalitangaza Jina la Bwana; Mpeni ukuu Mungu wetu.Yeye Mwamba, kazi yake ni kamilifu; Maana, njia zake zote ni haki. Mungu wa uaminifu, asiye na uovu, Yeye ndiye mwenye haki na adili.”

Leo tutachukua muda moja kwa moja kutafakari kwa kina na mapana na marefu kuhusu hukumu za Mungu ambazo kimsingi ziko aina nne za hukumu ambazo tutaziangalia kwa kuzingatia vipengele vinne vifuatavyo sawa na ufunuo.

 

1.       Hukumu iliyoko sasa – Paroúsa Krisi

2.       Hukumu ya adhabu – Krima

3.       Hukumu isiyo ya adhabu – Krino

4.       Hukumu isiyotarajiwa – Aprosmenos   

 

Hukumu iliyoko sasa – Paroúsa Krisi

Hukumu hii kwa kiingereza inaitwa Present Judgement kwa kiyunani Paroúsa Krisi yaani hukumu hii inategemeana na mkao ulioko sasa wa hali ya kiroho za wanadamu, kama mwanadamu ameukubali mpango wa Mungu wa ukombozi kwa kumwamini Bwana Yesu kama Bwana na mwokozi wake huyo kwa sasa haukumiwi, na yule ambaye hajaukubali mpango wa Mungu wa ukombozi kupitia Yesu Kristo huyo amekwisha kuhukumiwa, Instant Judgement.au “Quckly Decision” “quicly judgemnt

Yohana 3:16-18 “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.     Maana Mungu hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye. Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa Mungu.”

Yohana 5:24 “Amin, amin, nawaambia, Yeye alisikiaye neno langu na kumwamini yeye aliyenipeleka yuna uzima wa milele; wala haingii hukumuni, bali amepita kutoka mautini kuingia uzimani.”

Kwa hiyo katika ulimwengu huu wako watu ambao wamehukumiwa tayari yaani hivi tunavyozungumza hapa wako watu wa aina mbili duniani na wote wanaendelea na shughuli zao wakiwa wamehukumiwa yaani wale wasiomwamini Yesu na kundi la pili ni watu ambao hawako chini ya hukumu hawahukumiwi hawa ni wale waliomuamini Bwana Yesu na kumkubali kama Bwana na mwokozi wao, Hukumu hii inaendelea ikiendeshwa na Roho Mtakatifu kupitia kazi anayoifanya sasa ya kuwashuhudia watu kwa habari ya dhambi, haki na hukumu, kila wakati na kila siku injili ihubiriwapo mtu akimpokea Yesu anahama kutoka upande wa wale waliohukumiwa kwenda upande wa wale wasiohukumiwa,Injili ikihubiriwa ukaikubali sasa uko nje ya hukumu, na ukiikataa uko hukumuni.

Yohana 16:7-8 “Lakini mimi nawaambia iliyo kweli; yawafaa ninyi mimi niondoke, kwa maana mimi nisipoondoka, huyo Msaidizi hatakuja kwenu; bali mimi nikienda zangu, nitampeleka kwenu. Naye akiisha kuja, huyo atauhakikisha ulimwengu kwa habari ya dhambi, na haki, na hukumu.”
             

Hukumu ya adhabu – Krima

Hii ni moja ya kundi la hukumu (Judgement or Condemnation) ambayo inahusiana na siku ya mwisho wakati Kristo atakapokalia kiti cha enzi cha hukumu na kumuhukumu kila mmoja kwa kadiri ya matendo yake hukumu hii pia inaitwa hukumu ya adhabu au hukumu ya aibu, siku ya hukumu hii kila mtu atasimama mbele ya kiti hicho cha hukumu cha Mungu na kutoa hesabu yake mwenyewe. Hukumu hii kiyunani Krima au Krinete maana yake to Condemn, au making a negative assessment of a person or thing, kufanya maamuzi hasi dhidi ya mtu au kitu.

Warumi 14:10-12 “Lakini wewe je! Mbona wamhukumu ndugu yako? Au wewe je! Mbona wamdharau ndugu yako? Kwa maana sisi sote tutasimama mbele ya kiti cha hukumu cha Mungu. Kwa kuwa imeandikwa, Kama niishivyo, anena Bwana, kila goti litapigwa mbele zangu; Na kila ulimi utamkiri Mungu. Basi ni hivyo, kila mtu miongoni mwetu atatoa habari zake mwenyewe mbele za Mungu.”

2Wakorintho 5:10 “Kwa maana imetupasa sisi sote kudhihirishwa mbele ya kiti cha hukumu cha Kristo, ili kila mtu apokee ijara ya mambo aliyotenda kwa mwili, kadiri alivyotenda, kwamba ni mema au mabaya.”


Daniel 12:2-3 “Tena, wengi wa hao walalao katika mavumbi ya nchi wataamka, wengine wapate uzima wa milele, wengine aibu na kudharauliwa milele. Na walio na hekima watang'aa kama mwangaza wa anga; na hao waongozao wengi kutenda haki watang'aa kama nyota milele na milele.”

Muhubiri 12:14 “Kwa maana Mungu ataleta hukumuni kila kazi, pamoja na kila neno la siri, likiwa jema au likiwa baya.”

Ufunuo 20:11-12 “Kisha nikaona kiti cha enzi, kikubwa, cheupe, na yeye aketiye juu yake; ambaye nchi na mbingu zikakimbia uso wake, na mahali pao hapakuonekana. Nikawaona wafu, wakubwa kwa wadogo, wamesimama mbele ya hicho kiti cha enzi; na vitabu vikafunguliwa; na kitabu kingine kikafunguliwa, ambacho ni cha uzima; na hao wafu wakahukumiwa katika mambo hayo yaliyoandikwa katika vile vitabu, sawasawa na matendo yao.”  
     

Ufufuo huu ni wa hukumu ya adhabu,(Krima) na itakuwa ni hukumu ya aibu kwa sababu Neno Krima linalotumika kuelezea hukumu ya adhabu lina maana ya hukumu isiyohukumu matokeo tu bali inayohusu utafiti wa kina na uzingativu wa kila kilichofanyika kuanzia kwenye dhamiri na machakato mzima wa tukio pamoja na uzito wa ushahidi na mazingira  katika mtazamo wa kibinadamu, lakini katika mtazamo wa kiungu hukumu hii inahusisha hukumu iliyo sawasawa na Haki ya Mungu na tabia yake, na kwa kuwa Mungu ni mkamilifu hukumu yake itakuwa sahihi  na madhara au adhabu itakayoambatana na hukumu hii itakuwa ni sahihi, kwa hiyo hukumu yake itakuwa ni matokeo na ufunuo ulio sahihi ukiingia ndani katika dhamiri ya mwanadamu kwa hiyo itakuwa ni hukumu ambayo hata yeye anayehukumiwa atakubaliana na ile adhabu atakayopewa au ataridhishwa na maamuzi ya jaji mkuu Yesu Kristo.   
     

Hukumu isiyo ya adhabu – Krino

Hukumu hii isiyo ya dhabu ni hukumu inayowahusu wale wote ambao wamemuamini Yesu Kristo hawa kimaandiko hawahusiki katika hukumu ya adhabu (Krima), na badala yake hawa wana adhabu iitwayo Krino hii ni hukumu isiyo ya adhabu imetajwa na Paulo Mtume katika:-

Warumi 8:1-2 “Sasa, basi, hakuna hukumu ya adhabu juu yao walio katika Kristo Yesu. Kwa sababu sheria ya Roho wa uzima ule ulio katika Kristo Yesu imeniacha huru, mbali na sheria ya dhambi na mauti

Warumi 8:33-34. “Ni nani atakayewashitaki wateule wa Mungu? Mungu ndiye mwenye kuwahesabia haki.Ni nani atakayewahukumia adhabu? Kristo Yesu ndiye aliyekufa; naam, na zaidi ya hayo, amefufuka katika wafu, naye yuko mkono wa kuume wa Mungu; tena ndiye anayetuombea.”

Krino ni hukumu isiyo ya adhabu ambayo itawahusu watu waliookolewa, yaani wale waliomuamini Yesu hawatakutana na hukumu ya adhabu lakini watakutana na hukumu itakayofuatilia kwa haki, kwanini mtu Fulani alifanya jambo Fulani na thawabu yake itakuwa ni thawabu gani? Hukumu hii katika tamaduni za kiyunani Mgeni rasmi hukaa katika kiti kinachoitwa Bema au jukwaa au sehemu maalumu iliyoinuka kwaajili ya kutoa thawabu, za kimichezo ambapo wanamichezo wanapata thawabu au medali kulingana na kazi waliyoifanya na hakuna madhara kwa waliokosa medali. Hii ni hukumu ya watakatifu ni hukumu ya kutoa hesabu mbele za Kristo kwa kile tulichofanya. Katika somo la ufahamu kuhusu maswala ya hukumu The doctrine of Judgement Krino kiyunani kwa kiingereza ni to separate, put asunder, to pick out, Select, choose, to approve, esteem, to prefer, to give an opinion, to determine, resolve, decree, ni hukumu ya kutenganisha, kuchanganua, kuchagua, kuidhinisha, kuthaminisha, kupendelea, kutoa maoni, kuazimia, kuthibitisha, kwa hiyo itakuwa ni hukumu ya kuja kuthibitisha nani anafaa kuwa nini katika ufalme wa Mungu na sio kwa kusudi la kuadhibu.

1Wakorintho 3:12-15 “Lakini kama mtu akijenga juu ya msingi huo, dhahabu au fedha au mawe ya thamani, au miti au majani au manyasi, kazi ya kila mtu itakuwa dhahiri. Maana siku ile itaidhihirisha, kwa kuwa yafunuliwa katika moto; na ule moto wenyewe utaijaribu kazi ya kila mtu, ni ya namna gani. Kazi ya mtu aliyoijenga juu yake ikikaa, atapata thawabu. Kazi ya mtu ikiteketea, atapata hasara; ila yeye mwenyewe ataokolewa; lakini ni kama kwa moto.”

Mathayo 25:14-28 “Maana ni mfano wa mtu atakaye kusafiri, aliwaita watumwa wake, akaweka kwao mali zake. Akampa mmoja talanta tano, na mmoja talanta mbili, na mmoja talanta moja; kila mtu kwa kadiri ya uwezo wake; akasafiri. Mara yule aliyepokea talanta tano akaenda, akafanya biashara nazo, akachuma faida talanta nyingine tano. Vile vile na yule mwenye mbili, yeye naye akachuma nyingine mbili faida. Lakini yule aliyepokea moja alikwenda akafukua chini, akaificha fedha ya bwana wake. Baada ya siku nyingi akaja bwana wa watumwa wale, akafanya hesabu nao. Akaja yule aliyepokea talanta tano, akaleta talanta nyingine tano, akisema, Bwana, uliweka kwangu talanta tano; tazama, talanta nyingine tano nilizopata faida. Bwana wake akamwambia, Vema, mtumwa mwema na mwaminifu; ulikuwa mwaminifu kwa machache, nitakuweka juu ya mengi; ingia katika furaha ya bwana wako. Akaja na yule aliyepokea talanta mbili, akasema, Bwana, uliweka kwangu talanta mbili; tazama, talanta nyingine mbili nilizopata faida. Bwana wake akamwambia, Vema, mtumwa mwema na mwaminifu; ulikuwa mwaminifu kwa machache, nitakuweka juu ya mengi; ingia katika furaha ya bwana wako. Akaja na yule aliyepokea talanta moja, akasema, Bwana, nalitambua ya kuwa wewe u mtu mgumu, wavuna usipopanda, wakusanya usipotawanya;basi nikaogopa, nikaenda nikaificha talanta yako katika ardhi; tazama, unayo iliyo yako. Bwana wake akajibu, akamwambia, Wewe mtumwa mbaya na mlegevu, ulijua ya kuwa navuna nisipopanda, nakusanya nisipotawanya; basi, ilikupasa kuiweka fedha yangu kwa watoao riba; nami nikija ningalipata iliyo yangu na faida yake. Basi, mnyang'anyeni talanta hiyo, mpeni yule aliye nazo talanta kumi

Mathayo 24:45-46 “Ni nani basi yule mtumwa mwaminifu mwenye akili, ambaye bwana wake alimweka juu ya nyumba yake, awape watu chakula kwa wakati wake? Heri mtumwa yule, ambaye bwana wake ajapo atamkuta akifanya hivyo.”

Hukumu hii ni hukumu ya watakatifu, kila mtu aliyeokolewa anapaswa kumtumikia Mungu, na Kristo atakapokuja kulinyakua kanisa, pale mawinguni itakuwepo nafasi ya kutoa taji na karamu ya mwana kondoo wakati huu kila mkristo atahukumiwa sawa na kazi aliyoifanya na jinsi na namna alivyoitumia talanta aliyopewa kwa uaminifu au vinginevyo na hapo thawabu zitatolewa, hakutakuwa na adhabu lakini kila mtu atastahili heshima yake kulingana na bidii, akili, muda na namna tunavyojitoa kwa Mungu ikiwa ni pamoja na kuwalisha watu wake, kwa hiyo kama sisi ni wachungaji tuwalishe watu chakula yaani neno la Mungu kwa wakati wake, kama una kipawa chochote kile kitumie kwa kadiri uwezavvyo na kwa kadiri ya neema huku ukiwa na dhamiri safi kwa sababu hukumu hii ni hukumu isiyoepukika pia katika hukumu hii hakuna mtu anayeweza kuwashitaki watu wa Mungu kwa sababu zozote wala hakuna mtu anayeweza kutuhukumu na kudai kuwa hawa ni wakosa, hukumu hii ni hukumu isiyo na madhara.        
    

Hukumu isiyotarajiwa – Aprosmenos

Katika hukumu zote zilizotajwa hapo juu, hii ndio hukumu itakayoshangaza watu kuliko hukumu zote, katika hukumu hii maamuzi atakayoyatoa Yesu Kristo yatadhihirisha uwezo wake mkubwa na hekima yake kubwa na ile hali ya kuwa yeye ni Bwana na hakuna mtu wa kumuamulia lolote wala kutabiri lolote, hukumu hii inadhihirisha kwamba Mungu mwenyewe ana haki ya kuamua na uwezo wake wa kuhukumu ni wa hali ya juu na wa tofauti sana.
 

Hukumu hii iko katika maamuzi ya Mungu mwenyewe na inaitwa hukumu isiyotabirika katika lugha ya kiyunani linatumika neno hilo Aprosmenos ambalo kwa kiingereza ni unanticipated, unforeseen, unexpected, difficulties  predicted kwa hiyo ni hukumu isiyotegemewa, ni hukumu isiyotarajiwa, ni hukumu isiyotabirika ni hukumu ambayo ni ngumu kimatazamio, hukumu hii iko chini ya maamuzi ya Mungu mwenyewe bila kujali kuwa kuna haki au hakuna haki mfano lakini iko haki ambayo Mungu mwenyewe katika mtazamo wake huiona lakini wanadamu hawawezi.

Warumi 9:10-16 “Wala si hivyo tu, lakini Rebeka naye, akiisha kuchukua mimba kwa mume mmoja, naye ni Isaka, baba yetu, (kwa maana kabla hawajazaliwa wale watoto, wala hawajatenda neno jema wala baya, ili lisimame kusudi la Mungu la kuchagua, si kwa sababu ya matendo, bali kwa sababu ya nia yake aitaye), aliambiwa hivi, Mkubwa atamtumikia mdogo. Kama ilivyoandikwa, Nimempenda Yakobo, bali Esau nimemchukia.Tuseme nini basi? Kuna udhalimu kwa Mungu? Hasha! Maana amwambia Musa, Nitamrehemu yeye nimrehemuye, nitamhurumia yeye nimhurumiaye. Basi, kama ni hivyo, si katika uwezo wa yule atakaye, wala wa yule apigaye mbio; bali wa yule arehemuye, yaani, Mungu.”

Warumi 9:20-21 “La! Sivyo, Ee binadamu; wewe u nani umjibuye Mungu? Je! Kitu kilichoumbwa kimwambie yeye aliyekiumba, Kwani kuniumba hivi? Au mfinyanzi je! Hana amri juu ya udongo, kwa fungu moja la udongo kuumba chombo kimoja kiwe cha heshima, na kimoja kiwe hakina heshima? 

Unaona ili lisimame kusudi la Mungu la kuchagua Maneno haya yanaonyesha kuwa mwanadamu awaye yote anapokuwa na kesi mahakamani awe amekosa au awe hajakosea bado anakuwa na mashaka kwa sababu mwenye maamuzi ya mwisho ni hakimu au jaji mwenyewe, kwa hiyo ni muhimu kufahamu kuwa iko mamlaka ya Mungu mwenyewe inayoweza kuamua na kuhukumu hata kama jambo linaonekana kuwa sawa machoni pako mfano;

1.       Luka 10 38-42 “Ikawa katika kuenenda kwao aliingia katika kijiji kimoja; mwanamke mmoja jina lake Martha akamkaribisha nyumbani kwake.Naye alikuwa na umbu lake aitwaye Mariamu, aliyeketi miguuni pake Yesu, akasikiliza maneno yake.Lakini Martha alikuwa akihangaika kwa utumishi mwingi; akamwendea, akasema, Bwana, huoni vibaya hivyo ndugu yangu alivyoniacha nitumike peke yangu? Basi mwambie anisaidie.Bwana akajibu akamwambia, Martha, Martha, unasumbuka na kufadhaika kwa ajili ya vitu vingi; lakini kinatakiwa kitu kimoja tu; na Mariamu amelichagua fungu lililo jema, ambalo hataondolewa.”

Kwa mila na tamaduni za kimashariki wewe na mimi tunge muhukumu Mariamu kama binti mvivu na tungemkubali Martha kama mwanamke mchapakazi, lakini pale Martha alipoinua kinywa chake kumuhukumu Mariamu Bwana katika hukumu yake isiyotarajiwa anahukumu kuwa Martha ni changamoto kubwa sana na Mariamu ndiye yuko sahihi. Martha alikuwa na makosa makubwa sana kuliko Mariamu, Martha alikuwa akimfokea Yesu!  BWANA HUONI VIBAYA? Ndugu yangu alivyoniacha nitumike peke yangu?

Kumsikiliza Yesu ndio tukio la Heshima kubwa sana, na alikuwa akipokea Baraka kubwa za ushirika na Yesu, ambapo Martha kwa sababu ya kulalamika kwake alikuwa na msongo tu wa mawazo, haikuwa vibaya kuandaa kwaajili ya mgeni, lakini alijaa hukumu dhidi ya Yesu na Ndugu yake Mariamu, na kwa sababu hiyo alipoteza point katika hukumu kwa sababu ya manung’uniko

 

Wafilipi 2:14-15 “Yatendeni mambo yote pasipo manung'uniko wala mashindano,mpate kuwa wana wa Mungu wasio na lawama, wala udanganyifu, wasio na ila kati ya kizazi chenye ukaidi, kilichopotoka; ambao kati ya hao mnaonekana kuwa kama mianga katika ulimwengu,”

                 

Yesu hakumwambia Martha akae chini, kwani alikuwa anafanya jambo jema, na wala hakumwambia Mariamu inuka kwani naye alikuwa akifanya jambo jema, mmoja akimtumikia na mwingine akisikiliza,  wako wakristo na watumishi wa Mungu ambao hutumika sana, na wako ambao huomba sana na kutafakari wote wanaitenda kazi iliyo njema, kosa kubwa ni pale unapoanza kuwakosoa wengine na kufikiri kuwa wewe ndiye bora zaidi kwa sababu unafanya hicho unachikifanya, Jambo kubwa na la msingi na la muhimu ni uhusiano na Yesu Kristo, na Mariamu alikuwa ameligundua hilo, na hakuna mtu angeweza kumtenga na hilo, Mariamu kwa jicho la kibinadamu alionekana ni mvivu lakini kwa jicho la Yesu Mariamu alikuwa anampenda Yesu, alichukua muda kuwa na Yesu kwake Yesu alikuwa muhimu kuliko kupika, unalolifanya linaweza kuwa sio tatizo, lakini tatizo ni pale unapoanza kuamsha kinywa kwaajili ya wengine, Uhusiano wetu na Mungu ni jambo jema ambalo hakuna mtu anaweza kutuondolea. Mariamu alichagua fungu jema na hakuna wa kumuondolea, Ukichagua ushirika na Yesu hakuna mtu atakuondolea ushirika huo watakuondoa kwenye mengine lakini hakuna kitakachokutenga na Upendo wake Kristo.

 

2.       Marko 9:38-40 “Yohana akamjibu, akamwambia, Mwalimu, tulimwona mtu akitoa pepo kwa jina lako, ambaye hafuatani nasi; tukamkataza, kwa sababu hafuatani nasi. Yesu akasema, Msimkataze, kwa kuwa hakuna mtu atakayefanya mwujiza kwa jina langu akaweza mara kuninenea mabaya;kwa sababu asiye kinyume chetu, yu upande wetu.”

 

Hakuna mtu aliyekwenda kwa Yesu Kristo/Mungu akiwa anamshutumu mwingine na Yesu akakubaliana naye hata siku moja, kila wakati katika maisha ya Yesu alipoletewa kesi, Kesi hiyo iliwageukia walioleta, na hukumu kuwapata wao, katika tamaduni za kikanisa na madhehebu watu hujidhania kuwa wao ni wao na wao ndio wenye Yesu peke yao kama Yohana hapo, kwa hiyo walivyoona kuna anayetoa pepo kama wao lakini si wa dhehebu lao alitaka kuwazuia kuwanyima kibali, Lakini Yesu alikosoa vikali mtazamo wao.Wako watu wanaofikiri kuwa ni wao tu ndio wenye mamlaka au hatimiliki na Yesu, wao ndio bora, tabia ya aina hii inamuuzi sana Mungu, unaposhindana na kila mtu anayetumia jina la Yesu kwa kujifikiria kuwa wewe ndio wa muhimu na unapaswa kulitumia jina hilo unajiweka kwenye hatari ya kupingana na Yesu mwenyewe.

 

3.       Warumi 11:2-4 “Mungu hakuwasukumia mbali watu wake aliowajua tokea awali. Au hamjui yale yaliyonenwa na maandiko juu ya Eliya? Jinsi anavyowashitaki Waisraeli mbele za Mungu,Bwana, wamewaua manabii wako, wamezibomoa madhabahu zako, nami nimesalia peke yangu, nao wananitafuta roho yangu.Lakini ile jawabu ya Mungu yamwambiaje? Nimejisazia watu elfu saba wasiopiga goti mbele ya Baali.”

 

Eliya alikuwa nabii mkubwa sana wa Mungu, aliwahukumu waisrael kuwa wamewaua manabii wote wa Mungu na kuvunja madhabahu, zote za Bwana na kuabudu baali na kuwa ni yeye pakee amesalia (1Wafalme 19:10) Lakini Mungu alimjibu kuwa wako wengi ambao hawajapiga goti lao kwa baali, Mungu alikuwa anamthibitishia Eliya kuwa asijidhanie kuwa yuko pake yake Mungu ana watu wengi, hukumu ya Mungu wakati wote huthibitisha kuwa sisi ni wanadamu na hatuko sawa katika mitazamo yetu, Mungu ana jicho lake la kipekee katika kuyatazama mambo na hivyo tunapaswa kuwa wanyenyekevu sana na kuacha kuwashitaki watu wengine kwa Mungu.

 

4.       Katika mifano ya ufalme wa Mungu pia ambayo imebeba siri nyingi za Mungu utaweza kuona imejaa hekima na maarifa na uweza wa kiungu katika maamuzi ya namna ya kuhukumu, Yesu anafunua kuwa kuhukumu kwake kutakuwa mara zote kukiwaacha watu midomo wazi yatakuwa ni maamuzi ambayo yatawashangaza wengi kwa matokeo yake.

 

a.       Farisayo na mtoza ushuruLuka 18:9-14 “Akawaambia mfano huu watu waliojikinai ya kuwa wao ni wenye haki, wakiwadharau wengine wote. Watu wawili walipanda kwenda hekaluni kusali, mmoja Farisayo, wa pili mtoza ushuru. Yule Farisayo akasimama akiomba hivi moyoni mwake; Ee Mungu, nakushukuru kwa kuwa mimi si kama watu wengine, wanyang'anyi, wadhalimu, wazinzi, wala kama huyu mtoza ushuru.Mimi nafunga mara mbili kwa juma; hutoa zaka katika mapato yangu yote. Lakini yule mtoza ushuru alisimama mbali, wala hakuthubutu hata kuinua macho yake mbinguni, bali alijipiga-piga kifua akisema, Ee Mungu, uniwie radhi mimi mwenye dhambi.Nawaambia, huyu alishuka kwenda nyumbani kwake amehesabiwa haki kuliko yule; kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa.”

 

Katika mfano huu tunajifunza juu ya watu wawili waliopanda kwenda hekaluni kusali, mmoja alikuwa farisayo kwa hiyo ni wazi kuwa alikuwa myahudi wa madhehebu ya mafarisayo, alikuwa mcha Mungu na mtu aliyemwamini Mungu, pia alikuwa mtii kwa sheria (Torati) na aliielewa vema, na alikuwa mtu wa haki, hakutii tu sheria lakini alifanya zaidi ya sheria, kwa mujibu wa torati waisrael walitakiwa kufunga mara moja tu siku moja kwa mwaka (Siku ya upatanisho) lakini yeye alifunga mara mbili kila wiki  kwa hiyo alizidisha na kufanya zaidi ya sheria, Sheria ilimtaka mtu atoe fungu la kumi angalau ya sehemu Fulani tu ya mapato yake lakini yeye alitoa sehemu ya kumi ya kila aina ya kipato (mapato yangu yote) kwa hiyo hakuwa na dhambi, hakuwa myang’anyi, wala hakuwahi kudhulumu mtu, wala hakuwahi kuzini, kwa msingi huu basi kama ingelikuwa ni wewe na mimi farisayo huyu ni peponi moja kwa moja au tungekubaliana na sala yake na katika hukumu hatungemuhesabia kuwa hana shida yoyote Lakini hitimisho la Hakimu mkuu ni kuwa ajikwezaye atatushwa na ajishushae atakwezwa, Farisayo alikataliwa tatizo lilikuwa ni nini katika hukumu hii? Alijihesabia haki, alijidhania ya kuwa yeye ni mtakatifu, alijivuna, alipata kiburi cha kidini, hakufikiri kuwa naye anahitaji msamaha wa Mungu na rehema zake, alijifikiri ya kuwa anaweza kununua rehema za Mungu kwa matendo yake, alipiga vita wengine na kujiona ni mkamilifu kwa sababu ya matendo yake na kiburi, Katika macho ya Mungu alikataliwa Mungu huwapinga wenye kiburi na kuwapa neema wanyenyekevu, sio hivyo tu moyo wake ulijaa dharau dhidi ya watu wengine na alikuwa hana upendo, na zaidi ya yote alikalia kiti cha Mungu kwa kujifanya ndiye muhukumu,  

 

Mathayo 7:1-5 “Msihukumu, msije mkahukumiwa ninyi. Kwa kuwa hukumu ile mhukumuyo, ndiyo mtakayohukumiwa; na kipimo kile mpimiacho, ndicho mtakachopimiwa.Basi, mbona wakitazama kibanzi kilicho ndani ya jicho la ndugu yako, na boriti iliyo ndani ya jicho lako mwenyewe huiangalii? Au utamwambiaje nduguyo, Niache nikitoe kibanzi katika jicho lako; na kumbe! Mna boriti ndani ya jicho lako mwenyewe? Mnafiki wewe, itoe kwanza ile boriti katika jicho lako mwenyewe; ndipo utakapoona vema kukitoa kile kibanzi katika jicho la ndugu yako.”

 

Mathayo 23:23-24 “Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnalipa zaka za mnanaa na bizari na jira, lakini mmeacha mambo makuu ya sheria, yaani, adili, na rehema, na imani; hayo imewapasa kuyafanya, wala yale mengine msiyaache. Viongozi vipofu, wenye kuchuja mbu na kumeza ngamia.”

 

Farisayo alikataliwa katika hukumu, hii ndio hukumu ya kushangaza na isiyoweza kutabirika, tuna watu wengi sana wanaopanda kwenda kusali, tuna watu wengi sana wanafunga, sio wazinzi, ni wasafi lakini usafi huo ni wakwao wenyewe mioyoni mwao Mungu atawakataa, hukumu isiyotarajiwa itatufunulia mengi sana, tutaona mambo ya ajabu ya watu wote wanaojifikiria kuwa hawahitaji toba wamekamilika na wako safi lakini Yesu atawakataa hii itatushangaza ni hukumu isiyotarajiwa. Wote wenye juhudi ya kutenda mema na kudharau wengine kwa kujifikiri kuwa wao ni safi kuliko wengine, mahubiri yao yamejaa hukumu, maneno yao yamejaa kuhukumu wengine na kujifikiri kuwa wao wako sahihi na ni wasafi mno kumbe katika macho ya Mungu tunahitaji kuwa wanyenyekevu, na ni muhimu kwetu kukumbuka kuwa matendo mema sio kitu cha kushangaza kwa Mungu, tuliumbwa tukiwa wema, kwa hiyo unaweza kukuta mtu jhajamuamini Yesu na akawa ana matendo mema, Mungu anataka tuipokee zawadi ya wokobu kwa neema na kwa Imani na kutembea kwa neema na Imani, pasipo hiyo huwezi kumpendeza Mungu.

 

Waefeso 2:8-10 “Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu; wala si kwa matendo, mtu awaye yote asije akajisifu. Maana tu kazi yake, tuliumbwa katika Kristo Yesu, tutende matendo mema, ambayo tokea awali Mungu aliyatengeneza ili tuenende nayo.”    

 

b.      Wafanyakazi katika shamba za mizabibu – Mathayo 20:1-16 “Kwa maana ufalme wa mbinguni umefanana na mtu mwenye nyumba aliyetoka alfajiri kwenda kuajiri wakulima awapeleke katika shamba lake la mizabibu. Naye alipokwisha kupatana na wakulima kuwapa kutwa dinari, aliwapeleka katika shamba lake la mizabibu. Akatoka mnamo saa tatu, akaona wengine wamesimama sokoni wasiokuwa na kazi; na hao nao akawaambia, Enendeni nanyi katika shamba langu la mizabibu, na iliyo haki nitawapa. Wakaenda. Akatoka tena mnamo saa sita na saa kenda, akafanya vile vile. Hata kama saa kumi na moja akatoka, akakuta wengine wamesimama, akawaambia, Mbona mmesimama hapa mchana kutwa bila kazi?  Wakamwambia, Kwa sababu hakuna mtu aliyetuajiri. Akawaambia, enendeni nanyi katika shamba la mizabibu. Kulipokuchwa, yule bwana wa shamba akamwambia msimamizi wake, Waite wakulima, uwalipe ujira wao, ukianzia wa mwisho hata wa kwanza. Na walipokuja wale wa saa kumi na moja, walipokea kila mtu dinari. Na wale wa kwanza walipokuja, walidhani kwamba watapokea zaidi; na hao pia wakapokea kila mtu dinari. Basi wakiisha kuipokea, wakamnung'unikia mwenye nyumba, wakisema, Hao wa mwisho wametenda kazi saa moja tu, nawe umewasawazisha na sisi tuliostahimili taabu na hari za mchana kutwa.Naye akamjibu mmoja wao, akamwambia, Rafiki, sikudhulumu; hukupatana nami kwa dinari? Chukua iliyo yako, uende zako; napenda kumpa huyu wa mwisho sawa na wewe.Si halali yangu kutumia vilivyo vyangu kama nipendavyo? Au jicho lako limekuwa ovu kwa sababu ya mimi kuwa mwema? Vivyo hivyo wa mwisho watakuwa wa kwanza, na wa kwanza watakuwa wa mwisho

 

Kuna mengi ya kujifunza pia kuhusu hukumu ya Mungu katika mfano huu, sitaki kueleza kila kitu kilichomo katika mfano huu lakini mfano huu unazungumzia mwenye nyumba, Biblia ya kiingereza inatumia neno landowner yaani mwenye shamba ambaye alikuwa amekusudia kazi yake iishe, alitoka kutafuta wafanya kazi, kwaajili ya shamba lile, siku zile malipo ya siku nzima yalikuwa ni dinari, mwenye shamba aliajiri yeye mwenyewe aliajiri watu wa saa 12 alfajiri, kisha saa 6 kisha Saa 9 na kisha saa 11,  na alipatana nao kuwalipa (zingatia malipo kwa siku ni Dinari) au unaweza kuweka Elfu kumi kwa siku, kwa kazi ya masaa 12.  Hawa wengine waliajiriwa tu kwa mapenzi ya mwenye shamba na aliwaahidi atawapa haki yao, ilipofika jioni aliamuru wote walipwe akianza na wale wa saa 11 ambao kimsingi walifanya kazi saa moja tu. Hii ni kwa sababu mwenye shamba ni mkarimu, lakini walipolipwa wale walioajiriwa wa saa 12 alfajiri walilalamika na kulaumu kuwa mwenye shamba hakuwa ametenda haki kwa sababu wako watu wamefanya kazi saa moja tu na amewalipa sawa na wao waliofanya kazi tangu asubuhi, Kwa hiyo walimuhukumu mwenye shamba kwa kuwa mkarimu na mwema. Hii inatufundisha nini? Mungu anauwezo wa kuamua na lolote atakaloliamua sawa na ukarimu wake huna haki ya kulalamika kwa sababu hajakudhulumu yeye huweza kuamua kumrehemu yeyote yule na hatupaswi kuwa na wivu?

 

Warumi 9:18-21 “Basi, kama ni hivyo, atakaye kumrehemu humrehemu, na atakaye kumfanya mgumu humfanya mgumu. Basi, utaniambia, Mbona angali akilaumu? Kwa maana ni nani ashindanaye na kusudi lake?La! Sivyo, Ee binadamu; wewe u nani umjibuye Mungu? Je! Kitu kilichoumbwa kimwambie yeye aliyekiumba, Kwani kuniumba hivi? Au mfinyanzi je! Hana amri juu ya udongo, kwa fungu moja la udongo kuumba chombo kimoja kiwe cha heshima, na kimoja kiwe hakina heshima?

 

Waefeso 2:8-9 “Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu; wala si kwa matendo, mtu awaye yote asije akajisifu.”

 

Dinari inazungumzia wokovu, ambapo Mungu anaweza kumuokoa mtu wakati wowote na thawabu ikawa moja kama alivyomuokoa mwizi pale msalabani, lakini wale waliokuweko kazini wali lalamika mbona unatulipa sawa?  Mara kadhaa tumekasirika na kuona wivu pale Mungu anapombariki mwingine, na kumuinua kuliko sisi kwa mapenzi yake tunalalamika kwa sababu ya wivu, tunalalama na kumuona Mungu kama hayuko sawa vile ni kama anapendelea wakati tunapojilinganisha na wengine na wakati mwingine tumewapiga vita watu kwa sababu ya wivu wetu, tunafanya ujinga na Mungu anazo sababu za kutuhukumu kwa kuhukumu wema wake na ukarimu wake, wokovu ni kwa neema tu na kamwe hatuwezi kuutendea kazi, wale wanaofikiri kuwa kwa kazi zao watapata kibali kikubwa kwa Mungu wanajidanganya mfano huu unafunua vilevile hukumu isiyotarajiwa ya Mungu.

 

c.       Mfano wa yule kaka mkubwaLuka 15:11-32 “Akasema, Mtu mmoja alikuwa na wana wawili; yule mdogo akamwambia babaye, Baba, nipe sehemu ya mali inayoniangukia. Akawagawia vitu vyake. Hata baada ya siku si nyingi, yule mdogo akakusanya vyote, akasafiri kwenda nchi ya mbali; akatapanya mali zake huko kwa maisha ya uasherati. Alipokuwa amekwisha tumia vyote, njaa kuu iliingia nchi ile, yeye naye akaanza kuhitaji. Akaenda akashikamana na mwenyeji mmoja wa nchi ile; naye alimpeleka shambani kwake kulisha nguruwe. Akawa akitamani kujishibisha kwa maganda waliyokula nguruwe, wala hapana mtu aliyempa kitu. Alipozingatia moyoni mwake, alisema, Ni watumishi wangapi wa baba yangu wanaokula chakula na kusaza, na mimi hapa ninakufa kwa njaa. Nitaondoka, nitakwenda kwa baba yangu na kumwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako; sistahili kuitwa mwana wako tena; nifanye kama mmoja wa watumishi wako. Akaondoka, akaenda kwa babaye. Alipokuwa angali mbali, baba yake alimwona, akamwonea huruma, akaenda mbio akamwangukia shingoni, akambusu sana.Yule mwana akamwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako; sistahili kuitwa mwana wako tena. Lakini baba aliwaambia watumwa wake, Lileteni upesi vazi lililo bora, mkamvike; mtieni na pete kidoleni, na viatu miguuni; mleteni ndama yule aliyenona mkamchinje; nasi tule na kufurahi; kwa kuwa huyu mwanangu alikuwa amekufa, naye amefufuka; alikuwa amepotea, naye ameonekana. Wakaanza kushangilia. Basi, yule mwanawe mkubwa alikuwako shamba na alipokuwa akija na kuikaribia nyumba, alisikia sauti ya nyimbo na machezo. Akaita mtumishi mmoja, akamwuliza, Mambo haya, maana yake nini? Akamwambia, Ndugu yako amekuja, na baba yako amemchinja ndama aliyenona, kwa sababu amempata tena, yu mzima. Akakasirika, akakataa kuingia ndani. Basi babaye alitoka nje, akamsihi. Akamjibu baba yake, akasema, Tazama, mimi nimekutumikia miaka mingapi hii, wala sijakosa amri yako wakati wo wote, lakini hujanipa mimi mwana-mbuzi, nifanye furaha na rafiki zangu;lakini, alipokuja huyu mwana wako aliyekula vitu vyako pamoja na makahaba, umemchinjia yeye ndama aliyenona. Akamwambia, Mwanangu, wewe u pamoja nami sikuzote, na vyote nilivyo navyo ni vyako.Tena, kufanya furaha na shangwe ilipasa, kwa kuwa huyu ndugu yako alikuwa amekufa, naye amefufuka; alikuwa amepotea, naye ameonekana.”

 

Nauita mfano wa kaka mkubwa kwa sababu katika mtazamo wa Mungu ndiye aliyekuwa na matatizo makubwa zaidi ya Mwana mpotevu, Baba wa mwana mpotevu alikuwa anasikitika kumpoteza kijana wake na aliporejea nyumbani alilia akamkumbatia na kumvika mavazi mazuri kisha akamfanyia sherehe kubwa, Kaka mkubwa alikasirika, akasusa na kugoma kuingia ndani, akamuhukumu baba yake na mdogo wake, alimshutumu kuwa mdogo wake huyo ametapanya mali pamoja na makahaba, na baba yake ameonyesha ukirimu jambo ambalo hajawahi kulifanya kwa kaka mkubwa, kwa hiyo alijawa na hasira, na wivu na kulaumu ukarimu wa baba yake mfano huu kama mingine iliyotangulia unatahadharisha kuwa Mungu atakapohukumu wanadamu atafanya mapinduzi ambayo wale wanaojifikiria kuwa ni wenye haki watalia na kushangaa, wale wanaojifikiria kuwa hawajawahi kumkosea Mungu kwa lolote, basi wanaweza kumkosea Mungu kwa kuhukumu wengine, au kwa kumlaumu Mungu au maamuzi ya Mungu ya kikarimu, iko mifano Mingi ambayo muda usingeliweza kutosha kuichanganua lakini unaanza kuelewa

Kwaajili ya Hukumu hizi za kushangaza za Mungu, na tabia zake ni muhimu sana kuwa wanyenyekevu na kuogopa sana hukumu ya Mungu, hakuna kitu kinatisha kama hukumu ya Mungu, wakati wote kujifikiri kuwa sisi ndio tuko sawa na wenzetu hawako sawa, kunakuweka katika hatari ya kuingia katika hukumu isiyoepukika na hukumu za kushangaza kwaajili ya aina hii ya mtazamo ni lazima tukubali na kuelewa ya kuwa hata siku ya mwisho siku ya hukumu Mungu akisema nimekusudia kuwarehemu watu wote na watu wote nataka waingie peponi au katika ufalme wake je wewe na Mimi tutakubaliana na hukumu hiyo? Tutaona kuwa Mungu amehukumu kwa haki? au tutadhani kuwa Mungu ana upendeleo acha kujifikiri kuwa wewe ni bora zaidi kuliko wengine, acha kukomalia makosa ya wengine Mungu nadhani anataka tushughulike na maisha yetu zaidi kuliko ya wengine.

Mathayo 7:3-5 “Basi, mbona wakitazama kibanzi kilicho ndani ya jicho la ndugu yako, na boriti iliyo ndani ya jicho lako mwenyewe huiangalii? Au utamwambiaje nduguyo, Niache nikitoe kibanzi katika jicho lako; na kumbe! Mna boriti ndani ya jicho lako mwenyewe? Mnafiki wewe, itoe kwanza ile boriti katika jicho lako mwenyewe; ndipo utakapoona vema kukitoa kile kibanzi katika jicho la ndugu yako.”

Je utaweza kuiepuka hukumu ya Mungu? Ni hukumu isiyoepukika inatutaka tuwe wanyenyekevu sana sisi kama wanadamu hatuna cha kujivuna katika jambo lolote lile, wakati wote tuombe rehema na neema ya Mungu na kuendelea kumtafuta bwana kwa mioyo yetu yote, na zaidi ya yote turuhusu wakati wote neno la Mungu lituhukumu na kutubu pale linaposhughulika na maovu yetu, Mungu atatubariki na kwa neema yake atatufunulia kweli yetu yote Bwana yu karibu na moyo uliopondeka tutembee kwa unyenyekevu na kujishusha mbele za Mungu aliye hai.

Na Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye hekima

Tafadhali naomba maoni yako 0718990796

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni