Jumamosi, 21 Septemba 2024

Kwa nini hatuwezi kunyamaza!


Isaya 62:1-3 “Kwa ajili ya Sayuni sitanyamaza, na kwa ajili ya Yerusalemu sitatulia, hata haki yake itakapotokea kama mwangaza, na wokovu wake kama taa iwakayo. Na mataifa wataiona haki yako, na wafalme wote watauona utukufu wako; nawe utaitwa jina jipya, litakalotajwa na kinywa cha Bwana. Nawe utakuwa taji ya uzuri katika mkono wa Bwana, na kilemba cha kifalme mkononi mwa Mungu wako.”




Utangulizi:

Miaka mingi nyuma Muhubiri na mtumishi wa Mungu Bill Bright aliwahi kuhubiri ujumbe unaofanana na wa kwangu ambao aliuita “Why we cannot remain Silence” kwa tafasiri isiyo rasimi “kwanini hatuwezi kukaa kimya” ujumbe huo umehifadhiwa katika kitabu kiitwacho 50 Great sermon, Yeye alikuwa akizungumzia kuhusu umuhimu wa kuihubiri injili kutokana na Agizo kuu la Bwana wetu Yesu Kristo kwa kanisa na Dr Martin Luther king Jr aliyekuwa mtumishi wa Mungu na mpigania haki za weusi wakati wa ubaguzi  wa rangi kule Marekani aliwahi kusema “Our lives begin to end the day we become silent” pia kwa tafasiri isiyo rasmi ni kama anasema “Maisha yetu huanza kuisha siku tutakapokaa kimya” wote hawa walihubiri na kusema hayo katika mukhtadha tofauti na maandiko tofauti, Bill akizungumzia umuhimu wa agizo kuu hatuwezi kukaa kimya bila kuieneza injili, na Martin akizungumzia kutokuacha kukemea matendo ya  ubaguzi, Hatuwezi kukaa kimya bila kukemea matendo yasiyo ya haki ya kibaguzi,  Leo na mimi nakuja na ujumbe huu kwanini hatuwezi kunyamaza katika mlengo mwingine hasa nikitaka kusisitiza jinsi Roho Mtakatifu anavyofanya kazi ndani yetu ya kutufanya tutimize wajibu, alioweka ndani yetu; kwa hiyo mimi nazungumzia ni nani anayesababisha tusikae kimya, Roho Mtakatifu ambaye amemuita kila mmoja wetu kwa kazi zake maalumu pia anaweka ndani yetu Mzigo “burden” ambao anataka kila mmoja wetu aweze kuutimiza katika maisha yetu hapa Duniani na kwaajili ya hayo utaweza kuona ni vigumu kwetu kuwa na utulivu, bila kutimiza kile ambacho Mungu amekikusudia ndani yetu tutajifunza somo hili kwanini hatuwezi kunyamaza kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-


·         Maana ya kunyamaza.

·         Kwanini hatuwezi kunyamaza.

·         Mifano ya kibiblia ya watu walioshindwa kunyamaza.


Maana ya kunyamaza.

Ni muhimu kufahamu kuwa neno kunyamaza halina misamiati mingi katika lugha ya Kiebrania na kiyunani inayoweza kutosheleza kuelezea, Neno kunyamaza au kutulia au kukaa kimya katika kingereza ni neno “Quiet”, ambalo tafasiri yake ni without noise, absence of noise yaani paipo kelele, au bila ya kelele, Lakini  katika lugha ya kiebrania neno linalotumika kuelezea ukimya au utulivu ni neno tām – kwa kiingereza “Gentle” ambalo maana yake ni kutokuchukua hatua, yaani kwa mfano mtu anaweza kutenda kosa ambalo kiimani au kimila ni kosa kubwa sana ambalo linahitaji uchukue hatua kali lakini badala yake unatulia bila kuchukua hatua zozote wala kukemea wala kukosoa wala kusema, au mtu anaweza akawa anakusingizia au kusema maneno ya uzushi na uongo kukuhusu, au akijifanya anathibitisha kuwa wewe una kosa hili au lile kisha wewe hujibu kitu chochote huko kunaitwa kunyamaza  tām kwa kiebrania, kunyamaza kwingineko ni kupuuzia na kut4okuchangia lolote kwa kiyunani linatumika neno “Siōpaō” ambalo maana yake  kwa kiingereza ni “muteness”,  na neno lingine ni neno la Kiibrania “shākat” ambalo maana yake be “undisturbed” yaani kutokuwa na shughuli na mtu, kutokujisumbua na maswala ya watu kuachia kile kitu kiende kama kilivyo; huko ndio kunyamaza kunakotajwa katika maandiko.  Mfano:-

Mwanzo 34:1-7 “Basi Dina, binti Lea, ambaye Lea alimzalia Yakobo, akatoka kuwaona binti za nchi. Shekemu, mwana wa Hamori, Mhivi, mkuu wa nchi, akamwona akamtwaa, akalala naye, akambikiri.Moyo wake ukaambatana na Dina binti Yakobo, akampenda huyu msichana, akasema na huyu msichana kwa maneno mazuri. Shekemu akamwambia Hamori, babaye, akasema, Unipatie msichana huyu awe mke wangu. Basi Yakobo akasikia ya kwamba amembikiri Dina, binti yake. Na wanawe walikuwako pamoja na wanyama wake nyikani. YAKOBO AKANYAMAZA, hata walipokuja. Akatoka Hamori, babaye Shekemu, kumwendea Yakobo, aseme naye.Wanawe Yakobo waliposikia hayo, wakaja kutoka nyikani; nao wakasikitika sana, wakakasirika mno, kwa sababu amefanya upumbavu katika Israeli kwa kulala na binti Yakobo, neno lisilojuzu kutendeka.”

Mwanzo 35:21-22Kisha akasafiri Israeli akapiga hema yake upande wa pili wa mnara wa Ederi. Ikawa Israeli alipokuwa akikaa katika nchi ile, Reubeni akaenda akalala na Bilha, suria wa babaye; ISRAELI AKASIKIA HABARI. Basi hao wana wa Yakobo walikuwa kumi na wawili.”

Mwanzo 25:23-27 “BWANA akamwambia, Mataifa mawili yamo tumboni mwako, Na kabila mbili za watu watafarakana tangu tumboni mwako. Kabila moja litakuwa hodari kuliko la pili, Na mkubwa atamtumikia mdogo. Siku zake za kuzaa zilipotimia, tazama! Mapacha walikuwamo tumboni mwake. Wa kwanza akatoka, naye alikuwa mwekundu mwili wote kama vazi la nywele. Wakamwita jina lake Esau. Baadaye ndugu yake akatoka, na mkono wake unamshika Esau kisigino. Akaitwa jina lake Yakobo. Isaka alikuwa mwenye miaka sitini mkewe alipowazaa. Watoto wakakua, Esau alikuwa mtu ajuaye kuwinda wanyama, mtu wa nyikani, na YAKOBO ALIKUWA MTU MTULIVU, mwenye kukaa hemani.”

Mathayo 26:59-63 “Basi wakuu wa makuhani na baraza yote wakatafuta ushuhuda wa uongo juu ya Yesu, wapate kumwua;wasiuone wangawa walitokea mashahidi wa uongo wengi. Hata baadaye wawili wakatokea, wakasema, Huyu alisema, Naweza kulivunja hekalu la Mungu, na kulijenga kwa siku tatu. Kisha Kuhani Mkuu akasimama akamwambia, Hujibu neno? Hawa wanakushuhudia nini? Lakini, YESU AKANYAMAZA. Kuhani Mkuu akamwambia, Nakuapisha kwa Mungu aliye hai, utuambie kama wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu.”

Marko 14:55-61 “Basi wakuu wa makuhani na baraza yote wakatafuta ushuhuda juu ya Yesu wapate kumwua; wasione. Kwa maana wengi walimshuhudia uongo, walakini ushuhuda wao haukupatana. Hata wengine wakasimama, wakamshuhudia uongo, wakisema, Sisi tulimsikia akisema, Mimi nitalivunja hekalu hili lililofanyika kwa mikono, na katika siku tatu nitajenga jingine lisilofanyika kwa mikono. Wala hata hivi ushuhuda wao haukupatana. Kisha Kuhani Mkuu akasimama katikati, akamwuliza Yesu, akisema, Hujibu neno? Hawa wanakushuhudia nini? LAKINI AKANYAMAZA, WALA HAKUJIBU NENO. Kuhani Mkuu akamwuliza tena, akamwambia, Wewe ndiwe Kristo, Mwana wake Mtukufu?

Waamuzi 18:7 “Ndipo hao watu watano wakaenda zao, wakafika Laisha, wakawaona wale watu waliokuwamo ndani yake, jinsi walivyokaa salama salimini kwa mfano wa walivyokaa hao Wasidoni, wenye starehe na hifadhi, kwa maana hapakuwa na mtu katika nchi hiyo aliyekuwa na amri, aliyeweza kuwatweza katika neno lo lote, nao walikuwa wa mbali na hao Wasidoni, wala hawakuwa na shughuli na mtu ye yote.”                                

Katika vifungu vya maandiko hapo juu tunaona sasa matumizi na neno kunyamaza. Linavyotumika kwa Yakobo linatumika neno “tām” gentle hii inamaanisha kuwa Yakobo au Israel alikuwa ni mkimya au mtulivu kwa kuzaliwa kwa hiyo kukaa kimya ilikuwa ni tabia yake ambayo kimsingi watoto wake Simoni na Lawi hawakuwahi kukubaliana nayo, waliona ni ukimya unaopelekea hata kuonewa. Binti yake alipobakwa Yakobo alikaa kimya, nahata Reuben alipolala na suria wa baba yake Yakobo alisikia lakini alikaa kimya, kwa hiyo ni wazi kuwa alikuwa ni mtulivu mno upole uliokithiri, utulivu uliopittiliza, alikaa kimya.

Na kwa Bwana Yesu ukimya wake wakati akiwa anashitakiwa mashitaka ya uongo mbele ya mahakama ya kiyahudi yeye alinyamaza “Siōpaō” muteness Ukimya huu ni ukimya wa kupuuzia, au kuamua kupuuzia na kutokutilia maanani maswala ya kipuuzi. Usipoteze muda wako kujibu lolote unalozushiwa ambalo ni la uongo, Yesu watu walipomsingizia na kusema uongo hakujibu lolote alitulia kimya

Na ukimya unaozungumzwa katika andiko kutoka katika kitabu cha waamuzi linazunguiza utulivu wa kukaa kwa amani au bila kusumbuana na maswala ya watu “shākat” yaani “undisturbed” husumbuliwi wala husumbui, hushughuliki na jambo lolote la mtu wala wao hawashughuliki na wewe kwa hiyo unakaa salama kimyaa

Na neno lingine linalotumika katika maandiko ambalo kisingi ndilo tutakalolitumia leo ni neno la kiibrania “Chshh” ambalo maana yake to keep quiet, to hold peace, au to keep silence   Hili ndio linalotumiwa na Roho Mtakatifu kutokumfanya mtu atulie au awe na Amani au anyamaze wakati kuna mzigo ambao Mungu ameuweka ndani yake

Isaya 62:1-3 “Kwa ajili ya Sayuni sitanyamaza, na kwa ajili ya Yerusalemu sitatulia, hata haki yake itakapotokea kama mwangaza, na wokovu wake kama taa iwakayo. Na mataifa wataiona haki yako, na wafalme wote watauona utukufu wako; nawe utaitwa jina jipya, litakalotajwa na kinywa cha Bwana. Nawe utakuwa taji ya uzuri katika mkono wa Bwana, na kilemba cha kifalme mkononi mwa Mungu wako.”


Kwa nini hatuwezi kunyamaza

Roho Mtakatifu anapokuwa ndani yetu, moja ya kazi anayoifanya ni kukutaharakisha, kukupeleka katika kutimiza majukumu ambayo Mungu ameyakusudia na kuyaweka ndani yako, kwa hiyo yeye hukufanya wewe na mimi tusiweze kukaa kimya, Ni kazi ya Roho Mtakatifu kuwatia nguvu waamini na kuwasukuma moyoni kwa kuwanyima Amani, kwa kuwakoseha utulivu, kwa kuwahimiza na kutowafanya wanyamaze mpaka wametimiza kile ambacho Mungu amekikusudia kwa mtu huyo aweze kukitimiza, kwa hiyo Roho wa Mungu anafanyika “Catalyst” kichocheo  ambaye anainua mioyo yetu na kuweka mzigo na moyo na kutuwezesha kusema kile ambacho Mungu amekikusudia ili kitende kazi ndani yetu mfano kama Mungu anaweka neno ndani yetu basi, Roho Mtakatifu anachochea lile neno ambalo Mungu amelikusudia, tuliseme ili tuweze kulisema na inapotokea utaamua kukaa kimya kunatokea changamoto ndani yako zinazokunyima Amani itakayokupelekea ukaseme kila ambacho Mungu amekikusudia ni kwaajili ya Roho Mtakatifu kuweka kitu ndani yako au ndani yangu ndio tunakosa utulivu au uwezo wa kunyamaza “Chshh” kwanini hatuwezi kunyamaza? Ni kwa sababu Roho Mtakatifu haachi kufanya uchochezi ndani yetu!

Yeremia 1:6-8 “Ndipo niliposema, Aa, Bwana MUNGU! Tazama, siwezi kusema; maana mimi ni mtoto. Lakini Bwana akaniambia, Usiseme, Mimi ni mtoto; maana utakwenda kwa kila mtu nitakayekutuma kwake, nawe utasema kila neno nitakalokuamuru. Usiogope kwa sababu ya hao maana mimi nipo pamoja nawe nikuokoe, asema Bwana.”

Ezekiel 33:7-9 “Basi wewe, mwanadamu, nimekuweka kuwa mlinzi kwa nyumba ya Israeli; basi ulisikie neno hili kinywani mwangu, ukawape maonyo yangu. Nimwambiapo mtu mbaya, Ewe mtu mbaya, hakika utakufa, nawe husemi neno la kumwonya mtu huyo, aiache njia yake, mtu mbaya huyo atakufa katika uovu wake, lakini damu yake nitaitaka mkononi mwako. Walakini ukimwonya mtu mbaya kwa sababu ya njia yake, kusudi aiache; wala yeye asiiache; atakufa huyo katika uovu wake, lakini wewe umejiokoa roho yako.”

Kwa hiyo kumbe Mungu anapoweka neno lake au wajibu wake kwa mtumishi Fulani wa Mungu, Roho Mtakatifu huchochea na kumfanya mtu huyo kukosa utulivu mpaka atakapotimiza kile ambacho Mungu amekiweka, matukio ya aina hii yanaweza kuwekwa kwa waombaji, yanaweza kuwekwa kwa wajumbe wa kinabii ambao Mungu anataka wapeleke maonyo na kutia moyo, wajumbe wa kiinjilisti ambao Mungu anawataka waseme habari njema, wajumbe wa kialimu ambao Mungu anawataka wafundishe, wajumbe wa kiandishi ambao Mungu anawataka waandike “haya uyaonayo uyaandike!” , Wajumbe wa kichungaji ambao Mungu anaweka mzigo ndani yao wachunge na kulisha kundi la kondoo wa Bwana, wajumbe wa kitume ambao watapanda makanisa na kuipeleka injili kule Mungu anakotaka, Wajumbe wa kitaaluma ambao Mungu anataka wawake na kupanda taaluma katika jamii, wakati wote Mungu Roho Mtakatifu atawataharakisha watu wake wasikae kimya kwaajili ya kazi zote katika ufalme wa Mungu, yeye huhimiza na kutoa maelekezo kwa kila muhusika kwaajili ya kazi husika ambayo yeye anataka itimizwe

Ezra 5:1-2 “Basi manabii, Hagai nabii, na Zekaria mwana wa Ido, wakawafanyia unabii Wayahudi waliokuwako Yerusalemu na Yuda; waliwafanyia unabii kwa jina la Mungu wa Israeli. Ndipo akaondoka Zerubabeli, mwana wa Shealtieli, na Yoshua, mwana wa Yosadaki, wakaanza kuijenga nyumba ya Mungu iliyoko Yerusalemu; na pamoja nao walikuwa manabii wa Mungu, wakiwasaidia.”

Matendo 8:26-29 “Malaika wa Bwana akasema na Filipo, akamwambia, Ondoka ukaende upande wa kusini hata njia ile itelemkayo kutoka Yerusalemu kwenda Gaza; nayo ni jangwa. Naye akaondoka, akaenda; mara akamwona mtu wa Kushi, towashi, mwenye mamlaka chini ya Kandake malkia wa Kushi, aliyewekwa juu ya hazina yake yote; naye alikuwa amekwenda Yerusalemu kuabudu, akawa akirejea, ameketi garini mwake akisoma chuo cha nabii Isaya. Roho akamwambia Filipo, Sogea karibu na gari hili, ukashikamane nalo.”

Luka 2:25-35 “Na tazama, pale Yerusalemu palikuwa na mtu, jina lake Simeoni, naye ni mtu mwenye haki, mcha Mungu, akiitarajia faraja ya Israeli; na Roho Mtakatifu alikuwa juu yake.Naye alikuwa ameonywa na Roho Mtakatifu ya kwamba hataona mauti kabla ya kumwona Kristo wa Bwana. Basi akaja hekaluni ameongozwa na Roho; na wale wazazi walipomleta mtoto Yesu ndani, ili wamfanyie kama ilivyokuwa desturi ya sheria, yeye mwenyewe alimpokea mikononi mwake, akamshukuru Mungu, akisema,Sasa, Bwana, wamruhusu mtumishi wako, Kwa amani, kama ulivyosema; Kwa kuwa macho yangu yameuona wokovu wako,Uliouweka tayari machoni pa watu wote; Nuru ya kuwa mwangaza wa Mataifa, Na kuwa utukufu wa watu wako Israeli. Na babaye na mamaye walikuwa wakiyastaajabia hayo yaliyonenwa juu yake. Simeoni akawabariki, akamwambia Mariamu mama yake, Tazama, huyu amewekwa kwa kuanguka na kuinuka wengi walio katika Israeli, na kuwa ishara itakayonenewa. Nawe mwenyewe, upanga utaingia moyoni mwako, ili yafunuliwe mawazo ya mioyo mingi   

2Petro 1:20-21 “Mkijua neno hili kwanza, ya kwamba hakuna unabii katika maandiko upatao kufasiriwa kama apendavyo mtu fulani tu. Maana unabii haukuletwa po pote kwa mapenzi ya mwanadamu; bali wanadamu walinena yaliyotoka kwa Mungu, wakiongozwa na Roho Mtakatifu.”                       

Wakati wote Roho Mtakatifu aliwapa uchochezi manabii, mitume na watumishi mbalimbali wa Mungu kuweza kutoa ujumbe, kutabiri na kutia moyo au kuongoza katika haki ili mapenzi ya Mungu yaweze kufahamika na kutendeka katika jamii ya watu ambao Mungu aliwakusudia, Mungu Roho Mtakatifu anapokuwa amekusudia hilo na wewe ndie ambaye umekusudiwa upeleke ujumbe huo basi yeye hatakuacha unyamaze atakusukuma kwa jambo hilo, utaona moto ndani yako, utaona msukumo, utaona kukosa Amani, utaona kusumbuliwa utasikia kushikwa, kukamatwa, kupelekwa kutaharakishwa kuuzishwa mpaka umetenda kile ambacho kimekusudiwa naye


Mifano ya kibiblia ya watu walioshindwa kunyamaza.

Waamuzi 13:24-25 “Basi yule mwanamke akamzaa mtoto mwanamume akamwita jina lake Samsoni, mtoto huyu akakua, Bwana akambarikia. Roho ya Bwana ikaanza kumtaharakisha katika Mahane-dani, katikati ya Sora na Eshtaoli.”

Wote tunafahamu kuwa Samsoni alizaliwa kwa kusudi maalumu, na Mungu alikuwa amemuandaa kuwa mwokozi wa wana wa Israel ambao walikuwa wanaonewa na Wafilisti kwa wakati huo, tunasoma tu kuwa mara baada ya mtoto huyu kukua Roho ya Bwana ikaanza kumtaharakisha maana yake ikamnyima kutulia, ikamnyima kunyamaza Roho Mtakatifu alianza kuweka msukumo na kumfanya ajione hawezi kutulia ni lazima aseme alijiona hawezi kuwa utumwani yeye wala ndugu zake alijisikia kuwa ni lazima afanye kazi yake aliyopewa ya kuwaokoa wana wa Israel kama Jeshi la Mtu mmoja na alikuwa na hisia zilizokuwa zikimuelekeza au kumyima Amani mpaka atafute kisa ili mradi aweze kuwaokoa wana wa Israel, kwa hiyo tunajifunza hapa kuwa Mungu akikupa agizo huwezi kutulia kunakuwepo moto unaokutesa na kukusumbua ukikutaka utimize kusudi ambalo kwa sababu ya hilo ulizaliwa.       

Isaya 58:1-14 “Piga kelele, usiache, Paza sauti yako kama tarumbeta; Uwahubiri watu wangu kosa lao, Na nyumba ya Yakobo dhambi zao. Walakini wanitafuta kila siku; hupenda kujua njia zangu; kama vile taifa waliotenda haki, wasioacha sheria ya Mungu wao, hutaka kwangu amri za haki; hufurahi kumkaribia Mungu. Husema, Mbona tumefunga, lakini huoni? Mbona tumejitaabisha nafsi zetu, lakini huangalii? Fahamuni, siku ya kufunga kwenu mnatafuta anasa zenu wenyewe, na kuwalemea wote watendao kazi kwenu.

Tazama, ninyi mwafunga mpate kushindana na kugombana, na kupiga kwa ngumi ya uovu. Hamfungi siku hii ya leo hata kuisikizisha sauti yenu juu.  Je! Kufunga namna hii ni saumu niliyoichagua mimi? Je! Ni siku ya mtu kujitaabisha nafsi yake? Ni kuinama kichwa kama unyasi, na kutanda nguo za magunia na majivu chini yake? Je! Utasema ni siku ya kufunga, na ya kukubaliwa na Bwana?  Je! Saumu niliyoichagua, siyo ya namna hii? Kufungua vifungo vya uovu, kuzilegeza kamba za nira, kuwaacha huru walioonewa, na kwamba mvunje kila nira?  Je! Siyo kuwagawia wenye njaa chakula chako, na kuwaleta maskini waliotupwa nje nyumbani kwako? Umwonapo mtu aliye uchi, umvike nguo; wala usijifiche na mtu mwenye damu moja nawe? Ndipo nuru yako itakapopambazuka kama asubuhi, na afya yako itatokea mara; na haki yako itakutangulia; utukufu wa Bwana utakufuata nyuma ukulinde. Ndipo utaita, na Bwana ataitika; utalia, naye atasema, Mimi hapa. Kama ukiiondoa nira; isiwepo kati yako, wala kunyosha kidole, wala kunena maovu; na kama ukimkunjulia mtu mwenye njaa nafsi yako, na kuishibisha nafsi iliyoteswa; ndipo nuru yako itakapopambazuka gizani; na kiwi chako kitakuwa kama adhuhuri. Naye Bwana atakuongoza daima, ataishibisha nafsi yako mahali pasipokuwa na maji, na kuitia nguvu mifupa yako; nawe utakuwa kama bustani iliyotiwa maji, na kama chemchemi ambayo maji yake hayapungui.

Na watu wako watapajenga mahali palipokuwa ukiwa; utaiinua misingi ya vizazi vingi; nawe utaitwa, Mwenye kutengeneza mahali palipobomoka; na, Mwenye kurejeza njia za kukalia. Kama ukigeuza mguu wako usihalifu sabato, usifanye anasa yako siku ya utakatifu wangu; ukiita sabato siku ya furaha, na siku takatifu ya Bwana yenye heshima; ukiitukuza, kwa kutokuzifanya njia zako mwenyewe, wala kuyatafuta yakupendezayo, wala kusema maneno yako mwenyewe; ndipo utakapojifurahisha katika Bwana; nami nitakupandisha mahali pa nchi palipoinuka; nitakulisha urithi wa Yakobo baba yako; kwa maana kinywa cha Bwana kimenena hayo.”               

Nabii Isaya aliitwa na Mungu na Mungu alimtaka awaonye wana wa Israel na kuwaeleza kosa lao ili yamkini waweze kutubu, ujumbe wa makemeo wakati mwingine sio ujumbe mwepesi, kama mwanadamu wakati mwingine alisita na au aliingia hofu  na labda alitaka kuacha lakini Roho wa Mungu alimwambia piga kelele wala usiache paza sauti yako kama tarumbeta kwa nguvu onya juu ya unafiki, wa watu wa Mungu, wakati mwingine ni ngumu kuhubiri maneno magumu watu wanaweza kusema ya kuwa unawahukumu na hasa na wewe ukijijua kuwa u mwanadamu hivyo ilikuwa ni sahihi kwa Isaya kusita sita Lakini aliambiwa apige kelele kama tarumbeta awaonye watu, alipaswa kuwa muaminifu kuhubiri ujumbe wote wa Mungu kama ni toba anyooshe, kama ni rehema anyoooshe na asiseme tu maneno laini kama watu walivyokuwa wanataka kwaajili ya hayo Isaya hakunyamaza.

Isaya 58:1 “Piga kelele, usiache, Paza sauti yako kama tarumbeta; Uwahubiri watu wangu kosa lao, Na nyumba ya Yakobo dhambi zao.”

Wakati wote kumbe Roho wa Mungu anapokuwa juu yako kwaajili ya huduma ambayo Mungu ameiweka ndani yako ni ukweli ulio wazi hutatulia, wala hutanyamaza utafanya kile ambacho Mungu amekikusudia, kama ni kuwafungua watu, kama ni kuponya kama ni kujenga mioyo ya watu, kama ni kutangaza habari njema, yeye hatakuacha utulie atataka utangaze kile ambacho Mungu anataka kukifanywa kupitia wewe ilikuwa hivyo kwa Isaya nabii na ilikuwa hivyo kwa Masihi Bwana wetu Yesu.

Isaya 61:1-3 “Roho ya Bwana MUNGU i juu yangu; kwa sababu Bwana amenitia mafuta niwahubiri wanyenyekevu habari njema; amenituma ili kuwaganga waliovunjika moyo, kuwatangazia mateka uhuru wao, na hao waliofungwa habari za kufunguliwa kwao.Kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa, na siku ya kisasi cha Mungu wetu; kuwafariji wote waliao; kuwaagizia hao waliao katika Sayuni, wapewe taji ya maua badala ya majivu, mafuta ya furaha badala ya maombolezo, vazi la sifa badala ya roho nzito; wapate kuitwa miti ya haki, iliyopandwa na Bwana, ili atukuzwe.”

Ni maneno ya Nabii Isaya lakini vilevile ni ya Masihi, Yesu alipokuja duniani aliyatumia maneno haya, ni kazi ileile ya Roho Mtakatifu ambaye hataki  mtu mwenye agizo kunyamaza, Roho wa Mungu kupitia Yesu alitaka afungue kinywa chake na kuwahubiria wanyenyekevu habari njema, alitakiwa kuwaganga waliovunjika moyo, alitakiwa kutangaza uhuru kwa mateka, na wafungwa kuwatangazia kufunguliwa, na kuutangaza mwaka wa neema uliokubalika, wasingeliweza kunyamaza kimya katika hayo, na ndio maana tunamuona Yesu akizunguka toka mji mmoja kwenda mji mwingine na vijijini kila mahali akiifanya kazi hii asingeliweza kutulia kwa sababu Roho Mtakatifu alimpaka mafuta kwaajili ya hilo, kila mmoja kwa kusudi lake ambalo kwalo Mungu amekupaka mafuta lifanye kwa bidii na kwa uaminifu wote  na kwa usikivu mkubwa kwa Roho wa Mungu na utaona kuwa huna sababu za kunyamaza!

Isaya 62:1-3 “Kwa ajili ya Sayuni sitanyamaza, na kwa ajili ya Yerusalemu sitatulia, hata haki yake itakapotokea kama mwangaza, na wokovu wake kama taa iwakayo. Na mataifa wataiona haki yako, na wafalme wote watauona utukufu wako; nawe utaitwa jina jipya, litakalotajwa na kinywa cha Bwana. Nawe utakuwa taji ya uzuri katika mkono wa Bwana, na kilemba cha kifalme mkononi mwa Mungu wako.”

Isaya anazungumza kwa niaba ya mji wa Yerusalem yaani Sayuni akimaanisha Israel, kwamba pamoja na kukumbwa na matukio mbalimbali na kubomolewa na maadui lakini haitakuja itokee, mji huu usisimame, ni mji ambao uko kwenye mapenzi ya Mungu, ni mji uliowekewa waombezi, manabii, na waombolezaji maarufu, ambao wanauombea usiku na mchana ili kwamba ufalme wa Mungu uweze kusimama, Kama Mungu alivyomuinua Isaya bado anaendelea kuinua watu wanaoiombea Israel kila iitwapo leo katika kila kona za Dunia, wanaoitakia mema Israel wako kama jeshi, Yerusalem ni mji ambao Utawala halisi wa kimasihi utatawala na Kristo akiwa Mfalme wa utawala huo Wakristo wanapoomba katika sala ya Bwana ufalme wako uje na mapenzi ya Mungu yatimizwe hapa duniani kama mbinguni Mathayo 6:10 maana yake tunaomba pia kwamba Yesu arudi na kusimamisha utawala wake hapa duniani na ufalme huo na kiti chake cha Enzi kitakuwa Israel,Pale Yerusalem, Sayuni, Kwaajili ya Israel Hatuwezi kunyamaza

Yeremia 20:7-9 “Ee Bwana, umenihadaa, nami nimehadaika; wewe una nguvu kuliko mimi, ukashinda; nimekuwa kitu cha kuchekesha, mchana kutwa; kila mtu hunidhihaki.Maana kila ninenapo napiga kelele, nalia, Dhuluma na uharibifu! Kwa kuwa neno la Bwana limefanywa shutumu kwangu, na dhihaka, mchana kutwa. Nami nikisema, Sitamtaja, wala sitasema tena kwa jina lake; basi, ndipo moyoni mwangu kumekuwamo kama moto uwakao, uliofungwa ndani ya mifupa yangu, nami nimechoka kwa kustahimili, wala siwezi kujizuia.”             

Yeremia alitumwa na Mungu kumbuka kuwa Mungu aliweka maneno ndani yake na kumuamuru kuyasema haikuwa kitu rahisi kukubalika katika mioyo ya watu kiasi ambacho hata pamoja na kuwa Mungu alimwambia nitakuwa pamoja naye alikutana na magumu sana alitiwa gerezani, aliteswa alitupwa katika shimo  la matope ilifikia hatua alitaka kukaa kimya asiseme lakini kwa kadiri alivyokuwa akijitahidi akae kimya kuna nguvu ya kiungu iliyokuwa inamlazimisha kusema wivu wa kiungu ulijaa ndani yake na alipoona uovu uliokuwa ukiendelea na ujumbe aliopewa kusema maneno yalimuunguza akawa hawezi kuyafumbia mdomo alilazimika kutangaza kile ambacho Mungu alikuwa amemuagiza pamoja na kuwa ilimgharimu mateso makali na maumivu makubwa.

Yeremia 47:6-7 “Ee upanga wa Bwana, Siku ngapi zitapita kabla hujatulia? Ujitie katika ala yako; Pumzika, utulie.Utawezaje kutulia, Ikiwa Bwana amekupa agizo? Juu ya Ashkeloni na juu ya pwani, Ndipo alipoyaamuru hayo.”

Wafilisti walikuwa wanaikalia pwani ya Yuda na mara nyingi kihistoria kulikuwa na ugomvi kati ya nchi ya Israel na wafilisti,  Yeremia alitakiwa kutoa unabii wa kuwaonya wafilisti ya kuwa upanga wa Bwana utawahusu, ni kama Mungu alikuwa ameamuru hukumu kwa wafilisti kuwa upanga wa Bwana uipige Gaza na Ashkeloni, ilionekana kuwa hakutakuwa na utulivu kwa wafilisti, kila wakati Gaza itapigwa, hatujui kama nabii aliwaombea wafilisti angalau upanga utulie Lakini lilikuwa ni agizo la Mungu upanga ulikataa kutulia kwa sababu ulikuwa na agizo la Mungu, utawezaje kutulia ikiwa Bwana amekupa agizo? Kupigwa kwa Gaza ni agizo la kimaandiko na itaendelea kuwa hivyo kwa sababu ndivyo neno la Mungu linavyosema na Roho wa Mungu husukuma hukumu juu ya Gaza kwa sababu ni agizo lililoko katika neno lake.

Yoel 2:28-29 “Hata itakuwa, baada ya hayo, ya kwamba nitamimina roho yangu juu ya wote wenye mwili; na wana wenu, waume kwa wake, watatabiri, wazee wenu wataota ndoto, na vijana wenu wataona maono; tena juu ya watumishi wenu, wanaume kwa wanawake, katika siku zile, nitamimina roho yangu.”

Ni unabii wa maana sana kimsingi unahusiana na siku za mwisho na ujio wa Roho Mtakatifu kama alivyoona Yoel Roho Mtakatifu atakuja na kazi maalumu kwa kila watu na makundi na kila mmoja hataweza kukaaa kimya atasema tu, watatabiri, wanaona maono, wataota ndoto, kwa hiyo tunaweza kukubaliana wote ya kuwa ubatizo wa Roho Mtakatifu utasababisha na kumfanya kila mwanadamu kutokutulia, neno la Mungu linasema tena juu ya watumishi wangu, nini maana yake watumishi maana yake “Bond Servants” ni neno limetumika mara 800 katika maandiko likimaanisha ni watu wa kazi watumwa hawatatulia, kila atakayepewa Roho wa Mungu hataweza kuwa na utulivu atafanya kile ambacho Mungu ambaye ni bwana wetu amekusudia akifanye.  

Mika 3:8 “Bali mimi, hakika nimejaa nguvu kwa roho ya Bwana; nimejaa hukumu na uwezo; nimhubiri Yakobo kosa lake, na Israeli dhambi yake.”

Mika aliitwa kuwa msemaji kwa niaba ya Mungu yaani nabii, alinena kwa uweza wa Roho Mtakatifu, alitakiwa kuikemea dhambi katika nyumba ya Mungu na ilikuwa ni kazi aliyopewa pamoja na kuonyesha moyo wa Mungu, kutia moyo na kukatisha tamaa uovu, wakati wa Mika kulikuwa na manabii wa uongo wengi, waliokuwa wakiwakosesha watu wa Mungu kwa jumbe zisizo za kweli, lakini uweza wa Roho wa Bwana haukumpa Amani Mika alipewa kusema, alipewa kuonya, alipewa kutangaza hukumu, alipewa kutangaza rehema asingeliweza kunyamaza

Mika 3:5 “Bwana asema hivi katika habari za manabii wanaowakosesha watu wangu; hao waumao kwa meno yao, na kulia, Amani; na mtu awaye yote asiyetia kitu vinywani mwao, wao humwandalia vita.”

Mungu alimtaka Mika kukemea na kusema kweli, bila kujali kuwa liko kundi la manabii feki yaani wa uongo, Kanisa halipaswi kufuata shinikizo la watu Fulani ndani au nje ya nchi wanaotaka tuwe na mtindo Fulani unaofanana wa maisha hata kama mambo hayo ni uovu yako kinyume na Mungu na mila zetu, Kanisa ni lazima likemee bila huruma kile ambacho kinaonekana kuwa ni uongo na kuwa kiko kinyume na mapenzi ya Mungu, Mika hakufuata mkumbo alibaki katika zamu yake na kukemea kweli kweli kwa sababu nyuma yake kulikuwa na shinikizo la Roho Mtakatifu kwanini hatuwezi kunyamaza kwa sababu Roho wa Mungu anafanya hivyo ndani yetu, hakuna anayeweza kutulia!

Zekaria 4:6-9 “Akajibu akaniambia, akisema, Hili ndilo neno la Bwana kwa Zerubabeli, kusema, Si kwa uwezo, wala si kwa nguvu, bali ni kwa roho yangu, asema Bwana wa majeshi.Nani wewe, Ee mlima mkubwa? Mbele ya Zerubabeli utakuwa nchi tambarare; naye atalileta lile jiwe la kuwekwa juu kabisa pamoja na vigelegele vya, Neema, neema, ilikalie. Tena neno la Bwana likanijia, kusema, Mikono yake Zerubabeli imeiweka misingi ya nyumba hii, na mikono yake ndiyo itakayoimaliza; nawe utajua ya kuwa Bwana wa majeshi amenituma kwenu.”

Mungu alimuinua Zerubabeli kuijenga tena Nyumba ya Mungu katika mazingira magumu wakati Israel waliporejea kutoka utumwani Babeli yaani wayahudi, kazi hii ilikuwa ngumu kiasi ambacho kuna wakati watu walikuwa kama wameisusia, Lakini Mungu aliwainua manabii Habakuki, Zekaria na Malaki kuwatia moyo viongozi waliokuwa wanahusika na agizo la kuijenga nyumba ya Bwana walipokuwa wanasita sita Zekaria alipewa ujumbe kumtia Moyo Zerubabeli kuwa nyumba hiyo itajengeka tu sio kwa uweza wa kiserikali wala wa kijeshi bali Roho Mtakatifu, huyu atainua hari ya wajenzi na watajenga kwa uwezo wake hakuna mtu atakayeweza kutulia kwa sababu Roho wa Mungu atasababisha kazi yake itendeke na hakuna kikwazo chochote kitakachoweza kusimama mbele ya wajenzi.

Matendo 1:8 “Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi.”    

Ni tangazo la ujio wa Roho Mtakatifu kwa kanisa, mitume waliagizwa kusubiria ubatizo huo na walihakikishiwa kuwa watakapopokea ubatizo wa Roho Mtakatifu hawataweza kukaa kimya watasema, watahubiri, watathibitisha na kuwa wao ni mashahidi wa kweli kwaajili ya Yesu kristo, hatakuja kuwa na kizuizi watamtii Mungu kuliko wanadamu katika swala zima la kuhubiri injili.

Matendo 5:17-32 “Akaondoka Kuhani Mkuu na wote waliokuwa pamoja naye, (hao ndio walio wa madhehebu ya Masadukayo), wamejaa wivu, wakawakamata mitume wakawaweka ndani ya gereza; lakini malaika wa Bwana akafungua milango ya gereza usiku, akawatoa, akasema, Enendeni mkasimame hekaluni mkawaambie watu maneno yote ya Uzima huu. Nao waliposikia wakaenda alfajiri hekaluni, wakaanza kufundisha. Akaja Kuhani Mkuu nao waliokuwa pamoja naye, wakawakutanisha watu wa baraza, na wazee wote wa wana wa Israeli, wakatuma watu gerezani ili wawalete. Hata watumishi walipofika hawakuwaona gerezani, wakarudi wakatoa habari, wakisema, Gereza tumeikuta imefungwa salama, nao walinzi wamesimama mbele ya mlango; lakini tulipoufungua hatukukuta mtu ndani. Basi jemadari wa hekalu na wakuu wa makuhani waliposikia haya, wakaingiwa na shaka kwa ajili yao, litakuwaje jambo hilo. Mtu mmoja akaja akawapasha habari ya kwamba, Watu wale mliowaweka gerezani wako ndani ya hekalu, wamesimama wakiwafundisha watu. Ndipo yule jemadari akaenda pamoja na watumishi, wakawaleta, lakini si kwa nguvu, kwa maana waliogopa watu wasije wakawapiga kwa mawe. Walipowaleta, wakawaweka katika baraza. Kuhani Mkuu akawauliza, akisema, Je! Hatukuwaamuru ninyi kwa nguvu, msifundishe kwa jina hili? Nanyi, tazameni, mmeijaza Yerusalemu mafundisho yenu, na mnataka kuileta damu ya mtu yule juu yetu. Petro na mitume wakajibu, wakisema, Imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu. Mungu wa baba zetu alimfufua Yesu, ambaye ninyi mlimwua mkimtundika katika mti. Mtu huyo Mungu amemtukuza kwa mkono wake wa kuume, awe Mkuu na Mwokozi, awape Waisraeli toba na msamaha wa dhambi. Na sisi tu mashahidi wa mambo haya, pamoja na Roho Mtakatifu ambaye Mungu amewapa wote wamtiio.”

Mitume walikuwa na agizo la kuihubiri injili, na Mungu Roho Mtakatifu alikuwa amewabatiza kusudi waweze kulitimiza kusudi hilo pana la Mungu, hata hivyo walikutana na upinzani mkali kutoka kwa wazee wa kiyahudi wajulikanao kama Sanhedrin yaani mahakama kuu ya kiyahudi, hawa waliwakataza wasihurbiri wala wasiseme kitu kuhusu Yesu, waliwatia gerezani lakini hata hivyo malaika wa Bwana aliwafungulia hawawezi kunyamaza waliagizwa waendelee kufundisha na walifanya hivyo, wazee walikasirika sana  wakiwataka wakae kimyaa Petro  na mitume wakajibu hoja kuwa imetupasaa kumtii Mungu kuliko wanadamu, Roho Mtakatifu hutuwezesha kuwa na utii wa kiwango cha juu kwaajili ya kile ambacho tumeitiwa kukifanya na kufundisha na kulisema neno lake tunawezaje kunyamaza? Kanisa ndio maana hatuwezi kunyamaza na ndio maana hata mimi na wewe hatuwezi kunyamaza.    

Matendo 17:16 “Paulo alipokuwa akiwangojea huko Athene na kuona jinsi mji ule ulivyojaa sanamu, roho yake ilichukizwa sana ndani yake.”

Paulo mtume aliihubiri injili huko Thesalonike na Beroya, hata hivyo wayahudi wenye wivu walimuwinda na kutaka kumua, kwa hiyo wanafunzi waliookoka walimpeleka Paulo katika mji wa Athene ili awasubiri Timotheo na Sillas ambao walibaki katika miji ya awali, Neno la Mungu linatuambia  wakati alipokuwa akiwasubiri huko Athene aliona mji ule umejaa sanamu, roho yake ilichukizwa sana Katika kiingereza tunaambiwa hivi “his spirit was stirred in him” neno stirred katika kiyunani ni “Paroxunō” maana yake easily Provoked  yaani alichochewa, alipatwa na hasira ya kiungu au alisukumwa kutokukaa kimya, Roho Mtakatifu ndani ya Paulo mtume alipoona sanamu hakusubiri aliona itachelewesha akaanza kuhubiri, Roho wa Mungu hatakuacha unyamaze akiwa ameweka kitu au mzigo au wajibu ambao unatakiwa uutekeleze. Je wewe roho yako inachukizwa? Unapoona wanadamu wanaoana na mbwa? unachukizwa na kuona mwanaume akimpa binti yake mimba?, wanadamu wakilala na wanyama, madaktari wakifanya ngono na wagonjwa, watumishi wanapozini na washirika, matajiri wakipewa nafasi ya vyeo vikubwa makanisani, washirika wakiibiwa fedha na kutajirisha wahubiri, Wahubiri wakijilimbikizia mali, kampeni za kisiasa zikitapakaa makanisani, watu wakipeana sumu kwaajili ya nafasi za uongozi, watu wakiombewa bila kuongozwa sala ya toba, wanakwaya wakitembea wenyewe kwa wenyewe, wanamuziki wakiacha waume zao na ndoa zao kwa kisingizio cha wito, unanyamazaje wakati utoaji wa mimba umeingia makanisani hata wanandoa waliookoka siku hizi wanatoa mimba?, madawa ya kuleywa yakiuzwa kila mahali, rushwa na ushoga umetapakaa kila mahali, unanyamazaje wakati watu wakiwa wahanga wa picha za ngono? Uamsho ukisisitizwa bila utakatifu, mafundisho potofu yakiwa hayakemewi, watu wakiwa wanatekwa na kuuawa, mauaji ya kutisha yakisambaa, ulawiti na ubakaji uliokithiri, hali ya uchumi ikiendelea kuwa mbaya? Paulo mtume angekuwepo leo asingeliweza kunyamaza, ikiwa sanamu tu zilimsumbua sana sisi nasi hatunabudi kuhakikisha kuwa tunaifikia jamii na kuijenga kwa gharama yoyote ile na kamwe hatuwezi kunyamaza!, Roho Mtakatifu akiwa ndani yetu roho zetu zitachukizwa hatuwezi kunyamaza!

Warumi 1:16-17 “Kwa maana siionei haya Injili; kwa sababu ni uweza wa Mungu uuletao wokovu, kwa kila aaminiye, kwa Myahudi kwanza, na kwa Myunani pia. Kwa maana haki ya Mungu inadhihirishwa ndani yake, toka imani hata imani; kama ilivyoandikwa, Mwenye haki ataishi kwa imani.”                

Paulo mtume anaonyesha wazi kuwa haionei haya injili kwa sababu ni uweza wa Mungu uletao wokovu kwa watu waaminio, kutokana na uwezo mkubwa wa habari njema kuwasaidia wanadamu na kuwapa uzima wa milele bure kwa Imani katika Kristo Yesu Paulo anaona ana wajibu wa kutokuionea haya injili iwe ni kwa kufungwa au kudhaliliswa, au kuteswa kwa sababu zozote zile hawezi kuona aibu kwa sababu ya injili, maana yake pia hawezi kukaa kimya kwaajili ya injili ataendelea kuisema katika mazingira yoyote.

2Timotheo 1:7-9 “Maana Mungu hakutupa roho ya woga, bali ya nguvu na ya upendo na ya moyo wa kiasi.Basi usiuonee haya ushuhuda wa Bwana wetu, wala usinionee haya mimi mfungwa wake, bali uvumilie mabaya pamoja nami kwa ajili ya Injili, kwa kadiri ya nguvu ya Mungu; ambaye alituokoa akatuita kwa mwito mtakatifu, si kwa kadiri ya matendo yetu sisi, bali kwa kadiri ya makusudi yake yeye na neema yake. Neema hiyo tulipewa katika Kristo Yesu tangu milele,”

Paulo anamkumbusha Timotheo kutokuonea haya ushuhuda wa Bwana, kutokuionea haya ufungwa kwaajili ya injili, anamtaka avumilie mabaya kwaajili ya injili aendelee kwa kadiri ya nguvu za Mungu aliyewaita akimkumbusha kuwa Roho Mtakatifu sio Roho ya woga bali ni ya nguvu na upendo na moyo wa kiasi kwa hiyo haijalishi ni magumu kiasi gani anakutana nayo anamtaka aendelee na kazi ya wito mtakatifu kwa kusudi lile kuu, Roho Mtakatifu huondoa woga wote na kutupa ujasiri, na nguvu na upendo ili tuweze kusonga mbele kwa wito tulioitiwa hivyo hatuwezi kunyamaza, Ni yeye ambaye akiwa ndani yetu tutavurugwa, tutachukizwa na sanamu, tutataharakishwa hatutakubali uonevu wa ibilisi dhidi ya ndugu zetu, tutawaombea watu, tutawafungua watu, tutawapa watu mahitaji yao kwa msukumo wa Roho Mtakatifu ndani yetu ni yeye ni yeye ni yeye anayesababisha hatuwezi kunyamaza kamwe!

2Timotheo 2:8-9 “Mkumbuke Yesu Kristo, aliyefufuka katika wafu, wa uzao wa Daudi kama inenavyo injili yangu. Nami katika hiyo nimeteswa hata kufungwa kama mtenda mabaya; lakini neno la Mungu halifungwi.”

Mwisho Paulo mtume akiwa kifungoni anamkumbusha Timotheo kumkumbuka Yesu aliyefufuka katika wafu, ya kuwa uko ushindi katika maisha yetu ya kazi ya injili kama Daudi alivyoshinda Vita vyote kwa jinsi ya mwili, Yesu naye ameshinda vita vyote vya kiroho, kwa hiyo hata ingawa Paulo mtume alikuwa kifungoni, alimwambia Timotheo kuwa neno la Mungu halifungwi, akiwa kifungoni hakuweza kunyamaza na badala yake alianza kuandika nyaraka zenye kuwatia moyo waamini na watumishi wa Mungu na kuendelea kuwajenga, Katika nyakati zetu leo hata kama tutakuwa gerezani, injili itaendelea kwa sababu Roho Mtakatifu hatatuacha kunyamaza. Neno la Mungu halifungwi! Roho Mtakatifu hatatuacha tuwe na utulivu bila kutimiza ile huduma ya upatanisho aliyoiweka ndani yetu haleluyaa!

Hitimisho

Usinyamaze kwaajili ya kile ambacho Mungu amekuitia kukifanya uwepo wa Roho Mtakatifu katika maisha yetu unatufanya kuwa na msaidizi wa karibu ndani yetu, kiongozi ndani yetu, mwenye kututia nguvu, na anatutia nguvu na kutupa nguvu za ushawishi ndani yetu, Hatuna budi kumtii  na kukubali kuongozwa naye katika kuyatii mapenzi yake na tunapomtii atasema nasi na kutusukuma kama nguvu ya moto ndani yetu akiweka wivu, wa Bwana na kutusukuma katika kuyatii mapenzi yake kwa hiyo ni lazima kuhakikisha kuwa tunaihubiri injili kwa namna yoyote kila mmoja kwa kadiri ya wito wake alioitiwa na kamwe tusiache kwa sababu tukiacha watu watakengeuka, mwenye kuomba asiache kuomba, mwenye kuhubiri asinyamaze, mwenye kutoa asiache, mwenye kuangalia wafungwa asiache, mwenye kufariji wajane na yatima asiache, mwenye kushuhudia asiache, mwenye kufundisha asiache mwenye kusimamia asiache, mwenye kutia moyo asiache na mwenye kuandika kama mimi asiache hakuna anayeweza kutunyamazisha kwa sababu Roho wa Mungu anataka kila kitu kitimizwe ndani yetu kwa wakati wake! 

2Timotheo 4:1-5 “Nakuagiza mbele za Mungu, na mbele za Kristo Yesu, atakayewahukumu walio hai na waliokufa; kwa kufunuliwa kwake na kwa ufalme wake; lihubiri neno, uwe tayari, wakati ukufaao na wakati usiokufaa, karipia, kemea, na kuonya kwa uvumilivu wote na mafundisho. Maana utakuja wakati watakapoyakataa mafundisho yenye uzima; ila kwa kuzifuata nia zao wenyewe watajipatia waalimu makundi makundi, kwa kuwa wana masikio ya utafiti;nao watajiepusha wasisikie yaliyo kweli, na kuzigeukia hadithi za uongo.Bali wewe, uwe na kiasi katika mambo yote, vumilia mabaya, fanya kazi ya mhubiri wa Injili, timiliza huduma yako.”

Warumi 12:4-8 “Kwa kuwa kama vile katika mwili mmoja tuna viungo vingi, wala viungo vyote havitendi kazi moja; Vivyo hivyo na sisi tulio wengi tu mwili mmoja katika Kristo, na viungo, kila mmoja kwa mwenzake. Basi kwa kuwa tuna karama zilizo mbalimbali, kwa kadiri ya neema mliyopewa; ikiwa unabii, tutoe unabii kwa kadiri ya imani; ikiwa huduma, tuwemo katika huduma yetu; mwenye kufundisha, katika kufundisha kwake; mwenye kuonya, katika kuonya kwake; mwenye kukirimu, kwa moyo mweupe; mwenye kusimamia kwa bidii mwenye kurehemu, kwa furaha.”

Roho wa Mungu hututia nguvu katika maisha yetu kuishinda aibu, woga, na vikwazo na kutupa ujasiri na hali ya kutokuweza kukaa kimya akitenda kazi ndani yetu na kututia nguvu na ujasiri na kutuagiza kwa neno lake na kwa sababu hiyo hatuwezi kunyamaza, Martini Luther King Jr alikuwa mchungaji lakini wakati huo ulikuwa ni wakati wa ubaguzi mkubwa wa rangi nchini Marekani, alisimama sio tu kama Muhubiri lakini aliionyesha jamii kuwa matukio ya kibaguzi sio kitu sahihi, hakunyamaza kila lilipojitokeza tukio la kibaguzi na aliuawa kwaajili ya hilo, naamini kuwa Mungu alimtia nguvu, kutokukaa kimya na yeye alisema tutakaa kimya pale tu tutakapokuwa tumekufa, au kwa lugha nyingine Maisha yetu hufikia mwisho pale tu tunapoanza kukaa kimya kwaali ya maswala ya msingi Our lives begin to end the day we become silentBill Bright yeye alisema “Why we cannot remain Silence  kwanini hatuwezi kukaa kimya akikazia kwa sababu tuna agizo kuu la kuihubiri injili, na mimi nimesema kwanini hatuwezi kunyamaza kwa sababu Roho Mtakatifu yuko ndani yetu naye ndiye kichocheo na sababu kwanini hatuwezi kunyamaza.

Wewe nawe kamwe usikae kimya kwa kile ambacho Roho Mtakatifu amekuwekea ndani yako,  Endelea kupiga kelele kama ni za uamsho, kemea kama ni za kukemea manabii wa uongo, kama ni injili ihubiri, unazo sababu lukuki kwanini hauwezi kukaa kimya, tunazo sababu nyingi kwanini hatuwezi kunyamaza haleluyaaa! Uongezewe neema

Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima   

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni