Alhamisi, 10 Oktoba 2024

Wewe nawe utakuwa kama mmoja wa wapumbavu?


2Samuel 13:11-13 “Naye alipokwisha kuileta karibu naye, ili ale, Amnoni akamkamata, akamwambia, Njoo ulale nami, ndugu yangu. Naye akamjibu, La, sivyo, ndugu yangu, usinitenze nguvu; kwani haifai kutendeka hivi katika Israeli; usitende upumbavu huu. Nami nichukue wapi aibu yangu? Wewe nawe utakuwa kama mmoja wa wapumbavu wa Israeli. Basi, sasa, nakusihi, useme na mfalme; kwa maana hatakukataza kunioa.”      

   



Utangulizi

Mojawapo ya tatizo ambalo limeleta majuto makubwa sana duniani na kuwaingiza wanadamu wengi kwenye changamoto mbalimbali ni pamoja na Upumbavu!, amini usiamini upumbavu umegharimu maisha ya watu wengi sana, na ni kupitia upumbavu aidha wa kwetu wenyewe au wa mtu mwingine, wengi wetu tumejikuta katika matatizo na changamoto zilizogharimu maswala kadhaa katika maisha, na ndio maana unaweza kuona maandiko matakatifu yakisisitiza sana umuhimu wa kuitafuta hekima kwa gharama yoyote ile kwa sababu hekima ni bora sana kuliko madini yoyote yale ya thamani zikiwemo rubi au marijani, Hekima inasimama kama njia ya kutusaidia kuvuka katika dunia hii salama.

Mithali 8:10-11 “Pokea mafundisho yangu, wala si fedha, Na maarifa kuliko dhahabu safi. Maana hekima ni bora kuliko marijani; Wala vyote vinavyotamanika havilingani nayo.”

Kwa msingi huo tunapojifunza somo hili lenye kichwa “Wewe nawe utakuwa kama mmoja wa wapumbavu?” Maana yake ni nini? Maana yake leo tutazungumzia kwa kina na mapana na marefu jinsi tunavyoweza kukwepa kufanya upumbavu tukiwa hapa duniani na hatimaye kuona umuhimu wa kumuomba Mungu na kuifuata njia ya Hekima ili tuweze kufanikiwa katika maisha haya  na yale yajayo, tutajifunza somo hili Wewe nawe utakuwa kama mmoja wa wapumbavu ? kwa kuzingatia vipengele vitatu viafuatavyo:-

·         Maana ya neno Upumbavu

·         Wewe nawe utakuwa kama mmoja wa wapumbavu?

·         Chagua Hekima!

Maana ya neno Upumbavu

Neno upumbavu katika lugha ya kiingereza linaelezewa kwa misamiati mingi sana kama vile fool, lacking of good sense, lacking of good judgement, unwise, stupid, silly, Idiotic, na kadhalika, lakini neno maarufu sana linalotumika katika Biblia hususani agano la kale ambalo limeletwa kwetu kwa lugha ya kiebrania ni neno nãbhãl  neno hilo kimsingi katika tamaduni za kiebrania linachukuliwa kama mtu aliyekosa hekima au mtu aliyepuuzia hekima, mtu asiye na uadilifu, mtu baradhuli, mtu muovu, mtu mbaya, mtu asiyetenda haki, mtu mwenye kuaibisha, mtu anayezungumza pumba, au mtu asiye muungwana, aliekosa uungwana au asiyefunzwa uungwana, mtu wa hila, asiye na akili, au mtu mwenye akili na hekima akifanya jambo la kushangaza kinyume na akili yake au hekima au njia ya Mungu, kwa hiyo katika mtazamo wa kiungu kufanya upumbavu ni kufanya jambo ambali liko kinyume na neno.  

Isaya 32:5-8 “Mpumbavu hataitwa tena mwungwana, wala ayari hatasemwa kwamba ni karimu. Maana mpumbavu atanena yaliyo upumbavu, na moyo wake utafanya maovu, ili kutenda hila na kusema yasiyo kweli juu ya Bwana, ili kuziacha nafsi za watu wenye njaa hazina kitu, na kukikomesha kinywaji chake mwenye kiu. Tena vyombo vyake ayari ni vibaya; hutunga hila mbaya, ili kuwaangamiza wanyonge kwa maneno ya uongo, mtu mhitaji ajaposema maneno yenye haki. Bali mwungwana huwaza mambo ya kiungwana, naye hushika sana mambo ya kiungwana.”

Kwa hiyo katika maandiko, mtu asipofikiri katika kutenda kwake, au akifanya maamuzi mabaya na hata kufikiri vibaya maana yake ametenda kwa upumbavu, na jambo hilo linaweza kutugharimu katika maisha yetu kimwili na kiroho.

2Samuel 24:9-10 “Naye Yoabu akamtolea mfalme jumla ya hesabu ya watu; nao walikuwa wa Israeli mashujaa wenye kufuta panga mia nane elfu; nao wa Yuda walikuwa watu mia tano elfu. Ndipo moyo wake Daudi ukamchoma baada ya kuwahesabu hao watu. Naye Daudi akamwambia Bwana, Nimekosa sana kwa haya niliyoyafanya; lakini sasa, Ee Bwana, nakusihi uuondolee mbali uovu wa mtumishi wako; kwani nimefanya upumbavu kabisa.”        

Kwa hiyo lugha upumbavu katika maandiko inaweza kuwa na upana wa kiharibiko zaidi ya kukosa maarifa, au ukosefu wa ustaarabu na kama mwanadamu hatakuwa makini mtu awaye yote yule, wa ngazi yoyote ile anaweza kujikuta anafanya upumbavu! Bwana ampe neema kila mmoja wetu ili tusiwe miongoni mwa watu watakaofanya upumbavu na kujutia katika maisha yetu, Katika jina la Yesu Kristo ameen!

Wewe nawe utakuwa kama mmoja wa wapumbavu?

Wakati wowote ule tunapofanya jambo ambalo limeagizwa katika neno la Mungu na lina uhusiano na uadilifu hapo tunatenda kwa hekima, na wakati wowote ule tunapofanya jambo ambalo liko kinyume na mapenzi ya Mungu na swala zima la uvunjifu wa uadilifu maana yake tunakuwa tumetenda kwa upumbavu, kwa hiyo upumbavu ni dhambi, upumbavu ni ujinga na upumbavu unaweza kutuweka pabaya, upumbavu unaweza kuyagharimu maisha yetu na ya wengine, na kwa kweli tukiruhusu, wivu, chuki, choyo, ubinafsi, kupenda fedha, kupenda madaraka, kujivuna kutembea kwa kiburi, na kadhalika na hayo yakatawala nafsi zetu ni rahisi sana kujikuta tumefanya upumbavu, kwa hiyo utaweza kuona kuwa dhambi na upumbavu ni mapacha wanaotembea kwa ukaribu sana  na tuwapo duniani  tunapaswa kujihadhari sana tusifanye upumbavu, ili tuweze kuishi kwa Amani.

Katika andiko letu la Msingi, ambalo Roho Mtakatifu Mwalimu mkuu alinipa na ndiko nilikopata kichwa cha ujumbe wa somo hili, tunasoma habari za Amnoni kijana aliyejawa na tamaa na kumpenda dada yake waliozaliwa mama tofauti lakini kwa baba mmoja, kijana huyu alimtamani sana dada yake na kiasi ambacho aliandaa njama za kutaka kumbaka, dada huyu alimshauri vizuri kwamba kama unanipenda unaweza kuzungumza na mfalme baba yao na hatakuzuia kunioa, lakini yeye akizidiwa na tamaa aliendelea na mpango wake wa kutaka kumbaka, dada yake aliyeonekana kuwa na busara sana alimshauri kuwa kwa kutumia njia anayotaka kuitumia atakuwa kama mojawapo ya wapumbavu katika Israel, yaani licha ya kuwa amefanya dhambi lakini atakuwa amefanya upumbavu, hii maana yake ni nini? wakati wote tunapoacha kutumia busara katika jambo lolote lile na tukaachia hisia zetu na tamaa ya mioyo yetu ituongoze maana yake au kinyume chake tunachagua njia ya kipumbavu na swali hili litatuhusu wewe nawe utakuwa kama mmoja wa wapumbavu?, maandiko matakatifu yamejaa mifano mingi ya watu waliotenda kwa upumbavu ambayo sisi hatupaswi kuiigia, kwani yaliandikwa kwa kusudi la kutupa hekima sisi tunaoishi miisho ya zamani hizi ili tusifanye upumbavu, kwa mfano:-

1.       Ukiwaza moyoni kuwa hakuna Mungu – Maandiko yanaonya kuwa sio kusema tu lakini mtu awaye yote ambaye anawaza moyoni mwake kuwa hakuna Mungu kibiblia huyo ni mpumbavu, hajishughulishi kumtafuta Mungu, haamini kama Mungu yupo, huyo ni mtenda maovu, awaye yote yule ambaye anaishi kana kwamba hakuna Mungu naye ni mpumbavu, wote wanaoishi kwa ukaidi wakikataa miongozo ya Mungu, wakilikataa neno la Mungu, wakiwa hawamtafuti Mungu na wanaishi sawa tu mawazo yao hao wanakuwa wamekengeuka na jumla yaw azo la kimungu kwao katika maandiko ni kuwa wamepumbazika.

Zaburi 14:1-3 “Mpumbavu amesema moyoni, Hakuna Mungu; Wameharibu matendo yao na kuyafanya chukizo, Hakuna atendaye mema. Toka mbinguni Bwana aliwachungulia wanadamu, Aone kama yuko mtu mwenye akili, Amtafutaye Mungu. Wote wamepotoka, wameoza wote pamoja, Hakuna atendaye mema, La! Hata mmoja.

Zaburi 53:1-3 “Mpumbavu amesema moyoni, Hakuna Mungu; Wametenda uovu wa ufisadi na kuchukiza, Hakuna atendaye mema. Toka mbinguni MUNGU aliwachungulia wanadamu, Aone kama yuko mtu mwenye akili, Amtafutaye Mungu.Kila mtu amepotoka, wameoza wote pamoja, Hakuna atendaye mema, La! Hata mmoja.

2.       Anayeshauri mtu amwache Mungu – Wako watu ambao katika namna ya kushangaza sana wanaweza kukushauri umwache Mungu, au utafute msaada kwa miungu mingine kwa sababu ya changamoto unazozipitia na misimamo yako katika kumuamini Mungu mtu anayefanya hivyo au kutoa ushauri wa namna hiyo katika maandiko anatajwa kama mtu anayezungumza upumbavu au pumba. Aidha mtu awaye yeto akikubali kuyategemea mawazo yake na njia zake au njia za kibinadamu huyu naye anatenda kwa upumbavu

Ayubu 2:7-10 “Basi Shetani akatoka mbele za uso wa Bwana, akampiga Ayubu na majipu mabaya tangu wayo wa mguu hata utosi wa kichwa. Naye akashika kigae cha kujikunia; akaketi majivuni. Ndipo mkewe akamwambia, Je! Wewe hata sasa washikamana na utimilifu wako? Umkufuru Mungu, ukafe. Lakini yeye akamwambia, Wewe wanena kama mmoja wa hao wanawake wapumbavu anenavyo. Je! Tupate mema mkononi mwa Mungu, nasi tusipate na mabaya? Katika mambo hayo yote Ayubu hakufanya dhambi kwa midomo yake.”  

3.       Kuondoka bila kuaga – Umekaa na mtu kwa muda mrefu katika maisha yako, au mahali ambapo ulikuwa unafanya kazi, alafu ukaamua kuondoka bila kuaga, au kutokumuaga baba yako wa kiroho, na kuamua kutoroka, bila kuagana kwa Amani na kubarikiana tendo hilo kadhalika linaweza kuwa sio dhambi lakini sio la kiungwana  wala kistaarabu kwa hivyo katika maandiko ukilifanya unahesabika kuwa umefanya upumbavu.

Mwanzo 31:26-28 “Labani akamwambia Yakobo, Umefanya nini? Umenihadaa, ukawachukua binti zangu kama mateka waliotwaliwa kwa upanga. Mbona umekimbia kwa siri ukanihadaa, wala hukuniambia, nipate kuagana nawe uende zako kwa furaha, na nyimbo, na ngoma, na kinubi? Wala hukuniacha niwabusu wanangu, na binti zangu; basi umetenda upumbavu.”

4.       Kulala na binti ya watu kabla ya kumchumbia au kumuoa – kimaandiko unapolala na binti ya watu na ukambikiri, kabla ya kumuoa kwa madai kuwa utamuoa baadaye jambo la namna hii ni la kipumbavu katika tamaduni za kimaandiko na Israel. Huwezi kuishi kama mwana ndoa kabla ya ndoa kwa kufanya hivyo unajidhihirisha namna ambavyo umekosa adabu, umekosa heshima, umekosa maarifa huna hekima na umefanya upumbavu.

Mwanzo 34:1-7 “Basi Dina, binti Lea, ambaye Lea alimzalia Yakobo, akatoka kuwaona binti za nchi. Shekemu, mwana wa Hamori, Mhivi, mkuu wa nchi, akamwona akamtwaa, akalala naye, akambikiri. Moyo wake ukaambatana na Dina binti Yakobo, akampenda huyu msichana, akasema na huyu msichana kwa maneno mazuri. Shekemu akamwambia Hamori, babaye, akasema, Unipatie msichana huyu awe mke wangu. Basi Yakobo akasikia ya kwamba amembikiri Dina, binti yake. Na wanawe walikuwako pamoja na wanyama wake nyikani. Yakobo akanyamaza, hata walipokuja. Akatoka Hamori, babaye Shekemu, kumwendea Yakobo, aseme naye. Wanawe Yakobo waliposikia hayo, wakaja kutoka nyikani; nao wakasikitika sana, wakakasirika mno, kwa sababu amefanya upumbavu katika Israeli kwa kulala na binti Yakobo, neno lisilojuzu kutendeka.”           

5.       Kumdhalilisha mwanamke – tendo la mtu kumuoa mwanamke aliye bikira, kisha akafika ndani na ukamchukia kisha kumsingizia kuwa eti hakuwa na ubikira tendo la kumdhalilisha na kumuaibisha mwanamke katika Israel na katika swala zima la uadilifu ni kutenda upumbavu.

Kumbukumbu 22:13-21 “Mtu akitwaa mke, akamwingilia na kumchukia, kisha akamshitaki mambo ya aibu kumzushia jina baya, akasema, Nimemtwaa mwanamke huyu, nami nilipomkaribia sikuona kwake alama za ubikira; ndipo babaye yule kijana na mamaye watakapotwaa alama za yule kijana za ubikira, wawatolee wazee wa mji langoni; na baba yake yule kijana awaambie wazee, Mwanamume huyu nilimpa binti yangu awe mkewe, naye amchukia; angalieni, amemwekea mambo ya aibu, asema, Sikuona kwa binti yako alama za ubikira, nazo hizi ndizo alama za binti yangu za ubikira. Na wayakunjue yale mavazi mbele ya wazee wa mji. Basi wazee wa mji ule na wamtwae yule mtu mume na kumrudi, wamtoze shekeli mia za fedha, wampe babaye yule kijana, kwa kuwa amemzulia jina baya mwanamwali wa Israeli; naye awe mkewe; hana ruhusa ya kumwacha siku zake zote. Lakini likiwa ni kweli neno hili, la kutoonekana kwake yule kijana alama za ubikira; na wamtoe nje yule kijana mlangoni pa nyumba ya baba yake, na waume wa mji wake wampige kwa mawe hata afe; kwa vile alivyofanya upumbavu katika Israeli, kwa kufanya ukahaba katika nyumba ya baba yake; ndivyo utakavyoondoa uovu katikati yako.”

               

6.       Awaye yote anayeiba – Maandiko matakatifu yanaagiza kuwa tusiibe, lakini sio hivyo tu kila mmoja anaagizwa kuyatii maagizo ya Bwana na kulishika agano lake, kufanya jambo kinyume na hayo ni kufanya upumbavu, mtu anayeiba ni mpumbavu, amechagua njia isiyo ya kiungwana.

Yoshua 7:11-15 “Israeli wamefanya dhambi, naam, wamelivunja agano langu nililowaagiza; naam, wametwaa baadhi ya vitu vilivyowekwa wakfu; tena wameiba, tena wameficha na kuvitia pamoja na vitu vyao wenyewe. Ndiposa wana wa Israeli hawawezi kusimama mbele ya adui zao; wakawapa visogo adui zao, kwa sababu wamelaaniwa; mimi sitakuwa pamoja nanyi tena, msipokiharibu kitu kile mlicho nacho kilichowekwa wakfu. Haya! Inuka, uwatakase watu, ukaseme, Jitakaseni, mwe tayari kesho; maana Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi; Kitu kilichowekwa wakfu kiko katikati yako, Ee Israeli; huwezi kusimama mbele ya adui zako, hata mtakapokiondoa kile mlicho nacho kilichowekwa wakfu. Basi asubuhi mtaletwa karibu nami kabila kwa kabila; kisha itakuwa ya kwamba kabila ile atakayoitwaa Bwana itakaribia jamaa kwa jamaa; na jamaa ile atakayoitwaa Bwana itakaribia nyumba kwa nyumba; na nyumba ile atakayoitwaa Bwana itakaribia mtu kwa mtu. Tena itakuwa ya kwamba yeye atakayetwaliwa, naye anacho kitu kile kilichowekwa wakfu, atateketezwa kwa moto, yeye na vitu vyote alivyo navyo; kwa sababu amelivunja agano la Bwana, na kwa sababu ametenda upumbavu katika Israeli.”

7.       Kumbaka mwanamke -  Kumbaka mwanamke na kumuingilia kinyume cha maumbile, sio tu kuwa ni dhambi, lakini vilevie ni upumbavu, katika jamii, jambo hilo ni uovu ambao sio tu utakugharimu kufunguliwa mashitaka na kufungwa lakini kwa Mungu ni dhambi na ni uovu katika jamii.

Waamuzi 20:4-6 “Huyo Mlawi, huyo mume wa mwanamke aliyeuawa, akajibu na kusema, Mimi nilifikilia Gibea ulio wa Benyamini mimi na suria yangu, ili tulale. Nao watu waume wa Gibea wakaniondokea, na kuizingira hiyo nyumba pande zote juu yangu wakati wa usiku; walidhani kuniua, na suria wangu wakamtenza nguvu, hata amekufa.Basi nikamtwaa huyo suria yangu, na kumkata vipande, na kumpeleka katika nchi yote ya urithi wa Israeli; kwa sababu wametenda maovu makuu na upumbavu katika Israeli.”

8.       Tamaa na kutaka kulawiti ni upumbavu – jamii inapokuwa na watu ambao wanaona kuwa mapenzi ya jinsia moja kama jambo la kawaida maana yake jamii hiyo imepumbazika, usagaji ni upumbavu, ulawiti ni upumbavu, usagaji ni upumbavu, ni kukosa akili ni kukosa hekima kwa hiyo ukiiangalia dunia ya leo na swala zima la maovu yanayohusiana na ulawiti na tamaa ya aina hiyo utaweza kuwa na picha halisi kuwa watu hata pamoja na kuwa na elimu kubwa hivyo na marifa kuongezeka, dunia imekuwa na wapumbavu wengi sana.

Waamuzi 19:23-25 “Naye mtu mwenye nyumba akawatokea hapo nje, na kuwaambia, La, sivyo, ndugu zangu nawasihi msifanye uovu jinsi hii; kwa kuwa mtu huyu ameingia ndani ya nyumba yangu, msifanye upumbavu huu. Tazama, binti yangu yupo hapa, ni mwanamwali, na suria wake huyo mtu; nitawaleta hapa nje sasa nanyi watwezeni, na kuwatenda hayo myaonayo kuwa ni mema; lakini mtu huyu msimtende jambo la upumbavu namna hii. Lakini hao watu hawakukubali kumsikia; basi mtu huyo akamshika suria wake, na kumleta nje kwao; nao wakamjua, na kumtenda uovu usiku kucha hata asubuhi kisha kulipoanza kupambauka wakamwacha aende zake.”

Warumi 1:21-28 “kwa sababu, walipomjua Mungu hawakumtukuza kama ndiye Mungu wala kumshukuru; bali walipotea katika uzushi wao, na mioyo yao yenye ujinga ikatiwa giza. Wakijinena kuwa wenye hekima walipumbazika; wakaubadili utukufu wa Mungu asiye na uharibifu kwa mfano wa sura ya binadamu aliye na uharibifu, na ya ndege, na ya wanyama, na ya vitambaavyo. Kwa ajili ya hayo Mungu aliwaacha katika tamaa za mioyo yao, waufuate uchafu, hata wakavunjiana heshima miili yao. Kwa maana waliibadili kweli ya Mungu kuwa uongo, wakakisujudia kiumbe na kukiabudu badala ya Muumba anayehimidiwa milele. Amina. Hivyo Mungu aliwaacha wafuate tamaa zao za aibu, hata wanawake wakabadili matumizi ya asili kwa matumizi yasiyo ya asili; wanaume nao vivyo hivyo waliyaacha matumizi ya mke, ya asili, wakawakiana tamaa, wanaume wakiyatenda yasiyopasa, wakapata nafsini mwao malipo ya upotevu wao yaliyo haki yao.Na kama walivyokataa kuwa na Mungu katika fahamu zao, Mungu aliwaacha wafuate akili zao zisizofaa, wayafanye yasiyowapasa.”                   

9.       Kuropoka – nadhani umewahi kuishi na watu wanaoropoka, na utakuwa unajua madhara ya kuropoka, kuropoka ni kuzungumza kitu bila kufikiri, wako watu yaani kitakachomjia kichwani tu anakitekeleza kwa kusema au kuandika sms isiyofaa, unaweza kutuma ujumbe usiofaa kwa mke wa mtu, mume wa mtu, unaweza kuropoka mambo ya watu au siri za watu, au kutokwa na maneno yasiyo na maana kama mtu hana nidhamu katika kuzungumza kwake maana yake anashindwa kuudhibiti ulimi wake naye anaitwa mpumbavu

Mithali 14:3 “Katika kinywa cha mpumbavu mna fimbo ya kiburi, Bali midomo ya wenye hekima huwahifadhi. 

Mithali 12:15-16 “Njia ya mpumbavu imenyoka machoni pake mwenyewe; Bali yeye aliye na hekima husikiliza shauri. Ghadhabu ya mpumbavu hujulika mara; Bali mtu mwerevu husitiri aibu.”

10.   Kufanya dhambi – Kufanya dhambi ya aina yoyote ile kibiblia ilihesabika kuwa ni kufanya upumbavu, kwani kila dhambi licha ya kuwa uko msamaha wa Mungu na rehema zake lakini kwa kuwa Mungu ni mwenye haki wakati mwingine matokeo ya dhambi yanaweza kuendeleza madhara makubwa nje ya msamaha wa Mungu, mfano ukifanya uasherati ukapata mimba, na ukatubu kwa uasherati ule utasamehewa lakini mimba haitayeyuka kwa hiyo ulipaswa kufikiri kabla ya kutenda na kwa kutokufikiri umefanya upumbavu. Na au ukapata ukimwi, rehema za Mungu zinaweza kuwepo lakini na virusi vinaendelea kuwepo kwa sababu ulifanya upumbavu, hukutoa nafasi ya kufikiri kwa kina madhara unayoweza kuyapata. Kwa hiyo ni muhimu kukumbuka ya kuwa dhambi ina madhara yake na madhara yake ni mabaya sana katika maisha ya watu wote

Zaburi 38:3-5 “Hamna uzima katika mwili wangu Kwa sababu ya ghadhabu yako. Wala hamna amani mifupani mwangu Kwa sababu ya hatia zangu. Maana dhambi zangu zimenifunikiza kichwa, Kama mzigo mzito zimenilemea mno. Jeraha zangu zinanuka, zimeoza, Kwa sababu ya upumbavu wangu.”

Zaburi 69:3-5 “Nimechoka kwa kulia kwangu, Koo yangu imekauka. Macho yangu yamedhoofu Kwa kumngoja Mungu wangu. Wanaonichukia bure ni wengi Kuliko nywele za kichwa changu. Watakao kunikatilia mbali wamekuwa hodari, Adui zangu kwa sababu isiyo kweli. Hata mimi nalilipishwa kwa nguvu Vitu nisivyovichukua. Ee Mungu, unajua upumbavu wangu, Wala hukufichwa dhambi yangu.”

11.   Ukiruhusu hasira kukutawala – wako watu ambao kupitia hasira wamefanya mambo ya kijinga na kipumbavu na baadaye kujilaumu au kupata majuto, maandiko yanatutaka kujidhibiti, kujitia nidhamu, badala ya kujisifia kuwa wewe una hasira, hakikisha unajinidhamu kushindwa kufanya hivyo ni kuruhusu upumbavu.

Muhubiri 7:4-9 “Moyo wake mwenye hekima umo nyumbani mwa matanga, bali moyo wake mpumbavu umo nyumbani mwa furaha. Heri kusikia laumu ya wenye hekima, Kuliko mtu kusikia wimbo wa wapumbavu; Maana kama mlio wa miiba chini ya sufuria, Ndivyo kilivyo kicheko cha mpumbavu. Hayo nayo ni ubatili. Kweli jeuri humpumbaza mwenye hekima, Na rushwa huuharibu ufahamu. Heri mwisho wa neno kuliko mwanzo wake, Na mvumilivu rohoni kuliko mwenye roho ya kiburi. Usifanye haraka kukasirika rohoni mwako, Maana hasira hukaa kifuani mwa wapumbavu.”

12.   Kumtendea maovu mtu ambaye hana nia mbaya na wewe – wako watu wengine kwa sababu ya wivu tu wenye uchungu wanaweza kukutendea mabaya, au wanaweza kukusudia kutenda mabaya kwa watu ambao hawana nia wala wazo la kuwadhuru, kufanya jambo la namna hiyo ni machukizo sio kwa Mungu tu lakini ni upumbavu, kutafuta na kutaka kumdhuru mtu ambaye hana mpango wala nia ya kukudhuru.

1Samuel 26:18-21. “Akasema, Bwana wangu ananiwinda mimi mtumishi wake kwa sababu gani? Nimefanya nini mimi? Ni uovu gani nilio nao mkononi mwangu? Basi sasa, nakusihi, bwana wangu, mfalme, na asikie maneno ya mtumishi wake. Ikiwa ni Bwana aliyekuondokesha juu yangu, na akubali sadaka; bali ikiwa ni wanadamu, na walaaniwe mbele za Bwana; kwa sababu wamenifukuza leo, nisishikamane na urithi wa Bwana, wakisema, Enenda, katumikie miungu mingine.Basi sasa, isianguke damu yangu chini mbali na uso wa Bwana; maana mfalme wa Israeli ametoka ili kutafuta uhai wangu, kama vile mtu awindavyo kware mlimani.Ndipo Sauli akasema, Nimekosa; rudi, Daudi, mwanangu; maana sitakudhuru tena, kwa kuwa maisha yangu yalikuwa na thamani machoni pako leo; angalia, nimetenda upumbavu, nimekosa sana.”     

13.   Mtu anayefikiria maovu na mwenye mizaha - Maandiko yanataja vitu kadhaa vinavyomchukiza Mungu, ikiwa ni pamoja na moyo uwazao mabaya, yaani maswala hayo ni machukizo kwa Mungu, maana yake kule kufikiri na kuwaza namna ya kufanya maovu, ni kufikiri na kufanya dhambi hayo yanawekwa katika kundi moja la machukizo kwa Mungu, ambayo kimsingi nayo yanaitwa upumbavu katika maandiko kwa sababu moyoni ndiko chanzo cha kila kitu kibaya kwa hiyo kufikiri au kuwaza maovu ni kuwaza upumbavu na zaidi sana ikiwa ni pamoja na mizaha, kwa hiyo kila mmoja wetu ajichunge fikira zake na kujihadhari za mizaha.  

Mithali 6:16-19 “Kuna vitu sita anavyovichukia Bwana; Naam, viko saba vilivyo chukizo kwake. Macho ya kiburi, ulimi wa uongo, Na mikono imwagayo damu isiyo na hatia; Moyo uwazao mawazo mabaya; Miguu iliyo myepesi kukimbilia maovu;Shahidi wa uongo asemaye uongo; Naye apandaye mbegu za fitina kati ya ndugu.”

Mithali 24:9 “Fikira za mpumbavu ni dhambi, Na mwenye mzaha huwachukiza watu.”

14.   Mtu anayelipa maovu badala ya mema – kwa maana nyingine ni watu wasio na shukurani, wako watu ambao unaweza kuwatendea mema na kisha ukahitaji fadhili ndogo tu kutoka kwao lakini wakakulipa mabaya badala ya mema mfano wa aina hii ya upumbavu ndio uliofanywa na mtu mwenye kuitwa nabali ambayo ndio tafasiri ya somo hili Nabali maana yake mpumbavu ambaye alioa mwanamke muungwana au mwenye akili.

1Samuel 25:2-26 “Na huko Maoni kulikuwa na mtu mmoja, ambaye alikuwa na mali yake katika Karmeli; naye yule mtu alikuwa mkuu sana, mwenye kondoo elfu tatu na mbuzi elfu; naye alikuwa akiwakata manyoya kondoo zake huko Karmeli. Na jina la mtu huyo aliitwa Nabali; na jina la mkewe aliitwa Abigaili, na huyo mwanamke alikuwa mwenye akili njema, mzuri wa uso; bali yule mwanamume alikuwa hana adabu, tena mwovu katika matendo yake; naye alikuwa wa mbari ya Kalebu. Basi Daudi akasikia huko nyikani ya kuwa Nabali alikuwa katika kuwakata manyoya kondoo zake. Daudi akatuma vijana kumi, Daudi naye akawaambia hao vijana, Kweeni mwende Karmeli, na kumwendea huyu Nabali ili mnisalimie; na hivi ndivyo mtakavyomwambia huyu aishiye salama, Amani na iwe kwako, na amani nyumbani mwako, na amani kwao wote ulio nao. Nami sasa nimesikia ya kuwa una watu wanaokata manyoya kondoo zako; haya! Wachungaji wako wamekuwa pamoja nasi, wala hatukuwadhuru, wala hawakukosa kitu wakati wote walipokuwako huko Karmeli. Waulize vijana wako, nao watakuambia; basi na wakubaliwe vijana hawa machoni pako; maana tumekujia katika siku ya heri; uwape, nakusihi, cho chote kitakachokujia mkononi, uwape watumwa wako na mwanao Daudi. Basi walipofika vijana wake Daudi, wakamwambia Nabali sawasawa na maneno hayo yote kwa jina la Daudi, kisha wakanyamaza. Naye Nabali akawajibu wale watumishi wa Daudi, akasema, Huyu Daudi ni nani? Na mwana wa Yese ni nani? Siku hizi kuna watumwa wengi wanaomtoroka kila mtu bwana wake! Basi mimi je! Nitwae mkate wangu, na maji yangu, na machinjo yangu niliyowachinjia hao watu wangu wakatao manyoya kondoo zangu, na kuwapa watu ambao siwajui wametoka wapi? Basi vijana wake Daudi wakageuka, wakaenda zao, wakarudi, nao wakaja wakamwambia sawasawa na maneno hayo yote. Kisha Daudi akawaambia watu wake, Haya! Jifungeni kila mtu upanga wake. Nao wakajifunga kila mtu upanga wake; Daudi naye akajifunga upanga wake; nao wakapanda nyuma yake Daudi, wapata kama watu mia nne; na watu mia mbili wakakaa na vyombo vyao.Lakini kijana mmojawapo alimpasha habari Abigaili, mkewe Nabali, kasema, Tazama, Daudi alituma wajumbe kutoka nyikani waje ili kumsalimu bwana wetu, naye akawatukana. Walakini watu hawa walitutendea mema sana, wala hatukupata dhara, wala sisi hatukupotewa na kitu cho chote, wakati wote tulipofuatana nao, tulipokuwako mavueni; watu hao walikuwa boma kwetu usiku na mchana, wakati wote tulipokuwa nao tukiwachunga kondoo. Basi sasa ujue na kufikiri utakayotenda; kwa sababu yamekusudiwa mabaya juu ya bwana wetu, na juu ya nyumba yake yote; kwa kuwa yeye ni mtu asiyefaa kabisa, hata mtu hawezi kusema naye. Ndipo Abigaili akafanya haraka, akatwaa mikate mia mbili, na viriba viwili vya divai, na kondoo watano waliofanyizwa tayari, na vipimo vitano vya bisi, na vishada mia vya zabibu, na mikate ya tini mia mbili; akavipakia vitu hivi juu ya punda. Akawaambia vijana wake, Haya! Tangulieni mbele yangu; angalieni, mimi nawafuata. Ila hakumwambia mumewe, Nabali. Ikawa, alipokuwa amepanda punda wake, na kutelemka penye sitara ya mlima, tazama, Daudi na watu wake walikuwa wakishuka kumkabili; naye akawakuta. Basi Daudi alikuwa amesema, Hakika ni bure nilivyokuwa nikilinda nyikani yote aliyo nayo mtu huyu, asipotewe na kitu cho chote cha mali yake yote; naye amenilipa mabaya badala ya mema. Mungu naye awafanyie hivyo adui za Daudi, na kuzidi, nikimwachia katika wote walio wake hata mtoto mume mmoja, kutakapopambazuka asubuhi. Ndipo hapo Abigaili alipomwona Daudi, alifanya haraka kushuka juu ya punda wake, akamwangukia Daudi kifulifuli, akainama mpaka nchi. Akamwangukia miguuni pake, akasema, Juu yangu, bwana wangu, juu yangu mimi na uwe uovu; tafadhali mjakazi wako na anene masikioni mwako, nawe uyasikilize maneno ya mjakazi wako. Nakusihi, bwana wangu, wewe usimwangalie huyu mtu asiyefaa, yaani, Nabali; kwa maana kama lilivyo jina lake ndivyo alivyo yeye; jina lake ndilo Nabali, na upumbavu anao; lakini mimi, mjakazi wako, sikuwaona hao vijana wa bwana wangu aliowatuma. Basi sasa, bwana wangu, aishivyo Bwana, na iishivyo nafsi yako, kwa kuwa Bwana amekuzuia usimwage damu, tena usijilipize kisasi mkono wako mwenyewe, basi sasa adui zako, na hao wamtakiao bwana wangu mabaya, wawe kama Nabali.

15.   Mwanamke asiye na hekima – Biblia aidha pia ina maonyo mengi kuhusu mwanamke mcha Mungu, na mwenye hekima kuwa ni mwanamke anayeweza kusimamia nyumba yake vizuri, na maandiko yanaonyesha kuwa kama mwanamke hamchi Mungu nyumba yake haiwezi kusimama mwanamke asiye mcha Mungu anaweza kuhesabika kama mkaidi, asiyetaka kumtii Mumewe, hafundishiki, mbishi, mbinafsi, anayetawala nyumba, mchoyo kwa tendo la ndoa na anayeamua kumkomoa mumewe kwa tendo hilo, mvivu wa ibada, hajishushi, mumewe akipanda naye anapanda juu zaidi, anayependa usingizi, Mmbeya, hafanyi kazi kwa mikono yake mwenyewe, na majukumu ya mke anayapuuzia na kupenda starehe nyingine utaongezea mwenyewe mwanamke wa aina hiyo ndiye anayefikiriwa kuwa hana hekima na hivyo maandiko yanamuita mpumbavu.

Mithali 14:1-2 “Kila mwanamke aliye na hekima hujenga nyumba yake; Bali aliye mpumbavu huibomoa kwa mikono yake mwenyewe. Yeye aendaye kwa unyofu wake humcha Bwana; Bali aliye mkaidi katika njia zake humdharau.

Mithali 9:13-17 “Mwanamke mpumbavu hupiga kelele, Ni mjinga, hajui kitu.Hukaa mlangoni pa nyumba yake, Juu ya kiti mahali pa mjini palipoinuka, Apate kuwaita wapitao njiani, Waendao moja kwa moja katika njia zao. Kila aliye mjinga na aingie humu. Tena amwambia mtu aliyepungukiwa na akili, Maji yaliyoibiwa ni matamu, Na mkate ulioliwa kwa siri hupendeza.”

Mithali 21:9 “Ni afadhali kukaa katika pembe ya darini, Kuliko katika nyumba pana pamoja na mwanamke mgomvi.”

               

Mithali 21:19 “Ni afadhali kukaa katika nchi ya nyika; Kuliko na mwanamke mgomvi, mchokozi.”

               

Mithali 25:24 “Ni afadhali kukaa katika pembe ya darini, Kuliko katika nyumba pana pamoja na mwanamke mgomvi.

16.   Kutokumjua Mungu wala njia zake  Watu wanaweza kuwa na maarifa ya aina nyingine mfano maarifa ya kupanga ubaya, kufanya maovu, kutekeleza majungu, kuharibu mahusiano, lakini hawana maarifa wala akili ya kumtafuta Mungu, ziko nguvu za uovu ambazo watu wanazifanya ambazo kama zingeelekezwa katika kumtafuta Mungu na kuongeza maarifa ya kumjua Mungu watu wangekuwa mbali sana

Yeremia 4:22 “Kwa maana watu wangu ni wapumbavu, hawanijui; ni watoto waliopungukiwa na akili, wala hawana ufahamu; ni wenye akili katika kutenda mabaya, bali katika kutenda mema hawana maarifa.”

17.   Wanaoamini Manabii wa uongo – Wako manabii ambao kazi yao kubwa ni kuzungumza maneno ya kufariji watu, ilihali wakati mwingine suluhu ya uponyaji wa watu hao ni kuwaambia tu watubu dhambi zao, ziko changamoto nyingi sana duniani zinazosababishwa na dhambi kuliko hata wachawi na laana za ukoo, wakati mwingine mtu akisamehewa dhambi zake na uponyaji wake unakuja kama neno lake lisemavyo, akusamehe maovu yako yote, akuponya magonjwa yako yote, waambie watu kosa lao badala ya kuona maono ya ubatili na upumbavu, manabii wa uongo huona maono ya kipumbavu na hivyo kuzuia kuponywa kwako.

Maombolezo 2:13-14 “Nikushuhudie nini? Nikufananishe na nini, Ee Binti Yerusalemu? Nikusawazishe na nini, nipate kukufariji, Ee bikira binti Sayuni? Kwa maana uvunjifu wako ni mkuu kama bahari, Ni nani awezaye kukuponya? Manabii wako wameona maono kwa ajili yako Ya ubatili na upumbavu Wala hawakufunua uovu wako, Wapate kurudisha kufungwa kwako; Bali wameona mabashiri ya ubatili kwa ajili yako Na sababu za kuhamishwa.                

18.   Kutokulifanyia kazi neno la Mungu – kama watu wengi tungekuwa tunalitii neno la Mungu tungekuwa na mafanikio makubwa sana na ustawi mkubwa sana katika maswala yote ya mwili na roho lakini kwa bahati mbaya sana kulitii neno la Mungu limekuwa jambo gumu kwa kizazi hiki hata kama watu wanatii wengi huchagua maswala kadhaa ya kuyatii lakini neno la Mungu linatukumbusha kuyatii maagizo yote na kuyafanyia kazi maneno ya Mungu.

Yakobo 1:22-24 “Lakini iweni watendaji wa neno, wala si wasikiaji tu, hali mkijidanganya nafsi zenu.Kwa sababu mtu akiwa ni msikiaji wa neno tu, wala si mtendaji, mtu huyo ni kama mtu anayejiangalia uso wake katika kioo. Maana hujiangalia, kisha huenda zake, mara akasahau jinsi alivyo.

Mathayo 7:24-27 “Basi kila asikiaye hayo maneno yangu, na kuyafanya, atafananishwa na mtu mwenye akili, aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba; mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, isianguke; kwa maana misingi yake imewekwa juu ya mwamba. Na kila asikiaye hayo maneno yangu asiyafanye, atafananishwa na mtu mpumbavu, aliyejenga nyumba yake juu ya mchanga; mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, ikaanguka; nalo anguko lake likawa kubwa.”

19.   Kujilinganisha na wengine – Katika maisha haya Mungu amemuumba kila mwanadamu akiwa na baraka tofauti na karama na vipawa tofauti, kwa hiyo kimaandiko mwanadamua anyejilinganisha na mwingine au kuipima nafsi yake akiilinganisha nay a mtu mwingine mtu huyo hana akili na ni mpumbavu, kwa mujibu wa maandiko, hatupaswi kamwe kujilinganisha na wengine kwa sababu kila mwanadamu Mungu amemuumba kwa namna na jinsi ya aina yake kwa uhodari mkubwa!

2Wakorintho 10:11-18 “Mtu kama huyo na afikiri hivi, ya kwamba jinsi tulivyo kwa maneno katika nyaraka tusipokuwapo, ndivyo tulivyo kwa matendo tukiwapo. Kwa kuwa hatuthubutu kujihesabu pamoja na baadhi yao wanaojisifu wenyewe, wala kujilinganisha nao; bali wao wenyewe wakijipima nafsi zao na nafsi zao, na wakijilinganisha nafsi zao na nafsi zao, hawana akili. Lakini sisi hatutajisifu zaidi ya kadiri yetu; bali kwa kadiri ya kipimo tulichopimiwa na Mungu, yaani, kadiri ya kufika hata kwenu. Maana hatujitanui nafsi zetu kupita kadiri yetu, kana kwamba hatuwafikii ninyi; kwa sababu tulitangulia kufika mpaka kwenu katika injili ya Kristo; wala hatujisifu zaidi ya kadiri yetu, yaani, katika taabu za watu wengine; bali tukiwa na tumaini ya kwamba, imani yenu ikuapo, tutakuzwa kwenu kwa kadiri ya kipimo chetu, na kupata ziada; hata kuihubiri Injili katika nchi zilizo mbele kupita nchi zenu; tusijisifu katika kipimo cha mtu mwingine kwa mambo yaliyokwisha kutengenezwa. Lakini, Yeye ajisifuye, na ajisifu katika Bwana. Maana mtu mwenye kukubaliwa si yeye ajisifuye, bali yeye asifiwaye na Bwana.”

20.   Kutokujitayarisha kwa Mungu -  watu wote duniani wanapaswa kujiandaa kwaajili ya kukutana na Mungu, na kujiandaa kwaajili ya ujio wa Bwana wetu Yesu Kristo mara ya pili duniani, na kunyakuliwa kwa kanisa, kuishi maisha ya vuguvugu na kujidanganya kunaweza kuja kutuletea majuto na kilio na kusaga meno, Yesu mara kadhaa alisisitiza jamii kujiandaa kwaajili ya Mungu na awaye yote ambaye atakosa mbingu atakuwa amekosa kwaajili ya upumbavu, Bwana amtunze kila mmoja wetu asiikose mbingu katika jina la Yesu Kristo.

Luka 12:16-21 “Akawaambia mithali, akisema, Shamba la mtu mmoja tajiri lilikuwa limezaa sana; akaanza kuwaza moyoni mwake, akisema, Nifanyeje? Maana sina pa kuyaweka akiba mavuno yangu.  Akasema, Nitafanya hivi; nitazivunja ghala zangu, nijenge nyingine kubwa zaidi, na humo nitaweka nafaka yangu yote na vitu vyangu. Kisha, nitajiambia, Ee nafsi yangu, una vitu vyema vingi ulivyojiwekea akiba kwa miaka mingi; pumzika basi, ule, unywe, ufurahi. Lakini Mungu akamwambia, Mpumbavu wewe, usiku huu wa leo wanataka roho yako! Na vitu ulivyojiwekea tayari vitakuwa vya nani? Ndivyo alivyo mtu ajiwekeaye nafsi yake akiba, asijitajirishe kwa Mungu.

Mathayo 25:1-13 “Ndipo ufalme wa mbinguni utakapofanana na wanawali kumi, waliotwaa taa zao, wakatoka kwenda kumlaki bwana arusi. Watano wao walikuwa wapumbavu, na watano wenye busara. Wale waliokuwa wapumbavu walizitwaa taa zao, wasitwae na mafuta pamoja nao; bali wale wenye busara walitwaa mafuta katika vyombo vyao pamoja na taa zao. Hata bwana arusi alipokawia, wote wakasinzia wakalala usingizi. Lakini usiku wa manane, pakawa na kelele, Haya, bwana arusi; tokeni mwende kumlaki. Mara wakaondoka wanawali wale wote, wakazitengeneza taa zao. Wale wapumbavu wakawaambia wenye busara, Tupeni mafuta yenu kidogo; maana taa zetu zinazimika. Lakini wale wenye busara wakawajibu, wakisema, Sivyo; hayatatutosha sisi na ninyi; afadhali shikeni njia mwende kwa wauzao, mkajinunulie.Na hao walipokuwa wakienda kununua, bwana arusi akaja, nao waliokuwa tayari wakaingia pamoja naye arusini; mlango ukafungwa.Halafu wakaja na wale wanawali wengine, wakasema, Bwana, Bwana, utufungulie. Akajibu akasema, Amin, nawaambia, siwajui ninyi. Basi kesheni, kwa sababu hamwijui siku wala saa.

Chagua Hekima!

Tungeweza kuchambua maswala mengi sana yanayozungumzia upumbavu lakini muda usingelitosha, ni ukweli ulio wazi ya kuwa maandiko yanatuonyesha wazi kuwa upumbavu ni tatizo na janga zito sana kuliko hata dhambi zenyewe, kwani hakuna dhambi ambayo utaifanya na isiwe kuwa hukufanya upumbavu, ziko tabia mbaya nyingi sana ambazo mtu akizitenda kimaandiko anaitwa amefanya upumbavu, swali kubwa la kujiuliza Je wewe nawe utakuwa kama mmoja wa wapumbavu? Kama hutaki neno la Mungu linatushauri kuchagua hekima na hii ndio namna ya kuchagua hekima.

a.       Hekima ya kweli inapatikana kwa kumcha Mungu – Mithali 1:7 “Kumcha Bwana ni chanzo cha maarifa, Bali wapumbavu hudharau hekima na adabu”.

b.      Uko umuhimu wa kumuomba Mungu hekima – Yakobo 1:5-6  Lakini mtu wa kwenu akipungukiwa na hekima, na aombe dua kwa Mungu, awapaye wote, kwa ukarimu, wala hakemei; naye atapewa.Ila na aombe kwa imani, pasipo shaka yo yote; maana mwenye shaka ni kama wimbi la bahari lililochukuliwa na upepo, na kupeperushwa huku na huku.”

2Nyakati 1:7-12 “Usiku ule Mungu akamtokea Sulemani, akamwambia, Omba utakalo nikupe. Sulemani akamwambia Mungu, Umemfanyia baba yangu Daudi fadhili kuu, nawe umenimilikisha mimi badala yake. Basi sasa, Ee Bwana Mungu, na limyakinie baba yangu Daudi neno lako; maana umenitawaza niwe mfalme juu ya watu wengi kama mavumbi ya nchi. Basi sasa nipe hekima na maarifa, nijue kutoka na kuingia mbele ya watu hawa; kwa kuwa ni nani awezaye kuwahukumu watu wako hawa walio wengi? Naye Mungu akamwambia Sulemani, Kwa sababu neno hili lilikuwamo moyoni mwako, wala hukujitakia mali, wala utajiri, wala utukufu, wala maisha za wakuchukiao, wala hukujitakia maisha ya siku nyingi; bali umejitakia hekima na maarifa, upate kuwahukumu watu wangu, niliokutawaza juu yao; basi hekima na maarifa umepewa; nami nitakupa mali, na utajiri, na utukufu, kupita walivyokuwa navyo wafalme wote waliokuwa kabla yako, wala baada yako hapatakuwa na mtu atakayekuwa navyo.  

c.       Hekima ni ulinzi – ukiwa na hekima hakuna kitu kitaharibika kila kitu kitarahisishwa kama vile fedha ilivyo ulinzi hekima itatuhifadhi zaidi kuliko fedha, tutapunguza kuharibikiwa endapo tutachagua hekima, Hekima ni njema hekima ni bora.

 

Muhubiri 7:11-12 “Hekima ni njema, mfano wa urithi; Naam, nayo ni bora kwao walionao jua. Kwa maana hekima ni ulinzi, kama vile fedha ilivyo ulinzi; na ubora wa maarifa ni ya kwamba hekima humhifadhi yeye aliye nayo.”                

d.      Chagua Hekima – Mithali 8:4-11 “Enyi watu, nawaita ninyi; Na sauti yangu ni kwa wanadamu.Enyi wajinga, fahamuni werevu, Nanyi wapumbavu, mpate moyo wa kufahamu. Sikieni, maana nitasema yaliyo mazuri, Na kufumbua midomo yangu kutakuwa maadili. Maana kinywa changu kitasema kweli, Na uovu ni chukizo kwa midomo yangu. Maneno yote ya kinywa changu yana haki; Hapana hata neno lililopotoka au la ukaidi. Yote humwelea yule afahamuye, Yote huelekea mbele yao waliopata maarifa.Pokea mafundisho yangu, wala si fedha, Na maarifa kuliko dhahabu safi. Maana hekima ni bora kuliko marijani; Wala vyote vinavyotamanika havilingani nayo.”

Ni muhimu kujikumbusha tena ya kuwa kukosa hekima ni gharama kubwa sana, kwani kinyume cha kukosa hekima ni kuwa mpumbavu, kila unachokiona duniani hakiendi vizuri ni kwa sababu watu walifanya upumbavu, upumbavu ni gharama kubwa sana na umewagharimu wengi, majuto makubwa sana duniani yamechangiwa na upumbavu uliofanywa na watu, sisi kama watu wa Mungu tunapaswa kumuomba Mungu atupe akili, atupe hekima ili tusifanye upumbavu, ambao unaweza kuja kuyagharimu maisha yetu na maisha ya wengine, maandiko yanatutaka tutembee na wenye hekima nasi tutakuwa na hiyo hekima.

Mithali 13:20 “Enenda pamoja na wenye hekima, nawe utakuwa na hekima; Bali rafiki wa wapumbavu ataumia.”

Ni mwenye hekima gani ambaye unaweza kuambatana naye au kwenda naye naye atakuambukiza hekima? Kwa kawaida wenye hekima pia huishi maisha matakatifu na ni nani aliye mtakatifu ni Yesu Kristo ambaye yeye anaitwa Hekima yetu yeye ni mkuu kuliko Suleimani na ana hekima kuliko Sulemani.

1Wakorintho 1:20-24 “Yu wapi mwenye hekima? Yu wapi mwandishi? Yu wapi mlete hoja wa zamani hizi? Je! Mungu hakuifanya hekima ya dunia kuwa ni upumbavu? Kwa maana katika hekima ya Mungu, dunia isipopata kumjua Mungu kwa hekima yake, Mungu alipenda kuwaokoa waaminio kwa upuzi wa lile neno linalohubiriwa. Kwa sababu Wayahudi wanataka ishara, na Wayunani wanatafuta hekima;bali sisi tunamhubiri Kristo, aliyesulibiwa; kwa Wayahudi ni kikwazo, na kwa Wayunani ni upuzi; bali kwao waitwao, Wayahudi kwa Wayunani, ni Kristo, nguvu ya Mungu, na hekima ya Mungu.

Mathayo 12:41-42 “Watu wa Ninawi watasimama siku ya hukumu pamoja na watu wa kizazi hiki, nao watawahukumu kuwa wamekosa; kwa sababu wao walitubu kwa mahubiri ya Yona; na hapa yupo aliye mkuu kuliko Yona. Malkia wa kusini atasimama siku ya hukumu pamoja na watu wa kizazi hiki, naye atawahukumu kuwa wamekosa; kwa sababu yeye alikuja kutoka pande za mwisho za dunia ili asikie hekima ya Sulemani, na hapa yupo aliye mkuu kuliko Sulemani.”

Kwa kuwa Yesu ndiye hekima yetu natoa ushauri kama maandiko yasemavyo, mpokee Yesu aliye hekima yetu ili kwamba uweze kuishi maisha ya neema na kujifunza kuwa kama yeye na kuishi maisha yasiyo na majuto chagua hekima mchague Yesu.Kumchagua Yesu ni Kuchagua hekima, na kuishi sawa na neno la Mungu ni kufuata njia ya Hekima, Bwana ampe neema kila mmoja wetu kuishi na kuenenda kwa hekima katika jina la Yesu Kristo ameen.  

Rev. Innocent Samuel Kamote.

Mkuu wa wajenzi mwenye hekima.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni