Jumatano, 23 Oktoba 2024

Hapa yupo aliyemkuu kuliko Hekalu!


Mathayo 12:3-6 “Akawaambia, Hamkusoma alivyotenda Daudi, alipokuwa na njaa, yeye na wenziwe? jinsi alivyoingia katika nyumba ya Mungu, akaila mikate ile ya wonyesho, ambayo si halali kwake kuila wala kwa wale wenziwe, ila kwa makuhani peke yao? Wala hamkusoma katika torati, kwamba siku ya sabato makuhani hekaluni huinajisi sabato wasipate hatia? Lakini nawaambieni, kwamba hapa yupo aliye mkuu kuliko hekalu.”



Utangulizi:

Nyakati za agano la kale Hekalu la Mungu lilichukua nafasi muhimu  na kubwa sana katika maisha ya wanadamu hususani Wayahudi, katika uhusiano wao na Mungu, Hekalu ilikuwa ni nyumba pekee ambayo ilikuweko Yerusalem ambapo watu wangeweza kuabudu, kutoa dhabihu na kukutana na Mungu, Lakini katika namna ya kushangaza sana Yesu Kristo kwa maneno na vitendo alitangaza wazi kuwa yeye ni mkuu kuliko Hekalu!, Leo tutachukua muda kujifunza kwa kina na mapana na marefu kwa vipi Yesu ni mkuu kuliko Hekalu na hii ina maana gani kwa sisi kama wakristo!,Usemi huu sio tu kuwa una mapinduzi makubwa ya kiibada lakini una kitu cha maana sana cha kujifunza kuhusu Yesu Kristo, Tutajifunza somo hili Hapa yupo aliyemkuu kuliko Hekalu! Kwa kuzingatia vipengele vitatu muhimu vifuatavyo:-

·         Umuhimu wa Hekalu katika jamii ya Wayahudi

·         Hapa yupo aliyemkuu kuliko Hekalu

·         Mambo ya msingi ya kujifunza katika kanisa


Umuhimu wa Hekalu katika jamii ya Wayahudi.

Neno Hekalu kwa kiingereza “temple” katika kiibrania linatumika neno HEKHAL au BAYITH kwa kiyunani HIERON ambalo kimsingi ndio lilikuwa jina la Jumba la kifahari lililojengwa Pale Yerusalem kwaajili ya Ibada za Mungu wa Israel. Yako mahekalu mengine mengi duniani yaliyokuwa yamejengwa kwa miungu mingine, Lakini hekalu maarufu zaidi lilikuwa hekalu hili la Mungu wa Israel Lililojengwa na Mfalme Sulemani na hili ndilo tunalolizungumzia kwa kuunganisha na Neno la Yesu Kristo.

Wote tunafahamu kuwa Hekalu la Mungu kule Yerusalem lilikuwa ndio kiini kikubwa cha ibada za kiyahudi na lilishika sehemu kubwa sana ya maisha yao ya kiimani na kitamaduni, kwa wayahudi hekalu lilikuwa ni zaidi ya jengo la kawaida la kifahari, wao waliamini na ndivyo ilivyokuwa kwamba ni mahali ambapo Mungu alipachagua ili aweke jina lake hapo, hivyo palikuwa ni mahali akaapo Mungu pa kidunia, ambapo kwa mujibu wa torati iliwalazimu waende hapo, kwa kuwa ndipo alipopachagua Bwana Mungu wa Israel kama ilivyoagizwa mapema katika torati ya Musa.

Kumbukumbu 12:5-6 “Lakini mahali atakapochagua Bwana, Mungu wenu, katika kabila zenu zote, apaweke jina lake, maana, ni makao yake, elekezeni nyuso zenu hapo, nawe wende huko; pelekeni huko sadaka zenu za kuteketezwa, na dhabihu zenu, na zaka zenu, na sadaka ya kuinuliwa ya mikono yenu, na nadhiri zenu, na sadaka zenu za hiari, na wazaliwa wa kwanza wa makundi yenu ya ng'ombe na ya kondoo;”

Tofauti na masinagogi, Hekalu lilipaswa kuwa moja tu, tena Pale Yerusalem na ndipo mahali ambapo pekee pali ruhusiwa kutolewa dhabihu za kuteketezwa, kwaajili ya upatanisho wa dhambi, Hapo ndipo mahali ambapo Mungu alichagua kuwekeza uwepo wake mahali hapo, Palikuwa ni mahali patakatifu panapounganisha mbingu na inchi.

1Wafalme 8:10-13 “Ikawa, makuhani walipotoka katika patakatifu, nyumba ya Bwana ikajaa wingu; hata makuhani hawakuweza kusimama ili kufanya huduma yao, kwa sababu ya wingu lile; kwa kuwa nyumba ya Bwana ilikuwa imejaa utukufu wa Bwana.Ndipo Sulemani akanena, Bwana alisema ya kwamba atakaa katika giza nene. Hakika nimekujengea nyumba ya kukaa, iwe mahali pa makao yako milele.”

Hekaluni ndipo mahali ambapo dhabihu za kuteteketezwa na sadaka za upatanisho kwaajili ya dhambi zilifanyika, wakati ibada hizo zilikuwa haziwezi kufanyika popote wala kwenye masinagogi, kwa lugha nyingine Israel wasingeliweza kupata msamaha wa dhambi na kupatanishwa na Mungu pasipo kufanyika kwa ibada hizo hekaluni peke yake, kwa hiyo hekalu pekee lilikuwa lango la mbingu

Bwana Mungu wa Israel alikuwa amepakubali mahali pale na kutoa ahadi nyingi sana kuhusu Nyumba ya Bwana kwa watu wake, alipakubali kama mahali pa dhabihu, alipakubali pawe mahali pa makimbilio, alipakubali pawe mahali pa kupoza vita, mapigo na matukio yoyote magumu, na alipakubali pawe mahali ambapo mtu yeyote duniani akiomba lolote kuelekea hapo Mungu angesikia dua yake na kuponya kwa ujumla ni mahali muhimu sana kwa wote waliomuhitaji Mungu na wanaomuhitaji Mungu

2Nyakati 7:12-16 “Bwana akamtokea Sulemani usiku, akamwambia, Nimesikia uliyoyaomba, na mahali hapa nimejichagulia kuwa nyumba ya dhabihu. Nikizifunga mbingu isiwe mvua, tena nikiamuru nzige kula nchi, au nikiwapelekea watu wangu tauni; ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha njia zao mbaya; basi, nitasikia toka mbinguni, na kuwasamehe dhambi yao, na kuiponya nchi yao. Sasa macho yangu yatafumbuka, na masikio yangu yatasikiliza maombi ya watu waombao mahali hapa. Maana sasa nimeichagua nyumba hii na kuitakasa, ili kwamba jina langu lipate kuwako huko milele; yatakuwako na macho yangu, na moyo wangu daima.”

Kwa hiyo Hekalu lilikuwa ni sehemu muhimu ya Imani, Dini, tamaduni, utaifa na umoja wa wana wa Israel na wayahudi wote kutokana na mafundisho yao, kila wakati na kila mwaka zilikuwepo sikukuu muhimu sana ambazo ziliwakutanisha wayahudi pamoja kama hija zikiwapeleka Yerusalem na hivyo kuwa alama kubwa sana ya umoja wa kitaifa na kiimani, kitamaduni na kihistoria na sehemu muhimu ya utambulisho wa Mungu wa Israel kwa dunia nzima. Kuna maandiko mengi na zaburi nyingi zinazoonyesha umuhimu mkubwa wa nyumba hii ya Bwana na uweza na nguvu na mamlaka aliyokuwa ameiwekeza hapo kwa hiyo kwa ujumla:-

1.       Hekalu lilikuwa ni kiini cha Imani ya wayahudi wa kale na sehemu muhimu kwa ibada  ilikuwa ni mahali ambapo watu walilia na kupakumbuka sana walipokosa uhusiano na mahali hapo au walipokuwa mbali na mahali hapo

 

Zaburi 42:2-4 “Nafsi yangu inamwonea kiu MUNGU, Mungu aliye hai, Lini nitakapokuja nionekane mbele za Mungu? Machozi yangu yamekuwa chakula changu mchana na usiku, Pindi wanaponiambia mchana kutwa, Yuko wapi Mungu wako. Nayakumbuka hayo nikiweka wazi nafsi yangu ndani yangu, Jinsi nilivyokuwa nikienda na mkutano, Na kuwaongoza nyumbani kwa Mungu, Kwa sauti ya furaha na kusifu, mkutano wa sikukuu.”

 

Zaburi 137:1-5 “Kando ya mito ya Babeli ndiko tulikoketi, Tukalia tulipoikumbuka Sayuni. Katika miti iliyo katikati yake Tulivitundika vinubi vyetu. Maana huko waliotuchukua mateka Walitaka tuwaimbie; Na waliotuonea walitaka furaha; Tuimbieni baadhi ya nyimbo za Sayuni. Tuuimbeje wimbo wa Bwana Katika nchi ya ugeni? Ee Yerusalemu, nikikusahau wewe, Mkono wangu wa kuume na usahau.”

 

Zaburi 122:1-2 “Nalifurahi waliponiambia, Na twende nyumbani kwa Bwana. Miguu yetu imesimama Ndani ya malango yako, Ee Yerusalemu.”              

 

2.       Palikuwa ni mahali ambapo waliweza kutoa dhabihu, kuondoa au kuweka nadhiri kumuita Mungu na kupokea fadhili za Mungu

 

Zaburi 66:13-20 “Nitaingia nyumbani mwako na kafara; Nitaondoa kwako nadhiri zangu; Ambazo midomo yangu ilizinena; Kinywa changu kikazisema nilipokuwa taabuni. Kafara za vinono nitakutolea, Pamoja na fukizo la kondoo waume, Nitatoa ng'ombe pamoja na mbuzi. Njoni, sikieni, ninyi nyote mnaomcha Mungu, Nami nitayatangaza aliyonitendea roho yangu. Nalimwita kwa kinywa changu, Na sifa kuu zilikuwa chini ya ulimi wangu. Kama ningaliwaza maovu moyoni mwangu, Bwana asingesikia. Hakika Mungu amesikia; Ameisikiliza sauti ya maombi yangu. Na ahimidiwe Mungu asiyeyakataa maombi yangu, Wala kuniondolea fadhili zake.”

 

3.       Hekalu palikuwa ni mahali ambapo kila mtu wa Mungu nyakati za agano la kale alipaonea shauku au alipaonea hamu

 

Zaburi 23:6 “Hakika wema na fadhili zitanifuata Siku zote za maisha yangu; Nami nitakaa nyumbani mwa Bwana milele.”

 

Zaburi 27:4-5 “Neno Moja nimelitaka kwa Bwana, Nalo ndilo nitakalolitafuta, Nikae nyumbani mwa Bwana Siku zote za maisha yangu, Niutazame uzuri wa Bwana, Na kutafakari hekaluni mwake. Mradi atanisitiri bandani mwake siku ya mabaya, Atanisitiri katika sitara ya hema yake, Na kuniinua juu ya mwamba.”

 

Zaburi 122:1-2 “Nalifurahi waliponiambia, Na twende nyumbani kwa Bwana. Miguu yetu imesimama Ndani ya malango yako, Ee Yerusalemu.”

 

4.       Palikuwa ni mahali ambapo Israel walitembelea kila mwaka wakati wa sikukuu akiwepo Bwana Yesu mwenyewe alipokuwa kijana mdogo, na hii ilikuwa ni kwa mujibu wa maagizo ya torati ya Musa

 

Kumbukumbu 16:16-17 “Mara tatu kwa mwaka na watokee wanawaume wako wote mbele za Bwana, Mungu wako, mahali atakapochagua; katika sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu, na katika sikukuu ya majuma, na katika sikukuu ya vibanda; wala wasitokee mbele za Bwana mikono mitupu. Kila mtu na atoe kama awezavyo, kwa kadiri ya baraka ya Bwana, Mungu wako, alivyokupa.”

 

Matendo 2:5-11 “Na walikuwako Yerusalemu Wayahudi wakikaa, watu watauwa, watu wa kila taifa chini ya mbingu. Basi sauti hii iliposikiwa makutano walikutanika, wakashikwa na fadhaa, kwa kuwa kila mmoja aliwasikia wakisema kwa lugha yake mwenyewe. Wakashangaa wote, wakastaajabu wakiambiana, Tazama, hawa wote wasemao si Wagalilaya? Imekuwaje basi sisi kusikia kila mtu lugha yetu tuliyozaliwa nayo? Warparthi na Wamedi na Waelami, nao wakaao Mesopotamia, Uyahudi na Kapadokia, Ponto na Asia, Frigia na Pamfilia, Misri na pande za Libia karibu na Kirene, na wageni watokao Rumi, Wayahudi na waongofu, Wakrete na Waarabu; tunawasikia hawa wakisema kwa lugha zetu matendo makuu ya Mungu.”

 

Luka 2:41-51 “Basi, wazee wake huenda Yerusalemu kila mwaka, wakati wa sikukuu ya Pasaka. Na alipopata umri wake miaka kumi na miwili, walipanda kama ilivyokuwa desturi ya sikukuu; na walipokwisha kuzitimiza siku, wakati wa kurudi kwao, yule mtoto Yesu alibaki nyuma huko Yerusalemu, na wazee wake walikuwa hawana habari. Nao wakadhani ya kuwa yumo katika msafara; wakaenenda mwendo wa kutwa, wakawa wakimtafuta katika jamaa zao na wenzao; na walipomkosa, wakarejea Yerusalemu, huku wakimtafuta. Ikawa baada ya siku tatu wakamwona hekaluni, ameketi katikati ya waalimu, akiwasikiliza na kuwauliza maswali. Nao wote waliomsikia walistaajabia fahamu zake na majibu yake. Na walipomwona walishangaa, na mama yake akamwambia, Mwanangu, mbona umetutenda hivi? Tazama, baba yako na mimi tulikuwa tukikutafuta kwa huzuni. Akawaambia, Kwani kunitafuta? Hamkujua ya kuwa imenipasa kuwamo katika nyumba ya Baba yangu? Nao hawakuelewa na neno hilo alilowaambia. Akashuka pamoja nao mpaka Nazareti, naye alikuwa akiwatii; na mamaye aliyaweka hayo yote moyoni mwake.”

 

5.       Palikuwa ni mahali maalumu kwaajili ya maombi na ibada kwa wayahudi wote kokote waliko au sehemu maalumu ya muelekeo wa maombi (Prayer direction)

 

Isaya 56:5-7 “Nitawapa hawa nyumbani mwangu, na ndani ya kuta zangu, kumbukumbu na jina, lililo jema kuliko kuwa na wana na binti; nitawapa jina lidumulo milele, lisilokatiliwa mbali. Na wageni, walioandamana na Bwana ili wamhudumu, na kulipenda jina la Bwana, kuwa watumishi wake; kila aishikaye sabato asiivunje, na kulishika sana agano langu; Nitawaleta hao nao hata mlima wangu mtakatifu, na kuwafurahisha katika nyumba yangu ya sala; makafara yao na dhabihu zao zitakubaliwa juu ya madhabahu zangu; kwa maana nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala kwa mataifa yote.”        

 

Daniel 6:10 -11 “Hata Danieli, alipojua ya kuwa yale maandiko yamekwisha kutiwa sahihi, akaingia nyumbani mwake, (na madirisha katika chumba chake yalikuwa yamefunguliwa kukabili Yerusalemu;) akapiga magoti mara tatu kila siku, akasali, akashukuru mbele za Mungu wake, kama alivyokuwa akifanya tokea hapo. Basi watu hao wakakusanyika pamoja, wakamwona Danieli akiomba dua, na kusihi mbele za Mungu wake.”

 

6.       Palikuwa ni Mahali ambapo utukufu wa Mungu ulikaa – tangu nyakati za safari ya wana wa Israel Jangwani uwepo wa Mungu ulishuka katika nyumba ya Bwana iliyokuweko jangwani iliyojulikana kama Hema la kukutania, kimsingi Hema ya kukutania lilikuwa ni hekalu la muda linalohamishika na walipofika katika nchi ya kanaani Hekalu lilijengwa kwa mfano wa ile hema ya kukutania, uwepo huo wa Mungu ulionekana kwa jinsi ya macho ya kibinadamu kama wingu la utukufu ambalo kwa kiibrania lilitwa  Shekinah

 

Kutoka 33:9-10 “Ikawa Musa alipoingia humo hemani, ile nguzo ya wingu ikashuka, ikasimama mlangoni pa ile hema; naye BWANA akasema na Musa. Watu wote wakaiona nguzo ya wingu ikisimama penye mlango wa hema; watu wote wakaondoka wakasujudu, kila mtu mlangoni pa hema yake.”

 

Sio hivyo tu wakati mwingine malaika wa Bwana alijitokeza akijiunganisha na nguzo ile ya wingu, na malaika huyu wakati mwingine ilionekana wazi kuwa alimuwakilisha Bwana mwenyewe, na mara nyingi malaika huyu alijitokeza akiwa na mamlaka ya kiungu na Pengine alikuwa ni Yesu mwenyewe katika agano la kale

 

Kutoka 14:19 “Kisha malaika wa Mungu, aliyetangulia mbele ya jeshi la Israeli, akaondoka akaenda nyuma yao; na ile nguzo ya wingu ikaondoka hapo mbele yao, ikasimama nyuma yao;”

 

Wingu la utukufu wa Mungu wakati wote lilikuwa linawakilisha uwepo wa Mungu, Na ilikuwa ni shauku ya Mungu kuwa pamoja na watu wake, na uwepo huu ulijirudia kulikalia Hekalu lilipokuwa limejengwa na kuwekwa wakfu, aidha wakati mwingine ulionekana kama moto ulioshuka kutoka mbinguni na hii inaweza kutupa picha pana kuwa uko uwezekano kuwa kile kijiti alichokiona Musa kinawaka moto lakini hakiteketei ulikuwa ni uwepo huu wa Mungu na ule uliokaa usoni kwa Musa na kuufanya uso wake kung’aa

 

2Nyakati 7:1 “Basi Sulemani alipokwisha maombi hayo, moto ukashuka kutoka mbinguni, ukateketeza sadaka ya kuteketezwa na dhabihu; utukufu wa Bwana ukaijaza nyumba. Wala makuhani hawakuweza kuingia nyumbani mwa Bwana, kwa kuwa utukufu wa Bwana umeijaza nyumba ya Bwana.”             

 

Kimsingi uwepo huu wa Mungu uliokuwa ukionekana na kukaa katika hekalu na hema ya kukutania alikuwa ni Mungu mwenyewe,  nahii iko wazi kwa mujibu wa injili ya Yohana kuwa kumuona Yesu ni kuuona utukufu wa Mungu, Kristo anatafasiriwa kuwa ndiye mng’ao huo wa utukufu wa Mungu ndiye Shekinah mwenyewe, ambaye hakalu halina maana bila uwepo wake.

 

Yohana 1:14 “Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli.”      

 

Waebrania 1:1-3 “Mungu, ambaye alisema zamani na baba zetu katika manabii kwa sehemu nyingi na kwa njia nyingi, mwisho wa siku hizi amesema na sisi katika Mwana, aliyemweka kuwa mrithi wa yote, tena kwa yeye aliufanya ulimwengu. Yeye kwa kuwa ni mng'ao wa utukufu wake na chapa ya nafsi yake, akivichukua vyote kwa amri ya uweza wake, akiisha kufanya utakaso wa dhambi, aliketi mkono wa kuume wa Ukuu huko juu;”

                               

Nyumba hii ya Mungu ilikuwa ni ya Muhimu sana, na ilijengwa katika mlima wa Moriah mahali ambapo Inasadikiwa kuwa Ibrahimu alitaka kumtoa Isaka kama sadaka ya kuteketezwa, mahali ambapo Mfalme Daudi alipanunua lilipokuwa Shamba la Arauna Myebusi, ili aweze kutoa dhabihu hapo na kumjengea Mungu madhabahu, kihistoria Hekalu lilijengwa mara tatu La kwanza likiwa limejengwa na Suleimani, na baadaye Zerubabel na mwisho Herode mkuu alilikarabati na kulijenga kwaajili ya wayahudi na hili ndilo Hekalu ambalo Yesu alilitumia na baada ya kupoteza umuhimu wake na kuharibiwa ndipo mahali ambapo sasa inasimama nyumba ya kiislamu iitwayo Masjid Al - Aqsa  ambayo iko chini ya utawala wa Hashemites au Bani Hashem ukoo ambao ni uzao wa waarabu wanaotokana na ukoo wa Makuresh moja ya kabila za wana wa Ishmel  mwana wa Ibrahimu, ambapo ndio ufalme wa Jordan leo. Yako mambo mengi sana ambayo tungeweza kuzungumza kuhusu hekalu lakini natamani kumzungumzia Yeye aliye mkuu kuliko Hekalu lenyewe kwa sababu huyo ni wa Muhimu sana sasa kuliko hekalu halisi lililokuwako Yerusalem kwa wakati huo.

Hapa yupo aliyemkuu kuliko Hekalu 

Wote tunaweza kuona jinsi Hekalu lilivyokuwa ni nyumba muhimu sana kwa Wayahudi, na sasa Bwana wetu Yesu Kristo anapokuja na kukiri au kutangaza ya kuwa yeye ni Mkuu kuliko Hekalu maana yake anatamka kitu kikubwa sana cha kushangaza ambacho hatuna budi kutoa kipaumbele  na kuliangalia jambo hili kwa umakini mkubwa kwa sababu kwa tamko lake maana yake sheria zote na maswala yote ya msingi kuhusu Hekalu yanapoteza maana zake na mwelekeo mzima unaelekea kwake, wayahudi walikuwa wakifikiri kuwa hekalu ndilo lililokuwa linabeba uwepo wa Mungu kwa ukamilifu wake na sasa Yesu anaonyesha ya kuwa Uwepo ule wa Mungu sasa ni yeye mwenyewe.

1.       Hii ilikuwa na maana ya moja kwa moja kuwa Yesu ni Mungu – Hekalu ilikuwa ni mahali ambapo Mungu alipachagua kuweka jina lake hapo na uwepo wake ili aweze kuwa katikati ya watu au ili aweze kutimiza mpango wake wa kukaa pamoja na wanadamu yaani Mungu pamoja nasi.

 

Mathayo 1:21-23 “Naye atazaa mwana, nawe utamwita jina lake Yesu, maana, yeye ndiye atakayewaokoa watu wake na dhambi zao. Hayo yote yamekuwa, ili litimie neno lililonenwa na Bwana kwa ujumbe wa nabii akisema, Tazama, bikira atachukua mimba, Naye atazaa mwana; Nao watamwita jina lake Imanueli; Yaani, Mungu pamoja nasi.”

 

Hekalu lilikuwa linaufunga uwepo wa Mungu mahali pamoja lakini Yesu alikuwa akiufungua uwepo wa Mungu kwa ulimwengu mzima, yeye ni uwepo halisi wa Mungu na ndiye neno halisi la Mungu, watu walikuwa wakienda Hekaluni kumuabudu yeye na sasa kama yeye mwenyewe yupo maana yake uwepo wa ibada sasa hauna budi kuelekezwa kwake na yeye ndiye lango la Mbinguni, na ndiye kiini cha ibada na kumtukia yeye ni kuufikia uwepo wake.

 

Yohana 1:1-3, 14 “Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. Huyo mwanzo alikuwako kwa Mungu. Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika. 14 Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli.”     

 

2.       Yesu alikuwa akijitambulisha kuwa yeye ndio ukamilifu wa sadaka za dhabihu na ndiye kuhani mkuu halisi – Yesu alikuwa ndio dhabihu halisi na vile vile kuhani mkuu milele na milele, aliyatoa maisha yake mwenyewe kuwa dhabihu timilifu kwa ulimwengu na hivyo kukomesha mahitaji ya dhabihu za kawaida za wanyama zilizokuwa zikitolewa Hekaluni, kwani dhabihu yake yenye maana ingeweza kuwa dhabihu ya milele itakayofanya upatanisho wa moja kwa moja wa dhambi kwa wanadamu wote duniani bila kuhitaji hekalu

 

Waebrania 9:11-14 Lakini Kristo akiisha kuja, aliye kuhani mkuu wa mambo mema yatakayokuwapo, kwa hema iliyo kubwa na kamilifu zaidi, isiyofanyika kwa mikono, maana yake, isiyo ya ulimwengu huu, wala si kwa damu ya mbuzi na ndama, bali kwa damu yake mwenyewe aliingia mara moja tu katika Patakatifu, akiisha kupata ukombozi wa milele. Kwa maana, ikiwa damu ya mbuzi na mafahali na majivu ya ndama ya ng'ombe waliyonyunyiziwa wenye uchafu hutakasa hata kuusafisha mwili; basi si zaidi damu yake Kristo, ambaye kwamba kwa Roho wa milele alijitoa nafsi yake kwa Mungu kuwa sadaka isiyo na mawaa, itawasafisha dhamiri zenu na matendo mafu, mpate kumwabudu Mungu aliye hai?

 

Waebrania 10:8-12 “Hapo juu asemapo, Dhabihu na matoleo na sadaka za kuteketezwa na hizo za dhambi hukuzitaka, wala hukupendezwa nazo (zitolewazo kama ilivyoamuru torati), ndipo aliposema, Tazama, nimekuja niyafanye mapenzi yako. Aondoa la kwanza, ili kusudi alisimamishe la pili. Katika mapenzi hayo mmepata utakaso, kwa kutolewa mwili wa Yesu Kristo mara moja tu. Na kila kuhani husimama kila siku akifanya ibada, na kutoa dhabihu zile zile mara nyingi; ambazo haziwezi kabisa kuondoa dhambi. Lakini huyu, alipokwisha kutoa kwa ajili ya dhambi dhabihu moja idumuyo hata milele, aliketi mkono wa kuume wa Mungu;”

 

3.       Yesu ndiye njia ya kufikia uwepo wa Mungu – Wakati hekalu ndio ilikuwa njia ya kumfikia Mungu, Yesu anaonyesha kuwa yeye ndio njia ya moja kwa moja ya kuufikia uwepo wa Mungu, kupitia yeye tunaweza kukifikia kiti cha rehema cha Mungu kwa ujasiri na kupata rehema bila kupitia kokote.

 

Waebrania 4:14-16 “Basi, iwapo tunaye kuhani mkuu aliyeingia katika mbingu, Yesu, Mwana wa Mungu, na tuyashike sana maungamo yetu. Kwa kuwa hamna kuhani mkuu asiyeweza kuchukuana nasi katika mambo yetu ya udhaifu; bali yeye alijaribiwa sawasawa na sisi katika mambo yote, bila kufanya dhambi. Basi na tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji.”

 

Pazia katika hekalu lilipasuka katikati vipande viwili wakati Yesu anakata roho pale msalabani hii ilikuwa ikitufundisha wazi kuwa kikwazo kilichokuwa kinamzuia kila mmoja wetu kumfikia au kuufikia uwepo wa Mungu kimeondolewa na sasa kila mtu kwa wakati wake na kwa nafsi yake anaweza kumfikia Mungu kwa Imani katika damu ya Yesu na kukutana na mahitaji yake

 

Mathayo 27:50-51 “Naye Yesu akiisha kupaza sauti tena kwa nguvu, akaitoa roho yake. Na tazama, pazia la hekalu likapasuka vipande viwili toka juu hata chini; nchi ikatetemeka; miamba ikapasuka;”

 

4.       Yesu alikuwa akijitambulisha kuwa yeye ndiye mng’ao wa utukufu wa Mungu (Shekinah)

Yohana 1:14 “Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli.”      

 

Waebrania 1:1-3 “Mungu, ambaye alisema zamani na baba zetu katika manabii kwa sehemu nyingi na kwa njia nyingi, mwisho wa siku hizi amesema na sisi katika Mwana, aliyemweka kuwa mrithi wa yote, tena kwa yeye aliufanya ulimwengu. Yeye kwa kuwa ni mng'ao wa utukufu wake na chapa ya nafsi yake, akivichukua vyote kwa amri ya uweza wake, akiisha kufanya utakaso wa dhambi, aliketi mkono wa kuume wa Ukuu huko juu;”

 

5.       Yesu alikuwa akitukumbusha ya kuwa sisi ndio Hekalu halisi na kuwa yeye anakaa ndani yetu – Waandishi wa nyakati za karne ya kwanza nyakati za kanisa, waliendelea kutumia lugha ya hekalu si kwa kumaanisha jengo tena na badala yake walianza kumaanisha kuwa hekalu ni watu wa Mungu kila mtu aliyeokolewa ni kipande cha tofali katika hekalu hilo, ni sehemu ya kiungo katika mwili wa Kristo.

 

1Wakorintho 6:19-20 “Au hamjui ya kuwa mwili wenu ni hekalu la Roho Mtakatifu aliye ndani yenu, mliyepewa na Mungu? Wala ninyi si mali yenu wenyewe; maana mlinunuliwa kwa thamani. Sasa basi, mtukuzeni Mungu katika miili yenu

 

Badala ya watu kwenda kuutafuta uwepo wa Mungu kule Yerusalem lilikokuweko Hekalu, sisi kama hekalu la Mungu sasa tunapaswa kuubeba uwepo wa Mungu na kuupeleka duniani kote pale tulipo mpaka Yesu arudipo.

 

Mambo ya msingi ya kujifunza katika kanisa. 

1.       Kumuabudu Mungu katika roho na kweli – Ibada ya kweli haiitaji tena mahali Fulani pa ibada, hapa sisemi watu waache kwenda Kanisani, lakini namaanisha kuwa hatuhitaji tena kwenda hija Yerusalem kwaajili ya ibada kwani Mungu ni Roho na anapatikana kokote, kwa hiyo kila mtu anapaswa kuufungua moyo wake na kuuelekeza kwa Yesu kwaajili ya kumuabudu, kumuomba na kupeleka mahitaji yetu, aidha huitaji kweda milimani ingawa hakuna anayekuzuia kwenda huko kwaajili ya kutafuta utulivu na kuutafuta uso wa Mungu lakini ni lazima uelewe kuwa Mungu anapatikana popote pale  na yuko karibu na yeyote yule maadamu tu utauelekeza uso wako kwake.

 

Yohana 4:23-24 “Lakini saa inakuja, nayo sasa ipo, ambayo waabuduo halisi watamwabudu Baba katika roho na kweli. Kwa maana Baba awatafuta watu kama hao wamwabudu. Mungu ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli.”

 

2.       Kuzingatia umoja – Hekalu lilikuwa likiwaunganisha wayahudi wote duniani, kumkumbuka Mungu wao, tamaduni zao na utaifa wao na kuwakumbusha kuwa wao ni kitu kimoja, sisi nasi kupitia Yesu Kristo kama Kanisa tunapaswa kuelewa kuwa sisi ni kitu kimoja

 

Wagalatia 3:26-28 “Kwa kuwa ninyi nyote mmekuwa wana wa Mungu kwa njia ya imani katika Kristo Yesu. Maana ninyi nyote mliobatizwa katika Kristo mmemvaa Kristo. Hapana Myahudi wala Myunani. Hapana mtumwa wala huru. Hapana mtu mume wala mtu mke. Maana ninyi nyote mmekuwa mmoja katika Kristo Yesu.”

 

3.       Hakuna mauti tena hekaluni – Mara kadhaa tumesoma katika maandiko ya agano la kale kuwa wako watu ambao walikufa au walifia hekaluni kwa sababu ya kukiuka maswala mbalimbali na kanuni mbalimbali za hekaluni, Lakini Yesu anatangaza sasa kuwa kama jinsi ambavyo Daudi na wenzake, waliweza kula mikate ya wonyesho bila kufa (Kwa Sababu Daudi alikuwa na Yesu viunoni mwake) hali kadhalika kila amwendeaye Yesu tatapata uzima na uzima wa milele na hakuna mauti kwa mtu amwaminiye Yesu ambaye ni mkuu kuliko Hekalu

Mathayo 12:3-6 “Akawaambia, Hamkusoma alivyotenda Daudi, alipokuwa na njaa, yeye na wenziwe? jinsi alivyoingia katika nyumba ya Mungu, akaila mikate ile ya wonyesho, ambayo si halali kwake kuila wala kwa wale wenziwe, ila kwa makuhani peke yao? Wala hamkusoma katika torati, kwamba siku ya sabato makuhani hekaluni huinajisi sabato wasipate hatia? Lakini nawaambieni, kwamba hapa yupo aliye mkuu kuliko hekalu.”

Na. Rev. Innocent Samuel Kamote 

Mkuu wa wajenzi Mwenye Hekima.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni