Warumi 15:30-32 “Ndugu zangu, nawasihi kwa
Bwana wetu Yesu Kristo, na kwa upendo wa Roho, jitahidini pamoja nami katika
maombi yenu kwa ajili yangu mbele za Mungu; kwamba niokolewe na wale wasioamini
katika Uyahudi, na tena huduma yangu niliyo nayo huko Yerusalemu ikubalike kwa
watakatifu; nipate kufika kwenu kwa furaha, kama apendavyo Mungu, nikapate
kupumzika pamoja nanyi.”
Utangulizi:
Ni muhimu kwetu kama kanisa kuwa
na ufahamu, kuwa kuna changamoto kubwa katika kanisa la Mungu na changamoto mojawapo
kubwa ni hii ya kutokuwaombea watumishi
wa Mungu, changamoto hii inaweza kuwa inachangiwa na ufahamu finyu wa neno la
Mungu, au kutokutiliwa mkazo kwa fundisho hili muhimu na la msingi la kuwaombea
watumishi wa Mungu, Mtume, Nabii, Mwinjilisti, Mchungaji na Mwalimu asiyekuwa
na waombaji kwaajili yake hana tofauti na Askari aliyeingia vitani pake yake,
akishambuliwa yeye hakuna tena msaada mwingine, Ni muhimu kuwa na maarifa na
ufahamu ya kuwa kila huduma katika ufalme wa Mungu ina vita na mashambulizi
mengi ya upinzani wa ibilisi huelekezwa
kwa watumishi wa Mungu, tunapowaombea tunawasaidia katika ulimwengu wa roho
kuepushwa na mashambulizi makali na kuwawekea ulinzi dhidi ya utawala wa giza.
Mathayo 26:30-31 “Nao walipokwisha kuimba,
wakatoka nje kwenda mlima wa Mizeituni. Ndipo Yesu akawaambia, Ninyi nyote
mtachukizwa kwa ajili yangu usiku huu kwa kuwa imeandikwa, Nitampiga mchungaji,
na kondoo wa kundi watatawanyika.”
Wakati Mungu amewatenga watumishi
wake wawe kama chombo cha kuwakilisha kazi yake duniani, shetani naye
anawalenga wawe silaha maalumu ya kuharibu kazi ya Mungu, au anaweza kutumia
hila na mbinu mbalimbali kwa kusudi la kuwakwamisha ili kazi ya Mungu asiendelee
mbele na ndio maana kwa kujua hali ilivyo katika ulimwengu wa Roho Paulo Mtume
mara kwa mara aliwaomba watu wa makanisa mbalimbali wamuombee, tusipokuwa na watu wa kutuombea katika huduma zetu
tunajiweka katika hatari ya vita kali na kukabiliana na mashambulizi ya huduma
peke yako, Jambo ambalo linaweza kusababisha ukadhoofika mapema na kuchoka.
2Wathesalonike 3:1-4 “Hatimaye, ndugu,
tuombeeni, neno la Bwana liendelee, na kutukuzwa vile vile kama ilivyo kwenu;
tukaokolewe na watu wasio haki, wabaya; maana si wote walio na imani. Lakini
Bwana ni mwaminifu, atakayewafanya imara na kuwalinda na yule mwovu. Nasi
tumemtumaini Bwana kwa mambo yenu, kwamba mnayafanya tulivyowaagiza, tena
kwamba mtayafanya.”
Tutajifunza somo hili muhimu
Ndugu tuombeeni kwa kuzingatia vipengele vikuu vitatu vifuatavyo:-
·
Umuhimu wa kuwaombea watumishi wa Mungu.
·
Hatimaye ndugu tuombeeni.
·
Mifano ya watumishi wa Mungu waliokuwa na timu
za waombaji.
Umuhimu wa kuwaombea watumishi wa Mungu.
Ni muhimu kuwa na ufahamu na
maarifa kuwa watumishi wa Mungu wa aina zote wanahitaji maombi, na sio tu
kuombewa na washirika pekee lakini ikiwa
uko uwezekano pia wawe na timu yaani kikundi au watu maalumu ambao wanaifanya
kazi hiyo kwa uaminifu, Swala la kuombewa kwa watumishi wa Mungu ni swala la
kiroho kabisa, na ni la kibiblia, kuomba maombi kwa washirika wetu ni swala la
kibiblia na ni swala la unyenyekevu unaoonyesha kuwa tunahitaji neema ya Mungu
baadhi ya watumishi wa Mungu wanafikiri kuomba maombi kwa washirika na kuwa na
timu maalumu ya kuwaombea ni kuonyesha udhaifu, Jambo hili sio sahihi Kwani neno
la Mungu linaonyesha kuwa watumishi wa Mungu wanahitaji kuombewa, Nyakati za
Kanisa la kwanza walipoteza viongozi Muhimu sana wenye uwezo mkubwa sana katika
jamii ya Kikristo mpaka walipopata ufunuo wa kuhakikisha kuwa wanaomba kwa
nguvu na juhudi kubwa kwaajili ya wachungaji wao.
Matendo 6:8-13 “Na Stefano, akijaa neema na
uwezo, alikuwa akifanya maajabu na ishara kubwa katika watu. Lakini baadhi ya
watu wa sinagogi lililoitwa sinagogi la Mahuru, na la Wakirene, na la
Waiskanderia, na la wale wa Kilikia na Asia, wakaondoka na kujadiliana na
Stefano; lakini hawakuweza kushindana na hiyo hekima na huyo Roho aliyesema
naye. Hata wakashawishi watu waliosema, Tumemsikia mtu huyu akinena maneno ya
kumtukana Musa na Mungu. Wakawataharakisha watu na wazee na waandishi,
wakamwendea, wakamkamata, wakampeleka mbele ya baraza. Wakasimamisha mashahidi
wa uongo waliosema, Mtu huyu haachi kusema maneno ya kufuru juu ya mahali hapa
patakatifu na juu ya torati;”
Matendo 7:57-60 “Wakapiga kelele kwa sauti
kuu, wakaziba masikio yao, wakamrukia kwa nia moja, wakamtoa nje ya mji,
wakampiga kwa mawe. Nao mashahidi wakaweka nguo zao miguuni pa kijana mmoja
aliyeitwa Sauli. Wakampiga kwa mawe Stefano, naye akiomba, akisema, Bwana Yesu,
pokea roho yangu. Akapiga magoti, akalia kwa sauti kuu, Bwana, usiwahesabie
dhambi hii. Akiisha kusema haya akalala. Na Sauli alikuwa akiona vema kwa
kuuawa kwake.”
Matendo 12:1-5 “Panapo majira yale yale
Herode mfalme akanyosha mikono yake kuwatenda mabaya baadhi ya watu wa kanisa.
Akamwua Yakobo, ndugu yake Yohana, kwa upanga. Na akiona ya kuwa imewapendeza
Wayahudi akaendelea akamshika na Petro. Siku hizo zilikuwa siku za mikate
isiyochachwa. Alipokwisha kumkamata, akamweka gerezani akamtia mikononi mwa
vikosi vinne vya askari wanne wanne, wamlinde, akitaka baada ya Pasaka kumtoa
na kumweka mbele ya watu.Basi Petro akalindwa gerezani, nalo kanisa likamwomba
Mungu kwa juhudi kwa ajili yake.”
Tunaona jinsi nyakati za kanisa
la kwanza shetani alivyowatumia watu waovu kupinga kazi ya Mungu hasa kwa
kuwaua viongozi wa kanisa wale waliokuwa mstari wa mbele katika kuieneza kazi
ya injili, aliuawa Stefano na pia Yakobo Mtume ndugu yake Yohana, na Petro
akakamatwa, ni wazi kabisa huu ulikuwa ni mpango mkakati wa kishetani wa kutaka
kulidhoofisha kanisa, kwa hiyo hata kama kanisa lilikuwa linaomba sasa
waliongeza kasi ya kumuomba Mungu kwa juhudi kwaajili ya viongozi wengine,
tunasoma kuwa hata Petro alikamatwa lakini kanisa lilipoomba kwa juhudi Mungu
alimtuma malaika wake na Petro akawekwa huru, tangu wakati huu, viongozi na
washirika walielewa kuwa wanapaswa kuwalinda watumishi wa Mungu kwa maombi na
kuwaombea ili kazi ya kueneza neema hii iweze kusonga mbele, kazi ya Mungu ina
upinzani mkubwa na viongozi ndio wanaowindwa zaidi kwa sababu hiyo ni muhimu
sana kwa kanisa kuomba, kuwa na programu endelevu za maombi ya kimkakati
kuwaombea watumishi wa Mungu, kazi ya Mungu iweze kuendelea, ishara na miujiza
viweze kufanyika, Na neno la Mungu liendelee kuhubiriwa kwa ujasiri.
Matendo 4:21-31“Nao walipokwisha kuwatisha
tena wakawafungua, wasione njia ya kuwaadhibu, kwa sababu ya watu; kwa kuwa
watu wote walikuwa wakimtukuza Mungu kwa hayo yaliyotendeka; maana umri wake
yule mtu aliyefanyiwa ishara hii ya kuponya ulipita miaka arobaini. Hata walipofunguliwa,
wakaenda kwa watu wao, wakawapasha habari ya mambo yote waliyoambiwa na wakuu
wa makuhani na wazee. Nao waliposikia, wakampazia Mungu sauti zao kwa moyo
mmoja, wakisema, Mola, wewe ndiwe Mungu, ndiwe uliyefanya mbingu na nchi na
bahari na vitu vyote vilivyomo; nawe ulinena kwa Roho Mtakatifu kwa kinywa cha
babaetu Daudi, mtumishi wako, Mbona mataifa wamefanya ghasia, Na makabila
wametafakari ubatili? Wafalme wa dunia wamejipanga, Na wakuu wamefanya shauri
pamoja Juu ya Bwana na juu ya Kristo wake. Maana ni kweli, Herode na Pontio
Pilato pamoja na Mataifa na watu wa Israeli, walikusanyika katika mji huu juu
ya Mtumishi wako mtakatifu Yesu, uliyemtia mafuta, ili wafanye yote ambayo
mkono wako na mashauri yako yamekusudia tangu zamani yatokee. Basi sasa, Bwana,
yaangalie matisho yao; ukawajalie watumwa wako kunena neno lako kwa ujasiri
wote, ukinyosha mkono wako kuponya; ishara na maajabu vifanyike kwa jina la
Mtumishi wako mtakatifu Yesu. Hata walipokwisha kumwomba Mungu, mahali pale
walipokusanyika pakatikiswa, wote wakajaa Roho Mtakatifu, wakanena neno la
Mungu kwa ujasiri.”
Kwa hiyo kwa kuwaombea watumishi
wa Mungu kanisa linashiriki kuwatia moyo kiroho kwaajili ya huduma zao, kutunza
hisia zao, kuwaombea waweze kuwa na afya njema
na waweze kustahimili hasa wanapokutana na upinzani, waweze kubeba vema
majukumu ya kikanisa na wawe na nguvu wakati wa kupambana na vita vya kiroho,
kufanya hivyo pia ni njia ya kushiriki Baraka ya kazi wanayoifanya ya kuihubiri
injili kwa usahihi na kuwalinda dhidi ya yule muovu, Mungu awape hekima ya
maongozi, lakini zaidi ya yote ni njia ya kuonyesha upendo na ushirika pamoja
nao.
Maandiko yanaonyesha pia shetani
anaweza kuwazuia watumishi wa Mungu wasilifikie eneo Fulani kwa injili, Anga la
Thesalonike lilikuwa gumu kwa Paulo mtume alipohubiri Thesalonike alikutana na
upinzani mkali sana lakini sio hivyo tu hata alipotaka kurejea tena kwa kusudi
la kuwaimarisha Shetani alimzuia na watumishi wengine, kwa hiyo shetani ni adui
wa injili na ni adui wa wale wanaoipeleka injili anaweza kuwazuia wasifike eneo
Fulani
1Wathesalonike 2:17-18 “Lakini sisi, ndugu,
tukiwa tumefarakana nanyi kwa kitambo, kwa uso si kwa moyo, tulizidi kutamani
kwa shauku nyingi kuwaona nyuso zenu.Kwa hiyo tulitaka kuja kwenu, naam, mimi
Paulo, mara ya kwanza, na mara ya pili, na Shetani akatuzuia.”
Kama shetani anaweza kumzuia
Paulo Mtume na timu yake wasifike Thesalonike kuwaimarisha wakristo waliozaliwa
katika hali ya dhiki nyingi tena sio mara moja jiulize anashindwaje kutuzuia
wewe na mimi ambao hatuna mwombezi zaidi ya wake zetu, tena wakati mwingine
anatugonganisha nao ili maombi yetu yazuiliwe, tunahitaji maombi ya watu
waaminifu atakaotambua kile ambacho tumekibeba na kulia na kuomboleza na
kufunga kwaajili yetu.
Hatimaye ndugu tuombeeni
2Wathesalonike 3:1-4 “Hatimaye, ndugu,
tuombeeni, neno la Bwana liendelee, na kutukuzwa vile vile kama ilivyo kwenu; tukaokolewe
na watu wasio haki, wabaya; maana si wote walio na imani. Lakini Bwana ni
mwaminifu, atakayewafanya imara na kuwalinda na yule mwovu. Nasi tumemtumaini
Bwana kwa mambo yenu, kwamba mnayafanya tulivyowaagiza, tena kwamba mtayafanya.”
Wote tunafahamu kuwa Paulo Mtume
alikuwa ni moja ya viongozi hodari sana katika kuifanya kazi ya Mungu, Neno la
Mungu linaonyesha ya kuwa Paulo mtume alitumiwa na Mungu kwa viwango vikubwa na
vya juu sana katika kulijenga kanisa la Mungu, naweza kusema kuwa hakuna mtu
anaweza kudai kuwa yeye ni wa kiroho kumzidi Paulo Mtume neno la Mungu
linaonyesha ya kuwa alifanya kazi kuliko mitume wote, alipewa mafunuo makubwa
kuliko mtu yeyote, lakini pia alitumiwa na Mungu kufanya miujiza ya kupita
kawaida kwa mikono yake
1Wakorintho 15:9-10 “Maana mimi ni mdogo
katika mitume, nisiyestahili kuitwa mitume, kwa sababu naliliudhi Kanisa la
Mungu. Lakini kwa neema ya Mungu nimekuwa hivi nilivyo; na neema yake iliyo
kwangu ilikuwa si bure, bali nalizidi sana kufanya kazi kupita wao wote; wala
si mimi, bali ni neema ya Mungu pamoja nami.”
2Wakorintho 12:2-4 “Namjua mtu mmoja katika
Kristo, yapata sasa miaka kumi na minne, (kwamba alikuwa katika mwili sijui;
kwamba alikuwa nje ya mwili sijui; Mungu ajua). Mtu huyo alinyakuliwa juu mpaka
mbingu ya tatu. Nami namjua mtu huyo, (kwamba alikuwa katika mwili sijui;
kwamba alikuwa nje ya mwili sijui; Mungu ajua); ya kuwa alinyakuliwa mpaka
Peponi, akasikia maneno yasiyotamkika, ambayo haijuzu mwanadamu ayanene.”
Matendo 19:11-12 “Mungu akafanya kwa mikono
ya Paulo miujiza ya kupita kawaida; hata wagonjwa wakaletewa leso na nguo
zilizotoka mwilini mwake, magonjwa yao yakawaondokea, pepo wachafu wakawatoka.”
Hata pamoja na kutumiwa hivyo
sana na Mungu, na kupewa mafunuo makubwa sana na kufanya kazi ya Mungu kwa
neema kubwa kuliko mitume wote bado Paulo mtume kwa unyenyekevu mkubwa
alionekana katika nyaraka nyingi akiomba kuombewa, mara kwa mara utaona akiomba
maombi, ndugu tuombeeni, hatimaye ndugu tuombeeni, jitahidini pamoja nami
katika maombi, hakuwa na kiburi wala hakufikiri kuwa anaweza peke yake na
kumbuka kuwa yeye mwenyewe alikuwa mwombaji, watu wengi sana wa Mungu hawaijui
siri hii wanadhani kuomba kuombewa na washirika ni kuonyesha udhaifu, wanadhani ni sisi tu ndio wenye
wajibu wa kuwaombea washirika na ni kama
washirika hawapaswi kutuombea jambo hilo
sio sahihi, au kuwa na timu ya watu wanaoomba kwaajili yako au hata wanaoomba
pamoja nawe, huo sio udhaifu ni unyenyekevu na ni ukweli usiopingika kibiblia
kuwa tunahitaji kuombewa, tunahitaji watu waaminifu, waliojitoa wanaojua nini
wanakifanya kutuombea, tunahitaji maombi!
Warumi 15:30-32 “Ndugu zangu, nawasihi kwa
Bwana wetu Yesu Kristo, na kwa upendo wa Roho, jitahidini pamoja nami katika
maombi yenu kwa ajili yangu mbele za Mungu; kwamba niokolewe na wale wasioamini
katika Uyahudi, na tena huduma yangu niliyo nayo huko Yerusalemu ikubalike kwa
watakatifu; nipate kufika kwenu kwa furaha, kama apendavyo Mungu, nikapate
kupumzika pamoja nanyi.”
Waefeso 6:18-20 “kwa sala zote na maombi
mkisali kila wakati katika Roho, mkikesha kwa jambo hilo na kudumu katika
kuwaombea watakatifu wote; pia na kwa ajili yangu mimi, nipewe usemi kwa
kufumbua kinywa changu, ili niihubiri kwa ujasiri ile siri ya Injili; ambayo
kwa ajili yake mimi ni mjumbe katika minyororo; hata nipate ujasiri katika huyo
kunena jinsi inipasavyo kunena.”
Wakolosai 4:2-3 “Dumuni sana katika kuomba,
mkikesha katika kuomba huku na shukrani; mkituombea na sisi pia, kwamba Mungu
atufungulie mlango kwa lile neno lake, tuinene siri ya Kristo, ambayo kwa ajili
yake nimefungwa,”
2Wakorintho 1:9-11. “Naam, sisi wenyewe
tulikuwa na hukumu ya mauti katika nafsi zetu ili tusijitumainie nafsi zetu,
bali tumtumaini Mungu, awafufuaye wafu, aliyetuokoa sisi katika mauti kuu namna
ile; tena atatuokoa; ambaye tumemtumaini kwamba atazidi kutuokoa; ninyi nanyi
mkisaidiana nasi kwa ajili yetu katika kuomba, ili, kwa sababu ya ile karama
tupewayo sisi kwa msaada wa watu wengi, watu wengi watoe shukrani kwa ajili
yetu.”
Tunapowaombea watumishi wa Mungu
wanapewa ujasiri, wanatumiwa na Mungu kwa miujiza, neno la Mungu linaenea kwa
nguvu huku likishinda nguvu za upinzani, milango ya injili inafunguka,
wananusuriwa na hatari za namna mbalimbali, huduma inaenea katika mataifa mengi
kama wana kesi au wamefungwa minyororo inaachilia, lakini zaidi ya yote
wanalindwa ili kwamba wasipepetwe katika imani wala imani zao zisitindike, Yesu
alimuombea Petro awe imara, Imani yake
isitindike, ni maombi yet utu ndio yatakayowadumisha
watumishi wa Mungu na kuwafanya imara katika imani, mtumishi asiyeombewa hawezi
kusimama, washirika wasio na akili husengenya na kuwashutumu watumishi wa Mungu
wanapoingia majaribuni wakisahau kuwa hawajawahi hata siku moja kufanya wajibu
wao wa kumlilia Mungu kwaajili yao ili wasimame imara na kushinda vikwazo vyote
vinavyowakabili.
Luka 22:31-32. “Akasema, Simoni, Simoni,
tazama, Shetani amewataka ninyi apate kuwapepeta kama vile ngano; lakini
nimekuombea wewe ili imani yako isitindike; nawe utakapoongoka waimarishe ndugu
zako.”
Mifano ya watumishi wa Mungu waliokuwa na timu za waombaji
Kwa kufahamu siri hii ya kuwa
kila mtumishi wa Mungu anahitaji maombi, baadhi ya watumishi wa Mungu
waligundua kuwa kama Paulo Mtume aliyekuwa wa kiroho sana bado kuna nyakati
alihitaji maombi ni zaidi sana mimi na wewe tunahitaji maombi, ndugu unahitaji
kuombewa ninahitaji sana maombi yako pia, Katika historia ya kanisa, wahubiri
wengi waliotumiwa na Mungu na kuleta uamsho mkubwa hawakuwa wanategemea kipawa
na upako wao peke yao, wala maombi yao
peke yao lakini vile vile walikuwa na timu maalumu za waombaji waliobeba huduma
zao kwa maombi endelevu na ya kudumu!
John Wesley – alizaliwa june
28 1703 na kufariki 2March 1791 moja ya mwinjilisti mkubwa sana duniani na
mwanatheolojia maarufu ambaye likuwa sababu ya uamsho mkubwa wa kanisa la
Uingereza, alikuwa na vikundi vidogo vidogo vingi kama madarasa ya maombi,
hakuruhusu kufanya huduma bila nidhamu ya kiroho, alisababisha uamsho mkubwa
huko uingereza na kusababisha mabadiliko makubwa ya kijamii, maadili katika kazi na familia na kusababisha kanisa lililodumu hadi leo,
tunajifunza kwake kuwa maombi ya pamoja huzalisha mabadiliko ya kitaifa
Charles Finney – Ni moja ya wahubiri waliotumiwa sana na Mungu
kuleta uamsho mkubwa alizaliwa 29 August
1792 na kufariki mwaka 16 August
1875, alikuwa ni muhudumu wa kanisa la American
Presbyterian alijulikana sana kama
kiongozi wa uamsho mkubwa wa Pili katika Marekani, alikuwa akisimama kabla hata
ya kuhubiri watu walililia toba kabla ya mahubiri kuanza na kulikuwa na uamsho
mkubwa sana nyakati zake lakini yeye alisema wazi “Mahubiri yangu yalibebwa na Maombi ya Nash” Daniel Nash maarufu kama (Father
Nash) alikuwa mtu mmoja maalumu ambaye kazi yake ilikuwa ni kuomba bila
kukoma kabla ya Finney kuhubiri, Daniel
Nash alikuwa anaenda katika mji husika ambao Finney angehubiri kwa muda
kuanzia wiki au miezi kabla, akifunga na kuomba, Mahubiri yenye matokeo makubwa
sana hutanguliwa na maombi makubwa sana.
D. L Moody – Moja ya wainjilisti maarufu sana Duniani alizaliwa February 5 1837 na kufariki December
1899 jina lake kwa urefu ni Dwight Lyman
Moody maarufu kama D.L Moody mwinjilisti maarufu wa kimarekani alihubiri
injili na kusababisha maelefu ya watu kuokoka huko ulaya na Marekani, aliendelea
na huduma bila kuwa na Skendo injili ilienea kupitia yeye kizazi kwa
kizazi lakini yeye alikuwa na timu ya
waombaji waliokuwa wakikaa nyuma ya pazia wakati yeye alipokuwa anahubiri
alisema “Ni Afadhali nopate watu 10 wanaoomba kuliko 10,000 wanaonisikiliza”
mafanikio yoyote ya jukwaani ni matokeo ya kazi katika chumba cha maombi
Reinhard Bonnke – Muhubiri mkubwa sana Duniani chini ya huduma ya Christ for All nations (CfaN) amehubriri watu zaidi ya milioni 79 waliookoka katika huduma
yake, Mungu alimtumia kwa miujiza mikubwa wakati akihubiri Afrika, huduma yake
ilimuwezesha kutembelea bara zima, Muhubiri huyu mwenye asili ya Ujerumani
alikuwa na mtandao mkubwa sana wa kimataifa wa waombaji, ambao walifunga wiki
kadhaa na saa kadhaa kila alipokuwa akifanya mkutano wa injili Bonke alikuwa na
timu mahususi ya kuombea huduma yake kwa hiyo tunajifunza hapo kuwa Huduma
kubwa huitaji Jeshi kubwa la siri la waombaji.
Billy Graham – Moja ya wahubiri wakubwa walioheshimika sana
Marekani alizaliwa 7 November 1918
na kufariki 21 February 2018 alikuwa
na timu ya maombi iliyoitwa “The prayer
Partners” yeye hakuwahi kukubali mkutano wowote ufanyike bila maandalizi ya
maombi ya muda mrefu, Mungu alimpa neema ya kuhubiria maraisi wa aina
mbalimbali, mataifa mengi na mamilioni ya watu alikaa katika huduma kwa karibu
miaka 60 bila kuharibiwa na maswala ya fedha, umaarufu kiburi au wanawake,
tunajifunza kutoka kwake ya kuwa maombi hutunza sio huduma tu hata sifa nzuri
za muhubiri anayeombewa.
David Yonggi Cho – Mwanzilishi wa Kanisa la Yoido Full Gosple Church alizaliwa 14 February 1936 na kufariki 14
september 2021 ni moja ya waanzilishi wa maswala ya mlima wa maombi (Prayer Mountain) alitenga wachungaji na
waombaji kila wakati kwaajili ya kufunga na kuomba na kukemea au kupigana vita
vya kiroho, matokeo yake akawa ndiye mchungaji mwenye kanisa kubwa zaidi kuliko
watu wote duniani kwa nyakati zake, alichangia kwa kiasi kikubwa uamsho ulioko
Korea ya kusini, na alifanikiwa kwa kuanzisha mfumo wa cell groups au makanisa ya nyumbani ambao nao ulibebwa na maombi,
tunajifunza kutoka kwake kuwa kanisa linalotaka kukua kwa haraka lazima lijikite
katika mzizi wa kuomba.
Zachary Kakobe – Ni mwanzilishi wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship nchini Tanzania, moja ya makanisa ya
kipentekoste yenye asili yake nchini Tanzania na si kutoka nje, Muhubiri
maarufu sana mwenye kanisa kubwa huko Mwenge jijini Dar es Salaam, Mchungaji
Kakobe ana mfumo wa cell ziitwazo “Power
House” ambapo washirika katika maeneo mbalimbali kila mtaa waliko washirika
hukutana kila alhamisi kwa maombi mbalimbali ya kikanisa ikiwa ni pamoja na kumuombea
Mchungaji, aidha ana kikundi maalumu ya maombi kijulikanacho kwa jina la Ana
binti Fanuel ambao pamoja na mambo mengine humuombea Mchungaji sawasawa na
maelekezo yake kikundi hiki kinaundwa na wajane maalumu ambao hutunzwa na
kanisa, Matokeo yake Kanisa lake limeweza kuenea nchi nzima kwa muda mfupi,
kuna uamsho mkubwa sana unaofukuta chini kwa chini, washirikia wake wamejengwa
katika misingi ya kuomba kwa kuyataja maandiko, wanapenda mafundisho na
wanaishi kwa nidhamu. Alizaliwa 6 June
1955 huko, Kakonko, Kigoma, uamsho katika kanisa lake unakua kwa kasi
kupitia maombezi, semina na mikutano ya ndani kwa ndani, pamoja na yeye mwenyewe
kuwa mwombaji, Kakobe mara kwa mara amesisitiza kuombewa, kama ilivyokuwa kwa
Paulo mtume, Kumbe maombi yana nguvu ya kuwaleta maelefu kwa Yesu, kuwafanya
wanafunzi hata bila kuathiri, shughuli na utendaji wa maisha ya kawaida ya watu
na kujenga kanisa imara
Hitimisho!
Unapochunguza kwa makini mifano
hii michache ya wahubiri ambao Mungu aliwatumia kwa uamsho mkubwa sehemu mbalimbali
duniani utabaini kuwa maombi yanahusika kwa kiasi kikubwa, sitaki kusema kuwa
kila uamsho unaletwa na maombi lakini nataka kusema kuwa, mahuburi na uamsho wa
kina na endelevu unajengwa kwa maombi, watumishi wa Mungu tutake maombi kwa
washirika wetu, hata pamoja na sisi wenyewe kuwa waombaji, lakini pia tuwe na
timu za maombi watu wanaotuombea kwa kina, na sio vibaya kuwa na timu ya watu
wanaoomba pamoja nawe au wanaokuombea, Yesu alimtaka Petro, Yakobo na Yohana,
wakeshe au waombe pamoja naye, Licha ya kuwa alikuwa wa kiroho sana na ni mwana
wa Mungu, nadhani ni afadhali mara elfu kuwa na waombaji wanaokuombea kwa huduma yako kuliko kuwa na
walinzi wanaokulinda “Body guards”
Mathayo 26:36-38 “Kisha Yesu akaenda pamoja
nao mpaka bustani iitwayo Gethsemane, akawaambia wanafunzi wake, Ketini hapa,
hata niende kule nikaombe. Akamchukua Petro na wale wana wawili wa Zebedayo,
akaanza kuhuzunika na kusononeka.Ndipo akawaambia, Roho yangu ina huzuni nyingi
kiasi cha kufa; kaeni hapa, mkeshe pamoja nami.”
Mtumishi wa Mungu mwombe Mungu
akupe watu sahihi watakaokubebea mzigo katika maombi, omba Mungu akupe hekima
kuchagua watu wasiri waliojaa maisha ya maombi wanyenyekevu, waaminifu, wenye
upendo na mzigo au wajane wenye umri mkubwa wanaofanya kazi ya kuomboleza
kwaajili yako, waelezee maono yako au mzigo unaotaka wakubebee, wafundishe
masomo mbalimbali kuhusu kuomba, tengeneza mfumo au muda maalumu wa kuomba na
siku maalumu za kuomba, hata pamoja na
kuwa na idara za maombi, amini sana katika watu wachache ambao maalumu au
kipekee watakuwa wanakuombea, anza na watu wachache sana kikundi cha maombi
kinatakiwa kuwa na watu 3-12
tengenezeni mawasiliano ya siri, wafundishwe kuishi maisha ya kujitoa na
utakatifu, wenye matumizi mazuri ya kinywa wasio na mafarakano waandae kwa
mafundisho maalumu ya waombaji kwaajili ya mtumishi wa Mungu kisha anzeni
kuomba!
Na Rev. Innocent Samuel Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima
.jpg)

