Jumapili, 2 Agosti 2026

Wito wa kumtumikia Mungu katika huduma!


Matendo 13:1-3 “Na huko Antiokia katika kanisa lililokuwako palikuwa na manabii na waalimu, nao ni Barnaba, na Simeoni aitwaye Nigeri, na Lukio Mkirene, na Manaeni aliyekuwa ndugu wa kunyonya wa mfalme Herode, na Sauli. Basi hawa walipokuwa wakimfanyia Bwana ibada na kufunga, Roho Mtakatifu akasema, Nitengeeni Barnaba na Sauli kwa kazi ile niliyowaitia. Ndipo wakiisha kufunga na kuomba, wakaweka mikono yao juu yao, wakawaacha waende zao.”



Utangulizi:

Ni muhimu kufahamu kuwa Mungu anatoa wito kwa watu wake wote kuhakikisha ya kuwa wanamtumikia, Neno wito linamaanisha kualikwa na Mungu ili tuweze kutekeleza ajenda zake au kusudi lake ambalo amelikusudia yeye mwenyewe sawasawa na maagizo yaliyomo katika neno lake, Mungu huchagua watu wake wale anaowataka mwenyewe na kuwaalika wawe na ushirika naye na kisha awatume katika kazi yake ili kutekeleza mapenzi yake, kusudi lake na kazi yake hapa duniani na kwa sababu hiyo kuitikia wito wa kumtumikia Mungu ni utii usio na mashart

Marko 3:13-15 “Akapanda mlimani, akawaita aliowataka mwenyewe; wakamwendea. Akaweka watu kumi na wawili, wapate kuwa pamoja naye, na kwamba awatume kuhubiri, tena wawe na amri ya kutoa pepo.”

Kwa hiyo tangu nyakati za agano la kale Mungu amekuwa na tabia ya kuwaita na kuwachagua watu aliowataka mwenyewe kwaajili ya kutekeleza majukumu na makusudi yake yeye mwenyewe duniani, Kwa msingi huo kila mtu aliyeokoka anapaswa kuwa makini kumtumikia Mungu na kusikiliza sauti ya Mungu ili kutambua mapenzi ya Mungu katika maisha yake na kuwajibika mara moja katika kazi hii yenye Baraka na heshima kubwa, kwa bahati mbaya watu wengi sana hawapendi kumtumikia Mungu katika huduma mbalimbali Kanisani kwa kisingizio kuwa hawajaitwa, au kwa kutokuwa na ufahamu wanawajibika vipi, kwa hiyo leo tutachukua Muda kujifunza na kutafakari kwa pamoja somo hili muhimu kuhusu wito wa kumtumikia Mungu katika huduma kwa kuzingatia vipengele vikuu vitatu vifuatavyo:-


·         Maana ya neno wito katika maandiko.

·         Aina kuu tatu za wito katika huduma.

·         Jinsi Mungu anavyoita watu katika huduma.


Maana ya neno wito katika maandiko.

Ni muhimu kufahamu kuwa neno wito katika maandiko lina tajwa kwa lugha ya Kiebrania kwa neno “qara” na linatajwa kwa kiyunani kama neno “Kaleō” au “klēsis” ikimaanisha kuitwa, kutengwa, kuchaguliwa au kuteuliwa na Mungu kwa kusudi la kutimiza majukumu maalumu katika ajenda za Mungu, Kwa sababu hiyo wito sio mpango wala wazo la kibinadamu au shauku binafsi bali ni mpango kamili wa Mungu juu ya maisha ya mtu katika kusudi lake au kwa kazi maalumu, kwa hiyo wito katika huduma ni mualiko wa kumtumikia Mungu au kufanya kazi pamoja na Mungu katika kutimiza kusudi lake au ajenda zake mwenyewe hapa duniani kwa wakati maalumu.

Luka 5:27-29 “Baada ya hayo akatoka, akaona mtoza ushuru, jina lake Lawi, ameketi forodhani, akamwambia, Nifuate. Akaacha vyote, akaondoka, akamfuata. Na Lawi akamfanyia karamu kubwa nyumbani mwake; palikuwa na mkutano mkuu wa watoza ushuru na watu wengineo waliokuwa wameketi chakulani pamoja nao.”

Msingi mkuu wa Mungu anapomuita mtu kwanza anataka ushirika wa karibu na mtu huyo kisha ndipo amtume, kwa hiyo mtu aliyeitwa na aliyeitikia wito wa kumtumikia Mungu katika huduma anapaswa kuwa mtu mwenye ushirika wa karibu na Mungu, ushirika huu ni wa muhimu hata kabla ya kazi yenyewe

Yohana 21:15-17 “Basi walipokwisha kula, Yesu akamwambia Simoni Petro, Je! Simoni wa Yohana, wewe wanipenda kuliko hawa? Akamwambia, Naam, Bwana, wewe wajua kuwa nakupenda. Akamwambia, Lisha wana-kondoo wangu. Akamwambia tena mara ya pili, Simoni wa Yohana, wanipenda? Akamwambia, Ndiyo, Bwana, wewe wajua kuwa nakupenda. Akamwambia, Chunga kondoo zangu. Akamwambia mara ya tatu, Simoni wa Yohana, wanipenda? Petro alihuzunika kwa vile alivyomwambia mara ya tatu, Wanipenda? Akamwambia, Bwana, wewe wajua yote; wewe umetambua ya kuwa nakupenda. Yesu akamwambia, Lisha kondoo zangu.”

Marko 3:13-15 “Akapanda mlimani, akawaita aliowataka mwenyewe; wakamwendea. Akaweka watu kumi na wawili, wapate kuwa pamoja naye, na kwamba awatume kuhubiri, tena wawe na amri ya kutoa pepo.”

Kabla Mungu hajamuita mtu anataka ushirika na wewe anataka upendo wako na anataka uwe pamoja naye kisha ndipo akutume kuhubiri na kutoa pepo au kufanya huduma nyinginezo kwa niaba yake            

Aina kuu tatu za wito katika huduma.

Maandiko matakatifu yanaonyesha kuwa Mungu aliwaita watu kwa namna mbalimbali na kwaajili ya shughuli mbalimbali, kwa hiyo tunapozungumzia swala la wito tunazungumzia mada pana sana katika nyanja zote za kisiasa, kijamii na kiimani, na kisayansi, ukichunguza kwa kina utaweza kuona kuwa kote huko Mungu hufanya kazi ya kuwaita watu kwaajili ya makusudi mbalimbali, kwa hiyo wito hauko katika kuta za kanisa pekee unavuka mipaka na kwenda mbali zaidi ya vile tunavyofikiri, hata hivyo katika somo hili nataka kuzungumzia wito ambao unaishia ndani ya mipaka ya Kanisa pekee aina hizi za wito naweza kugawa katika makundi makuu muhimu matatu yafuatayo:-

·         Wito wa jumla katika wokovu

·         Wito wa jumla katika huduma

·         Wito maalumu katika huduma

Wito wa jumla katika wokovu – Wito huu wa ujumla katika wokovu ni wito unaotolewa na Mungu Roho Mtakatifu kwa jamii ya watu wote duniani ili wamuamini Bwana wetu Yesu Kristo kama mwokozi wao na kupokea uzima wa milele, huu ni wito unaotolewa kwa watu wote wamgeukie Mungu wamrudie yeye wamche yeye na kuwa na ushirika na yeye kwa hiyo watu wote duniani wanaalikwa kila iitwapo leo kupokea wito huu wa wokovu kwa imani.

Yohana 3:16-18 “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. Maana Mungu hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye. Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa Mungu.”

Mathayo 11:28-30 “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu; kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi.”

Warumi 8:28-30 “Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake. Maana wale aliowajua tangu asili, aliwachagua tangu asili wafananishwe na mfano wa Mwana wake, ili yeye awe mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi. Na wale aliowachagua tangu asili, hao akawaita; na wale aliowaita, hao akawahesabia haki; na wale aliowahesabia haki, hao akawatukuza.”

Wito katika wokovu ni mwaliko wa jumla kwa jamii ya watu wote duniani wa kila kabila, na kila taifa na kila tamaduni na lugha na imani, wote wanapewa mwaliko wa kumpokea Yesu Kama Bwana na mwokozi wa maisha yao baada ya kuisikia injili na kuiamini na wote wanaopokea mwito huu kwa hiyari yao bila kulazimishwa wanafanyika kuwa watoto wa Mungu

Yohana 1:12-13 “Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake; waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu.”

Wito huu pamoja na mambo mengine pia unajumuisha kuishi maisha matakatifu na kuwa na ushirika na Mungu kumfanania Yesu Kristo na kuwa na tabia au mwenendo mwema kama yeye aliyetuita alivyo kwa hiyo kila aliyeokoka anawajibu wa kuukulia wokovu, kukomaa na kuwa kama Yesu Kristo mwenyewe alivyokua, wito huu ni wa toba, ni wito wa utakatifu, ni wito wa kupumzishwa na kusamehewa dhambi na kurudishwa katika familia ya Mungu na kuwa na uhusiano naye na kumuabudu

1Petro 1:14-16 “Kama watoto wa kutii msijifananishe na tamaa zenu za kwanza za ujinga wenu; bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote; kwa maana imeandikwa, Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu.”

Wito wa jumla katika huduma.

Wakati msingi wa wito wa kwanza ni kutengeneza mahusiano yetu na Mungu, mojawapo ya majukumu yetu vile vile ni kumtumikia Mungu, kila mtu aliyeokoka ameitwa kumtumikia Mungu kwa hivyo wote tuliookolewa pia tuna wajibu wa kumtumikia Mungu katika majukumu mbalimbali katika mwili wa Kristo, wito huu ni wito wa jumla kwa watu waliookoka unaowekwa na Roho Mtakatifu ndani yetu na kutubebesha majukumu ya jumla katika kuonyesha upendo kwa wengine, kumtii Mungu, kumuabudu na kuwashirikisha wengine imani yetu, wito huu unamuhusu kila mtu katika kanisa na sio viongozi au wachungaji peke yao wito huu unaonekana tangu nyakati za agano la kale.

Kumbukumbu 10:12-13 “Na sasa, Israeli, Bwana, Mungu wako, anataka nini kwako, ila umche Bwana, Mungu wako, na kwenda katika njia zake zote, na kumpenda, na kumtumikia Bwana, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote; kuzishika amri za Bwana na sheria zake, ninazokuamuru leo, upate uheri?

Zaburi 100:1-3 “Mfanyieni Bwana shangwe, dunia yote; Mtumikieni Bwana kwa furaha; Njoni mbele zake kwa kuimba; Jueni kwamba Bwana ndiye Mungu; Ndiye aliyetuumba na sisi tu watu wake; Tu watu wake, na kondoo wa malisho yake.”

Warumi 12:6-11 “Basi kwa kuwa tuna karama zilizo mbalimbali, kwa kadiri ya neema mliyopewa; ikiwa unabii, tutoe unabii kwa kadiri ya imani; ikiwa huduma, tuwemo katika huduma yetu; mwenye kufundisha, katika kufundisha kwake; mwenye kuonya, katika kuonya kwake; mwenye kukirimu, kwa moyo mweupe; mwenye kusimamia kwa bidii mwenye kurehemu, kwa furaha. Pendo na lisiwe na unafiki lichukieni lililo ovu, mkiambatana na lililo jema. Kwa pendo la udugu, mpendane ninyi kwa ninyi; kwa heshima mkiwatanguliza wenzenu; kwa bidii, si walegevu; mkiwa na juhudi katika roho zenu; mkimtumikia Bwana;”

Mathayo 28:18-20 “Yesu akaja kwao, akasema nao, akawaambia, Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.”

Unaona maandiko yana maagizo mengi ambapo kila mtu aliyeokolewa amepewa wajibu na anaagizwa kutumika, kila mtu aliyeokoka anaagizwa kuihubiri injili, anaagizwa kuomba anaagizwa kutoa anaagizwa kuwatumikia wengine anaagizwa kufungua na kupanda makanisa anaagizwa kufanya huduma zote, pamoja na mambo mengine tofauti ni kuwa watu hawa waliookolewa walioitwa katika wito wa ujumla watafanya kazi zao za kawaida huku wakifanya kazi za huduma kwa mujibu wa ratiba za maisha yao, na ratiba za kikanisa za kutumika kila iitwapo leo, aina hii ya wito ni wito wa ujumla katika wokovu ambapo waamini wanaagizwa kutumia vipawa vyao kumtumikia Mungu kwa  kadiri ya neema, wito huu unajumuisha kumuwakilisha Mungu popote tulipo pia iwe ni nyumbani au kazini au shuleni wewe ni wakili wa Yesu Kristo na unatumika pale ulipo kama chumvi na kama nuru.

Wito maalumu katika huduma

Wito huu au aina hii ya wito hutolewa kwa uwezo wa Roho Myakatifu kwa waamini kumuwezesha mtu huyo kusikia sauti ya Mungu kwa njia mbalimbali na kuamua kucha kila kitu hata kazi kwa kusudi la kumtumikia Mungu moja kwa moja katika kazi yake akiwa na huduma ya aidha mtume, au nabii, au mwinjilisti au mchungaji na au mwalimu aina hii pia ya huduma huwa inaambatana na huduma za kimaongozi katika kanisa na wakati mwingine karama mbalimbali za Roho Mtakatifu kuwawezesha watu hao kuuhudumia mwili wa Kristo kwa kuujenga na kuukamilisha

Waefeso 4:11-13 “Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu; kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe; hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani na kumfahamu sana Mwana wa Mungu, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo;”

Jinsi Mungu anavyoita watu katika huduma.

Linapokuja swala la wito maalumu katika huduma watu wengi sana huwa wanajiuliza nitajuaje kama nina wito, tunapojifunza kipengele hiki kinachozungumzia jinsi Mungu anavyoita watu katika huduma tutapata ufahamu namna na jinsi Mungu anavyosema nasi kuhususiana na wito wetu kujifunza kuhusu swala hili kutatusaidia kutembea kwa uhakika katika huduma tukiwa na uhakika kuwa hatukubahatisha katika swala zima la kumtumikia Mungu katika kazi hii maalumu, Neno la Mungu linaainisha njia mbalimbali ambazo Mungu alizitumia kuwaita watu wake katika wito maalumu

1.       Mungu anaweza kumuita mtu kwa sauti yake moja kwa moja  - wakati mwingine Mungu huwaita watumishi wake moja kwa moja kwa sauti yake katika mifumo anayoijua yeye mwenyewe  watumishi wa Mungu kama Musa, Samuel na Paulo waliitwa moja kwa moja katika huduma kwa kuisikia sauti ya Bwana  wazi wazi moja ona

 

Kutoka 3:1-10 “Basi huyo Musa alikuwa akilichunga kundi la Yethro mkwewe, kuhani wa Midiani; akaliongoza kundi nyuma ya jangwa, akafika mpaka mlima wa Mungu, hata Horebu. Malaika wa BWANA akamtokea, katika mwali wa moto uliotoka katikati ya kijiti; akatazama, na kumbe! Kile kijiti kiliwaka moto, nacho kijiti hakikuteketea. Musa akasema, Nitageuka sasa, niyaone maono haya makubwa, na sababu kijiti hiki hakiteketei. BWANA alipoona ya kuwa amegeuka ili atazame, Mungu akamwita kutoka katikati ya kile kijiti, akasema, Musa! Musa! Akasema, Mimi hapa. Naye akasema, Usikaribie hapa; vua viatu vyako miguuni mwako; maana mahali hapo unaposimama ni nchi takatifu. Tena akasema, Mimi ni Mungu wa baba yako, Mungu wa Ibrahimu, Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo. Musa akaficha uso wake; kwa maana aliogopa kumwangalia Mungu. BWANA akasema, Hakika nimeyaona mateso ya watu wangu walioko Misri, nami nimekisikia kilio chao kwa sababu ya wasimamizi wao; maana nayajua maumivu yao; nami nimeshuka ili niwaokoe na mikono ya Wamisri, niwapandishe kutoka nchi ile, hata nchi njema, kisha pana; nchi ijaayo maziwa na asali; hata mahali pa Mkanaani, na Mhiti, na Mwamori, na Mperizi, na Mhivi, na Myebusi. Basi, tazama, kilio cha wana wa Israeli kimenifikilia; tena nimeyaona hayo mateso ambayo Wamisri wanawatesa. Haya, basi, nitakutuma sasa kwa Farao, ili upate kuwatoa watu wangu, hao wana wa Israeli, katika Misri.”

 

1Samuel 3:1-10 “Basi, mtoto Samweli akamtumikia Bwana mbele ya Eli. Na neno la Bwana lilikuwa adimu siku zile; hapakuwa na mafunuo dhahiri. Ikawa wakati huo, Eli alipokuwa amelala mahali pake (tena macho yake yalikuwa yameanza kupofuka, hata asiweze kuona), na taa ya Mungu ilikuwa haijazimika bado, na Samweli alikuwa amelala katika hekalu la Bwana, palipokuwa na sanduku la Mungu; basi, wakati huo Bwana akamwita Samweli; naye akasema, Mimi hapa. Akamwendea Eli kwa haraka, akasema, Mimi hapa; kwa maana uliniita. Akasema, Sikukuita; kalale tena. Naye akaenda, akalala tena.Bwana akaita mara ya pili, Samweli! Samweli! Akaondoka akamwendea Eli, akasema, Mimi hapa; kwa maana uliniita. Akajibu, Sikukuita, mwanangu; kalale tena. Basi Samweli alikuwa hamjui Bwana bado, na neno la Bwana lilikuwa bado halijafunuliwa kwake. Bwana akamwita Samweli mara ya tatu. Naye akaondoka akamwendea Eli, akasema, Mimi hapa; kwa maana uliniita. Ndipo Eli akatambua ya kuwa Bwana ndiye aliyemwita yule mtoto. Kwa hivyo Eli akamwambia Samweli, Enenda, kalale; itakuwa, akikuita, utasema, Nena, Bwana; kwa kuwa mtumishi wako anasikia. Basi Samweli akaenda akalala mahali pake. Bwana akaja, akasimama, akaita vile vile kama kwanza, Samweli! Samweli! Ndipo Samweli akasema, Nena, Bwana; kwa kuwa mtumishi wako anasikia.”

 

Matendo 9:1-6 “Lakini Sauli, akizidi kutisha na kuwaza kuwaua wanafunzi wa Bwana, akamwendea Kuhani Mkuu, akataka ampe barua za kuenda Dameski zilizoandikwa kwa masinagogi, ili akiona watu wa Njia hii, waume kwa wake, awafunge na kuwaleta Yerusalemu. Hata alipokuwa akisafiri, ikawa anakaribia Dameski; ghafula ikamwangaza kote kote nuru kutoka mbinguni. Akaanguka chini, akasikia sauti ikimwambia, Sauli, Sauli, mbona waniudhi? Akasema, U nani wewe, Bwana? Naye akasema, Mimi ndimi Yesu unayeniudhi wewe. Lakini simama, uingie mjini, nawe utaambiwa yakupasayo kutenda.”

 

2.       Mungu anaweza kuita watumishi wake kupitia maono – Maandiko yanaonyesha kuwa kwa njia ya maono pia Mungu anaweza kumuita mtu katika kazi yake maalumu na ikawa na ufanisi mkubwa, Nabii Isaya alipokea wito wake kupitia Maono na Mungu alimtumia kwa kiwango kikubwa sana  

 

Isaya 6:1-10. “Katika mwaka ule aliokufa mfalme Uzia nalimwona Bwana ameketi katika kiti cha enzi, kilicho juu sana na kuinuliwa sana, na pindo za vazi lake zikalijaza hekalu. Juu yake walisimama maserafi; kila mmoja alikuwa na mabawa sita; kwa mawili alifunika uso wake, na kwa mawili alifunika miguu yake, na kwa mawili aliruka. Wakaitana, kila mmoja na mwenzake, wakisema, Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, ni Bwana wa majeshi; dunia yote imejaa utukufu wake. Na misingi ya vizingiti ikatikisika kwa sababu ya sauti yake aliyelia, nayo nyumba ikajaa moshi. Ndipo niliposema, Ole wangu! Kwa maana nimepotea; kwa sababu mimi ni mtu mwenye midomo michafu, nami ninakaa kati ya watu wenye midomo michafu; na macho yangu yamemwona Mfalme, Bwana wa majeshi.Kisha mmoja wa maserafi wale akaruka akanikaribia; naye alikuwa na kaa la moto mkononi mwake, ambalo alikuwa amelitwaa kwa makoleo toka juu ya madhabahu; akanigusa kinywa changu kwa kaa hilo, akaniambia, Tazama, hili limekugusa midomo yako, na uovu wako umeondolewa, na dhambi yako imefunikwa. Kisha nikaisikia sauti ya Bwana, akisema, Nimtume nani, naye ni nani atakayekwenda kwa ajili yetu? Ndipo niliposema, Mimi hapa, nitume mimi. Naye akaniambia, Enenda, ukawaambie watu hawa, Fulizeni kusikia, lakini msifahamu; fulizeni kutazama, lakini msione. Uunoneshe moyo wa watu hawa, ukayatie uzito masikio yao, ukayafumbe macho yao; wasije wakaona kwa macho yao, na kusikia kwa masikio yao, na kufahamu kwa mioyo yao, na kurejea na kuponywa.

 

3.       Mungu anaweza kuita watumishi wake kupitia ndoto – Mungu hutumia ndoto pia kufunua kusudu lake, mpango wake na agenda zake wito maalumu wa Yusufu ulifunuliwa kupitia ndoto mapema sana katika maisha yake tangu akiwa mdogo kuwa Mungu angemtumia, kupitia hili tunaweza kujifunza hapa na kutambua ya kuwa Mungu ameita baadhi ya watu wake kumtumikia kwa kutumia njia anazoona kuwa inafaa ikiwa ni pamoja na ndoto, Mungu anatumia njia ambayo muhusika ataelewa kwa urahisi au njia hiyo inaeleweka kwa mtu huyo.

 

Mwanzo 37:5-11 “Yusufu akaota ndoto, akawapa ndugu zake habari, nao wakazidi kumchukia; akawaambia, Tafadhalini, sikieni ndoto hii niliyoiota. Tazama, sisi tulikuwa tukifunga miganda shambani, kumbe! Mganda wangu ukaondoka ukasimama, na tazama, miganda yenu ikazunguka ikainama mbele ya mganda wangu. Ndugu zake wakamwambia, Je! Kweli wewe utatumiliki sisi? Nawe utatutawala sisi? Wakazidi kumchukia kwa ajili ya ndoto yake, na kwa maneno yake. Akaota tena ndoto nyingine, akawaambia ndugu zake, akasema, Angalieni, nimeota ndoto nyingine; na tazama, jua na mwezi na nyota kumi na moja zikaniinamia. Akawaambia baba yake na ndugu zake; baba yake akamkemea akamwambia, Ni ndoto gani hii uliyoiota? Je! Mimi na mama yako na ndugu zako tutakuja tukusujudie hata nchi? Ndugu zake wakamhusudu; bali baba yake akalihifadhi neno hili.”

 

4.       Mungu huweza kuita watumishi wake kupitia mtumishi wake au nabii – Wako watu kadhaa katika maandiko ambao waliitwa katika kazi maalumu kupitia manabii, Nabii alifunuliwa na kumtia mafuta yule aliyekusudiwa katika wito fulani, kwa mfano ufalme wa Sauli, au ufalme wa Daudi,  au  nabii Elisha hawa waliitwa kupitia nabii au mtumishi wa Mungu aliyekuwako wakati huo, wao kupitia ujuzi na sauti ya Roho Mtakatifu wanaweza kumjua na kumbaini mtu ambaye Mungu amemuita katika huduma  na akafaa kwaajili ya utumishi huo uliokusudiwa!

 

1Samuel 9:15-20 “Basi Bwana alikuwa amemfunulia Samweli, siku moja kabla Sauli hajamwendea, akisema, Kesho, wakati kama huu, nitakuletea mtu kutoka nchi ya Benyamini, nawe mtie mafuta ili awe mkuu juu ya watu wangu Israeli, naye atawaokoa watu wangu na mikono ya Wafilisti; maana nimewaangalia watu wangu, kwa sababu kilio chao kimenifikilia. Hata Samweli alipomwona Sauli, Bwana akamwambia, Huyu ndiye niliyekuambia habari zake; huyu ndiye atakayewamiliki watu wangu. Ndipo Sauli akamkaribia Samweli langoni, akasema, Tafadhali, uniambie, nyumba ya mwonaji iko wapi? Samweli akamjibu Sauli, akasema, Mimi ndimi mwonaji; tangulia mbele yangu ukwee mpaka mahali pa juu, kwa maana mtakula pamoja nami leo; kisha, asubuhi nitakuacha uende zako, nami nitakuambia yote uliyo nayo moyoni mwako. Na wale punda zako waliopotea siku hizi tatu, usijiudhi kwa ajili yao; maana wameonekana. Na yote yaliyotamanika katika Israeli amewekewa nani? Si wewe, na nyumba yote ya baba yako?

 

1Samuel 16:13 “Ndipo Samweli akaitwaa pembe yenye mafuta, akamtia mafuta kati ya ndugu zake; na roho ya Bwana ikamjilia Daudi kwa nguvu tangu siku ile. Basi Samweli akaondoka, akaenda zake Rama.”  

 

1Wafalme 19:19-21 “Basi, akaondoka huko, akamkuta Elisha mwana wa Shafati, aliyekuwa akilima, mwenye jozi za ng'ombe kumi na mbili mbele yake, na yeye mwenyewe alikuwa pamoja na lile la kumi na mbili. Eliya akapita karibu naye, akatupa vazi lake juu yake. Naye akawaacha ng'ombe, akamfuata Eliya mbio, akasema, Nipe ruhusa, nakuomba, nimbusu baba yangu na mama yangu, kisha mimi nitakufuata. Akamwambia, Enenda, urudi; ni nini niliyokutendea? Akarudi akiacha kumfuata, akatwaa lile jozi la ng'ombe, akawachinja, akatokosa nyama zao kwa ile miti ya ng'ombe, akawapa watu, wakala. Kisha akainuka, akamfuata Eliya, akamhudumia.”

 

5.       Mungu huweza kuwaita watumishi wake kupitia malaika – Wakati mwingine Mungu humtuma malaika wake kuweza kuwasilisha ujumbe wa jukumu lake kwa mtumishi wake anayekusudiwa, Katika maandikio iko mifano mingi lakini tutaangalia mifano michache ya watu kadhaa kama Gideoni na Mariam mama yake Yesu ambao walipewa kazi maalumu kwa ujumbe wa malaika

 

Waamuzi 6:11-14 “Malaika wa Bwana akaenda akaketi chini ya mwaloni uliokuwa katika Ofra, uliokuwa mali yake Yoashi, Mwabiezeri; na mwanawe Gideoni alikuwa akipepeta ngano ndani ya shinikizo, ili kuificha machoni pa Wamidiani. Malaika wa Bwana akamtokea, akamwambia, Bwana yu pamoja nawe, Ee shujaa. Gideoni akamwambia, Ee Bwana wangu, ikiwa Bwana yu pamoja nasi, mbona mambo haya yote yametupata? Yako wapi matendo yake ya ajabu, waliyotuhadithia baba zetu, wakisema, Je! Siye Bwana, aliyetuleta huku kutoka Misri? Ila sasa ametutupa, naye ametutia katika mikono ya Midiani. Bwana akamtazama, akasema, Enenda kwa uwezo wako huu, ukawaokoe Israeli na mkono wa Midiani. Je! Si mimi ninayekutuma? 

 

Luka 1:26-33 “Mwezi wa sita, malaika Gabrieli alitumwa na Mungu kwenda mpaka mji wa Galilaya, jina lake Nazareti, kwa mwanamwali bikira aliyekuwa ameposwa na mtu, jina lake Yusufu, wa mbari ya Daudi; na jina lake bikira huyo ni Mariamu. Akaingia nyumbani kwake akasema, Salamu, uliyepewa neema, Bwana yu pamoja nawe. Naye akafadhaika sana kwa ajili ya maneno yake, akawaza moyoni, Salamu hii ni ya namna gani? Malaika akamwambia, Usiogope, Mariamu, kwa maana umepata neema kwa Mungu. Tazama, utachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; na jina lake utamwita Yesu. Huyo atakuwa mkuu, ataitwa Mwana wa Aliye juu, na Bwana Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi, baba yake. Ataimiliki nyumba ya Yakobo hata milele, na ufalme wake utakuwa hauna mwisho.”

 

6.       Mungu huweza kuwaita watumishi wake kupitia Roho wake Mtakatifu – Ikumbukwe kuwa njia zote hizo Roho Mtakatifu ambaye ndiye Bwana wa mavuno anazitumia katika kuhakikisha kuwa wanapatikana watenda kazi katika mashamba yake lakini hutokea wakati mwingine mwenyewe akazungumza moja kwa moja kwa njia ya unabii na kumuita au kumtaka mtu katika huduma maalumu

 

Matendo 13:1-3 “Na huko Antiokia katika kanisa lililokuwako palikuwa na manabii na waalimu, nao ni Barnaba, na Simeoni aitwaye Nigeri, na Lukio Mkirene, na Manaeni aliyekuwa ndugu wa kunyonya wa mfalme Herode, na Sauli. Basi hawa walipokuwa wakimfanyia Bwana ibada na kufunga, Roho Mtakatifu akasema, Nitengeeni Barnaba na Sauli kwa kazi ile niliyowaitia. Ndipo wakiisha kufunga na kuomba, wakaweka mikono yao juu yao, wakawaacha waende zao.”

 

7.       Mungu huweza kuwaita watumishi wake Kupitia Yesu Kristo mwenyewe – Wanafunzi wale kumi na wawili walikuwa ni chaguo la Yesu Kristo mwenyewe na aliwaita kama alivyopenda yeye mwenyewe hata sasa Yesu Kristo bado anaita watu wake kama apendavyo kwa njia mbalimbali na wakati mwingine yeye mwenyewe. Hata hivyo ni muhimu kuelewa kuwa katika njia hizo zote hakuna iliyobora zaidi kuliko nyingine kwa sababu zote ni njia ambazo yeye mwenyewe anazitumia kuwapata watu wa kumtumikia katika huduma maalumu, kwa hoyo mtumishi aliyetokewa na Yesu mwenyewe na kuitwa katika wito haimaanishi kuwa anaubora kushinda aliyeitwa kwa njia nyingine, kwani kimaandiko hizo zote ni nnia anazozitumia Mungu kufahamisha watu wake namna anavyowahitaji katika huduma.

 

Mathayo 4:18-19 “Naye alipokuwa akitembea kando ya bahari ya Galilaya, aliona ndugu wawili, Simoni aitwaye Petro, na Andrea nduguye, wakitupa jarife baharini; kwa maana walikuwa wavuvi. Akawaambia, Nifuateni, nami nitawafanya kuwa wavuvi wa watu.Mara wakaziacha nyavu zao, wakamfuata.”

 

Mathayo 9:9. “Naye Yesu alipokuwa akipita kutoka huko aliona mtu ameketi forodhani, aitwaye Mathayo, akamwambia, Nifuate. Akaondoka, akamfuata.”                                    

Kwa hiyo tunajifunza kuwa ni Mungu mwenyewe ndiye anayeita watu wake katika huduma, na kwa sababu hiyo hakuna mtu ajitwaliaye heshima hii, wakati Mungu anapomuita mtu kwaajili ya huduma mtu huyo huwekewa kitu cha ziada na neema ya juu zaidi ili aweze kuwahudumia wengine, Hata hivyo bado hatuwezi kuwaachia hao peke yao walioitwa katika wito maalumu wa huduma kwa sababu kazi ya Mungu ni pana na hivyo wale wote ambao hawatakuwa wameitwa katika wito maalumu wanabaki katika wito wa ujumla wa kumtumikia Mungu na wakifanya kwa uaminifu na utii kazi ya Mungu itasonga mbele na kuwa Baraka kubwa kwa jamii, Unaweza kujua wito wako kupitia neno la Mungu, kupitia maombi, kupitia shuhuda za huduma za watu unao wahudumia, kuthibitishwa na viongozi, na amani ya moyo, wito ni zawadi, wito ni heshima, wito ni kuaminiwa, wito ni wajibu na kwa sababu hiyo kama Mungu amekuweka katika ajenda zake basi wewe ni wa muhimu sana itikia sauti ya Mungu leo ukamtumikie.

Yohana 12:26 “Yeye aipendaye nafsi yake ataiangamiza; naye aichukiaye nafsi yake katika ulimwengu huu ataisalimisha hata uzima wa milele.Mtu akinitumikia, na anifuate; nami nilipo, ndipo na mtumishi wangu atakapokuwapo. Tena mtu akinitumikia, Baba atamheshimu.”

Waebrania 3:14-15 “Kwa maana tumekuwa washirika wa Kristo, kama tukishikamana na mwanzo wa uthabiti wetu kwa nguvu mpaka mwisho; hapo inenwapo, Leo, kama mtaisikia sauti yake, Msifanye migumu mioyo yenu, Kama wakati wa kukasirisha.”                    

Na Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni