Matendo 13:1-3 “Na huko Antiokia katika
kanisa lililokuwako palikuwa na manabii na waalimu, nao ni Barnaba, na Simeoni
aitwaye Nigeri, na Lukio Mkirene, na Manaeni aliyekuwa ndugu wa kunyonya wa
mfalme Herode, na Sauli. Basi hawa walipokuwa wakimfanyia Bwana ibada na kufunga,
Roho Mtakatifu akasema, Nitengeeni Barnaba na Sauli kwa kazi ile niliyowaitia.
Ndipo wakiisha kufunga na kuomba, wakaweka mikono yao juu yao, wakawaacha
waende zao.”
Ni muhimu kufahamu kuwa Mungu
anatoa wito kwa watu wake wote kuhakikisha ya kuwa wanamtumikia, Neno wito
linamaanisha kualikwa na Mungu ili tuweze kutekeleza ajenda zake au kusudi lake
ambalo amelikusudia yeye mwenyewe sawasawa na maagizo yaliyomo katika neno lake,
Mungu huchagua watu wake wale anaowataka mwenyewe na kuwaalika wawe na ushirika
naye na kisha awatume katika kazi yake ili kutekeleza mapenzi yake, kusudi lake
na kazi yake hapa duniani na kwa sababu hiyo kuitikia wito wa kumtumikia Mungu
ni utii usio na mashart
Marko 3:13-15 “Akapanda mlimani, akawaita
aliowataka mwenyewe; wakamwendea. Akaweka watu kumi na wawili, wapate kuwa
pamoja naye, na kwamba awatume kuhubiri, tena wawe na amri ya kutoa pepo.”
Kwa hiyo tangu nyakati za agano
la kale Mungu amekuwa na tabia ya kuwaita na kuwachagua watu aliowataka
mwenyewe kwaajili ya kutekeleza majukumu na makusudi yake yeye mwenyewe
duniani, Kwa msingi huo kila mtu aliyeokoka anapaswa kuwa makini kumtumikia
Mungu na kusikiliza sauti ya Mungu ili kutambua mapenzi ya Mungu katika maisha
yake na kuwajibika mara moja katika kazi hii yenye Baraka na heshima kubwa, kwa
bahati mbaya watu wengi sana hawapendi kumtumikia Mungu katika huduma
mbalimbali Kanisani kwa kisingizio kuwa hawajaitwa, au kwa kutokuwa na ufahamu
wanawajibika vipi, kwa hiyo leo tutachukua Muda kujifunza na kutafakari kwa
pamoja somo hili muhimu kuhusu wito wa kumtumikia Mungu katika huduma kwa
kuzingatia vipengele vikuu vitatu vifuatavyo:-
·
Maana ya neno
wito katika maandiko.
·
Aina kuu
tatu za wito katika huduma.
·
Jinsi
Mungu anavyoita watu katika huduma.
Maana ya neno wito katika maandiko.
Ni muhimu kufahamu kuwa neno wito
katika maandiko lina tajwa kwa lugha ya Kiebrania kwa neno “qara” na linatajwa kwa kiyunani kama neno “Kaleō”
au “klēsis” ikimaanisha kuitwa,
kutengwa, kuchaguliwa au kuteuliwa na Mungu kwa kusudi la kutimiza majukumu
maalumu katika ajenda za Mungu, Kwa sababu hiyo wito sio mpango wala wazo la
kibinadamu au shauku binafsi bali ni mpango kamili wa Mungu juu ya maisha ya
mtu katika kusudi lake au kwa kazi maalumu, kwa hiyo wito katika huduma ni mualiko
wa kumtumikia Mungu au kufanya kazi pamoja na Mungu katika kutimiza kusudi lake
au ajenda zake mwenyewe hapa duniani kwa wakati maalumu.
Luka 5:27-29 “Baada ya hayo akatoka, akaona
mtoza ushuru, jina lake Lawi, ameketi forodhani, akamwambia, Nifuate. Akaacha
vyote, akaondoka, akamfuata. Na Lawi akamfanyia karamu kubwa nyumbani mwake;
palikuwa na mkutano mkuu wa watoza ushuru na watu wengineo waliokuwa wameketi
chakulani pamoja nao.”
Msingi mkuu wa Mungu anapomuita
mtu kwanza anataka ushirika wa karibu na mtu huyo kisha ndipo amtume, kwa hiyo
mtu aliyeitwa na aliyeitikia wito wa kumtumikia Mungu katika huduma anapaswa
kuwa mtu mwenye ushirika wa karibu na Mungu, ushirika huu ni wa muhimu hata
kabla ya kazi yenyewe
Yohana 21:15-17 “Basi walipokwisha kula, Yesu
akamwambia Simoni Petro, Je! Simoni wa Yohana, wewe wanipenda kuliko hawa?
Akamwambia, Naam, Bwana, wewe wajua kuwa nakupenda. Akamwambia, Lisha
wana-kondoo wangu. Akamwambia tena mara ya pili, Simoni wa Yohana, wanipenda?
Akamwambia, Ndiyo, Bwana, wewe wajua kuwa nakupenda. Akamwambia, Chunga kondoo
zangu. Akamwambia mara ya tatu, Simoni wa Yohana, wanipenda? Petro alihuzunika
kwa vile alivyomwambia mara ya tatu, Wanipenda? Akamwambia, Bwana, wewe wajua yote;
wewe umetambua ya kuwa nakupenda. Yesu akamwambia, Lisha kondoo zangu.”
Marko 3:13-15 “Akapanda mlimani, akawaita
aliowataka mwenyewe; wakamwendea. Akaweka watu kumi na wawili, wapate kuwa
pamoja naye, na kwamba awatume kuhubiri, tena wawe na amri ya kutoa pepo.”
Kabla Mungu hajamuita mtu anataka
ushirika na wewe anataka upendo wako na anataka uwe pamoja naye kisha ndipo
akutume kuhubiri na kutoa pepo au kufanya huduma nyinginezo kwa niaba yake
Aina kuu tatu za wito katika huduma.
Maandiko matakatifu yanaonyesha
kuwa Mungu aliwaita watu kwa namna mbalimbali na kwaajili ya shughuli
mbalimbali, kwa hiyo tunapozungumzia swala la wito tunazungumzia mada pana sana
katika nyanja zote za kisiasa, kijamii na kiimani, na kisayansi, ukichunguza
kwa kina utaweza kuona kuwa kote huko Mungu hufanya kazi ya kuwaita watu
kwaajili ya makusudi mbalimbali, kwa hiyo wito hauko katika kuta za kanisa
pekee unavuka mipaka na kwenda mbali zaidi ya vile tunavyofikiri, hata hivyo
katika somo hili nataka kuzungumzia wito ambao unaishia ndani ya mipaka ya
Kanisa pekee aina hizi za wito naweza kugawa katika makundi makuu muhimu matatu
yafuatayo:-
·
Wito wa jumla
katika wokovu
·
Wito wa
jumla katika huduma
·
Wito
maalumu katika huduma
Wito wa jumla katika wokovu – Wito huu wa ujumla katika wokovu ni
wito unaotolewa na Mungu Roho Mtakatifu kwa jamii ya watu wote duniani ili
wamuamini Bwana wetu Yesu Kristo kama mwokozi wao na kupokea uzima wa milele,
huu ni wito unaotolewa kwa watu wote wamgeukie Mungu wamrudie yeye wamche yeye
na kuwa na ushirika na yeye kwa hiyo
watu wote duniani wanaalikwa kila iitwapo leo kupokea wito huu wa wokovu kwa
imani.
Yohana 3:16-18 “Kwa maana jinsi hii Mungu
aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye
asipotee, bali awe na uzima wa milele. Maana Mungu hakumtuma Mwana ulimwenguni
ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye. Amwaminiye yeye hahukumiwi;
asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa
Mungu.”
Mathayo 11:28-30 “Njoni kwangu, ninyi nyote
msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jitieni nira yangu,
mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata
raha nafsini mwenu; kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi.”
Warumi 8:28-30 “Nasi twajua ya kuwa katika
mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema,
yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake. Maana wale aliowajua tangu asili,
aliwachagua tangu asili wafananishwe na mfano wa Mwana wake, ili yeye awe
mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi. Na wale aliowachagua tangu asili,
hao akawaita; na wale aliowaita, hao akawahesabia haki; na wale aliowahesabia
haki, hao akawatukuza.”
Wito katika wokovu ni mwaliko wa
jumla kwa jamii ya watu wote duniani wa kila kabila, na kila taifa na kila
tamaduni na lugha na imani, wote wanapewa mwaliko wa kumpokea Yesu Kama Bwana
na mwokozi wa maisha yao baada ya kuisikia injili na kuiamini na wote
wanaopokea mwito huu kwa hiyari yao bila kulazimishwa wanafanyika kuwa watoto
wa Mungu
Yohana 1:12-13 “Bali wote waliompokea
aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake;
waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya
mtu, bali kwa Mungu.”
Wito huu pamoja na mambo mengine
pia unajumuisha kuishi maisha matakatifu na kuwa na ushirika na Mungu
kumfanania Yesu Kristo na kuwa na tabia au mwenendo mwema kama yeye aliyetuita
alivyo kwa hiyo kila aliyeokoka anawajibu wa kuukulia wokovu, kukomaa na kuwa
kama Yesu Kristo mwenyewe alivyokua, wito huu ni wa toba, ni wito wa utakatifu,
ni wito wa kupumzishwa na kusamehewa dhambi na kurudishwa katika familia ya
Mungu na kuwa na uhusiano naye na kumuabudu
1Petro 1:14-16 “Kama watoto wa kutii
msijifananishe na tamaa zenu za kwanza za ujinga wenu; bali kama yeye
aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu
wote; kwa maana imeandikwa, Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu.”
Wito wa jumla katika huduma.
Wakati msingi wa wito wa kwanza
ni kutengeneza mahusiano yetu na Mungu, mojawapo ya majukumu yetu vile vile ni
kumtumikia Mungu, kila mtu aliyeokoka ameitwa kumtumikia Mungu kwa hivyo wote
tuliookolewa pia tuna wajibu wa kumtumikia Mungu katika majukumu mbalimbali
katika mwili wa Kristo, wito huu ni wito wa jumla kwa watu waliookoka unaowekwa
na Roho Mtakatifu ndani yetu na kutubebesha majukumu ya jumla katika kuonyesha
upendo kwa wengine, kumtii Mungu, kumuabudu na kuwashirikisha wengine imani
yetu, wito huu unamuhusu kila mtu katika kanisa na sio viongozi au wachungaji
peke yao wito huu unaonekana tangu nyakati za agano la kale.
Kumbukumbu 10:12-13 “Na sasa, Israeli,
Bwana, Mungu wako, anataka nini kwako, ila umche Bwana, Mungu wako, na kwenda
katika njia zake zote, na kumpenda, na kumtumikia Bwana, Mungu wako, kwa moyo
wako wote, na kwa roho yako yote; kuzishika amri za Bwana na sheria zake,
ninazokuamuru leo, upate uheri? ”
Zaburi 100:1-3 “Mfanyieni Bwana shangwe,
dunia yote; Mtumikieni Bwana kwa furaha; Njoni mbele zake kwa kuimba; Jueni
kwamba Bwana ndiye Mungu; Ndiye aliyetuumba na sisi tu watu wake; Tu watu wake,
na kondoo wa malisho yake.”
Warumi 12:6-11 “Basi kwa kuwa tuna karama
zilizo mbalimbali, kwa kadiri ya neema mliyopewa; ikiwa unabii, tutoe unabii
kwa kadiri ya imani; ikiwa huduma, tuwemo katika huduma yetu; mwenye
kufundisha, katika kufundisha kwake; mwenye kuonya, katika kuonya kwake; mwenye
kukirimu, kwa moyo mweupe; mwenye kusimamia kwa bidii mwenye kurehemu, kwa
furaha. Pendo na lisiwe na unafiki lichukieni lililo ovu, mkiambatana na lililo
jema. Kwa pendo la udugu, mpendane ninyi kwa ninyi; kwa heshima mkiwatanguliza
wenzenu; kwa bidii, si walegevu; mkiwa na juhudi katika roho zenu; mkimtumikia
Bwana;”
Mathayo 28:18-20 “Yesu akaja kwao, akasema
nao, akawaambia, Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. Basi, enendeni,
mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana,
na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na
tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari.”
Unaona maandiko yana maagizo
mengi ambapo kila mtu aliyeokolewa amepewa wajibu na anaagizwa kutumika, kila
mtu aliyeokoka anaagizwa kuihubiri injili, anaagizwa kuomba anaagizwa kutoa
anaagizwa kuwatumikia wengine anaagizwa kufungua na kupanda makanisa anaagizwa
kufanya huduma zote, pamoja na mambo mengine tofauti ni kuwa watu hawa
waliookolewa walioitwa katika wito wa ujumla watafanya kazi zao za kawaida huku
wakifanya kazi za huduma kwa mujibu wa ratiba za maisha yao, na ratiba za
kikanisa za kutumika kila iitwapo leo, aina hii ya wito ni wito wa ujumla
katika wokovu ambapo waamini wanaagizwa kutumia vipawa vyao kumtumikia Mungu
kwa kadiri ya neema, wito huu
unajumuisha kumuwakilisha Mungu popote tulipo pia iwe ni nyumbani au kazini au
shuleni wewe ni wakili wa Yesu Kristo na unatumika pale ulipo kama chumvi na
kama nuru.
Wito maalumu katika huduma
Wito huu au aina hii ya wito
hutolewa kwa uwezo wa Roho Myakatifu kwa waamini kumuwezesha mtu huyo kusikia
sauti ya Mungu kwa njia mbalimbali na kuamua kucha kila kitu hata kazi kwa
kusudi la kumtumikia Mungu moja kwa moja katika kazi yake akiwa na huduma ya
aidha mtume, au nabii, au mwinjilisti au mchungaji na au mwalimu aina hii pia
ya huduma huwa inaambatana na huduma za kimaongozi katika kanisa na wakati
mwingine karama mbalimbali za Roho Mtakatifu kuwawezesha watu hao kuuhudumia
mwili wa Kristo kwa kuujenga na kuukamilisha
Waefeso 4:11-13 “Naye alitoa wengine kuwa
mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji
na waalimu; kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma
itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe; hata na sisi sote tutakapoufikia umoja
wa imani na kumfahamu sana Mwana wa Mungu, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika
kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo;”
Jinsi Mungu anavyoita watu katika huduma.
Linapokuja swala la wito maalumu
katika huduma watu wengi sana huwa wanajiuliza nitajuaje kama nina wito,
tunapojifunza kipengele hiki kinachozungumzia jinsi Mungu anavyoita watu katika
huduma tutapata ufahamu namna na jinsi Mungu anavyosema nasi kuhususiana na
wito wetu kujifunza kuhusu swala hili kutatusaidia kutembea kwa uhakika katika
huduma tukiwa na uhakika kuwa hatukubahatisha katika swala zima la kumtumikia
Mungu katika kazi hii maalumu, Neno la Mungu linaainisha njia mbalimbali ambazo
Mungu alizitumia kuwaita watu wake katika wito maalumu
1.
Mungu
anaweza kumuita mtu kwa sauti yake moja kwa moja - wakati mwingine Mungu huwaita watumishi
wake moja kwa moja kwa sauti yake katika mifumo anayoijua yeye mwenyewe watumishi wa Mungu kama Musa, Samuel na Paulo
waliitwa moja kwa moja katika huduma kwa kuisikia sauti ya Bwana wazi wazi moja ona
Kutoka 3:1-10 “Basi huyo Musa alikuwa akilichunga kundi la Yethro
mkwewe, kuhani wa Midiani; akaliongoza kundi nyuma ya jangwa, akafika mpaka
mlima wa Mungu, hata Horebu. Malaika wa BWANA akamtokea, katika mwali wa moto
uliotoka katikati ya kijiti; akatazama, na kumbe! Kile kijiti kiliwaka moto,
nacho kijiti hakikuteketea. Musa akasema, Nitageuka sasa, niyaone maono haya
makubwa, na sababu kijiti hiki hakiteketei. BWANA alipoona ya kuwa amegeuka ili
atazame, Mungu akamwita kutoka katikati ya kile kijiti, akasema, Musa! Musa!
Akasema, Mimi hapa. Naye akasema, Usikaribie hapa; vua viatu vyako miguuni
mwako; maana mahali hapo unaposimama ni nchi takatifu. Tena akasema, Mimi ni
Mungu wa baba yako, Mungu wa Ibrahimu, Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo. Musa
akaficha uso wake; kwa maana aliogopa kumwangalia Mungu. BWANA akasema, Hakika
nimeyaona mateso ya watu wangu walioko Misri, nami nimekisikia kilio chao kwa
sababu ya wasimamizi wao; maana nayajua maumivu yao; nami nimeshuka ili
niwaokoe na mikono ya Wamisri, niwapandishe kutoka nchi ile, hata nchi njema,
kisha pana; nchi ijaayo maziwa na asali; hata mahali pa Mkanaani, na Mhiti, na
Mwamori, na Mperizi, na Mhivi, na Myebusi. Basi, tazama, kilio cha wana wa
Israeli kimenifikilia; tena nimeyaona hayo mateso ambayo Wamisri wanawatesa.
Haya, basi, nitakutuma sasa kwa Farao, ili upate kuwatoa watu wangu, hao wana
wa Israeli, katika Misri.”
1Samuel 3:1-10
“Basi, mtoto Samweli akamtumikia Bwana mbele ya
Eli. Na neno la Bwana lilikuwa adimu siku zile; hapakuwa na mafunuo dhahiri.
Ikawa wakati huo, Eli alipokuwa amelala mahali pake (tena macho yake yalikuwa
yameanza kupofuka, hata asiweze kuona), na taa ya Mungu ilikuwa haijazimika
bado, na Samweli alikuwa amelala katika hekalu la Bwana, palipokuwa na sanduku
la Mungu; basi, wakati huo Bwana akamwita Samweli; naye akasema, Mimi hapa.
Akamwendea Eli kwa haraka, akasema, Mimi hapa; kwa maana uliniita. Akasema,
Sikukuita; kalale tena. Naye akaenda, akalala tena.Bwana akaita mara ya pili,
Samweli! Samweli! Akaondoka akamwendea Eli, akasema, Mimi hapa; kwa maana
uliniita. Akajibu, Sikukuita, mwanangu; kalale tena. Basi Samweli alikuwa
hamjui Bwana bado, na neno la Bwana lilikuwa bado halijafunuliwa kwake. Bwana
akamwita Samweli mara ya tatu. Naye akaondoka akamwendea Eli, akasema, Mimi
hapa; kwa maana uliniita. Ndipo Eli akatambua ya kuwa Bwana ndiye aliyemwita
yule mtoto. Kwa hivyo Eli akamwambia Samweli, Enenda, kalale; itakuwa,
akikuita, utasema, Nena, Bwana; kwa kuwa mtumishi wako anasikia. Basi Samweli
akaenda akalala mahali pake. Bwana akaja, akasimama, akaita vile vile kama
kwanza, Samweli! Samweli! Ndipo Samweli akasema, Nena, Bwana; kwa kuwa mtumishi
wako anasikia.”
Matendo 9:1-6 “Lakini Sauli, akizidi kutisha na kuwaza kuwaua wanafunzi
wa Bwana, akamwendea Kuhani Mkuu, akataka ampe barua za kuenda Dameski
zilizoandikwa kwa masinagogi, ili akiona watu wa Njia hii, waume kwa wake,
awafunge na kuwaleta Yerusalemu. Hata alipokuwa akisafiri, ikawa anakaribia
Dameski; ghafula ikamwangaza kote kote nuru kutoka mbinguni. Akaanguka chini,
akasikia sauti ikimwambia, Sauli, Sauli, mbona waniudhi? Akasema, U nani wewe,
Bwana? Naye akasema, Mimi ndimi Yesu unayeniudhi wewe. Lakini simama, uingie
mjini, nawe utaambiwa yakupasayo kutenda.”
2. Mungu anaweza kuita watumishi wake kupitia
maono – Maandiko yanaonyesha kuwa kwa njia ya maono pia Mungu anaweza
kumuita mtu katika kazi yake maalumu na ikawa na ufanisi mkubwa, Nabii Isaya
alipokea wito wake kupitia Maono na Mungu alimtumia kwa kiwango kikubwa sana
Isaya 6:1-10. “Katika mwaka ule aliokufa mfalme Uzia nalimwona Bwana
ameketi katika kiti cha enzi, kilicho juu sana na kuinuliwa sana, na pindo za
vazi lake zikalijaza hekalu. Juu yake walisimama maserafi; kila mmoja alikuwa
na mabawa sita; kwa mawili alifunika uso wake, na kwa mawili alifunika miguu
yake, na kwa mawili aliruka. Wakaitana, kila mmoja na mwenzake, wakisema,
Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, ni Bwana wa majeshi; dunia yote imejaa utukufu
wake. Na misingi ya vizingiti ikatikisika kwa sababu ya sauti yake aliyelia,
nayo nyumba ikajaa moshi. Ndipo niliposema, Ole wangu! Kwa maana nimepotea; kwa
sababu mimi ni mtu mwenye midomo michafu, nami ninakaa kati ya watu wenye
midomo michafu; na macho yangu yamemwona Mfalme, Bwana wa majeshi.Kisha mmoja
wa maserafi wale akaruka akanikaribia; naye alikuwa na kaa la moto mkononi
mwake, ambalo alikuwa amelitwaa kwa makoleo toka juu ya madhabahu; akanigusa
kinywa changu kwa kaa hilo, akaniambia, Tazama, hili limekugusa midomo yako, na
uovu wako umeondolewa, na dhambi yako imefunikwa. Kisha nikaisikia sauti ya
Bwana, akisema, Nimtume nani, naye ni nani atakayekwenda kwa ajili yetu? Ndipo
niliposema, Mimi hapa, nitume mimi. Naye akaniambia, Enenda, ukawaambie watu
hawa, Fulizeni kusikia, lakini msifahamu; fulizeni kutazama, lakini msione.
Uunoneshe moyo wa watu hawa, ukayatie uzito masikio yao, ukayafumbe macho yao;
wasije wakaona kwa macho yao, na kusikia kwa masikio yao, na kufahamu kwa mioyo
yao, na kurejea na kuponywa.”
3. Mungu anaweza kuita watumishi wake kupitia
ndoto – Mungu hutumia ndoto pia kufunua kusudu lake, mpango wake na agenda
zake wito maalumu wa Yusufu ulifunuliwa kupitia ndoto mapema sana katika maisha
yake tangu akiwa mdogo kuwa Mungu angemtumia, kupitia hili tunaweza kujifunza
hapa na kutambua ya kuwa Mungu ameita baadhi ya watu wake kumtumikia kwa
kutumia njia anazoona kuwa inafaa ikiwa ni pamoja na ndoto, Mungu anatumia njia ambayo muhusika ataelewa kwa urahisi au njia
hiyo inaeleweka kwa mtu huyo.
Mwanzo 37:5-11
“Yusufu akaota ndoto, akawapa ndugu zake habari,
nao wakazidi kumchukia; akawaambia, Tafadhalini, sikieni ndoto hii niliyoiota. Tazama,
sisi tulikuwa tukifunga miganda shambani, kumbe! Mganda wangu ukaondoka
ukasimama, na tazama, miganda yenu ikazunguka ikainama mbele ya mganda wangu. Ndugu
zake wakamwambia, Je! Kweli wewe utatumiliki sisi? Nawe utatutawala sisi?
Wakazidi kumchukia kwa ajili ya ndoto yake, na kwa maneno yake. Akaota tena
ndoto nyingine, akawaambia ndugu zake, akasema, Angalieni, nimeota ndoto
nyingine; na tazama, jua na mwezi na nyota kumi na moja zikaniinamia. Akawaambia
baba yake na ndugu zake; baba yake akamkemea akamwambia, Ni ndoto gani hii
uliyoiota? Je! Mimi na mama yako na ndugu zako tutakuja tukusujudie hata nchi? Ndugu
zake wakamhusudu; bali baba yake akalihifadhi neno hili.”
4. Mungu huweza kuita watumishi wake kupitia
mtumishi wake au nabii – Wako watu kadhaa katika maandiko ambao waliitwa
katika kazi maalumu kupitia manabii, Nabii alifunuliwa na kumtia mafuta yule
aliyekusudiwa katika wito fulani, kwa mfano ufalme wa Sauli, au ufalme wa
Daudi, au nabii Elisha hawa waliitwa kupitia nabii au
mtumishi wa Mungu aliyekuwako wakati huo, wao kupitia ujuzi na sauti ya Roho Mtakatifu
wanaweza kumjua na kumbaini mtu ambaye Mungu amemuita katika huduma na
akafaa kwaajili ya utumishi huo uliokusudiwa!
1Samuel 9:15-20
“Basi Bwana alikuwa amemfunulia Samweli, siku moja
kabla Sauli hajamwendea, akisema, Kesho, wakati kama huu, nitakuletea mtu
kutoka nchi ya Benyamini, nawe mtie mafuta ili awe mkuu juu ya watu wangu
Israeli, naye atawaokoa watu wangu na mikono ya Wafilisti; maana nimewaangalia
watu wangu, kwa sababu kilio chao kimenifikilia. Hata Samweli alipomwona Sauli,
Bwana akamwambia, Huyu ndiye niliyekuambia habari zake; huyu ndiye
atakayewamiliki watu wangu. Ndipo Sauli akamkaribia Samweli langoni, akasema,
Tafadhali, uniambie, nyumba ya mwonaji iko wapi? Samweli akamjibu Sauli,
akasema, Mimi ndimi mwonaji; tangulia mbele yangu ukwee mpaka mahali pa juu,
kwa maana mtakula pamoja nami leo; kisha, asubuhi nitakuacha uende zako, nami
nitakuambia yote uliyo nayo moyoni mwako. Na wale punda zako waliopotea siku
hizi tatu, usijiudhi kwa ajili yao; maana wameonekana. Na yote yaliyotamanika
katika Israeli amewekewa nani? Si wewe, na nyumba yote ya baba yako? ”
1Samuel 16:13 “Ndipo Samweli akaitwaa pembe yenye mafuta, akamtia mafuta
kati ya ndugu zake; na roho ya Bwana ikamjilia Daudi kwa nguvu tangu siku ile.
Basi Samweli akaondoka, akaenda zake Rama.”
1Wafalme
19:19-21 “Basi, akaondoka huko, akamkuta Elisha
mwana wa Shafati, aliyekuwa akilima, mwenye jozi za ng'ombe kumi na mbili mbele
yake, na yeye mwenyewe alikuwa pamoja na lile la kumi na mbili. Eliya akapita
karibu naye, akatupa vazi lake juu yake. Naye akawaacha ng'ombe, akamfuata
Eliya mbio, akasema, Nipe ruhusa, nakuomba, nimbusu baba yangu na mama yangu,
kisha mimi nitakufuata. Akamwambia, Enenda, urudi; ni nini niliyokutendea?
Akarudi akiacha kumfuata, akatwaa lile jozi la ng'ombe, akawachinja, akatokosa
nyama zao kwa ile miti ya ng'ombe, akawapa watu, wakala. Kisha akainuka,
akamfuata Eliya, akamhudumia.”
5. Mungu huweza kuwaita watumishi wake kupitia
malaika – Wakati mwingine Mungu humtuma malaika wake kuweza kuwasilisha
ujumbe wa jukumu lake kwa mtumishi wake anayekusudiwa, Katika maandikio iko
mifano mingi lakini tutaangalia mifano michache ya watu kadhaa kama Gideoni na
Mariam mama yake Yesu ambao walipewa kazi maalumu kwa ujumbe wa malaika
Waamuzi 6:11-14
“Malaika wa Bwana akaenda akaketi chini ya mwaloni
uliokuwa katika Ofra, uliokuwa mali yake Yoashi, Mwabiezeri; na mwanawe Gideoni
alikuwa akipepeta ngano ndani ya shinikizo, ili kuificha machoni pa Wamidiani.
Malaika wa Bwana akamtokea, akamwambia, Bwana yu pamoja nawe, Ee shujaa.
Gideoni akamwambia, Ee Bwana wangu, ikiwa Bwana yu pamoja nasi, mbona mambo
haya yote yametupata? Yako wapi matendo yake ya ajabu, waliyotuhadithia baba
zetu, wakisema, Je! Siye Bwana, aliyetuleta huku kutoka Misri? Ila sasa
ametutupa, naye ametutia katika mikono ya Midiani. Bwana akamtazama, akasema,
Enenda kwa uwezo wako huu, ukawaokoe Israeli na mkono wa Midiani. Je! Si mimi
ninayekutuma?”
Luka 1:26-33 “Mwezi wa sita, malaika Gabrieli alitumwa na Mungu kwenda
mpaka mji wa Galilaya, jina lake Nazareti, kwa mwanamwali bikira aliyekuwa
ameposwa na mtu, jina lake Yusufu, wa mbari ya Daudi; na jina lake bikira huyo
ni Mariamu. Akaingia nyumbani kwake akasema, Salamu, uliyepewa neema, Bwana yu
pamoja nawe. Naye akafadhaika sana kwa ajili ya maneno yake, akawaza moyoni,
Salamu hii ni ya namna gani? Malaika akamwambia, Usiogope, Mariamu, kwa maana
umepata neema kwa Mungu. Tazama, utachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; na
jina lake utamwita Yesu. Huyo atakuwa mkuu, ataitwa Mwana wa Aliye juu, na
Bwana Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi, baba yake. Ataimiliki nyumba ya
Yakobo hata milele, na ufalme wake utakuwa hauna mwisho.”
6. Mungu huweza kuwaita watumishi wake kupitia
Roho wake Mtakatifu – Ikumbukwe kuwa njia zote hizo Roho Mtakatifu ambaye
ndiye Bwana wa mavuno anazitumia katika kuhakikisha kuwa wanapatikana watenda
kazi katika mashamba yake lakini hutokea wakati mwingine mwenyewe akazungumza
moja kwa moja kwa njia ya unabii na kumuita au kumtaka mtu katika huduma
maalumu
Matendo 13:1-3
“Na huko Antiokia katika kanisa lililokuwako
palikuwa na manabii na waalimu, nao ni Barnaba, na Simeoni aitwaye Nigeri, na
Lukio Mkirene, na Manaeni aliyekuwa ndugu wa kunyonya wa mfalme Herode, na
Sauli. Basi hawa walipokuwa wakimfanyia Bwana ibada na kufunga, Roho Mtakatifu
akasema, Nitengeeni Barnaba na Sauli kwa kazi ile niliyowaitia. Ndipo wakiisha
kufunga na kuomba, wakaweka mikono yao juu yao, wakawaacha waende zao.”
7. Mungu huweza kuwaita watumishi wake Kupitia
Yesu Kristo mwenyewe – Wanafunzi wale kumi na wawili walikuwa ni chaguo la
Yesu Kristo mwenyewe na aliwaita kama alivyopenda yeye mwenyewe hata sasa Yesu
Kristo bado anaita watu wake kama apendavyo kwa njia mbalimbali na wakati
mwingine yeye mwenyewe. Hata hivyo ni muhimu kuelewa kuwa katika njia hizo zote
hakuna iliyobora zaidi kuliko nyingine kwa sababu zote ni njia ambazo yeye
mwenyewe anazitumia kuwapata watu wa kumtumikia katika huduma maalumu, kwa hoyo
mtumishi aliyetokewa na Yesu mwenyewe na kuitwa katika wito haimaanishi kuwa
anaubora kushinda aliyeitwa kwa njia nyingine, kwani kimaandiko hizo zote ni
nnia anazozitumia Mungu kufahamisha watu wake namna anavyowahitaji katika
huduma.
Mathayo 4:18-19
“Naye alipokuwa akitembea kando ya bahari ya
Galilaya, aliona ndugu wawili, Simoni aitwaye Petro, na Andrea nduguye,
wakitupa jarife baharini; kwa maana walikuwa wavuvi. Akawaambia, Nifuateni,
nami nitawafanya kuwa wavuvi wa watu.Mara wakaziacha nyavu zao, wakamfuata.”
Mathayo 9:9. “Naye Yesu alipokuwa akipita kutoka huko aliona mtu
ameketi forodhani, aitwaye Mathayo, akamwambia, Nifuate. Akaondoka, akamfuata.”
Kwa hiyo tunajifunza kuwa ni
Mungu mwenyewe ndiye anayeita watu wake katika huduma, na kwa sababu hiyo hakuna
mtu ajitwaliaye heshima hii, wakati Mungu anapomuita mtu kwaajili ya huduma mtu
huyo huwekewa kitu cha ziada na neema ya juu zaidi ili aweze kuwahudumia
wengine, Hata hivyo bado hatuwezi kuwaachia hao peke yao walioitwa katika wito
maalumu wa huduma kwa sababu kazi ya Mungu ni pana na hivyo wale wote ambao
hawatakuwa wameitwa katika wito maalumu wanabaki katika wito wa ujumla wa
kumtumikia Mungu na wakifanya kwa uaminifu na utii kazi ya Mungu itasonga mbele
na kuwa Baraka kubwa kwa jamii, Unaweza kujua wito wako kupitia neno la Mungu,
kupitia maombi, kupitia shuhuda za huduma za watu unao wahudumia, kuthibitishwa
na viongozi, na amani ya moyo, wito ni zawadi, wito ni heshima, wito ni
kuaminiwa, wito ni wajibu na kwa sababu hiyo kama Mungu amekuweka katika ajenda
zake basi wewe ni wa muhimu sana itikia sauti ya Mungu leo ukamtumikie.
Yohana 12:26 “Yeye aipendaye nafsi yake
ataiangamiza; naye aichukiaye nafsi yake katika ulimwengu huu ataisalimisha
hata uzima wa milele.Mtu akinitumikia, na anifuate; nami nilipo, ndipo na
mtumishi wangu atakapokuwapo. Tena mtu akinitumikia, Baba atamheshimu.”
Waebrania 3:14-15 “Kwa maana tumekuwa
washirika wa Kristo, kama tukishikamana na mwanzo wa uthabiti wetu kwa nguvu
mpaka mwisho; hapo inenwapo, Leo, kama mtaisikia sauti yake, Msifanye migumu
mioyo yenu, Kama wakati wa kukasirisha.”
Na Rev. Innocent Samuel Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima
.jpg)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni