Jumapili, 4 Januari 2026

Kuzingirwa kwa ukigo usioonekana!

 

Ayubu 1:7-9 “Bwana akamwuliza Shetani, Umetoka wapi wewe? Ndipo Shetani akamjibu Bwana, na kusema, Natoka katika kuzunguka-zunguka duniani, na katika kutembea huku na huku humo. Kisha Bwana akamwuliza Shetani, Je! Umemwangalia huyo mtumishi wangu Ayubu? Kwa kuwa hapana mmoja aliye kama yeye duniani, mtu mkamilifu na mwelekevu, mwenye kumcha Mungu na kuepukana na uovu. Ndipo Shetani akamjibu Bwana, na kusema, Je! Huyo Ayubu yuamcha Bwana bure? Wewe hukumzingira kwa ukigo pande zote, pamoja na nyumba yake, na vitu vyote alivyo navyo? Kazi za mikono yake umezibarikia, nayo mali yake imeongezeka katika nchi.”



Utangulizi:

Leo tunalenga kujifunza au kujikumbusha juu ya ulinzi wa Mungu usioonekana kwa watu wanaomwamini Mungu, katika kifungu cha maandiko ya msingi tunafunuliwa moja ya jambo la msingi lililoko katika ulimwengu wa roho ambalo macho yetu hayawezi kuona na huu ni ulinzi wa Mungu kupitia Malaika, Ukuta wa moto, Ukuta wa shaba, na wigo au ukigo usioonekana ambao kimsingi unawekwa na Mungu mwenyewe kwa watu wake, siri hii ya ukigo wa ulinzi uliowekwa na Mungu inafunuliwa na Shetani mwenyewe ambaye anakiri kuwa alikuwa hawezi kumshambulia Ayubu kwa sababu Mungu alikuwa amemuwekea ukigo pande zote, pamoja na nyumba yake, na vitu vyote alivyo navyo, ulinzi huu wa Mungu ni ulinzi usioonekana, ni ulinzi wa kiroho unaotokana na uhusiano wetu na Mungu na ni ulinzi unaowekwa na Mungu mwenyewe katika ulimwenguwa roho.

Zekaria 2:5 “Kwa maana mimi, asema Bwana, nitakuwa ukuta wa moto kuuzunguka pande zote, nami nitakuwa huo utukufu ndani yake.”

Yeremia 15:20-21 “Nami nitakufanya kuwa kama ukuta wa boma la shaba juu ya watu hawa; nao watapigana nawe; lakini hawatakushinda; maana mimi nipo pamoja nawe, ili nikuokoe, na kukuponya, asema Bwana. Nami nitakuokoa na mkono wa watu wabaya, nami nitakukomboa katika mkono wao wenye kutisha.”

Kwa msingi huo leo, tutachukua muda kujifunza somo hili Kuzingirwa kwa ukigo usioonekana kwa kuzingatia vipengele vikuu vitatu vifuatavyo:-

·         Maana ya ukigo usioonekana.

·         Kuzingirwa kwa ukigo usioonekana.

·         Jinsi ya kuzingirwa na ukigo usioonekana.


Maana ya ukigo usioonekana.

Siri ya kwamba watu wanaomcha Mungu wanazingirwa na ukigo pande zote inawekwa wazi kwa mara ya kwanza na Shetani mwenyewe wakati wa mazungumzo yake na Mungu katika ulimwengu wa roho kuhusu Mtumishi wa Mungu Ayubu aliyekuwako huku Duniani, Shetani katika mazungumzo yake na Mungu anaonekana kumjua vema Ayubu, kwa sababu hakuuliza ni Ayubu yupi? Na tena inaonekana wazi alikuwa anafahamu Ayubu anaishi wapi? Alikuwa anamfahamu Ayubu vizuri nje ndani na bila shaka alikuwa anafahamu kuwa Ayubu ni Mtumishi wa Mungu ambaye alikuwa mwaminifu kama maandiko yasemavyo, habari hii inatufunulia kwa kina kuwa kuna uwezekano wasaidizi wa shetani yaani mapepo na wenye mamlaka na wakuu wa giza kwa namna Fulani wamewahi kuwa na mpango mkakati wa kumshambulia Ayubu na huenda walishindwa, na walitoa taarifa kwa bwana wao kuwa Yule Bwana hawezekani analindwa na nguvu za Mungu, na inawezekana hatimaye hata Shetani mwenyewe alijaribu kumtembelea Ayubu na kujaribu kutaka kusababisha uharibifu lakini mbinu zilishindikana, ilibainika wazi kuwa Ayubu anazingirwa na ulinzi maalumu wa Mungu, na kila anachikifanya Mungu amekibariki.       

Ayubu 1:7-9 “Bwana akamwuliza Shetani, Umetoka wapi wewe? Ndipo Shetani akamjibu Bwana, na kusema, Natoka katika kuzunguka-zunguka duniani, na katika kutembea huku na huku humo. Kisha Bwana akamwuliza Shetani, Je! Umemwangalia huyo mtumishi wangu Ayubu? Kwa kuwa hapana mmoja aliye kama yeye duniani, mtu mkamilifu na mwelekevu, mwenye kumcha Mungu na kuepukana na uovu. Ndipo Shetani akamjibu Bwana, na kusema, Je! Huyo Ayubu yuamcha Bwana bure? Wewe hukumzingira kwa ukigo pande zote, pamoja na nyumba yake, na vitu vyote alivyo navyo? Kazi za mikono yake umezibarikia, nayo mali yake imeongezeka katika nchi.”

Tunafunuliwa hapo kuwa ulinzi huu wa Mungu ambao hapo unatajwa kama UKIGO sio ulinzi unaoweza kuonekana kwa macho ya nyama, ni ulinzi maalumu unaotokana na uhusiano bora kati ya Ayubu na Mungu, inawezekana Ayubu hakuwa anaujua, wala hakuna mtu aliyeweza kuuona kwa macho lakini Shetani katika ulimwengu wa roho alifahamu kuwa Ayubu anazingirwa na ukigo pande zote, ulinzi huu wa Mungu hautokani na juhudi zetu wala haki yetu kwa hiyo sio sisi tunaoweza kuuweka ulinzi huo bali Bwana mwenyewe anawalinda watu wake, hii ni zawadi ya kila aaminiye.

1Petro 1:3-5 “Ahimidiwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kwa rehema zake nyingi alituzaa mara ya pili ili tupate tumaini lenye uzima kwa kufufuka kwake Yesu Kristo katika wafu; tupate na urithi usioharibika, usio na uchafu, usionyauka, uliotunzwa mbinguni kwa ajili yenu. Nanyi mnalindwa na nguvu za Mungu kwa njia ya imani hata mpate wokovu ulio tayari kufunuliwa wakati wa mwisho.”

Sasa ulinzi huo maalumu wa Mungu au nguvu za Mungu zinatotulinda kwa mujibu wa Shetani ameziita ukigo, UKIGO hasa ni nini? Neno ukigo linalotumika katika maandiko hapo katika Lugha ya Kiebrania linasomeka neno “sûk” au neno ώuk” ambalo linatamkwa sook kwa Kiingereza “Hedge” ambalo maana yake ni Ukuta au Ukingo maalumu unaomzingira mtu kwa kusudi la kuweka mipaka ili asizuriwe, it’s a way of protecting oneself against quality loss of financial, circumstances, health garden, properties, flocks etc. ni njia ya kulinda ubora wa mtu, uchumi, mazingira, afya, bustani, mali, na mifugo ili isipatwe madhara  hii ni maana ya kawaida ya UKIGO lakini Ukigo aliouona Shetani katika maisha ya Ayubu ulikuwa ni ukigo wa kiroho, yaani ukigo usioonekana “An unseen hedge” huu sasa ukigo usiionekana ni ukigo wa kiroho unaowekwa na Mungu kwa mtu aliyeokoka kumuwezesha mtu huyo kuwa na ulinzi wa Mungu kwa habari ya maisha yake na mali zake, uchumi wake, afya yake, watoto wake, mifugo yake mashamba yake na kadhalika, An unseen hedge is a spiritual barrier of divine protection placed by God around belivers and their possessions. Kwa hiyo mtu anayemcha Mungu analindwa na Mungu katika ulimwengu wa roho kiasi ambacho shetani analalamika kuwa hawezi kusababisha uharibifu katika jambo lolote kwa sababu Mungu anakulinda.

Kuzingirwa kwa ukigo usioonekana.

Kwa hiyo sasa tunapata ufahamu ya kuwa kila mtu aliyeokoka, kila amwaminiye Mungu, kila aliyeamini, analindwa na Mungu katika ulimwengu wa roho bila yeye mwenyewe kutambua na unaweza kulitambua hilo endapo utaruhusiwa kuona kwa macho ya rohoni, Neno la Mungu linatufunulia hivyo kwamba kila mtu aliyeokoka anazingirwa na UKIGO usioonekana, ulinzi huu hauonekani kwa macho lakini ni halisi, ni ulinzi wa kiroho na hauwezi kuonekana kwa macho ya nyama, ni ulinzi unaowekwa na Mungu mwenyewe na sio kwa jitihada za kibinadamu, ulinzi huu unazunguka Maisha yako, uhai wako, afya yako, familia yako, mali zako, watu wako, mazingira yako, Tunaweza kujifunza kutokana na Nabii Elisha nyakati za agano la kale namna na jinsi alivyokuwa na utambuzi ya kuwa uko ulinzi katika ulimwengu usioonekana kwa macho ambao unawazingira watu wa Mungu pande zote ona

2Wafalme 6:15-17 “Hata asubuhi na mapema mtumishi wake yule mtu wa Mungu alipoondoka, na kwenda nje, kumbe! Pana jeshi la watu, na farasi na magari, wameuzingira mji ule. Mtumishi wake akamwambia, Ole wetu! Bwana wangu, tufanyeje? Akamjibu, Usiogope; maana walio pamoja nasi ni wengi kuliko wale walio pamoja nao. Elisha akaomba, akasema, Ee Bwana, nakusihi, mfumbue macho yake, apate kuona. Bwana akamfumbua macho yule mtumishi; naye akaona; na tazama, kile kilima kilikuwa kimejaa farasi na magari ya moto yaliyomzunguka Elisha pande zote.”

Unaona hapo tunaona kuwa Elisha alikuwa na ufahamu kuwa analindwa na jeshi kubwa sana la malaika wasioonekana kwa macho ya nyama lakini alipomuombea mtumishi wake naye alipewa uwezo wa kuona na kugundua kuwa kulikuwa na magari ya farasi ya moto yaliyowazunguka pande zote, huu ulikuwa ukigo wa kiroho unaowazingira watumishi wa Mungu pande zote, mtu mmoja alisema ikiwa Elisha wa agano la kale alilindwa kiasi hiki ni wazi kuwa waamini katika Kristo nyakati hizi za agano jipya wanalindwa zaidi na nguvu za Mungu na ukigo usioonekana  katika ulimwengu wa roho, kuliko Elisha ambaye Yesu alikuwa hajamfia Msalabani, ikieleza namna watu wa Mungu wanavyolindwa Biblia iko wazi kwamba kila aliyemwamini Yesu analindwa iwe anajua au hajui

Marko 16:15-18 “Akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa. Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya; watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya.”

Awaye yote ambaye anamtegemea Mungu na kumcha yeye na kuendelea kukaa katika uwepo wa Mungu kimsingi anajiweka katika ulinzi wa Mungu, kwa sababu hiyo kimsingi kila mtu anayemtumainia Mungu anajiweka katika kuzingirwa kwa ukigo usioonekana, inaweza kuwa malaika, ama ukuta wa moto au ukuta wa shaba na kadhalika na ni Mungu ndiye anayetulinda kupiria serikali yake ya mbinguni, ile mamlaka ya kiungu inahusika na ulinzi wetu

Zaburi 91:1-11 “Aketiye mahali pa siri pake Aliye juu Atakaa katika uvuli wake Mwenyezi. Nitasema, Bwana ndiye kimbilio langu na ngome yangu, Mungu wangu nitakayemtumaini. Maana Yeye atakuokoa na mtego wa mwindaji, Na katika tauni iharibuyo. Kwa manyoya yake atakufunika, Chini ya mbawa zake utapata kimbilio; Uaminifu wake ni ngao na kigao. Hutaogopa hofu ya usiku, Wala mshale urukao mchana, Wala tauni ipitayo gizani, Wala uele uharibuo adhuhuri, Ijapo watu elfu waanguka ubavuni pako. Naam, kumi elfu mkono wako wa kuume! Hata hivyo hautakukaribia wewe. Ila kwa macho yako utatazama, Na kuyaona malipo ya wasio haki. Kwa kuwa Wewe Bwana ndiwe kimbilio langu; Umemfanya Aliye juu kuwa makao yako. Mabaya hayatakupata wewe, Wala tauni haitaikaribia hema yako. Kwa kuwa atakuagizia malaika zake Wakulinde katika njia zako zote.”

Daniel 6:18-22 “Kisha mfalme akaenda nyumbani kwake, akakesha usiku kucha, akafunga; na vinanda havikuletwa mbele yake; na usingizi wake ukampaa. Asubuhi mfalme akaondoka mapema, akaenda kwa haraka mpaka penye lile tundu la simba. Naye alipolikaribia lile tundu, akamlilia Danieli kwa sauti ya huzuni; mfalme akanena; akamwambia Danieli, Ee Danieli, mtumishi wa Mungu aliye hai, je! Mungu wako, unayemtumikia daima, aweza kukuponya na simba hawa? Ndipo Danieli akamwambia mfalme, Ee mfalme, uishi milele. Mungu wangu amemtuma malaika wake, naye ameyafumba makanwa ya simba, nao hawakunidhuru; kwa kuwa mbele zake mimi nalionekana kuwa sina hatia; tena, mbele yako, Ee mfalme, sikukosa neno.”

Kwa msingi huo kupitia maandiko haya na ufunuo wa neno la Mungu tunajifunza hapa kuwa mtu anayemtegemea na kumtumainia Mungu anazingirwa kwa ukigo usioonekana katika ulimwengu wa roho ni pale tu unapokuwa na macho ya rohoni na unapolielewa neno la Mungu ndipo unapoweza kuelewa ya kuwa katika ulimwengu wa roho tunao ukigo usioonekana yaani tunao ulinzi usioonekana kwa macho.                             

Jinsi ya kuzingirwa na ukigo usioonekana.

Tunahakikishiwa kuwa ukigo usioonekana ni Dhahiri kwa watu wa Mungu, na ni wa muhimu, lakini swali kubwa ni kuwa tunawezaje kuzingirwa na ukigo huu usiioonekana je tunaweza kuomba ulinzi wa Mungu? Maandiko yanaonyesha wazi kuwa sio dhambi kuomba ulinzi wa Mungu, japokuwa Mungu mwenyewe huwa anawalinda watu wake kwa hiyari yake na mapenzi yake, Shetani alipolaumu kuhusu ulinzi wa Ayubu alisema wewe umemzingira kwa ukigo pande zote maana yake ilikuwa ni Mungu kwa hiyari yake na kwa mapenzi yake alimlinda Ayubu

Ayubu 1:7-10 “Bwana akamwuliza Shetani, Umetoka wapi wewe? Ndipo Shetani akamjibu Bwana, na kusema, Natoka katika kuzunguka-zunguka duniani, na katika kutembea huku na huku humo. Kisha Bwana akamwuliza Shetani, Je! Umemwangalia huyo mtumishi wangu Ayubu? Kwa kuwa hapana mmoja aliye kama yeye duniani, mtu mkamilifu na mwelekevu, mwenye kumcha Mungu na kuepukana na uovu. Ndipo Shetani akamjibu Bwana, na kusema, Je! Huyo Ayubu yuamcha Bwana bure? Wewe hukumzingira kwa ukigo pande zote, pamoja na nyumba yake, na vitu vyote alivyo navyo? Kazi za mikono yake umezibarikia, nayo mali yake imeongezeka katika nchi.”

Hata hivyo ingawa ulinzi wa Mungu ni tukio la hiyari linalofanywa na Mungu mwenyewe maandiko hayakatazi kuomba ulinzi wa Mungu, viko viashiria kadhaa wa kadha vya kimaandiko vinavyotuthibitishia kuwa tunaweza kuomba ulinzi wa Mungu na huu ni ukweli usioweza kupingika, mfano katika sala ya Bwana iliyofundishwa na Bwana Yesu kuna sehemu ya kujiombea ulinzi, lakini sio hivyo tu Yesu katika maombi yake yeye mwenyewe alituombea ulinzi

Mathayo 6:13 “Na usitutie majaribuni, lakini utuokoe na yule mwovu. [Kwa kuwa ufalme ni wako, na nguvu, na utukufu, hata milele. Amina.]”   

Yohana 17:14-16 “Mimi nimewapa neno lako; na ulimwengu umewachukia; kwa kuwa wao si wa ulimwengu, kama mimi nisivyo wa ulimwengu. Mimi siombi kwamba uwatoe katika ulimwengu; bali uwalinde na yule mwovu. Wao si wa ulimwengu, kama mimi nisivyo wa ulimwengu.”

Ezra 8:21-23 “Ndipo nikaamuru kufunga, hapo penye mto Ahava, ili tupate kujinyenyekeza mbele za Mungu, na kutafuta kwake njia iliyonyoka, kwa ajili yetu sisi wenyewe, na kwa ajili ya watoto wetu, na kwa mali yetu yote. Maana naliona haya kumwomba mfalme kikosi cha askari na wapanda farasi, ili kutusaidia juu ya adui njiani; kwa maana tulikuwa tumesema na mfalme, tukinena, Mkono wa Mungu u juu ya watu wote wamtafutao, kuwatendea mema; bali uweza wake na ghadhabu yake ni kinyume cha wote wamwachao. Basi tukafunga, tukamsihi Mungu wetu kwa ajili ya hayo; naye akatutakabali.”

Kwa hiyo tunajifunza ya kwamba mojawapo ya njia ya kuzingirwa na ukigo usioonekana ni pamoja na kuomba ulinzi wa Mungu kwaajili yetu japo kuwa swala la kulindwa na Mungu liko katika mikono yake, na sisi tu mali yake  

Njia nyingine ya kukaribisha ulinzi wa Mungu au kuzingirwa na ukigo usioonekana katika maisha yetu ni kuwa na Maisha ya kumcha Mungu, Neno la Mungu linathuthibitishia ya kuwa Mungu huwazingira kwa ngao wale wanaotembea katika haki yaani wale wanaomcha Mungu.

Zaburi 5:11-12 “Nao wote wanaokukimbilia watafurahi; Watapiga daima kelele za furaha. Kwa kuwa Wewe unawahifadhi, Walipendao jina lako watakufurahia. Kwa maana Wewe utambariki mwenye haki; Bwana, utamzungushia radhi kama ngao.”

Zaburi 34:7-9 “Malaika wa Bwana hufanya kituo, Akiwazungukia wamchao na kuwaokoa. Onjeni mwone ya kuwa Bwana yu mwema; Heri mtu yule anayemtumaini. Mcheni Bwana, enyi watakatifu wake, Yaani, wamchao hawahitaji kitu.”

Ulinzi wa Mungu unathibitika wazi kwa wale wanaomcha Mungu, ni muhimu kufahamu kuwa ahadi za Mungu zinategemea (Conditional) pande zote mbili, Mungu anatoa ahadi ya kutupigania na kutulinda lakini ni wajibu wetu kumtii, kama utaharibu ukigo wako wewe mwenyewe utauharibu kwa kutokuwa mwaminifu kwa Mungu na hapo ni lazima utakula mkong’oto, hapa nisikupake mafuta kwa mgongo wa chupa niweke wazi kuwa kama ukimkosea Mungu huna budi kutubu na kurekebisha kwa haraka usitegemee ulinzi wa Mungu wakati wa kuasi kinyume na mapenzi yake ndio maana siku hizi hata walokole wanarogwa! Wanarogwaje kwa sababu wanaishi maisha ya kawaida na kuendelea katika dhambi huku wakidhani Mungu anatendelea kuwa mlinzi kwao tuambiane ukweli usimpe ibilisi nafasi, Mungu alimuhakikishia Joshua ushindi yaani maana yake pamoja na ulinzi lakini sharti ilikuwa lazima atende sawasawa  na yote yaliyoandika katika kitabu cha torati ya Musa vinginevyo unapigwa ona:-

Yoshua 1:5-7 “Hapatakuwa mtu ye yote atakayeweza kusimama mbele yako siku zote za maisha yako; kama nilivyokuwa pamoja na Musa, ndivyo nitakavyokuwa pamoja na wewe; sitakupungukia wala sitakuacha.Uwe hodari na moyo wa ushujaa, maana ni wewe utakayewarithisha watu hawa nchi hii niliyowaapia baba zao ya kwamba nitawapa. Uwe hodari tu na ushujaa mwingi, uangalie kutenda sawasawa na sheria yote aliyokuamuru Musa mtumishi wangu; usiiache, kwenda mkono wa kuume, au wa kushoto, upate kufanikiwa sana kila uendako.”

Yoshua 7:1-12 “Lakini wana wa Israeli walifanya dhambi katika kitu kilichowekwa wakfu; maana Akani, mwana wa Karmi, mwana wa Zabdi, mwana wa Zera, wa kabila ya Yuda, alitwaa baadhi ya vitu vilivyowekwa wakfu; hasira ya Bwana ikawaka juu ya wana wa Israeli. Kisha Yoshua akatuma watu kutoka Yeriko mpaka mji wa Ai, ulio karibu na Bethaveni, upande wa mashariki wa Betheli, akawaambia, akisema, Pandeni juu mkaipeleleze nchi, basi wakapanda juu wakaupeleleza Ai. Wakarejea kwa Yoshua wakamwambia, Wasiende watu wote, ila waende watu kama elfu mbili, tatu, wakaupige Ai; usiwataabishe watu wote kwa kuwaendesha huko; maana watu hao ni wachache tu. Basi watu wakaenda huko wapata elfu tatu tu; nao wakakimbia mbele ya watu wa Ai. Watu wa Ai wakawapiga watu kama thelathini na sita; wakawafuatia kutoka mbele ya mlango mpaka Shebarimu, wakawapiga huko kwenye matelemko; mioyo ya watu ikayeyuka, ikawa kama maji. Yoshua akararua mavazi yake, akaanguka kifudifudi mbele ya sanduku la Bwana hata jioni, yeye na wazee wa Israeli; wakatia mavumbi vichwani mwao. Yoshua akasema, Ee Bwana MUNGU, kwa nini umewavusha watu hawa mto wa Yordani, ili kututia katika mikono ya Waamori, na kutuangamiza? Laiti tungelikuwa radhi kukaa ng'ambo ya Yordani Ee Bwana, niseme nini baada ya Israeli kuwapa visogo adui zao? Maana Wakanaani na wenyeji wote wa nchi hii watasikia habari hii, nao watatuzingira, na kulifuta jina letu katika nchi. Nawe utafanya nini kwa ajili ya jina lako kuu? Bwana akamwambia Yoshua, Haya! Inuka, mbona umeanguka kifudifudi hivi? Israeli wamefanya dhambi, naam, wamelivunja agano langu nililowaagiza; naam, wametwaa baadhi ya vitu vilivyowekwa wakfu; tena wameiba, tena wameficha na kuvitia pamoja na vitu vyao wenyewe. Ndiposa wana wa Israeli hawawezi kusimama mbele ya adui zao; wakawapa visogo adui zao, kwa sababu wamelaaniwa; mimi sitakuwa pamoja nanyi tena, msipokiharibu kitu kile mlicho nacho kilichowekwa wakfu.”

Kumbukumbu 1:41-45 “Ndipo mkanijibu, mkaniambia, Sisi tumefanya dhambi juu ya Bwana, tutakwea kupigana kwa mfano wa yote tuliyoamriwa na Bwana. Mkajifunga kila mtu silaha zake za vita, mkafanya wepesi kukwea mlimani. Bwana akaniambia, Uwaambie, Msiende, wala msipigane; kwani mimi si kati yenu; msije mkapigwa mbele ya adui zenu. Basi niliwaambia, msinisikize, bali mliasi amri ya Bwana, mkajikinai, na kukwea mlimani. Na Waamori waliokuwa wakikaa katika mlima huo, waliwatokea juu yenu, wakawafukuza, kama wafukuzwao na nyuki, wakawapomoshea Seiri mpaka Horma. Mkarudi mkalia mbele za Bwana; Bwana asiisikize sauti yenu, wala hakuelekeza masikio yake kwenu.”             

Neno la Mungu linatufundisha wazi hapo kuwa ulinzi wa Mungu ni Dhahiri kwa wale wamchao, lakini kama tukimuasi tunakuwa tumeharibu ukigo unaotuzingira na kwa sababu hiyo ni rahisi kushindwa na kushambuliwa na inaweza kuwa aibu kwetu, kama watu wanamtaka Mungu basi wamtake jumla jumla na sio nusu nusu, Neno la Mungu linasema yeye abomoaye boma nyoka watamuuma

Muhubiri 10:8-9 “Mwenye kuchimba shimo atatumbukia ndani yake; Na yeye abomoaye boma, nyoka atamwuma. Mwenye kuchonga mawe ataumizwa kwayo; Naye apasuaye miti huona hatari katika hiyo.”    

Kama hujaokoka na unahitaji ulinzi wa Mungu basi ni vema ukampokea Yesu,awe bwana na mwokozi wa maisha yako, Damu ya Yesu ni ulinzi na usalama wa maisha yako na Yule muharibifu anapoona alama ya damu yeye atapita juu yako na hataleta madhara katika nyumba yako kwa sababu umeiamini ile kazi iliyofanywa naye pale Msalabani.

Kutoka 12:12-13 “Maana nitapita kati ya nchi ya Misri usiku huo, nami nitawapiga wazaliwa wa kwanza wote katika nchi ya Misri, wa mwanadamu na wa mnyama; nami nitafanya hukumu juu ya miungu yote ya Misri; Mimi ndimi BWANA. Na ile damu itakuwa ishara kwenu katika zile nyumba mtakazokuwamo; nami nitakapoiona ile damu, nitapita juu yenu, lisiwapate pigo lo lote likawaharibu, nitakapoipiga nchi ya Misri.”

Kuzingirwa na ukigo usioonekana ni swala la uhakika kwa wana wa Mungu, Nanyi mnalindwa na nguvu za Mungu, ukweli tunaweza tusione kwa macho kile kinachoendelea katika ulimwengu wa roho lakini neno la Mungu linatuhibitishia kuwa tunalindwa, malaika wapo, ukuta wa moto uko unatuzunguka na mbingu zinatambua uwepo wetu na mahitaji yetu na wema wake utatuzunguka

Zakarika 2:5 “Kwa maana mimi, asema Bwana, nitakuwa ukuta wa moto kuuzunguka pande zote, nami nitakuwa huo utukufu ndani yake.”

Na. Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima        

Alhamisi, 1 Januari 2026

Nyakati za kuburudishwa!


Matendo 3:18-20 “Lakini mambo yale aliyohubiri Mungu tangu zamani kwa kinywa cha manabii wake wote, ya kwamba Kristo wake atateswa, ameyatimiza hivyo. Tubuni basi, mrejee, ili dhambi zenu zifutwe, zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwako kwake Bwana; apate kumtuma Kristo Yesu mliyewekewa tangu zamani;”




Utangulizi:

Kwa kawaida mojawapo la hitaji kubwa la kila mwanadamu duniani ni pamoja na kupata wakati wa kupumzika au kuburudishwa, Mwanadamu anapopata pumziko na kuburudishwa anapata nafasi ya kuwa na utulivu na kujijenga upya kimwili, kiakili, kihisia, kiroho na kisaikolojia, hivyo kumwezesha kupata nafasi ya kujijenga na kujitia nguvu kwa upya, Mwanadamu sio mashine au robot kwa sababu hiyo anaweza kuchoshwa na mambo mengi na hivyo anahitaji kupumzika, wakati huo wa mapumziko mwanadamu anahitaji kuburudishwa ili aweze kuwa vizuri kwaajili ya majukumu mengine mazuri zaidi, Mungu anafahamu sana kuwa wanadamu wanahitaji mapumziko ili waweze kujijenga upya.

Mathayo 11:28-29 “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu;”

Mapumziko ya mwanadamu yanaweza kumsaidia mwanadamu kuwa na nguvu katika maeneo yote ya maisha, kuwa na uwezo wa kustahimili migandamizo ya mawazo, kujenga mawazo mapya, kuwa na uwezo wa kutafakari, kupunguza mawazo, kuabudu, kupumzisha akili, kupokea mtazamo mpya, kuwa na mitazamo chanya, kusahau maumivu, na kuleta ufanisi unaomuondoa mwanadamu katika kuishi maisha ya mambo yanayojirudia rudia tena na tena kwa hiyo kuburudika ni hitaji kubwa la kiroho la Mwanadamu na ndio maana wanadamu wana likizo, mapumziko na usingizi n.k. ili kujikarabati, hata hivyo leo tutaangalia kwa undani na kwa kina namna ambayo Mungu huleta nyakati za kuburudishwa kwa wanadamu hasa pale wanapotubu na kurejea na kupokea msamaha wa Mungu kwa imani katika Kristo Yesu. Tutajifunza somo hili Nyakati za kuburudishwa kwa kuzingatia maswala muhimu yafuatayo:-

·         Maana ya nyakati za kuburudishwa.

·         Mwanadamu na nyakati za kuburudishwa.

·         Jinsi ya kuwa na nyakati za kuburudishwa.

Maana ya nyakati za kuburudishwa.

Matendo 3:18-20 “Lakini mambo yale aliyohubiri Mungu tangu zamani kwa kinywa cha manabii wake wote, ya kwamba Kristo wake atateswa, ameyatimiza hivyo. Tubuni basi, mrejee, ili dhambi zenu zifutwe, zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwako kwake Bwana; apate kumtuma Kristo Yesu mliyewekewa tangu zamani;”

Tunaona katika kifungu hiki neno la Mungu likizungumzia na kuwaita watu watubu na kurejesha uhusiano wao na Mungu ili kwamba wapate nyakati za kuburudishwa kwa uwepo wa Bwana, ni muhimu kwetu sasa kujiuliza kwamba neno kuburudishwa hasa lina maana gani?, Neno kuburudishwa kimsingi linalotajwa hapo katika neno la asili la Kiyunani linasomeka kama “Anapsuxis” au “Anapaύō” kwa kiingereza “refreshing” – Properly a recovery of breath ambalo maana yake ni kupumzika, kuhuishwa, kutulia ili kupata nguvu kwa upya, kujipa unafuu, kujituliza, kupunga upepo, kutuliza akili, kutuliza roho mwili na nafsi,  au kuvuta pumzi, kuburudika, kujipa nafasi, raha, kupata pumzi mpya, kurejeshea nguvu zilizopotea, kurudishia pumzi kwa usawia!.

Kutoka 23:12 “Siku sita utafanya kazi yako, na siku ya saba utapumzika; ili kwamba ng'ombe wako na punda wako wapate kupumzika, kisha mwana wa mjakazi wako na mgeni wapate kuburudika.”

2Samuel 16:13-14 “Basi wakaendelea njiani Daudi na watu wake; Shimei naye akaaendelea juu ya ubavu wa kile kilima, kwa kumkabili, huku akiendelea, akilaani, akimtupia mawe, na kurusha mavumbi. Naye mfalme na watu wake wote waliokuwa pamoja naye wakafika, wamechoka sana; naye akajiburudisha huko.”

1Wakorintho 16:17-18 “Nami nafurahi kwa sababu ya kuja kwao Stefana na Fortunato na Akaiko; maana hawa wamenikirimia kwa wingi yale niliyopungukiwa kwenu. Maana wameniburudisha roho yangu, na roho zenu pia; basi wajueni sana watu kama hao.”

Warumi 15:30-32 “Ndugu zangu, nawasihi kwa Bwana wetu Yesu Kristo, na kwa upendo wa Roho, jitahidini pamoja nami katika maombi yenu kwa ajili yangu mbele za Mungu; kwamba niokolewe na wale wasioamini katika Uyahudi, na tena huduma yangu niliyo nayo huko Yerusalemu ikubalike kwa watakatifu;nipate kufika kwenu kwa furaha, kama apendavyo Mungu, nikapate kupumzika pamoja nanyi.”

Kwa hiyo kimsingi kupumzika kwa mwanadamu kuna uhusiano mkubwa sana na uwepo wa Mungu Roho Mtakatifu, Mwanadamu anaweza kujipa raha au pumziko la kimwili tu lakini pumziko hilo sio pumziko la uhakika likilinganishwa na pumziko analolitoa Bwana wetu Yesu Kristo endapo mtu atampokea, tunafunuliwa katika andiko hilo kwamba, mwanadamu awapo dhambini yuko katika wakati wa kutumikishwa, yuko matesoni, anafanyishwa kazi bila hiyari yake, anatumikishwa na Shetani bila kupenda anateseka na kuelemewa na mizigo  na mateso ya aina mbalimbali na kuwa Pumziko la kweli linapatikana kwa kukubali mwaliko wake Yesu Kristo pekee, aidha mwanadamu anapokuwa katika magonjwa pia yuko vitani mwili wake unapigana kupambana na magonjwa lakini anapopokea uponyaji wa mwili wake nafsi yake na roho yake anapata nafasi ya kupumzika na Yesu Kristo anauwezo wa kutoa pumziko hilo kuanzia nasfini mwetu anauwezo wa kutupumzisha.

Mathayo 11:28-29 “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu;”

Kwa hiyo tunajifunza hapo kuwa nyakati za kuburudishwa ni wakati ambapo Mungu anampa mwanadamu pumzi mpya ya uhai, na kuuhisha roho yake iliyochoka na kukata tamaa kwa sababu ya mapito ya dunia baada ya kukubali toba na kumuamini Bwana Yesu kama Bwana na mwokozi.

Mwanadamu na nyakati za kuburudishwa.

Kila mwanadamu anahitaji nyakati za kuburudishwa aliyeokoka na hata asiyeokoka wote wanahitaji burudiko la kweli kwa sababu ya uchovu wa safari za duniani, Mwanadamu aliumbwa awe na nyakati za kuburudika na kupumzika kila wakati na kila siku, Mungu alipomuweka mwanadamu katika bustani ya Edeni alimuwekea mwanadamu mazingira ya mapumziko na wakati wa kuwa na ushirika na yeye, anguko la mwanadamu limesababisha upungufu mkubwa katika maisha ya mwanadamu, Mwanadamu ni kiumbe na ni kiumbe cha kibaiolojia, chenye utashi na akili na hisia lakini zenye mipaka, baada ya anguko mwanadamu amewekewa mazingira magumu ya kula kwa jasho, kushambuliwa na adui zake, uadui wetu mapepo na na shetani, michongoma na miiba kutuzalia na kuzaa kwa uchungu adhabu zote zile zilizotamkwa na Mungu zimemwekea mwanadamu mazingira ya kuchoka kiroho, kimwili, kiakili, kisaokolojia na kibailojia, hivi vyote vinamfanya mwanadamu kuwa mchovu katika safari ya maisha na kumfanya mwanadamu awe mwenye kuhitaji mapumziko.

Mwanzo 3:9-19 “BWANA Mungu akamwita Adamu, akamwambia, Uko wapi? Akasema, Nalisikia sauti yako bustanini, nikaogopa kwa kuwa mimi ni uchi; nikajificha. Akasema, Ni nani aliyekuambia ya kuwa u uchi? Je! Umekula wewe matunda ya mti niliyokuagiza usiyale? Adamu akasema, Huyo mwanamke uliyenipa awe pamoja nami ndiye aliyenipa matunda ya mti huo, nikala. BWANA Mungu akamwambia mwanamke, Nini hili ulilolifanya? Mwanamke akasema, Nyoka alinidanganya, nikala. BWANA Mungu akamwambia nyoka, Kwa sababu umeyafanya hayo, umelaaniwa wewe kuliko wanyama wote, na kuliko hayawani wote walioko mwituni; kwa tumbo utakwenda, na mavumbi utakula siku zote za maisha yako; nami nitaweka uadui kati yako na huyo mwanamke, na kati ya uzao wako na uzao wake; huo utakuponda kichwa, na wewe utamponda kisigino. Akamwambia mwanamke, Hakika nitakuzidishia uchungu wako, na kuzaa kwako; kwa utungu utazaa watoto; na tamaa yako itakuwa kwa mumeo, naye atakutawala. Akamwambia Adamu, Kwa kuwa umeisikiliza sauti ya mke wako, ukala matunda ya mti ambao nalikuagiza, nikisema, Usiyale; ardhi imelaaniwa kwa ajili yako; kwa uchungu utakula mazao yake siku zote za maisha yako; michongoma na miiba itakuzalia, nawe utakula mboga za kondeni; kwa jasho la uso wako utakula chakula, hata utakapoirudia ardhi, ambayo katika hiyo ulitwaliwa; kwa maana u mavumbi wewe, nawe mavumbini utarudi.

Tangu baada ya anguko la mwanadamu, hitaji la kupumzika limekuwa ni sehemu ya uhitaji mkubwa wa mwanadamu, sio kimwili tu na hata kiroho na nafsi, hitaji la kupumzika na kuburudika linaonyesha kuwa mwanadamu sio kiumbe mkamilifu na wala hajitoshelezi bila Mungu, na kama mtu anaweza kushindana na hitaji la kuburudika na kupumzika ni wazi kuwa anashindana na asili, kwani hata zaidi ya maisha ya asili mwanadamu anahitaji kuburudika kiroho na hapo ndipo anapopata Amani, kugundua kusudi la kuwepo kwake na kujikuta anakamilika kwa hiyo katika ulimwengu wa anguko tunahitaji pumziko, Dhambi imeleta uhitaji mkubwa wa mapumziko, wanadamu walianza kutafuta faraja kila wakati katika safari ya maisha mara baada ya anguko ona

Mwanzo 4:20-22 “Ada akamzaa Yabali; huyo ndiye baba yao wakaao katika hema na kufuga wanyama. Na jina la nduguye aliitwa Yubali; huyo ndiye baba yao wapigao kinubi na filimbi. Sila naye akamzaa Tubal-kaini, mfua kila chombo cha kukatia, cha shaba na cha chuma; na umbu lake Tubal-kaini alikuwa Naama.”

Wanadamu walioanguka walijaribu kufanya mambo mbalimbali ya kuwaletea burudani ikiwa ni pamoja na kugundua na kutengeneza vyombo vya muziki kama kinubi na filimbi ili kujaribu kujituliza lakini hata hivyo faraja hizo zote walizojibunia wanadamu hazikuweza kuwaletea amani             ya kweli.

-          Utumwa wa dhambi unachosha - Dhambi ilikuwa imemtenganisha mwanadamu na Mungu, maovu yetu yaliuficha uso wake roho ya mwanadamu ikakumbwa na ukavu na kukosekana kwa utoshelevu bila utoshelevu wa kiungu kwa kweli mwanadamu anakabiliwa na uchovu na ukavu na hitaji la burudiko la mwili nafsi na roho

 

Isaya 59:1-2 “Tazama, mkono wa Bwana haukupunguka, hata usiweze kuokoa wala sikio lake si zito, hata lisiweze kusikia; lakini maovu yenu yamewafarikisha ninyi na Mungu wenu, na dhambi zenu zimeuficha uso wake msiuone, hata hataki kusikia.”

 

Zaburi 32:3-4 “Niliponyamaza mifupa yangu ilichakaa Kwa kuugua kwangu mchana kutwa. Kwa maana mchana na usiku Mkono wako ulinilemea. Jasho langu likakauka hata nikawa Kama nchi kavu wakati wa kaskazi.”       

 

Moyo wa mwanadamu ni kama ardhi kavu wakati wa joto au kiangazi, uwepo wa Mungu ni kama maji, wakati roho zetu zinapokaukiwa tunahitaji nyakati za kuburudishwa na burudiko hili na kiu hii inaweza kutimizwa na Mungu peke yake na haiwezi kupozwa na mwanadamu wala katika mazingira ya kibinadamu.

 

-          Kila mwanadamu anachoka – Ukiwa mwanadamu katika safari hii ya maisha kuna kuchoka, watu wanachoka kimwili kiroho na Kisaikolojia, nafsini mwao na wanaumia kwa hiyo kila mwanadamu anahitaji kutiwa nguvu kwa upya na anayeweza kuwapa nguvu wanaochoka na kuzimia ni Bwana mwenyewe kupitia uwepo wake.  

 

Isaya 40:29-31 “Huwapa nguvu wazimiao, humwongezea nguvu yeye asiyekuwa na uwezo. Hata vijana watazimia na kuchoka, na wanaume vijana wataanguka;bali wao wamngojeao Bwana watapata nguvu mpya; watapanda juu kwa mbawa kama tai; watapiga mbio, wala hawatachoka; watakwenda kwa miguu, wala hawatazimia.”

 

-          Mateso yanachosha sana – Kwa kuwa mwanadamu hakuumbiwa shida anapopita katika changamoto na shida za aina mbalimbali hatimaye anachoka, unapokuwa mtumwa wa mazingira, unapokosa uhuru wako mwenyewe, unapotumikishwa na kutumiwa unazidiwa na mateso na kwa sababu hiyo unachoka na kujikuta unahitaji kupumzika

 

Maombolezo 5:1-5 “Ee Bwana, kumbuka yaliyotupata; Utazame na kuiona aibu yetu. Urithi wetu umegeuka kuwa mali ya wageni; Na nyumba zetu kuwa mali ya makafiri. Tumekuwa yatima waliofiwa na baba; Mama zetu wamekuwa kama wajane.Tumekunywa maji yetu kwa fedha; Kuni zetu twauziwa.Watufuatiao wa juu ya shingo zetu; Tumechoka tusipate raha yo yote.”

 

-                Hata kutenda mema kunachosha - Mwanadamu anapotenda mema na wakati mrefu ukapita bila kuona matokeo pia anaweza kuchoka, unaomba, unatoa, unamlilia Mungu, unafunga unakesha lakini huoni matokeo wakati mwingine pia unaweza kuzimia moyo, unatendea mema watu wanakulipa maovu, unafadhili watu wanakuchukulia poa au kukutumia kwa faida hii nayo inachosha kutokana na hali hii watu pia huweza kuchoka kutenda mema.

 

Wagalatia 6:9-10 “Tena tusichoke katika kutenda mema; maana tutavuna kwa wakati wake, tusipozimia roho. Kwa hiyo kadiri tupatavyo nafasi na tuwatendee watu wote mema; na hasa jamaa ya waaminio.”

Kutokana na changamoto za aina mbalimbali anazokuwa amezipitia mwanadamu kila wakati changamoto hizo zinakuchosha na hivyo unajikuta kuwa unahitaji wakati wa kuburudishwa, ukiishi maisha ya utauwa utaudhiwa, ukiishi maisha ya anasa na dhambi utatumikishwa na shetani kwa ujumla duniani tunayo dhiki hata hivyo habari njema ni kuwa ziko nyakati za kuburudishwa hizi ni nyakati zinapatikana kwa toba na kufutiwa dhambi na kupewa wakati wa kuburudishwa, yaani ubatizo wa Roho Mtakatifu, Petro ndiye anatufunulia swala hili katika hutuba yake sikuya Pentekoste anaonyesha kuwa katika Bwana kuna kuburudishwa kila mwanadamu anahitaji nyakati hizi anahitaji burudiko la mwili wake, nasi yake na roho.  Na burudiko hili linapatikana kwa kurejesha uhusiano wetu na Mungu, baada ya toba Roho Mtakatifu anaposhuka ndani ya mwamini anamwezesha kuishi maisha yenye burudiko

Matendo 3:18-20 “Lakini mambo yale aliyohubiri Mungu tangu zamani kwa kinywa cha manabii wake wote, ya kwamba Kristo wake atateswa, ameyatimiza hivyo. Tubuni basi, mrejee, ili dhambi zenu zifutwe, zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwako kwake Bwana; apate kumtuma Kristo Yesu mliyewekewa tangu zamani;”

Jinsi ya kuwa na nyakati za kuburudishwa.

Mungu katika hekima yake anafahamu kuwa wanadamu wanahitaji nyakati za kuburudhishwa na kwa sababu hiyo neno lake limejaa ahadi za kuburudishwa.

Yeremia 31:23-25 “Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Watatumia tena neno hili katika nchi ya Yuda, na katika miji yake, nitakapowarudisha mateka yao; Bwana na akubariki, Ee kao la haki, Ee mlima wa utakatifu. Na Yuda, na miji yake yote, watakaa humo pamoja; wakulima, nao waendao huko na huko pamoja na makundi yao. Kwa maana nimeishibisha roho yenye uchovu, nami nimeiridhisha kila roho yenye huzuni.”

Zaburi 68:8-10 “Nchi ilitetemeka Naam, mbingu zilidondoka usoni pa Mungu; Hata Sinai usoni pa Mungu; Mungu wa Israeli.Ee Mungu, ulinyesha mvua ya neema; Urithi wako ulipochoka uliutia nguvu. Kabila yako ilifanya kao lake huko; Ee Mungu, kwa wema wako uliwaruzuku walioonewa.”

Petro anaunganisha toba kama njia ya kuleta amani na burudiko la kweli kwa mwanadamu, lakini zaidi sana anazungumzia ile ahadi ya Roho Mtakatifu ndani ya mtu aliyeamini kwa kutubu dhambi zake kwa kumaanisha kuziacha na kuzijutia, ni ukweli ulio wazi kwa kila mtu kuwa ukijazwa Roho Mtakatifu unakuwa na wakati wa kuburudisha, Petro alikuwa anamzungumzia Roho Mtakatifu ndani ya mwamini anakuwa ni kama maji ya kunywa  na kuoga wakati wa joto, aliyeokoka anakuwa ni kama maji ya mito inayotiririka, Hakuna jambo linaleta furaha na amani kama kumpokea Roho Mtakatifu muulize kila mtu ambaye amejazwa Roho Mtakatifu atakuelezea jinsi ilivyo furaha kubwa sana hata unapopita katika magumu yeye anakupa burudiko lisiloweza kuelezeka.

Matendo 4:24-31. “Hata walipofunguliwa, wakaenda kwa watu wao, wakawapasha habari ya mambo yote waliyoambiwa na wakuu wa makuhani na wazee. Nao waliposikia, wakampazia Mungu sauti zao kwa moyo mmoja, wakisema, Mola, wewe ndiwe Mungu, ndiwe uliyefanya mbingu na nchi na bahari na vitu vyote vilivyomo; nawe ulinena kwa Roho Mtakatifu kwa kinywa cha babaetu Daudi, mtumishi wako, Mbona mataifa wamefanya ghasia, Na makabila wametafakari ubatili? Wafalme wa dunia wamejipanga, Na wakuu wamefanya shauri pamoja Juu ya Bwana na juu ya Kristo wake. Maana ni kweli, Herode na Pontio Pilato pamoja na Mataifa na watu wa Israeli, walikusanyika katika mji huu juu ya Mtumishi wako mtakatifu Yesu, uliyemtia mafuta, ili wafanye yote ambayo mkono wako na mashauri yako yamekusudia tangu zamani yatokee. Basi sasa, Bwana, yaangalie matisho yao; ukawajalie watumwa wako kunena neno lako kwa ujasiri wote, ukinyosha mkono wako kuponya; ishara na maajabu vifanyike kwa jina la Mtumishi wako mtakatifu Yesu.Hata walipokwisha kumwomba Mungu, mahali pale walipokusanyika pakatikiswa, wote wakajaa Roho Mtakatifu, wakanena neno la Mungu kwa ujasiri.”

2Wakorintho 4:8-9 “Pande zote twadhikika, bali hatusongwi; twaona shaka, bali hatukati tamaa; twaudhiwa, bali hatuachwi; twatupwa chini, bali hatuangamizwi;”

Uwepo wa Roho Mtakatifu ndani ya mtu aliyemwamini Yesu unayafanya maisha kuwa burudani kila wakati unamfanya mtu aliyemwamini Bwana asitikiswe na lolote, awe na nguvu ya kustahimili kwa sababu hata kama kwa nje anateseka kwa ndani kuna bubujiko la burudiko kubwa ndani yake, Roho Mtakatifu anatoa nguvu ya kustahimili, anatoa msaada wa uungu ndani yetu kushinda kila vikwazo vya kibinadamu na vya asili anatutia nguvu analihuisha neno la Mungu ndani yetu na kulifanya liwe na uhai na kukuwezesha kustahimili anakupa neema ya kuliona pendo la Mungu katika mateso na magumu na anakupa kuwacheka na kuwahurumia wanaodhani wanaweza kukukwaza kwa sababu zozote zile ndani yako maneno haya yanakuwa hai na halisi ndani ya mtu aliyeokoka.

Warumi 8:35-39 “Ni nani atakayetutenga na upendo wa Kristo? Je! Ni dhiki au shida, au adha, au njaa, au uchi, au hatari, au upanga? Kama ilivyoandikwa, ya kwamba, Kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa, Tumehesabiwa kuwa kama kondoo wa kuchinjwa. Lakini katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda. Kwa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo, wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho chote hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu.”                                

Waebrania 12:26-29 “ambaye sauti yake iliitetemesha nchi wakati ule; lakini sasa ameahidi akisema, Mara moja tena nitatetemesha si nchi tu, bali na mbingu pia. Lakini neno lile, Mara moja tena, ladhihirisha kuhamishwa vile viwezavyo kutetemeshwa, kama vitu vilivyoumbwa, vitu visivyoweza kutetemeshwa vikae. Basi kwa kuwa tunapokea ufalme usioweza kutetemeshwa, na mwe na neema, ambayo kwa hiyo tumtolee Mungu ibada ya kumpendeza, pamoja na unyenyekevu na kicho; maana Mungu wetu ni moto ulao.”

Uwepo wa Mungu ukitembea pamoja nawe ni lazima utapoata raha, raha maana yake refreshment yaani kuburudishwa ni katika uwepo wa Mungu kila mmoja wetu ataweza kubudurika hakuna namna nyingine tunapouanza mwendo wa mwaka huu mpya wa 2026 kila mmoja wetu ajikite katika kuutafuta uwepo wa Mungu, Kufanya kazi kwa bidii kutafuta fedha kwa njia za halali bila kuacha kuutafuta uso wa Bwana kwa bidii ili atupe raha, Bwana Mungu na atembee pamoja nawe katika mwaka huu na akupe nyakati za kuburudishwa katika jina la Yesu Kristo aliye hai, ulivyotembea katika nyakati ngumu na za majaribio imetosha sasa ni wakati wako wa kuburudishwa Mungu yuko tayari kutoa raha, na burudiko kwa wanadamu wote waliookolewa n ahata wasiookolewa kila mmoja wetu anahitaji kuburudishwa nami kama Petro alivyotangaza zikujie nyakati za kuburudishwa nakutangazia kuwa tayari kwa kuburudishwa, Pokea uwepo wa Bwana maishani mwako uwe na wakati wa kuburudishwa, mtii Mungu na itii sauti yake zipate kuja nayakati za kuburudishwa kwako katika jina la Yesu Kristo aliye hai. 

Kutoka 33:14-17 “Akasema, Uso wangu utakwenda pamoja nawe, nami nitakupa raha. Naye akamwambia, Uso wako usipokwenda pamoja nami, usituchukue kutoka hapa.Kwa maana itajulikanaje kuwa nimepata neema mbele zako, mimi na watu wako? Siyo kwa sababu unakwenda pamoja nasi, hata mimi na watu wako tutengwe na watu wote walio juu ya uso wa nchi? BWANA akamwambia Musa, Nitafanya na neno hili ulilolinena, kwa maana umepata neema mbele zangu, nami nakujua jina lako.”             

Na. Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima.

Jumanne, 30 Desemba 2025

Tengeneza mambo ya nyumba yako!

 


2Wafalme 20:1-3 “Siku hizo Hezekia akaugua, akawa katika hatari ya kufa. Isaya, nabii, mwana wa Amozi, akamjia akamwambia, Bwana asema hivi, Tengeza mambo ya nyumba yako; maana utakufa, wala hutapona. Basi Hezekia akajigeuza, akaelekeza uso wake ukutani, akamwomba Bwana akasema, Nakusihi, Bwana, ukumbuke sasa, jinsi nilivyokwenda mbele zako katika kweli na kwa moyo mkamilifu, na kutenda yaliyo mema machoni pako. Hezekia akalia sana sana.”


Utangulizi:

Moja ya wafalme na watawala wa ufalme wa Yuda aliyekuwa mwaminifu sana ni pamoja na Hezekia, Ni mfalme aliyemcha Mungu na kufanya mapinduzi makubwa ya uamsho ikiwa ni pamoja na kurejesha ibada ya Mungu wa kweli katika Hekalu lililokuwako Yerusalem na kukomesha kabisa ibada za kipagani, taarifa zake zinapatikana katika kitabu cha Wafalme wa pili, Nyakati wa pili na kitabu cha nabii Isaya, ambako kote anasifiwa kama mtawala mcha Mungu, ambaye alimtegemea Mungu hata wakati wa vita mbalimbali, Yeye alikuwa ni wa uzao wa Daudi na anayefikiriwa kama moja ya viongozi wacha Mungu sana, hata hivyo habari yake maarufu zaidi ni pamoja na habari zake za kuugua sana na akiwa katika kuugua huko akapokea onyo kali kupitia nabii Isaya kuwa atengeneze mambo ya nyumba yake kwani atakufa  na wala hatapona, jambo lilopelekea yeye kumlilia Mungu na kuomba kwa machozi.

Isaya 38:1-3 “Siku hizo Hezekia aliugua, akawa katika hatari ya kufa; na Isaya nabii, mwana wa Amozi, akaenda kwa mfalme, akamwambia, Bwana asema hivi, Tengeneza mambo ya nyumba yako; maana utakufa, wala hutapona. Basi Hezekia akajigeuza, akaelekeza uso wake ukutani, akamwomba Bwana, akasema, Ee Bwana, kumbuka haya, nakusihi, kwamba nimekwenda mbele zako katika kweli na kwa moyo mkamilifu, na kutenda yaliyo mema machoni pako. Hezekia akalia sana sana.”

Mara kadhaa tumehubiri sana kuhusu kisa hiki na kuonyesha nguvu za maombi na hasa maombi ya kulia sana na machozi na tumehubiri vile vile kuhusu swala zima la Hezekia kuongezwa miaka 15, lakini ni vigumu sana kuwasikia wahubiri wakieleza ni kwa nini mfalme huyu mwaminifu alitakiwa atengeneze mambo ya nyumba yake? Na ni kwa nini alipewa karipio kali kuwa hatapona bali atakufa? Tena akiwa anaumwa! Na kwanini Mungu alikuwa ameahirisha mpango wake na kumuongezea miaka? Ni changamoto gani ilikuweko nyuma ya karipio hili ambalo kimsingi linaweza kuwa ndio sababu ya mkasa huu mzima! Leo Roho Mtakatifu anatuwekea wazi, kuhusiana na swala hilo. Tutajifunza somo hili tengeneza mambo ya nyumba yako kwa kuligawa katika vipengele vikuu vitatu muhimu vifuatavyo:-

 

·         Tengeneza mambo ya nyumba yako.

·         Sababu za kutengeneza mambo ya nyumba yako.

·         Jinsi ya kutengeneza mambo ya nyumba yako.


Tengeneza mambo ya nyumba yako.

Isaya 38:1 “Siku hizo Hezekia aliugua, akawa katika hatari ya kufa; na Isaya nabii, mwana wa Amozi, akaenda kwa mfalme, akamwambia, Bwana asema hivi, Tengeneza mambo ya nyumba yako; maana utakufa, wala hutapona.”

Hezekia aliyekuwa mfalme mwaminifu katika utawala wa Yuda, ambaye alisababisha mabadiliko makubwa sana ya kiimani na kuleta uamsho mkubwa sana, alitakasa Hekalu, na kuharibu madhabahu za kipagani na ibada za sanamu, na kurejesha ibada sahihi za Mungu aliye hai, na sikukuu za Pasaka tofauti na Ahazi baba yake, Hezekia alikuwa mtu wa imani na maombi, mtu aliyemtegemea sana Mungu kiasi ambacho aliwahi kushinda vita kwa kupiganiwa na Malaika baada ya kuitisha mfungo na Mungu akaingilia kati dhidi ya majeshi ya Waashuru chini ya Senakeribu.

2Nyakati 32:20-22 “Na kwa ajili ya hayo Hezekia mfalme, na Isaya nabii, mwana wa Amozi, wakaomba, wakalia hata mbinguni. Naye Bwana akatuma malaika aliyewakatia mbali mashujaa wote, na majemadari, na maakida, matuoni mwa mfalme wa Ashuru. Basi akarudia nchi yake mwenye haya ya uso. Naye alipoingia nyumbani mwa mungu wake, wale waliotoka viunoni mwake mwenyewe wakamwangamiza humo kwa upanga. Ndivyo Bwana alivyomwokoa Hezekia, na wenyeji wa Yerusalemu, na mkono wa Senakeribu, mfalme wa Ashuru, na mikononi mwa wote, akawaongoza pande zote.”

Hezekia pia alijenga mradi wa maji maarufu kama mfereji wa Hezekia (Hezekiah’s tunnel) unaopitisha maji chini kwa chini katika mji wa Yerusalem wa zamani kama njia ya kujikinga na maadui endapo atazingirwa pande zote mfereji huo maarufu wa maji uko hata siku za leo, Anatambuliwa kama moja ya wafalme maarufu sana na mfano mzuri wa kuigwa akionyesha imani kwa Mungu na maombi na anatajwa katika ukoo wa masihi katika agano jipya kwenye kitabu cha Mathayo kama moja ya mababu waliomleta Yesu Kristo ulimwenguni kwa uzao wa Daudi. Ona:-

Mathayo 1:6-9 “Yese akamzaa mfalme Daudi. Daudi akamzaa Sulemani kwa yule mke wa Uria; Sulemani akamzaa Rehoboamu; Rehoboamu akamzaa Abiya; Abiya akamzaa Asa; Asa akamzaa Yehoshafati; Yehoshafati akamzaa Yoramu; Yoramu akamzaa Uzia; Uzia akamzaa Yothamu; Yothamu akamzaa Ahazi; Ahazi akamzaa Hezekia;

Hata pamoja na sifa hizi njema tunaona ghafla baadae alianza kuugua jipu baya sana na akiwa katika maradhi haya mabaya na katika hali ya kuugua na kuumwa, Isaya nabii anatumwa na Mungu kwenda kumpa ujumbe ya kwamba atakufa na wala hatapona na hivyo atengeneze mambo ya nyumba yake, kwa nini mfalme huyu mwadilifu anatamkiwa maneno makali hivi ya kutisha tena akiwa katika wakati wa kuumwa? Na kwa nini onyo alilopewa na nabii linaonekana kuwa ni onyo kali sana na kisha katika namna ya kushangaza baada ya kuomba kwake linaahirishwa kwa haraka baada ya maombi na anaongezewa miaka 15? Nini kilipelekea Hezekia apewe onyo hili kali Tengeneza mambo ya nyumba yako maana utakufa wala hutapona, tunajifunza nini kwenye hili?

Isaya 38:1 “Siku hizo Hezekia aliugua, akawa katika hatari ya kufa; na Isaya nabii, mwana wa Amozi, akaenda kwa mfalme, akamwambia, Bwana asema hivi, Tengeneza mambo ya nyumba yako; maana utakufa, wala hutapona.”

Sababu za kutengeneza mambo ya nyumba yako.

Mungu alimtuma nabii Isaya kumuonya Mfalme Hezekia na kumtaka atengeneze mambo ya nyumba yake, kwa ujumla sababu za kwanini onyo hili lilikuwa kali kiasi hiki haliko wazi sana katika Biblia Lakini unaweza kupata picha ya wazi kwamba Hezekia alikuwa na kiburi na ubinafsi uliopitiliza ambao ungeweza kuzuia mapenzi ya Mungu, alikuwa ni mtu aliyejihesabia haki kupita kawaida na hakuwa mtu mwenye kuamini haki ya wengine, Mfalme Hezekia alinyooshwa katika ugonjwa mzito na angekufa kweli, lakini Mungu hawezi kujipinga mwenyewe hivyo alimuongeza miaka 15 kwa sababu maalumu na za msingi sana ambazo tutaziangalia hapa:-

1.       Hezekia alikuwa ni mfalme ambaye hakuwa ameoa wala hakuwa anataka kuoa kwa mujibu wa maelezo ya tamaduni za kiyahudi Hezekia alikuwa anaogopa kuwa akioa na kuzaa mtoto anaweza kuzaa watoto wasio na haki na wasiomcha Mungu kama alivyo yeye na hivyo wangeweza kumuudhi Mungu, hivyo alijiamini mwenyewe na kujihesabia haki, akidhani kuwa wengine hawataweza kuwa kama yeye, kwa hiyo aliamini ni afadhali asioe kuliko kuoa na kuzaa watoto watakaomkosea Mungu, Mungu alichukizwa sana na mawazo ya Hezekia kwa sababu kama angelikufa bila kuzaa watoto, utawala wa Yuda ungekosa mfalme wa nasaba ya Daudi jambo ambalo lingevunja ahadi ya  mpango wa Mungu kwa utawala wa kudumu kwa uzao wa Daudi;-

 

2Samuel 7:12-16 “Nawe siku zako zitakapotimia, ukalala na baba zako, nitainua mzao wako nyuma yako, atakayetoka viunoni mwako, nami nitaufanya imara ufalme wake. Yeye ndiye atakayejenga nyumba kwa jina langu, nacho kiti cha enzi cha ufalme wake nitakifanya imara milele. Mimi nitakuwa baba yake, naye atakuwa mwanangu; akitenda maovu nitamwadhibu kwa fimbo ya binadamu na kwa mapigo ya wanadamu; lakini fadhili zangu hazitamwondoka, kama vile nilivyomwondolea Sauli, niliyemwondoa mbele yako. Na nyumba yako, na ufalme wako, vitathibitishwa milele mbele yako. Nacho kiti chako kitafanywa imara milele.”

 

Mwanzo 49:8-10 “Yuda, ndugu zako watakusifu, Mkono wako utakuwa shingoni mwa adui zako. Wana wa baba yako watakuinamia.Yuda ni mwana-simba, Kutoka katika mawindo, mwanangu, umepanda; Aliinama akajilaza kama simba, Na kama simba mke; ni nani atakayemwamsha? Fimbo ya enzi haitaondoka katika Yuda, Wala mfanya sheria kati ya miguu yake, Hata atakapokuja Yeye, mwenye milki, Ambaye mataifa watamtii.”

 

2.       Hezekia  alikuwa ni mfalme asiyetazama mbali; hata wakati anaumwa kwa muda mrefu bado alikuwa hafikirii lolote kuhusu uongozi ujao, alikuwa amejaa ubinafsi akijifikiri yeye mwenyewe, Mungu alimchungulia wakati anaumwa ikaonekana kuwa anafikiria kumaliza vizuri na Mungu lakini hakuwaza kamwe kuandaa kiongozi mwingine kwaajili ya kuendeleza uongozi ujao baada yake, wala hakuwaza kuwa watu wake wataongozwaje, alikuwa mfalme mwema na wa kiroho lakini mbinafsi, Mrithi alitakiwa kuandaliwa aone shughuli za kifalme na kujifunza maswala ya utawala hata kabla ya kifo chake lakini yeye hakuliangalia hilo, Neno tengeneza mambo ya nyumba yako katika lugha ya kiebrania ni “tsâvâh” ambalo maana yake kwa kiingereza ni appoint, au command au charge, set officially, arrange, determine, give orders, give instruction, show direction, chagua, Amuru, weka mtu mbadala, tangaza, andaa mrithi wako, amua, weka utaratibu, toa maelekezo, onyesha muelekeo lilikuwa ni agizo ambalo lingemfanya Hezekia akili zake zimrudie na afikiri kwa kina, nani anaweza kumrithi katika kiti cha ufalme baada yake,Kama yeye atakufa nini kitafuata, Sababu zake hazikuwa za msingi kwa Mungu, woga wake na hofu yake haikuwa na maana kwa Mungu, swala la uzao wake watakuaje watamcha Mungu au la, halikuwa linamuhusu  huwezi kuingilia na kuamua mambo ya Mungu ndani ya mtu mwingine ni kazi ya Mungu kujua nani atakuwa mwema au itakuwaje, ni wajibu wa Mungu kujua kuwa ajaye atafaa watu wake ama itakuwaje sio wewe, Kwa hiyo Hezekia alitakiwa kuoa na kuzaa na kumuandaa mfalme ajaye ili baada yake kazi ya Mungu iendelee, na uzao wa Daudi uendelee, yeye hakufanya hivyo, Musa aliandaa mtu ambaye angeshika madaraka baada yake  na Daudi aliandaa utaratibu wa mfalme ajaye na hata majukumu yake watu walijua baada ya Daudi nini kitafuata, Mungu alimuagiza hata Eliya kumuandaa Elisha kuwa nabii baada yake na alumuandaa hivyo mapema, kumbe viongozi huandaliwa:-

 

Hesabu 27: 18-23 “Bwana akamwambia Musa, Mtwae Yoshua, mwana wa Nuni, mtu mwenye roho ndani yake, ukamwekee mkono wako; kisha ukamweke mbele ya Eleazari kuhani, na mbele ya mkutano wote; ukampe mausia mbele ya macho yao. Nawe utaweka juu yake sehemu ya heshima yako, ili mkutano wote wa wana wa Israeli wapate kutii. Naye atasimama mbele ya Eleazari kuhani, naye atamwulizia kwa hukumu ya ile Urimu mbele za Bwana; kwa neno lake watatoka, na kwa neno lake wataingia; yeye na wana wa Israeli wote pamoja naye, mkutano wote pia. Musa akafanya kama Bwana alivyomwamuru; akamtwaa Yoshua, akamweka mbele ya Eleazari kuhani, na mbele ya mkutano wote;kisha akaweka mikono yake juu yake, akampa mausia, kama Bwana alivyosema kwa mkono wa Musa.”

 

1Nyakati 28:1-9 “Kisha Daudi akawakusanya huko Yerusalemu wakuu wote wa Israeli, wakuu wa kabila, na maakida wa vikosi wenye kumtumikia mfalme kwa zamu, na maakida wa maelfu, na maakida wa mamia, na wenye kutawala juu ya mali na milki za mfalme, na za wanawe, pamoja na matowashi, na mashujaa, naam, waume mashujaa wote. Ndipo Daudi mfalme akasimama kwa miguu yake, akasema, Nisikilizeni, ndugu zangu, na watu wangu; Mimi nalikuwa na nia ya kuijenga nyumba ya kustarehe kwa ajili ya sanduku la agano la Bwana, na kiti cha kuwekea miguu yake cha Mungu wetu; hata nalikuwa nimeweka tayari kwa kujenga. Lakini Mungu akaniambia, Wewe hutajenga nyumba kwa ajili ya jina langu, kwa sababu umekuwa mtu wa vita, nawe umemwaga damu. Walakini Bwana, Mungu wa Israeli, alinichagua katika nyumba yote ya babangu kuwa mfalme juu ya Israeli milele, kwa kuwa amemchagua Yuda awe mkuu; na katika nyumba ya Yuda, alichagua nyumba ya babangu, na miongoni mwa wana wa babangu, aliniridhia mimi ili kunitawaza niwe mfalme juu ya Israeli wote; tena katika wana wangu wote (kwani Bwana amenipa wana wengi), amemchagua Sulemani mwanangu ili aketi juu ya kiti cha enzi cha ufalme wa Bwana, juu ya Israeli. Akaniambia, Sulemani, mwanao, ndiye atakayeijenga nyumba yangu na nyua zangu; kwa kuwa nimemchagua awe mwanangu, nami nitakuwa babaye. Na ufalme wake nitauweka imara milele, akijitia kwa bidii kuzitenda amri zangu na hukumu zangu, kama hivi leo. Basi sasa, machoni pa Israeli wote, hilo kusanyiko la Bwana, na masikioni pa Mungu wetu, angalieni na kuzitafuta amri zote za Bwana, Mungu wenu, ili mpate kuimiliki nchi hii njema, na kuwarithisha wana wenu baada yenu hata milele. Nawe, Sulemani mwanangu, mjue Mungu wa baba yako, ukamtumikie kwa moyo mkamilifu, na kwa nia ya kumkubali; kwa kuwa Bwana hutafuta-tafuta mioyo yote, na kuyatambua mawazo yote ya fikira; ukimtafuta, ataonekana nawe; ukimwacha, atakutupa milele.”

 

1Wafalme 19:15-17 “Bwana akamwambia, Enenda, urudi njia ya jangwa la Dameski; ukifika, mtie mafuta Hazaeli awe mfalme wa Shamu. Na Yehu mwana wa Nimshi mtie mafuta awe mfalme wa Israeli; na Elisha mwana wa Shafati wa Abel-Mehola mtie mafuta awe nabii mahali pako.Na itakuwa atakayeokoka na upanga wa Hazaeli, Yehu atamwua; na atakayeokoka na upanga wa Yehu, Elisha atamwua.”

 

3.       Hezekia alikuwa anaamuriwa kuweka utaratibu, alikuwa ni kiongozi mzuri sana na mwema lakini alikuwa haandai utaratibu, angeacha mambo hayana hata muelekeo baada ya kifo chake, je hujawahi kuona viongozi wanaanzisha taasisi kisha wakifa wao nazo zinakufa? Watu wanaobaki wanakuwa hawajui hata la kufanya wote wanamtegemea yeye tu, Mungu ni Mungu wa utaratibu, Hezekia alikuwa hafiriki lolote kuhusu utaratibu utakuwaje baada yake wakati wenzake waliomtangulia walikuwa ni watu walioweka utaratibu yeye hata mke wa kuoa alikuwa anaogopa kuwa hatapata mke mcha Mungu na hivyo hatakuwa na watoto wazuri wala haonyeshi mrithi wake ni nani na nini kifanyike baada yake, kwa kufanya hivi ni kama alikuwa anazuia mpango wa Mungu wa baadaye, kila kiongozi kuanzia ngazi ya kifamilia anapaswa kukumbuka kuwa sisi ni wapitaji duniani, na baada ya kuongoza kwetu basi lazima aweko kiongozi mwingine na taratibu za baadae

 

Yehoshafati aliweka utaratibu mzuri sana wa kiserikali na kimaamuzi kabla ya kifo chake, Hezekia yeye alikaa kimya tu, anaugua na haweki mipango mingine vizuri, yalikuwa ni mawazo mabaya hakuwa kiongozi mbaya alimcha Mungu lakini hakuwa akifikiri zaidi ya mambo katika jicho la kiungu, hakuwaza kazi ya Mungu baada yake itakuwaje, kiongozi ambaye angemrithi angekosa hata pa kuanzia hajui aanzie wapi, hii ilikuwa changamoto yake ona mfano wa Yehoshafati yeye aliweka taratibu nzuri za kimaongozi na kiserikali ona!

 

2Nyakati 19:4-11 “Na Yehoshafati akakaa Yerusalemu; akatoka tena kwenda kati ya watu toka Beer-sheba mpaka milima ya Efraimu, akawarudisha kwa Bwana, Mungu wa baba zao. Akasimamisha makadhi katika nchi, katikati ya miji yote yenye maboma ya Yuda, mji kwa mji; akawaambia hao makadhi, Angalieni myafanyayo; kwa kuwa hammfanyii mwanadamu hukumu, ila Bwana; naye yupo pamoja nanyi katika neno la hukumu. Basi sasa hofu ya Bwana na iwe juu yenu; angalieni mkaifanye; kwa maana kwa Bwana, Mungu wetu, hapana uovu, wala kujali nafsi za watu, wala kupokea zawadi.Tena katika Yerusalemu Yehoshafati akasimamisha wa Walawi na makuhani, na wakuu wa mbari za mababa wa Israeli wawe kwa hukumu ya Bwana, na kwa mateto. Nao wakarudi Yerusalemu. Akawaagiza, akasema, Ndivyo mtakavyotenda kwa hofu ya Bwana, kwa uaminifu, na kwa moyo kamili. Na kila mara watakapowajia na teto ndugu zenu wakaao mijini mwao, kati ya damu na damu, kati ya torati na amri, sheria na hukumu, mtawaonya, wasiingie hatiani mbele za Bwana, mkajiliwa na ghadhabu ninyi na ndugu zenu; fanyeni haya wala hamtakuwa na hatia.Tena angalieni, Amaria, kuhani mkuu, yu juu yenu kwa maneno yote ya Bwana; naye Zebadia, mwana wa Ishmaeli, jemadari wa nyumba ya Yuda, kwa maneno yote ya mfalme; Walawi nao watakuwa wasimamizi mbele yenu. Jitieni nguvu, mtende, naye Bwana awe pamoja nao walio wema.”

Hata hivyo jambo jema ni kuwa baada ya maonyo Hezekia aliutafuta uso wa Mungu, aligeukia ukutani na kutafuta uso wa Mungu, aliomba na kulia sana alijutia tabia yake na ubinafsi wake aliokuwa nao, alimkumbusha Mungu jinsi alivyotembea kwa uaminifu alilia na kujutia kosa lake na Mungu alimrehemu haraka na kumuongezea Muda wa kufanya maandalizi, ni katika muda huu wa nyongeza ndipo alipooa na ndani ya miaka mitatu alizaliwa Manase

Isaya 38:2-6 “Basi Hezekia akajigeuza, akaelekeza uso wake ukutani, akamwomba Bwana, akasema, Ee Bwana, kumbuka haya, nakusihi, kwamba nimekwenda mbele zako katika kweli na kwa moyo mkamilifu, na kutenda yaliyo mema machoni pako. Hezekia akalia sana sana. Ikawa, neno la Bwana likamjia Isaya, kusema, Enenda ukamwambie Hezekia, Bwana, Mungu wa Daudi, baba yako, asema hivi, Mimi nimeyasikia maombi yako, nimeyaona machozi yako; tazama, nitaziongeza siku zako, kiasi cha miaka kumi na mitano. Nami nitakuokoa wewe, na mji huu, na mkono wa mfalme wa Ashuru, nami nitaulinda mji huu.”

Jinsi ya kutengeneza mambo ya nyumba yako

Kuna mambo kadhaa ya kujifunza kutoka kwa maisha ya Hezekia na mkasa huu, waalimu wa Kiyahudi wanaelezea ya kuwa Hezekia alioa haraka sana baada ya kuponywa na alimuoa mwanamke ambaye alikuwa ni binti wa nabii Isaya baada ya kukemewa na kuponywa, Nabii Isaya alimuelekeza jinsi ya kutengeneza mambo ya nyumba yake alitakiwa kuoa haraka hata bila kujali kuwa wazao wake watakuwa wema au wabaya, hakutakiwa kuogopa mambo yajayo wala kuharibu yanayobaki,alitakiwa kuweka utaratibu na kuandaa mrithi wa kifalme kwaajili ya Daudi mtumishi wa Mungu ili ahadi ya Mungu itimie, Mfalme Hezekia alimuoa “Hefsiba” ambaye alikuwa ni binti wa nabii Isaya  na miaka mitatu baada ya kuponywa kwake walifanikiwa kumpata mtoto aliyeitwa Manase, huyu akawa mfalme mpya hata hivyo akawa muovu sana kuliko wafalme wote katika Yuda, aliwahi kumtoa mwane sadaka ya kuteketezwa,akajihusha na waganga na wachawi na ibada za sanamu na kuabudu malaika na machukizo ya kila aina

Isaya 62:4-5 “Hutaitwa tena Aliyeachwa, wala nchi yako haitaitwa tena, Ukiwa; bali utaitwa Hefsiba; na nchi yako Beula; kwa kuwa Bwana anakufurahia, na nchi yako itaolewa.Maana kama vile kijana amwoavyo mwanamwali, ndivyo wana wako watakavyokuoa wewe; na kama vile bwana arusi amfurahiavyo bibi arusi, ndivyo Mungu wako atakavyokufurahia wewe.”

2Wafalme 21:1-6 “Manase alikuwa na umri wa miaka kumi na miwili alipoanza kutawala; akatawala miaka hamsini na mitano katika Yerusalemu, na jina la mamaye aliitwa Hefziba. Akafanya yaliyo mabaya machoni pa Bwana, sawasawa na machukizo ya mataifa, aliowafukuza Bwana mbele ya wana wa Israeli. Kwa maana akapajenga tena mahali pa juu alipopaharibu Hezekia baba yake; akamjengea Baali madhabahu, akafanya Ashera kama alivyofanya Ahabu mfalme wa Israeli. Akajiinama mbele ya jeshi lote la mbinguni na kulitumikia. Akazijenga madhabahu ndani ya nyumba ya Bwana, napo ndipo alipopanena Bwana, Katika Yerusalemu nitaliweka jina langu. Akajenga madhabahu kwa ajili ya jeshi lote la mbinguni katika behewa mbili za nyumba ya Bwana. Akampitisha mwanawe motoni, akatazama bao, akafanya uganga, akajishughulisha na hao wenye pepo wa utambuzi, na wachawi; akafanya mabaya mengi machoni pa Bwana, hata kumkasirisha.”

Mambo ya kujifunza:-  

1.       Hakuna mtu mwenye uhakika na kesho, kesho iko mikononi mwa Mungu tu, Hezekia ingawa alikuwa mwema lakini bado alikumbushwa kuwa kuna kifo na akapokea taarifa hizo bila kutarajia, kwa kawaida huwa tunajisahau kama wanadamu tunadhani tutaendelea kuwepo siku zote, uzima huu unatupa kiburi, pumzi hii inatufanya tufikiri ubovu ni wa wengine na kifo ni cha wengine, tunajifikiri sisi tu, hatufurahii kuandaa wengine, hatufikirii uhai wa taasisi wakati ujao, maisha ya mwanadamu ni kama mvuke tu, na kama ua la kondeni, usisahau kuwa kuna kifo, hata Musa alikumbushwa na Mungu akamuandaa Yoshua, Eliya alimuandaa Elisha, Paulo Mtume alimuanda Timotheo na wengine, wewe na mimi tunataka tukizimika wengine waone giza tu hicho ni kiburi na sio mpango wa Mungu.

 

Ayubu 14:1-2 “Mwanadamu aliyezaliwa na mwanamke Siku zake za kuishi si nyingi, naye hujaa taabu. Yeye huchanua kama vile ua, kisha hukatwa; Hukimbia kama kivuli, wala hakai kamwe

 

2.       Kutengeneza mambo ya nyumba yako sio agizo kwa Hezekia tu, ni agizo la kila mtu, iandae familia yako, andaa waandae kwaajili ya mambo yajayo, andaa mahusiano mazuri na watu, andaa  kwa kuondoa madeni ya kimwili na kiroho hakikisha yanalipwa, kumbuka kuweka maagizo, kumbuka kuna maisha baada ya kazi, kuna maisha baada ya kustaafu, kuna kutafuta kwa bidii kuwa na amani na watu wote, wewe na mimi hatutakuwepo milele tuache ubinafsi, Ondoa kinyongo chako moyoni, usijiweke katika nafasi ya Mungu, acha kuhukumu wengine na kudhani kuwa uko wewe peke yako Mungu anao watu wengi sana na anaweza kuwatumia, lakini ni wajibu wetu kuwaandaa na wengine waweze kutimiza hivyo Majukumu ya mbeleni.

 

Kutokujiayarisha kwa maswala ya Mungu kunaitwa upumbavu katika maandiko, lakini tukihesabu siku zetu fupi za kuweko duniani na tukazitumie vizuri ikiwa ni pamoja na kuwa tayari tunaitwa wenye hekima na akili

 

Zaburi 90:10-12 “Siku za miaka yetu ni miaka sabini, Na ikiwa tuna nguvu miaka themanini; Na kiburi chake ni taabu na ubatili, Maana chapita upesi tukatokomea mara.Ni nani aujuaye uweza wa hasira yako? Na ghadhabu yako kama ipasavyo kicho chako? Basi, utujulishe kuzihesabu siku zetu, Tujipatie moyo wa hekima.”

 

Luka 12:15-21 “Akawaambia, Angalieni, jilindeni na choyo, maana uzima wa mtu haumo katika wingi wa vitu vyake alivyo navyo. Akawaambia mithali, akisema, Shamba la mtu mmoja tajiri lilikuwa limezaa sana; akaanza kuwaza moyoni mwake, akisema, Nifanyeje? Maana sina pa kuyaweka akiba mavuno yangu. Akasema, Nitafanya hivi; nitazivunja ghala zangu, nijenge nyingine kubwa zaidi, na humo nitaweka nafaka yangu yote na vitu vyangu. Kisha, nitajiambia, Ee nafsi yangu, una vitu vyema vingi ulivyojiwekea akiba kwa miaka mingi; pumzika basi, ule, unywe, ufurahi. Lakini Mungu akamwambia, Mpumbavu wewe, usiku huu wa leo wanataka roho yako! Na vitu ulivyojiwekea tayari vitakuwa vya nani? Ndivyo alivyo mtu ajiwekeaye nafsi yake akiba, asijitajirishe kwa Mungu.” 

 

3.       Fanya mambo yao yote kwa uaminifu, Hezekia alikuwa mwaminifu na uaminifu wake ulikuja kumkomboa baadaye, Mungu alimuongezea umri kwa sababu alikuwa mwaminifu na alikubali mapenzi ya Mungu baada ya kuponywa jipu lake sugu, kumbuka wakati wowote unaweza kufa, hata kama wewe u mwema usisubiri tangazo la kifo ndipo uanze kujiandaa, je umeandaa watoto wako wa kiroho, umeandaa viongozi wajao, ndoa yako iko vizuri, watoto wako wamefundishwa njia za Bwana, je umesamehe waliokukosea, je una Amani na watu wote, je kwa Mungu uhusiano wako uko salama, Geuka ukutani leo ujifanyie tathimini wewe na Mungu wako kama mambo yako yako sawa sawa au la kama kuna kwa kutengeneza tubu, tengeneza mambo ya nyumba yako

 

2Petro 3:9 “Bwana hakawii kuitimiza ahadi yake, kama wengine wanavyokudhani kukawia, bali huvumilia kwenu, maana hapendi mtu ye yote apotee, bali wote wafikilie toba.”

 

4.        Unyenyekevu ni nyenzo ya thamani kubwa, - Kuugua kwa Hezekia kulimkumbusha swala zima la unyenyekevu, alipopewa taarifa za kutokupona alionyesha ya kuwa anamtegemea Mungu, alijinyenyekeza kwa Mungu wake, ni mfalme lakini aliamini katika maombi, alitubu na hakujihesabia haki, alipopona na kuongezwa maiaka 15 aliitumia vema kukamilisha kazi iliyosalia mbele yake kwa uaminifu, Hezekia alijifunza wazi kuwa iko sauti ya Mungu wakati tunapougua, lazima tujifunze na kujua kuwa Mungu anataka jambo gani lifanyike wakati wa kuugua kwetu na Hezekia aliyajua mapenzi ya Mungu na alijua dhambi zake akatubu

 

Isaya 38:17-20 “Tazama; nalikuwa na uchungu mwingi kwa ajili ya amani yangu; Lakini kwa kunipenda umeniokoa na shimo la uharibifu; Kwa maana umezitupa dhambi zangu zote nyuma yako. Kwa kuwa kuzimu hakuwezi kukusifu; mauti haiwezi kukuadhimisha; Wale washukao shimoni hawawezi kuitarajia kweli yako. Aliye hai, naam, aliye hai, ndiye atakayekusifu, kama mimi leo; Baba atawajulisha watoto kweli yako.Bwana yu tayari kunipa wokovu. Basi, kwa vinubi tutaziimba nyimbo zangu, Siku zote za maisha yetu nyumbani mwa Bwana.”

Na. Rev, Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima

Jumamosi, 27 Desemba 2025

Kupata na kujuta!

 


1Timotheo 6:6-10 “Walakini utauwa pamoja na kuridhika ni faida kubwa. Kwa maana hatukuja na kitu duniani, tena hatuwezi kutoka na kitu; ila tukiwa na chakula na nguo tutaridhika na vitu hivyo. Lakini hao watakao kuwa na mali huanguka katika majaribu na tanzi, na tamaa nyingi zisizo na maana, zenye kudhuru, ziwatosazo wanadamu katika upotevu na uharibifu. Maana shina moja la mabaya ya kila namna ni kupenda fedha; ambayo wengine hali wakiitamani hiyo wamefarakana na Imani, na kujichoma kwa maumivu mengi.”




Utangulizi

Bila shaka umewahi kushuhudia katika maisha haya kama mwanadamu kuwa unaweza kuwa na hamu au shauku ya kupata kitu fulani na ukapambana mpaka ukakipata na baada ya kuwa umekipata ukaanza kujuta moyoni, Hali hii inaweza ikatokea mara baada ya kufanya maamuzi kadhaa katika maisha yetu kisha baada ya maamuzi hayo unasikia hisia za majuto, unajiona kama umefanya maamuzi duni, ya kijinga na kipumbavu au kama umefanya makosa ya kiufundi umekosea malengo, au hujafanya maamuzi sahihi, wakati mwingine maamuzi ya aina hiyo yanaweza kuleta uchungu na hisia hasi na kuathiri afya na maendeleo ya mtu, kimwili, kiroho na kisaikolojia, ingawa kujuta pia kunaweza kujenga hisia chanya na kumfanya mtu kufanya maamuzi mazuri baadaye, maa na yake ni nini?, si kila kitu tunachikitaka na kufanikiwa kukipata duniani kinaweza kutuletea furaha, viko vitu vingine tunaweza tukavitamani sana lakini baada ya kuvipata vinaweza kuwa chanzo cha maumivu makubwa na huzuni na majuto, vitu hivyo inaweza kuwa mali, fedha, vyeo, mahusiano na kadhalika ambavyo tumevipigania kuvipata kwa shauku/tamaa lakini baadaye vinatuletea maumivu.

Yakobo 4:3 “Vita vyatoka wapi, na mapigano yaliyoko kati yenu yatoka wapi? Si humu, katika tamaa zenu zifanyazo vita katika viungo vyenu? Mwatamani, wala hamna kitu, mwaua na kuona wivu, wala hamwezi kupata. Mwafanya vita na kupigana, wala hamna kitu kwa kuwa hamwombi! Hata mwaomba, wala hampati kwa sababu mwaomba vibaya, ili mvitumie kwa tamaa zenu. Enyi wazinzi, hamjui ya kwamba kuwa rafiki wa dunia ni kuwa adui wa Mungu? Basi kila atakaye kuwa rafiki wa dunia hujifanya kuwa adui wa Mungu.”

Watu wengi sana duniani wametamani sana kupata mali, vyeo, na hata mahusiano Fulani kwa tamaa zao, lakini baadaye walijuta na kulia machozi, ni muhimu sana kupata lolote tunalolitamani katika mapenzi ya Mungu na sio kwa tamaa ya kibinadamu, sio kila kitu tunachokitaka duniani kinaweza kutupa raha, na furaha, vingine vinaweza kutuletea maumivu, uchungu na majuto, mengi, wengi wamejilaumu wenyewe, kujikosoa na kujisikia vibaya au kukata tamaa kwa sababu ya hali hii “Getting and regretting” yaani kupata na kujuta kisaikolojia tendo hili linaitwa “Cognitive dissonance” ambalo ni tendo la kukosa raha, baada ya mambo kwenda kinyume na ulivyoamini!

Leo kwa msingi huo tutachukua muda kujifunza somo hili Kupata na kujuta kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo;-

·         Maana ya kupata na kujuta

·         Kupata na kujuta.

·         Jinsi ya kupata katika mpango wa Mungu


Maana ya kupata na kujuta

Kupata na kujuta ni tendo la kupata huzuni, kukata tamaa, kupata masononeko katika akili yanayokuja baada ya kupata jambo fulani ambalo ulitarajia kuwa litakupa furaha lakini ukajutia kuwa haikuwa kama ulivyokuwa unafikiri, na ukatamani kama ungelifanya vinginevyo, hii ni mojawapo ya sehemu ya kawaida katika maisha ambayo imewakumba watu wengi, aidha baada ya kupata nafasi fulani nzuri na kushindwa kuitumia au kupata nafasi fulani wakaitumia lakini isilete furaha au matarajio uliyoyafikiri, tendo hilo kisaokolojia linaitwa Cognitive dissonance – Psychological conflict resulting from incongruous beliefs and attitudes held simultaneously, kwa Kiswahili tunaweza kusema Majuto ni Matokeo ya mgogoro wa kisaikolojia unaotokana na kutokuenda sawa kwa kile ulichikiamini au kukitarajia sawa na mtazamo ulioufikiria, Kwa Kiebrania linatumika neno “Nâcham” naw- kham kimatamshi,  kwa kiingereza to sigh – physical and emotional response to strong feeling like grief, regret, repent Kwa mfano Mungu alipomuumba mwanadamu, aliatarajia wanadamu wataishi kwa shukurani na utii kwa Mungu, lakini badala yake  wanadamu wakaanza kuishi tofauti na kile Mungu alichokuwa amekitarajia kwa hiyo Mungu alijuta, aidha Mungu alijuta pia alipomtawaza Sauli akijua kuwa atatii yote anayomwagiza, lakini Sauli alirudi nyuma asifuate aliyoagizwa na Mungu

Mwanzo 6: 1-6 “Ikawa wanadamu walipoanza kuzidi usoni pa nchi na wana wa kike walizaliwa kwao, wana wa Mungu waliwaona hao binti za wanadamu ya kuwa ni wazuri; wakajitwalia wake wo wote waliowachagua. BWANA akasema, Roho yangu haitashindana na mwanadamu milele, kwa kuwa yeye naye ni nyama; basi siku zake zitakuwa miaka mia na ishirini. Nao Wanefili walikuwako duniani siku zile; tena, baada ya hayo, wana wa Mungu walipoingia kwa binti za binadamu, wakazaa nao wana; hao ndiyo waliokuwa watu hodari zamani, watu wenye sifa. BWANA akaona ya kuwa maovu ya mwanadamu ni makubwa duniani na kwamba kila kusudi analowaza moyoni mwake ni baya tu sikuzote. BWANA akaghairi kwa kuwa amemfanya mwanadamu duniani, akahuzunika moyo.”

1Samuel 15:10-11 “Ndipo neno la Bwana likamjia Samweli, kusema, Najuta kwa sababu nimemtawaza Sauli awe mfalme; maana amerudi nyuma, asinifuate, wala hakufanya nilivyomwamuru. Samweli akasikitika, akamlilia Bwana usiku kucha.”                

Katika maandiko yote hayo lugha ya kiebrania inayotumika ni “Nâcham” ikimaanisha kuwa Mungu alijuta baada ya kuwa alifanya jambo kwa nia njema lakini baadaye hakupata matokeo kama yale aliyokuwa ameyaamini au kuyategemea au kuyatarajia huu ni mfano sasa wa kupata na kujuta, Katika maisha, kupata na kujuta kumewatokea watu wengi sana na kunaendelea kuwatokea, Bwana ampe neema kila mmoja wetu asitembee katika maisha ya majuto na badala yake aweze kufurahia maisha, Mungu akupe akili hizo na ufahamu huo, isitokee ukaja kujuta katika maisha yako Ameeeeen

Kupata na kujuta.

Kila mwanadamu anapaswa kuwa makini sana katika maeneo yote ya maamuzi katika maisha yake kwani kanuni inayotumika hapo ndiyo ambayo inaweza kutuletea furaha au majuto, endapo maamuzi yetu yatafanyika yakiwa yanaongozwa na tamaa na misukumo ya kibinadamu bila kuzingatia ua kufikiri sana katika upana wake kwa njia za kiungu na kutimiza mapenzi ya Mungu tunaweza kujikuta tunaingia katika kundi la watu wanaojuta katika maisha yao, Neno llinatuasa:-

Mithali 3:5-7 “Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote, Wala usizitegemee akili zako mwenyewe; Katika njia zako zote mkiri yeye, Naye atayanyosha mapito yako. Usiwe mwenye hekima machoni pako; Mche Bwana, ukajiepushe na uovu.”   

Maandiko yanaonyesha kuwa wako watu wengi sana ambao walitazama kitu kwa mitazamo yao na kukitamani lakini bila kuzingatia mapenzi ya Mungu na wakapata lakini walijuta sana baadaye

-          Hawa – Mwanzo 3:6-7 “Mwanamke alipoona ya kuwa ule mti wafaa kwa chakula, wapendeza macho, nao ni mti wa kutamanika kwa maarifa, basi alitwaa katika matunda yake akala, akampa na mumewe, naye akala. Wakafumbuliwa macho wote wawili wakajijua kuwa wa uchi, wakashona majani ya mtini, wakajifanyia nguo.”

 

Adamu na Hawa walijutia sana katika maisha yao na vizazi vyao swala zima la kutokumtii Mungu na kufuata mapenzi yao kwa kula mti waliokatazwa na Mungu, wao waliutamani ule mti na katika fikira zao walifikiri wanaweza kupata furaha wakala kwa tamaa ya kufanana na Mungu, na kwa masikitiko makubwa wakagundua kuwa wameingia matatizoni na wamekuwa uchi kabisa, uamuzi wao uliwapa kujuta siku zote za maisha yao kupata na kujuta

 

-          Lutu – alifanya uamuzi wa kuchagua kuishi katika bonde la Sodoma ambalo kwa macho ya kawaida liloonekana kuwa kama bonde la Mungu, ardhi ilikuwa nzuri yenye kuvutia na akaamua kuishi huko nadhani pia alioa huko, alipata lakini alitoka na majuto kwani alipoteza kila kitu alichokuwa nacho na hata mkewe pia na kujikuta akiishi katika pango akiwa masikini na asiyekuwa na kitu, na kuishia katika uvunjifu mkubwa wa kimaadili uliochagiwa bintize.

 

Mwanzo 13:10-13 “Lutu akainua macho yake, akaliona Bonde lote la Yordani, ya kwamba lote pia lina maji, kabla BWANA hajaharibu Sodoma na Gomora, lilikuwa kama bustani ya BWANA, kama nchi ya Misri hapo unapokwenda Soari. Basi Lutu akajichagulia Bonde lote la Yordani; Lutu akasafiri kwenda upande wa mashariki; wakatengana wao kwa wao. Abramu akakaa katika nchi ya Kanaani, na Lutu akakaa katika miji ya lile Bonde; akajongeza hema yake mpaka Sodoma.Lakini watu wa Sodoma walikuwa wabaya, wenye kufanya dhambi nyingi sana juu ya BWANA.”

 

Mwanzo 19:26-30 “Lakini mkewe Lutu akatazama nyuma yake, akawa nguzo ya chumvi. Ibrahimu akatoka asubuhi kwenda mahali aliposimama mbele za BWANA, naye akatazama upande wa Sodoma na Gomora na nchi yote ya hilo Bonde, akaona, na tazama, moshi wa nchi ukapanda, kama moshi wa tanuru. Ikawa Mungu alipoiharibu miji ya Bondeni, Mungu akamkumbuka Ibrahimu, akamtoa Lutu katika maangamizi alipoiangamiza miji hiyo aliyokaa Lutu.Lutu akapanda kutoka Soari akakaa mlimani, na binti zake wawili pamoja naye, kwa sababu aliogopa kukaa katika Soari. Akakaa katika pango, yeye na binti zake wawili.”

 

-          Amnoni mwana wa Daudi alimpenda sana Tamari binti ya baba yake alimpenda sana mpaka akawa anakonda na kuumwa, alimtamani sana alimpenda mno ndio maandiko yanavyotueleza mpaka akapanga mikakati ya kumpata kwa hila, hata hivyo baada ya kumpata tu neno la Mungu linasema alimchukia machukio makuu sana kuliko yale mapenzi aliyokuwa amempenda kwanza jambo hili lilimfanya apate lakini ajute

 

2Samuel 13:11-19 “Naye alipokwisha kuileta karibu naye, ili ale, Amnoni akamkamata, akamwambia, Njoo ulale nami, ndugu yangu. Naye akamjibu, La, sivyo, ndugu yangu, usinitenze nguvu; kwani haifai kutendeka hivi katika Israeli; usitende upumbavu huu. Nami nichukue wapi aibu yangu? Wewe nawe utakuwa kama mmoja wa wapumbavu wa Israeli. Basi, sasa, nakusihi, useme na mfalme; kwa maana hatakukataza kunioa. Walakini yeye hakukubali kusikiliza sauti yake; naye akiwa na nguvu kuliko yeye, akamtenza nguvu, akalala naye. Kisha Amnoni akamchukia machukio makuu sana; kwa kuwa machukio aliyomchukia yakawa makuu kuliko yale mapenzi aliyokuwa amempenda kwanza. Amnoni akamwambia, Ondoka, nenda zako. Naye akamwambia, Sivyo, kwa kuwa mabaya haya ya kunitoa ni makuu kuliko yale uliyonitendea. Lakini alikataa kumsikiliza. Ndipo akamwita mtumishi wake aliyemtumikia, akasema, Mtoe sasa mwanamke huyu kwangu, ukafunge mlango nyuma yake. Naye alikuwa amevaa kanzu ndefu; kwa kuwa kwa nguo hizo huvikwa binti za mfalme waliokuwa wanawali. Ndipo mtumishi wake akamleta nje, akafunga mlango nyuma yake. Naye Tamari akatia majivu kichwani mwake, akairarua hiyo kanzu ndefu yake aliyoivaa, akaweka mkono kichwani akaenda zake huku akilia kwa sauti.”

 

 

-          Yuda Iskariote – alitamani sana fedha, alifahamu au kudhani ya kuwa anaweza kumsaliti Yesu Kwa vipande 30 vya fedha, akidhani kuwa labda Yesu angeliponyoka katika mikono ya adui zake, hakufikiri kwa kina zaidi ya tamaa zake lakini baadaye alijutia sana umauzi wake alizitupa fedha hizo na kwenda kujinyonga, kupata fedha sio kubaya lakini kutafuta fedha nje ya mapenzi ya Mungu au kufanya mambo kwa tamaa ni jambo baya sana linaloweza kutuletea majuto, Kwa hiyo Yusa alifanikuwa kupata fedha kwa kumsaliti yetu Lakini alijutia

 

Mathayo 26:14-16 “Wakati huo mmoja wa wale Thenashara, jina lake Yuda Iskariote, aliwaendea wakuu wa makuhani, akasema, Ni nini mtakachonipa, nami nitamsaliti kwenu? Wakampimia vipande thelathini vya fedha. Tokea wakati huo akawa akitafuta nafasi apate kumsaliti.”

               

Mathayo 27:1-5 “Na ilipokuwa asubuhi, wakuu wa makuhani wote na wazee wa watu wakafanya shauri juu ya Yesu, wapate kumwua; wakamfunga, wakamchukua, wakampeleka kwa Pilato aliyekuwa liwali. Kisha Yuda, yule mwenye kumsaliti, alipoona ya kuwa amekwisha kuhukumiwa, alijuta, akawarudishia wakuu wa makuhani na wazee vile vipande thelathini vya fedha, akasema, Nalikosa nilipoisaliti damu isiyo na hatia. Wakasema, Basi, haya yatupasani sisi? Yaangalie haya wewe mwenyewe. Akavitupa vile vipande vya fedha katika hekalu, akaondoka; akaenda, akajinyonga.”

Kusudi la Mungu ni kumtunza mwanadamu na maumivu mengi, kumlinda mwanadamu dhidi ya tamaa, kumkumbusha mwanadamu ya kuwa anapaswa sana kumtegemea Mungu katika maamuzi yake yote na njia zake zote, wanadamu wengi sana waliookoka na wale wasiookoka wamejikuta katika madhara makubwa kwa sababu ya kuongozwa na tamaa na matakwa yao wenyewe, ni vema kila unapofika wakati wa kufanya maamuzi watu wakawa wanautafuta uso wa Mungu kwa bidii ili kuyapata mapenzi ya Mungu badala ya kuzifuata njia zetu wenyewe ambazo baadaye zinaweza kutuletea majuto, Neno la Mungu linayo maelekezo ya kutosha ya namna ya kupata yale tuyatakayo katika mapenzi ya Mungu na ikiwa hivyo katika maisha yetu tutaepuka kwa kiwango kikubwa kujuta.

Mithali 14:12-14 “Iko njia ionekanayo kuwa sawa machoni pa mtu, Lakini mwisho wake ni njia za mauti. Hata wakati wa kucheka moyo huwa na huzuni; Na mwisho wa furaha ni uzito wa moyo. Ageukaye moyoni hushiba njia zake mwenyewe; Na mtu mwema ataridhika nafsini mwake.”

Jinsi ya kupata katika mpango wa Mungu

Maisha yamejaa majuto mengi sana wako watu wanajuta kwa sababu mbalimbali katika maisha walipata lakini wanajuta, ukifanya utafiti, wako watu wamechoka mno mioyo yao imejaa simamzi na uchungu kwa sababu walipata au walifanya jitihada za kupata lakini wanajuta kwa namna moja ama nyingine, yale waliyoyapigania ili wapate yalileta majuto badala ya furaha, yale yaliowapotezea muda mwingi sana wakawekeza huko yakawalipa mabaya wasiotarajia, sasa wanajuta, wako wanaojuta kwa sababu, Walipopata kazi, walifanya kazi kwa bidii na kwa kujituma sana lakini hawakutoa muda wa kutosha kwa familia zao, marafiki zao na ndugu na jamaa, wakati wote walikuwa bize na kazi zao lakini walipojikuta wako vitandani na wanakaribia kufa walijuta kwa sababu kazi walizipata  na fedha walizipata lakini walijikuta wanafanya kazi sana na kutumia masaa mengi makazini na wakakosa wakati muhimu wa kuwa na familia zao, nahata kuwaweka sawa watoto wao, wanakuja kubaini watoto wamepotoka, wamekuwa bila upendo wa baba na mama,

Wako waliokataa wachumba zao kwa sababu walichelewa kuwaoa kwa sababu ya umasikini, nitamsubiria mpaka lini, mtu akaamua kuolewa na kijana aliyejitokeza kwa sababu ana kazi nzuri na gari nzuri, na pesa bila kujiuliza alivipataje lakini baada ya maisha kuendelea maisha yalitoa majibu tofauti, walipoteza upendo wa dhati kwa sababu ya vitu vinavyoonekana kwa muda sasa wanajuta

Wako watu ambao hawakuishi maisha yao halisi, na badala yake waliishi maisha ya kuigiza, wakitaka kuwafurahisha wengine walifurahia kusifiwa na kutambuliwa na watu, hawakuchagua ndoto zao walichagua ndoto za wazazi wao, hawakuchagua waume au wake waliowapenda wakachagua wale waliopendekezwa kwao na wachungaji, mabosi wao na vinginevyo, hawakuchagua kazi zao na fani zao walichagua kile dunia inakitaka kwaajili yao na wakawekeza muda wao huko na sasa wanajuta

Wako watu ambao wanajuta kwa sababu hawakuwa na muda wa kutunza afya zao, waliishi maisha ya hovyo, mabaya, hawakuwa na muda wa kutengeneza na watu, waliharibu mahusiano, na watu, familia zao na kupuuzia mapatano, na sasa wanajuta, wako waliopuuzia  muda wa kulala, muda wa kufanya mazoezi, walikunywa misoda na mavitu ya Super-market na sasa wanagundua kuwa wameharibu kila kitu wana huzuni kwa sababu hawakufanya mazoezi, wana huzuni kwa sababu hawakuzingatia lishe bora, wana huzuni, kwa sababu hawakufanya mapatano, wana huzuni kwa sababu hawakuwa wanalala usingizi wa kutosha afya zimeharibika na sasa wanajuta, wako hata waliokuwa wakifunga kwa kusudi la kuutafuta uso wa Bwana lakini walifunga hovyo hovyo bila kuzingatia kanuni za afya na sasa wana madonda ya tumbo, na hawawezi kufunga tena na wanajuta

Wako watu ambao wanajuta kwa sababu hawakuwekeza, hawakuweka akiba za kutosha hawakufikiri mambo ya baadaye sasa ni masikini, hawana fedha, hawakuwekeza mashamba wala mifugo hawakujali tabia zao zitawaletea matunda gani ya baadaye na sasa wanajuta, hawakupanga wanazaa watoto wangapi na kwa kiasi gani, wao kila kilichotokea kiliwatokea kama bahati tu, wako wanaojuta kwa usaliti, kupigania vyeo wakavipata lakini baadaye wakajuta hata kwanini walipigania vyeo hivyo, kutaka umaarufu, kuoa au kuolewa na watu wasio sahihi na kadhalika na sasa wao wako Jehanamu ya moto wa ndoa zao wakati wengine wako Paradiso umepata lakini unajuta!, wako waliozalishwa wakiwa nyumbani, waliona raha kujirusha lakini sasa wanajuta, wako ambao wameolewa na kuachika, wako waliotoa talaka na wanajuta, wako waliodai talaka na sasa wanajuta  hii ndio hali halisi ya Dunia pale tunapofanya mambo na kuchagua mambo kwa kuyapa uthamani wa kwetu wenyewe machoni petu wenyewe na kufanya mambo ambayo yanaweza kutufurahisha kwa muda mfupi badala ya kuwaza yatakayotufurahisha kwa muda mrefu, chaguzi za namna hiyo ni chaguzi za kiesharati kwa mujibu wa maelekezo ya kimaandiko, mwesharati ni mtu anayewaza kumaliza haja zake za muda mfupi tu na ikamgharimu maisha yake, badala ya kufikiri mbele hii ilikuwa changamoto ya Esau ambaye alijuta sana baadaye baada ya kuuza urithi wake kwa sikumoja.

Waebrania 12:16-17 “Asiwepo mwasherati wala asiyemcha Mungu, kama Esau, aliyeuuza urithi wake wa mzaliwa wa kwanza kwa ajili ya chakula kimoja. Maana mwajua ya kuwa hata alipotaka baadaye kuirithi Baraka, alikataliwa (maana hakuona nafasi ya kutubu), ijapokuwa aliitafuta sana kwa machozi.”

Wewe hapo ulipo ulitamani nini na ukakitafuta na kukipigania kwa nguvu zako zote na ukakipata lakini sasa unajuta moyoni, wako watu wengi wenye majuto ya kila aina hapa duniani na wewe sio wa kwanza sisi kama wanadamu tunaweza kufanya maamuzi ambayo baadae yanaweza kutuletea majuto makubwa sana katika mioyo yetu! Tufanyeje tujiue, turudi nyuma hapana tunashauriwa cha kufanya Na maandiko  

Ufanyeje sasa ili usishi kwa majuto?

Mungu wakati mwingine anatutaka tuwe na subira, subira hupita njia ndefu na ngumu sana na ndio maana watu wengi hawaipendi njia hii, ni njia ngumu lakini inaweza kutuletea matokeo mazuri ya kiungu na kuiungwana unajua Mungu hufanya mambo kwa wakati, lakini mwanadamu hutaka matokeo ya haraka na ni vigumu kwetu kuvumilia na kusubiri wakati wa Mungu, kwa haraka zetu.

Muhubiri 3:11 “Kila kitu amekifanya kizuri kwa wakati wake; tena ameiweka hiyo milele ndani ya mioyo yao; ila kwa jinsi mwanadamu asivyoweza kuivumbua kazi ya Mungu anayoifanya, tangu mwanzo hata mwisho.”

Mungu anatutaka tutangulize faida za kiroho kabla ya zile faida za mwilini, wengi wanaopitia njia za majuto ni wale ambao tunafikiri kwa jinsi ya mwili, kwa kuangalia vinavyoonekana na kupuuzia vile visivyoonekana ambayo kwa asili ni vya milele na hutupa furaha ya kudumu, ni lazima tuutafute kwanza ufalme wa Mungu na haki yake na mengine yote tutazidishiwa

Luka 12:16-21 “Akawaambia mithali, akisema, Shamba la mtu mmoja tajiri lilikuwa limezaa sana; akaanza kuwaza moyoni mwake, akisema, Nifanyeje? Maana sina pa kuyaweka akiba mavuno yangu. Akasema, Nitafanya hivi; nitazivunja ghala zangu, nijenge nyingine kubwa zaidi, na humo nitaweka nafaka yangu yote na vitu vyangu. Kisha, nitajiambia, Ee nafsi yangu, una vitu vyema vingi ulivyojiwekea akiba kwa miaka mingi; pumzika basi, ule, unywe, ufurahi. Lakini Mungu akamwambia, Mpumbavu wewe, usiku huu wa leo wanataka roho yako! Na vitu ulivyojiwekea tayari vitakuwa vya nani? Ndivyo alivyo mtu ajiwekeaye nafsi yake akiba, asijitajirishe kwa Mungu.”

Nadhani kila unapofikia wakati wowote katika maisha mahali ambapo tunataka kufanya uamuzi basi ni vema sana tukatafuta sana mapenzi ya Mungu na uongozi wa Mungu neno linasema usizitegemee akili zako mwenyewe bali katika njia zako zote mtegemee Mungu

Warumi 8:13-16 “kwa maana kama tukiishi kwa kufuata mambo ya mwili, mwataka kufa; bali kama mkiyafisha matendo ya mwili kwa Roho, mtaishi. Kwa kuwa wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu, hao ndio wana wa Mungu. Kwa kuwa hamkupokea tena roho wa utumwa iletayo hofu; bali mlipokea roho ya kufanywa wana, ambayo kwa hiyo twalia, Aba, yaani, Baba. Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu;”

Mithali 3:5-7 “Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote, Wala usizitegemee akili zako mwenyewe; Katika njia zako zote mkiri yeye, Naye atayanyosha mapito yako. Usiwe mwenye hekima machoni pako; Mche Bwana, ukajiepushe na uovu.”

Linda dhamiri yako wakati wote unapotaka jambo - unataka hicho unachokitaka kwa sababu gani? Mungu huangalia nia ya moyo na kuhukumu kulingana na nia ya moyo, kama kuna kitu unakihitaji lakini kwa tamaa unaweza usipewe au unaweza ukapewa lakini kikakutokea puani

Hesabu 11:18-20 “Kisha uwaambie watu hawa, Jitakaseni nafsi zenu kabla ya kesho, nanyi mtakula nyama; kwa maana mmelia masikioni mwa Bwana, mkisema, Ni nani atakayetupa nyama, tule? Maana huko Misri tulikuwa na uheri. Basi kwa sababu hiyo Bwana atawapa nyama, nanyi mtakula.Hamtakula siku moja, wala siku mbili, wala siku tano, wala siku kumi, wala siku ishirini; lakini mtakula muda wa mwezi mzima, hata hapo nyama hiyo itakapotoka katika mianzi ya pua zenu, nanyi mtaikinai, kwa sababu mmemkataa Bwana aliye kati yenu, na kulia mbele zake, mkisema, Tulitoka Misri kwa maana gani?

Hata kama tumemkosea Mungu na ikaleta majuto katika maisha yetu, ni Muhimu kwetu tukamrudia Mungu huyo huyo, kwa toba, kukiri, na kuutafuta uso wake tena, Upendo wa Mungu na rehema zake hauna mipaka, tukinyenyekea kwake atatupokea tena kama ilivyokuwa kwa mwana mpotevu, kupoteza kwetu sio mwisho wa maisha, kwani Baba wa rehema anayi nafasi nyingine, ttutafute uwepo wake naye atatutia nguvu na kuturejesha tena

Luka 15:17-20 “Alipozingatia moyoni mwake, alisema, Ni watumishi wangapi wa baba yangu wanaokula chakula na kusaza, na mimi hapa ninakufa kwa njaa. Nitaondoka, nitakwenda kwa baba yangu na kumwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako; sistahili kuitwa mwana wako tena; nifanye kama mmoja wa watumishi wako. Akaondoka, akaenda kwa babaye. Alipokuwa angali mbali, baba yake alimwona, akamwonea huruma, akaenda mbio akamwangukia shingoni, akambusu sana.”

Hitimisho:

Mpango wa kamili wa Mungu ni kila mmoja wetu kuyafurahia maisha, Mungu kama Baba aliye mwema anatufikiria mema na yuko kwaajili yetu, lakini pia yule muovu yuko, hata hivyo pamoja na kuweko kwa yule muovu, na majaribu mbalimbali mpango wa Mungu ni kuhakikisha ya kuwa anatubariki na kutupa mambo ya kudumu ambayo kimsingi hatachanganya nayo na huzuni wala majuto. Baraka za kweli kutoka kwa Mungu ni zile zinazokuja kwetu na hazituletei majuto, ukipata katika mpango wa Mungu bila ya hila, utaufurahia uwepo wa Mungu maisha yako yote, Bwana ampe neema kila mmoja wetu kuwa na Baraka za Mungu zisizo changamana na huzuni wala majuto. Amen

Mithali 10:22 “Baraka ya Bwana hutajirisha, Wala hachanganyi huzuni nayo.”

 

Na. Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima