Mstari wa Msingi Luka 11;1 “Ikawa
alipokuwa mahali Fulani akiomba , alipokwisha mmoja katika wanafunzi wake
alimwambia Bwana tufundishe sisi kusali kama vile Yohana alivyowafundisha
wanafunzi wake”
Maombi yana uhusiano mkubwa na Ukristo wetu
Mara tu baada ya mtu kuokoka na kufanyika mtoto wa Mungu Yohana 1;12 inakuja shauku na hamu kubwa ya mtu huyo kutaka kuwasiliana na Mungu
aliye baba yake wa Mbinguni. Mawasiliano
hayo yanafanyika kwa njia ya maombi, Yesu kristo kiongozi mkuu wa wokovu wetu
waebrania 2;10 alikuwa mwombaji mkuu, Alfajiri na mapema sana alikuwa anakwenda
mahali pasipokuwa na watu akawa anaomba
Marko 1;35 Jioni pia alikuwa akifanya maombi Marko 6;46-47 wakati mwingine pia
alikuwa akifanya maombi usiku kucha Luka
6;12 Yesu alichukua muda mrefu wa kuomba
mpaka akalia sana na machozi Waebrania 5;7 , hakukubali kutingwa sana na
shughuli na kukosa muda wa kuomba, wakati mwingine hata katikati ya kilele cha
shughuli zake alikuwa akijiepusha na kwenda mahali pasipokuwa na watu na kuomba
Luka 5;15-16 wakati mwingine aliomba mpaka hari yake au jasho lake likawa kama matone ya damu yakidondoka katika inchi Luka 22;44 Mara
nyingi aliwaambia wanafunzi wake waombe ili wasiingie majaribuni halafu yeye akajitenga mbali kidogo nao na
kuendelea kuomba , wanafunzi wake walipojaribu kuomba waliishiwa na maneno hata
ikawa kwao vigumu kuomba hata kidogo Luka 22;39-41 Mathayo 26;40-41 na ndipo
wanafunzi wake walipoona ni vema kumuomba awafundishe jinsi ya kuomba ni
makusudi ya somo hili sasa kujifunza jinsi ya kuomba , Yesu kristo alikuwa
muombaji na alikuwa ni kielelezo chetu Mtu awaye yote aliyeokoka hawezi kufika
mbali katika wokovu wake kama akiwa sio
muombaji tutajifunza somo hili jinsi ya kuomba kwa kuzingatia vipengele vitano
vifuatavyo
·
Mikao inayofaa kwa ajili ya maombi
·
Swala la kuomba kwa sauti kubwa
·
Swala la kuomba kwa kufumba macho au kufumbua
macho
·
Umuhimu wa kuomba kwa jina la Yesu.
·
Matumizi ya sala ya Bwana katika Maombi
Mikao inayofaa kwa ajili ya maombi.
Wako watu wengi sana wanaofikiri
kuwa wakati wote mtu anapotaka kumuomba Mungu ni lazima awe amepiga magoti, hii
sio sahii kwani tunaweza kumuomba Mungu katika mikao tofauti tofauti katika namna nyingine pia kutegemea na
nafasi, Kupiga magoti ni jambo linalimfurahisha Mungu sana wakati wa kuomba Isaya 45;23. Lakini hata
hivyo kuna njia nyingi za kibiblia za jinsi ya kuomba zifuatazo ni baadhi ya
njia zilizomo kwenye Biblia
a. Kupiga
magoti – Tunaona mifano katika Luka 22;41Yesu, Katika Daniel 6;10 Daniel,
katika Zaburi 95;6 Daudi, katika Matendo ya mitume 7;60Stefano, katika Matendo
9;40Petro na katika matendo 20;36,21;5
Paulo mtume na watu wengine.
b. Kupiga
magoti na kukunjua mikono kuelekea mbinguni – Mfalme Sulemani katika 1Wafalme
8;54, 2Nyakati 6;13, na pia Ezra kuhani katika Ezra 9;5.
c. Kuinamisha
kichwa Mwanzo 24;26,Kutoka 4;31, 12;27
na 34;8
d. Kuanguka
kifulifuli uso kugusa Ardhi - Tunaona mfano wa Yesu Mathayo 26; 39. Yehoshafati
2Nyakati 20;18 Eliya 1wafalme 18;42,Yoshua katika Yoshua 5;14,Musa na Haruni katika Hesabu 20;6
e. Kusimama
– Marko 11;25,Luka 18;11
f.
Kusimama na kukunjua mikono kuelekea mbinguni –
1Wafalme 8;22
Hizo zote hapo juu ni njia zinazo
faa kwaajili ya kumuomba Mungu ni mazingira tu ndiyo yatakayoamua njia gani
itumike, kwa mfano huwezi kupiga magoti ukiwa stendi ya mabasi au katika kanisa
lisilo na sakafu Lakini kama mazingira ni mazuri na yanaruhusu kupiga magoti
kufanya hivyo sio tatizo Daniel 6;10, wala sio busara kugusa uso chini mpaka
utoke sugu ili watu wajue kuwa wewe ni muombaji maombi ya jinsi hii ni ya
kinafiki Mathayo 6;1-5, Biblia inatufundisha kuwa mambo yote yatendeke kwa uzuri na kwa utaratibu 1Koritho 14;40 kwa
msingi huo inatupasa kuchagua ni wapi na
ipinjia ipi inafaa na kuitumia kwa mfano
ukiwa una usingizi ukapiga magoti ili kuomba ni rahisi kulala usingizi hapo
njia sahii ni kusimama na kutembea huku unaomba itakusaidia kutokulala unaona.
Swala la kuomba kwa sauti kubwa
Kumekuwako na utata wa
kitheolojia kuhusu kuomba kwa sauti kubwa ikifikiriwa kuwa kufanya hivyo ni
kupayuka payuka kunakotajwa katika Mathayo 6;7-8 lakini tafasiri hiyo sio
halali katika Biblia ya kiingereza King James Version ambayo ni tafasiri iliyo
karibu na lugha za asili zilizoleta Biblia kwetu kiibrania na kiyunani Mathayo
6;7 husomeka hivi “But when ye pray use not vain repetitions as the heathen do”
kwa msingi huo kupayuka payuka ni kurudia rudia maneno yale yale kama kasuku
hii ilifanywa na mataifa kwa sababu hawajui kuomba hawana maneno mengi ya kutosha kujieleza
mbele za Mungu. Hivyo kuomba kwa kupaza sauti sio kupayuka Biblia imejaa mifano
ya watu wengi ambao waliomba kwa kupaza sauti na hata kulia sana machozi kama
alivyofanya Bwana Yesu Biblia inatoa ushauri wa kufanya hivyo
Waamuzi 2;4,21;21Samuel 30;3-4
Mithali 2;3-6 zaburi 77;1 Matendo 4;24
kuomba kimya kimya au kwa kupaza sauti kote ni sawa mbele za Mungu nako
pia kunategemea na mzingira, kwa mfano sio busara kufanya hivyo kwenye nyumba
ya kupanga au mahakamani ukiwa kizimbani
au wakati mumeo anayepinga wokovu akiwa chumbani anakusikia ukimuombea Niokoe
na Mume huyu mkaidi anayepinga wokovu n.k. maswala kama hayo ungeweza kuyaomba
kimyakimya Mathayo 7;6.
Swala la kuomba kwa kufumba macho au kufumbua macho.
Swala la kufumba macho au
kufumbua ni swala linalohusiana na maswala ya kisaikolojia kwa Mungu hakuna sharti Yeye huweza kuwasiliana
na mwanadamu hata akiwa amelala usingizi kwa njia ya ndoto, na hii haina maana
kuwa ukifumbua macho ndo kuna kitu utakiona
wakati mwingine mtu anaweza kuona maono akiwa amefumbua macho na macho hutumika kuyaona maono hayo lakini roho zetu huitwa zimezimia kwani
tunakuwa hatuko katika hali ya kawaida
Matendo 10;9-12 wakati mwingine kufumbua macho kunaweza kusababisha
kuingiza picha au mambo ambayo yatatutoa katika kuzingatia mwelekeo wetu kwa
Mungu kwahiyo hili nalo ni swala la kisaikolojia na kimazingira kwa mfano kama
unaendesha gari unaweza kuomba lakini sio kwa kufunika macho
Umuhimu wa kuomba kwa jina la Yesu.
Kuomba kibiblia ni kuomba kupitia
jina la Yesu hili ni jambo la muhimu namna yoyote ya kutumia vitu
vilivyochongwa au kutengenezwa kwa shaba, mbao, dhahabu , fedha n.k na kuvisimamisha kati yetu na Mungu na kuviangalia wakati wa kuomba na kuvitaja ,
kuvitumia, kuviangalia au kuvitafakari
na kufikiri kuwa vitafanikisha sala zetu hiyo ni ibada ya sanamu ambayo
ni machukizo makubwa mbele za Mungu
Kutoka 20;4-5,1Yohana 5;21,1Wakoritho 10;14 Isaya 31;7, Sanamu yoyote au lozari
na vitu vyote vya jinsi hiyo siyo sehemu ya maelekezo ya jinsi ya kuomba katika
Biblia , Mungu ni Roho nao wamwabuduo au kumuomba wanapaswa kumuabudu katika
roho na kweli na siyo kwa kutumia kitu chochote kinachoonekana Yohana 4;23-24,
aidha ni muhimu kufahamu kuwa kuwaomba wafu pia ni chukizo kubwa mbele za Mungu
Kumbukumbu 18;9-12, kuwaomba watakatifu ambao wamekwisha kufa kama Petro,
Yohana, Paulo, Bikira Maria, Yusufu .n.k watuombee sio sahii kibiblia kila
mmoja anapaswa kuomba mwenyewe na kuzungumza na Mungu kwa jina la Yesu na
ukifanya hivyo anakusikia na kupokea dua zako,
Kila mtoto wa Mungu ana haki sawa
kabisa na mwenziwe anapoomba kila
aombaye hupokea Yohana 16;24, Luka 11;9-11 Biblia inaonyesha kuwa ni wawili tu
wanaotuombea hao ni Yesu Kristo na Roho
Matakatifu nao hufanya hivyo bila sisi kuwaomba watuombee 1Yohana 2;1 Warumi
8;26-27 Tukifanya jinsi neno la Mungu linavyotuongoza na kulitii ndipo tutakapofanikiwa
katika njia zetu Zaburi 119;9, aidha ni muhimu kufahamu kuwa kuwaombea wafu pia
siyo sahii Biblia inasema katika Waebrania
9;27 kuwa mtu amewekewa kufa mara moja tu na baada ya kifo ni hukumu,
tunaweza kuomba kwa ajili ya wale walio hai ili waokolewe kabla hawajafa lakini
inapotokea mtu amekufa hakuna kinachoweza kubadilika 1Yohana 5;14-16
Maombi yetu ili yaweze kuwa na
mafanikio inatupasa kumuomba Mungu baba kwa kupitia jina la Yesu Yohana 16;23,
sio maelekezo ya Biblia kumuomba Mungu kupitia Mariam kwa mawazo potofu eti ukipitia kwa mama wa
Mungu ndio utajibiwa kwa sababu kina
mama wana huruma ni muhimu kufahamu Kua
Maria kamwe sio mama wa Mungu Mungu hana mama wala Baba hana mwanzo wa siku zake
wala mwisho wa siku zake hali kadhalika
kwa Yesu Kristo hivyo hivyo Waebrania 7;3 Yesu hakuanzia maisha yake tumboni
mwa Mariamu yeye alikuwepo hata kabla ya
Ibrahimu hajazaliwa Yohana 8;58, Yesu ndiye aliyeufanya ulimwengu Waebrania 1;2
katika Yesu kila kitu kiliumbwa
Wakolosai 1;13-17 Yeye ndiye aliyemuumba Musa Waebrania 3;1-4 na pia
ndiye aliyemuumba Maria na watu wote,
aliyeumbwa hawezi kuwa mama wa aliyemuumba Biblia inaonyesha kuwa Maria
mwenyewe alihusika katika kumuomba Mungu
pamoja na wanafunzi wa Yesu Matendo 1;4,12-14 Bikira Maria kamwe hawezi
kujiita mama wa Mungu kinyume chake alijiita mjakazi wa Bwana yaani mtumwa wa kike wa Bwana Biblia inasema
katika Luka 1;38 “Mariam akasema Tazama mimi ni mjakazi wa Bwana”
Matumizi ya sala ya Bwana katika Maombi
Mathayo 6;9-13 Yesu Kristo alipowafundisha
wanafunzi wake kuomba aliwaelekeza kuomba kwa misingi inayojulikana kama sala
ya Bwana, kimsingi hakuwa anamaanisha waitamke kama ilivyo na kuimaliza kama
kasuku kama watu wengi wanavyofikiri , Biblia inaposema katika Mathayo 6;9
“Basi ninyi salini hivi baba yetu uliye mbinguni……” Tafasiri ya kiingereza ya
King James Version inasema “After this manner therefore pray Ye” tafasiri ya
kiingereza ya LIVING BIBLE inasema Pray alon these lines” Katika Luka 11;2 kwa
msingi huo kinachozungumzwa hapa ni kuwa sala ya bwana ni mafundisho ya msingi
ya kutumia katika maombi, kilichozungumzwa ni kuomba kupitia misingi hii kila
tunapotaka kuomba Luka 9;54 Mathayo 20;20-22 Kutamka sala ya bwana kama ilivyo
ingeweza kuchukua dakika mbili tu na isingelikuwa suluhisho la kufundisha
maombi ambao wao walikuwa wakitaka kujifunza kuomba kwa muda mwingi wa
kutosha kama alivyokuwa akiomba Bwana
Yesu vinginevyo Yesu hangeshangazwa na
wanafunzi wake kulala usingizi ikiwa sala Yenyewe ingeweza kuchukua dakika
chache. Mafundisho mengi aliyokuwa akiyatoa Bwana Yesu Mara nyingi yalikuwa
yakihitaji ufafanuzi Mathayo 13;36, na pia mafundisho ambayo wanafunzi waliweza
kuyaelewa leo yanahitaji ufafanuzi
Mathayo 13;51 Mengine ambayo yalikuwa magumu kueleweka kwa wanafunzi kwa
mfano habari za kuteseka kufa na kufufuka sio tatizo kubwa kueleweka leo Marko
9;30-32, Luka 24;44-45 na ndio maana kanisa linahitaji waalimu ambao wanaweza
kufunuliwa na Roho wa Mungu Neno lake
ili kulilisha kanisa 1Wakoritho 2;10.
JINSI YA KUOMBA KWA KUTUMIA SALA YA BWANA.
Baba yetu uliye mbinguni.Mathayo 6;9.
Tunapokuja kumuomba Mungu
inatupasa kufahamu kuwa Yeye ni baba yetu, kama unaweza kuwasiliana na baba
yako wa duniani anayejishughulisha
na na mahitaji yetu na kuyajali ni muhimu kufahamu kuwa Hatupaswi kumuomba
Mungu tukidhani kuwa yuko mbali ni lazima tuweke mawazo yetu kuwa Mungu ni baba
yetu na kuwa yuko karibu mno tunapomuomba Zaburi 145;18,Zaburi 119;151 103;13
Fahamu kuwa ni baba mwenye upendo mwenye uwezo anayejishughulisha sana na mambo yetu 1Petro 5;6-7 hatupaswi kufikiri kuwa yeye hatujali Zaburi
37;28 Isaya 49;14-16,1Wakoritho 10;10. Aidha uhusiano wetu na Mungu lazima uwe
wa baba na mwana maana yake kama hujazaliwa mara ya Pili huwezi kuwa na
uhusiano wa aina hiyo.
Misingi Saba ya kufuata katika maombi yetu Kama alivyotufundisha Yesu
Kristo
1.
Jina
lako litukuzwe Mathayo 6;9.
Maombi yetu
yanapaswa kuanza kwa kumtukuza Mungu na kumsifu si busara kuanza kumimina shida
tulizo nazo mtukuze Mungu kwa uweza wake
na uumbaji mfano Zaburi 104;5-28, mtukuze kwa wingi wa Rehema na huruma zake
Zaburi 103;8 na pia unaweza kumtukuza kwa matendo yake makuu aliyokutendea
Zaburi 106
2. Ufalme wako uje Mathayo 6;9 Baada ya
kuokolewa ujue kuwa umetolewa katika ufalme wa giza au utawala wa shetani hivyo inakupasa kuwakumbuka wengine omba watu
waokolewe katika taifa lako, ombea wale wasio na mafundisho na kuombea kazi ya
Mungu ikiwa ni pamoja na Bwana wa mavuno kupeleka watenda kazi katika kazi yake
Waebrania 12;14 Mathayo 9;37-38.1Wakoritho 10;24,Wafilipi 2;4 Warumi 15;1
3. Mapenzi yako yatimizwe hapa duniani kama
huko mbinguni Mathayo 6;10 mapenzi ya Mungu kutimizwa ni watu kuishi sawa na Neno lake tumuombe
Mungu kwaajili ya serikali na wanaotawala duniani 1Timotheo 2;1-4,Mithali 21;1
ombea lolote lililo kinyume na mapenzi
ya Mungu lililotawala duniani mambo kama
rushwa, vita, njaa uonevu, kuzuia Neno la Mungu, kuenea kwa uislamu n.k
4. Utupe leo riziki Yetu Mathayo 6;11 Ni mapenzi ya Mungu baba
yetu kuwa kila mtoto wake apate riziki yake kila siku kuna riziki za aina nyingi Afya Marko 7;25-27, Yeremia 30;17, 33;6
Chakula nguo nazo ni aina za riziki
Zaburi 37;25,1Timotheo 6;8 zaburi 34;10 pia unaweza kuomba kwaajili ya mahitaji
ya wengine na mahitaji mengine
5. Utusamehe Deni zetu kama sisi nasi
tunavyowasamehe wadeni wetu Mathayo 6;12
Deni zinazozungumzwa hapa ni makosa au dhambi Luka 11;4
katika maombi Mungu anatutazamia tuangalie mahali tulipomtenda dhambi
kwa kuwaza kusema na kutenda kwani
dhambi ni kizuizi cha maombi lakini wakati
huohuo tunapaswa kuwasamehe wengine au kupatana na watu tuliokosana nao Luka
17;4 kwani kama hatujasamehe dhambi zetu
pia zinakuwa ngumu kusameheka Mathayo 6;14-15.
6. Na usitutie majaribuni lakini utuokoe na
Yule mwovu kwa kuwa ufalme ni wako na nguvu na utukufu hata milele Mathayo
6;13, ni muhimu kufahamu kuwa Mungu hamjaribu mtu Yakobo 1;13-14 lakini shetani
hatuwazii mema watu wa Mungu na ndiye ambaye anazunguka huko na huko akitafuta
mtu ammeze 1Petro 5;8 Kwa kuwa Mungu ni
mwenye nguvu zote inatupasa kumuomba atuokoe na mipango ya shetani Luka 10;18-19Mathayo 18;18,Daniel 10;11-13
Kemea mipango yote ya shetani juu ya watu wote na kanisa pia kazi ya Mungu na namna yoyote ya kuwazuia watu wasilielekee
Neno la Mungu.
7. Amina Mathayo 6;13 Neno hili amina
maana yake ni na iwe hivyo, baada ya maombi amini kuwa imekuwa sawasawa na kuomba
kwako Marko 11;24 Hivyo mshukuru Mungu kwa imani kwamba umepokea uliyoyaomba
1Thesalonike 5;18 Endelea kuwa mtu wa maombi Yeremia 33;3 penda pia kuwa mwenye
kushiriki siku za maombi kanisani ambako uatajifunza kutoka kwa watu wenye
uzoefu mkubwa wa kuomba na kupata changamoto. Mithali 27;17.
Amina maana nyingine ya Muhimu:ni Jina la Yesu. Huu ni ujumbe kutoka kwa yeye aitwaye "Amina" Ufu.3:14
JibuFutaAmina
JibuFuta