Alhamisi, 28 Septemba 2017

Nguvu ya Umoja!



Andiko la Msingi: Yohana 17:21Wote wawe na umoja; kama wewe, Baba, ulivyo ndani yangu, nami ndani yako; hao nao wawe ndani yetu; ili ulimwengu upate kusadiki ya kwamba wewe ndiwe uliyenituma.”


Umoja ni hali ya kuungana kushikamana na kushirikiana au kufanya mambo kwa nia moja hata kuwa kitu kimoja, kadiri watu wanavyokuwa na umoja wanakuwa na mwanya mkubwa sana wa kufanikiwa katika kila jambo wanalolifanya na kulikusudia hakuna cha kuwazuia kwa kufahamu umuhimu wa Umoja Yesu aliwaombea wanafunzi wake wawe na umoja.

Ujumbe.

Wakati fulani kulikuwa na Mzee mmoja aliyeishi na vijana wake watatu huko kijijini, vijana hao walikuwa ni wachapa kazi hodari, hata hivyo walikuwa na tabia ya kugombana sana kila wakati, Mzee wao alijaribu kufanya kila njia ili kuwapatanisha lakini ilishindikana. Ingawa wanakijiji walishukuru na kufurahia utendaji wao wa kazi na bidii waliyokuwa nayo, lakini waliwatania kutokana na ugomvi wao.

Miezi ilipita ikatokea kuwa yule mzee alianza kuugua, aliwaita vijana wake na kuwataka wawe na umoja , lakini hawakusikiliza, aliamua kuwafundisha kivitendo, ili kwamba wasahau tofauti zao na kuungana

Mzee aliwaita vijana na kuwaambia “Nitawapa fimbo nyingi sana na kuzigawanya kwa kila mmoja nataka avunje fimbo hiyo mara mbili, yeye atakayevunja fimbo kwa haraka atapata zawadi”.
Vijana wakakubali.

Mzee aliwapa kundi la fimbo kumikumi kila mmoja na aliwaambia wazivunje vipande vipande, vija na walifanya hivyo kwa dakika chahe sana na kisha wakaanza kugombana kuwa ni nani amekuwa wakwanza

Mzee aliwaambia “wanangu wapendwa kazi bado, Sasa nitawapa kundi moja moja lenye fimbo kumikumi zilizofungwa pamoja na sasa utatakiwa kuvunja kundi zima la fimbo bila kuzitenganisha”
Vijana walikubali na kuanza kutaka kuvunja kundi la fimbo kumikumi kila mmoja na lake, kila mmoja alijaribu kufanya kila aliwezalo ili wazivunje lakini ilishindikana, kisha walitoa taarifa kwa baba yao.

Mzee wao aliwaambia wanangu angalia jinsi mlivyoweza kuvunja fimbo moja moja zilizokuwa peke yake kila moja  kwa urahisi sana, lakini hamkuweza kuzivunja fimbo za aina hiyohiyo zililipokuwa pamoja, kama mtakuwa mnagombana kila wakati na kutengana ni rahisi kwenu kushindwa , Lakini kama mtaungana na kuwa kitu kimoja hakuna atakayewaweza tafadhali sana nawaomba make pamoja

Vijana walielewa nguvu ya umoja na wakamuahidi mzee wao kuwa watakaa pamoja kwa gharama yoyote!.

Kuna nguvu ya mafanikio makubwa katika umoja, kuna siri katika umoja, Kanisa likikaa kwa umoja, ndugu wakikaa kwa umoja, wanandoa wakikaa kwa umoja, familia zikikaa kwa umoja kwaya zikikaa kwa umoja bendi zikikaa kwa umoja, wafanya kazi wakikaa kwa umoja, na taifa letu tukiungana na kuwa kitu kimoja hakuna jambo litaweza kuzuiliwa kwetu

Mwanzo 11:1-7Nchi yote ilikuwa na lugha moja na usemi mmoja. Ikawa watu waliposafiri pande za mashariki waliona nchi tambarare katika nchi ya Shinari; wakakaa huko.Wakaambiana, Haya, na tufanye matofali tukayachome moto. Walikuwa na matofali badala ya mawe, na lami badala ya chokaa. Wakasema, Haya, na tujijengee mji, na mnara, na kilele chake kifike mbinguni, tujifanyie jina; ili tusipate kutawanyika usoni pa nchi yote. BWANA akashuka ili auone mji na mnara waliokuwa wakiujenga wanadamu. BWANA akasema, Tazama, watu hawa ni taifa moja, na lugha yao ni moja; na haya ndiyo wanayoanza kuyafanya, wala sasa hawatazuiliwa neno wanalokusudia kulifanya. Haya, na tushuke huko, tuwachafulie usemi wao ili wasisikilizane maneno wao kwa wao.”

“Ni wazi kuwa Mungu mwenyewe anatambua Nguvu ya umoja anasema wala sasa hawatazuiliwa neno wanalokusudia kulifanya” kumbe watu wakiwa na umoja kuna kuwa na nguvu kubwa ya mafanikio na ndio maana shetani hupenda kupanda mbegu ya mafarakano ili yasiwepo mafanikio. Umoja unaleta upako wa kiroho kama upako wa Haruni, Zaburi 133:1-3Tazama, jinsi ilivyo vema, na kupendeza, Ndugu wakae pamoja, kwa umoja.Ni kama mafuta mazuri kichwani, Yashukayo ndevuni, ndevu za Haruni, Yashukayo mpaka upindo wa mavazi yake. Kama umande wa Hermoni ushukao milimani pa Sayuni. Maana ndiko Bwana alikoamuru baraka, Naam, uzima hata milele”.

Unaona kuna Baraka katika kukaa kwa umoja kinyume chake kuna laana katika mafarakano kaangalie nyumba na familia na ndoa ambazo hawaishi kugombana uone kama kuna maendeleo, angalia pia mataifa wanaopigana wenyewe kwa wenyewe, tukikaa kwa umoja Upako utatiririka kutoka kwa kuhani mkuu Yesu Kristo na kutuletea Baraka wote

Walawi 26:8Na watu watano wa kwenu watawafukuza watu mia, na watu mia wa kwenu watawafukuza watu elfu kumi; na adui zenu wataanguka mbele yenu kwa upanga.

Na Kumbukumbu la torati 32:3 inasema “Mmoja angefukuzaje watu elfu, Wawili wangekimbizaje elfu kumi….

Umoja unaleta ushindi wa kiroho, kupitia umoja kunakuwa na nguvu kubwa ya kumshinda shetani, umoja unazalisha nguvu iitwayo “Mastermind” ambayo ni kama nguvu ya nyuklia inayosababisha kusudi lake liweze kutimia, hakuna kitakachozuiliwa kama watu watakuwa na umoja katika lile wanalokusudia kulifanya.

Na Rev. Innocent Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima.  

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni