Jumapili, 7 Juni 2020

Mungu kwetu sisi ni Kimbilio na Nguvu!


Zaburi 46:1-3Mungu kwetu sisi ni kimbilio na nguvu, Msaada utakaoonekana tele wakati wa mateso. Kwa hiyo hatutaogopa ijapobadilika nchi, Ijapotetemeka milima moyoni mwa bahari.  Maji yake yajapovuma na kuumuka, Ijapopepesuka milima kwa kiburi chake.”




Utangulizi:


Moja ya matukio muhimu sana ambayo Dunia inaweza kuwa imejifunza katika wakati huu wa Corona ni pamoja na kukubaliana na Neno la Mungu kuwa Mungu ndio asili kuu ya usalama wa mwanadamu; kukitokea vita, au serikali zetu zote zenye nguvu duniani zikashindwa, au kukitokea matukio mabaya ya kutisha ambayo hata wenye nguvu duniani wanaogopa, sisi tunapaswa kuelewa kuwa kiko chanzo kimoja kikubwa cha usalama ambacho ni Mungu!

Watu wenye uwezo wa kufikiri Duniani kama alivyo rais wa Tanzania Dr. John Pombe Joseph Magufuli walikaa na kutafakari kwa kina na kugundua kuwa, hakuna kinachoweza kutuponya iwe ni maendeleo makubwa duniani, iwe ni elimu, iwe ni sayansi na technolojia, vyote haviwezi kuwa na majibu ya usalama wa kweli leo isipokuwa Mungu, Tumejifunza leo kuwa lolote linaweza kutokea hata kwa sekunde moja tu na likaondoa usalama na vyote vikashindwa kutusaidia isipokuwa maombi na kumtegemea Mungu  vina uwezo mkubwa sana!

Rais wetu alifunga siku kadhaa kule Dodoma, maombi yake binafsi, lakini vilevile alitangaza maombi ya kitaifa kwa siku tatu, na akayaona majibu ya maombi na kisha akatoa muongozo na kisha akatangaza shukurani na Tanzania ikawa na utulivu wa hali ya juu! Kwa nini kwa sababu yeye kama rais ana serikali ana nguvu na ni mwana sayansi, lakini alitambua kuwa msaada wa kweli unatoka kwa Mungu! Hakuna ulinzi mwingine wowote isipokuwa kumgeukia Mungu tu  na kumtegemea ona


Zaburi 46:8-10 “Njoni myatazame matendo ya Bwana, Jinsi alivyofanya ukiwa katika nchi. Avikomesha vita hata mwisho wa dunia; Avunja uta, akata mkuki, achoma moto magari. Acheni, mjue ya kuwa Mimi ni Mungu, Nitakuzwa katika mataifa, nitakuzwa katika nchi. Bwana wa majeshi yu pamoja nasi, Mungu wa Yakobo ni ngome yetu.


Mungu tu ndiye wa kutumainiwa Na ni Mungu tu ndiye Mlinzi wa kweli, Niliposikia habari wakati wa tatizo la Corona mwanzoni zilikuwa na utishio mkubwa sana hasa niliposikia Prince Charles yaani mtoto wa malikia naye ameugua corona unajua nini? Hawa ndio watu wanaolindwa zaidi Duniani kuliko mru yeyote Kikosi cha kumlinda malikia  kinaitwa SCOTLAND YARD SQUARD Kikosi hiki kinamlinda malikia na familia yake kwa masaa 24 na kina makomandoo waliofuzu mafunzo mbalimbali wapatao 185,  wao pia wana jina lingine maarufu kama RPS yaani ROYAL PROTECTION SQUAD ukiacha kuwa wanalindwa, watoto na wajukuu wa malikia wenywe ni askari waliofuzu na kushiriki vita za aina mbalimbali, Gharama za ulinzi wa wajukuu wa malkia Prince William na Prince Harry pekee unagharimu paundi laki tano 500.000.  Paundi moja kwa sasa ni sawa na shilingi za kitanzania 2900 hivi 500,000 X 2900 = 1,450,000,000 kwa mwaka wanalindwa na vifaa vya kisasa zaidi, Hapo hatujaeleza gharama za ulinzi wa malikia na mwanae mkubwa Prince Charles, Ikiwa mtu mkubwa kama huyu anaweza kupata virusi vya Corona  sembuse wewe mbwa mfu tu!  Je unadhani unakula vizuri kuliko yeye? Je unadhani unachekiwa afya vizuri kuliko yeye? Je unadhani una madaktari bingwa na hodari kuliko yeye?

Huwezi kuponyoka bila Mungu, Daudi alielewa kuwa kuna siri ya ziada katika Mungu, ni Mungu pekee ndiye anayeweza kutulinda na sio kinginecho


Zaburi 20:6-8 “Sasa najua kuwa Bwana amwokoa masihi wake;Atamjibu kutoka mbingu zake takatifu. Hawa wanataja magari na hawa farasi, Bali sisi tutalitaja jina la Bwana, Mungu wetu.Wao wameinama na kuanguka, Bali sisi tumeinuka na kusimama.


Mungu anatusubiri tu tuuitie msaada wake tutambue kuwa yeye atatujibu na hatutategemea mbinu za kibinadamu pekee bali Mungu atatokeza msaada katika kila hatari inayotukabili katika siku zetu duniani, Tunapomkimbilia yeye hatupaswi kuogopa chochote tunapaswa kusimama kwa imani na kutambua ya kuwa Bwana atakaa imara katika kiti chake cha enzi na kudhibiti kila kinachoinuka mbele yetu!

Zaburi 46:1-3Mungu kwetu sisi ni kimbilio na nguvu, Msaada utakaoonekana tele wakati wa mateso. Kwa hiyo hatutaogopa ijapobadilika nchi, Ijapotetemeka milima moyoni mwa bahari.  Maji yake yajapovuma na kuumuka, Ijapopepesuka milima kwa kiburi chake.”
Ulinzi wetu na usalama wetu unapatikana kwa imani kutoka kwa Mungu na sio mazingira yanayotuzunguka, yeye Bwana ni mwenye nguvu yeye ndio Ngome, imani yetu inapaswa kumsadiki yeye kuwa yuko mahali kote na ndiye anayetupa tumaini ni Mungu aliyejitambulisha kwetu kwa Israel yaani Mungu wa Yakobo

Zaburi 46:7, “Bwana wa majeshi yu pamoja nasi, Mungu wa Yakobo ni ngome yetu.” Tana mstari wa 11 “Bwana wa majeshi yu pamoja nasi, Mungu wa Yakobo ni ngome yetu. 

Mungu anataka tumtegemee yeye tumtumaini yeye na hapendi tutegemee vitu na mambo mengine, yeye hutupa amani hata wakati wa hofu kubwa inayoikumba dunia yeye humwaga Baraka kwa watu wote wanaomtegemea

Yeremia 17:5-7 “Bwana asema hivi, Amelaaniwa mtu yule amtegemeaye mwanadamu, Amfanyaye mwanadamu kuwa kinga yake Na moyoni mwake amemwacha Bwana. Maana atakuwa kama fukara nyikani, Hataona yatakapotokea mema; Bali atakaa jangwani palipo ukame, Katika nchi ya chumvi isiyokaliwa na watu. Amebarikiwa mtu yule anayemtegemea Bwana, Ambaye Bwana ni tumaini lake”.

Mungu atupe imani thabiti sana wakati huu, tumtegemee yeye  na hata wakati wa hatari na majanga tumkumbuke yeye, tuendelee kuutegemea uwepo wake na ulinzi wake kwa sababu uwepo wake ni amani kubwa sana bila kujali nini kinatokea, Ayubu alipoteza kila kitu lakini alisimama imara kwa sababu alimtegemea Mungu, Wamtumainio Bwana ni kama Mlima sayuni hautatikisika wakaa milele, Zaburi 125:1 wengi wamepoteza uhai na kufa katika wakati huu wa Corona kwa sababu ya hofu na kutokuwa na imani kwa Mungu, hapa Tanzania watu wengi pia waliogopa lakini ashukuriwe Mungu kwamba tuna Rais anayemcha Mungu, na amekuwa sio rais tu bali ni mlezi wa kiroho wa taifa. Alisimama katika imani kuliko hata viongozi wa kiroho wengine, na aliwakosoa vikali hata wale waliofunga nyumba za ibada ! na kuwakumbusha kuwa imara kama Daniel Shadrack meshak na Abednego.
Mungu wetu habadiliki na kanuni zake ni zilezile, Mungu yuleyule aliyetenda kazi nyakati za agano la kale ndiye anayetenda kazi hata sasa, Biblia inasema hivi

Zaburi 105:5 “Kwa kuwa Bwana ndiye mwema; Rehema zake ni za milele; Na uaminifu wake vizazi na vizazi inasema

Tukimtegemea Mungu tutakuwa salama katika ulimwengu usio salama, tuendelee kutegemea yeye na kusimama katika nafasi yetu, tunapoiangalia hali halisi leo tutaweza kukubaliana kabisa kuwa ulimwenguni sio mahali salama lakini imani yetu ikisimama katika neno la Mungu na ahadi zake na wote tukasimama imara katika imani na kuondoa hofu na kuwa na ujasriri  hakuna kitu kitakuja kututikisa duniani.

1Wakoritho 16:13 “Kesheni, simameni imara katika Imani, fanyeni kiume, mkawe hodari.” Biblia inasema

Isaya 26:3 “Utamlinda yeye ambaye moyo wake umekutegemea Katika amani kamilifu, kwa kuwa anakutumaini.”

Rev. Innocent Kamote
Mkuu wa Wajenzi mwenye Hekima!
0718990796

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni