Alhamisi, 10 Februari 2022

Mimi ni ngao yako na thawabu yako kubwa sana !


Mwanzo 15:1Baada ya mambo hayo neno la BWANA likamjia Abramu katika njozi, likinena, Usiogope, Abramu, Mimi ni ngao yako, na thawabu yako kubwa sana.”



Utangulizi:

Mojawapo ya sehemu muhimu sana katika maandiko ambapo unaweza kupata faraja ya kiungu ni pamoja na eneo hili ambapo tunasoma kuwa Mungu alisema na Abraham katika njozi na kumtia Moyo kwa maneno makubwa matatu muhimu sana, USIOGOPE, MIMI NI NGAO YAKO NA THAWABU YAKO KUBWA SANA, Maneno haya ya muhimu ambayo ndio sehemu kuu ya somo letu kwa leo yana umuhimu mkubwa sana, Sio kwa Abrahamu tu bali na kwetu sisi katika nyakati hizi za leo!

Mwanzo 15:1Baada ya mambo hayo neno la BWANA likamjia Abramu katika njozi, likinena, Usiogope, Abramu, Mimi ni ngao yako, na thawabu yako kubwa sana.”

Kimsingi Biblia inapotumia maneno Neno la Bwana likamjia likisema, hapo maana yake Mungu anazungumza na Abrahamu kama nabii, kwa hiyo kimsingi lugha hii ni ya kinabii na unaweza kuiona Lugha hii ikitumika katika vitabu vya kinabii, lakini sio hivyo tu Neno la Bwana pia hutumika kumwakilisha Kristo, na kwa sababu hiyo maneno haya ya kutia moyo yanazungumza sio na Abraham tu bali na kila mmoja anayeisikia sauti hii kwa msingi huo tutajifunza somo hili MIMI NI NGAO YAKO NA THAWABU YAKO KUBWA SANA Kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-

·         Kuondolewa kwa  Hofu za maisha 

·         Ahadi ya Ulinzi wa Mungu

·         Ahadi ya Mafanikio kwa kuwa na Mungu

Kuondolewa kwa Hofu za Maisha!

Mwanzo 15:1Baada ya mambo hayo neno la BWANA likamjia Abramu katika njozi, likinena, Usiogope, Abramu, Mimi ni ngao yako, na thawabu yako kubwa sana.”

Ni neno lenye kutia moyo kuliko namna tunavyoweza kufikiri, Katika maandiko haya kwanza kabisa Mungu anataka kumuondoa hofu Abrahamu kutokana na hofu ya maisha yake. Biblia inaanza kwa kusema “baada ya mambo hayo…”  Neno la bwana lilimjia katika Njozi kusema Usiogope, hii maana yake ni kuwa kulikuwa na aina Fulani ya hofu katika maisha ya Abrahamu, Biblia inasema baada ya mambo haya ni yepi? Abrahamu alikuwa ametoka kupigana na wafalme kadhaa wa kanaani na kumuokoa Nduguye Lutu, Pamoja na mfalme wa Sodoma, na Gomorah kwa kuwa Lutu aliishi huko akamuokoa pamoja na mali zake zote,Lakini vilevile alimsaidia mfalme wa Salem  na wengineo ona

Mwanzo 14:1-19Ikawa siku za Amrafeli mfalme wa Shinari, na Arioko mfalme wa Elasari, na Kedorlaoma mfalme wa Elamu na Tidali mfalme wa Goimu, walifanya vita na Bera mfalme wa Sodoma na Birsha mfalme wa Gomora, na Shinabu mfalme wa Adma, na Shemeberi mfalme wa Seboimu, na mfalme wa Bela, ndio Soari. Hawa wote wakakutana panapo bonde la Sidimu, kwenye Bahari ya Chumvi. Miaka kumi na miwili walimtumikia Kedorlaoma, hata mwaka wa kumi na tatu wakaasi. Na mwaka wa kumi na nne akaja Kedorlaoma na wafalme waliokuwa pamoja naye, wakawapiga Warefai katika Ashteroth-karnaimu, na Wazuzi katika Hamu, na Waemi katika Shawe-kiryathaimu, na Wahori katika mlima wao Seiri, mpaka Elparani iliyo karibu na jangwa. Kisha wakarudi wakaja mpaka Enmisfati, ndio Kadeshi, wakapiga nchi yote ya Waamaleki, na Waamori waliokaa Hasason-tamari. Mfalme wa Sodoma, na mfalme wa Gomora, na mfalme wa Adma, na mfalme wa Seboimu, na mfalme wa Bela, ndio Soari, wakatoka wakapanga vita panapo bonde la Sidimu; wapigane na Kedorlaoma mfalme wa Elamu, na Tidali mfalme wa Goimu, na Amrafeli mfalme wa Shinari, na Arioko mfalme wa Elasari, wafalme wanne juu ya wale watano. Na bonde la Sidimu lilikuwa limejaa mashimo ya lami. Nao wafalme wa Sodoma na Gomora wakakimbia, wakaanguka huko, nao waliosalia wakakimbia milimani. Wakachukua mali zote za Sodoma na Gomora na vyakula vyao vyote, wakaenda zao. Wakamtwaa Lutu, mwana wa nduguye Abramu, aliyekaa huko Sodoma, na mali yake, wakaenda zao. Mtu mmoja aliyeponyoka akaenda, akampasha habari Abramu Mwebrania; naye amekaa panapo mialoni ya Mamre, yule Mwamori, ndugu ya Eshkoli, na ndugu ya Aneri, na hao walikuwa wamepatana na Abramu. Abramu aliposikia ya kwamba nduguye ametekwa mateka, akawapa silaha vijana wake, waliozaliwa katika nyumba yake, watu mia tatu na kumi na wanane, akawafuata mpaka Dani. Akajipanga apigane nao usiku, yeye na watumwa wake, akawapiga, akawafukuza mpaka Hoba, ulioko upande wa kushoto wa Dameski. Naye akarudisha mali zote, akamrudisha na Lutu nduguye na mali zake, na wanawake pia, na watu. Abramu aliporudi kutoka kumpiga Kedorlaoma na wale wafalme waliokuwa pamoja naye, mfalme wa Sodoma akatoka amlaki katika bonde la Shawe, nalo ni Bonde la Mfalme. Na Melkizedeki mfalme wa Salemu akaleta mkate na divai, naye alikuwa kuhani wa Mungu Aliye juu sana.  Akambariki, akasema, Abramu na abarikiwe na Mungu Aliye juu sana, Muumba mbingu na nchi

 Abrahamu alikuwa amepata ushindi mkubwa sana dhidi ya maadui zake, aliwashinda wafalme wenye nguvu na wakubwa sana tena waliokuwa wameungana lakini nadhani alipokuwa ametulia tayari alikuwa na mawazo kuwa hatakuwa na amani kwani adui zake watajipanga kwa vita tena dhidi yake na hasa kwa sababu yeye ni mgeni  katiika incho ya wakanaani bila shaka akiwa na mawazo haya, Ni wazi sana katika vita za kizamani katika biblia pale unapopata ushindi mkubwa haimaanishi kuwa uko salama kwani ilikuwa lazima adui akajipange tena kwa mbinu nyingine na ili aweze kuja tena kwa namna nyingine kivita, ni katika utaratibu kama huu adui yetu shetani huwa ana jipanga tena anapokuwa ameshindwa vita ili kuja kwa mbinu nyingine na kutushambulia kwa sababu kama hizi lazima Abrahamu alikuwa na mawazo kuwa huenda vita kali zitamkabili tena, Kutoka kwa wapinzani wake na huenda watakuja na timu kubwa zaidi,  sasa Neno la Mungu linamjia na kumtaka asiogope, aache kuwaza dhidi ya vita  kwani Mungu aliyempa ushindi anamuhakikishia kuwa hakuna kitakachoweza kusimama mbele yake tena Mungu alikuwa akimthibitishia Abrahamu kuwa yeye atakuwa pamoja naye na kuwa asiogope sawa tu na namna alivyomwambia Yoshua, ona :-

Yoshua 1:  5-9 “Hapatakuwa mtu ye yote atakayeweza kusimama mbele yako siku zote za maisha yako; kama nilivyokuwa pamoja na Musa, ndivyo nitakavyokuwa pamoja na wewe; sitakupungukia wala sitakuacha. Uwe hodari na moyo wa ushujaa, maana ni wewe utakayewarithisha watu hawa nchi hii niliyowaapia baba zao ya kwamba nitawapa. Uwe hodari tu na ushujaa mwingi, uangalie kutenda sawasawa na sheria yote aliyokuamuru Musa mtumishi wangu; usiiache, kwenda mkono wa kuume, au wa kushoto, upate kufanikiwa sana kila uendako. Kitabu hiki cha torati kisiondoke kinywani mwako, bali yatafakari maneno yake mchana na usiku, upate kuangalia kutenda sawasawa na maneno yote yaliyoandikwa humo; maana ndipo utakapoifanikisha njia yako, kisha ndipo utakapositawi sana. Je! Si mimi niliyekuamuru? Uwe hodari na moyo wa ushujaa; usiogope wala usifadhaike; kwa kuwa Bwana, Mungu wako, yu pamoja nawe kila uendako.”

Wakati wote Mungu anapotaka kuthibitisha kuwa yuko pamoja nasi anatuita kwa majina yetu ili kwamba akutie Moyo haijalishi ni hofu ya aina gani iko mbele yako jambo kubwa na la msingi ni kuwa usiogope haijalishi umezungukwa ana adui pande zote au wanaojipanga kukushambulia ni wenye nguvu au ni wengi bado kwa Mungu hawawezi kutoboa na kufanikiwa dhidi yako hivyo usiogope hapa Mungu hataki wewe na mimi tuwe na hofu za maisha yetu, Yuko Mungu anayetulinda anayejishughulisha sana na mambo yetu hivyo hatupaswi kuogopa, Mpenzi Mungu amenituma nikuhakikihie kuwa usiogope, usiogope, usiogope.

Ahadi ya Ulinzi wa Mungu

Baada ya Mungu kumuondolea Hofu Abrahamu kwa kumwambia asiogope Mungu anamuhakikishia Abrahamu ulinzi, anamthibitishia kuwa yeye ni ngao yake na hivyo atamlinda dhidi ya adui zake wote haijalishi ni wengi kiasi gani na wala haijalishi wana nguvu kwa kiwango gani kama jinsi ambavyo Yesu Kristo ni ngao yetu ndivyo Mungu anavyomthibitishia Abrahamu na sisi kuwa yeye ni ngao yetu na kuwa yuko pamoja nasi Maandiko yanamtaja Mungu kama ngao yetu mara nyingi sana hususani katika zaburi ona

Zaburi 3:1-3 “Bwana, watesi wangu wamezidi kuwa wengi, Ni wengi wanaonishambulia, Ni wengi wanaoiambia nafsi yangu, Hana wokovu huyu kwa Mungu. Na Wewe, Bwana, U ngao yangu pande zote, Utukufu wangu na mwinua kichwa changu

Zaburi 7:9-11 “Ubaya wao wasio haki na ukome, Lakini umthibitishe mwenye haki. Kwa maana mjaribu mioyo na viuno Ndiye Mungu aliye mwenye haki. Ngao yangu ina Mungu, Awaokoaye wanyofu wa moyo. Mungu ni mwamuzi mwenye haki, Naam, Mungu aghadhibikaye kila siku.”

Zaburi 28:7-8 “Bwana ni nguvu zangu na ngao yangu. Moyo wangu umemtumaini, Nami nimesaidiwa; Basi, moyo wangu unashangilia, Na kwa wimbo wangu nitamshukuru. Bwana ni nguvu za watu wake, Naye ni ngome ya wokovu kwa masihi wake

Zaburi 33:19-21 “Yeye huwaponya nafsi zao na mauti, Na kuwahuisha wakati wa njaa. Nafsi zetu zinamngoja Bwana; Yeye ndiye msaada wetu na ngao yetu. Maana mioyo yetu itamfurahia, Kwa kuwa tumelitumainia jina lake takatifu.”

Zaburi 84:9-12 “Ee Mungu, ngao yetu, uangalie, Umtazame uso masihi wako.Hakika siku moja katika nyua zako Ni bora kuliko siku elfu. Ningependa kuwa bawabu nyumbani mwa Mungu wangu, Kuliko kukaa katika hema za uovu. Kwa kuwa Bwana, Mungu, ni jua na ngao, Bwana atatoa neema na utukufu. Hatawanyima kitu chema Hao waendao kwa ukamilifu. Ee Bwana wa majeshi, Heri mwanadamu anayekutumaini Wewe.

Zaburi 89:18 “Maana ngao yetu ina Bwana, Na mfalme wetu ni wake Mtakatifu wa Israeli.”

Muda usingeweza kutosha kuziona ahadi za Mungu kwa kila Mtu amchaye na kumtegemea yeye kama Mungu alivyomwambia Abrahamu na kumuahidi kuwa yeye ni ngao yeke, Mungu ni ngao kwa kila anayemtegemea ukimtegemea yeye Mungu hatakuangusha wala hatakuacha atakupa ushindi mmoja mpaka ushindi mwingine na atakulinda hakuna silaha itafanikiwa juu yako, hakuna mbinu itatoboa dhidi yako Mungu atakutetea kama alivyomthibitishia Abrahamu leo neno la Mungu linatuthibitishia ulinzi wetu na kutueleza wazi kuwa tunalindwa na nguvu za Mungu

 1Petro 1:5 “Nanyi mnalindwa na nguvu za Mungu kwa njia ya imani hata mpate wokovu ulio tayari kufunuliwa wakati wa mwisho.”

Ahadi ya Mafanikio kwa kuwa na Mungu.

Mwanzo 15:1Baada ya mambo hayo neno la BWANA likamjia Abramu katika njozi, likinena, Usiogope, Abramu, Mimi ni ngao yako, na thawabu yako kubwa sana.” Licha ya Mungu kumwambia Abrahamu asiogope na kuwa yeye ni ngao yake lakini Mungu vilevile alimthibitishia Abrahamu kuwa yeye ni thawabu yake kubwa sana, kwa nini ? Abrahamu aliteka nyara nyingi sana ambazo aliruhusu wafalme jirani wazichukue, sio hivyo tu Abraham alihakikisha kuwa mali za wenyewe za wafalme wote waliokuwa wamepora na mwana wa ndugu yake Lutu wote walirejeshewa mali zote zilizotekwa nyara na maadui, Jambo hili lilionekana kama ujinga Abrahamu hakutaka mwanadamu ajisifu kuwa ametajirishwa na wanadamu Abrahamu aliamua kuacha mali na kijitegemeza kwa Mungu ona

Mwanzo 14:21-23 “Mfalme wa Sodoma akamwambia Abramu, Nipe mimi hao watu, na hizo mali uchukue wewe. Abramu akamwambia mfalme wa Sodoma, Nimeinua mkono wangu kwa BWANA, Mungu Aliye juu sana, Muumba mbingu na nchi, ya kuwa sitatwaa uzi wala gidamu ya kiatu wala cho chote kilicho chako, usije ukasema, Nimemtajirisha Abramu;”

Abrahamu alikuwa amejiapiza kwa Mungu nimeinua mkono wangu kwa Mungu maana yake nimeapa, hakutaka kuwa na mali ambazo asili yake ni wanadamu mali hizi zingeliweza kuleta utajiri mkubwa sana huenda alionekana mjinga kwa kuzikataa, Abrahamu hakutaka mali za udhalimu, Mungu alikuwa amemuahidi kuwa atambariki, kwa hiyo asili ya Baraka zake ilipaswa kuwa Mungu mwenyewe na sio mali za udhalimu au zinazotokana na kuteka nyara !

Mungu alimtia Moyo Abrahamu kuwa Yeye ni thawabu yake kubwa sana hii ilikuwa ni ahadi kubwa ya kuwa Mungu atamfanikisha Abrahamu kwa neema na utukufu mkubwa sana kwani kuwa na Mungu ambaye ndio chanzo cha utajiri ni muhimu zaidi kuliko kuwa na utajiri usiotokana na  Mungu, chanzo chake kikuu na mafanikio ni MUngu, Neno la Mungu leo linatukumbusha kuwa Yesu kwetu ni thawabu yetu kubwa sana ni utajiri mkubwa sana ni utoshelevu wa hali ya juu kuwa na Yesu kunalipa kuliko kuwa na mali, magari na nyumba na fedha ambazo asili yake sio Yesu, kuwa na mali na kutokuwa na Yesu machoni pa Mungu ni uduni,umasikini na uchi, Lakini kumpata Yesu ni zaidi

Ufunuo 3:17-18 “Kwa kuwa wasema, Mimi ni tajiri, nimejitajirisha, wala sina haja ya kitu; nawe hujui ya kuwa wewe u mnyonge, na mwenye mashaka, na maskini, na kipofu, na uchi. Nakupa shauri, ununue kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto, upate kuwa tajiri, na mavazi meupe upate kuvaa, aibu ya uchi wako isionekane, na dawa ya macho ya kujipaka macho yako, upate kuona.”       

Yesu anatushauri kuwa utajiri wa kweli ni kununua kwake yaani ni kumuamini yeye ambaye ndio chanzo cha utajiri wa kudumu, Mungu ametuahidi mafanikio makubwa sana hakuna kitu atatunyima yeye anasema tafuteni kwanza ufalme wa Mungu na haki yake na mengine yote mtazidishiwa Hakuna sababu ya kujisumbukia na kutafuta mali na fedha na mavazi na chakula tusumbuke kumtafuta Yesu na mambo mengine yote mtazidishiwa

Mathayo 6:25-33 “Kwa sababu hiyo nawaambieni, Msisumbukie maisha yenu, mle nini au mnywe nini; wala miili yenu, mvae nini. Maisha je! Si zaidi ya chakula, na mwili zaidi ya mavazi? Waangalieni ndege wa angani, ya kwamba hawapandi, wala hawavuni, wala hawakusanyi ghalani; na Baba yenu wa mbinguni huwalisha hao. Ninyi je! Si bora kupita hao?  Ni yupi kwenu ambaye akijisumbua aweza kujiongeza kimo chake hata mkono mmoja? Na mavazi, ya nini kuyasumbukia? Fikirini maua ya mashamba, jinsi yameavyo; hayafanyi kazi, wala hayasokoti nami nawaambia, ya kwamba hata Sulemani katika fahari yake yote hakuvikwa vizuri kama mojawapo la hayo. Basi, ikiwa Mungu huyavika hivi majani ya kondeni, yaliyopo leo, na kesho hutupwa kalibuni, je! Hatazidi sana kuwavika ninyi, enyi wa imani haba? Msisumbuke, basi, mkisema, Tule nini? Au Tunywe nini? Au Tuvae nini? Kwa maana hayo yote Mataifa huyatafuta; kwa sababu Baba yenu wa mbinguni anajua ya kuwa mnahitaji hayo yote. Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa.”

Yesu ni thawabu yetu kubwa sana

Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima 


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni