Ijumaa, 8 Novemba 2024

Tajiri lakini masikini


Ufunuo 3:14-19. “Na kwa malaika wa kanisa lililoko Laodikia andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye Amina, Shahidi aliye mwaminifu na wa kweli, mwanzo wa kuumba kwa Mungu. Nayajua matendo yako, ya kuwa hu baridi wala hu moto; ingekuwa heri kama ungekuwa baridi au moto. Basi, kwa sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika kinywa changu. Kwa kuwa wasema, Mimi ni tajiri, nimejitajirisha, wala sina haja ya kitu; nawe hujui ya kuwa wewe u mnyonge, na mwenye mashaka, na maskini, na kipofu, na uchi. Nakupa shauri, ununue kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto, upate kuwa tajiri, na mavazi meupe upate kuvaa, aibu ya uchi wako isionekane, na dawa ya macho ya kujipaka macho yako, upate kuona.Wote niwapendao mimi nawakemea, na kuwarudi; basi uwe na bidii, ukatubu.”


Utangulizi:

Katika kitabu cha Ufunuo 3:17 “Kwa kuwa wasema, Mimi ni tajiri, nimejitajirisha, wala sina haja ya kitu; nawe hujui ya kuwa wewe u mnyonge, na mwenye mashaka, na maskini, na kipofu, na uchi.”

Kutoka katika kifungu kikuu cha somo letu tunakutana na maneno mazito ya Yesu Kristo kwa kanisa lililokuwako Laodikia. Katika mstari huo Yesu anakemea na kutujulisha hali ya kiroho ya Kanisa lililokuwako Laodikia ya kuwa wamepoteza kabisa hali yao ya kuwa matajiri wa kiroho na badala yake wamekuwa wakijivunia utajiri wa mwilini na kusahau kile ambacho wanatakiwa kukipa kipaumbele, katika maisha ya kiroho. Katika ujumbe huu leo Roho Mtakatifu ambaye ndiye Mwalimu wetu mkuu anataka kutukumbusha umuhimu wa maneno hayo kwa kutufundisha ili tuweze kujifunza na kuchukua tahadhari katika siku zetu za leo, tutajifunza somo hili “Tajiri lakini masikini” kwa kuzingatia vipengele vikuu vitatu vifuatavyo:-

·         Kwa kanisa lililoko Laodikia

·         Hali ya kiroho katika kanisa lililokuwako Laodikia

·         Tajiri lakini Masikini     

  

Kwa Kanisa lililoko Laodikia

Laodekia ulikuwa ni moja ya miji mikubwa sana na mizuri iliyokuwako katika Asia katika bonde la Lycos jimbo la Phrygia eneo ambalo yalikuwako makanisa saba yanayotawa katika kitabu cha ufunuo ambayo kimsingi yalikuwako kijiografia katika Adia ndogo yaani eneo la Asia linalopakana na ulaya iliko inchi ya Uturuki leo.au Eneo lililojulikana kama Kapadokia, Eneo hilo lilibarikiwa sana nyakati za karne ya kwanza kwa kuikubali injili na kuwa maeneo yenye utajiri wa Kikristo kutokana na kuhudumiwa na mitume pamoja na watenda kazi waliokuwa wameiva vya kutosha katika kuifanya kazi ya Bwana kwa kueneza injili na kufundisha.

Ufunuo 1:11 “ikisema, Haya uyaonayo uyaandike katika chuo, ukayapeleke kwa hayo makanisa saba: Efeso, na Smirna, na Pergamo, na Thiatira, na Sardi, na Filadelfia, na Laodikia.”

Tofauti na historia ya miji mingine iliyotajwa katika maaandiko hayo hapo, Laodekia ni mji uliojengwa na mfalme Antiochus II kati ya mwaka 261-246 BC Kabla ya Kristo, na mji huu ukapewa jina la mke wa mfalme huyo Malikia aliyeitwa Laodikia, kwa kiingereza LAODICEA na kwa kiyunani Laodikia, Jina Laodikia ni muunganiko wa maneno mawili ya kiyunani “Laos” ambalo maana yake ni Common People ambalo kwa Kiswahili ni watu wa kawaida na neno “dike” ambalo maana yake ni Justice kwa Kiswahili haki kwa watu wa kawaida, Hiyyo maana kamili ya Laodikia ni watu wa haki au mtu mwenye haki, au Popular Judgement au Popular Approval ambalo maana yake mwenye kukubalika sana na watu wa kawaida, au wenye umaarufu, Mji huu uliundwa kwa pamoja na mkusanyiko wa Wayahudi na Wasiria ambao walisafirishwa kutoka Babeli mpaka katika miji ya Phrygia na Lydia huku Laodekia ukiwa ndio mji uliokuwa katika njia kuu, Kutokana na makazi ya kijiografia ulilokuwa mji huu, Mji ulikuwa na mafanikio makubwa sana kibiashara kiuchumi na viwanda, Kulikuwa na maendeleo makubwa ya viwanda vya nguo, chuo cha madawa ya tiba na hasa dawa za macho na dawa nyinginezo na mafanikio makubwa sana ya kiuchumi, Walaodikia walikuwa na ufugaji wa kondoo wazuri waliozalisha manyoya yaliopelekwa kiwandani na kuzalisha nguo za viwango vya juu sana, kwa hiyo watu wa Laodekia pia walivaa vizuri sana na kuuza nguo za hali ya juu, pia walikuwa watengenezaji wazuri wa Mazuria “Carpets” jambo ambalo mpaka siku za leo Mazuria kutoka Uturuki yamekuwa na umaarufu mkubwa sana duniani, kimsingi Laodekia pia ulikuwa ni mji wenye Benki kubwa yenye utajiri mkubwa wa fedha katika Asia na ulikuwa ni mji wa watu wenye mafanikio makubwa sana, Mji huu ulikuwa na bomba kubwa la maji yaliyotengenezwa kutoka katika chemichemi iliyokuwa ikitoa maji ya moto huko Hierapolis mji ulioko maili sita hivi kutoka Laodikia, maji hayo yalifika mjini na wanawake walikuwa wakichota maji hayo na kupeleka majumbani mwao, maji yao yalifika nyumbani yakiwa vuguvugu, na au wakati mwingine yakiwa yamepoa. Paulo Mtume aliwahi kuwaandikia waraka wakristo waliokuwako Laodikia, katika kanisa lililokuwako huko na kuagiza kuwa wausome kwa kubadilishana na ule wa Wakolosai, Hata hivyo kwa bahati mbaya waraka huo wa Paulo Mtume kwa Walaodikia haukuweza kupatikana zaidi ya maelezo yake, kwa hiyo inakisiwa ya kuwa waraka wa Paulo mtume kwa walaodikia huenda ulipotea au kuna uwezekano ukawa ni pamoja na ule wa Wakolosai.  

Wakolosai 4:15-16 “Wasalimuni ndugu walioko Laodikia, na Nimfa, na kanisa lililo katika nyumba yake.Waraka huu ukiisha kusomwa kwenu fanyeni kwamba usomwe katika kanisa la Walaodikia pia; na ule wa Laodikia usomwe na ninyi.”

Kutokana na Mafanikio makubwa ya ukazi wa mji huu watu wake nao walifanikiwa sana na kuwa matajiri mno, Kanisa lilipoanzishwa katika mji huu lilikuwa na washirika waliokuwa vizuri kifedha na wenye mafanikio makubwa sana ya utajiri na umiliki wa mali za dunia, Kanisa lilianzishwa hapa na moja ya watenda kazi pamoja na Paulo Mtume aliyeitwa Epafra, kwa hiyo wakati Paulo mtume anaandika waraka kwa Wakolosai alikuwa bado hajautembelea mji huu wa Kolosai na Laodikia na kanisa lililokuwako, Kama tunavyoweza kuona akitamani kuwatembelea wale ambao hawakuwa wameuona uso wake, Paulo mtume wakati huu alikuwa Efeso kwa hiyo ni wazi kuwa Epafra mtenda kazi pamoja naye alihubiri katika miji hiyo na kufungua makanisa katika Kolosai, Laodikia na Hierapoli na kutoa ripoti kwa Paulo mtume ambaye aliamua kuwaandikia kwa kusudi la kuwatia moyo waamini wa eneo hilo. Akifurahishwa na maendeleo yao kiroho na utumishi wa Epafra. Angalia:-

Wakolosai 1:3-8 “Twamshukuru Mungu, Baba yake Bwana wetu Yesu Kristo, siku zote tukiwaombea; tangu tuliposikia habari za imani yenu katika Kristo Yesu, na upendo mlio nao kwa watakatifu wote; kwa sababu ya tumaini mlilowekewa akiba mbinguni; ambalo habari zake mlizisikia zamani kwa neno la kweli ya Injili; iliyofika kwenu, kama ilivyo katika ulimwengu wote, na kuzaa matunda na kukua, kama inavyokua kwenu pia, tangu siku mlipoisikia mkaifahamu sana neema ya Mungu katika kweli; kama mlivyofundishwa na Epafra, mjoli wetu mpenzi, aliye mhudumu mwaminifu wa Kristo kwa ajili yenu; naye alitueleza upendo wenu katika Roho.”

Wakolosai 2:1-3 “Maana nataka ninyi mjue jinsi ilivyo kuu juhudi yangu niliyo nayo kwa ajili yenu, na kwa ajili ya wale wa Laodikia, na wale wasioniona uso wangu katika mwili; ili wafarijiwe mioyo yao, wakiunganishwa katika upendo, wakapate utajiri wote wa kufahamu kwa hakika, wapate kujua kabisa siri ya Mungu, yaani, Kristo; ambaye ndani yake yeye hazina zote za hekima na maarifa zimesitirika.”

Wakolosai 4:12-13 “Epafra, aliye mtu wa kwenu, mtumwa wa Yesu Kristo, awasalimu, akifanya bidii siku zote kwa ajili yenu katika maombi yake, ili kwamba msimame wakamilifu na kuthibitika sana katika mapenzi yote ya Mungu. Maana namshuhudia kwamba ana juhudi nyingi kwa ajili yenu, na kwa ajili ya hao walioko Laodikia, na kwa ajili ya hao walioko Hierapoli.”        

Kutokana na mafanikio waliyokuwa nao watu hao walijiamini sana kwa sababu hata kanisa lilikuwa na hali nzuri ya kifedha na kiuchumi, na kimsingi Mungu anapenda sana watu wake wafanikiwe wamiliki fedha na uchumi kwa sababu kazi ya Mungu pia hufanikiwa sana kama tutakuwa na waamini ambao wako vizuri kiuchumi na kifedha, watu wa Laodekia walikuwa watu wavumilivu sana na waaminifu mno, mji wao ulikuwa na historia ya kukumbwa na matetemeko, na uko wakati mji huu uliathiriwa vibaya na tetemeko kubwa na kuharibiwa na uongozi wa Rumi ulitaka kuwapa msaada wa kifedha kwaajili ya kuujenga tena mji huo, lakini wakazi wake waliamua kujichangisha wenyewe na wakaujenga mji huo kwa ubora zaidi ya kwanza tukio hili  lilikuwa ni kati ya mwaka wa 60-68 AD kwa hiyo unaweza kupata picha kuwa walikuwa ni watu wanaojitosheleza na hawakuhitaji msaada hali iliyowapa kujiamini sana. Kwa hiyo Kanisa la Laodikia walikuwa matajiri sana.

Hali ya kiroho katika kanisa lililokuwako Laodikia

Kimsingi hali ya kanisa wakati linaanzishwa ilikuwa ni nzuri na njema sana Epafra alimpa Paulo mtume taarifa njema ya maendeleo ya makanisa hayo na Paulo Mtume alikubali na kuwandikia waraka wa kuwatia moyo akiwaombea neema ya kupata kumjua Yesu zaidi, na kuwa na hekima na ufahamu wa hazina zote za mbinguni, hata hivyo baada ya miaka mingi baadaye kutoka mwaka wa 60 mpaka wakati kitabu cha ufunuo kinaandikwa yaani mwaka wa 95-100 hivi Kanisa hili lilianza kuathiriwa na tabia za mkuu wa anga wa mji ule, na hivyo kanisa lilianza kupoteza sifa njema lililokuwa nazo awali, na ndio maana Yesu katika waraka wake kupitia Yohana kwenye kitabu cha ufunuo aliwakemea ili aweze kuwarekebisha na kuwatia moyo ili waweze kuwa washindi apate kukaa nao katika kiti cha enzi mbinguni, Kanisa lilianza kufunga mlango kwa Kristo na kuamini ya kuwa wanajitosheleza kwa kila hali jambo lililopelekea kubaki na utajiri wao wa kiuchumi lakini kuwa masikini sana katika maswala ya kiroho na kuanza kutia aibu kama watu walio uchi mbele za Kristo.

Ufunuo 3:14-21 “Na kwa malaika wa kanisa lililoko Laodikia andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye Amina, Shahidi aliye mwaminifu na wa kweli, mwanzo wa kuumba kwa Mungu. Nayajua matendo yako, ya kuwa hu baridi wala hu moto; ingekuwa heri kama ungekuwa baridi au moto. Basi, kwa sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika kinywa changu.Kwa kuwa wasema, Mimi ni tajiri, nimejitajirisha, wala sina haja ya kitu; nawe hujui ya kuwa wewe u mnyonge, na mwenye mashaka, na maskini, na kipofu, na uchi. Nakupa shauri, ununue kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto, upate kuwa tajiri, na mavazi meupe upate kuvaa, aibu ya uchi wako isionekane, na dawa ya macho ya kujipaka macho yako, upate kuona. Wote niwapendao mimi nawakemea, na kuwarudi; basi uwe na bidii, ukatubu.Tazama, nasimama mlangoni, nabisha; mtu akiisikia sauti yangu, na kuufungua mlango, nitaingia kwake, nami nitakula pamoja naye, na yeye pamoja nami. Yeye ashindaye, nitampa kuketi pamoja nami katika kiti changu cha enzi, kama mimi nilivyoshinda nikaketi pamoja na Baba yangu katika kiti chake cha enzi.”    

Katika kifungu hiki tunaweza kuona ni changamoto gani ambazo zilikuwa zinalikumba kanisa la Laodikia na jinsi Yesu Kristo alivyokuwa akishughulikia changamoto zao ambazo zilikuwa zikiwasumbua

1.       Ufahamu finyu kuhusu Yesu Kristo – Kanisa la Laodikia lilikuwa limeathiriwa na baadhi ya mafundisho ya waanostisizim na waariyan (Gnosticism and Arians) ambao kimsingi walimuona Yesu Kristo kama ambaye hayuko sawa na Mungu, na kuwa Kristo ni Roho iliyoumbwa na Mungu, na ambaye yuko juu kidogo ya wanadamu na malaika lakini yuko chini ya Mungu, kwa hiyo kulikuwa na mashaka sana kuhusu uungu wa Yesu Kristo, kama tu leo tunavyoweza kuona baadhi ya watumishi wa Mungu wakianza kuropoka na kupoteza muelekeo kuhusu uungu wa Yesu Kristo, wao walianza vizuri wakiamini katika uungu wa Yesu Kristo na katika hali duni na ya umasikini, lakini walipofanikiwa kupitia jina la Yesu na kufanikiwa na kuwa matajiri na kuwa na kila kitu, mavazi, magari, na kadhalika wanaaza kutamka wazi wazi na kukanusha uwepo wa Mungu Baba na Mwana na Roho Mtakatifu wakilihesabu fundisho hilo kuwa ni mapokeo, Mafanikio yoyote ya kimwili yakitupa kiburi na kuanza kupuuzia misingi ya Imani ikiwepo uungu wa Yesu au utatu wa Mungu na kudhani kuwa fundisho hili ni la kizushi huo ni mwanzo wa kujifikiria kuwa tumetajirika, na kuwa tuna mavazi mazuri, na kuwa tuna akiba ya kutosha lakini kwa Mungu ni uchi masikini na mnyonge na mwanzo wa kufilisika kiroho.

 

Yesu aliwaeleza Walaodikia ya kuwa Yeye ni Amina, na ni shahidi aliye mwaminifu na mwanzo wa kuumba kwa Mungu. Ona 

 

Ufunuo 3:14 “Na kwa malaika wa kanisa lililoko Laodikia andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye Amina, Shahidi aliye mwaminifu na wa kweli, MWANZO WA KUUMBA KWA MUNGU.”  

 

Yesu alikuwa na maana gani katika kifungu hiki? Yesu alikuwa anajifunua kwa Walaodikia kwamba wanapaswa kumuamini yeye, wanapaswa kuamini fundisho la kweli walilopata kulisikia kutoka kwa Mitume kuhusu Yesu ya kwamba yeye ni Bwana, kwa hiyo hawapaswi kumpuuzia Yesu na kuanza kumfungia mlango kwa kudhani ya kuwa Yesu, Yeye sio wa kuaminiwa, yeye yuko chini ya Mungu, na yuko juu ya malaika kiasi tu, wao waliacha kumuona Yesu kama kiini cha Baraka zao na mafanikio yao na hivyo waliweka Imani katika uchumi na maendeleo makubwa waliyokuwa nayo.  Kwa hiyo Yesu aliwajibu:-

 

a.       Yeye ni Amina – Hali ya kiroho ya washirika wa Laodikia ilikuwa mbaya wengi wa wanafunzi wake Pale Laodikia walikuwa tayari wametia shaka kuhusu Yesu Kristo iwapo kweli yeye ni Mungu? Licha ya mafanikio yao makubwa ya kimwili lakini hali yao ya kiroho ilianza kuwa mbaya kwa sababu walianza kuukana uungu wa Yesu Kristo na kumshushia thamani, Yesu akitaka kusema na watu hawa ili apate mwitikio wao anajiita yeye ni Amina – Neno amina maana yake ni Hakika, Ni kweli, Kwa hiyo Yesu alitaka kuwahakikishia kuwa anazungumza kweli na kuwathibitishia ukweli kuwa Yeye ni Mungu, Licha ya kuwa yeye ni Mungu lakini pia ni Msema kweli na kila kinachozungumzwa katika neno lake ni hakika na kweli na kila kilichoahidiwa katika neno lake ni kweli, Yesu ni wa uhakika na hakuna ubabaishaji kumuhusu yeye,  Matumizi ya Amina kwa Yesu Kristo yalikuwa ni uthibitisho ya kuwa yeye ni Mungu kamili na wa kweli na ndio ufunuo mkamilifu na wa mwisho wa Mungu.Yeye kweli ni Alpha na Omega.

 

2Wakorintho 1:20 “Maana ahadi zote za Mungu zilizopo katika yeye ni Ndiyo; tena kwa hiyo katika yeye ni Amin; Mungu apate kutukuzwa kwa sisi.”

 

b.      Shahidi aliye Mwaminifu – Yesu alikuwa kweli anamwakilisha Mungu, yeye ni chapa ya nafsi ya Mungu akiwakilisha asili na tabia ya uungu, Hakuna ufunuo mwingine zaidi wa Mungu Zaidi ya Yesu Kristo, Mungu alizungumza na manabii kwa njia nyingi na namna nyingi lakini siku hizi za mwisho amejifunua kwa Yesu Kristo, Yesu anaposema yeye ni Amina, Shahidi aliye mwaminifu, alikuwa akifafanua ukweli kwamba hakuna Zaidi yake na kuwa walaodikia wanapaswa kumuamini kwani Mungu hawezi kusema uongo. “Pistos martus” Shahidi mwaminifu, mfia Imani wa kweli.

 

Waebrania 1:1-2 “Mungu, ambaye alisema zamani na baba zetu katika manabii kwa sehemu nyingi na kwa njia nyingi, mwisho wa siku hizi amesema na sisi katika Mwana, aliyemweka kuwa mrithi wa yote, tena kwa yeye aliufanya ulimwengu.”               

 

Tito1:2 – “katika tumaini la uzima wa milele, ambao Mungu asiyeweza kusema uongo aliuahidi tangu milele;”

       

Wakolosai 1:13-15 – Naye alituokoa katika nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa pendo lake; ambaye katika yeye tuna ukombozi, yaani, msamaha wa dhambi; naye ni mfano wa Mungu asiyeonekana, mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote.”

 

Yohana 14:6 – “Yesu akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi.”

 

Yesu alikuwa akimaanisha kuwa kumfungia mlango yeye ni kwenda upotevuni, kama kanisa linaamua kumuona Yesu kuwa sio kitu basi ni lazima kanisa lielewe kuwa linajifungia njia ya kumfikia Mungu baba kwa namna yoyote ile, Yesu anajiita Amina, na anajiita Shahidi aliye mwaminifu ili kulithibitishia kanisa ya kuwa hakuna wokovu katika mwingine isipokuwa yeye, na kuwa ni yeye aliye juu ya yote na hivyo wanapaswa kumuamini na kuonda shaka kumuhusu. Kiongozi yeyote wa kanisa au kanisa lolote lile linalopunguza Heshima ya Yesu Kristo linapunguza Heshima ya Mungu vile vile na ufunuo wa kweli ambao Mungu amejifunua katika neno lake!

 

c.       Mwanzo wa kuumba kwa Mungu – maneno Mwanzo wa kuumba kwa Mungu na maneno Mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote yote yana maana moja, waalimu wa uongo walieneza habari ya kuwa Yesu ni mwanadamu wa kawaida tu na kuwa tofauti yake na viumbe wengine ni kuwa yeye aliumbwa kwanza,  Lakini Yesu alijitambulisha kuwa yeye ni mwanzo wa kuumba kwa Mungu sawa tu na kusema ni mzaliwa wa Kwanza wa viumbe vyote, kwa hiyo walaodikia waliamini kuwa Yesu hayuko sawa na Mungu wala sio Mungu, bali ni kiumbe cha kwanza kuumbwa na Mungu, sawa na Adamu kama mwanadamu wa kwanza kuumbwa na Mungu, Yesu aliliweka sawa fundisho hilo kwa kuwajibu kuwa Yeye ni Mwanzo wa kuumba kwa Mungu ona:-

 

Ufunuo 3:14 “Na kwa malaika wa kanisa lililoko Laodikia andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye Amina, Shahidi aliye mwaminifu na wa kweli, MWANZO WA KUUMBA KWA MUNGU.”

 

Maneno hayo mwanzo wa kuumba kwa Mungu yanasomeka hivi katika Biblia ya kiingereza ya King James Version (KJV) na Katika Biblia ya kiingereza ya New Internation Version (NIV)

 

Revelation 3:14 “And unto the angel of the church of Laodiceans write; these this saith the Amen, the faithful and true witness, THE BEGINNING OF CREATION OF GOD

 

Revelation 3:14 “To the angel of the church in Laodicea write; these are the words of the Amen, The faithful and true witness, THE RULER OF GOD’S CREATION

 

Na yanasomeka hivi katika biblia ya kiyunani

 

Revelation 3:14 “Kai angelos ekklēsia Laodikeus grapho; hode hēde tode lego Amēn, pistos kai alēthinos martus, archē ktisis theos

 

Neno hilo Archē maana yake ni Chief or rank or application of order in terms of time and place

 

Sawa na matumizi ya neno

 

Wakolosai 1:15 “naye ni mfano wa Mungu asiyeonekana, mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote.” “Hos hē ho esti eikōn aoratos Theos prōtotokos pas ktisis

 

Kwa hiyo neno Archē ambalo ni Oder na neno prōtotokos kwa kiingereza protocal  yanamaanisha WA KWANZA KATIKA CHEO na sio wa kwanza kuumbwa kwa hiyo Yesu ni Mungu ni kwa kwanza kuwepo kabla hata ya kuweko kwa Muda, yuko juu ya kila kitu, Kwa hiyo Yesu ni Mungu sawa tu na yanavyoeleza maandiko, Lakini watu wa Laodikia walikuwa wamedanganyika wakifikiri kuwa Yesu aliumbwa kwanza na kwa hiyo walianza kupoteza Imani na Yesu, walipoteza Imani kwa neno lake na wakidhani ya kuwa yeye sio shahidi wa kweli, Kristo alikuwa akiwaonyesha ya kuwa yeye ni wakuaminiwa, na alikuwa kwaajili ya kweli na kuwa yeye ni Mungu, “Mimi ni Amina, shahidi aliye muaminifu mwanzo wa kuumbwa kwa Mungu

 

Fundisho kuhusu uungu wa Yesu Kristo sio fundisho la uzushi, wala fundisho hilo halikuingizwa kwa hila na mkutano wa aina yoyote wa viongozi, fundisho kuhusu uungu wa Yesu ni fundisho la kibiblia tangu wakati wa agano la kale na kuthibitishwa na wakati wa agano jipya, malengo yote na kusudi lote la maandiko ni kumuhusu Yesu Kristo yeye ndio Mwokozi wa wanadamu, wanadamu hawawezi kujikoa wenyewe, wanadamu wanahitaji Mungu kwaajili ya wokovu. Na kwa sababu hiyo kama Yesu angelikuwa mwanadamu wa kawaida asingeliweza kufaa kuwa mwokozi.

 

Maandiko yenyewe ndiyo yanayomuelezea Yesu Kristo kuwa ni Mungu na jambo hili liko wazi hata bila kuhitaji ufafanuzi mwingi kwa mfano nabii Isaya alipotabiri kuhusu kuzaliwa kwa masihi haya ndio maneno yake ambayo kimsingi aliyatumia kumuelezea Yesu Kristo ona:-

 

Isaya 7:14 “.Kwa hiyo Bwana mwenyewe atawapa ishara. Tazama, bikira atachukua mimba, atazaa mtoto mwanamume, naye atamwita jina lake Imanueli.”

 

Isaya 9:6-7 “Maana kwa ajili yetu mtoto amezaliwa, Tumepewa mtoto mwanamume; Na uweza wa kifalme utakuwa begani mwake; Naye ataitwa Jina Lake, Mshauri wa ajabu, Mungu mwenye nguvu, Baba wa milele, Mfalme wa amani. Maongeo ya enzi yake na amani Hayatakuwa na mwisho kamwe, Katika kiti cha enzi cha Daudi na ufalme wake; Kuuthibitisha na kuutegemeza Kwa hukumu na kwa haki, Tangu sasa na hata milele. Wivu wa Bwana wa majeshi ndio utakaotenda hayo.”

 

Mfalme Daudi anamuona Yesu kuwa sio mwanae bali ni Mungu ona

 

Mathayo 22:41-45 “Na Mafarisayo walipokusanyika, Yesu aliwauliza, akisema, Mwaonaje katika habari za Kristo? Ni mwana wa nani? Wakamwambia, Ni wa Daudi. Akawauliza, Imekuwaje basi Daudi katika Roho kumwita Bwana, akisema, Bwana alimwambia Bwana wangu, Uketi mkono wangu wa kuume, Hata niwawekapo adui zako Kuwa chini ya miguu yako? Basi, Daudi akimwita Bwana, amekuwaje ni mwanawe?

 

Maandiko yanatuthibitishia kuwa Yesu ni Mungu, na ni muumbaji wa kila kitu na kuwa kila kitu kilitokana na Yeye

 

Yohana 1:1-3,14 “Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu.Huyo mwanzo alikuwako kwa Mungu.Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika.14 Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli.”

 

Kwa hiyo ni wazi kuwa Yesu alikuwa akijitambulisha kama Mungu kwa Kanisa la Laodikia akiwataka wamuamini, Kristo alikuwa akijimbainisha kuwa kanisa ni mali yake na kwa sababu hiyo ana mamlaka ya kuwakemea na kuwarekebisha na kuwa anajua mapungufu yao na anawaona jinsi ambavyo wamepoa kiroho na kuwa vuguvugu na kuwa na mapungufu Hakuna jambo la hatari sana duniani kama kanisa lililopoa yaani wakristo wa kimwili, Kanisa au wakristo waliopoa wanajijua kuwa wamepoa na wanaweza kutubu, lakini wale walio vuguvugu hujihesabia haki na kujidhani ya kuwa hawahitaji kutubu, Yesu analionya kanisa la Laodikia ambao wanajidhani kuwa wako salama wakijifikiri kuwa ni matajiri wa kiroho lakini walikuwa wakijidanganya wenyewe, kwa sababu katika uhalisia Yesu alikuwa anawaona kuwa Masikini, wanyonge na vipofu na uchi, maana yake hawakuwa na vazi la haki ya Mungu, Mji wao waliokuwa wakiuishi na mazingira yake yaliathiri hali zao za kiroho, hii ni wazi kuwa mkuu wa anga wa eneo Fulani kwa sifa zozote alizonazo huathiri hali ya kiroho ya mazingira yake, Laodikia uliitwa mji wa haki lakini Kanisa lilikuwa halina haki, Laodikia ulikuwa na viwanda vya nguo Lakini kanisa Yesu analiona liko uchi, Laodikia walikuwa hodari katika tiba hasa za macho, lakini Yesu analiona kanisa likiwa kipofu, Kulikuwa na maji ya vugu vugu na chemichemi za maji ya moto, Lakini Yesu alikuwa analiona kanisa liko vuguvugu, Laodikia ulikuwa mji wenye dhahabu lakini Yesu aliwashauri kununua kwake dhahabu iliyo safi Zaidi, kiburi cha mafanikio ya mwilini waliyokuwa nayo kiliwapiga upofu wa kiroho na wakajikuta wanamfungia Kristo Yesu nje ya mioyo yao, Yesu alikuwa bado anawapenda na ndio maana aliwakemea na bado aliahidi kuwa anaendelea kugonga mlango na kuwa wakikubali kumfungulia ataingia kwao na kufanya makazi nao.

                         

2.       Mimi ni tajiri, nimejitajirisha, wala sina haja ya kitu;

 

Kanisa la Laodikia lilikuwa katika eneo tajiri sana lililojulikana kwa Benki kubwa ya fedha, viwanda vya nguo, shule za utabibu na madawa, jambo ambalo lilikuwa na mchango mkubwa sana katika mafanikio ya kimaisha ya waamini wa kanisa pia, kwa hiyo walijivunia Utajiri na walijiona kuwa hawahitaji kitu, hawahitaji msaada Neno tajiri katika kiyunani linatumika kama neno “plousios” ambalo lina maana ya Material wealth and abundance yaani utajiri wa mali na mafanikio mengi ya mwilini, mafanikio haya yaliwapa kujiamini na kujiona kuwa wanatosha, jambo lililopelekea wawe na upofu wa kujiona katika hali zao za kiroho, Yesu aliwakemea na kuwajulisha kuwa walikuwa duni mno kuliko walivyokuwa wakijifikiri.

 

Ufunuo 3:17 “Kwa kuwa wasema, Mimi ni tajiri, nimejitajirisha, wala sina haja ya kitu; nawe hujui ya kuwa wewe u mnyonge, na mwenye mashaka, na maskini, na kipofu, na uchi.”

 

Yesu aliwakemea kwa kiburi na majivuno ya mwilini kiroho walikuwa ni wanyonge, wenye mashaka, na masikini na kipofu na uchi. Kimsingi walikuwa wanamuhitaji Yesu kwa wingi kama alivyotamani Paulo mtume katika dua yake kwamba waijue siri ya Mungu yaani Yesu Kristo. Lakini badala yake changamoto zifuatazo ziliwaandama walikuwa:-

 

Wanyonge – Wretched - talaiporos - wenye msiba na mateso, wasioridhika na wasio na Amani.

Wenye mashaka – Pitiable - eleeinos - wenye kutia huruma kwa sababu ya hali yao

Masikini - Poor – Ptochos – masikini wa kutupwa na mtu liyefilisika, chikoraa

Kipofu - Blind – typhlos – kipofu asiyeweza kuona kwa macho wala kupambanua kwa akili

Uchi- Naked- gymnos – aliyewekwa wazi aliyefumaniwa – akiwa hana nguo, kwa aibu

 

Wakati kanisa la Laodikia wakizungukwa na mazingira yanayoonekana kuwa na mafanikio makubwa kiukweli hali yao ya kiroho ilikuwa tofauti na mwonekao wao wa ndani, Yesu alikuwa akiliona kanisa hili kama kanisa lililoathiriwa na majivuno na kiburi, kwa sababu ya mafanikio ya nje wakati hali yao ya kutembea na Yesu ni mbaya sana, hawakuwa na lolote ambalo Yesu aliliona na kulisifia tofauti na makanisa mengine yale sita, Hali yao ya kujifikiri hawahitaji kitu iliwaongoza katika kupoa kiroho na kuwa vuguvugu, kuchukuliana na mafundisho potofu, kutokuitetea imani, na kupoa kiroho huku wakibaki na hali ya udunia uliokithiri jambo ambalo lilipelekea Yesu awakemee.

 

Ufunuo 3:16 “Basi, kwa sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika kinywa changu.”

               

Yesu aliwataka watubu na kubadilika aliwataka waifahamu hali yao ya ndani ambayo ni mbaya sana 

 

Ufunuo 3:18 “Nakupa shauri, ununue kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto, upate kuwa tajiri, na mavazi meupe upate kuvaa, aibu ya uchi wako isionekane, na dawa ya macho ya kujipaka macho yako, upate kuona.”

 

Utajiri wa kweli ni utajiri wa kiroho ambao unapatikana kwa Imani na uvumilivu, Yesu anawashauri wanunue kwake vazi lililo bora, jeupe, waufunike uchi wao, Huku akiwataka wapate dawa ya kuona vizuri kwani macho yao na akili zao zimepofushwa, haki ya kweli ni ile inayopatikana kwa njia ya imani katika Kristo Yesu, na ni kupitia yeye tunaweza kuangaziwa na kuiona nuru ya Mungu itakayotupa ufahamu utakaotufanya tutembee kwa unyenyekevu. Haimaanishi kuwa Yeu yuko kinyume na utajiri na mafanikio ya mwilini, Lakini Yesu alitaka hali yao ya nje ingeanzia ndani yaani wangekuwa matajiri ndani katika roho zao kwanza lakini badala yake ikawa kinyume, Bwana alipe neema kanisa la leo, kuwa na utajiri wa rohoni na mwilini na mafanikio ya rohoni na mwilini pia.

Tajiri lakini Masikini

Kanisa la Laodikia linaweza kuwa linawakilisha mtu fulani au kanisa fulani, katika siku za leo watu huoanisha mafanikio ya kimwili na mafanikio ya kiroho, wanadhani kumiliki mali na kuwa na mafanikio ni kuwa sawa kiroho au ni kuwa na baraka kubwa za Rohoni, jambo ambalo linawapelekea watu kuwa na kiburi na majivuno, Hali ya mafanikio ya kimwili na kuwa na vitu vingi vya mwilini sio mbaya lakini vina mchango mkubwa sana wa kutupa kiburi na majivuno na zaidi sana kuziba masikio yetu na macho yetu ya rohoni yanayoweza kusaidia kuona uhalisia wetu na hali zetu za kiroho, Lazima wakati wote tukumbuke kujipima kuwa ujasiri wetu unatokana na nini? mali tulizo nazo au hali yetu ya kiroho, Yesu Kristo akiwa ndio mzabibu wa kweli?

Maneno ya Bwana Yesu yanamkumbusha kila mmoja wetu leo kujipima kiroho chake na kujiangalia hali yake ya kiroho na kutafuta kwa kina na mapana na marefu utajiri wa Rohoni, na uhusiano wenye nguvu na Yesu Kristo Bwana wetu Bwana wa utukufu, hatuna budi kuwa na moyo mkubwa wa kuutafuta mafanikio ya kiroho yaani utajiri wa imani na mengine yakawa ni maswala yanayofuata tu

Yakobo 2:5 “Ndugu zangu wapenzi, sikilizeni, Je! Mungu hakuwachagua maskini wa dunia wawe matajiri wa imani na warithi wa ufalme aliowaahidia wampendao?

Mathayo 6:33 “Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote mtazidishiwa.”

Yesu analitaka kanisa la Laodikia kubadilika au kugeuka, toba maana yake ni kugeuka, na kuwa waendelee kuutafuta uhusiano wao na yeye, ili waweze kuvikwa haki ya Kristo na kufuata muongozo wake, na kupata ufahamu wa Rohoni, na kubaki wakiwa wanyenyekevu, kutambua kuwa hakuna kitu wanahitaji na cha Muhimu duniani kama uhusiano wetu na Mungu, Tunamuhitaji Mungu katika kila eneo la maisha yetu, sisi wenyewe na mali zetu hatutoshi bila Mungu, tunamuhitaji Mungu. Mungu ndiye kila kitu katika maisha yetu!

Mungu sio kuwa hafurahii mafanikio Yetu, Mungu anafurahia sana sisi tufanikiwe lakini kamwe hatupaswi kumsahau Mungu wakati wa mafanikio, tatizo kubwa la kanisa la Laodikia walimfungia Yesu Mlango, walimuona hana maana tena, kwa sababu ya mafanikio yao kielimu, kimazingira, na mavazi na madawa na mabenki na maendeleo ya viwanda na uchumi imara na kila kitu hivyo walifikiri kuwa na hali zao za ndani zimebaki salama walijiona ni matajiri kumbe walikuwa masikini sana na uchi, wanyonge na wenye kuhitaji hifadhi, kujiona bora kuliko wengine ni kiburi na majivuno, kuwalaumu wengine kwa sababu zozote zile ni kujiona una kila kitu, wako watu leo wanaofikiri kuwa sasa hawamuhitaji Yesu kwa sababu wamejitosheleza katika kila kitu lakini Yesu akiwaangalia ni masikini, wako uchi na ni wanyonge, lolote lile ambalo linatupa kiburi katika maisha yetu lazima tuliweke kando na kutembea kwa unyenyekevu, tukimtegemea Mungu, na kumuamini yeye kwaajili ya mahitaji yetu yote.

Leo hii unawasikia watu wakisema Yesu Sio Mungu na ni watumishi wa Mungu lakini wanapata wapi ujasiri wa kutamka hayo leo hii ni kwa sababu sasa wametajirika kimwili, wameshiba ni kwa sababu wamefanikiwa na kwa sababu wamekuwa maarufu, na wamekuwa maarufu mpaka kufikia ngazi ya kupunguza umaarufu wa Yesu Kristo, lakini kiroho wamefilisika, hawasomi biblia kwa kina na kujua ya kuwa maandiko yenyewe ndio yanayosema Yesu ni Mungu na sio watu Fulani walioamua kuwa Yesu awe Mungu hiyo maana yake ni nini ni kwa sababu wameshiba, wamefanikiwa, ni maarufu, wanajulikana sasa wanaanza kumkufuru yeye aliyewaita na kumfungia mlango kaa nje Yesu wewe ni kiumbe tu wewe sio Mungu! Kanisa la Laodikia linawakilisha kanisa la leo ambao walifikiri kuwa wanaweza kujitosheleza, na Yesu alikuwa amefungiwa nje, ni wazi kuwa kanisa la Laodikia linawakilisha kanisa la siku za mwisho kihistoria ambalo litakumbwa na ukengeufu mkubwa, pamoja na kuwa na mafaniko ya kiuchumi na utajiri wa vitu vyenye kuonekana.

Utajiri mwingine ambao watu wanajivunia ni ule wa kufikiri kuwa wametimiza sheria yote ya Mungu na kuwa hakuna kitu wamebakiza! Lakini Kristo anapowaangalia anaona kuwa kuna changamoto kubwa zimebakia ndani yao.

Luka 18:18-24 “Tena, mtu mkubwa mmoja alimwuliza, akisema, Mwalimu mwema, nifanye nini ili nipate kuurithi uzima wa milele? Yesu akamwambia, Mbona unaniita mwema? Hakuna aliye mwema ila mmoja, naye ndiye Mungu. Wazijua amri; Usizini, Usiue, Usiibe, Usishuhudie uongo, Waheshimu baba yako na mama yako. Akasema, Hayo yote nimeyashika tangu utoto wangu. Yesu aliposikia hayo alimwambia, Umepungukiwa na neno moja bado; viuze ulivyo navyo vyote, ukawagawanyie maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni; kisha, njoo unifuate. Lakini aliposikia hayo alihuzunika sana, maana alikuwa na mali nyingi. Yesu alipoona vile alisema, Kwa shida gani wenye mali watauingia ufalme wa Mungu!

Hii ni aina nyingine ya utajiri, ni utajiri ambao mafarisayo wengi walikuwa nao, sijui kama watu wa leo wanaweza kuwa na utajiri huu, huu ni utajiri wa kujihesabia haki, kuishi maisha ya haki ni mpango wa Mungu lakini hatupaswi kutembea katika kiburi cha kidini na kudhani kuwa tunaweza kumnunua Mungu kwa matendo yetu, ni vigumu sana kujiona namna tulivyo na kiburi lakini Mungu anakiona na kwa Roho wake Mtakatifu anaweza kuikagua mioyo yetu na kuchunguza nia zetu na kutuonyesha namna na jinsi tunavyojifikiria kuwa ni bora kwa sababu tumetimiza kila kitu ambacho tunadhani ni matakwa ya sheria za kidini kama alivyokuwa mtu huyo hapo juu lakini kumbe dhambi ya ubinafsi ilikuwa inamuandama na hakuweza hata kushinda akionya juu ya tatizo hilo Yesu alitoa mfano huu kabla katika sura hiyo hiyo

Luka 18:9-14 “Akawaambia mfano huu watu waliojikinai ya kuwa wao ni wenye haki, wakiwadharau wengine wote. Watu wawili walipanda kwenda hekaluni kusali, mmoja Farisayo, wa pili mtoza ushuru. Yule Farisayo akasimama akiomba hivi moyoni mwake; Ee Mungu, nakushukuru kwa kuwa mimi si kama watu wengine, wanyang'anyi, wadhalimu, wazinzi, wala kama huyu mtoza ushuru. Mimi nafunga mara mbili kwa juma; hutoa zaka katika mapato yangu yote. Lakini yule mtoza ushuru alisimama mbali, wala hakuthubutu hata kuinua macho yake mbinguni, bali alijipiga-piga kifua akisema, Ee Mungu, uniwie radhi mimi mwenye dhambi.Nawaambia, huyu alishuka kwenda nyumbani kwake amehesabiwa haki kuliko yule; kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa.”

Hii ni aina nyingine ya mtu kujifikiri kuwa amejitosheleza lakini Yesu akipima anaona kuna changamoto kubwa ya watu kujihesabia haki, linapokuja swala la kuwa mbele za Mungu sisi ni masikini na vipofu na uchi, ni haki yake Yesu Kristo tu inayotosha kutusaidia kufanya kuhesabiwa haki mbele za Mungu na wala sio kwa juhudi zetu. Wakati unapojifikiria kuwa u tajiri kumbe Yesu anakuona ni masikini, wakati unapofikiri kuwa u mwenye haki, Yesu anakuona u uchi kabisa Bwana ampe neema kila mmoja wetu kumfanya Yesu Kristo kuwa utoshelevu wetu katika jina la Yesu Kristo amen!

Na Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye hekima.      

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni