2Wafalme 1:2-4 “Na Ahazia akaanguka katika dirisha la chumba chake orofani,
katika Samaria, akaugua; akatuma wajumbe, akawaambia, Enendeni mkaulize kwa
Baal-zebubu, mungu wa Ekroni, kwamba nitapona ugonjwa huu. Lakini malaika wa
Bwana akamwambia Eliya Mtishbi, Ondoka, uende ukaonane na wale wajumbe wa
mfalme wa Samaria, ukawaambie, Je! Ni kwa sababu hapana Mungu katika Israeli,
hata mnakwenda kuuliza kwa Baal-zebubu, mungu wa Ekroni? Basi sasa, Bwana asema
hivi, Hutashuka katika kile kitanda ulichokipanda, bali hakika utakufa. Eliya
akaondoka.”
Utangulizi:
Wakati wa Ahazia Mfalme wa Israel
alipougua alituma wajumbe kwenda kuuliza kwa miungu ya kikanaani kwa habari ya
afya yake badala ya kuuliza kutoka kwa Mungu wa Israel, Tukio hilo lilimuudhi
sana Mungu na malaika wa Bwana alimtuma Eliya Nabii kwenda kumuonya mfalme huyo
kwa swali kali na kwa kumkemea na kumpa jibu kutoka kwa Mungu; Je ni kwa sababu
hakuna Mungu katika Israel, hata mnakwenda kuuliza kwa Baal-Zebubu mungu wa
Ekroni? Swali hili linaonekana kuwa ni
lenye kushangaza sana na linalotupa kujifunza kwa kina na mapana na marefu
namna na jinsi ambavyo Mungu anakasirishwa sana na watu wanaojihusisha na maswala
ya ushirikina na matokeo mabaya ya kuacha kumtegemea Mungu, hii ni kwa sababu
tangu mwanzo Mungu alikuwa amekwisha kuwaonya wana wa Israel kutokujihusisha na
maswala ya kishirikina ikiwa ni pamoja na kuwaendea wenye pepo, wachawi na
mambo yanayofanana na hayo;
Mambo ya walawi 19:31 “Msiwaendee wenye pepo, wala wachawi; msiwatafute; ili
kutiwa unajisi na wao; Mimi ndimi BWANA, Mungu wenu.”
Kwa ujumla lilikuwa ni jambo la
kusikitisha sana ya kwamba mtu kutoka katika taifa la Mungu anatuma wajumbe
kwenda kutafuta msaada kwa miungu ya kigeni, miungu isiyo na nguvu na kuacha
kumtegemea Mungu aliye hai, Mungu alimtuma nabii wake kuwahi wajumbe hao na
kumpa majibu yanayoonyesha ya kuwa mfalme huyo atakufa na kuwa hatashuka katika
kitanda alichokipanda jibu hili linakuwa kali kwa sababu mfalme huyu alimuasi
Mungu na hakutaka kuuelekeza moyo wake kwa Mungu aliye hai jambo ambalo lilikuwa
ni dharau kubwa sana yenye kuonyesha ya kuwa Mungu hana Msaada kwa watu wake
jambo ambalo liko kinyume na ukweli wa kimaandiko, Neno la Mungu linatufundisha
ya kuwa Mungu kwetu sisi ni kimbilio na nguvu na msaada uonekanao tele wakati
wa mateso.
Zaburi 46:1-3 “Mungu kwetu sisi ni kimbilio na nguvu, Msaada utakaoonekana
tele wakati wa mateso. Kwa hiyo hatutaogopa ijapobadilika nchi, Ijapotetemeka
milima moyoni mwa bahari. Maji yake yajapovuma na kuumuka, Ijapopepesuka milima
kwa kiburi chake.”
Kwa sababu hii leo tutachukua
muda kujifunza kwa kina na mapana na marefu kuhusiana na swala zima la namna na
jinsi Mungu anavyochukizwa na ushirikina na jinsi tunavyopaswa kumtegemea yeye
katika maisha yetu yote. Tutajifunza somo hili “Je ni kwa sababu hakuna Mungu katika Israel” kwa kuzingatia
vipengele vitatu vifuatavyo:-
·
Onyo la
kutokujihusisha na ushirikina.
·
Madhara
ya ushirikina.
·
Je ni kwa
sababu Hakuna Mungu katika Israel?.
Onyo la kutokujihusisha na ushirikina.
Moja ya changamoto kubwa sana
inayoikabili dunia ya wakati wa leo ni pamoja na kuwepo kwa watu wanaoamini
katika ushirikina, yaani watu ambao wanamuamini Mungu lakini wakati huo huo
wanaamini katika ushirikina!, Neno ushirikina katika lugha ya kiyunani ni “Deisidaimonia” ambalo ni muunganiko wa maneno mawili Deis na Demon deis – Delivering to,
demon or deity ambalo kwa kiingereza ni “Superstition” maana yake ni tendo la Mwanadamu aliyeumbwa na Mungu,
kuacha kutafuta msaada kwa Mungu aliyemuumba na kwenda kutafuta msaada wa
kimwili au kiroho kupitia watu wenye nguvu za giza, yaani wajumbe wa shetani na
mapepo wakiwemo wachawi na waganga wa kienyeji, wasihiri, wapiga ramli, wapiga
bao, wanga na kadhalika, kwa makusudi ya kujilinda, kupona, kuhukumu, kulaani,
na ama kudhuru wengine, au kwa kusudi la kuwashinda wengine,au kwaajili ya
kupata kibali na kukubalika au kumchafulia mwingine asipate kibali au
kukubalika kwenye michezo, siasa, kugombea vyeo n.k. Kitendo hiki kinaitwa
kitendo cha kumshirikisha Mungu na mashetani na ni kitendo ambacho kimekatazwa
katika maandiko.
1Wakorintho 10:19-21 “Basi niseme nini? Ya kwamba kile kilichotolewa sadaka kwa
sanamu ni kitu? Au ya kwamba sanamu ni kitu? Sivyo, lakini vitu vile wavitoavyo
sadaka wavitoa kwa mashetani, wala si kwa Mungu; nami sipendi ninyi
kushirikiana na mashetani. Hamwezi kunywea kikombe cha Bwana na kikombe cha
mashetani. Hamwezi kushirikiana katika meza ya Bwana na katika meza ya
mashetani.”
Kwa hiyo ushirikina ni kitendo
cha Mtu aliyeumbwa na Mungu kushirikiana na mashetani, Ni kitendo cha kuacha
kuamini na kuitegemea nguvu ya Mungu na kuzitegemea nguvu mbaya za giza,
kwaajili ya kujilinda, kupona, kuondoa nuksi, mikosi au balaa au pia kwaajili
ya kulaani au kuwatakia mabaya watu wengine, kuwadhuru na kuwaumiza, Mungu wetu
ni Mungu mwenye wivu, hafurahii kabisa kitendo cha mwanadamu kuacha kumtumainia
yeye wakati tunapokuwa katika changamoto mbalimbali na badala yake
tukajielekeza katika kutafuta msaada kwa miungu hii ni machukizo kwake.Kumbuka
ya kuwa nyuma ya sanamu na miungu yote shetani yuko nyuma yake!
Kutoka 20:3-5 “Usiwe na miungu mingine ila mimi.Usijifanyie sanamu ya
kuchonga, wala mfano wa kitu cho chote kilicho juu mbinguni, wala kilicho chini
duniani, wala kilicho majini chini ya dunia. Usivisujudie wala kuvitumikia; kwa
kuwa mimi, BWANA, Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu; nawapatiliza wana maovu ya
baba zao, hata kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukiao,”
Mungu alikuwa amewaonya wana wa
Israel mara kwa mara kuacha kabisa kuwaendea waganga na wachawi, na wapiga bao
na ramli na wale wote wanaofanana na hao, Mungu alikuwa anataka kuwalinda watu
wake na tabia ya kishirikina, kwa bahati mbaya sana nyakati za leo watu wengi
sana wanaamini katika ushirikina, pamoja na maendeleo makubwa ya sayansi na
teknolojia na mpanuko mkubwa sana wa kitaaluma na elimu inasikitisha kuona kuwa
bado wako watu wanaamini sana katika nguvu za giza kuliko kumuamini Mungu,
vitendo vya ushirikina vimetapakaa na kuenea kila mahali, mashuleni, makazini,
katika biashara na wakati mwingine mpaka makanisani, hizi ni habari za kusikitisha
sana, neno la Mungu linatukumbusha tena na tena kuacha kabisa kujishirikisha na
maswala ya aina hii kama tunavyoweza kuona na kujifunza katika maandiko.
Kumbukumbu 18:9-13 “Utakapokwisha kuingia katika nchi akupayo Bwana, Mungu wako
usijifunze kutenda kwa mfano wa machukizo ya mataifa yale. Asionekane kwako mtu
ampitishaye mwanawe au binti yake kati ya moto, wala asionekane mtu atazamaye
bao, wala mtu atazamaye nyakati mbaya, wala mwenye kubashiri, wala msihiri,
wala mtu alogaye kwa kupiga mafundo, wala mtu apandishaye pepo, wala mchawi,
wala mtu awaombaye wafu. Kwa maana mtu atendaye hayo ni chukizo kwa Bwana;
kisha ni kwa sababu ya hayo Bwana, Mungu wako, anawafukuza mbele yako. Uwe
mkamilifu kwa Bwana, Mungu wako.”
Kutoka 22:18 “Usimwache mwanamke mchawi kuishi.”
Walawi 19:26,28 “26.Msile kitu cho chote pamoja na damu yake; wala msifanye
kuloga, wala kutumia utambuzi. 28. Msichanje chale yo yote katika nyama ya
miili yenu kwa ajili ya wafu, wala msiandike alama miilini mwenu; mimi ndimi
BWANA.”
Walawi 20:26-27 “Nanyi mtakuwa watakatifu kwangu mimi; kwa kuwa mimi BWANA
ni mtakatifu nami nimewatenga ninyi na mataifa, ili kwamba mwe wangu. Tena mtu
mume au mtu mke aliye na pepo, au aliye mchawi, hakika atauawa; watawapiga kwa
mawe; damu yao itakuwa juu yao.”
Kwa hiyo unapoyachunguza maandiko
utaweza kugundua kuwa katika Torati Mungu alikataza kila aina ya ushirikina na
uchawi Mungu alikataza watu wanaotoa kafara za watoto wao, alikataza kupiga
ramli au kupiga bao, alikataza kutazama nyakati mbaya, alikataza wenye
kubashiri, alikataza wenye kuroga kwa kupiga mafundo, usinga, alikataza kupunga
au kupandisha pepo, alikataza kujihusisha na uchawi, alikataza kuabudu mizimu
au kuomba wafu, alikataza kuchanjwa chale, alikataza kuchora tattoo, alikataza
kutumia pepo wa utambuzi, au wenye kutabana na akiweka wazi katika Israel kuwa
watu wa aina hiyo wauawe iwe ni mwanamme au iwe mwanamke na aliahidi kuwa
atavikomesha kabisa vitu hivyo wakati wa ujio wa masihi.
Mika 5:12-15 “nami nitakatilia mbali uchawi, usiwe mkononi mwako; wala
hutakuwa tena na watu wenye kutabana; nami nitakatilia mbali sanamu zako na
nguzo zako, zitoke kati yako; wala hutaiabudu tena kazi ya mikono yako. Nami
nitayang'oa maashera yenu, yasiwe kati yako; nami nitaiangamiza miji yako. Nami
nitajilipiza kisasi katika hasira na ghadhabu juu ya mataifa wasiosikiliza.”
Kwa hiyo kujihusisha na
ushirikina kwa namna yoyote ile na kwa sababu zozote zile ni dhambi kubwa na
mbaya na hatari sana kwa namna Mungu anavyoielezea katika maandiko, Lakini kwa
bahati mbaya nyakati za leo watu wanajihusisha na uchawi na kutafuta hata namna
ya kujiunga na freemason na vikundi vingine vya kichawi, kumekuwepo na watu
wanaojihusisha na uchawi kila mahali lakini pia kumekuwepo na watu wanaowategemea
wachawi na waganga kwaajili ya kuwakomesha watu, kwaajili ya kujilinda,
kwaajili ya masomo, kwaajili ya vyeo, kwaajili ya kupendwa au kumfunga mke au
mume au bosi, kushinda uchaguzi, kupata madini, kupata utajiri, kufanya
biashara, kuuza bidhaa, kuugua, kuumiza
wengine, kuharibia kibali wengine kuua wengine, kufitinisha wengine au kuondoa nuksi na mikosi na balaa na
kadhalika, hayo yote ni uasi mbele za Mungu na Mungu anachukizwa sana na wale
wote wanaojihusisha na maswala yote hayo.
Madhara ya ushirikina.
Kama jinsi ambavyo tumeona katika
mstari wa Msingi, yaliyomkuta mfalme Ahazia, uchawi na uganga husababisha
madhara makubwa sana katika maisha ya kila mwanadamu, awaye yote ambaye
atajiingiza katiia kutafuta msaada kwa miungu mingine badala ya Mungu aliye hai
ni sawa tu na kuwa umeamua kumuabudu shetani, kwa sababu shetani ndiye
anayewatumia hao na aina zote za wachawi ili kuwachepusha watu watoke nje ya
tegemeo la Mungu aliye hai na wa kweli alafu wamuabudu yeye, Maandiko yanaonyesha
ya kuwa, kuna madhara makubwa sana kwa watu wanaojihusisha na ushirikina na
kuabudu miungu mingine badala ya Mungu mwenye nguvu wa kweli unapoacha
kumtafuta Mungu na kuwaendea waganga na wachawi moja kwa moja unajiweka katika
hatari ya kufa kama tulivyoona jinsi Mungu anavyochukizwa na hayo wakati wa
mfalme Ahazia. Ahazia alimuacha Mungu aliye hai na kumuendea Baalzebubu au Ba’al zebuli alijulikana nyakati za biblia kama mungu wa ekroni
aliyeabudiwa na wafilisti katika mji wa Ekroni mungu huyu alijulikana kama
Bwana wa mainzi the Lord of flies,
lakini pia alijulikana kama mkuu wa mapepo, yaani Shetani mwenyewe mungu huyu
aliabudiwa na wakanaani, kuiendea miungi yoyote ya kienyeji ikiwa ni pamoja na
mizimu kunamuudhi sana Mungu na ni ushirikina na Kushiriki ushirikina, aidha
kwa kwenda kutafuta msaada kwao au kuwa mhudumu wa ushirikina au kuuamini na
kuutegemea kunakufanya hivi:-
1.
Unajiweka
katika hatari ya kufa.
2Wafalme 1:2-4 “Na Ahazia akaanguka katika dirisha
la chumba chake orofani, katika Samaria, akaugua; akatuma wajumbe, akawaambia,
Enendeni mkaulize kwa Baal-zebubu, mungu wa Ekroni, kwamba nitapona ugonjwa
huu. Lakini malaika wa Bwana akamwambia Eliya Mtishbi, Ondoka, uende ukaonane
na wale wajumbe wa mfalme wa Samaria, ukawaambie, Je! Ni kwa sababu hapana
Mungu katika Israeli, hata mnakwenda kuuliza kwa Baal-zebubu, mungu wa Ekroni?
Basi sasa, Bwana asema hivi, Hutashuka katika kile kitanda ulichokipanda, bali
hakika utakufa. Eliya akaondoka.”
1Nyakati 10:13-14. “Basi Sauli alikufa kwa
sababu ya kosa lake alilomkosa Bwana, kwa sababu ya neno la Bwana,
asilolishika; na tena kwa kutaka shauri kwa mwenye pepo wa utambuzi, aulize
kwake, asiulize kwa Bwana; kwa hiyo akamwua, na ufalme akamgeuzia Daudi, mwana
wa Yese.”
2.
Unajiweka
kwenye hatari ya kutupwa katika ziwa la Moto.
Ufunuo21:7-8 “Yeye ashindaye atayarithi haya, nami
nitakuwa Mungu wake, naye atakuwa mwanangu. Bali waoga, na wasioamini, na
wachukizao, na wauaji, na wazinzi, na wachawi, na hao waabuduo sanamu, na
waongo wote, sehemu yao ni katika lile ziwa liwakalo moto na kiberiti. Hii
ndiyo mauti ya pili.”
3.
Unajiweka
katika hatari ya kukataliwa na Mungu.
1Samuel 15:23 “Kwani kuasi ni kama dhambi ya
uchawi, Na ukaidi ni kama ukafiri na vinyago; Kwa kuwa umelikataa neno la
Bwana, Yeye naye amekukataa wewe usiwe mfalme.”
4.
Unaamsha
hasira za Mungu kwaajili yako.
2Nyakati 33:6 “Tena akawapitisha wanawe motoni
katika bonde la mwana wa Hinomu; akatazama bao, akabashiri, akafanya uganga,
akajishughulisha na hao wenye pepo wa utambuzi, na wachawi; akafanya mabaya
mengi machoni pa Bwana, hata kumkasirisha
5.
Unajitia
unajisi.
Mambo ya walawi 19:31 “Msiwaendee
wenye pepo, wala wachawi; msiwatafute; ili kutiwa unajisi na wao; Mimi ndimi
BWANA, Mungu wenu.”
6.
Unajiweka
katika hatari ya kukaziwa uso wa Mungu.
Mambo ya walawi 20:2-6 “Tena uwaambie
wana wa Israeli, Mtu awaye yote miongoni mwa wana wa Israeli, au miongoni mwa
wageni waketio katika Israeli, atakayetoa katika kizazi chake na kumpa Moleki,
sharti atauawa; wenyeji wa nchi watampiga kwa mawe. Mimi nami nitamkazia uso
wangu mtu huyo, nami nitamkatilia mbali na watu wake; kwa kuwa ametoa katika
kizazi chake na kumpa Moleki, ili kupatia unajisi patakatifu pangu, na
kulinajisi jina langu takatifu. Tena kama wenyeji wa nchi wakimfumbia macho mtu
huyo kwa njia yo yote, hapo atoapo katika kizazi chake na kumpa Moleki,
wasimwue; ndipo mimi nitamkazia uso wangu mtu huyo, na jamaa zake, nami nitamkatilia
mbali, na hao wote wamwandamao katika uzinifu, ili kufanya uzinifu pamoja na
Moleki, watengwe mbali na watu wao. Na mtu yule atakayewaendea wenye pepo, na
wachawi, ili kuzini pamoja nao, nitakaza uso wangu juu ya mtu yule, nitamtenga
na watu wake.”
7.
Unajiweka
katika nafasi ya kupatwa na mabaya na Misiba.
Wakati mwingine
unapoona mikosi imekuandama na unaandamwa na mambo mabaya sana unapaswa
kujihoji na kujiangalia ni kwa nini kwani uchawi na uganga unaleta kiburi na
kujifikiri wewe ndiye wewe lakini Mungu ameahidi kuwapiga kwa mapigo makuu
wachawi na kuwamaliza kabisa kwa misiba na ubaya
Isaya 47:8-14 “Sasa, basi, sikia haya, wewe
upendaye anasa, ukaaye na kujiona salama, wewe usemaye moyoni mwako, Mimi
ndiye, wala hapana mwingine zaidi yangu mimi; sitaketi mfano wa mjane, wala
sitajua kufiwa na watoto; lakini mambo haya mawili yatakupata katika dakika
moja siku moja, kufiwa na watoto, na ujane; yatakupata kiasi kitimilifu, uchawi
wako ujapokuwa mwingi, na uganga wako mwingi mno. Maana umeutumainia ubaya
wako; umesema, Hapana anionaye; hekima yako, na maarifa yako yamekupotosha,
nawe umesema moyoni mwako, Mimi ndiye, wala hapana mwingine zaidi yangu
mimi.Kwa sababu hiyo ubaya utakupata; wala hutajua kutopoa kwake; na msiba
utakuangukia; hutaweza kuuondoa; na ukiwa utakupata kwa ghafula, usioujua.
Simama sasa na uganga wako, na wingi wa uchawi wako, uliojitaabisha nao tangu
ujana wako; labda utaweza kupata faida, labda utaweza kushinda. Umechoka kwa
wingi wa mashauri yako; basi, na wasimame hao wajuao falaki, wazitazamao nyota,
watabirio kila mwezi mambo ya mwezi huo, wakakuokoe na mambo
yatakayokupata.Tazama, watakuwa kama mabua makavu; moto utawateketeza;
hawatajiokoa na nguvu za mwali wa moto; hautakuwa kaa la kukota moto, wala moto
wa kukaa karibu nao”.
8.
Unajiweka
katika hatari ya kutokuurithi ufalme wa Mungu.
Wagalatia 5:19-21 “Basi matendo ya mwili ni dhahiri,
ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi,
wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda, ulevi, ulafi, na mambo
yanayofanana na hayo, katika hayo nawaambia mapema, kama nilivyokwisha
kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa
Mungu.”
Kuna madhara
makubwa mno kwa sababu ushirikina unakuweka katika nafasi ya kufa kimwili na
kiroho, utakufa kimwili na utatupa katika ziwa liwakalo moto, huwezi kuingia
katika ufalme wa Mungu, unajitia unajisi yaani unajiingiza katika mikosi zaidi,
unaweza kuvamiwa na mapepo, unaamsha hasira za Mungu juu yako, unamfanya Mungu
akukazie uso wake na unajiweka katika hatari ya kukosa ufalme wa Mungu,
unapoyaangalia hayo kwa makini utaweza kuona maisha magumu sana ambayo mtu
anayeshiriki ushirikina anajitengenezea, unajitengeneza laana mikosi na balaa
na umasikini uliokithiri hii ni kwa sababu Mungu akikukazia uzo wake
akakukasirikia nani anaweza
kukupatanisha naye.
1Samuel 2:25 “Mtu mmoja akimkosa mwenzake, Mungu
atamhukumu; lakini mtu akimkosa Bwana, ni nani atakayemtetea? Lakini
hawakuisikia sauti ya baba yao, kwa sababu Bwana amekusudia kuwaua.”
9.
Unajiweka
katika nafasi ya kupingana na Mungu.
2Timotheo 3:8 “Na kama vile Yane na Yambre
walivyopingana na Musa, vivyo hivyo na hawa wanapingana na ile kweli; ni watu
walioharibika akili zao, wamekataliwa kwa mambo ya imani.”
Yana na Yambre
wanataja kwa majina katika agano jipya walikuwa ni wachawi ambao walipingana na
Musa na Haruni mbele ya Farao, na kumfanya farao aendelee kuwa na Moyo Mgumu
asiamini kweli ya Mungu, wachawi hawa wakati Musa alipoitupa fimbo yake ikawa
nyoka nao walizitupa fimbo zao kuwa nyoka, lakini Nyoka wa Musa aliwameza nyoka
wa wagaganga wa farao, Mungu huwaona wavhawi na waganga kuwa ni maadui wa
Imani, kazi yao kubwa ni kupotosha njia za Mungu zilizonyooka ili wanadamu
wasiziamini
Matendo 13:5-12 “Na walipokuwa katika Salami
wakalihubiri neno la Mungu katika masinagogi ya Wayahudi, nao walikuwa naye
Yohana kuwa mtumishi wao. Walipokwisha kupita katikati ya kisiwa chote mpaka
Pafo, wakaona mtu mmoja, mchawi, nabii wa uongo, Myahudi jina lake Bar-Yesu;
mtu huyu alikuwa pamoja na liwali Sergio Paulo, mtu mwenye akili. Yeye liwali
akawaita Barnaba na Sauli waje kwake, akataka kulisikia neno la Mungu. Lakini
Elima, yule mchawi (maana ndiyo tafsiri ya jina lake), akashindana nao, akitaka
kumtia yule liwali moyo wa kuiacha ile imani. Lakini Sauli, ambaye ndiye Paulo,
akijaa Roho Mtakatifu, akamkazia macho, akasema, Ewe mwenye kujaa hila na uovu
wote, mwana wa Ibilisi, adui wa haki yote, huachi kuzipotoa njia za Bwana
zilizonyoka? Basi, angalia, mkono wa Bwana u juu yako, nawe utakuwa kipofu,
usilione jua kwa muda. Mara kiwi kikamwangukia na giza, akazunguka-zunguka na
kumtafuta mtu wa kumshika mkono na kumwongoza.Ndipo yule liwali, alipoyaona
yaliyotendeka, akaamini, akiyastaajabia mafundisho ya Bwana.”
Unaona maandiko
yanaonyesha wazi kuwa wachawi na waganga ni maadui wa Imani, kazi yao kubwa ni
kuchepusha ibada kutoka kwa Mungu aliye hai kuelekea kwa shetani, wana ni
makuhani wa mashetani ni maajenti wa shetani, kazi zo ni kupingana na Mungu
aliye hai ili wanadamu wasimuamini Mungu na wawategemee wao, na kuwaingiza
katika kuishi kwa kutegemea na kuamini ushirikina, Mtu anaye waendea au
anayejishughulisha na ushirikina ni adui wa Mungu na ni mtu anayepingana na
Mungu.
Je ni kwa sababu Hakuna Mungu katika Israel?.
2Wafalme 1:2-4 “Na Ahazia akaanguka katika dirisha la chumba chake orofani,
katika Samaria, akaugua; akatuma wajumbe, akawaambia, Enendeni mkaulize kwa
Baal-zebubu, mungu wa Ekroni, kwamba nitapona ugonjwa huu. Lakini malaika wa
Bwana akamwambia Eliya Mtishbi, Ondoka, uende ukaonane na wale wajumbe wa
mfalme wa Samaria, ukawaambie, Je! Ni kwa sababu hapana Mungu katika Israeli,
hata mnakwenda kuuliza kwa Baal-zebubu, mungu wa Ekroni? Basi sasa, Bwana asema
hivi, Hutashuka katika kile kitanda ulichokipanda, bali hakika utakufa. Eliya
akaondoka.”
Lilikuwa swali la mshangao kutoka
kwa Mungu kupitia nabii wake kumuuliza Mfalme mwasi ambaye Mungu alikusudia
kumuua, alithibitishiwa kuwa atakufa kwa hakika hii inatufundisha kuwa kama
unajua ya kuwa yuko Mungu aliye hai, na kisha ukaenda kuiabudu au kuuliza au
kutegemea kwa wachawi kinyume na Mungu aliye hai ni wazi kuwa unajiweka katika
hatua ya kujibainisha kwa Mungu kuwa humuamini na wala humtegemei, na Mungu
anachukizwa na wasiomwamini wala wasiomtegemea yeye, Kugeukia miungu mingine au
wachawi na waganga kunamaanisha kuwa
unamwambia Mungu kuwa yeye hawezi, kukuokoa wala kukusaidia, na unajibainisha
kuwa wewe ni muasi na humtaki, na kwa
sababu hiyo ni sawa na kama umemvunjia heshima na kuonyesha Mungu kuwa ni wa
kupuuziwa tu, wachawi waliomjua Mungu kule Efeso waliikiri imani na walimuamini
Bwana Yesu na wakaachana na vifaa vyao vya uchawi na wakavichoma moto na
kumbuka kuwa vilikuwa vya thamani kubwa sana lakini hawakujali walipogundua
kuwa yuko Mungu aliye hai na ni yeye pekee ndiye wa kutumainiwa!
Matendo 19:17-20 “Habari hii ikajulikana na Wayahudi wote na Wayunani
waliokaa Efeso, hofu ikawaingia wote, na jina la Bwana Yesu likatukuzwa. Na
wengi wa wale walioamini wakaja wakaungama, wakidhihirisha matendo yao. Na watu
wengi katika wale waliotumia mambo ya uganga wakakusanya vitabu vyao,
wakavichoma moto mbele ya watu wote; wakafanya hesabu ya thamani yake, wakaona
ya kwamba yapata fedha hamsini elfu. Hivyo ndivyo neno la Bwana lilivyozidi na
kushinda kwa nguvu.”
Neno la Mungu linaonyesha kuwa
kwenda kuuliza habari kwa wenye pepo ni kwenda kuuliza kwa watu waliokufa na
kwa sababu hiyo watu wa namna hiyo watapata tabu sana, watakuwa katika giza
nene, mambo yao hayatafanikiwa wengi wameharibu maisha yao kwa sababu ya kutokumtumainia
Mungu na kuwatumainia wachawi, Mungu alichukizwa na Ahazia kwa sababu hakutaka
kuuliza kutoka kwake na badala yake alielekeza shingo yake katika ushirikina!
Na Mungu alimuhakikishia kuwa atakufa hii maana yake sio kimwili tu, lakini
atatengwa mbali na Mungu.
Isaya 8:19-22 “Na wakati watakapokuambia, Tafuta habari kwa watu wenye
pepo na kwa wachawi; waliao kama ndege na kunong'ona; je! Haiwapasi watu
kutafuta habari kwa Mungu wao? Je! Waende kwa watu waliokufa kwa ajili ya watu
walio hai? Na waende kwa sheria na ushuhuda; ikiwa hawasemi sawasawa na neno
hili, bila shaka kwa hao hapana asubuhi. Nao watapita katikati yake,
wamedhikika sana na kuwa na njaa; na itakuwa watakapoona njaa, watalalamika na
kuapa kwa mfalme wao, na kwa Mungu wao, na kuelekeza nyuso zao juu; nao
wataiangalia nchi, na, tazama, shida na giza; hapana changamko kwa sababu ya
dhiki; nao watafukuzwa na kuingia katika giza kubwa.”
Mungu anataka watu wake waache
kuamini wachawi na badala yake waiamini Injili, Injili yaani habari njema ina
nguvu sana na iko juu ya wachawi, kuna tumaini katika injili, injili ni matendo
ya Mungu yaliyo makuu zaidi ya uchawi, injili inafunua jinsi Mungu wetu aliyejifunua
kwa Ibrahimu na Isaka na Yakobo, Mungu wa Israel kuwa ni Mungu mwenye nguvu
kubwa sana ikiwa mtu awaye yote anataka mafanikio na Baraka kubwa sana za Mungu
basi hatuna budi kuiamini injili na kumuamini Bwana wetu Yesu kwa kumfanya kuwa
Bwana na mwokozi wa maisha yetu, Kazi yake kubwa aliyoifanya msalabani inatosha
kabisa kuleta ukombozi wa mwanadamu katika maeneo yote na mwenyewe alisema
imekwisha akimaanisha kuwa hakuna alichobakiza ambacho kinahusu shida na
changamoto za wanadamu ambacho kinaweza kuwa na nguvu kuipita kazi yake
aliyoifanya pale msalabani, kimsingi wachawi, wenyewe wanapaswa kuiamini injili
na kuachana kabisa na uchawi na kuchoma moto mikoba yao na vifaa vyao vya
uchawi na kumuamini Bwana Yesu ili iweze kuwa Baraka kubwa katika maisha yao.
Matendo 8:9-13 “Na mtu mmoja, jina lake Simoni, hapo kwanza alikuwa
akifanya uchawi katika mji ule, akiwashangaza watu wa taifa la Wasamaria,
akisema ya kuwa yeye ni mtu mkubwa. Wote wakamsikiliza tangu mdogo hata mkubwa,
wakisema, Mtu huyu ni uweza wa Mungu, ule Mkuu.Wakamsikiliza, kwa maana
amewashangaza muda mwingi kwa uchawi wake. Lakini walipomwamini Filipo,
akizihubiri habari njema za ufalme wa Mungu, na jina lake Yesu Kristo,
wakabatizwa, wanaume na wanawake. Na yeye Simoni mwenyewe aliamini akabatizwa,
akashikamana na Filipo; akashangaa alipoziona ishara na miujiza mikubwa
inayotendeka.”
Kwa kila mtu aliyeokoka yaani
kila mtu anayemuamini Bwana Yesu na kumfanya yeye kuwa Bwana na mwokozi wa
maisha yake hana budi kuweka Imani yake kwa Mungu wetu na kwa Bwana wetu Yesu
Kristo ukijua na kuamini ya kuwa kwake yeye hakuna uchawi wala uganga
utakaoweza kufanya kazi juu yako, wewe mkristo utaumizwa ikiwa tu utaondoa
imani yako kwa Mungu wa Israel, lakini kama unaamini katika Yesu Kristo fahamu
wazi kuwa hakuna uganga wala uchawi utakaoweza kufua dafu dhidi yako kwa sababu
imeandikwa, Mungu wetu ana nguvu Biblia inasema kama nguvu za nyati kwa hiyo
uchawi hauwezi kitu, kwako wala haukuwezi.
Hesabu 23:22-23 “Mungu amewaleta kutoka Misri, Naye ana nguvu kama nguvu za
nyati. Hakika hapana uchawi juu ya Yakobo, Wala hapana uganga juu ya Israeli.
Sasa habari za Yakobo na Israeli zitasemwa, Ni mambo gani aliyoyatenda Mungu!”
Aidha sisi tumepewa jina la Yesu
ambalo tunaweza kulitumia na kuliitia wakati wa changamoto za aina yoyote na
jina hili lina nguvu, lina mamlaka, lina uwezo na kila atakayeliitia jina hili
ataokolewa katika hali yoyote anayoipitia.
Matendo 4:9-12 “kama tukiulizwa leo habari ya jambo jema alilofanyiwa yule
mtu dhaifu, jinsi alivyoponywa, jueni ninyi nyote na watu wote wa Israeli ya
kuwa kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, ambaye ninyi mlimsulibisha, na Mungu
akamfufua katika wafu, kwa jina hilo mtu huyu anasimama ali mzima mbele yenu.
Yeye ndiye jiwe lile lililodharauliwa na ninyi waashi, nalo limewekwa kuwa jiwe
kuu la pembeni. Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana
jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa
kwalo.”
Wafilipi 2:9-11 “Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina
lile lipitalo kila jina; ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya
mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi; na kila ulimi ukiri ya kuwa
YESU KRISTO NI BWANA, kwa utukufu wa Mungu Baba.”
Jina la Yesu lina nguvu, na
mamlaka na tunaweza kulitumia jina hili kuamuru jambo lolote lile na likawa na
mafanikio makubwa katika ulimwengu wa roho na ulimwengu wa mwili, kwa sababu
hiyo hatupaswi kuogopa chochote tunaweza kulitumia na kulitumainia jina hili na
tukapata mafanikio makubwa na mpenyo katika kila eneo ikiwa ni pamoja na
kusambaratisha na kuharibu nguvu zote za giza, Yesu ameamuru tuzishughulikie
nguvu za giza na ametupa amri ya kukanyaga nyoka na nge na nguvu zote za yule
adui na kuwa hakuna kitu kitakachotudhuru
Luka 10:18-20 “Akawaambia, Nilimwona Shetani, akianguka kutoka mbinguni
kama umeme.Tazama, nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na nge, na nguvu zote za
yule adui, wala hakuna kitu kitakachowadhuru.Lakini, msifurahi kwa vile pepo
wanavyowatii; bali furahini kwa sababu majina yenu yameandikwa mbinguni.”
Isaya 54:17 “Kila silaha itakayofanyika juu yako haitafanikiwa na kila
ulimi utakaoinuka juu yako katika hukumu utauhukumu kuwa mkosa. Huu ndio urithi
wa watumishi wa Bwana, na haki yao inayotoka kwangu mimi, asema Bwana.”
Hitimisho:
Ujumbe huu unatukumbusha ya kuwa
Mungu ni Mungu mwenye wivu, na kuwa anataka tumtegemee yeye na kumuamini yeye,
lakini ukijiingiza katika ushirikina utapata madhara makubwa sana huenda
ulikuwa hujajifunza hili sasa umejifunza haribu kabisa kila kitu kinachotokana
na uganga na uchawi na waonye wengine waache kujihushisha na ushirikina na
badala yake wamwamini Mungu na kujua ya kuwa Mungu atawakomboa kutoka katika
kila changamoto inayowakabili kwa sababu uwezo huo upo kwa jina la Yesu Kristo
mwana wa Mungu aliye hai.
Na. Rev. Innocent Samuel Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni