Matendo 4:24-30 “Nao waliposikia, wakampazia Mungu sauti zao kwa moyo mmoja,
wakisema, Mola, wewe ndiwe Mungu, ndiwe uliyefanya mbingu na nchi na bahari na
vitu vyote vilivyomo; nawe ulinena kwa Roho Mtakatifu kwa kinywa cha babaetu
Daudi, mtumishi wako, Mbona mataifa wamefanya ghasia, Na makabila wametafakari
ubatili? Wafalme wa dunia wamejipanga, Na wakuu wamefanya shauri pamoja Juu ya
Bwana na juu ya Kristo wake. Maana ni kweli, Herode na Pontio Pilato pamoja na
Mataifa na watu wa Israeli, walikusanyika katika mji huu juu ya Mtumishi wako
mtakatifu Yesu, uliyemtia mafuta, ili wafanye yote ambayo mkono wako na
mashauri yako yamekusudia tangu zamani yatokee. Basi sasa, Bwana, yaangalie
matisho yao; ukawajalie watumwa wako kunena neno lako kwa ujasiri wote,
ukinyosha mkono wako kuponya; ishara na maajabu vifanyike kwa jina la Mtumishi
wako mtakatifu Yesu.”
Utangulizi:
Mojawapo ya changamoto kubwa
inayoikabili jamii katika nyakati za leo ni pamoja na tatizo la majungu
Makazini, Majungu makazini yameweza kuathiri kwa kiwango kikubwa maisha na
mahusiano ya watu katika mazingira ya kazi pamoja na ufanisi wao na kusababisha
maumivu makubwa kwa watu wengi, wengine walifungwa magerezani, wengine
walitupwa katika makanwa ya simba, wengine walisingiziwa makosa makubwa ya
ubakaji, wengine walifanyiwa ghasia na wengine waliuawa na wengine
walifitinishwa, wengine wameumizwa mioyo kwa sababu ya kuwepo kwa majungu
makazini na wengi wa wale wanaoumizwa ni wale wasio na hatia wenye mioyo
mororo, Uwepo wa majungu makazini, serikalini, makanisani na katika mashirika
ya kiserikali na yasiyo ya kiserikali, Kwenye biashara, mitaani, katika ndoa na maeneo mengine yamesababisha maumivu mengi
sana katika jamii, Hata hivyo maandiko au neno la Mungu linawatia moyo wale
wote wanaofanyiwa majungu au fitina kutokuogopa na kuhakikisha kuwa wakati wote
wanalitukuza jina la Mungu na kumuhofu yeye hata wakati wanapopitia changamoto
ngumu katika majungu watakayoyapitia na kuwahakikishia kuwa hata katika hayo
Mungu yuko pamoja nao.
Isaya 8:10-13 “Fanyeni shauri pamoja, nalo litabatilika; Semeni neno,
lakini halitasimama; Kwa maana Mungu yu pamoja nasi. Maana Bwana aliniambia
hivi, kwa mkono hodari, akanifundisha nisiende katika njia ya watu hawa,
akisema,Msiseme, Ni FITINA (Majungu), katika habari za mambo yote ambayo watu
hawa watasema, Ni FITINA (Majungu); msihofu kwa hofu yao, wala msiogope. Bwana
wa majeshi ndiye mtakayemtakasa; na awe yeye hofu yenu, na awe yeye utisho wenu.”
Kwa hiyo neno la Mungu
linaonyesha kuwa watu wa Mungu wanaweza kuathiriwa na majungu (Fitina) katika
mazingira yao ya shughuli za kila siku lakini hawapaswi kuogopa na wanapaswa
kumtakasa Mungu katika mapito hayo kwani Mungu atakuwa pamoja nao, Kwa sababu hiyo
basi, Leo tutachukua muda kujifunza kwa kina na mapana na marefu kuhusu Tatizo
la majungu makazini, tutajifunza somo hili Tatizo la Majungu Makazini kwa
kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-
·
Maana ya
Majungu.
·
Tatizo la
majungu makazini.
·
Jinsi ya
kukabiliana na tatizo la Majungu.
Maana ya Majungu.
Majungu ni moja ya changamoto kubwa
ambayo imeumiza mioyo ya watu wengi katika jamii, Majungu yako kila mahali
katika jamii, yapo makazini, yapo mashuleni, yapo katika taasisi za kiserikali
na zisizo za kiserikali, yapo makanisani na maeneo mengine mengi, kwa ujumla
majungu ni sehemu ya maisha ya mwanadamu, kama jinsi ambavyo dhambi ni moja ya
tatizo kubwa la aina mwanadamu hali kadhalika miongoni mwa dhambi hizo ni
pamoja na dhambi hii ya majungu. Kimsingi sio rahisi kukuta neno majungu moja
kwa moja katika maandiko, msamiati huu wa neno Majungu haujatumika katika
maandiko lakini hii haimaanishi kuwa majungu hayajatajwa katika maandiko, majungu
yametajwa katika maandiko kwa lugha nyingine kama tutakavyojifunza mbele kidogo
Majungu hasa ni nini?
Neno majungu linamaanisha
Mazungumzo, mipango au mikakati, inayofanywa na watu wengine, kumhusu mtu
mwingine asiyekuwepo, au hata akiwepo kwa kujadili yale yanayofikiriwa kuwa ni
mapungufu, au udhaifu, au kuharibu hadhi ya mtu huyo hususani mwenyewe
anapokuwa hayupo, au hata akiwepo. Majungu pia yanaweza kuchukua sura nyingine
ambapo watu wanaokufanyia majungu wanapanga mkakati wa kukuharibia kwa
mazungumzo yao, au kwa kushambulia sifa zako, au kwa kukushitakia au kukuchongea
kwa wakubwa au watu ili ikiwezekana usikubalike au upatwe na madhara, Majungu
yanaweza kuwa ni matokeo ya ubinafsi, wivu na fitina walizo nazo wahusika au
wivu wenye uchungu, husuda, katika biblia neno linalotumika kuhusu majungu
katika Kiswahili ni “FITINA” na
katika kiingereza ni “CONSPIRACY” au
“CONFEDERACY” yaani watu
wanaokubaliana au kupatana kumfanyia mabaya mtu mwingine kwa kusudi la
kumuharibia, kumpindua, kumkwamisha, kumchafulia sifa zake, kumuondoa kazini,
kumshusha cheo, kumhamisha kwa sababu mbalimbali ikiwepo hata wivu na kadhalika,
kufanya shauri (mjadala) wa kifitina au kumfanyia ghasia kwa kusudi la
kumkwamisha kwa kiibrania “Berīth”
au “Kesher” litokanalo na neno “Kāshar” Maneno haya yote yana maana
ya Conspiracy ambayo kwa kiingereza
maana yake inasomeka hivi “Conspiracy
means an agreement to falsely indict an innocent person of felony” – tafasiri
yake kwa Kiswahili ni Mipango au
makubaliano au njama zinazopangwa kwa kusudi la kumpachikia mtu asiye na hatia
au kumchafua mtu asiye na hatia. Au kumuharibia, au kupanga njama za uasi,
njama za fitina, njama za uchochezi na kadhalika. Sababu kubwa ikiwa ni wivu,
wivu wenye uchungu, husuda na ubinafsi, au tamaa, kutokujiamini na udhaifu
mwingine wa kibinadamu. Wakati mwingine kwa sababu ya mtu kufikiri kuwa
atachukua nafasi yako.
2Samuel 15:10-12 “Lakini Absalomu akapeleka wapelelezi katika kabila zote za
Israeli kusema, Mara mtakaposikia sauti ya tarumbeta, ndipo mtakaposema
Absalomu anamilikl huko Hebroni. Na watu mia mbili walioalikwa wakatoka
Yerusalemu pamoja na Absalomu, wakaenda katika ujinga wao wasijue neno lo lote.
Absalomu naye akatuma kumwita Ahithofeli Mgiloni, mshauri wake Daudi, kutoka
katika mji wake, yaani, Gilo, alipokuwa akitoa dhabihu. FITINA yao ikawa na
nguvu; maana watu waliokuwa pamoja na Absalomu wakazidi kuwa wengi.”
2Wafalme 12:19-21 “Basi mambo yote ya Yoashi yaliyosalia, na yote
aliyoyafanya, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Yuda?
Nao watumishi wake wakaondoka, wakafanya FITINA, wakamwua Yoashi katika nyumba
ya Milo, hapo panaposhukia Sila. Kwa maana Yozakari mwana wa Shimeathi, na
Yehozabadi mwana wa Shomeri, watumishi wake, wakampiga, naye akafa; wakamzika
pamoja na babaze mjini mwa Daudi. Na Amazia mwanawe akatawala mahali pake.”
Zaburi 2:1-2 “Mbona mataifa wanafanya ghasia, Na makabila wanatafakari
ubatili? Wafalme wa dunia wanajipanga, Na wakuu wanafanya shauri pamoja, Juu ya
Bwana, Na juu ya masihi wake.”
Kwa hiyo neno “Fitina” linaweza kumaanisha neno “Majungu” sasa basi watu wengi sana
wameumizwa katika mioyo yao makazini na katika maisha na maeneo mbalimbali kwa
sababu ya fitina, wengine wameuawa, wengine wamefungwa, wengine wamepotezewa
heshima na wengine wamechafuliwa sifa zao na kuhujumiwa na kuumizwa mioyo kwa
sababu ya majungu (yaani fitina, njama)
maandiko yanaonyesha mifano ya watu wengi sana ambao walifanyiwa fitina
na majungu na ghasia akiwepo Bwana wetu Yesu Kristo, Mungu augange moyo wako
kama wewe ni moja ya waathirika wa fitina na majungu yanayokukuta kazini, na
katika maisha haya. Uongezewe neema sana!
Mungu amekataza majungu Katika
neno lake amekataa aina yoyote ya uvumi wa uongo dhidi ya mtu hata kama wale
wanaotengeneza majungu hayo wako wengi, maonyo hayo hayana budi kuzingatiwa.
Kutoka 23:1-2 “Usivumishe habari za uongo; usitie mkono wako pamoja na
mwovu, kuwa shahidi wa udhalimu.Usiandamane na mkutano kutenda uovu; wala
usitie ushahidi wako katika neno lo lote kwa kugeukia kando na kuandamana na
mkutano ili kupotoa hukumu;”
Tatizo la majungu makazini.
Tatizo la majungu au fitina sio
tatizo jipya duniani ni changamoto ya siku nyingi sana tangu kuumbwa kwa
mwanadamu, kwa hiyo majungu ni sehemu ya kawaida ya maisha, wakati mwingine
watu wanaweza kukukalia kikao mara unapokuwa haupo na unaporejea unakuta mada
zinabadilishwa, kila mahali kuna aina yake ya majungu au FITINA
hata makanisani katika taasisi za kidini na kiroho, unaweza wakati mwingine
ukasikia na unaweza wakati mwingine usisikie wala usijue kuwa watu wanakuwazia
nini lakini nako kuna majungu, Na usipokuwa mwangalifu hata wewe unaweza
kujikuta ukishiriki na wengine katika kumfanyia majungu (FITINA) mtu mwingine Neno la Mungu yaani Biblia limejaa mifano ya
watu kibao ambao walifanyiwa majungu katika maisha yao na katika mazingira
mbali mbali, unaweza kufanyiwa majungu kwa sababu ya kibali kikubwa ulicho
nacho, unaweza kutendewa majungu ili watu wakuchafue, unaweza kufanyiwa
majungu, ili uhamishwe, au ili ushushwe cheo, au ili ufukuzwe kazi, au ili
uumizwe na kadhalika, dunia ni uwanja wa fujo na kwa sababu hiyo tatizo la
fitina na majungu liko kila mahali unaweza kufanyiwa fitina wakati mwingine ili
ikiwezekana uachane hata na mumeo au mkeo, hapa iko mifano michache kati ya
mingi sana ya watu waliofanyiwa fitina au majungu katika Biblia kwa sababu
mbalimbali na wengine walipata madhara na kuuawa na wengine Mungu aliingilia
kati na kuwasaidia, hali hii ndiyo
inayowakuta watu mahali pa kazi, inawakuta watu katika taasisi, inawakuta watu
katika huduma, inawakuta watu katika biashara, inawakuta watu mashuleni,
inawakuta watu katika jamii na kila mahali aliko mwanadamu majungu hayakosekani.
1.
Wana
wa Israel dhidi ya Yusufu – Yusufu alifanyiwa majungu na ndugu zake, wana
wa Israel ndugu wa baba mmoja, kutokana na nafasi aliyokuwa nayo na kibali na
upendo mkubwa alioupata kutoka kwa baba yake, pamoja na jinsi Mungu alivyosema
naye kuhusu maisha yake ya baadaye basi watu walimuonea wivu na kuanza
kumshambulia walimteta na walianza kupanga njama jinsi na namna ya kumpoteza
katika maisha yake ili yamkini ndoto zake zisiweze kutimia.
Mwanzo 37:18-20 “Wakamwona toka mbali, na kabla
hajawakaribia, wakafanya shauri juu yake ili wamwue.Wakasemezana wao kwa wao,
Tazama, yule bwana wa ndoto anakuja. Haya, twende, tukamwue na kumtupa katika
birika mojawapo, nasi tutasema, Mnyama mkali amemla; kisha tutaona zitakuwaje
ndoto zake.”
Aidha ukiacha
majungu yaliyofanywa na ndugu zake, Yusufu pia alifanyiwa majungu kazini kwa
kupachikiwa kesi na mke wa Potifa kwamba eti alitaka kumbaka jambo
lililopelekea Yusufu kuwekwa gerezani kwa miaka karibu 13 Lakini wakati wote
maandiko yanatuambia kuwa Mungu alikuwa pamoja naye!
Mwanzo 39:2-20 “BWANA akawa pamoja na Yusufu, naye
akasitawi; naye alikuwa katika nyumba ya bwana wake, yule Mmisri. Bwana wake
akaona ya kwamba BWANA yu pamoja naye, na ya kuwa BWANA anafanikisha mambo yote
mkononi mwake. Yusufu akaona neema machoni pake, akamtumikia. Naye akamweka awe
msimamizi juu ya nyumba yake, na yote yaliyomo akayaweka mkononi mwake. Ikawa
tokea wakati alipomweka awe msimamizi juu ya nyumba yake, na vyote vilivyomo,
BWANA akabariki nyumba ya yule Mmisri kwa ajili ya Yusufu. Mbaraka wa BWANA
ukawa juu ya vyote alivyokuwa navyo katika nyumba, na katika shamba. Akayaacha
yote aliyokuwa nayo mkononi mwa Yusufu; wala hakujua habari za kitu cho chote
chake, ila hicho chakula alichokula tu. Ikawa baada ya mambo hayo, mke wa bwana
wake akamtamani Yusufu, akamwambia, Lala nami. Lakini akakataa, akamwambia mke
wa bwana wake, Tazama, bwana wangu hajui kitu kilichowekwa kwangu nyumbani, na
vyote alivyo navyo amevitia mkononi mwangu. Hakuna mkuu katika nyumba hii
kuliko mimi, wala hakunizuilia kitu cho chote ila wewe, kwa kuwa wewe u mkewe.
Nifanyeje ubaya huu mkubwa nikamkose Mungu? Akawa akizidi kusema na Yusufu siku
baada ya siku, lakini hakumsikia alale naye, wala aongee naye. Ikawa, siku
moja, akaingia nyumbani atende kazi yake, wala hapakuwa na mtu katika watu wa
nyumbani humo ndani; huyo mwanamke akamshika nguo zake, akisema, Lala nami.
Yusufu akaiacha nguo yake mkononi mwake, akakimbia, akatoka nje. Ikawa alipoona
ya kwamba amemwachilia nguo yake mkononi mwake, naye amekimbia nje, akawaita
watu wa nyumbani mwake, akasema nao, akinena, Angalieni, ametuletea mtu
Mwebrania atufanyie dhihaka. Ameingia kwangu, ili alale nami, nikalia kwa sauti
kuu. Ikawa, aliposikia ya kuwa nimepaza sauti yangu na kulia, aliiacha nguo
yake kwangu, akakimbia, akatoka nje. Basi akaiweka ile nguo kwake hata bwana
wake aje nyumbani. Naye akamwambia kama maneno hayo, akisema, Yule mtumwa
Mwebrania uliyemleta kwetu, aliingia kwangu anidhihaki. Ikawa nilipopaza sauti
yangu, nikalia, akaacha nguo yake kwangu akakimbia nje. Ikawa bwana wake
aliposikia maneno ya mkewe aliyomwambia, akisema, Mtumwa wako amenitendea mambo
kama haya, hasira yake ikawaka. Bwana wake akamtwaa Yusufu, akamtia gerezani,
mahali walipofungwa wafungwa wa mfalme, naye akawamo humo gerezani.”
Wanadamu wana
wivu wenye uchungu, wakati wote wanapotamani nafasi uliyo nayo, au kuhofia
kibali ulicho nacho na kuona au kudhani unafanikiwa wivu huwashika na huanza
kufanya mashauri ya namna na jinsi ya kukuharibia, au wanapojihisi hawatoshi,
hawako salama na kadhalika majungu huibuka, kwa hiyo uharibifu huo unaweza
kufanywa kwa mbinu na njia mbalimbali lakini mara nyingi sana majungu husukumwa
na chuki na wivu wa kile ulicho nacho na baraka za Mungu zilizoko juu yako.
2. Haruni na Miriam dhidi ya Musa – Haruni
na Mariamu walianza kufikiri vibaya kinyume na Musa, walianza chokochoko ambazo
kama Mungu asingezidhibiti zingekuja kugeuka fitina majungu na uasi lakini
Mungu aliwakemea haraka sana na kusimama upande wa Musa na kumtetea, na zaidi
sana mke wa Musa, Mungu aliwaacha na mara moja Miriam akawa mwenye ukoma Kama
sio Musa kuwaombea hali ingekuwa mbaya kwani Haruni alimsihi Musa asiwahesabie
dhambi ile kukawa na Rehema za Mungu.
Hesabu 12:1-11 “Kisha Miriamu na Haruni wakamnenea
Musa kwa sababu ya mwanamke Mkushi aliyekuwa amemwoa; maana, alikuwa amemwoa
mwanamke Mkushi. Wakasema, Je! Ni kweli Bwana amenena na Musa tu? Hakunena na
sisi pia? Bwana akasikia maneno yao. Basi huyo mtu, huyo Musa, alikuwa mpole
sana zaidi ya wanadamu wote waliokuwa juu ya uso wa nchi. Bwana akanena ghafula
na Musa, na Haruni na Miriamu, na kuwaambia, Tokeni nje ninyi watatu, mwende
hemani mwa kukutania. Basi hao watatu wakatoka nje.Bwana akashuka katika nguzo
ya wingu akasimama pale mlangoni pa Hema, akawaita Haruni na Miriamu, nao
wakatoka nje wote wawili.Kisha akawaambia, Sikizeni basi maneno yangu; Akiwapo
nabii kati yenu, Mimi, Bwana, nitajifunua kwake katika maono, Nitasema naye
katika ndoto. Sivyo ilivyo kwa mtumishi wangu, Musa; Yeye ni mwaminifu katika
nyumba yangu yote; Kwake nitanena mdomo kwa mdomo, Maana, waziwazi wala si kwa
mafumbo; Na umbo la Bwana yeye ataliona. Mbona basi ninyi hamkuogopa Kumnenea
mtumishi wangu, huyo Musa? Hasira za Bwana zikawaka juu yao; naye akaenda zake.
Kisha hilo wingu likaondoka kutoka pale juu ya hema; na tazama, Miriamu akawa
mwenye ukoma, mweupe kama theluji; Haruni akamwangalia Miriamu, na tazama, yu
mwenye ukoma. Kisha Haruni akamwambia Musa, Ee bwana wangu nakusihi sana usituwekee
dhambi juu yetu, kwa kuwa tumefanya ya upumbavu, na kufanya dhambi.”
3.
Maliwali
120 dhidi ya Daniel – Maliwali
walishikwa na wivu kwa sababu ya mafanikio makubwa ya Daniel kama mkuu wao, na
wakaanza majungu na fitina ni namna gani watapata sababu za kushitaki, kwa hiyo
walikuja na wazo au muswada kwa Mfalme kukubaliana kwamba asaini kuwa watu
wasiabudu mungu yeyote kwa siku 30 isipokuwa kwa Mfalme tu na mtu atakayefanya kinyume na hilo atupwe
kwenye tundu la Simba, lakini pamoja na hayo bado utaona Kuwa Mungu alikuwa
pamoja naye na kumlinda Daniel dhidi ya makanwa yote ya Simba na mwisho wa siku
wale waliomfanyia fitina na majungu ndio waliokuja kutupwa katika simba
Daniel 6:1-9 “Ilimpendeza Dario kuweka juu ya
ufalme maliwali mia na ishirini, wawe juu ya ufalme wote; na juu yao akaweka
wakubwa watatu, na Danieli alikuwa mmoja wao; ili maliwali hawa watoe hesabu
kwao, mfalme asipate hasara. Basi Danieli huyo alipata sifa kuliko wakubwa na
maliwali, kwa kuwa roho bora ilikuwa ndani yake; naye mfalme akaazimu kumweka
juu ya ufalme wote. Basi mawaziri na maamiri wakatafuta sana kupata sababu za
kumshitaki Danieli kwa habari za mambo ya ufalme; lakini hawakuweza kuona
sababu wala kosa; kwa maana alikuwa mwaminifu, wala halikuonekana kosa wala
hatia ndani yake. Ndipo wale watu wakasema, Hatutapata sababu ya kumshitaki
Danieli huyo, tusipoipata katika mambo ya sheria ya Mungu wake. Basi wale
mawaziri na maamiri wakakusanyika pamoja mbele ya mfalme, wakamwambia hivi,
Mfalme Dario, uishi milele. Mawaziri wote wa ufalme, na manaibu, na maamiri, na
madiwani, na maliwali wamefanya shauri pamoja ili kuweka amri ya kifalme; na
kupiga marufuku, ya kwamba mtu ye yote atakayeomba dua kwa Mungu awaye yote, au
kwa mtu awaye yote, katika muda wa siku thelathini, ila kwako, Ee mfalme
atatupwa katika tundu la simba. Sasa, Ee mfalme, piga marufuku, ukatie sahihi
maandiko haya, yasibadilike, kama ilivyo sheria ya Wamedi na Waajemi, isiyoweza
kubadilika.Basi mfalme Dario akayatia sahihi maandiko yale, na ile marufuku.”
4.
Watu
wa Yerusalem dhidi na Nabii Yeremia – Mungu alimjulisha Yeremia mapema kuwa
watu wamepanga shauri yaani njama, au majungu kwa kusudi la kumfutilia mbali
Yeremia na kazi zake za kinabii, yaani wamfutilie mbali yeye na kazi yake yote
mti na matunda yake, na walitaka kuhakikisha ya kuwa hata jina lake halitajwi
tena kabisa katika nchi ya walio hai, Lakini Mungu alimfunulia Yeremia kuhusu
swala hilo na akaamua kumuomba Mungu ampe neema ya kuona kisasi juu ya adui
zake waliokusudia swala hilo.
Yeremia 11:18-20 “Tena Bwana akanijulisha haya, nami
nikayajua; ndipo uliponionyesha matendo yao. Lakini mimi nalikuwa kama
mwana-kondoo mpole, achukuliwaye kwenda kuchinjwa; wala sikujua ya kuwa
wamefanya mashauri kinyume changu, wakisema, Na tuuharibu mti pamoja na matunda
yake, na tumkatilie mbali atoke katika nchi ya walio hai, ili jina lake
lisikumbukwe tena. Lakini, Ee Bwana wa majeshi, uhukumuye haki, ujaribuye viuno
na moyo, nijalie kuona kisasi chako juu yao; kwa maana nimekufunulia wewe neno
langu.”
5.
Wayahudi
40 dhidi ya Paulo Mtume – Hawa walikula njama za kutaka kumuua Paulo mtume
na waliapa kuwa hawatakula wala kunywa mpaka wamemuua Paulo mtume, walikwenda
kwa wakuu wa makuhani na kuwaeleza mpango wao kuwa wao wameweka nadhiri kuwa
hawatakula wala kunywa mpaka wamemuua Paulo Mtume, lakini utaweza kuona tena
kuwa Mungu alisimama na mtumishi wake na kumtumia Akida wa Askari wa kirumi
kuyaokoa maisha ya Paulo, kumbuka Mungu anaona majungu yote unayokusudiwa!.
Matendo 23:11-23 “Usiku ule Bwana akasimama karibu
naye, akasema, Uwe na moyo mkuu; kwa sababu, kama ulivyonishuhudia habari zangu
Yerusalemu, imekupasa kunishuhudia vivyo hivyo Rumi nako.Kulipopambauka,
Wayahudi wakafanya mapatano, wakajifunga kwa kiapo kwamba hawatakula wala
hawatakunywa hata wamwue Paulo.Na hao walioapiana hivyo walipata zaidi ya watu
arobaini. Nao wakaenda kwa wakuu wa makuhani na wazee, wakasema, Tumejifunga
kwa kiapo tusionje kitu hata tumwue Paulo. Basi sasa ninyi pamoja na wazee wa
baraza mwambieni jemadari amlete chini kwenu, kana kwamba mnataka kujua habari
zake vizuri zaidi; na sisi tu tayari kumwua kabla hajakaribia. Mjomba wake
Paulo akasikia habari za kuotea kwao, akaenda akaingia ndani ya ngome akampasha
Paulo habari. Paulo akamwita akida mmoja, akasema, Mchukue kijana huyu kwa
jemadari; maana ana neno la kumwarifu. Basi akamchukua, akampeleka kwa
jemadari, akamwambia, Paulo, yule mfungwa, aliniita akataka nikuletee kijana
huyu kwa kuwa ana neno la kukuambia.Yule jemadari akamshika mkono akajitenga
pamoja naye kando, akamwuliza kwa faragha, Una neno gani utakalo kuniarifu?
Akasema Wayahudi wamepatana kukuomba umlete Paulo chini kesho, ukamweke mbele
ya baraza, kana kwamba wanataka kupata habari zake kwa usahihi zaidi.Basi wewe
usikubali; kwa maana watu zaidi ya arobaini wanamwotea, wamejifunga kwa kiapo
wasile wala wasinywe hata watakapomwua; nao sasa wako tayari, wakiitazamia
ahadi kwako.Basi yule jemadari akamwacha kijana aende zake, akimwagiza,
Usimwambie mtu awaye yote ya kwamba umeniarifu haya.Akawaita maakida wawili,
akasema, Wekeni tayari askari mia mbili kwenda Kaisaria, na askari wapanda
farasi sabini, na wenye mikuki mia mbili, kwa saa tatu ya usiku. Akawaambia
kuweka wanyama tayari wampandishe Paulo, na kumchukua salama kwa Feliki liwali.”
6.
Yezebeli
dhidi ya Nabothi – Nabothi alikuwa na shamba la urithi wa familia yake, na
shamba hili lilitamaniwa na mfalme, ili alitumie yeye, Lakini Nabothi
alimkatalia kwa vile lilikuwa shamba la urithi na urithi hauuzwi wala
kubadilishwa, jambo hili lilimuhuzunisha mfalme mwenye tamaa, na mkewe yaani
malkia aliyeitwa Yezebeli yeye alimwambia usihangaike, yeye akapanga njama za
kumsingizia Naboth kesi ya kumtukana Mungu na mfalme kwa wazee wa mji na
kutengeneza ushahidi wa uongo na kwa sababu hiyo Nabothi aliuawa na damu isiyo na hatia ikamwagika kwa
sababu nya tamaa ya mfalme na majungu ya Yezebeli
1Wafalme 21:1-19 “Ikawa baada ya hayo, Nabothi
Myezreeli alikuwa na shamba la mizabibu katika Yezreeli, karibu na nyumba ya
kifalme ya Ahabu mfalme wa Samaria. Ahabu akasema na Nabothi, akamwambia, Nipe
shamba lako la mizabibu nilifanye shamba la mboga, maana ni karibu na nyumba
yangu; nami nitakupa badala yake shamba la mizabibu lililo zuri zaidi; au
ukipenda, nitakupa fedha sawasawa na thamani yake. Nabothi akamwambia Ahabu,
Bwana apishe mbali nikupe wewe urithi wa baba zangu. Basi Ahabu akaenda
nyumbani kwake, ana moyo mzito, tena amekasirika, kwa sababu ya neno lile
aliloambiwa na Nabothi Myezreeli, akisema, Sitakupa urithi wa baba zangu.
Akajilaza kitandani pake, akageuza uso wake, akakataa kula. Lakini Yezebeli
mkewe akamwendea, akamwambia, Kwa nini roho yako ina huzuni hata usile chakula?
Akamwambia, Kwa sababu nimesema na Nabothi Myezreeli, nikamwambia, Unipe shamba
lako la mizabibu kwa fedha, au, ukipenda, nitakupa shamba la mizabibu lingine
badala yake. Akajibu, Sitakupa shamba langu la mizabibu. Yezebeli mkewe
akamwambia, Je! Sasa wewe unaumiliki ufalme wa Israeli? Ondoka, ule chakula,
moyo wako ufurahi; mimi nitakupa shamba la mizabibu la Nabothi Myezreeli. Basi,
akaandika nyaraka kwa jina la Ahabu, akazitia muhuri yake, akazipeleka zile
nyaraka kwa wazee, na kwa watu wenye nguvu waliokuwa katika mji wake, waliokaa
pamoja na Nabothi. Akaandika katika zile nyaraka, akasema, Pigeni mbiu ya watu
kufunga, mkamweke Nabothi juu mbele ya watu, mkainue watu wawili, watu
wasiofaa, ili wamshitaki, na kumshuhudia, kunena, Umemtukana Mungu na mfalme.
Kisha mchukueni nje, mkampige kwa mawe, ili afe.Wale wazee wa mji wake, na
walio wenye nguvu waliokaa mjini mwake, wakafanya kama Yezebeli alivyowaagiza,
kama ilivyoandikwa katika nyaraka alizowapelekea. Wakapiga mbiu ya watu
kufunga, wakamweka Nabothi juu mbele ya watu. Na hao watu wawili, watu
wasiofaa, wakaingia, wakaketi mbele yake; wale watu wasiofaa wakamshuhudia
Nabothi mbele ya watu, wakasema, Nabothi amemtukana Mungu na mfalme. Ndipo
wakamchukua nje ya mji, wakampiga kwa mawe hata akafa. Wakampelekea Yezebeli
habari, wakasema, Nabothi amepigwa kwa mawe, amekufa. Ikawa Yezebeli aliposikia
ya kwamba Nabothi amepigwa kwa mawe na kufa, Yezebeli akamwambia Ahabu, Inuka,
ulitamalaki shamba la mizabibu la Nabothi Myezreeli, alilokataa kukupa kwa
fedha, maana Nabothi hako hai, lakini amekufa. Ikawa Ahabu aliposikia ya kwamba
Nabothi amekufa, akaondoka, alitelemkie shamba la mizabibu la Nabothi
Myezreeli, ili alitamalaki. Neno la Bwana likamjia Eliya Mtishbi, kusema, Ondoka,
ushuke, ukutane na Ahabu mfalme wa Israeli, akaaye katika Samaria; yuko katika
shamba la mizabibu la Nabothi, ndiko alikoshukia ili alitamalaki. Ukamwambie, ukisema,
Bwana asema hivi, Je! Umeua, ukatamalaki? Nawe utamwambia, kusema, Bwana asema
hivi, Mahali pale mbwa walipoiramba damu ya Nabothi, mbwa watairamba na damu
yako, naam, damu yako.”
7.
Wakuu
wa dini dhidi ya Yesu – Tangu mwanzoni mwa huduma ya Yesu Kristo ni ukweli
ulio wazi kuwa wakuu wa dini hawakufurahishwa na huduma na utendaji wa Yesu
Kristo ambaye kimsingi huduma yake na utendaji wake ulikuwa na mvuto mkubwa
sana kwa maelefu ya watu, Maadui wa Yesu Kristo wakiongozwa na kuhani mkuu na
wazee waliketi kwa siri katika nyumba ya Kayafa na kuyapanga majungu agenda kuu
ikiwa ni jinsi na namna ya kumnasa, kumkamata
na hatimaye kumuua Yesu
Mathayo 26:3-5 “Wakati ule wakuu wa makuhani, na
wazee wa watu, wakakusanyika katika behewa ya Kuhani Mkuu, jina lake Kayafa;
wakafanya shauri pamoja, ili wamkamate Yesu kwa hila na kumwua.Lakini wakasema,
Isiwe wakati wa sikukuu, isije ikatokea ghasia katika watu.”
Jinsi ya kukabiliana na tatizo la Majungu.
Maandiko yanasema mtaifahamu
kweli nayo kweli itawaweka huru, moja ya jambo la msingi na la muhimu ni
kutambua kuwa majungu yapo na yapo kila mahali yanaweza kuweko kazini, katika
jamii, katika kazi, katika familia na hata kutoka miongoni mwa wapendwa na
ndugu, hakuna mwanadamu anaweza kufurahia ustwai wako, ndugu zake Yusufu
hawakufurahia ustawi wake, mawaziri hawakufurahia ustawi wa Daniel, na la
kushangaza kabisa hata Haruni na Miriam walimsengenya Musa, lakini hata
viongozi wa dini walipanga njama za kumuua nabii Yeremia na kuufutilia mbali unabii wake na Yesu
na hata njama za kulinda kaburi ili asifufuke, na njama za kupoteza
ushahidi wa kufufuka kwake na rushwa ikatolewa kwa askari, wasiseme
kilichotokea, hivyo ndivyo jamii ilivyo, watu wengi kwa kutokujua wameumizwa
sana mioyo yao, wametesa nafsi zao kwa sababu wamefanyiwa ukatili ambao
hawakuwahi kuutarajia maandiko yanatuelekeza nini cha kufanya tunapoishi katika
jamii yenye majungu unapaswa kufahamu kuwa Mungu wetu halali wala hasinzii na
kuwa anajua kila kinachoendelea na anaona na atalipa tu hapa yako maswala
kadhaa ya kufanya.
1.
Tambua
Mungu ni mkuu kuliko majungu – fahamu ya kuwa madhara ya majungu hayawezi
kuvuka mpaka wa mwenyezi, kama kuna kitu hatupaswi kuogopa basi ni majungu, na
kama kuna kitu tunapaswa kuogopa basi tumuogope Mungu, lakini mwanadamu hana
uwezo wa kukufanya lolote walimfanyia Yesu fitina na wakamuua lakini Mungu
akamfufua siku ya tatu, hakuna mpango wowote wa Mungu kwako utakaoharibiwa.
Isaya 8:10-13 “Fanyeni shauri pamoja, nalo
litabatilika; Semeni neno, lakini halitasimama; Kwa maana Mungu yu pamoja nasi.
Maana Bwana aliniambia hivi, kwa mkono hodari, akanifundisha nisiende katika
njia ya watu hawa, akisema,Msiseme, Ni FITINA (Majungu), katika habari za mambo
yote ambayo watu hawa watasema, Ni FITINA (Majungu); msihofu kwa hofu yao, wala
msiogope. Bwana wa majeshi ndiye mtakayemtakasa; na awe yeye hofu yenu, na awe
yeye utisho wenu.”
Mfanye Bwana
kuwa ndio hofu yako neno Bwana wa majeshi ndiye mtakayemtakasa kwa kiebrania
mtakayemtakasa linasomeka kama “Qadas”
kimatamshi “kah-dash” ambalo maana
yake Bwana awe ndiye hofu yako, kwa hiyo hakuna sababu ya kuwaogopa wanadamu na
badala yake tumuogope Mungu.
Zaburi 27:1-4 “Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu,
Nimwogope nani? Bwana ni ngome ya uzima wangu, Nimhofu nani? Watenda mabaya
waliponikaribia, Wanile nyama yangu, Watesi wangu na adui zangu, Walijikwaa
wakaanguka. Jeshi lijapojipanga kupigana nami, Moyo wangu hautaogopa. Vita
vijaponitokea, Hata hapo nitatumaini. Neno Moja nimelitaka kwa Bwana, Nalo
ndilo nitakalolitafuta, Nikae nyumbani mwa Bwana Siku zote za maisha yangu,
Niutazame uzuri wa Bwana, Na kutafakari hekaluni mwake.”
2.
Jiepushe
na maneno yasiyo na maana – wakati mwingine majungu hayo hupelekwa kwa
viongozi na kwa bahati mbaya wako viongozi ambao kila kitu kinachopelekwa kwao
wanadhani ni kweli na hawajua kuwa wako watu wazushi na wapika majungu, wakati
wote maandiko yanatutaka kujiepusha na maneno yasiyo na maana na watu wenye tabia za uzushi na fitina na
majungu na hasa kama yanamuhusu Mtumishi wa Mungu
2Timotheo 2:16-18 “Jiepushe na maneno yasiyo na maana,
ambayo si ya dini; kwa kuwa wataendelea zaidi katika maovu,na neno lao litaenea
kama donda-ndugu. Miongoni mwa hao wamo Himenayo na Fileto, walioikosa ile
kweli, wakisema ya kwamba kiyama imekwisha kuwapo, hata kuipindua imani ya watu
kadha wa kadha.”
1Timotheo 5:19 “Usikubali mashitaka juu ya mzee, ila
kwa vinywa vya mashahidi wawili au watatu.”
3.
Kataa
kujadili lolote lisolompa Mungu utukufu – kwa kawaida watu wanapojadili
mambo yaliyo manajisi nao hunajisika
maandiko yanasema kila kwenye wingi wa maneno hakukosi kuwa na dhambi,
kwakristo hawana budi kuhakikisha kuwa wanatunza ndimi zao kwa sabahu ulimi ni
kiungo kinachoweza kuleta madhara makubwa ikiwa ni pamoja na kuwadhuru watu
wengine na watu wasio na hatia
Mithali 10:18-19 “Yeye afichaye chuki ana midomo ya
uongo, Na yeye asingiziaye ni mpumbavu.Katika wingi wa maneno hapakosi kuwa na
maovu; Bali yeye azuiaye midomo yake hufanya akili.”
Wafilipi 4:8 “Hatimaye, ndugu zangu, mambo yo yote
yaliyo ya kweli, yo yote yaliyo ya staha, yo yote yaliyo ya haki, yo yote
yaliyo safi, yo yote yenye kupendeza, yo yote yenye sifa njema; ukiwapo wema wo
wote, ikiwapo sifa nzuri yo yote, yatafakarini hayo.”
Yakobo 3:1-8 “Ndugu zangu, msiwe waalimu wengi,
mkijua ya kuwa mtapata hukumu kubwa zaidi. Maana twajikwaa sisi sote pia katika
mambo mengi. Mtu asiyejikwaa katika kunena, huyo ni mtu mkamilifu, awezaye kuuzuia
na mwili wake wote kama kwa lijamu. Angalieni, twatia lijamu katika vinywa vya
farasi, ili wamtii, hivi twageuza mwili wao wote. Tena angalieni merikebu;
ingawa ni kubwa kama nini, na kuchukuliwa na pepo kali, zageuzwa na usukani
mdogo sana, ko kote anakoazimia kwenda nahodha.Vivyo hivyo ulimi nao ni kiungo
kidogo, nao hujivuna majivuno makuu. Angalieni jinsi moto mdogo uwashavyo msitu
mkubwa sana. Nao ulimi ni moto; ule ulimwengu wa uovu, ule ulimi, umewekwa
katika viungo vyetu, nao ndio uutiao mwili wote unajisi, huuwasha moto mfulizo
wa maumbile, nao huwashwa moto na jehanum. Maana kila aina ya wanyama, na ya
ndege, na ya vitambaavyo, na ya vitu vilivyomo baharini, vinafugika, navyo
vimekwisha kufugwa na wanadamu.Bali ulimi hakuna awezaye kuufuga; ni uovu
usiotulia, umejaa sumu iletayo mauti.”
4.
Majungu
hayawezi kututenga na upendo wa Mungu – katika matukio yote ya fitina na
majungu tuliyojifunza waliyofanyiwa watakatifu waliotutangulia utaweza kuona
wote Mungu alikuwa pamoja nao kwa hiyo kila mtu wa Mungu anapokutana na fitina
na majungu kazini anapaswa kukumbuka kuwa Mungu yuko upande wetu na zaidi ya
yote walioko upande wetu ni wengi kuliko wale wanaotutafuta.
Warumi 8:31-39 “Basi, tuseme nini juu ya hayo? Mungu
akiwapo upande wetu, ni nani aliye juu yetu? Yeye asiyemwachilia Mwana wake
mwenyewe, bali alimtoa kwa ajili yetu sisi sote, atakosaje kutukirimia na mambo
yote pamoja naye? Ni nani atakayewashitaki wateule wa Mungu? Mungu ndiye mwenye
kuwahesabia haki. Ni nani atakayewahukumia adhabu? Kristo Yesu ndiye aliyekufa;
naam, na zaidi ya hayo, amefufuka katika wafu, naye yuko mkono wa kuume wa
Mungu; tena ndiye anayetuombea. Ni nani atakayetutenga na upendo wa Kristo? Je!
Ni dhiki au shida, au adha, au njaa, au uchi, au hatari, au upanga? Kama
ilivyoandikwa, ya kwamba, Kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa, Tumehesabiwa
kuwa kama kondoo wa kuchinjwa. Lakini katika mambo hayo yote tunashinda, na
zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda. Kwa maana nimekwisha kujua hakika ya
kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala
yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo, wala yaliyo juu, wala yaliyo
chini, wala kiumbe kinginecho chote hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu
ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu.”
2Wafalme 6:15-16 “Hata asubuhi na mapema mtumishi wake
yule mtu wa Mungu alipoondoka, na kwenda nje, kumbe! Pana jeshi la watu, na
farasi na magari, wameuzingira mji ule. Mtumishi wake akamwambia, Ole wetu!
Bwana wangu, tufanyeje? Akamjibu, Usiogope; maana walio pamoja nasi ni wengi
kuliko wale walio pamoja nao.”
5.
Kumbuka
kuwa tuko vitani – kila mtu wa Mungu popote alipo anapaswa kufahamu kuwa
ana vita, na majungu ni sehemu ya vita hiyo, kutokana na kuwa mwema, kusema
kweli, kutokupokea rushwa, na hata ustawi wako wivu unaweza kuinuka tu na watu
wakaanza kupika majungu kama sehemu ya mashambulizi yako na familia yako na
ustawi wako kwa sababu ya wokovu wetu na sifa zetu tulizo nazo kwa Mungu
shetani atatupiga vita, vita kali sana, kwa kuwa tuko vitani kila wakati tumia
sila za kiroho. Shetani anaitwa mshitaki wetu, wakati mwingine atatushitaki kwa
uwongo, waliomshitaki Yesu walifanya vile kwa fitina tu
Mathayo 27:15-18 “Basi wakati wa siku kuu, liwali
desturi yake huwafungulia mkutano mfungwa mmoja waliyemtaka. Basi palikuwa na
mfungwa mashuhuri siku zile, aitwaye Baraba. Basi walipokutanika, Pilato
akawaambia, Mnataka niwafungulie yupi? Yule Baraba, au Yesu aitwaye Kristo? Kwa
maana alijua ya kuwa wamemtoa kwa husuda.”
2Wakorintho 10:3-6 “Maana ingawa tunaenenda
katika mwili, hatufanyi vita kwa jinsi ya mwili; (maana silaha za vita vyetu si
za mwili, bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome;) tukiangusha
mawazo na kila kitu kilichoinuka, kijiinuacho juu ya elimu ya Mungu; na
tukiteka nyara kila fikira ipate kumtii Kristo; tena tukiwa tayari kupatiliza
maasi yote, kutii kwenu kutakapotimia.”
Waefeso 6:10-13 “Hatimaye, mzidi kuwa hodari katika
Bwana na katika uweza wa nguvu zake. Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza
kuzipinga hila za Shetani. Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na
nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya
majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho.Kwa sababu hiyo twaeni silaha
zote za Mungu, mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza
yote, kusimama.”
6.
Usishiriki
majungu bali uyakemee – majungu yanaambukiza hivyo yanaweza kumnasa mtu
yeyote dhaifu asiye na ujuzi kuhusu neno la Mungu na asiye na akili
iliyopanuka, lakini watu wakomavu wanakemea habari zozote za uvumi na uzushi,
kushiriki majungu ni kushiriki matendo yasiyozaa ya giza
Waefeso 5:11-14 “Wala msishirikiane na matendo
yasiyozaa ya giza, bali myakemee; kwa kuwa yanayotendeka kwao kwa siri, ni aibu
hata kuyanena. Lakini yote yaliyokemewa hudhihirishwa na nuru maana kila
kilichodhihirika ni nuru.Hivyo husema, Amka, wewe usinziaye, Ufufuke katika
wafu, Na Kristo atakuangaza.”
Kutoka 23:1-2 “Usivumishe habari za uongo; usitie
mkono wako pamoja na mwovu, kuwa shahidi wa udhalimu.Usiandamane na mkutano
kutenda uovu; wala usitie ushahidi wako katika neno lo lote kwa kugeukia kando
na kuandamana na mkutano ili kupotoa hukumu;”
7.
Kumbuka
fitina inaweza kuwepo hata kanisani – Watu wengi waliookoka huwa wanaumia
sana wanapofanyiwa fitina na wakristo wenzao, au kama ni mtumishi wa Mungu
anapofanyiwa fitina na watumishi wenzake, hii huleta maumivu makubwa zaidi kwa
sababu kila mmoja labda hutarajia majungu na fitina vitoke kwa watu wasiomjua
Mungu, Lakini nakutaarifu utambue kuwa jaribu halishagui mlango wa kuingilia au
kutokea linaweza kutoka hata miongoni mwa watu wa Mungu, Kanisa zuri kama lile
lililokuwako Korintho washirika walikuwa na majungu na fitina kiasi hata cha
kuwa na makundi kanisani
1Wakorintho 1:10-13 “Basi ndugu,
nawasihi, kwa jina la Bwana wetu Yesu Kristo, kwamba nyote mnene mamoja; wala
pasiwe kwenu faraka, bali mhitimu katika nia moja na shauri moja. Kwa maana,
ndugu zangu, nimearifiwa habari zenu na wale walio wa nyumbani mwa Kloe, ya
kwamba iko fitina kwenu. Basi, maana yangu ni hii, ya kwamba kila mtu wa kwenu
kusema, Mimi ni wa Paulo, na, Mimi ni wa Apolo, na, Mimi ni wa Kefa, na, Mimi
ni wa Kristo. Je! Kristo amegawanyika? Je! Paulo alisulibiwa kwa ajili yenu? Au
je! Mlibatizwa kwa jina la Paulo? ”
8.
Kumbuka
kuwa majungu ni silaha ya shetani – Mojawapo ya silaha anayoitumia shetani
kuwashambulia watu wa Mungu ni pamoja na majungu, majungu ni mashitaka ya
kupikwa, Shetani alipika majungu kwaajili ya Ayubu, na pia alipika majungu
kwajili ya kuhani mkuu Yoshua, ilimradi tu Mungu aondoe mkono wake kisha
shetani apate sababu ya kushambulia yeye ni baba wa majungu na hivyo
usishangazwe akiwatumia watu wale anaowatumia ni watoto wake, ni kazi ya
shetani kuwapikia majungu watu wa Mungu, kwa hiyo kila uyaonapo hayo
yakifanyika kokote kule kumbuka na ujue ni kazi za shetani, na ukimuomba Mungu
atakupa ushindi dhidi ya majungu hayo.
Yohana 8:44 “Ninyi ni wa baba yenu, Ibilisi, na
tamaa za baba yenu ndizo mpendazo kuzitenda. Yeye alikuwa mwuaji tangu mwanzo;
wala hakusimama katika kweli, kwa kuwa hamna hiyo kweli ndani yake. Asemapo
uongo, husema yaliyo yake mwenyewe; kwa sababu yeye ni mwongo, na baba wa huo.”
Ayubu 1:6-11 “Ilikuwa, siku moja ambayo hao wana
wa Mungu walikwenda kujihudhurisha mbele za Bwana, Shetani naye akaenda kati
yao. Bwana akamwuliza Shetani, Umetoka wapi wewe? Ndipo Shetani akamjibu Bwana,
na kusema, Natoka katika kuzunguka-zunguka duniani, na katika kutembea huku na
huku humo. Kisha Bwana akamwuliza Shetani, Je! Umemwangalia huyo mtumishi wangu
Ayubu? Kwa kuwa hapana mmoja aliye kama yeye duniani, mtu mkamilifu na
mwelekevu, mwenye kumcha Mungu na kuepukana na uovu. Ndipo Shetani akamjibu
Bwana, na kusema, Je! Huyo Ayubu yuamcha Bwana bure? Wewe hukumzingira kwa
ukigo pande zote, pamoja na nyumba yake, na vitu vyote alivyo navyo? Kazi za
mikono yake umezibarikia, nayo mali yake imeongezeka katika nchi. Lakini nyosha
mkono wako sasa, uyaguse hayo yote aliyo nayo, naye atakukufuru mbele za uso
wako.”
Zekaria 3:1-4 “Kisha akanionyesha Yoshua, kuhani
mkuu, amesimama mbele ya malaika wa Bwana, na Shetani amesimama mkono wake wa
kuume ili kushindana naye. Bwana akamwambia Shetani, Bwana na akukemee Ewe
Shetani; naam, Bwana, aliyechagua Yerusalemu, na akukemee; je! Hiki si kinga
kilichotolewa motoni? Basi, Yoshua alikuwa amevaa nguo chafu sana, naye alikuwa
akisimama mbele ya malaika. Naye huyo akajibu, akawaambia wale waliosimama
mbele yake, akisema, Mvueni nguo hizi zenye uchafu. Kisha akamwambia yeye,
Tazama, nimekuondolea uovu wako, nami nitakuvika mavazi ya thamani nyingi.”
9.
Kumbuka
Mungu anawacheka wanaofanya Majungu – Mungu anawacheka wakati wote wafanya
majungu kwa sababu njia za Mungu ziko juu sana hakuna mtu anaweza kushindana na
kusudi la Mungu, kwa hiyo hata kama majungu yanaonekana kana kwamba
yatafanikiwa ni muhimu kufahamu kuwa Mungu atatumia njia hiyo kutokeza mlango
mwingine wa mafanikio hivyo kumbuka usiogope
Ayubu 42:2 “Najua ya kuwa waweza kufanya mambo
yote, Na ya kuwa makusudi yako hayawezi kuzuilika.”
Zaburi 2:1-5 “Mbona mataifa wanafanya ghasia, Na
makabila wanatafakari ubatili? Wafalme wa dunia wanajipanga, Na wakuu wanafanya
shauri pamoja, Juu ya Bwana, Na juu ya masihi wake.Na tuvipasue vifungo vyao,
Na kuzitupia mbali nasi kamba zao.Yeye aketiye mbinguni anacheka, Bwana
anawafanyia dhihaka.Ndipo atakaposema nao kwa hasira yake, Na kuwafadhaisha kwa
ghadhabu yake.”
Na Rev. Innocent Samuel Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni