Jumatano, 20 Novemba 2024

Tatizo la majungu makazini!


Matendo 4:24-30 “Nao waliposikia, wakampazia Mungu sauti zao kwa moyo mmoja, wakisema, Mola, wewe ndiwe Mungu, ndiwe uliyefanya mbingu na nchi na bahari na vitu vyote vilivyomo; nawe ulinena kwa Roho Mtakatifu kwa kinywa cha babaetu Daudi, mtumishi wako, Mbona mataifa wamefanya ghasia, Na makabila wametafakari ubatili? Wafalme wa dunia wamejipanga, Na wakuu wamefanya shauri pamoja Juu ya Bwana na juu ya Kristo wake. Maana ni kweli, Herode na Pontio Pilato pamoja na Mataifa na watu wa Israeli, walikusanyika katika mji huu juu ya Mtumishi wako mtakatifu Yesu, uliyemtia mafuta, ili wafanye yote ambayo mkono wako na mashauri yako yamekusudia tangu zamani yatokee. Basi sasa, Bwana, yaangalie matisho yao; ukawajalie watumwa wako kunena neno lako kwa ujasiri wote, ukinyosha mkono wako kuponya; ishara na maajabu vifanyike kwa jina la Mtumishi wako mtakatifu Yesu.”




Utangulizi:

Mojawapo ya changamoto kubwa inayoikabili jamii katika nyakati za leo ni pamoja na tatizo la majungu Makazini, Majungu makazini yameweza kuathiri kwa kiwango kikubwa maisha na mahusiano ya watu katika mazingira ya kazi pamoja na ufanisi wao na kusababisha maumivu makubwa kwa watu wengi, wengine walifungwa magerezani, wengine walitupwa katika makanwa ya simba, wengine walisingiziwa makosa makubwa ya ubakaji, wengine walifanyiwa ghasia na wengine waliuawa na wengine walifitinishwa, wengine wameumizwa mioyo kwa sababu ya kuwepo kwa majungu makazini na wengi wa wale wanaoumizwa ni wale wasio na hatia wenye mioyo mororo, Uwepo wa majungu makazini, serikalini, makanisani na katika mashirika ya kiserikali na yasiyo ya kiserikali, Kwenye biashara, mitaani, katika ndoa  na maeneo mengine yamesababisha maumivu mengi sana katika jamii, Hata hivyo maandiko au neno la Mungu linawatia moyo wale wote wanaofanyiwa majungu au fitina kutokuogopa na kuhakikisha kuwa wakati wote wanalitukuza jina la Mungu na kumuhofu yeye hata wakati wanapopitia changamoto ngumu katika majungu watakayoyapitia na kuwahakikishia kuwa hata katika hayo Mungu yuko pamoja nao.

Isaya 8:10-13 “Fanyeni shauri pamoja, nalo litabatilika; Semeni neno, lakini halitasimama; Kwa maana Mungu yu pamoja nasi. Maana Bwana aliniambia hivi, kwa mkono hodari, akanifundisha nisiende katika njia ya watu hawa, akisema,Msiseme, Ni FITINA (Majungu), katika habari za mambo yote ambayo watu hawa watasema, Ni FITINA (Majungu); msihofu kwa hofu yao, wala msiogope. Bwana wa majeshi ndiye mtakayemtakasa; na awe yeye hofu yenu, na awe yeye utisho wenu.”

Kwa hiyo neno la Mungu linaonyesha kuwa watu wa Mungu wanaweza kuathiriwa na majungu (Fitina) katika mazingira yao ya shughuli za kila siku lakini hawapaswi kuogopa na wanapaswa kumtakasa Mungu katika mapito hayo kwani Mungu atakuwa pamoja nao, Kwa sababu hiyo basi, Leo tutachukua muda kujifunza kwa kina na mapana na marefu kuhusu Tatizo la majungu makazini, tutajifunza somo hili Tatizo la Majungu Makazini kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-

 

·         Maana ya Majungu.

·         Tatizo la majungu makazini.

·         Jinsi ya kukabiliana na tatizo la Majungu.

 

Maana ya Majungu.

Majungu ni moja ya changamoto kubwa ambayo imeumiza mioyo ya watu wengi katika jamii, Majungu yako kila mahali katika jamii, yapo makazini, yapo mashuleni, yapo katika taasisi za kiserikali na zisizo za kiserikali, yapo makanisani na maeneo mengine mengi, kwa ujumla majungu ni sehemu ya maisha ya mwanadamu, kama jinsi ambavyo dhambi ni moja ya tatizo kubwa la aina mwanadamu hali kadhalika miongoni mwa dhambi hizo ni pamoja na dhambi hii ya majungu. Kimsingi sio rahisi kukuta neno majungu moja kwa moja katika maandiko, msamiati huu wa neno Majungu haujatumika katika maandiko lakini hii haimaanishi kuwa majungu hayajatajwa katika maandiko, majungu yametajwa katika maandiko kwa lugha nyingine kama tutakavyojifunza mbele kidogo Majungu hasa ni nini?

Neno majungu linamaanisha Mazungumzo, mipango au mikakati, inayofanywa na watu wengine, kumhusu mtu mwingine asiyekuwepo, au hata akiwepo kwa kujadili yale yanayofikiriwa kuwa ni mapungufu, au udhaifu, au kuharibu hadhi ya mtu huyo hususani mwenyewe anapokuwa hayupo, au hata akiwepo. Majungu pia yanaweza kuchukua sura nyingine ambapo watu wanaokufanyia majungu wanapanga mkakati wa kukuharibia kwa mazungumzo yao, au kwa kushambulia sifa zako, au kwa kukushitakia au kukuchongea kwa wakubwa au watu ili ikiwezekana usikubalike au upatwe na madhara, Majungu yanaweza kuwa ni matokeo ya ubinafsi, wivu na fitina walizo nazo wahusika au wivu wenye uchungu, husuda, katika biblia neno linalotumika kuhusu majungu katika Kiswahili ni “FITINA” na katika kiingereza ni “CONSPIRACY” au “CONFEDERACY”  yaani watu wanaokubaliana au kupatana kumfanyia mabaya mtu mwingine kwa kusudi la kumuharibia, kumpindua, kumkwamisha, kumchafulia sifa zake, kumuondoa kazini, kumshusha cheo, kumhamisha kwa sababu mbalimbali ikiwepo hata wivu na kadhalika, kufanya shauri (mjadala) wa kifitina au kumfanyia ghasia kwa kusudi la kumkwamisha kwa kiibrania  “Berīth” au “Kesher” litokanalo na neno “Kāshar” Maneno haya yote yana maana ya Conspiracy ambayo kwa kiingereza maana yake inasomeka hivi “Conspiracy means an agreement to falsely indict an innocent person of felony” – tafasiri yake kwa Kiswahili ni Mipango au makubaliano au njama zinazopangwa kwa kusudi la kumpachikia mtu asiye na hatia au kumchafua mtu asiye na hatia. Au kumuharibia, au kupanga njama za uasi, njama za fitina, njama za uchochezi na kadhalika. Sababu kubwa ikiwa ni wivu, wivu wenye uchungu, husuda na ubinafsi, au tamaa, kutokujiamini na udhaifu mwingine wa kibinadamu. Wakati mwingine kwa sababu ya mtu kufikiri kuwa atachukua nafasi yako.

2Samuel 15:10-12 “Lakini Absalomu akapeleka wapelelezi katika kabila zote za Israeli kusema, Mara mtakaposikia sauti ya tarumbeta, ndipo mtakaposema Absalomu anamilikl huko Hebroni. Na watu mia mbili walioalikwa wakatoka Yerusalemu pamoja na Absalomu, wakaenda katika ujinga wao wasijue neno lo lote. Absalomu naye akatuma kumwita Ahithofeli Mgiloni, mshauri wake Daudi, kutoka katika mji wake, yaani, Gilo, alipokuwa akitoa dhabihu. FITINA yao ikawa na nguvu; maana watu waliokuwa pamoja na Absalomu wakazidi kuwa wengi.”    

2Wafalme 12:19-21 “Basi mambo yote ya Yoashi yaliyosalia, na yote aliyoyafanya, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Yuda? Nao watumishi wake wakaondoka, wakafanya FITINA, wakamwua Yoashi katika nyumba ya Milo, hapo panaposhukia Sila. Kwa maana Yozakari mwana wa Shimeathi, na Yehozabadi mwana wa Shomeri, watumishi wake, wakampiga, naye akafa; wakamzika pamoja na babaze mjini mwa Daudi. Na Amazia mwanawe akatawala mahali pake.”

Zaburi 2:1-2 “Mbona mataifa wanafanya ghasia, Na makabila wanatafakari ubatili? Wafalme wa dunia wanajipanga, Na wakuu wanafanya shauri pamoja, Juu ya Bwana, Na juu ya masihi wake.”

Kwa hiyo neno “Fitina” linaweza kumaanisha neno “Majungu” sasa basi watu wengi sana wameumizwa katika mioyo yao makazini na katika maisha na maeneo mbalimbali kwa sababu ya fitina, wengine wameuawa, wengine wamefungwa, wengine wamepotezewa heshima na wengine wamechafuliwa sifa zao na kuhujumiwa na kuumizwa mioyo kwa sababu ya majungu (yaani fitina, njama)  maandiko yanaonyesha mifano ya watu wengi sana ambao walifanyiwa fitina na majungu na ghasia akiwepo Bwana wetu Yesu Kristo, Mungu augange moyo wako kama wewe ni moja ya waathirika wa fitina na majungu yanayokukuta kazini, na katika maisha haya. Uongezewe neema sana!

Mungu amekataza majungu Katika neno lake amekataa aina yoyote ya uvumi wa uongo dhidi ya mtu hata kama wale wanaotengeneza majungu hayo wako wengi, maonyo hayo hayana budi kuzingatiwa.

Kutoka 23:1-2 “Usivumishe habari za uongo; usitie mkono wako pamoja na mwovu, kuwa shahidi wa udhalimu.Usiandamane na mkutano kutenda uovu; wala usitie ushahidi wako katika neno lo lote kwa kugeukia kando na kuandamana na mkutano ili kupotoa hukumu;”               

Tatizo la majungu makazini.

Tatizo la majungu au fitina sio tatizo jipya duniani ni changamoto ya siku nyingi sana tangu kuumbwa kwa mwanadamu, kwa hiyo majungu ni sehemu ya kawaida ya maisha, wakati mwingine watu wanaweza kukukalia kikao mara unapokuwa haupo na unaporejea unakuta mada zinabadilishwa, kila mahali kuna aina yake ya majungu  au FITINA hata makanisani katika taasisi za kidini na kiroho, unaweza wakati mwingine ukasikia na unaweza wakati mwingine usisikie wala usijue kuwa watu wanakuwazia nini lakini nako kuna majungu, Na usipokuwa mwangalifu hata wewe unaweza kujikuta ukishiriki na wengine katika kumfanyia majungu (FITINA) mtu mwingine Neno la Mungu yaani Biblia limejaa mifano ya watu kibao ambao walifanyiwa majungu katika maisha yao na katika mazingira mbali mbali, unaweza kufanyiwa majungu kwa sababu ya kibali kikubwa ulicho nacho, unaweza kutendewa majungu ili watu wakuchafue, unaweza kufanyiwa majungu, ili uhamishwe, au ili ushushwe cheo, au ili ufukuzwe kazi, au ili uumizwe na kadhalika, dunia ni uwanja wa fujo na kwa sababu hiyo tatizo la fitina na majungu liko kila mahali unaweza kufanyiwa fitina wakati mwingine ili ikiwezekana uachane hata na mumeo au mkeo, hapa iko mifano michache kati ya mingi sana ya watu waliofanyiwa fitina au majungu katika Biblia kwa sababu mbalimbali na wengine walipata madhara na kuuawa na wengine Mungu aliingilia kati  na kuwasaidia, hali hii ndiyo inayowakuta watu mahali pa kazi, inawakuta watu katika taasisi, inawakuta watu katika huduma, inawakuta watu katika biashara, inawakuta watu mashuleni, inawakuta watu katika jamii na kila mahali aliko mwanadamu majungu hayakosekani.

1.       Wana wa Israel dhidi ya Yusufu – Yusufu alifanyiwa majungu na ndugu zake, wana wa Israel ndugu wa baba mmoja, kutokana na nafasi aliyokuwa nayo na kibali na upendo mkubwa alioupata kutoka kwa baba yake, pamoja na jinsi Mungu alivyosema naye kuhusu maisha yake ya baadaye basi watu walimuonea wivu na kuanza kumshambulia walimteta na walianza kupanga njama jinsi na namna ya kumpoteza katika maisha yake ili yamkini ndoto zake zisiweze kutimia.

 

Mwanzo 37:18-20 “Wakamwona toka mbali, na kabla hajawakaribia, wakafanya shauri juu yake ili wamwue.Wakasemezana wao kwa wao, Tazama, yule bwana wa ndoto anakuja. Haya, twende, tukamwue na kumtupa katika birika mojawapo, nasi tutasema, Mnyama mkali amemla; kisha tutaona zitakuwaje ndoto zake.”

 

Aidha ukiacha majungu yaliyofanywa na ndugu zake, Yusufu pia alifanyiwa majungu kazini kwa kupachikiwa kesi na mke wa Potifa kwamba eti alitaka kumbaka jambo lililopelekea Yusufu kuwekwa gerezani kwa miaka karibu 13 Lakini wakati wote maandiko yanatuambia kuwa Mungu alikuwa pamoja naye!

 

Mwanzo 39:2-20 “BWANA akawa pamoja na Yusufu, naye akasitawi; naye alikuwa katika nyumba ya bwana wake, yule Mmisri. Bwana wake akaona ya kwamba BWANA yu pamoja naye, na ya kuwa BWANA anafanikisha mambo yote mkononi mwake. Yusufu akaona neema machoni pake, akamtumikia. Naye akamweka awe msimamizi juu ya nyumba yake, na yote yaliyomo akayaweka mkononi mwake. Ikawa tokea wakati alipomweka awe msimamizi juu ya nyumba yake, na vyote vilivyomo, BWANA akabariki nyumba ya yule Mmisri kwa ajili ya Yusufu. Mbaraka wa BWANA ukawa juu ya vyote alivyokuwa navyo katika nyumba, na katika shamba. Akayaacha yote aliyokuwa nayo mkononi mwa Yusufu; wala hakujua habari za kitu cho chote chake, ila hicho chakula alichokula tu. Ikawa baada ya mambo hayo, mke wa bwana wake akamtamani Yusufu, akamwambia, Lala nami. Lakini akakataa, akamwambia mke wa bwana wake, Tazama, bwana wangu hajui kitu kilichowekwa kwangu nyumbani, na vyote alivyo navyo amevitia mkononi mwangu. Hakuna mkuu katika nyumba hii kuliko mimi, wala hakunizuilia kitu cho chote ila wewe, kwa kuwa wewe u mkewe. Nifanyeje ubaya huu mkubwa nikamkose Mungu? Akawa akizidi kusema na Yusufu siku baada ya siku, lakini hakumsikia alale naye, wala aongee naye. Ikawa, siku moja, akaingia nyumbani atende kazi yake, wala hapakuwa na mtu katika watu wa nyumbani humo ndani; huyo mwanamke akamshika nguo zake, akisema, Lala nami. Yusufu akaiacha nguo yake mkononi mwake, akakimbia, akatoka nje. Ikawa alipoona ya kwamba amemwachilia nguo yake mkononi mwake, naye amekimbia nje, akawaita watu wa nyumbani mwake, akasema nao, akinena, Angalieni, ametuletea mtu Mwebrania atufanyie dhihaka. Ameingia kwangu, ili alale nami, nikalia kwa sauti kuu. Ikawa, aliposikia ya kuwa nimepaza sauti yangu na kulia, aliiacha nguo yake kwangu, akakimbia, akatoka nje. Basi akaiweka ile nguo kwake hata bwana wake aje nyumbani. Naye akamwambia kama maneno hayo, akisema, Yule mtumwa Mwebrania uliyemleta kwetu, aliingia kwangu anidhihaki. Ikawa nilipopaza sauti yangu, nikalia, akaacha nguo yake kwangu akakimbia nje. Ikawa bwana wake aliposikia maneno ya mkewe aliyomwambia, akisema, Mtumwa wako amenitendea mambo kama haya, hasira yake ikawaka. Bwana wake akamtwaa Yusufu, akamtia gerezani, mahali walipofungwa wafungwa wa mfalme, naye akawamo humo gerezani.”

 

Wanadamu wana wivu wenye uchungu, wakati wote wanapotamani nafasi uliyo nayo, au kuhofia kibali ulicho nacho na kuona au kudhani unafanikiwa wivu huwashika na huanza kufanya mashauri ya namna na jinsi ya kukuharibia, au wanapojihisi hawatoshi, hawako salama na kadhalika majungu huibuka, kwa hiyo uharibifu huo unaweza kufanywa kwa mbinu na njia mbalimbali lakini mara nyingi sana majungu husukumwa na chuki na wivu wa kile ulicho nacho na baraka za Mungu zilizoko juu yako. 

 

2.       Haruni na Miriam dhidi ya Musa – Haruni na Mariamu walianza kufikiri vibaya kinyume na Musa, walianza chokochoko ambazo kama Mungu asingezidhibiti zingekuja kugeuka fitina majungu na uasi lakini Mungu aliwakemea haraka sana na kusimama upande wa Musa na kumtetea, na zaidi sana mke wa Musa, Mungu aliwaacha na mara moja Miriam akawa mwenye ukoma Kama sio Musa kuwaombea hali ingekuwa mbaya kwani Haruni alimsihi Musa asiwahesabie dhambi ile kukawa na Rehema za Mungu.  

 

Hesabu 12:1-11 “Kisha Miriamu na Haruni wakamnenea Musa kwa sababu ya mwanamke Mkushi aliyekuwa amemwoa; maana, alikuwa amemwoa mwanamke Mkushi. Wakasema, Je! Ni kweli Bwana amenena na Musa tu? Hakunena na sisi pia? Bwana akasikia maneno yao. Basi huyo mtu, huyo Musa, alikuwa mpole sana zaidi ya wanadamu wote waliokuwa juu ya uso wa nchi. Bwana akanena ghafula na Musa, na Haruni na Miriamu, na kuwaambia, Tokeni nje ninyi watatu, mwende hemani mwa kukutania. Basi hao watatu wakatoka nje.Bwana akashuka katika nguzo ya wingu akasimama pale mlangoni pa Hema, akawaita Haruni na Miriamu, nao wakatoka nje wote wawili.Kisha akawaambia, Sikizeni basi maneno yangu; Akiwapo nabii kati yenu, Mimi, Bwana, nitajifunua kwake katika maono, Nitasema naye katika ndoto. Sivyo ilivyo kwa mtumishi wangu, Musa; Yeye ni mwaminifu katika nyumba yangu yote; Kwake nitanena mdomo kwa mdomo, Maana, waziwazi wala si kwa mafumbo; Na umbo la Bwana yeye ataliona. Mbona basi ninyi hamkuogopa Kumnenea mtumishi wangu, huyo Musa? Hasira za Bwana zikawaka juu yao; naye akaenda zake. Kisha hilo wingu likaondoka kutoka pale juu ya hema; na tazama, Miriamu akawa mwenye ukoma, mweupe kama theluji; Haruni akamwangalia Miriamu, na tazama, yu mwenye ukoma. Kisha Haruni akamwambia Musa, Ee bwana wangu nakusihi sana usituwekee dhambi juu yetu, kwa kuwa tumefanya ya upumbavu, na kufanya dhambi.”

 

3.       Maliwali 120 dhidi ya Daniel –  Maliwali walishikwa na wivu kwa sababu ya mafanikio makubwa ya Daniel kama mkuu wao, na wakaanza majungu na fitina ni namna gani watapata sababu za kushitaki, kwa hiyo walikuja na wazo au muswada kwa Mfalme kukubaliana kwamba asaini kuwa watu wasiabudu mungu yeyote kwa siku 30 isipokuwa kwa Mfalme tu  na mtu atakayefanya kinyume na hilo atupwe kwenye tundu la Simba, lakini pamoja na hayo bado utaona Kuwa Mungu alikuwa pamoja naye na kumlinda Daniel dhidi ya makanwa yote ya Simba na mwisho wa siku wale waliomfanyia fitina na majungu ndio waliokuja kutupwa katika simba

 

Daniel 6:1-9 “Ilimpendeza Dario kuweka juu ya ufalme maliwali mia na ishirini, wawe juu ya ufalme wote; na juu yao akaweka wakubwa watatu, na Danieli alikuwa mmoja wao; ili maliwali hawa watoe hesabu kwao, mfalme asipate hasara. Basi Danieli huyo alipata sifa kuliko wakubwa na maliwali, kwa kuwa roho bora ilikuwa ndani yake; naye mfalme akaazimu kumweka juu ya ufalme wote. Basi mawaziri na maamiri wakatafuta sana kupata sababu za kumshitaki Danieli kwa habari za mambo ya ufalme; lakini hawakuweza kuona sababu wala kosa; kwa maana alikuwa mwaminifu, wala halikuonekana kosa wala hatia ndani yake. Ndipo wale watu wakasema, Hatutapata sababu ya kumshitaki Danieli huyo, tusipoipata katika mambo ya sheria ya Mungu wake. Basi wale mawaziri na maamiri wakakusanyika pamoja mbele ya mfalme, wakamwambia hivi, Mfalme Dario, uishi milele. Mawaziri wote wa ufalme, na manaibu, na maamiri, na madiwani, na maliwali wamefanya shauri pamoja ili kuweka amri ya kifalme; na kupiga marufuku, ya kwamba mtu ye yote atakayeomba dua kwa Mungu awaye yote, au kwa mtu awaye yote, katika muda wa siku thelathini, ila kwako, Ee mfalme atatupwa katika tundu la simba. Sasa, Ee mfalme, piga marufuku, ukatie sahihi maandiko haya, yasibadilike, kama ilivyo sheria ya Wamedi na Waajemi, isiyoweza kubadilika.Basi mfalme Dario akayatia sahihi maandiko yale, na ile marufuku.”

 

4.       Watu wa Yerusalem dhidi na Nabii Yeremia – Mungu alimjulisha Yeremia mapema kuwa watu wamepanga shauri yaani njama, au majungu kwa kusudi la kumfutilia mbali Yeremia na kazi zake za kinabii, yaani wamfutilie mbali yeye na kazi yake yote mti na matunda yake, na walitaka kuhakikisha ya kuwa hata jina lake halitajwi tena kabisa katika nchi ya walio hai, Lakini Mungu alimfunulia Yeremia kuhusu swala hilo na akaamua kumuomba Mungu ampe neema ya kuona kisasi juu ya adui zake waliokusudia swala hilo.

 

Yeremia 11:18-20 “Tena Bwana akanijulisha haya, nami nikayajua; ndipo uliponionyesha matendo yao. Lakini mimi nalikuwa kama mwana-kondoo mpole, achukuliwaye kwenda kuchinjwa; wala sikujua ya kuwa wamefanya mashauri kinyume changu, wakisema, Na tuuharibu mti pamoja na matunda yake, na tumkatilie mbali atoke katika nchi ya walio hai, ili jina lake lisikumbukwe tena. Lakini, Ee Bwana wa majeshi, uhukumuye haki, ujaribuye viuno na moyo, nijalie kuona kisasi chako juu yao; kwa maana nimekufunulia wewe neno langu.”

 

5.       Wayahudi 40 dhidi ya Paulo Mtume – Hawa walikula njama za kutaka kumuua Paulo mtume na waliapa kuwa hawatakula wala kunywa mpaka wamemuua Paulo mtume, walikwenda kwa wakuu wa makuhani na kuwaeleza mpango wao kuwa wao wameweka nadhiri kuwa hawatakula wala kunywa mpaka wamemuua Paulo Mtume, lakini utaweza kuona tena kuwa Mungu alisimama na mtumishi wake na kumtumia Akida wa Askari wa kirumi kuyaokoa maisha ya Paulo, kumbuka Mungu anaona majungu yote unayokusudiwa!.

 

Matendo 23:11-23 “Usiku ule Bwana akasimama karibu naye, akasema, Uwe na moyo mkuu; kwa sababu, kama ulivyonishuhudia habari zangu Yerusalemu, imekupasa kunishuhudia vivyo hivyo Rumi nako.Kulipopambauka, Wayahudi wakafanya mapatano, wakajifunga kwa kiapo kwamba hawatakula wala hawatakunywa hata wamwue Paulo.Na hao walioapiana hivyo walipata zaidi ya watu arobaini. Nao wakaenda kwa wakuu wa makuhani na wazee, wakasema, Tumejifunga kwa kiapo tusionje kitu hata tumwue Paulo. Basi sasa ninyi pamoja na wazee wa baraza mwambieni jemadari amlete chini kwenu, kana kwamba mnataka kujua habari zake vizuri zaidi; na sisi tu tayari kumwua kabla hajakaribia. Mjomba wake Paulo akasikia habari za kuotea kwao, akaenda akaingia ndani ya ngome akampasha Paulo habari. Paulo akamwita akida mmoja, akasema, Mchukue kijana huyu kwa jemadari; maana ana neno la kumwarifu. Basi akamchukua, akampeleka kwa jemadari, akamwambia, Paulo, yule mfungwa, aliniita akataka nikuletee kijana huyu kwa kuwa ana neno la kukuambia.Yule jemadari akamshika mkono akajitenga pamoja naye kando, akamwuliza kwa faragha, Una neno gani utakalo kuniarifu? Akasema Wayahudi wamepatana kukuomba umlete Paulo chini kesho, ukamweke mbele ya baraza, kana kwamba wanataka kupata habari zake kwa usahihi zaidi.Basi wewe usikubali; kwa maana watu zaidi ya arobaini wanamwotea, wamejifunga kwa kiapo wasile wala wasinywe hata watakapomwua; nao sasa wako tayari, wakiitazamia ahadi kwako.Basi yule jemadari akamwacha kijana aende zake, akimwagiza, Usimwambie mtu awaye yote ya kwamba umeniarifu haya.Akawaita maakida wawili, akasema, Wekeni tayari askari mia mbili kwenda Kaisaria, na askari wapanda farasi sabini, na wenye mikuki mia mbili, kwa saa tatu ya usiku. Akawaambia kuweka wanyama tayari wampandishe Paulo, na kumchukua salama kwa Feliki liwali.”

 

6.       Yezebeli dhidi ya Nabothi – Nabothi alikuwa na shamba la urithi wa familia yake, na shamba hili lilitamaniwa na mfalme, ili alitumie yeye, Lakini Nabothi alimkatalia kwa vile lilikuwa shamba la urithi na urithi hauuzwi wala kubadilishwa, jambo hili lilimuhuzunisha mfalme mwenye tamaa, na mkewe yaani malkia aliyeitwa Yezebeli yeye  alimwambia usihangaike, yeye akapanga njama za kumsingizia Naboth kesi ya kumtukana Mungu na mfalme kwa wazee wa mji na kutengeneza ushahidi wa uongo na kwa sababu hiyo Nabothi aliuawa na damu isiyo na hatia ikamwagika kwa sababu nya tamaa ya mfalme na majungu ya Yezebeli

 

1Wafalme 21:1-19 “Ikawa baada ya hayo, Nabothi Myezreeli alikuwa na shamba la mizabibu katika Yezreeli, karibu na nyumba ya kifalme ya Ahabu mfalme wa Samaria. Ahabu akasema na Nabothi, akamwambia, Nipe shamba lako la mizabibu nilifanye shamba la mboga, maana ni karibu na nyumba yangu; nami nitakupa badala yake shamba la mizabibu lililo zuri zaidi; au ukipenda, nitakupa fedha sawasawa na thamani yake. Nabothi akamwambia Ahabu, Bwana apishe mbali nikupe wewe urithi wa baba zangu. Basi Ahabu akaenda nyumbani kwake, ana moyo mzito, tena amekasirika, kwa sababu ya neno lile aliloambiwa na Nabothi Myezreeli, akisema, Sitakupa urithi wa baba zangu. Akajilaza kitandani pake, akageuza uso wake, akakataa kula. Lakini Yezebeli mkewe akamwendea, akamwambia, Kwa nini roho yako ina huzuni hata usile chakula? Akamwambia, Kwa sababu nimesema na Nabothi Myezreeli, nikamwambia, Unipe shamba lako la mizabibu kwa fedha, au, ukipenda, nitakupa shamba la mizabibu lingine badala yake. Akajibu, Sitakupa shamba langu la mizabibu. Yezebeli mkewe akamwambia, Je! Sasa wewe unaumiliki ufalme wa Israeli? Ondoka, ule chakula, moyo wako ufurahi; mimi nitakupa shamba la mizabibu la Nabothi Myezreeli. Basi, akaandika nyaraka kwa jina la Ahabu, akazitia muhuri yake, akazipeleka zile nyaraka kwa wazee, na kwa watu wenye nguvu waliokuwa katika mji wake, waliokaa pamoja na Nabothi. Akaandika katika zile nyaraka, akasema, Pigeni mbiu ya watu kufunga, mkamweke Nabothi juu mbele ya watu, mkainue watu wawili, watu wasiofaa, ili wamshitaki, na kumshuhudia, kunena, Umemtukana Mungu na mfalme. Kisha mchukueni nje, mkampige kwa mawe, ili afe.Wale wazee wa mji wake, na walio wenye nguvu waliokaa mjini mwake, wakafanya kama Yezebeli alivyowaagiza, kama ilivyoandikwa katika nyaraka alizowapelekea. Wakapiga mbiu ya watu kufunga, wakamweka Nabothi juu mbele ya watu. Na hao watu wawili, watu wasiofaa, wakaingia, wakaketi mbele yake; wale watu wasiofaa wakamshuhudia Nabothi mbele ya watu, wakasema, Nabothi amemtukana Mungu na mfalme. Ndipo wakamchukua nje ya mji, wakampiga kwa mawe hata akafa. Wakampelekea Yezebeli habari, wakasema, Nabothi amepigwa kwa mawe, amekufa. Ikawa Yezebeli aliposikia ya kwamba Nabothi amepigwa kwa mawe na kufa, Yezebeli akamwambia Ahabu, Inuka, ulitamalaki shamba la mizabibu la Nabothi Myezreeli, alilokataa kukupa kwa fedha, maana Nabothi hako hai, lakini amekufa. Ikawa Ahabu aliposikia ya kwamba Nabothi amekufa, akaondoka, alitelemkie shamba la mizabibu la Nabothi Myezreeli, ili alitamalaki. Neno la Bwana likamjia Eliya Mtishbi, kusema, Ondoka, ushuke, ukutane na Ahabu mfalme wa Israeli, akaaye katika Samaria; yuko katika shamba la mizabibu la Nabothi, ndiko alikoshukia ili alitamalaki. Ukamwambie, ukisema, Bwana asema hivi, Je! Umeua, ukatamalaki? Nawe utamwambia, kusema, Bwana asema hivi, Mahali pale mbwa walipoiramba damu ya Nabothi, mbwa watairamba na damu yako, naam, damu yako.”

 

7.       Wakuu wa dini dhidi ya Yesu – Tangu mwanzoni mwa huduma ya Yesu Kristo ni ukweli ulio wazi kuwa wakuu wa dini hawakufurahishwa na huduma na utendaji wa Yesu Kristo ambaye kimsingi huduma yake na utendaji wake ulikuwa na mvuto mkubwa sana kwa maelefu ya watu, Maadui wa Yesu Kristo wakiongozwa na kuhani mkuu na wazee waliketi kwa siri katika nyumba ya Kayafa na kuyapanga majungu agenda kuu ikiwa ni jinsi na namna ya kumnasa, kumkamata  na hatimaye kumuua Yesu

 

Mathayo 26:3-5 “Wakati ule wakuu wa makuhani, na wazee wa watu, wakakusanyika katika behewa ya Kuhani Mkuu, jina lake Kayafa; wakafanya shauri pamoja, ili wamkamate Yesu kwa hila na kumwua.Lakini wakasema, Isiwe wakati wa sikukuu, isije ikatokea ghasia katika watu.”     

Jinsi ya kukabiliana na tatizo la Majungu.

Maandiko yanasema mtaifahamu kweli nayo kweli itawaweka huru, moja ya jambo la msingi na la muhimu ni kutambua kuwa majungu yapo na yapo kila mahali yanaweza kuweko kazini, katika jamii, katika kazi, katika familia na hata kutoka miongoni mwa wapendwa na ndugu, hakuna mwanadamu anaweza kufurahia ustwai wako, ndugu zake Yusufu hawakufurahia ustawi wake, mawaziri hawakufurahia ustawi wa Daniel, na la kushangaza kabisa hata Haruni na Miriam walimsengenya Musa, lakini hata viongozi wa dini walipanga njama za kumuua nabii Yeremia na  kuufutilia mbali unabii wake  na Yesu  na hata njama za kulinda kaburi ili asifufuke, na njama za kupoteza ushahidi wa kufufuka kwake na rushwa ikatolewa kwa askari, wasiseme kilichotokea, hivyo ndivyo jamii ilivyo, watu wengi kwa kutokujua wameumizwa sana mioyo yao, wametesa nafsi zao kwa sababu wamefanyiwa ukatili ambao hawakuwahi kuutarajia maandiko yanatuelekeza nini cha kufanya tunapoishi katika jamii yenye majungu unapaswa kufahamu kuwa Mungu wetu halali wala hasinzii na kuwa anajua kila kinachoendelea na anaona na atalipa tu hapa yako maswala kadhaa ya kufanya.

1.       Tambua Mungu ni mkuu kuliko majungu – fahamu ya kuwa madhara ya majungu hayawezi kuvuka mpaka wa mwenyezi, kama kuna kitu hatupaswi kuogopa basi ni majungu, na kama kuna kitu tunapaswa kuogopa basi tumuogope Mungu, lakini mwanadamu hana uwezo wa kukufanya lolote walimfanyia Yesu fitina na wakamuua lakini Mungu akamfufua siku ya tatu, hakuna mpango wowote wa Mungu kwako utakaoharibiwa.

 

Isaya 8:10-13 “Fanyeni shauri pamoja, nalo litabatilika; Semeni neno, lakini halitasimama; Kwa maana Mungu yu pamoja nasi. Maana Bwana aliniambia hivi, kwa mkono hodari, akanifundisha nisiende katika njia ya watu hawa, akisema,Msiseme, Ni FITINA (Majungu), katika habari za mambo yote ambayo watu hawa watasema, Ni FITINA (Majungu); msihofu kwa hofu yao, wala msiogope. Bwana wa majeshi ndiye mtakayemtakasa; na awe yeye hofu yenu, na awe yeye utisho wenu.”

 

Mfanye Bwana kuwa ndio hofu yako neno Bwana wa majeshi ndiye mtakayemtakasa kwa kiebrania mtakayemtakasa linasomeka kama “Qadas” kimatamshi “kah-dash” ambalo maana yake Bwana awe ndiye hofu yako, kwa hiyo hakuna sababu ya kuwaogopa wanadamu na badala yake tumuogope Mungu.

 

Zaburi 27:1-4 “Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu, Nimwogope nani? Bwana ni ngome ya uzima wangu, Nimhofu nani? Watenda mabaya waliponikaribia, Wanile nyama yangu, Watesi wangu na adui zangu, Walijikwaa wakaanguka. Jeshi lijapojipanga kupigana nami, Moyo wangu hautaogopa. Vita vijaponitokea, Hata hapo nitatumaini. Neno Moja nimelitaka kwa Bwana, Nalo ndilo nitakalolitafuta, Nikae nyumbani mwa Bwana Siku zote za maisha yangu, Niutazame uzuri wa Bwana, Na kutafakari hekaluni mwake.”

 

2.       Jiepushe na maneno yasiyo na maana – wakati mwingine majungu hayo hupelekwa kwa viongozi na kwa bahati mbaya wako viongozi ambao kila kitu kinachopelekwa kwao wanadhani ni kweli na hawajua kuwa wako watu wazushi na wapika majungu, wakati wote maandiko yanatutaka kujiepusha na maneno yasiyo na maana  na watu wenye tabia za uzushi na fitina na majungu na hasa kama yanamuhusu Mtumishi wa Mungu

 

2Timotheo 2:16-18 “Jiepushe na maneno yasiyo na maana, ambayo si ya dini; kwa kuwa wataendelea zaidi katika maovu,na neno lao litaenea kama donda-ndugu. Miongoni mwa hao wamo Himenayo na Fileto, walioikosa ile kweli, wakisema ya kwamba kiyama imekwisha kuwapo, hata kuipindua imani ya watu kadha wa kadha.”

 

1Timotheo 5:19 “Usikubali mashitaka juu ya mzee, ila kwa vinywa vya mashahidi wawili au watatu.”

 

3.       Kataa kujadili lolote lisolompa Mungu utukufu – kwa kawaida watu wanapojadili mambo yaliyo manajisi nao hunajisika  maandiko yanasema kila kwenye wingi wa maneno hakukosi kuwa na dhambi, kwakristo hawana budi kuhakikisha kuwa wanatunza ndimi zao kwa sabahu ulimi ni kiungo kinachoweza kuleta madhara makubwa ikiwa ni pamoja na kuwadhuru watu wengine na watu wasio na hatia  

 

Mithali 10:18-19 “Yeye afichaye chuki ana midomo ya uongo, Na yeye asingiziaye ni mpumbavu.Katika wingi wa maneno hapakosi kuwa na maovu; Bali yeye azuiaye midomo yake hufanya akili.”

 

Wafilipi 4:8 “Hatimaye, ndugu zangu, mambo yo yote yaliyo ya kweli, yo yote yaliyo ya staha, yo yote yaliyo ya haki, yo yote yaliyo safi, yo yote yenye kupendeza, yo yote yenye sifa njema; ukiwapo wema wo wote, ikiwapo sifa nzuri yo yote, yatafakarini hayo.”

 

Yakobo 3:1-8 “Ndugu zangu, msiwe waalimu wengi, mkijua ya kuwa mtapata hukumu kubwa zaidi. Maana twajikwaa sisi sote pia katika mambo mengi. Mtu asiyejikwaa katika kunena, huyo ni mtu mkamilifu, awezaye kuuzuia na mwili wake wote kama kwa lijamu. Angalieni, twatia lijamu katika vinywa vya farasi, ili wamtii, hivi twageuza mwili wao wote. Tena angalieni merikebu; ingawa ni kubwa kama nini, na kuchukuliwa na pepo kali, zageuzwa na usukani mdogo sana, ko kote anakoazimia kwenda nahodha.Vivyo hivyo ulimi nao ni kiungo kidogo, nao hujivuna majivuno makuu. Angalieni jinsi moto mdogo uwashavyo msitu mkubwa sana. Nao ulimi ni moto; ule ulimwengu wa uovu, ule ulimi, umewekwa katika viungo vyetu, nao ndio uutiao mwili wote unajisi, huuwasha moto mfulizo wa maumbile, nao huwashwa moto na jehanum. Maana kila aina ya wanyama, na ya ndege, na ya vitambaavyo, na ya vitu vilivyomo baharini, vinafugika, navyo vimekwisha kufugwa na wanadamu.Bali ulimi hakuna awezaye kuufuga; ni uovu usiotulia, umejaa sumu iletayo mauti.”

 

4.       Majungu hayawezi kututenga na upendo wa Mungu – katika matukio yote ya fitina na majungu tuliyojifunza waliyofanyiwa watakatifu waliotutangulia utaweza kuona wote Mungu alikuwa pamoja nao kwa hiyo kila mtu wa Mungu anapokutana na fitina na majungu kazini anapaswa kukumbuka kuwa Mungu yuko upande wetu na zaidi ya yote walioko upande wetu ni wengi kuliko wale wanaotutafuta.

 

Warumi 8:31-39 “Basi, tuseme nini juu ya hayo? Mungu akiwapo upande wetu, ni nani aliye juu yetu? Yeye asiyemwachilia Mwana wake mwenyewe, bali alimtoa kwa ajili yetu sisi sote, atakosaje kutukirimia na mambo yote pamoja naye? Ni nani atakayewashitaki wateule wa Mungu? Mungu ndiye mwenye kuwahesabia haki. Ni nani atakayewahukumia adhabu? Kristo Yesu ndiye aliyekufa; naam, na zaidi ya hayo, amefufuka katika wafu, naye yuko mkono wa kuume wa Mungu; tena ndiye anayetuombea. Ni nani atakayetutenga na upendo wa Kristo? Je! Ni dhiki au shida, au adha, au njaa, au uchi, au hatari, au upanga? Kama ilivyoandikwa, ya kwamba, Kwa ajili yako tunauawa mchana kutwa, Tumehesabiwa kuwa kama kondoo wa kuchinjwa. Lakini katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda. Kwa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo, wala wenye uwezo, wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho chote hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu.”

 

2Wafalme 6:15-16 “Hata asubuhi na mapema mtumishi wake yule mtu wa Mungu alipoondoka, na kwenda nje, kumbe! Pana jeshi la watu, na farasi na magari, wameuzingira mji ule. Mtumishi wake akamwambia, Ole wetu! Bwana wangu, tufanyeje? Akamjibu, Usiogope; maana walio pamoja nasi ni wengi kuliko wale walio pamoja nao.”    

               

5.       Kumbuka kuwa tuko vitani – kila mtu wa Mungu popote alipo anapaswa kufahamu kuwa ana vita, na majungu ni sehemu ya vita hiyo, kutokana na kuwa mwema, kusema kweli, kutokupokea rushwa, na hata ustawi wako wivu unaweza kuinuka tu na watu wakaanza kupika majungu kama sehemu ya mashambulizi yako na familia yako na ustawi wako kwa sababu ya wokovu wetu na sifa zetu tulizo nazo kwa Mungu shetani atatupiga vita, vita kali sana, kwa kuwa tuko vitani kila wakati tumia sila za kiroho. Shetani anaitwa mshitaki wetu, wakati mwingine atatushitaki kwa uwongo, waliomshitaki Yesu walifanya vile kwa fitina tu

 

Mathayo 27:15-18 “Basi wakati wa siku kuu, liwali desturi yake huwafungulia mkutano mfungwa mmoja waliyemtaka. Basi palikuwa na mfungwa mashuhuri siku zile, aitwaye Baraba. Basi walipokutanika, Pilato akawaambia, Mnataka niwafungulie yupi? Yule Baraba, au Yesu aitwaye Kristo? Kwa maana alijua ya kuwa wamemtoa kwa husuda.”

 

2Wakorintho 10:3-6 “Maana ingawa tunaenenda katika mwili, hatufanyi vita kwa jinsi ya mwili; (maana silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome;) tukiangusha mawazo na kila kitu kilichoinuka, kijiinuacho juu ya elimu ya Mungu; na tukiteka nyara kila fikira ipate kumtii Kristo; tena tukiwa tayari kupatiliza maasi yote, kutii kwenu kutakapotimia.”

 

Waefeso 6:10-13 “Hatimaye, mzidi kuwa hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake. Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani. Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho.Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama.”   

 

6.       Usishiriki majungu bali uyakemee – majungu yanaambukiza hivyo yanaweza kumnasa mtu yeyote dhaifu asiye na ujuzi kuhusu neno la Mungu na asiye na akili iliyopanuka, lakini watu wakomavu wanakemea habari zozote za uvumi na uzushi, kushiriki majungu ni kushiriki matendo yasiyozaa ya giza

 

Waefeso 5:11-14 “Wala msishirikiane na matendo yasiyozaa ya giza, bali myakemee; kwa kuwa yanayotendeka kwao kwa siri, ni aibu hata kuyanena. Lakini yote yaliyokemewa hudhihirishwa na nuru maana kila kilichodhihirika ni nuru.Hivyo husema, Amka, wewe usinziaye, Ufufuke katika wafu, Na Kristo atakuangaza.”

 

Kutoka 23:1-2 “Usivumishe habari za uongo; usitie mkono wako pamoja na mwovu, kuwa shahidi wa udhalimu.Usiandamane na mkutano kutenda uovu; wala usitie ushahidi wako katika neno lo lote kwa kugeukia kando na kuandamana na mkutano ili kupotoa hukumu;”

 

7.       Kumbuka fitina inaweza kuwepo hata kanisani – Watu wengi waliookoka huwa wanaumia sana wanapofanyiwa fitina na wakristo wenzao, au kama ni mtumishi wa Mungu anapofanyiwa fitina na watumishi wenzake, hii huleta maumivu makubwa zaidi kwa sababu kila mmoja labda hutarajia majungu na fitina vitoke kwa watu wasiomjua Mungu, Lakini nakutaarifu utambue kuwa jaribu halishagui mlango wa kuingilia au kutokea linaweza kutoka hata miongoni mwa watu wa Mungu, Kanisa zuri kama lile lililokuwako Korintho washirika walikuwa na majungu na fitina kiasi hata cha kuwa na makundi kanisani

 

1Wakorintho 1:10-13 “Basi ndugu, nawasihi, kwa jina la Bwana wetu Yesu Kristo, kwamba nyote mnene mamoja; wala pasiwe kwenu faraka, bali mhitimu katika nia moja na shauri moja. Kwa maana, ndugu zangu, nimearifiwa habari zenu na wale walio wa nyumbani mwa Kloe, ya kwamba iko fitina kwenu. Basi, maana yangu ni hii, ya kwamba kila mtu wa kwenu kusema, Mimi ni wa Paulo, na, Mimi ni wa Apolo, na, Mimi ni wa Kefa, na, Mimi ni wa Kristo. Je! Kristo amegawanyika? Je! Paulo alisulibiwa kwa ajili yenu? Au je! Mlibatizwa kwa jina la Paulo?  

 

8.       Kumbuka kuwa majungu ni silaha ya shetani – Mojawapo ya silaha anayoitumia shetani kuwashambulia watu wa Mungu ni pamoja na majungu, majungu ni mashitaka ya kupikwa, Shetani alipika majungu kwaajili ya Ayubu, na pia alipika majungu kwajili ya kuhani mkuu Yoshua, ilimradi tu Mungu aondoe mkono wake kisha shetani apate sababu ya kushambulia yeye ni baba wa majungu na hivyo usishangazwe akiwatumia watu wale anaowatumia ni watoto wake, ni kazi ya shetani kuwapikia majungu watu wa Mungu, kwa hiyo kila uyaonapo hayo yakifanyika kokote kule kumbuka na ujue ni kazi za shetani, na ukimuomba Mungu atakupa ushindi dhidi ya majungu hayo.

 

Yohana 8:44 “Ninyi ni wa baba yenu, Ibilisi, na tamaa za baba yenu ndizo mpendazo kuzitenda. Yeye alikuwa mwuaji tangu mwanzo; wala hakusimama katika kweli, kwa kuwa hamna hiyo kweli ndani yake. Asemapo uongo, husema yaliyo yake mwenyewe; kwa sababu yeye ni mwongo, na baba wa huo.”

 

Ayubu 1:6-11 “Ilikuwa, siku moja ambayo hao wana wa Mungu walikwenda kujihudhurisha mbele za Bwana, Shetani naye akaenda kati yao. Bwana akamwuliza Shetani, Umetoka wapi wewe? Ndipo Shetani akamjibu Bwana, na kusema, Natoka katika kuzunguka-zunguka duniani, na katika kutembea huku na huku humo. Kisha Bwana akamwuliza Shetani, Je! Umemwangalia huyo mtumishi wangu Ayubu? Kwa kuwa hapana mmoja aliye kama yeye duniani, mtu mkamilifu na mwelekevu, mwenye kumcha Mungu na kuepukana na uovu. Ndipo Shetani akamjibu Bwana, na kusema, Je! Huyo Ayubu yuamcha Bwana bure? Wewe hukumzingira kwa ukigo pande zote, pamoja na nyumba yake, na vitu vyote alivyo navyo? Kazi za mikono yake umezibarikia, nayo mali yake imeongezeka katika nchi. Lakini nyosha mkono wako sasa, uyaguse hayo yote aliyo nayo, naye atakukufuru mbele za uso wako.”    

 

Zekaria 3:1-4 “Kisha akanionyesha Yoshua, kuhani mkuu, amesimama mbele ya malaika wa Bwana, na Shetani amesimama mkono wake wa kuume ili kushindana naye. Bwana akamwambia Shetani, Bwana na akukemee Ewe Shetani; naam, Bwana, aliyechagua Yerusalemu, na akukemee; je! Hiki si kinga kilichotolewa motoni? Basi, Yoshua alikuwa amevaa nguo chafu sana, naye alikuwa akisimama mbele ya malaika. Naye huyo akajibu, akawaambia wale waliosimama mbele yake, akisema, Mvueni nguo hizi zenye uchafu. Kisha akamwambia yeye, Tazama, nimekuondolea uovu wako, nami nitakuvika mavazi ya thamani nyingi.”

 

9.       Kumbuka Mungu anawacheka wanaofanya Majungu – Mungu anawacheka wakati wote wafanya majungu kwa sababu njia za Mungu ziko juu sana hakuna mtu anaweza kushindana na kusudi la Mungu, kwa hiyo hata kama majungu yanaonekana kana kwamba yatafanikiwa ni muhimu kufahamu kuwa Mungu atatumia njia hiyo kutokeza mlango mwingine wa mafanikio hivyo kumbuka usiogope

 

Ayubu 42:2 “Najua ya kuwa waweza kufanya mambo yote, Na ya kuwa makusudi yako hayawezi kuzuilika.”

 

Zaburi 2:1-5 “Mbona mataifa wanafanya ghasia, Na makabila wanatafakari ubatili? Wafalme wa dunia wanajipanga, Na wakuu wanafanya shauri pamoja, Juu ya Bwana, Na juu ya masihi wake.Na tuvipasue vifungo vyao, Na kuzitupia mbali nasi kamba zao.Yeye aketiye mbinguni anacheka, Bwana anawafanyia dhihaka.Ndipo atakaposema nao kwa hasira yake, Na kuwafadhaisha kwa ghadhabu yake.”

 

Na Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!

Hakuna maoni: