Filemoni 1:9-15 “lakini, kwa ajili ya
upendo nakusihi, kwa kuwa ni kama nilivyo, Paulo mzee, na sasa mfungwa wa
Kristo Yesu pia. Nakusihi kwa ajili ya mtoto wangu niliyemzaa katika vifungo
vyangu, yaani, Onesimo; ambaye zamani alikuwa hakufai, bali sasa akufaa sana,
wewe na mimi pia; niliyemtuma kwako, yeye mwenyewe, maana ni moyo wangu hasa;
ambaye mimi nalitaka akae kwangu, apate kunitumikia badala yako katika vifungo
vya Injili. Lakini sikutaka kutenda neno lo lote isipokuwa kwa shauri lako, ili
kwamba wema wako usiwe kama kwa lazima, bali kwa hiari. Maana, labda ndiyo
sababu alitengwa nawe kwa muda, ili uwe naye tena milele;”
Utangulizi:
Moja ya kitabu ambacho kinazungumzia vizuri huduma nzima ya wokovu pamoja na upatanishi ni pamoja na kitabu cha Filemoni, Katika kitabu hiki ambacho kinaunganisha watu wakuu watatu, Onesmo ambaye ni mkosaji, Filemoni aliyekosewa na Paulo mtume kama mpatanishi,Paulo mtume ambaye anasimama kama mpatanishi hapa anamtaka Filemoni amkubali Onesmo ambaye alimkosea hapo awali na sasa amejirekebisha baada ya kukutana na Yesu Kristo akiwa gerezani, somo kubwa tunalojifunza hapa ni kuwa je mtu aliyekukosea, au aliyekosea anapokuwa amejirudi, je unaendelea kumuhesabu kama mhalifu? Au utamkubali? wako baadhi ya wapendwa ambao kama mtu alikosea wakati Fulani basi wataendelea kumuhesabu kama mhalifu miaka yake yote na hawako tayari kuachana na stori za zamani kuhusu maisha ya mtu na badala yake wanatumiwa na Shetani kuendelea kugandamiza watu wa Mungu ambao maisha yao yamebadilika. Msimamo wa aina hiyo unapingana kabisa na uwezo na utendaji wa Mungu ambaye hubadilisha maisha ya watu siku hadi siku kwa kadiri watu hao wanavyokubali kujiachia katika neema ya Mungu iwezayo kubadilisha na maisha yetu sote.
1Timotheo 1:12-16 “Nami namshukuru Kristo
Yesu Bwana wetu, aliyenitia nguvu kwa sababu aliniona kuwa mwaminifu, akaniweka
katika utumishi wake; ingawa hapo kwanza nalikuwa mtukanaji, mwenye kuudhi
watu, mwenye jeuri, lakini nalipata rehema kwa kuwa nalitenda hivyo kwa ujinga,
na kwa kutokuwa na imani. Na neema ya Bwana wetu ilizidi sana, pamoja na imani
na pendo lililo katika Kristo Yesu. Ni neno la kuaminiwa, tena lastahili
kukubalika kabisa, ya kwamba Kristo Yesu alikuja ulimwenguni awaokoe wenye
dhambi; ambao wa kwanza wao ni mimi. Lakini kwa ajili hii nalipata rehema, ili
katika mimi wa kwanza, Yesu Kristo audhihirishe uvumilivu wake wote; niwe
kielelezo kwa wale watakaomwamini baadaye, wapate uzima wa milele.”
Maisha ya kiroho ni Mchakato,
ambao unahitaji uvumilivu, ikiwa ni pamoja na kuwavumilia watu ili wabadilike
na tena waokolewe na tena wakue kiroho na tena na kuwasamehe na kuamini katika
nguvu ya Damu ya Yesu yenye uwezo wa kubadilisha watu, Paulo ni mdau na mfano
wa mchakato wa mabadiliko hayo, katika kitabu cha Filemoni leo yako mambo
ya kujifunza kuhusiana na swala hilo hasa kwa mabadiliko aliyoyapata mtumwa wa
Filemoni aliyeitwa Onesmo ambaye, Mungu alimuokoa na kuyabadili maisha yake
kabisa, tutajifunza somo hili Uwezo wa kuwakubali wengine kwa kuzingatia vipengele
vinne vifuatavyo:-
·
Wajibu wa Mkristo anapokosewa
·
Kuendeleza uwezo wa kusamehe
·
Kuendeleza uwezo wa kuwakubali wengine
·
Kuendeleza uwezo wa kupenda kama Yesu
Wajibu wa Mkristo anapokosewa
Filemoni 1:10-18 “Nakusihi kwa ajili ya
mtoto wangu niliyemzaa katika vifungo vyangu, yaani, Onesimo; ambaye zamani
alikuwa hakufai, bali sasa akufaa sana, wewe na mimi pia; niliyemtuma kwako,
yeye mwenyewe, maana ni moyo wangu hasa; ambaye mimi nalitaka akae kwangu,
apate kunitumikia badala yako katika vifungo vya Injili.Lakini sikutaka kutenda
neno lo lote isipokuwa kwa shauri lako, ili kwamba wema wako usiwe kama kwa
lazima, bali kwa hiari. Maana, labda ndiyo sababu alitengwa nawe kwa muda, ili
uwe naye tena milele; tokea sasa, si kama mtumwa, bali zaidi ya mtumwa, ndugu
mpendwa; kwangu mimi sana, na kwako wewe zaidi sana, katika mwili na katika
Bwana. Basi kama ukiniona mimi kuwa mshirika nawe, mpokee huyu kama mimi
mwenyewe. Na kama amekudhulumu, au unamwia kitu, ukiandike hicho juu yangu.”
Onesmo alikuwa ni mtumwa wa
Filemoni, Nyakati za Biblia karne ya kwanza kumiliki watumwa kwa watu waliokuwa
na uchumi mkubwa lilikuwa ni swala la kawaida, na Onesmo alikuwa ni Mtumwa wa
Filemoni, Mtumwa huyu hakuwa mwaminifu na pia alikuwa hajaokoka, hivyo
alimtoroka Filemoni na kukimbia mbali huku akimwibia Filemoni na kumsababishia
hasara ya fedha nyingi katika wakati ule mtumwa alikuwa ananunuliwa kwa dinari 500, dinari moja kwa kawaida ni sawa
na Shilingi za Tanzania 8,575.29/- kwa hiyo Dinari mia 500 ni sawa na shilingi 4,287,645/- kwa hiyo licha ya fedha
alizoiba Onesmo yeye mwenyewe alikuwa ni ghali kwa kiwango cha milioni nne na
laki mbili na mia sita arobaini na tano za mwaka 1952, hukumu ya mtumwa aliyekimbia katika utawala wa Kirumi
ilikuwa ni kifo, Lakini hata hivyo mtumwa huyu aliwekwa gerezani, na kwa neema ya Mungu lilikuwa ni gereza lile
lile alilokuwa amefungwa Paulo mtume, kwa hiyo Paulo alimuhubiri Kristo kwa mfungwa
huyu na kumlea kiroho gerezani na akapokea badiliko kubwa sana, Sasa mfungwa
huyu alikuwa amepata nafasi ya kutoka na kukubali kurejea kwa Filemoni, na
ndipo Paulo anamwandikia Filemoni ili aweze kumsamehe! Je ungelikuwa ni wewe
ungeweza kumsamehe? Kukoseana ni jambo la kawaida katika maisha haya, ni ukweli
ulioko kama tu sisi nasi tunavyomkosea Mungu mara kadhaa, Lakini hata hivyo kwa
upande wa Binadamu uwezo wetu na degree (Viwango) zetu na mitazamo yetu
inatofautiana sana je Neno la Mungu
linatuelekeza nini mtu anapokukosea?
Mathayo 18:7 “Ole ni wa ulimwengu kwa
sababu ya mambo ya kukosesha! Maana hayana budi kuja mambo ya kukosesha; lakini
ole wake mtu yule aliletaye jambo la kukosesha!”
Luka 17:1-3 “Akawaambia wanafunzi wake,
Makwazo hayana budi kuja, lakini ole wake mtu yule ambaye yaja kwa sababu yake!
Ingemfaa zaidi mtu huyo jiwe la kusagia lifungwe shingoni mwake, akatupwe
baharini, kuliko kumkosesha mmojawapo wa wadogo hawa. Jilindeni; kama ndugu
yako akikosa, mwonye; akitubu msamehe.”
Biblia haiungi mkono watu
kukoseana lakini inaonya pia wale wenye kukosesha hata hivyo kwa watu wa Mungu
tunapaswa kusamehe, hatupaswi kuwa kama watu wa ulimwengu huu au wale wa jicho
kwa jicho na jino kwa jino, sisi tunapaswa kuhakikisha kuwa Mungu anatukuzwa
kwa namna yoyote ile pale watu wanapotukosea, kwa hiyo Onesmo alikuwa
amebadilika, injili ilikuwa imembadilisha na Paulo namuomba Filemoni sasa
ampokee Onesmo kwa sababu sasa amebadilika, tunajifunza kuwa tunapaswa kuwa na
Rehema na kuwakubali tena watu waliowahi kufanya makosa kana kwamba hawajawahi
kukosea kwani hivyo ndivyo Mungu anavyotufanyia na sisi pale tulipokuwa
tumewahi kumkosea
Isaya 43:25 “Mimi, naam, mimi, ndimi
niyafutaye makosa yako kwa ajili yangu mwenyewe, wala sitazikumbuka dhambi zako.”
Mathayo 5:38-41 “Mmesikia kwamba imenenwa,
Jicho kwa jicho, na jino kwa jino; Lakini mimi nawaambia, Msishindane na mtu
mwovu; lakini mtu akupigaye shavu la kuume, mgeuzie na la pili. Na mtu atakaye
kukushitaki na kuitwaa kanzu yako, mwachie na joho pia. Na mtu
atakayekulazimisha mwendo wa maili moja, nenda naye mbili.”
Jifunze kuachilia, jifunze kuwa kama Mungu, jifunze kuwakubali kwa upya watu waliokosea na wakajirekebisha, wahesabie kuwa ni wenye kufaa sana kuliko mwanzo, Paulo anaonyesha kuwa Onesmo sasa anamfaa sio tu Filemoni hata na yeye na kama isingelikuwa ni mtumwa wake huenda yeye angemchukua ili amtumikie katika vifungo vyake.
Kuendeleza uwezo wa kusamehe
Filemoni 1:10-12 “Nakusihi kwa ajili ya
mtoto wangu niliyemzaa katika vifungo vyangu, yaani, Onesimo; ambaye zamani
alikuwa hakufai, bali sasa akufaa sana, wewe na mimi pia; niliyemtuma kwako,
yeye mwenyewe, maana ni moyo wangu hasa;”
Kusamehe ni moja ya tabia ya
Kikristo, Paulo mtume hapa anaonyesha umuhimu mkubwa na uwezo wake wa kusamehe,
na kuonyesha kuwa ana moyo sio wa kusamehe tu bali wa kukubali na kuwahurumia wengine, anamuombea Msamaha
Onesmo, lakini yeye anamkubali kama mwanae aliyemzaa huko gerezani na anasema
huyu ni moyo wake hasa, kumbuka ni vigumu sana kwa wachungaji wa leo na
wakristo wa leo kumkubali mtu aliyewahi kukosea kwa kiwango kama hiki, Je
unaweza kumuita mkosaji aliyetubu na kubadilika na kusema huyu ni moyo wangu
hasa? Wakati mwingine tunakosa huruma na kuwakandamiza wengine kupitia makosa
waliyowahi kuyafanya, na kuyahubiri kwa kukandamiza ili yamkini wasikubalike
tena, wengi wetu ni kama hatuamini katika mchakato wa Mungu kubadilisha mtu
aliyekosea, ni muhimu kukumbuka kuwa damu ya Yesu Kristo iliyomwagika kwa
wokovu iko rahisi sana kumsafisha aliyeokolewa na akakosea, Mkristo aliyekomaa
kiroho ana uwezo wa kuendeleza moyo wa kusamehe na kumuhesabu mwingine kuwa
yuko sawa kama hajawahi kukosea, Onesmo hakuwa tatizo tena kwa Paulo mtume
Lakini kazi ilikuwa kwa Filemoni, je ataweza kumkubali tena mtumwa yule
aliyemuingizia hasara? Paulo kwa waraka
huu anauandaa moyo wa Filemoni kuendeleza uwezo wa kusamehe, tusiwe na uchungu
tena, tuwe na huruma na tusamehe.
Waefeso 4:31-32 “Uchungu wote na ghadhabu
na hasira na kelele na matukano yaondoke kwenu, pamoja na kila namna ya ubaya;
tena iweni wafadhili ninyi kwa ninyi, wenye huruma, mkasameheane kama na Mungu
katika Kristo alivyowasamehe ninyi.”
Kama tumeamua kumfuata Kristo,
basi ni lazima kuuiga moyo wake, yeye hakuwa mnafiki kama tulivyo leo, leo hii
unaweza hata usikaribishwe katika makanisa Fulani kwa sababu tu wana historia
yako ya nyuma kwamba uliwahi kukosea na pengine wala hawajawahi kuthibitisha
kama yalikuwa makosa hasa, pengine hata ulichafuliwa tu, lakini watu
wakakushikia bango kana kwamba wana funguo za mbinguni, dini leo zimejaa watu
wanafiki wakubwa sana ambao wamejaa ufarisayo wakimuhubiri Kristo huku
wakiwafungia watu mlango huo huo wa Yesu Kristo kwa mioyo yao mizito isiyotaka
kuachilia, Paulo Mtume alikuwa tofauti na anamshihi Filemoni ambaye pia alimzaa
kiroho na kanisa lilikuwa katika nyumba yake kwamba yeye asiwe mfano wa hao
bali ampokee Onesmo, Paulo anasema hata kama unamdai Yeye yuko tayari kulipa,
Petro alimkana Yesu mara tatu, lakini jambo la kushangaza ni kuwa Yesu
alipofufuka mtu wa kwanza kumtaja miongoni mwa wanafunzi wake ilikuwa ni Petro
tena kwa agizo la malaika
Luka 22:54-62 “Wakamkamata, wakamchukua,
wakaenda naye nyumbani kwa Kuhani Mkuu. Na Petro alimfuata kwa mbali. Na
walipokwisha washa moto katikati ya kiwanja, waliketi pamoja, naye Petro
akaketi kati yao. Ndipo mjakazi mmoja akamwona ameketi mwangani, akamkazia
macho akasema, Na huyu alikuwa pamoja naye. Akakana, akisema, Ee mwanamke,
simjui. Baadaye kitambo mtu mwingine alimwona akasema, Wewe nawe u mmoja wao.
Petro akasema, Ee mtu, si mimi. Halafu, yapata saa moja, mtu mwingine alikaza
kusema, Hakika na huyu alikuwa pamoja naye, kwa kuwa yeye pia ni Mgalilaya.
Petro akasema, Ee mtu, sijui usemalo. Na papo hapo alipokuwa katika kusema,
jogoo aliwika. Bwana akageuka akamtazama Petro. Petro akalikumbuka lile neno la
Bwana jinsi alivyomwambia, Leo kabla hajawika jogoo utanikana mara tatu.
Akatoka nje akalia kwa majonzi.”
Marko 16:6-7 “Naye akawaambia, Msistaajabu;
mnamtafuta Yesu Mnazareti, aliyesulibiwa; amefufuka; hayupo hapa; patazameni
mahali walipomweka. Lakini enendeni zenu, mkawaambie wanafunzi wake, na Petro,
ya kwamba awatangulia kwenda Galilaya; huko mtamwona, kama alivyowaambia.”
Kwa nini unadhani Yesu
aliwaagizia malaika kuwaambia wale wanawake kuwa wakawaambie wanafunzi wake na
Petro pia ingawa Petro alikuwa amemkana Yesu mara tatu? Hii inatufundisha kuwa
Yesu alimwamini Petro, alimpenda na hakuyahesabu yaliyotokea nyuma kuwa ni kitu
cha kushikilia na sasa anaenda mbali zaidi anampa majukumu ya kulisha kondoo
zake, jambo kama hili linaweza kufanywa na watu au watumishi wenye moyo mkubwa
kama wa Yesu au Paulo mtume watu waliozoezwa kusamehe wengine na kuwaamini kwa
upya!
Yohana 21:15-17 “Basi walipokwisha kula,
Yesu akamwambia Simoni Petro, Je! Simoni wa Yohana, wewe wanipenda kuliko hawa?
Akamwambia, Naam, Bwana, wewe wajua kuwa nakupenda. Akamwambia, Lisha
wana-kondoo wangu. Akamwambia tena mara ya pili, Simoni wa Yohana, wanipenda?
Akamwambia, Ndiyo, Bwana, wewe wajua kuwa nakupenda. Akamwambia, Chunga kondoo
zangu. Akamwambia mara ya tatu, Simoni wa Yohana, wanipenda? Petro alihuzunika
kwa vile alivyomwambia mara ya tatu, Wanipenda? Akamwambia, Bwana, wewe wajua
yote; wewe umetambua ya kuwa nakupenda. Yesu akamwambia, Lisha kondoo zangu.”
Maandiko yameamuru kusamehe pale
mtu anapokosea na kutubu, na ni muhimu kwetu kuwaamini tena kama Mungu
amewaamini tena wewe ni nani usiyewaamini, wakati mwingine tunaweza kukaza
shingo zetu kuwakataa kwa sababu ya wivu na uchanga wa kiroho, wako watu kwa
uchanga wao hufikiri kuwa wengine hawana mchango tena kwa mwili wa Kristo,
wanadhani kama mioyo yao ilivyo ya kifarisayo
basi na Yesu yuko hivyo hivyo, hii ni roho ya kujihesabia haki.
Wakolosai 3:12-13 “Basi, kwa kuwa mmekuwa
wateule wa Mungu, watakatifu wapendwao, jivikeni moyo wa rehema, utu wema, unyenyekevu,
upole, uvumilivu, mkichukuliana, na kusameheana, mtu akiwa na sababu ya
kumlaumu mwenzake; kama Bwana alivyowasamehe ninyi, vivyo na ninyi. Zaidi ya hayo yote jivikeni upendo, ndio
kifungo cha ukamilifu.”
Kuendeleza uwezo wa kuwakubali wengine
Filemoni 1:15-17. “Maana, labda ndiyo
sababu alitengwa nawe kwa muda, ili uwe naye tena milele; tokea sasa, si kama
mtumwa, bali zaidi ya mtumwa, ndugu mpendwa; kwangu mimi sana, na kwako wewe
zaidi sana, katika mwili na katika Bwana. Basi kama ukiniona mimi kuwa mshirika
nawe, mpokee huyu kama mimi mwenyewe.”
Wakati Onesmo alipokuwa anatoroka
alikuwa mwenye dhambi, mhalifu na mtumwa, Lakini alipokuwa anarejea sasa ni
Mtakatifu na ndugu katika Bwana ni zaidi ya mtumwa anamfaa Filemoni na anamfaa
Paulo Mtume, Paulo anamuomba Filemoni amkubali, Paulo anataka Filemoni
aendeleze uwezo wa kuwakubali wengine, Je wewe unaweza kumkubali? Mtu
aliyekosea na sasa amerudi kwako upya?
Kama wakristo tunapaswa kuwa na moyo wa kuwakubali wengine bila kujali
yaliyotokea nyuma katika historia yao, Hakuna kiwango cha kusema unamkubali
huyu na huyu unamshusha chini kidogo kwa sababu eti alikuwa hivi au vile
kumbuka mfano wa mwana mpotevu
Wagalatia 3:28-29. “Hapana Myahudi wala
Myunani. Hapana mtumwa wala huru. Hapana mtu mume wala mtu mke. Maana ninyi
nyote mmekuwa mmoja katika Kristo Yesu. Na kama ninyi ni wa Kristo, basi,
mmekuwa uzao wa Ibrahimu, na warithi sawasawa na ahadi.”
Luka 15:25-32 “Basi, yule mwanawe mkubwa
alikuwako shamba na alipokuwa akija na kuikaribia nyumba, alisikia sauti ya nyimbo
na machezo. Akaita mtumishi mmoja, akamwuliza, Mambo haya, maana yake nini?
Akamwambia, Ndugu yako amekuja, na baba yako amemchinja ndama aliyenona, kwa
sababu amempata tena, yu mzima. Akakasirika, akakataa kuingia ndani. Basi
babaye alitoka nje, akamsihi. Akamjibu baba yake, akasema, Tazama, mimi
nimekutumikia miaka mingapi hii, wala sijakosa amri yako wakati wo wote, lakini
hujanipa mimi mwana-mbuzi, nifanye furaha na rafiki zangu; lakini, alipokuja
huyu mwana wako aliyekula vitu vyako pamoja na makahaba, umemchinjia yeye ndama
aliyenona. Akamwambia, Mwanangu, wewe u pamoja nami sikuzote, na vyote nilivyo
navyo ni vyako. Tena, kufanya furaha na shangwe ilipasa, kwa kuwa huyu ndugu
yako alikuwa amekufa, naye amefufuka; alikuwa amepotea, naye ameonekana.”
Ni Imani yangu kuwa utakuwa ka ma
Paulo mtume na utakuwa kama Filemon wao bila shaka walimkubali Onesmo, lakini
kama wewe hukubali huna tofauti na yule mwana mkubwa ambaye alikasirika wakati
baba yake alipompokea mwana wake aliyekuwa amepotea, endeleza uwezo wa
kuwakubali wengine. Paulo mtume alitaka Onesmo apokelewe na Philemoni kana
kwamba Filemoni anampokea Paulo Mtume hii ni kiwango cha juu sana cha
kukubaliwa kwa Onesmo!
Kuendeleza uwezo wa kupenda kama Yesu
Filemoni 1:4-7 “Namshukuru Mungu wangu sikuzote,
nikikukumbuka katika maombi yangu; nikisikia habari za upendo wako na imani
uliyo nayo kwa Bwana Yesu na kwa watakatifu wote; ili kwamba ushirika wa imani
yako ufanye kazi yake, katika ujuzi wa kila kitu chema kilicho kwetu, katika
Kristo. Maana nalikuwa na furaha nyingi na faraja kwa sababu ya upendo wako,
kwa kuwa mioyo ya watakatifu imeburudishwa nawe, ndugu yangu.”
Filemoni 1:21 “Kwa kuwa nakuamini kutii
kwako ndiyo maana nimekuandikia, nikijua ya kuwa utafanya zaidi ya hayo
nisemayo.”
Paulo alikuwa anamfahamu Filemoni
kama lilivyo jina lake maana ya jina PHILEMON maana yake Mpendwa/Mpenzi Filemoni alikuwa
mwanafunzi wa Paulo Mtume alikuwa vizuri kiuchumi kulikuwa na Kanisa nyumbani
mwake alikuwa ni mtumishi wa Mungu alikuwa na upendo sana lakini pia alikuwa
mtii kwa Paulo mtume, kwa hiyo Paulo hakuwa na shaka juu ya agizo lake
kupokelewa na kukubalika kwa Onesmus, Filemoni alikuwa na uwezo huo, wako
watumishi hawana uwezo wa kupokea mtu aliyekosea lakini wako watumishi wenye
uwezo mkubwa wa kutokuhukumu na kuwapokea kwa mikono miwili wale waliokosea na
kuwahesabu kuwa wanastahili, tendo la aina hii linaendeleza na kukuza uwezo wa
kupenda kama Yesu Kristo, Yesu alitupenda pasipo sababu, tunapokuwa na upendo
kwa wengine bila kujali walifanya nini na historia yao ya nyuma ikoje
tunaendeleza kile ambacho Kristo alifanya kwetu, maisha ya aina hiyo ni zaidi
ya injili.
1Yohana 2:9-11“Yeye asemaye kwamba yumo nuruni, naye amchukia ndugu
yake, yumo gizani hata sasa. Yeye ampendaye ndugu yake, akaa katika nuru, wala
ndani yake hamna kikwazo. Bali yeye amchukiaye ndugu yake, yu katika giza, tena
anakwenda katika giza, wala hajui aendako, kwa sababu giza imempofusha macho.”
Ikiwa katika moyo wako kuna mtu
unamchukia basi unajiumiza mwenywe, haujiweki katika nafasi ya kufurahia
msamaha na upendo wa Mungu unabaki gizani, kwa hiyo jipime sana na jichunguze
kama uko katika upendo wa kweli na kama hauna siku nzuri na saa nzuri ya kuanza
ni sasa, anza kujenga mazoezi ya kupenda nje ya mipaka ya kawaida kama Yesu
Kristo aliagiza kuwapenda maadui zetu, iweje tushindwe kuendeleza kuwapenda
wale tu waliokosea zamani na sasa hawako kama zamani tena? Paulo alimkubali
sana Onesmo, na alikuwa anamuamini Filemoni kwamba angeliweza kabisa kubeba
agizo la waraka wake kwa kumkubali Onesmo na kumuhesabu kama ndugu
Filemoni 1:8-20 “Kwa hiyo, nijapokuwa nina ujasiri katika Kristo kukuagiza
likupasalo; lakini, kwa ajili ya upendo nakusihi, kwa kuwa ni kama nilivyo,
Paulo mzee, na sasa mfungwa wa Kristo Yesu pia. Nakusihi kwa ajili ya mtoto wangu niliyemzaa katika vifungo
vyangu, yaani, Onesimo; ambaye zamani alikuwa hakufai, bali sasa akufaa sana,
wewe na mimi pia; niliyemtuma kwako, yeye mwenyewe, maana ni moyo wangu hasa; ambaye
mimi nalitaka akae kwangu, apate kunitumikia badala yako katika vifungo vya
Injili. Lakini sikutaka kutenda neno lo lote isipokuwa kwa shauri lako, ili
kwamba wema wako usiwe kama kwa lazima, bali kwa hiari. Maana, labda ndiyo sababu
alitengwa nawe kwa muda, ili uwe naye tena milele; tokea sasa, si kama mtumwa,
bali zaidi ya mtumwa, ndugu mpendwa; kwangu mimi sana, na kwako wewe zaidi
sana, katika mwili na katika Bwana. Basi kama ukiniona mimi kuwa mshirika nawe,
mpokee huyu kama mimi mwenyewe. Na kama amekudhulumu, au unamwia kitu,
ukiandike hicho juu yangu. Mimi Paulo nimeandika kwa mkono wangu mwenyewe, mimi
nitalipa. Sikuambii kwamba nakuwia hata nafsi yako. Naam, ndugu yangu, nipate
faida kwako katika Bwana; uniburudishe moyo wangu katika Kristo.”
Na Rev. Innocent Samuel Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni