Jumapili, 13 Septemba 2026

Waraka huu ukiisha kusomwa kwenu!

 


Wakolosai 4:15-18 “Wasalimuni ndugu walioko Laodikia, na Nimfa, na kanisa lililo katika nyumba yake. Waraka huu ukiisha kusomwa kwenu fanyeni kwamba usomwe katika kanisa la Walaodikia pia; na ule wa Laodikia usomwe na ninyi. Mwambieni Arkipo, iangalie sana huduma ile uliyopewa katika Bwana, ili uitimize. Salamu yangu mimi Paulo, kwa mkono wangu mwenyewe. Kumbukeni kufungwa kwangu. Neema na iwe pamoja nanyi.”



Utangulizi:

Ni muhimu kufahamu kuwa katika nyakati hizi tulizo nazo taarifa husambaa kwa haraka sana kwa njia ya simu, mitandao ya kijamii, televisheni, redio, magazeti na kadhalika, Lakini nyakati za kanisa la Kwanza taarifa zilikuwa zinasambaa kwa kupitia nyaraka tena katika mazingira magumu sana, Paulo mtume aliyekuwa Gerezani alikuwa anataka nyaraka zake anazoziandikia kanisa zisambae kutoka katika kanisa moja na kwenda kanisa lingine kama njia ya kufikisha ujumbe wa injili na mafundisho ya Bwana, Kwa hivyo barua zilikuwa zikizunguka kutoka kanisa moja kwenda kanisa lingine, Paulo hakutaka Neno la Mungu libaki katika kanisa moja tu, badala yake alitaka ziyafikie makanisa yote, Na huu ni ujumbe muhimu sana kwa kanisa la Mungu katika nyakati zetu,Neno la Mungu halipaswi kuwa hatimiliki ya kanisa moja tu na badala yake ujumbe wa neno la Mungu unapaswa kuwafikia watu wote Ona :-

Wakolosai 4:15-18 “Wasalimuni ndugu walioko Laodikia, na Nimfa, na kanisa lililo katika nyumba yake. Waraka huu ukiisha kusomwa kwenu fanyeni kwamba usomwe katika kanisa la Walaodikia pia; na ule wa Laodikia usomwe na ninyi. Mwambieni Arkipo, Iangalie sana huduma ile uliyopewa katika Bwana, ili uitimize. Salamu yangu mimi Paulo, kwa mkono wangu mwenyewe. Kumbukeni kufungwa kwangu. Neema na iwe pamoja nanyi.”

Katika kifungu hiki cha msingi cha neno la Mungu ambacho tunajifunza leo, tunasoma maelekezo ya Paulo Mtume kwa kanisa la Kolosai kwamba waraka wao wahakikishe unasomwa katika kanisa la Laodikia na ule wa Laodikia usomwe na wao, hii inatufundisha somo muhimu sana ya kuwa Neno au ujumbe wa neno la Mungu unaotumiwa na Kanisa moja au aliopewa mtumishi wa Mungu kwaajili ya Kanisa fulani, unaweza pia kutumiwa na Kanisa lingine  kwa makusudi ya kujengana, kutiana moyo, kuhudumia mwili wa Kristo na  kwaajili ya shughuli za kimaongozi, kwa kufanya hivi kanisa litakuwa na umoja na litahitimu katika nia moja.

Waraka wa Kolosai unaweza kusomwa na Laodikia na ule wa Laodikia unaweza kusomwa Kolosai, hii inatufundisha wazi kuwa nyakati za kanisa la kwanza nyaraka za Paulo Mtume na huenda hata na za mitume wengine zilisomwa vilevile katika makanisa mengine na hivyo ufunuo wa hekima wa neno la Mungu  na miongozo mbalimbali ingeweza kuwa na faida na kusaidia kanisa lingine. Na sio hivyo tu mafundisho ya mitume yangelisaidia Kanisa ulimwenguni kote kujenga umoja wa kikanisa na ushirikiano, hii haitofautiani hata kidogo na swala la Paulo mtume kumuagiza Timotheo kuhubiri kile alichokisikia kwake na kuwakabidhi watu waaminifu watakaofaa kuwafundisha wengine:-

2Timotheo 2:2 “Na mambo yale uliyoyasikia kwangu mbele ya mashahidi wengi, hayo uwakabidhi watu waaminifu watakaofaa kuwafundisha na wengine.”

Kwa msingi huo tunajifunza hapa kwamba waraka yaani ujumbe wa Mungu wa kanisa “A” unaweza pia kusomwa “Kuhubiriwa” na Kanisa “B” na ule wa Kanisa “B” ukasomwa  “Kuhubiriwa” na Kanisa “A”, Mungu anapomtumia mtumishi wake kuleta ujumbe kwa Kanisa lake la mahali pamoja, ujumbe huo, huweza kuwafaa watu wa Kanisa lingine, hiki ndicho tunachojifunza kutokana na maelekezo ya Paulo mtume, Jambo kubwa la msingi ni mtumishi wa Mungu kukaa katika hali ya maombi na kuutafasiri ujumbe anaojifunza kutoka kwa wengine katika mazingira ya watu wa Kanisa lake, kwa utulivu huku ukimpa nafasi Roho Mtakatifu kwa sababu yeye ndiye Mwalimu wetu Mkuu.

Na jambo hili linafaa zaidi kama Kanisa au watu wa mahali hapo wanapitia changamoto zinazofanana kama ilivyokuwa kwa Kolosai na Laodikia, aidha inaweza kuwa vema kufanya hivyo kwa sababu sio kila mtu anaweza kuwa mpishi hata kama wote ni familia moja na tunakaa katika nyumba moja, Mungu amewapa neema wengine kuwa na uwezo wa kuandaa jumbe kutokana na mazingira ya utulivu waliyo nayo au karama ya ualimu waliyo nayo na mwingine anaruhusiwa kutumia ikiwa ataona vyema kufanya hivyo na kama itampendeza Roho Mtakatifu kwani Roho Mtakatifu ni mmoja pia. Kufanya hivyo sio kufanya wizi wa kitaarifa “Plagiarism” kwani ujumbe wa Mungu sio taarifa bali ni mafundisho kwa kanisa lote. Kwa sababu hiyo Leo tutachukua muda kujifunza na kutafakari ujumbe wa somo hili lenye kichwa “Waraka huu ukiisha kusomwa kwenu!” kwa kuzingatia vipengele vitatu vofuatavyo:-

·         Waraka huu ukiisha kusomwa kwenu!

·         Fanyeni kwamba usomwe katika kanisa lingine.

·         Faida ya kushirikishana ujumbe wa neno la Mungu.

Waraka huu ukiisha kusomwa kwenu!

Ni muhimu kufahamu kuwa katika Barua yake kwa Wakolosai, Paulo mtume anawapa maagizo ya wazi kuhusu kushirikiana waraka wake na Kanisa lingine la Laodikia. Maagizo haya yanatufundisha  na kutuonyesha umuhimu wa kushirikiana ujumbe wa neno la Mungu na makanisa mengine tofauti tofauti, kwani ujumbe huo una umuhimu wa kipekee kwa Kanisa linapokuja swala la kushirikiana na kuhubiri neno la Mungu, Kanisa ni mwili wa Kristo na kwa sababu hiyo uko umuhimu wa kuhudumiana na ndivyo neno la Mungu linavyoagiza.

1Petro 4:10-11 “kila mmoja kwa kadiri alivyoipokea karama, itumieni kwa kuhudumiana; kama mawakili wema wa neema mbalimbali za Mungu. Mtu akisema, na aseme kama mausia ya Mungu; mtu akihudumu, na ahudumu kwa nguvu anazojaliwa na Mungu; ili Mungu atukuzwe katika mambo yote kwa Yesu Kristo. Utukufu na uweza una yeye hata milele na milele. Amina.”

Wakolosai, Walaodikia na Hierapoli yalikuwa ni makanisa yaliyoanzishwa na Epafra katika Asia ndogo, Epafra ni moja ya watumishi wa Mungu anayetajwa katika waraka wa Wakolosai na Filemoni, alikuwa ni muhubiri wa injili aliyekuwa na umuhimu mkubwa sana katika Kanisa la Kolosai na ni wazi kuwa alihusika kulianzisha Kanisa hilo pamoja na mengine yaliyokuwa Asia na alikuwa akiwaombea sana Wakolosai, Walaodikia na Hierapoli, Lakini pia alikuwa ni mtendakazi wa karibu sana wa Paulo mtume na waliwahi kufungwa pamoja naye gerezani kwaajili ya injili. Ona:-

Wakolosai 4:12-13 “Epafra, aliye mtu wa kwenu, mtumwa wa Yesu Kristo, awasalimu, akifanya bidii siku zote kwa ajili yenu katika maombi yake, ili kwamba msimame wakamilifu na kuthibitika sana katika mapenzi yote ya Mungu. Maana namshuhudia kwamba ana juhudi nyingi kwa ajili yenu, na kwa ajili ya hao walioko Laodikia, na kwa ajili ya hao walioko Hierapoli.”

Filemoni 1:23 “Na pamoja na hayo uniwekee tayari mahali pa kukaa; maana nataraji ya kwamba kwa maombi yenu mtajaliwa kunipata. Epafra, aliyefungwa pamoja nami katika Kristo Yesu, akusalimu;”

Paulo Mtume akiwa na Epafra anaandika waraka kwa Wakolosai na huenda aliandika na waraka mwingine kwa kanisa la Laodikia ambao kwa bahati mbaya hauko katika Biblia yetu leo au inawezekana ulipotea lakini anawaagiza Wakolosai kuwa waraka aliowaandikia wakiisha kuusoma wahakikishe unasomwa na watu wa Laodikia na ule wa Laodikia usomwe pia na Wakolosai, kwa nini Paulo anatoa agizo hili?

1.       Paulo alitaka watu washirikiane kweli ya injili  - Alifahamu kuwa ujumbe wake wa injili ulikuwa na umuhimu mkubwa kwa ulimwengu mzima, alikuwa anatambua kuwa Kanisa ni mwili mmoja na kwa vile waraka wake kwa Wakolosai ulikuwa na mafundisho ya msingi kumuhusu Yesu kama kichwa cha Kanisa na kweli kuhusu wokovu alitamani waraka huo huo ufike Laodikia ili kwamba mafundisho yake yaweze kuwafikiwa wakristo wengi Duniani na wote wajengwe kuwa na imani moja, Paulo alifahamu kuwa neno la Mungu lina pumzi ya Mungu na kwa sababu hiyo linafaa kwa mafundisho sio ya kanisa fulani tu  kla mahali pamoja bali na makanisa mengine:-

 

2Timotheo 3:14-17 “Bali wewe ukae katika mambo yale uliyofundishwa na kuhakikishwa, kwa maana unajua ni akina nani ambao ulijifunza kwao; na ya kuwa tangu utoto umeyajua maandiko matakatifu, ambayo yaweza kukuhekimisha hata upate wokovu kwa imani iliyo katika Kristo Yesu. Kila andiko, lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki; ili mtu wa Mungu awe kamili, amekamilishwa apate kutenda kila tendo jema.”

 

2.       Paulo mtume alitaka makanisa yote yakabiliane na mafundisho ya uongo – Makanisa yote ya Kolosai na Laodikia yalikuwa yakikabiliwa na changamoto ya mafundisho ya uongo yakiwemo yale ya Kiyahudi yanayochanganya kweli ya injili na sheria za kiyahudi (Jewish legalism) na mafundisho ya “Gnosticism” waliokazia kuwa dhambi ni ujinga na wokovu unaletwa na ufahamu au maarifa, aidha pia watu walikuwa wakifundisha maono na ndoto ambazo kimsingi hazikuwa kweli ya neno la Mungu,Walifundisha kushika sabato, kuandama mwezi na baadhi ya maswala ya sheria tofauti na kweli ya injili, Yalikuweko pia mafundisho yahusuyo kuutesa mwili, msishike, msiguse wala msionje (Asceticism) Paulo alitaka makanisa yote yapokee mafundisho safi na ya kweli yanayomzingatia Kristo, sio hivyo tu Mitume walitaka mafundisho yao yaenezwe katika makanisa yote na watu wayashike, na kama mtu haleti mafundisho hayo waliagiza asikaribishwe, wala wasitamani kula naye maana kufanya hivyo ni kuunga mkono mafundisho potofu. Adui wa Kolosai alikuwa ndiye adui wa Laodikia kwa hiyo kwa kushirikiana nyaraka za kitume makanisa yote yangeimarika kwa fundisho sahihi.

 

Wakolosai 2:16-19 “Basi, mtu asiwahukumu ninyi katika vyakula au vinywaji, au kwa sababu ya sikukuu au mwandamo wa mwezi, au sabato; mambo hayo ni kivuli cha mambo yajayo; bali mwili ni wa Kristo. Mtu asiwanyang'anye thawabu yenu, kwa kunyenyekea kwa mapenzi yake mwenyewe tu, na kuabudu malaika, akijitia katika maono yake na kujivuna bure, kwa akili zake za kimwili; wala hakishiki Kichwa, ambacho kwa yeye mwili wote ukiruzukiwa na kuungamanishwa kwa viungo na mishipa, hukua kwa maongeo yatokayo kwa Mungu.”      

 

2Yohana 1:7-10 “Kwa maana wadanganyifu wengi wametokea duniani, wasiokiri ya kuwa Yesu Kristo yuaja katika mwili. Huyo ndiye yule mdanganyifu na mpinga Kristo. Jiangalieni nafsi zenu msiyapoteze mliyoyatenda, bali mpokee thawabu timilifu.Kila apitaye cheo, wala asidumu katika mafundisho ya Kristo, yeye hana Mungu. Yeye adumuye katika mafundisho hayo, huyo ana Baba na Mwana pia. Mtu akija kwenu, naye haleti mafundisho hayo, msimkaribishe nyumbani mwenu, wala msimpe salamu.”

 

3.       Paulo alitaka kanisa linie mamoja Kanisa ni mwili mmoja – Ingawa Kanisa la Kolosai na Laodikia yalikuwa katika sehemu tofauti au miji mbalimbali tofauti kushirikiana kwao nyaraka au mafundisho ya mtume kulimaanisha kuwa Kanisa ni mwili mmoja, Paulo alilenga kuyafanya makanisa haya kuwa ndugu na kutaka kuimarisha uhusiano katika ya kanisa moja na jingine kwa hiyo kushirikiana mafundisho halikuwa jambo baya, Biblia inapoelezea kuwa Kanisa ni mwili mmoja bado pia inaelezea ya kuwa lina viungo vingi, kwa maana hiyo ingawa Kanisa ni moja lakini lina karama na utendaji tofauti tofauti, lakini ingawa mwili ni mmoja  na una viungo vingi hiyo haimaanishi kwamba mwili unaweza kula chakula tofauti tofauti kwaajili ya kila kiungo, chakula ni kimoja, kwa hiyo Kanisa ni moja na utendaji ni tofauti, tunaujenga mwili ule ule!

 

1Wakorintho 12:12-27 “Maana kama vile mwili ni mmoja, nao una viungo vingi, na viungo vyote vya mwili ule, navyo ni vingi, ni mwili mmoja; vivyo hivyo na Kristo.Kwa maana katika Roho mmoja sisi sote tulibatizwa kuwa mwili mmoja, kwamba tu Wayahudi, au kwamba tu Wayunani; ikiwa tu watumwa au ikiwa tu huru; nasi sote tulinyweshwa Roho mmoja.Kwa maana mwili si kiungo kimoja, bali ni vingi. Mguu ukisema, Kwa kuwa mimi si mkono, mimi si wa mwili; je! Si wa mwili kwa sababu hiyo? Na sikio likisema, Kwa kuwa mimi si jicho, mimi si la mwili; je! Si la mwili kwa sababu hiyo? Kama mwili wote ukiwa jicho, ku wapi kusikia? Kama wote ni sikio ku wapi kunusa? Bali Mungu amevitia viungo kila kimoja katika mwili kama alivyotaka. Lakini kama vyote vingekuwa kiungo kimoja, mwili ungekuwa wapi? Lakini sasa viungo ni vingi, ila mwili ni mmoja. Na jicho haliwezi kuuambia mkono, Sina haja na wewe; wala tena kichwa hakiwezi kuiambia miguu, Sina haja na ninyi. Bali zaidi sana vile viungo vya mwili vidhaniwavyo kuwa vinyonge zaidi vyahitajiwa zaidi. Na vile viungo vya mwili vidhaniwavyo kuwa havina heshima, viungo vile twavipa heshima zaidi; na viungo vyetu visivyo na uzuri vina uzuri zaidi sana. Kwa maana viungo vyetu vilivyo na uzuri havina uhitaji; bali Mungu ameuungamanisha mwili, na kukipa heshima zaidi kile kiungo kilichopungukiwa; ili kusiwe na faraka katika mwili, bali viungo vitunzane kila kiungo na mwenziwe. Na kiungo kimoja kikiumia, viungo vyote huumia nacho, na kiungo kimoja kikitukuzwa, viungo vyote hufurahi pamoja nacho. Basi ninyi mmekuwa mwili wa Kristo, na viungo kila kimoja peke yake.”

 

4.       Paulo Mtume alitaka kuweka sawa mtazamo wa kitheolojia kuhusu ubora wa Kristo – Nyaraka yake ilikuwa inabeba mtazamo sahihi wa ubora wa Yesu Kristo na sadaka yake ya upatanisho aliyoitoa msalabani, Paulo anamuelezea Yesu Kristo kwa mtazamo wa juu sana akionyesha kuwa Yeye ni Muumba wa vitu vyote na kuwa katika yeye unakaa utimilifu wote wa Mungu na kwa sababu hiyo alitaka ujumbe huu ueleweke wazi kwa makanisa yote ambayo kimsingi yalikuwa yanashirikiana eneo moja la kijiografia na hivyo ilikuwa ni wazi kuwa mafundisho yanayoshusha heshima ya Kristo yangeweza kuyaathiri makanisa yote mawili na zaidi hivyo kubadilishana nyaraka kungelifanya wawe na msimamo mmoja  na kauli moja na uhakika kutoka kwa mtume

 

Wakolosai 1:15-20 “naye ni mfano wa Mungu asiyeonekana, mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote. Kwa kuwa katika yeye vitu vyote viliumbwa, vilivyo mbinguni na vilivyo juu ya nchi, vinavyoonekana na visivyoonekana; ikiwa ni vitu vya enzi, au usultani, au enzi, au mamlaka; vitu vyote viliumbwa kwa njia yake, na kwa ajili yake. Naye amekuwako kabla ya vitu vyote, na vitu vyote hushikana katika yeye. Naye ndiye kichwa cha mwili, yaani, cha kanisa; naye ni mwanzo, ni mzaliwa wa kwanza katika wafu, ili kwamba awe mtangulizi katika yote. Kwa kuwa katika yeye ilipendeza utimilifu wote ukae; na kwa yeye kuvipatanisha vitu vyote na nafsi yake akiisha kufanya amani kwa damu ya msalaba wake; kwa yeye, ikiwa ni vitu vilivyo juu ya nchi, au vilivyo mbinguni.”

 

Wakolosai 2:13-15 “Na ninyi mlipokuwa mmekufa kwa sababu ya makosa yenu na kutokutahiriwa kwa mwili wenu, aliwafanya hai pamoja naye, akiisha kutusamehe makosa yote; akiisha kuifuta ile hati iliyoandikwa ya kutushitaki kwa hukumu zake, iliyokuwa na uadui kwetu; akaiondoa isiwepo tena, akaigongomea msalabani; akiisha kuzivua enzi na mamlaka, na kuzifanya kuwa mkogo kwa ujasiri, akizishangilia katika msalaba huo.               

 

5.       Paulo alikuwa na ufahamu kuwa ujumbe anaouandika haukuwa kwaajili ya kanisa la mahali pamoja tu, ulikuwa pia kwaajili ya sehemu nyingine, Hakuna kanisa ambalo linaweza kudai kuwa fundisho walilonalo ni la kwao peke yao, wala muhubiri mmoja kudhani kuwa ujumbe anaopewa na Roho Mtakatifu ni wa kwake tu, Nataka nikuhakikishie kuna wachoyo wengi sana wana jumbe hawaandiki, wala hawazirushi katika mitandao ya kijamii kwa sababu wanadhani ni za kwao tu na za kanisa lake la mahali pamoja au wanataka kuzifanyia biashara “you cant monopolize the Gospel as if it belongs  you alone” “huwezi kuhodhi injili kana kwamba ni mali yako pekee” Mungu hajakuita kwaajili ya kanisa la mahali pamoja tu sidhani kama uko wito wa namna hiyo Mungu ametuita kwaajili ya mataifa yote, unaporejea kwenye kanisa lako la mahali pamoja umerudi tu kwenye nyumba yako, au kituo chako cha nyumbani lakini linapokluja swala la injili sio ya mahali pamoja ni ya dunia nzima. Pailo mtume alikuwa anafahamu asili ya witio wake kuwa jni wito kwa mataifa yote, na agizo kuu pia limeagiza kwamba injili ihubiriwe ulimwenguni kote enendendi ulimwenguni kote!

 

Matendo 9:15-16. “Lakini Bwana akamwambia, Nenda tu; kwa maana huyu ni chombo kiteule kwangu, alichukue Jina langu mbele ya Mataifa, na wafalme, na wana wa Israeli. Maana nitamwonyesha yalivyo mengi yatakayompasa kuteswa kwa ajili ya Jina langu.”

 

Warumi 11:13 “Lakini nasema na ninyi, mlio watu wa Mataifa. Basi, kwa kadiri nilivyo mtume wa watu wa Mataifa, naitukuza huduma iliyo yangu, nipate kuwatia wivu walio damu moja na mimi na kuwaokoa baadhi yao.”

 

Wagalatia 1:15-16 “Lakini Mungu, aliyenitenga tangu tumboni mwa mama yangu, akaniita kwa neema yake, alipoona vema kumdhihirisha Mwanawe ndani yangu, ili niwahubiri Mataifa habari zake; mara sikufanya shauri na watu wenye mwili na damu;”     

 

Mwanzo 12:1-3 “BWANA akamwambia Abramu, Toka wewe katika nchi yako, na jamaa zako, na nyumba ya baba yako, uende mpaka nchi nitakayokuonyesha; nami nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa, na kukubariki, na kulikuza jina lako; nawe uwe baraka;nami nitawabariki wakubarikio, naye akulaaniye nitamlaani; na katika wewe jamaa zote za dunia watabarikiwa.”

 

Unaona Mungu anapomuita mtumishi wake hamuiti kwaajili ya kanisa la mahali pamoja tu, kujidhania kuwa umeitwa kwaajili ya sehemu moja tu ni kosa la kiufundi, wewe ni sauti ya Mungu kutoka pale ulipo kuelekea kila mahali ulimwenguni, Mungu aliponiita mimi katika huduma hii, aliniambia nitakufanya kuwa fundi mkuu utatengeneza matofali, kisha utawapa watu wataijenga nyumba yangu kila mahali ulimwenguni, ndio maana ya mkuu wa wajenzi, tunaujenga mwili wa Kristo, mtu akitumia jumbe zangu nafurahi sana kwa sababu kile ambacho Mungu amenipa kinaenea duniani kote, na haya ndio mapenzi ya Mungu, na tangu nimeanza kufanya hivyo sijawahi kupungukiwa na jumbe, Roho Mtakatifu amekuwa mwaminifu akinipa Jumbe kila wakati kwaajili yenu,  kwaajili ya mwili wa Kristo, zitumieni kama Bwana anavyowaongoza, sijisikii vibaya watu wakihudumu na kuhubiri jumbe zangu kwa sababu zimekuwa Baraka kubwa kila mahali ulimwenguni, zinawafikia watu Msumbiji, Kongo, Kenya, Rwanda, Burundi, Marekani, Tanzania na maeneo mbalimbali na hii ni furaha yangu! Na kama wewe unavyobarikiwa na kushangaa, na mimi baada ya kumaliza kuandaa, huwa nabarikiwa na ninashangaa, kwamba hivi mimi nawezaje kuwa natengeneza jumbe kali namna hii sio mimi ni Roho wa Mungu! Utukufu ni wake!

Fanyeni kwamba usomwe katika kanisa lingine.

Kimsingi neno la Mungu linaonyesha kuwa sio dhambi kwa watumishi wa Mungu kushirikishana mafundisho, Neno la Mungu linaonyesha kuwa mafundisho yanapokelewa, yanahifadhiwa, na yanapitishwa kutoka kizazi kimoja hata kizazi kingine na kwa sababu hiyo tunajifunza kwamba sio dhambi kufundisha kile ulichofundishwa na ukawafundisha watu wengine!

2Timotheo 2:2 “Na mambo yale uliyoyasikia kwangu mbele ya mashahidi wengi, hayo uwakabidhi watu waaminifu watakaofaa kuwafundisha na wengine.”

Kila mtumishi wa Mungu ana wajibika kutunza maudhui sahihi ya mafundisho au maneno aliyoyasikia au kuyasoma kutoka kwa wale waliojaliwa kuandika neno la Mungu, kufundisha kwa usahihi na kwa uaminifu  kile ulichojifunza kutoka kwa wale unaowaamini au wale wenye imani moja na wewe, Mungu anachokitaka ni ile kweli ilindwe, wakati huo huo tusiache kusoma na kuchimba maandiko na kujiachia mbele za Roho Mtakatifu ili tuweze kupokea ufunuo sahihi unaoendana sawa na neno la Mungu, tunatofautiana neema, mtazamo na uzoefu na karama au vipawa kwa hiyo kila mmoja atafanya kwa kadiri ya neema aliyopewa, Kabla ya kuandika injili yake Luka alikuwa amesoma injili zilizotangulia kuandikwa na nyingine, kama injili ya Marko na Mathayo, hivyo yeye naye aliamua kuandika kwa jinsi yake japokuwa injili zote zina lengo lile lile la kuelezea maisha na mafundisho ya Bwana, Marko, Mathayo na Luka zinaitwa injili zinazofanana. “Synoptic Gospel” Lakini zikiwa na lengo moja, hata hivyo Luka anaandika katika namna inayovutia zaidi na alifanya hivyo baada ya kufanya utafiti wa kutosha ona:-

Luka 1:1-4 “Kwa kuwa watu wengi wametia mikono kutunga kwa taratibu habari za mambo yale yaliyotimizwa katikati yetu, kama walivyotuhadithia wale waliokuwa mashahidi wenye kuyaona, na watumishi wa lile neno tokea mwanzo, nimeona vema mimi nami, kwa kuwa nimejitafutia usahihi wa mambo hayo yote tangu mwanzo, kukuandikia kwa taratibu, Theofilo mtukufu,upate kujua hakika ya mambo yale uliyofundishwa.”

Unaona Mathayo, Marko, Luka na hata Yohana wote wanaandika habari za Yesu Kristo mafundisho yake na matendo yake lakini kila mmoja akiwa na kionjo tofauti kwa aina yake,  basi tuupeleke ujumbe wa injili kwa watu wote kwa kadiri ya neema ya Mungu kila mtu kwa kionjo chake lakini lengo likiwa moja kujenga mwili wa Yesu yaani kanisa.

Paulo anachoagiza sasa anataka makanisa yote yashirikiane neno la Mungu, Mungu anaweza kuzungumza na Kanisa lake kupitia ujumbe mmoja, Kanisa la Kolosai na Laodikia walipaswa kushirikiana neno la Mungu lakini pia walifanya hivyo kwa makanisa mengine, ushirikiano wa neno la Mungu ulipunguza gharama, ulisaidia kuwa na sauti ya umoja, kujilinda na mafundisho ya uongo, Kanisa kuwa na fundisho lililo sahihi kwa pamoja, kwa hiyo Kanisa la Kolosai linapokea Waraka wa Paulo na kanisa la Laodikia linapokea waraka wa Paulo, Kisha Laodikia wanawashirikisha Kolosai na Kolosai wanawashirikisha Laodikia, wote wanapata kopi na wote wanakuwa salama, huu ndio mpango na makusudi ya Mungu. 

Wakolosai 4:15-18 “Wasalimuni ndugu walioko Laodikia, na Nimfa, na kanisa lililo katika nyumba yake. Waraka huu ukiisha kusomwa kwenu fanyeni kwamba usomwe katika kanisa la Walaodikia pia; na ule wa Laodikia usomwe na ninyi. Mwambieni Arkipo, iangalie sana huduma ile uliyopewa katika Bwana, ili uitimize. Salamu yangu mimi Paulo, kwa mkono wangu mwenyewe. Kumbukeni kufungwa kwangu. Neema na iwe pamoja nanyi.”

Faida ya kushirikishana ujumbe wa neno la Mungu.

Wakristo wanaposhirikiana neno la Mungu kuna faida kadhaa zinajitokeza katika mwili wa Kristo zinaweza kuwepo faida nyingi sana lakini kikubwa wote tunahitimu katika nia moja na kunena mamoja, kukuza imani yetu pamoja, kukua kiroho pamoja, kujilinda katika imani kwa pamoja na kutokutofautiana kwa kiwango kikubwa kati ya Kanisa moja na lingine, kimisimamo na kimafundisho.

1Wakorintho 1:10-13. “Basi ndugu, nawasihi, kwa jina la Bwana wetu Yesu Kristo, kwamba nyote mnene mamoja; wala pasiwe kwenu faraka, bali mhitimu katika nia moja na shauri moja. Kwa maana, ndugu zangu, nimearifiwa habari zenu na wale walio wa nyumbani mwa Kloe, ya kwamba iko fitina kwenu. Basi, maana yangu ni hii, ya kwamba kila mtu wa kwenu kusema, Mimi ni wa Paulo, na, Mimi ni wa Apolo, na, Mimi ni wa Kefa, na, Mimi ni wa Kristo. Je! Kristo amegawanyika? Je! Paulo alisulibiwa kwa ajili yenu? Au je! Mlibatizwa kwa jina la Paulo?

1Petro 2:2-5 “Kama watoto wachanga waliozaliwa sasa yatamanini maziwa ya akili yasiyoghoshiwa, ili kwa hayo mpate kuukulia wokovu; ikiwa mmeonja ya kwamba Bwana ni mwenye fadhili. Mmwendee yeye, jiwe lililo hai, lililokataliwa na wanadamu, bali kwa Mungu ni teule, lenye heshima. Ninyi nanyi, kama mawe yaliyo hai, mmejengwa mwe nyumba ya Roho, ukuhani mtakatifu, mtoe dhabihu za roho, zinazokubaliwa na Mungu, kwa njia ya Yesu Kristo.”

Wakolosai 1:26-28 “siri ile iliyofichwa tangu zamani zote na tangu vizazi vyote, bali sasa imefunuliwa kwa watakatifu wake; ambao Mungu alipenda kuwajulisha jinsi ulivyo utajiri wa utukufu wa siri hii katika Mataifa, nao ni Kristo ndani yenu, tumaini la utukufu ambaye sisi tunamhubiri habari zake tukimwonya kila mtu, na kumfundisha kila mtu katika hekima yote, tupate kumleta kila mtu mtimilifu katika Kristo”.

Ukiacha kuhitimu katika nia moja, kuukulia wokovu kwa viwango vinavyoendana, kuwa watumilifu kama Kristo, vile vile Kanisa tunaweza kujihami na mafundisho ya uongo yanayoingia kwa kasi hususani katika nyakati hizi za mwisho, Kanisa la Kolosai liliingiliwa na mafundisho ya uongo ambayo kama wao walitahadharishwa ingelikuwa rahisi kwa Kanisa la Laodikia pia kuchukua tahadhari mapema kabla hayajawakuta.

Wakolosai 2:6-8 “Basi kama mlivyompokea Kristo Yesu, Bwana, enendeni vivyo hivyo katika yeye; wenye shina na wenye kujengwa katika yeye; mmefanywa imara kwa imani, kama mlivyofundishwa; mkizidi kutoa shukrani. Angalieni mtu asiwafanye mateka kwa elimu yake ya bure na madanganyo matupu, kwa jinsi ya mapokeo ya wanadamu, kwa jinsi ya mafundisho ya awali ya ulimwengu, wala si kwa jinsi ya Kristo. Maana katika yeye unakaa utimilifu wote wa Mungu, kwa jinsi ya kimwili.”

Unaona kwa tahadhari kama hii basi uongo unadhibitiwa mapema, wakristo wanaweza kushauriana na kutiana moyo, na umoja wa makanisa unaimarika na mwili wa Kristo unajengwa

Inarahisisha kuenea kwa injili, Paulo mtume alikuwa kizuizini, alikuwa amefungwa lakini neno la Mungu halifungwi, Paulo angeliweza kama mtume kuufikisha ujumbe katika makanisa hata bila yaye ye kufika  na injili ingeenea na ingeenea kwa usahihi, injili inawafikia watu wengi zaidi, kila Kanisa linafanyika kituo cha injili, Kanisa linaimarika, makanisa yanazaliwa, imani inajengwa, Paulo alitambua ya kuwa ana kitu na kitu hicho kinatakiwa kuwafikia watu wengi, akiwa amefungwa angewezaje kuufikisha ujumbe ni kwa kuandika, kuishirikisha injili kila mahali ni agizo la Kristo

Marko 16:15-16 “Akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa.”

1Petro 3:15 “Mwe tayari siku zote kumjibu kila mtu awaulizaye habari za tumaini lililo ndani yenu; lakini kwa upole na kwa hofu.”

Warumi 1:1-6 “Paulo, mtumwa wa Kristo Yesu, aliyeitwa kuwa mtume, na kutengwa aihubiri Injili ya Mungu;ambayo Mungu amekwisha kuiahidi kwa kinywa cha manabii wake katika maandiko matakatifu; yaani, habari za Mwanawe, aliyezaliwa katika ukoo wa Daudi kwa jinsi ya mwili,na kudhihirishwa kwa uweza kuwa Mwana wa Mungu, kwa jinsi ya roho ya utakatifu, kwa ufufuo wa wafu, Yesu Kristo Bwana wetu; ambaye katika yeye tulipokea neema na utume ili mataifa yote wapate kujitiisha kwa imani, kwa ajili ya jina lake; ambao katika hao ninyi mmekuwa wateule wa Yesu Kristo;”

Hitimisho:

Kwa hiyo tunajifunza ya kuwa nyakati za Kanisa la Kwanza mitume walishirikisha watu wote neno la Mungu na mafundisho yao, baadae nyaraka hizo zilikuswanywa pamoja na kufanyika neno la Mungu yaani Biblia tuliyo nayo, hata hivyo Biblia inahitaji utaalamu kuitafasiri na sio watu wote wanaweza lakini wale walioitwa kuwa walimu wanaweza kufanya huduma yao kwa bidii na kuwasaidia wakristo kuifahamu kweli ya neno la Mungu kwa jumbe zao, kwa hiyo ni vema ujumbe huu ukawafikia makanisa yote endapo utabaini kuwa unaweza kuwasaidia na jumbe nyinginezo zote, waraka huu ukiisha kusomwa kwenu, fanyeni kwamba usomwe katika Kanisa lingine na faida yake utaiona Bwana atupe neema, kumfundisha kila mtu neno la Mungu ili injili iweze kuwafikia watu wote kwa utukufu wa Mungu Baba mwenyewe

Warumi 12:4-8 “Kwa kuwa kama vile katika mwili mmoja tuna viungo vingi, wala viungo vyote havitendi kazi moja; Vivyo hivyo na sisi tulio wengi tu mwili mmoja katika Kristo, na viungo, kila mmoja kwa mwenzake. Basi kwa kuwa tuna karama zilizo mbalimbali, kwa kadiri ya neema mliyopewa; ikiwa unabii, tutoe unabii kwa kadiri ya imani; ikiwa huduma, tuwemo katika huduma yetu; mwenye kufundisha, katika kufundisha kwake; mwenye kuonya, katika kuonya kwake; mwenye kukirimu, kwa moyo mweupe; mwenye kusimamia kwa bidii mwenye kurehemu, kwa furaha.”

Wakolosai 4:16-18. “Waraka huu ukiisha kusomwa kwenu fanyeni kwamba usomwe katika kanisa la Walaodikia pia; na ule wa Laodikia usomwe na ninyi.Mwambieni Arkipo, Iangalie sana huduma ile uliyopewa katika Bwana, ili uitimize. Salamu yangu mimi Paulo, kwa mkono wangu mwenyewe. Kumbukeni kufungwa kwangu. Neema na iwe pamoja nanyi.”                

Na Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye hekima

Hakuna maoni: