Ijumaa, 15 Novemba 2024

Je ni kwa sababu Hakuna Mungu Katika Israel?


2Wafalme 1:2-4 “Na Ahazia akaanguka katika dirisha la chumba chake orofani, katika Samaria, akaugua; akatuma wajumbe, akawaambia, Enendeni mkaulize kwa Baal-zebubu, mungu wa Ekroni, kwamba nitapona ugonjwa huu. Lakini malaika wa Bwana akamwambia Eliya Mtishbi, Ondoka, uende ukaonane na wale wajumbe wa mfalme wa Samaria, ukawaambie, Je! Ni kwa sababu hapana Mungu katika Israeli, hata mnakwenda kuuliza kwa Baal-zebubu, mungu wa Ekroni? Basi sasa, Bwana asema hivi, Hutashuka katika kile kitanda ulichokipanda, bali hakika utakufa. Eliya akaondoka.”



Utangulizi:

Wakati wa Ahazia Mfalme wa Israel alipougua alituma wajumbe kwenda kuuliza kwa miungu ya kikanaani kwa habari ya afya yake badala ya kuuliza kutoka kwa Mungu wa Israel, Tukio hilo lilimuudhi sana Mungu na malaika wa Bwana alimtuma Eliya Nabii kwenda kumuonya mfalme huyo kwa swali kali na kwa kumkemea na kumpa jibu kutoka kwa Mungu; Je ni kwa sababu hakuna Mungu katika Israel, hata mnakwenda kuuliza kwa Baal-Zebubu mungu wa Ekroni?  Swali hili linaonekana kuwa ni lenye kushangaza sana na linalotupa kujifunza kwa kina na mapana na marefu namna na jinsi ambavyo Mungu anakasirishwa sana na watu wanaojihusisha na maswala ya ushirikina na matokeo mabaya ya kuacha kumtegemea Mungu, hii ni kwa sababu tangu mwanzo Mungu alikuwa amekwisha kuwaonya wana wa Israel kutokujihusisha na maswala ya kishirikina ikiwa ni pamoja na kuwaendea wenye pepo, wachawi na mambo yanayofanana na hayo;

Mambo ya walawi 19:31 “Msiwaendee wenye pepo, wala wachawi; msiwatafute; ili kutiwa unajisi na wao; Mimi ndimi BWANA, Mungu wenu.”

Kwa ujumla lilikuwa ni jambo la kusikitisha sana ya kwamba mtu kutoka katika taifa la Mungu anatuma wajumbe kwenda kutafuta msaada kwa miungu ya kigeni, miungu isiyo na nguvu na kuacha kumtegemea Mungu aliye hai, Mungu alimtuma nabii wake kuwahi wajumbe hao na kumpa majibu yanayoonyesha ya kuwa mfalme huyo atakufa na kuwa hatashuka katika kitanda alichokipanda jibu hili linakuwa kali kwa sababu mfalme huyu alimuasi Mungu na hakutaka kuuelekeza moyo wake kwa Mungu aliye hai jambo ambalo lilikuwa ni dharau kubwa sana yenye kuonyesha ya kuwa Mungu hana Msaada kwa watu wake jambo ambalo liko kinyume na ukweli wa kimaandiko, Neno la Mungu linatufundisha ya kuwa Mungu kwetu sisi ni kimbilio na nguvu na msaada uonekanao tele wakati wa mateso.

Zaburi 46:1-3 “Mungu kwetu sisi ni kimbilio na nguvu, Msaada utakaoonekana tele wakati wa mateso. Kwa hiyo hatutaogopa ijapobadilika nchi, Ijapotetemeka milima moyoni mwa bahari. Maji yake yajapovuma na kuumuka, Ijapopepesuka milima kwa kiburi chake.”

Kwa sababu hii leo tutachukua muda kujifunza kwa kina na mapana na marefu kuhusiana na swala zima la namna na jinsi Mungu anavyochukizwa na ushirikina na jinsi tunavyopaswa kumtegemea yeye katika maisha yetu yote. Tutajifunza somo hili “Je ni kwa sababu hakuna Mungu katika Israel” kwa kuzingatia vipengele vitatu vifuatavyo:-


·         Onyo la kutokujihusisha na ushirikina.

·         Madhara ya ushirikina.

·         Je ni kwa sababu Hakuna Mungu katika Israel?.


Onyo la kutokujihusisha na ushirikina.

Moja ya changamoto kubwa sana inayoikabili dunia ya wakati wa leo ni pamoja na kuwepo kwa watu wanaoamini katika ushirikina, yaani watu ambao wanamuamini Mungu lakini wakati huo huo wanaamini katika ushirikina!, Neno ushirikina katika lugha ya kiyunani ni “Deisidaimonia ambalo ni muunganiko wa maneno mawili Deis na Demon deis – Delivering to, demon or deity ambalo kwa kiingereza ni “Superstition” maana yake ni tendo la Mwanadamu aliyeumbwa na Mungu, kuacha kutafuta msaada kwa Mungu aliyemuumba na kwenda kutafuta msaada wa kimwili au kiroho kupitia watu wenye nguvu za giza, yaani wajumbe wa shetani na mapepo wakiwemo wachawi na waganga wa kienyeji, wasihiri, wapiga ramli, wapiga bao, wanga na kadhalika, kwa makusudi ya kujilinda, kupona, kuhukumu, kulaani, na ama kudhuru wengine, au kwa kusudi la kuwashinda wengine,au kwaajili ya kupata kibali na kukubalika au kumchafulia mwingine asipate kibali au kukubalika kwenye michezo, siasa, kugombea vyeo n.k. Kitendo hiki kinaitwa kitendo cha kumshirikisha Mungu na mashetani na ni kitendo ambacho kimekatazwa katika maandiko.

1Wakorintho 10:19-21 “Basi niseme nini? Ya kwamba kile kilichotolewa sadaka kwa sanamu ni kitu? Au ya kwamba sanamu ni kitu? Sivyo, lakini vitu vile wavitoavyo sadaka wavitoa kwa mashetani, wala si kwa Mungu; nami sipendi ninyi kushirikiana na mashetani. Hamwezi kunywea kikombe cha Bwana na kikombe cha mashetani. Hamwezi kushirikiana katika meza ya Bwana na katika meza ya mashetani.”

Kwa hiyo ushirikina ni kitendo cha Mtu aliyeumbwa na Mungu kushirikiana na mashetani, Ni kitendo cha kuacha kuamini na kuitegemea nguvu ya Mungu na kuzitegemea nguvu mbaya za giza, kwaajili ya kujilinda, kupona, kuondoa nuksi, mikosi au balaa au pia kwaajili ya kulaani au kuwatakia mabaya watu wengine, kuwadhuru na kuwaumiza, Mungu wetu ni Mungu mwenye wivu, hafurahii kabisa kitendo cha mwanadamu kuacha kumtumainia yeye wakati tunapokuwa katika changamoto mbalimbali na badala yake tukajielekeza katika kutafuta msaada kwa miungu hii ni machukizo kwake.Kumbuka ya kuwa nyuma ya sanamu na miungu yote shetani yuko nyuma yake!

Kutoka 20:3-5 “Usiwe na miungu mingine ila mimi.Usijifanyie sanamu ya kuchonga, wala mfano wa kitu cho chote kilicho juu mbinguni, wala kilicho chini duniani, wala kilicho majini chini ya dunia. Usivisujudie wala kuvitumikia; kwa kuwa mimi, BWANA, Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu; nawapatiliza wana maovu ya baba zao, hata kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukiao,”

Mungu alikuwa amewaonya wana wa Israel mara kwa mara kuacha kabisa kuwaendea waganga na wachawi, na wapiga bao na ramli na wale wote wanaofanana na hao, Mungu alikuwa anataka kuwalinda watu wake na tabia ya kishirikina, kwa bahati mbaya sana nyakati za leo watu wengi sana wanaamini katika ushirikina, pamoja na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia na mpanuko mkubwa sana wa kitaaluma na elimu inasikitisha kuona kuwa bado wako watu wanaamini sana katika nguvu za giza kuliko kumuamini Mungu, vitendo vya ushirikina vimetapakaa na kuenea kila mahali, mashuleni, makazini, katika biashara na wakati mwingine mpaka makanisani, hizi ni habari za kusikitisha sana, neno la Mungu linatukumbusha tena na tena kuacha kabisa kujishirikisha na maswala ya aina hii kama tunavyoweza kuona na kujifunza katika maandiko.

Kumbukumbu 18:9-13 “Utakapokwisha kuingia katika nchi akupayo Bwana, Mungu wako usijifunze kutenda kwa mfano wa machukizo ya mataifa yale. Asionekane kwako mtu ampitishaye mwanawe au binti yake kati ya moto, wala asionekane mtu atazamaye bao, wala mtu atazamaye nyakati mbaya, wala mwenye kubashiri, wala msihiri, wala mtu alogaye kwa kupiga mafundo, wala mtu apandishaye pepo, wala mchawi, wala mtu awaombaye wafu. Kwa maana mtu atendaye hayo ni chukizo kwa Bwana; kisha ni kwa sababu ya hayo Bwana, Mungu wako, anawafukuza mbele yako. Uwe mkamilifu kwa Bwana, Mungu wako.”

Kutoka 22:18 “Usimwache mwanamke mchawi kuishi.”

Walawi 19:26,28 “26.Msile kitu cho chote pamoja na damu yake; wala msifanye kuloga, wala kutumia utambuzi. 28. Msichanje chale yo yote katika nyama ya miili yenu kwa ajili ya wafu, wala msiandike alama miilini mwenu; mimi ndimi BWANA.”           

Walawi 20:26-27 “Nanyi mtakuwa watakatifu kwangu mimi; kwa kuwa mimi BWANA ni mtakatifu nami nimewatenga ninyi na mataifa, ili kwamba mwe wangu. Tena mtu mume au mtu mke aliye na pepo, au aliye mchawi, hakika atauawa; watawapiga kwa mawe; damu yao itakuwa juu yao.”

Kwa hiyo unapoyachunguza maandiko utaweza kugundua kuwa katika Torati Mungu alikataza kila aina ya ushirikina na uchawi Mungu alikataza watu wanaotoa kafara za watoto wao, alikataza kupiga ramli au kupiga bao, alikataza kutazama nyakati mbaya, alikataza wenye kubashiri, alikataza wenye kuroga kwa kupiga mafundo, usinga, alikataza kupunga au kupandisha pepo, alikataza kujihusisha na uchawi, alikataza kuabudu mizimu au kuomba wafu, alikataza kuchanjwa chale, alikataza kuchora tattoo, alikataza kutumia pepo wa utambuzi, au wenye kutabana na akiweka wazi katika Israel kuwa watu wa aina hiyo wauawe iwe ni mwanamme au iwe mwanamke na aliahidi kuwa atavikomesha kabisa vitu hivyo wakati wa ujio wa masihi.

Mika 5:12-15 “nami nitakatilia mbali uchawi, usiwe mkononi mwako; wala hutakuwa tena na watu wenye kutabana; nami nitakatilia mbali sanamu zako na nguzo zako, zitoke kati yako; wala hutaiabudu tena kazi ya mikono yako. Nami nitayang'oa maashera yenu, yasiwe kati yako; nami nitaiangamiza miji yako. Nami nitajilipiza kisasi katika hasira na ghadhabu juu ya mataifa wasiosikiliza.”

Kwa hiyo kujihusisha na ushirikina kwa namna yoyote ile na kwa sababu zozote zile ni dhambi kubwa na mbaya na hatari sana kwa namna Mungu anavyoielezea katika maandiko, Lakini kwa bahati mbaya nyakati za leo watu wanajihusisha na uchawi na kutafuta hata namna ya kujiunga na freemason na vikundi vingine vya kichawi, kumekuwepo na watu wanaojihusisha na uchawi kila mahali lakini pia kumekuwepo na watu wanaowategemea wachawi na waganga kwaajili ya kuwakomesha watu, kwaajili ya kujilinda, kwaajili ya masomo, kwaajili ya vyeo, kwaajili ya kupendwa au kumfunga mke au mume au bosi, kushinda uchaguzi, kupata madini, kupata utajiri, kufanya biashara, kuuza bidhaa,  kuugua, kuumiza wengine, kuharibia kibali wengine kuua wengine, kufitinisha wengine  au kuondoa nuksi na mikosi na balaa na kadhalika, hayo yote ni uasi mbele za Mungu na Mungu anachukizwa sana na wale wote wanaojihusisha na maswala yote hayo.

Madhara ya ushirikina.

Kama jinsi ambavyo tumeona katika mstari wa Msingi, yaliyomkuta mfalme Ahazia, uchawi na uganga husababisha madhara makubwa sana katika maisha ya kila mwanadamu, awaye yote ambaye atajiingiza katiia kutafuta msaada kwa miungu mingine badala ya Mungu aliye hai ni sawa tu na kuwa umeamua kumuabudu shetani, kwa sababu shetani ndiye anayewatumia hao na aina zote za wachawi ili kuwachepusha watu watoke nje ya tegemeo la Mungu aliye hai na wa kweli alafu wamuabudu yeye, Maandiko yanaonyesha ya kuwa, kuna madhara makubwa sana kwa watu wanaojihusisha na ushirikina na kuabudu miungu mingine badala ya Mungu mwenye nguvu wa kweli unapoacha kumtafuta Mungu na kuwaendea waganga na wachawi moja kwa moja unajiweka katika hatari ya kufa kama tulivyoona jinsi Mungu anavyochukizwa na hayo wakati wa mfalme Ahazia. Ahazia alimuacha Mungu aliye hai na kumuendea Baalzebubu au Ba’al zebuli alijulikana nyakati za biblia kama mungu wa ekroni aliyeabudiwa na wafilisti katika mji wa Ekroni mungu huyu alijulikana kama Bwana wa mainzi the Lord of flies, lakini pia alijulikana kama mkuu wa mapepo, yaani Shetani mwenyewe mungu huyu aliabudiwa na wakanaani, kuiendea miungi yoyote ya kienyeji ikiwa ni pamoja na mizimu kunamuudhi sana Mungu na ni ushirikina na Kushiriki ushirikina, aidha kwa kwenda kutafuta msaada kwao au kuwa mhudumu wa ushirikina au kuuamini na kuutegemea kunakufanya hivi:-

1.       Unajiweka katika hatari ya kufa.

 

2Wafalme 1:2-4 “Na Ahazia akaanguka katika dirisha la chumba chake orofani, katika Samaria, akaugua; akatuma wajumbe, akawaambia, Enendeni mkaulize kwa Baal-zebubu, mungu wa Ekroni, kwamba nitapona ugonjwa huu. Lakini malaika wa Bwana akamwambia Eliya Mtishbi, Ondoka, uende ukaonane na wale wajumbe wa mfalme wa Samaria, ukawaambie, Je! Ni kwa sababu hapana Mungu katika Israeli, hata mnakwenda kuuliza kwa Baal-zebubu, mungu wa Ekroni? Basi sasa, Bwana asema hivi, Hutashuka katika kile kitanda ulichokipanda, bali hakika utakufa. Eliya akaondoka.”

 

1Nyakati 10:13-14. “Basi Sauli alikufa kwa sababu ya kosa lake alilomkosa Bwana, kwa sababu ya neno la Bwana, asilolishika; na tena kwa kutaka shauri kwa mwenye pepo wa utambuzi, aulize kwake, asiulize kwa Bwana; kwa hiyo akamwua, na ufalme akamgeuzia Daudi, mwana wa Yese.”

 

2.       Unajiweka kwenye hatari ya kutupwa katika ziwa la Moto.

 

Ufunuo21:7-8 “Yeye ashindaye atayarithi haya, nami nitakuwa Mungu wake, naye atakuwa mwanangu. Bali waoga, na wasioamini, na wachukizao, na wauaji, na wazinzi, na wachawi, na hao waabuduo sanamu, na waongo wote, sehemu yao ni katika lile ziwa liwakalo moto na kiberiti. Hii ndiyo mauti ya pili.”             

 

3.       Unajiweka katika hatari ya kukataliwa na Mungu.

 

1Samuel 15:23 “Kwani kuasi ni kama dhambi ya uchawi, Na ukaidi ni kama ukafiri na vinyago; Kwa kuwa umelikataa neno la Bwana, Yeye naye amekukataa wewe usiwe mfalme.”

 

4.       Unaamsha hasira za Mungu kwaajili yako.

 

2Nyakati 33:6 “Tena akawapitisha wanawe motoni katika bonde la mwana wa Hinomu; akatazama bao, akabashiri, akafanya uganga, akajishughulisha na hao wenye pepo wa utambuzi, na wachawi; akafanya mabaya mengi machoni pa Bwana, hata kumkasirisha

 

5.       Unajitia unajisi.

 

Mambo ya walawi 19:31 “Msiwaendee wenye pepo, wala wachawi; msiwatafute; ili kutiwa unajisi na wao; Mimi ndimi BWANA, Mungu wenu.”

 

6.       Unajiweka katika hatari ya kukaziwa uso wa Mungu.

Mambo ya walawi 20:2-6 “Tena uwaambie wana wa Israeli, Mtu awaye yote miongoni mwa wana wa Israeli, au miongoni mwa wageni waketio katika Israeli, atakayetoa katika kizazi chake na kumpa Moleki, sharti atauawa; wenyeji wa nchi watampiga kwa mawe. Mimi nami nitamkazia uso wangu mtu huyo, nami nitamkatilia mbali na watu wake; kwa kuwa ametoa katika kizazi chake na kumpa Moleki, ili kupatia unajisi patakatifu pangu, na kulinajisi jina langu takatifu. Tena kama wenyeji wa nchi wakimfumbia macho mtu huyo kwa njia yo yote, hapo atoapo katika kizazi chake na kumpa Moleki, wasimwue; ndipo mimi nitamkazia uso wangu mtu huyo, na jamaa zake, nami nitamkatilia mbali, na hao wote wamwandamao katika uzinifu, ili kufanya uzinifu pamoja na Moleki, watengwe mbali na watu wao. Na mtu yule atakayewaendea wenye pepo, na wachawi, ili kuzini pamoja nao, nitakaza uso wangu juu ya mtu yule, nitamtenga na watu wake.”

7.       Unajiweka katika nafasi ya kupatwa na mabaya na Misiba.

 

Wakati mwingine unapoona mikosi imekuandama na unaandamwa na mambo mabaya sana unapaswa kujihoji na kujiangalia ni kwa nini kwani uchawi na uganga unaleta kiburi na kujifikiri wewe ndiye wewe lakini Mungu ameahidi kuwapiga kwa mapigo makuu wachawi na kuwamaliza kabisa kwa misiba na ubaya          

 

Isaya 47:8-14 “Sasa, basi, sikia haya, wewe upendaye anasa, ukaaye na kujiona salama, wewe usemaye moyoni mwako, Mimi ndiye, wala hapana mwingine zaidi yangu mimi; sitaketi mfano wa mjane, wala sitajua kufiwa na watoto; lakini mambo haya mawili yatakupata katika dakika moja siku moja, kufiwa na watoto, na ujane; yatakupata kiasi kitimilifu, uchawi wako ujapokuwa mwingi, na uganga wako mwingi mno. Maana umeutumainia ubaya wako; umesema, Hapana anionaye; hekima yako, na maarifa yako yamekupotosha, nawe umesema moyoni mwako, Mimi ndiye, wala hapana mwingine zaidi yangu mimi.Kwa sababu hiyo ubaya utakupata; wala hutajua kutopoa kwake; na msiba utakuangukia; hutaweza kuuondoa; na ukiwa utakupata kwa ghafula, usioujua. Simama sasa na uganga wako, na wingi wa uchawi wako, uliojitaabisha nao tangu ujana wako; labda utaweza kupata faida, labda utaweza kushinda. Umechoka kwa wingi wa mashauri yako; basi, na wasimame hao wajuao falaki, wazitazamao nyota, watabirio kila mwezi mambo ya mwezi huo, wakakuokoe na mambo yatakayokupata.Tazama, watakuwa kama mabua makavu; moto utawateketeza; hawatajiokoa na nguvu za mwali wa moto; hautakuwa kaa la kukota moto, wala moto wa kukaa karibu nao”.

 

8.       Unajiweka katika hatari ya kutokuurithi ufalme wa Mungu.

 

Wagalatia 5:19-21 “Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo, katika hayo nawaambia mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu.”

 

Kuna madhara makubwa mno kwa sababu ushirikina unakuweka katika nafasi ya kufa kimwili na kiroho, utakufa kimwili na utatupa katika ziwa liwakalo moto, huwezi kuingia katika ufalme wa Mungu, unajitia unajisi yaani unajiingiza katika mikosi zaidi, unaweza kuvamiwa na mapepo, unaamsha hasira za Mungu juu yako, unamfanya Mungu akukazie uso wake na unajiweka katika hatari ya kukosa ufalme wa Mungu, unapoyaangalia hayo kwa makini utaweza kuona maisha magumu sana ambayo mtu anayeshiriki ushirikina anajitengenezea, unajitengeneza laana mikosi na balaa na umasikini uliokithiri hii ni kwa sababu Mungu akikukazia uzo wake akakukasirikia  nani anaweza kukupatanisha naye.

 

1Samuel 2:25 “Mtu mmoja akimkosa mwenzake, Mungu atamhukumu; lakini mtu akimkosa Bwana, ni nani atakayemtetea? Lakini hawakuisikia sauti ya baba yao, kwa sababu Bwana amekusudia kuwaua.”

 

9.       Unajiweka katika nafasi ya kupingana na Mungu.

 

2Timotheo 3:8 “Na kama vile Yane na Yambre walivyopingana na Musa, vivyo hivyo na hawa wanapingana na ile kweli; ni watu walioharibika akili zao, wamekataliwa kwa mambo ya imani.”

 

Yana na Yambre wanataja kwa majina katika agano jipya walikuwa ni wachawi ambao walipingana na Musa na Haruni mbele ya Farao, na kumfanya farao aendelee kuwa na Moyo Mgumu asiamini kweli ya Mungu, wachawi hawa wakati Musa alipoitupa fimbo yake ikawa nyoka nao walizitupa fimbo zao kuwa nyoka, lakini Nyoka wa Musa aliwameza nyoka wa wagaganga wa farao, Mungu huwaona wavhawi na waganga kuwa ni maadui wa Imani, kazi yao kubwa ni kupotosha njia za Mungu zilizonyooka ili wanadamu wasiziamini

 

Matendo 13:5-12 “Na walipokuwa katika Salami wakalihubiri neno la Mungu katika masinagogi ya Wayahudi, nao walikuwa naye Yohana kuwa mtumishi wao. Walipokwisha kupita katikati ya kisiwa chote mpaka Pafo, wakaona mtu mmoja, mchawi, nabii wa uongo, Myahudi jina lake Bar-Yesu; mtu huyu alikuwa pamoja na liwali Sergio Paulo, mtu mwenye akili. Yeye liwali akawaita Barnaba na Sauli waje kwake, akataka kulisikia neno la Mungu. Lakini Elima, yule mchawi (maana ndiyo tafsiri ya jina lake), akashindana nao, akitaka kumtia yule liwali moyo wa kuiacha ile imani. Lakini Sauli, ambaye ndiye Paulo, akijaa Roho Mtakatifu, akamkazia macho, akasema, Ewe mwenye kujaa hila na uovu wote, mwana wa Ibilisi, adui wa haki yote, huachi kuzipotoa njia za Bwana zilizonyoka? Basi, angalia, mkono wa Bwana u juu yako, nawe utakuwa kipofu, usilione jua kwa muda. Mara kiwi kikamwangukia na giza, akazunguka-zunguka na kumtafuta mtu wa kumshika mkono na kumwongoza.Ndipo yule liwali, alipoyaona yaliyotendeka, akaamini, akiyastaajabia mafundisho ya Bwana.”

 

Unaona maandiko yanaonyesha wazi kuwa wachawi na waganga ni maadui wa Imani, kazi yao kubwa ni kuchepusha ibada kutoka kwa Mungu aliye hai kuelekea kwa shetani, wana ni makuhani wa mashetani ni maajenti wa shetani, kazi zo ni kupingana na Mungu aliye hai ili wanadamu wasimuamini Mungu na wawategemee wao, na kuwaingiza katika kuishi kwa kutegemea na kuamini ushirikina, Mtu anaye waendea au anayejishughulisha na ushirikina ni adui wa Mungu na ni mtu anayepingana na Mungu.

 

Je ni kwa sababu Hakuna Mungu katika Israel?.

2Wafalme 1:2-4 “Na Ahazia akaanguka katika dirisha la chumba chake orofani, katika Samaria, akaugua; akatuma wajumbe, akawaambia, Enendeni mkaulize kwa Baal-zebubu, mungu wa Ekroni, kwamba nitapona ugonjwa huu. Lakini malaika wa Bwana akamwambia Eliya Mtishbi, Ondoka, uende ukaonane na wale wajumbe wa mfalme wa Samaria, ukawaambie, Je! Ni kwa sababu hapana Mungu katika Israeli, hata mnakwenda kuuliza kwa Baal-zebubu, mungu wa Ekroni? Basi sasa, Bwana asema hivi, Hutashuka katika kile kitanda ulichokipanda, bali hakika utakufa. Eliya akaondoka.”

Lilikuwa swali la mshangao kutoka kwa Mungu kupitia nabii wake kumuuliza Mfalme mwasi ambaye Mungu alikusudia kumuua, alithibitishiwa kuwa atakufa kwa hakika hii inatufundisha kuwa kama unajua ya kuwa yuko Mungu aliye hai, na kisha ukaenda kuiabudu au kuuliza au kutegemea kwa wachawi kinyume na Mungu aliye hai ni wazi kuwa unajiweka katika hatua ya kujibainisha kwa Mungu kuwa humuamini na wala humtegemei, na Mungu anachukizwa na wasiomwamini wala wasiomtegemea yeye, Kugeukia miungu mingine au wachawi na waganga kunamaanisha  kuwa unamwambia Mungu kuwa yeye hawezi, kukuokoa wala kukusaidia, na unajibainisha kuwa wewe ni muasi  na humtaki, na kwa sababu hiyo ni sawa na kama umemvunjia heshima na kuonyesha Mungu kuwa ni wa kupuuziwa tu, wachawi waliomjua Mungu kule Efeso waliikiri imani na walimuamini Bwana Yesu na wakaachana na vifaa vyao vya uchawi na wakavichoma moto na kumbuka kuwa vilikuwa vya thamani kubwa sana lakini hawakujali walipogundua kuwa yuko Mungu aliye hai na ni yeye pekee ndiye wa kutumainiwa!

Matendo 19:17-20 “Habari hii ikajulikana na Wayahudi wote na Wayunani waliokaa Efeso, hofu ikawaingia wote, na jina la Bwana Yesu likatukuzwa. Na wengi wa wale walioamini wakaja wakaungama, wakidhihirisha matendo yao. Na watu wengi katika wale waliotumia mambo ya uganga wakakusanya vitabu vyao, wakavichoma moto mbele ya watu wote; wakafanya hesabu ya thamani yake, wakaona ya kwamba yapata fedha hamsini elfu. Hivyo ndivyo neno la Bwana lilivyozidi na kushinda kwa nguvu.”

Neno la Mungu linaonyesha kuwa kwenda kuuliza habari kwa wenye pepo ni kwenda kuuliza kwa watu waliokufa na kwa sababu hiyo watu wa namna hiyo watapata tabu sana, watakuwa katika giza nene, mambo yao hayatafanikiwa wengi wameharibu maisha yao kwa sababu ya kutokumtumainia Mungu na kuwatumainia wachawi, Mungu alichukizwa na Ahazia kwa sababu hakutaka kuuliza kutoka kwake na badala yake alielekeza shingo yake katika ushirikina! Na Mungu alimuhakikishia kuwa atakufa hii maana yake sio kimwili tu, lakini atatengwa mbali na Mungu.

Isaya 8:19-22 “Na wakati watakapokuambia, Tafuta habari kwa watu wenye pepo na kwa wachawi; waliao kama ndege na kunong'ona; je! Haiwapasi watu kutafuta habari kwa Mungu wao? Je! Waende kwa watu waliokufa kwa ajili ya watu walio hai? Na waende kwa sheria na ushuhuda; ikiwa hawasemi sawasawa na neno hili, bila shaka kwa hao hapana asubuhi. Nao watapita katikati yake, wamedhikika sana na kuwa na njaa; na itakuwa watakapoona njaa, watalalamika na kuapa kwa mfalme wao, na kwa Mungu wao, na kuelekeza nyuso zao juu; nao wataiangalia nchi, na, tazama, shida na giza; hapana changamko kwa sababu ya dhiki; nao watafukuzwa na kuingia katika giza kubwa.”

Mungu anataka watu wake waache kuamini wachawi na badala yake waiamini Injili, Injili yaani habari njema ina nguvu sana na iko juu ya wachawi, kuna tumaini katika injili, injili ni matendo ya Mungu yaliyo makuu zaidi ya uchawi, injili inafunua jinsi Mungu wetu aliyejifunua kwa Ibrahimu na Isaka na Yakobo, Mungu wa Israel kuwa ni Mungu mwenye nguvu kubwa sana ikiwa mtu awaye yote anataka mafanikio na Baraka kubwa sana za Mungu basi hatuna budi kuiamini injili na kumuamini Bwana wetu Yesu kwa kumfanya kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yetu, Kazi yake kubwa aliyoifanya msalabani inatosha kabisa kuleta ukombozi wa mwanadamu  katika maeneo yote na mwenyewe alisema imekwisha akimaanisha kuwa hakuna alichobakiza ambacho kinahusu shida na changamoto za wanadamu ambacho kinaweza kuwa na nguvu kuipita kazi yake aliyoifanya pale msalabani, kimsingi wachawi, wenyewe wanapaswa kuiamini injili na kuachana kabisa na uchawi na kuchoma moto mikoba yao na vifaa vyao vya uchawi na kumuamini Bwana Yesu ili iweze kuwa Baraka kubwa katika maisha yao.

Matendo 8:9-13 “Na mtu mmoja, jina lake Simoni, hapo kwanza alikuwa akifanya uchawi katika mji ule, akiwashangaza watu wa taifa la Wasamaria, akisema ya kuwa yeye ni mtu mkubwa. Wote wakamsikiliza tangu mdogo hata mkubwa, wakisema, Mtu huyu ni uweza wa Mungu, ule Mkuu.Wakamsikiliza, kwa maana amewashangaza muda mwingi kwa uchawi wake. Lakini walipomwamini Filipo, akizihubiri habari njema za ufalme wa Mungu, na jina lake Yesu Kristo, wakabatizwa, wanaume na wanawake. Na yeye Simoni mwenyewe aliamini akabatizwa, akashikamana na Filipo; akashangaa alipoziona ishara na miujiza mikubwa inayotendeka.”

Kwa kila mtu aliyeokoka yaani kila mtu anayemuamini Bwana Yesu na kumfanya yeye kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yake hana budi kuweka Imani yake kwa Mungu wetu na kwa Bwana wetu Yesu Kristo ukijua na kuamini ya kuwa kwake yeye hakuna uchawi wala uganga utakaoweza kufanya kazi juu yako, wewe mkristo utaumizwa ikiwa tu utaondoa imani yako kwa Mungu wa Israel, lakini kama unaamini katika Yesu Kristo fahamu wazi kuwa hakuna uganga wala uchawi utakaoweza kufua dafu dhidi yako kwa sababu imeandikwa, Mungu wetu ana nguvu Biblia inasema kama nguvu za nyati kwa hiyo uchawi hauwezi kitu, kwako wala haukuwezi.

Hesabu 23:22-23 “Mungu amewaleta kutoka Misri, Naye ana nguvu kama nguvu za nyati. Hakika hapana uchawi juu ya Yakobo, Wala hapana uganga juu ya Israeli. Sasa habari za Yakobo na Israeli zitasemwa, Ni mambo gani aliyoyatenda Mungu!

Aidha sisi tumepewa jina la Yesu ambalo tunaweza kulitumia na kuliitia wakati wa changamoto za aina yoyote na jina hili lina nguvu, lina mamlaka, lina uwezo na kila atakayeliitia jina hili ataokolewa katika hali yoyote anayoipitia.

Matendo 4:9-12 “kama tukiulizwa leo habari ya jambo jema alilofanyiwa yule mtu dhaifu, jinsi alivyoponywa, jueni ninyi nyote na watu wote wa Israeli ya kuwa kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, ambaye ninyi mlimsulibisha, na Mungu akamfufua katika wafu, kwa jina hilo mtu huyu anasimama ali mzima mbele yenu. Yeye ndiye jiwe lile lililodharauliwa na ninyi waashi, nalo limewekwa kuwa jiwe kuu la pembeni. Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo.”

Wafilipi 2:9-11 “Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina; ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi; na kila ulimi ukiri ya kuwa YESU KRISTO NI BWANA, kwa utukufu wa Mungu Baba.”

Jina la Yesu lina nguvu, na mamlaka na tunaweza kulitumia jina hili kuamuru jambo lolote lile na likawa na mafanikio makubwa katika ulimwengu wa roho na ulimwengu wa mwili, kwa sababu hiyo hatupaswi kuogopa chochote tunaweza kulitumia na kulitumainia jina hili na tukapata mafanikio makubwa na mpenyo katika kila eneo ikiwa ni pamoja na kusambaratisha na kuharibu nguvu zote za giza, Yesu ameamuru tuzishughulikie nguvu za giza na ametupa amri ya kukanyaga nyoka na nge na nguvu zote za yule adui na kuwa hakuna kitu kitakachotudhuru

Luka 10:18-20 “Akawaambia, Nilimwona Shetani, akianguka kutoka mbinguni kama umeme.Tazama, nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na nge, na nguvu zote za yule adui, wala hakuna kitu kitakachowadhuru.Lakini, msifurahi kwa vile pepo wanavyowatii; bali furahini kwa sababu majina yenu yameandikwa mbinguni.”

Isaya 54:17 “Kila silaha itakayofanyika juu yako haitafanikiwa na kila ulimi utakaoinuka juu yako katika hukumu utauhukumu kuwa mkosa. Huu ndio urithi wa watumishi wa Bwana, na haki yao inayotoka kwangu mimi, asema Bwana.”                

Hitimisho:

Ujumbe huu unatukumbusha ya kuwa Mungu ni Mungu mwenye wivu, na kuwa anataka tumtegemee yeye na kumuamini yeye, lakini ukijiingiza katika ushirikina utapata madhara makubwa sana huenda ulikuwa hujajifunza hili sasa umejifunza haribu kabisa kila kitu kinachotokana na uganga na uchawi na waonye wengine waache kujihushisha na ushirikina na badala yake wamwamini Mungu na kujua ya kuwa Mungu atawakomboa kutoka katika kila changamoto inayowakabili kwa sababu uwezo huo upo kwa jina la Yesu Kristo mwana wa Mungu aliye hai.

Na. Rev. Innocent Samuel Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima       

Hakuna maoni: