John 2:19. “Destroy this temple . and I will raise it again in three days”
Utangulizi.
Ni muhimu kufahamu kuwa moja ya matamko
ya Yesu Kristo yaliyowahi kulete utata, mojawapo ni tamko hili “Livunjeni
Hekalu hili nami katika siku tatu nitalisimamisha”, Tamko hili liliweza
kutumiwa na maadui wa Yesu Kristo kama moja ya ushahidi mkubwa wa kumshitaki
Yesu wakati wa kuhukumiwa kwake Marko
14:58 “Sisi
tulimsikia akisema, Mimi nitalivunja hekalu hili lililofanyika kwa mikono, na
katika siku tatu nitajenga jingine lisilofanyika kwa mikono.” Na Mathayo 26:59-61 “Basi wakuu wa makuhani na baraza yote wakatafuta
ushuhuda wa uongo juu ya Yesu, wapate kumwua; wasiuone wangawa walitokea
mashahidi wa uongo wengi. Hata baadaye wawili wakatokea, wakasema, Huyu
alisema, Naweza kulivunja hekalu la Mungu, na kulijenga kwa siku tatu.”
Unaweza kuona jinsi ambavyo matamshi haya yalivyoweza kutafasiriwa kwa utata na
wale waliotafuta kumhukumu Yesu Kristo, usemi huu unaweza kubaki kuwa tata hata
kwa jamii yetu leo kama hatutaweza kumsikiliza Mwalimu mkuu Roho Mtakatifu ili
kwamba atusaidie kuyaelewa maandiko haya na kupata maana muhimu zilizokusudiwa,
Ni kwa makusudi hayo basi leo tunachukua muda kujifunza kuhusu usemi huu wa
Yesu “LIVUNJENI HEKALU HILI, NAMI KATIKA
SIKU TATU NITALISIMAMISHA” usemi huu wenye nguvu Baba na autumie kumjenga
kila mmoja wetu katika jina la Yesu Kristo amen. Tutajifunza somo hili kwa
kuzingatia vipengele viwili vifuatavyo:-
·
Maana ya Hekalu.
·
Livunjeni Hekalu hili nami katika siku tatu
nitalisimamisha!
Maana ya Hekalu.
Ni muhimu kufahamu kuwa Jina
Hekalu limetokana na jina la kiingereza cha zamani “HEKAHAL” ambalo maana yake ni “main building” au “Hall”, ambalo pia
lilitafasiriwea kama neno “Temple”
kwa kiingereza cha zamani, Katika lugha ya kiebrania neno Hekalu linatumika
kama “BEIT YHWH” yaani nyumba ya
Mungu au “BEIT HA ELOHIM” yaani
nyumba ya Mungu, na neno nyumba yangu ni “BEIT”
au BEITEKHA”
Kwa kawaida kwa mara ya kwanza neno hekalu lilitumika
kumaanisha nyumba ya Mungu ambayo ilikuwa ni hema ya kukutania iliyokuwako
Shilo 1Samuel 1:9 “Ndipo Hana akainuka, walipokwisha kula na kunywa huko Shilo.
Naye Eli, kuhani, alikuwa akiketi kitini pake penye mwimo wa HEKALU la Bwana.”
Katika agano Jipya neno hekalu limekuwa
na maana pana zaidi na zenye tafasiri
kadhaa kadhaa:-
1. Hekalu
linamaanisha mwili wa Yesu Kristo Yohana
2:19, 2:21
2. Hekalu
pia humaanisha mtu aliyemwamini Yesu Kristo 1Wakoritho 3:16-17
3. Hekalu
pia humaanisha Kanisa yaani watu waliomwamini Yesu Kristo Waefeso 2:21
4. Lakini
mbinguni pia kunaitwa hekalu Ufunuo 7:5
5. Lakini
yako pia majengo ya miungu mingine ambayo pia huitwa hekalu hapa duniani mfano
ni lile hekalu na mungu mke Diana au Artremi Matendo 19:27.
Ni muhimu kufahamu hata hivyo
kibiblia na kwa mujibu wa Imani ya kiyahudi na Kikristo kwa ujumla neno hekalu
lilitumika zaidi kumaanisha nyumba ya Mungu iliyokuwako katika mlima Sayuni
kwaajili ya kumuabudu Mungu, hili lilitwa Hekalu 1Falme 6:17, Nyumba ya Mungu 2Wafalme
11:10, Hekalu takatifu Zaburi 79:1,
Nyumba ya Bwana 2Nyakati 23:5, 12,
Nyumba ya Mungu wa Yakobo Isaya 2:3
Nyumba ya utukufu Isaya 60:7, Nyumba ya sala Isaya
56:7, Mathayo 21:13 Nyumba ya
sadaka 2Nyakati 7:12 Patakatifu 2Nyakati 36:17 Mlima wa nyumba ya Mungu
Isaya 2:2 Patakatifu nyumba ya uzuri
Isaya 64:11 Mlima mtakatifu Isaya
27:13 Mahali kwa Bwana 1Nyakati 29:1
Hema la ushuhuda 2Nyakati 24:6
Sayuni Zaburi 74:2, 84:7 na Yesu
aliita Nyumba ya baba yangu Yohana 2:16.
Livunjeni Hekalu hili nami katika siku tatu nitalisimamisha!
Yohana 2:19-21. “Yesu akajibu, akawaambia, Livunjeni hekalu hili, nami katika
siku tatu nitalisimamisha. Basi Wayahudi wakasema, Hekalu hili lilijengwa
katika muda wa miaka arobaini na sita, nawe utalisimamisha katika siku tatu?
Lakini yeye alinena habari za hekalu la mwili wake.”
Kimsingi wakati Yesu alipokuwa
akiyatamka maneno haya Wayahudi walifikiri kuwa Yesu alikuwa akizungumza juu ya
Hekalu ambalo lilikuwa limekarabatiwa na Herode mnamo karne ya 19 Kabla ya
Yesu, Hekalu hilo la kifahari ambalo wayahudi walikuwa wanajivunia lilikuwa
limechukua muda wa miaka 46 hivi, Yesu
hakujisumbua kutoa ufafanuzi wa maana ya meneo haya, Wanafunzi wake tu ndio
walioelewa kuwa Yesu alikuwa akizungumza juu ya mwili wake na juu ya uhai wake
kwamba yeye ana uwezo wa kuutoa uhai wake na kuutwaa tena Yohana 10:17-18 “Ndiposa Baba anipenda, kwa sababu nautoa uhai wangu ili
niutwae tena. Hakuna mtu aniondoleaye, bali mimi nautoa mwenyewe. Nami ninao
uweza wa kuutoa, ninao na uweza wa kuutwaa tena. Agizo hilo nalilipokea kwa
Baba yangu.” Wayahudi walikuwa hawako
tayari kumpokea Yesu na walikuwa tayari wamekwisha kupanga mpango wa
kumwangamiza Yesu, Kwa hiyo Yesu alikuwa akizungumza habari ya mpango wao na
kifo chake, hivyo usemi huu waoa hawakuuelewa lakini wanafunzi waliuelewa
baadaye kuwa Yesu alikuwa anazungumza habari ya kusulubiwa kwake kufa na
kufufuka, kwa hiyo Yesu alipofufuka siku ya tatu wanafunzi walishangaa neno la
Mungu na unabii wa Yesu Kristo mwenyewe , hivyo walitambua kuwa kufa kwa Yesu
Kristo halikuwa tukio la bahati mbaya bali ulikuwa ni mpango wa Mungu kwaajili
ya uzima wa milele.
Usemi huu ulikuwa usemi wenye
kuonyesha nguvu kubwa na uweza wa Yesu Kristo, kwamba yeye ni mweny nguvu na
anazo funguo za mauti na za kuzimu yaani ana mamlaka yote hata leo Yesu bado
analiangalia kanisa lake na hekalu lake ambao ni sisi wanadamu, kutokana na
kazi za shetani katika maisha ya mwanadamu na kazi zake ulimwenguni pamoja na anguko
la Mwanadamu, kumekuweko na hali za kutokumcha
Mungu, kuipenda dunia tamaa na kila aina ya dhambi na vimekuwa ni matokeo makubwa ya kumomonyoka
kwa uadilifu wa mwanadamu katika maisha yake
na kumekuwa ni mwanzo wa kaburi, Mwanadamu kwa asili ndani yake ameumbwa
na Mungu kuwa Hekalu, Mioyo yetu iliumbwa na Mungu kwa kusudi la kuifanya kuwa
nyumba ya ibada ya kwa Roho Mtakatifu, mioyo yetu imekusudiwa kuwa nyumba ya
Mungu aliye hai, lakini kutokana na ubinafsi, dhambi na tamaa za dunia watu na ibilisi wameharibu maisha yao matakatifu
na kupungukiwa na utukufu wa Mungu, wameharibu nyumba ya Mungu kwa nyundo na
mawe na mashoka wameweka chukizo la uharibifu mahali patakatifu, wamelinajisi
hekalu, wameharibu dhamira zao na hazina hisia ya hofu ya Mungu kabisa, kila
wanachokiwaza wanadamu, walichojaza mioyoni mwao, katika maamuzi yao na mapenzi
yao uwepo wa Mungu umepewa nafasi ndogo sana au umenyimwa kabisa kuweko katika
nafasi ya Moyo wa Binadamu
Ulimwengu umekuwa wa tofauti sana
wanadamu wameharibika badala ya kuchagua mema wamechagua mabaya, maovu
yanaonekana kuwa ni sifa na wema unaonekana kuwa ni ujinga Yesu alilijua hilo
mapema inasikitisha kuwa watu walimchagua Baraba aliyekuwa muhaini na
kumsulubisha Yesu aliyekuwa akiponya Magonjwa yao na kutoa muda wake
akiwafundisha njia za Mungu kwa usahihi zaidi, Yesu alijua kuwa ni kwa kupitia
kulinda heshima zao na tamaa zao na ubinafsi wao viongozi wa dini wana makusudi
ya kumuua na hivyo kuleta uharibifu wa Mwili wake kama Hekalu la Roho Mtakatifu
na shetani ameaharibu mioyo ya wanadamu ili kuleta uharibifu ndani yao ziko
roho za uharibifu zimetumwa kukuharibia kila walichikifanya wanadamu katika
dhamiri zao na mioyo yao ni uharibifu wa hekalu la Mungu.
Yesu akijua uweza na mamlaka alio
nao alizungumza juu yamauti yake lakini pia anazungumza juu ya mauti yako na
kwa ujasiri najua kuwa anao uwezo wa kurejesha tena, kile ambacho shetani
ameharibu katika maisha yako yeye ana uwezo wa kukarabati ndani na Muda mfupi
kama utampa maisha, yeye atafukuza wafanya biashara miungu na mapepo
yanayoharibu maisha yako na atayahuisha tena kwa nguvu alizonazo, siku tatu
inamaanisha kwa kazi yake aliyoifanya , kwa kusulubiwa na kufa na kufufuka
inamaanisha ukweli kuwa alikufa kwa dhambi zetu na amefufukwa kwaajili ya haki
Yesu ni wazi kuwa kwa kazi aliyoifanya msalabani inauwezo wa kumjenga na
kumrejesha upya mwanadamu wa aina yoyotena kabila lolote na aliyeharibika kwa
kiwangochopchote na mtu huyo akawa makazi ya roho mtakatifu wa Mungu,
haijalishi sasa una miaka mingapi, haijalishi tatizo lako lina miaka mingapi
Mungu anataka uamini kazi iliyofanyika msalabani kwamba ina nguvu za kipekee za
kufanya kitu kipya katika maisha yako, Ndio maana Yesu Hakushughulika kuhesabu
miaka ya hekalu kujengwa Yeye amesema livunje na ndani ya siku tatu
atalisimamisha, Hekalu lililokuwa limejengwa kwa miaka 46 hata hivyo lilikuwa
bado halijakamilika, Lakini kazi aliyoifanya yesu ni kamilifu kama ulimkubali
yeye atalijenga hekalu tena atakamilisha mapungufu yako na atalijenga Hekalu
lako bila nyundo kusikika
1Wafalme 6:7 “Na nyumba ilipokuwa ikijengwa, ikajengwa kwa mawe yaliokwisha kuchongwa chimboni; wala nyundo, wala shoka, wala chombo cha chuma cho chote, sauti yake haikusikiwa ilipokuwa ikijengwa nyumba.”
Ni Yesu Kristo pekee ndiye mwenye
uwezo wa kulijenga Hekalu lake bila kelele, wakati mwingine tumepiga nyundo,
tumetumia shoka na vyombo vya chuma katika kuwajenga wanadamu Lakini Yesu
anaweza kumjenga awaye yote bila Kelele, Leo atakujenga wewe pia bila kelele za
wanadamu.
Na mkuu wa wajenzi mwenye Hekima
Rev. Innocent Kamote.