Jumapili, 30 Oktoba 2016

Bwana atasimama pamoja nawe!


Andiko: 2 Timotheo 4:16-18
 
16. Katika jawabu langu la kwanza hakuna mtu aliyesimama upande wangu, bali wote waliniacha; naomba wasihesabiwe hatia kwa jambo hilo. 17. Lakini Bwana alisimama pamoja nami akanitia nguvu, ili kwa kazi yangu ule ujumbe utangazwe kwa utimilifu, hata wasikie Mataifa yote; nami nikaokolewa katika kinywa cha simba. 18. Bwana ataniokoa na kila neno baya, na kunihifadhi hata nifike ufalme wake wa mbinguni. Utukufu una Yeye milele na milele. Amina

Kuokolewa katika kinywa cha Simba 

Utangulizi:

Ni muhimu kufahamu kuwa Nyakati za kanisa la kwanza wakristo walipitia vipindi mbalimbali vya Mateso na kulikuwa na aina kuu mbili za maadui, walikuweko maadui wa nje wa kanisa na wa ndani, wote walikuwa ni hatari sana, katika mwaka wa 54-68 baada ya Kristo Mateso ya Kanisa yaliongezeka sana na ndugu wengi katika Kristo waliuawa, kwani mfalme katili zaidi kuliko wote alitawala aliyejulikana kama “NERO CLAUDIUS” wakati huu ulikuwa wakati mgumu sana na hasa kwa viongozi wa Kanisa na washirika pia, Paulo mtume wakati huu aliandika waraka wake wa mwisho ili kumtia moyo Timotheo kuendelea kusimamia kanisa la Mungu bila kuogopa Mateso.

Licha ya Paulo mtume kumtia moyo Timotheo lakini vilevile alijitia Moyo yeye mwenyewe ingawa wakati huu alifahamu kuwa atakufa na kuwa huduma yake ilikuwa imefika mwisho, lakini aliandika waraka huu akiwa kifungoni Rumi na mtawala Nero akiwa hataki kabisa kusikia Injili ikihubiriwa, lakini hata wakristo na ndugu waliokuwa pamoja na Mtume Paulo walikimbia na hakuna mtu alitaka kusimama upande wake hivyo wakati huu Paulo alivunjika moyo na kukata tamaa lakini katika mistari hii hapo juu kuna mambo Muhimu ya kujifunza kutoka kwake

·         Lakini Bwana alisimama Pamoja nami
·         Kuokolewa katika kinywa cha Simba
·         Kuokolewa na kila neno baya.

Lakini Bwana alisimama Pamoja nani

Paulo ingawa alikuwa anajua kuwa mwisho wake umekaribia na kuwa sasa anamiminwa "2Timotheo 4:6-7" hakutaka Timotheo akate tamaa yeye alikuwa na ujuzi kamili ya kuwa Bwana angesimama pamoja naye, Mungu kusimama pamoja naye halikuwa jambo geni katika maisha ya huduma yake, Mara kadhaa kila alipokutana na jambo gumu hata kukaribia kutaka kufa Yesu alikuwa Pamoja naye, Neno KUWA PAMOJA, AU KUWA KARIBU kwa Kiyunani ni “PARISTEMI” kiingereza chake place beside, put at disposal, to present, to stand before, to provide, or come to aid or present offer na standing near, tafasiri rahisi ya Kiswahili ni “KUWEPO KWA KUSUDI LA KUSAIDIA” Neno kama hilo limetumika mara kadhaa katika huduma ya Paulo 

Matendo 23:11Usiku ule Bwana akasimama karibu naye, akasema, Uwe na moyo mkuu; kwa sababu, kama ulivyonishuhudia habari zangu Yerusalemu, imekupasa kunishuhudia vivyo hivyo Rumi nako.”

Matendo 27:23 - 25 “23. Kwa maana usiku huu wa leo malaika wa Mungu yule ambaye mimi ni wake, naye ndiye nimwabuduye, alisimama karibu nami, 24. akaniambia, Usiogope, Paulo, huna budi kusimama mbele ya Kaisari; tena, tazama, Mungu amekupa watu wote wanaosafiri pamoja nawe. 25. Basi, wanaume, changamkeni; kwa sababu namwamini Mungu, ya kwamba yatakuwa vile vile kama nilivyoambiwa.

Ni kawaida ya Mungu kuwepo karibu nasi na kutoa msaada pale tunapohitaji msaada wake ama pale watu wengine wanapokuwa wameshindwa kutoa msaada, Inaonekana wazi kuwa alipokuwa Gerezani Bwana alimtia nguvu, Mungu ataendelea kututia nguvu mpaka dakika ya mwisho

Kuokolewa katika kinywa cha Simba

Paulo mtume anazungumza jambo lingine lililokuwa likiwakabili watu wa nyakati za Kanisa la kwanza na Bwana pia alimuokoa nalo na hii ilikuwa ni kuokolewa katika kinywa cha samba, Nyakati za Kanisa la kwanza wakati wa mateso kulikuwa na samba wa aina tatu waliokuwa wakilisumbua kanisa

·         Simba wa kawaida wanyama – Hawa walikuwa wakitumika kuwatesa wakristo kila mtu aliyesimama kuihubiri injili na kumkiri Yesu kuwa ni Bwana kama akikamatwa auwakikamatwa walitupwa viwanjani na kufunguliwa simba wenye njaa na kuwatafuna wakristo, watu wengi katika maombi yao waliomba waokolewa na simba hao, huenda Paulo mtume pia alimuomba Mungu akaokolewe na simba wakristo wengi waliomba muujiza utokee kama Daniel lakini walitafunwa hivyo hofu kubwa iliingia 

·         Simba aliwakilisha mtawala wa Rumi – Nero Claudio alikuwa ni mtawala katili aliyeuawa wakristo wengi bila Huruma na hivyo wakristo wengi walimuogopa na walitumia jina simba pia kama lugha ya mficho dhidi ya mtawala katili

·         Simba aliwakilisha Shetani  - katika wakati huu kwa kweli shetani alikuwa amekasirika kama simba akipania kabisa kuisambaratisha injili kwa kulisambaratisha kanisa sura ya shetani ilionekana wazi kupitia Nero na simba halisi waliokuwa wakitumiwa kama njia ya mateso 1Petro 5:8Mwe na kiasi na kukesha; kwa kuwa mshitaki wenu Ibilisi, kama simba angurumaye, huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze.” Kukesha ni kuomba Yesu alisema Ombeni ili msije mkaingia majaribuni

Kuokolewa na kila neno baya 

Ni muhimu kufahamu kuwa mitume kamwe hawakuwa wanaogopa kufa lakini walikuwa wanaogopa kusalitiwa na watu wa baya ndani ya injili “deliver me from every evil work” Neno baya au evil katika kiyunani ni “PONEROS  ambalo kiingereza chake ni  The negative moral quality of a person or action opposed to God and his goodness” Paulo alijiombea kuwa asije akamkosea Mungu akapoteza Ufalme wa mbinguni, Paulo alijiombea kumaliza vizuri mwendo wake, kuvipiga vita vilivyo vizuri vya imani, alijiombea asinenwe vibaya asichafuke kwaajili ya injili, Mungu na awe karibu na kila mmoja wetu na kutupa msaada na kutuokoa na kinywa cha simba na kutuokoka na kila neno baya.

Na. Rev. Innocent Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima

Alhamisi, 27 Oktoba 2016

Mabaya hayatakupata wewe!



Mstari wa Msingi: Zaburi 91:10
 
Mabaya hayatakupata wewe, wala tauni haitakaribia hema yako!”


Utangulizi:

Zaburi hii ni mojawapo kati ya Zaburi zilizotungwa na kuandikwa na Daudi, Inaonekana wazi kabisa zaburi hii ikizungumzia pigo la ugonjwa wa Tauni, ambayo Mungu aliipiga Israel kuokana na kosa la Daudi kuwahesabia wanajeshi wake na kusahau kuwa ushindi unatoka kwa Mungu, katika wakati huu Mungu aliruhusu malaika wake na kuua watu wapatao 70 elfu kwa muda mfupi sana kutoka Dani mpaka Beersheba na sasa malaika wa Bwana alikuwa anaelekea kuuharibu Yerusalem  unaweza kuona vema habari hii katika 2Samuel 24: 10-17

10. Ndipo moyo wake Daudi ukamchoma baada ya kuwahesabu hao watu. Naye Daudi akamwambia Bwana, Nimekosa sana kwa haya niliyoyafanya; lakini sasa, Ee Bwana, nakusihi uuondolee mbali uovu wa mtumishi wako; kwani nimefanya upumbavu kabisa. 11. Na Daudi alipoondoka asubuhi, neno la Bwana likamjia nabii Gadi, mwonaji wake Daudi, kusema, 12. Nenda, ukanene na Daudi, Bwana asema hivi, Nakuwekea mambo matatu; katika haya uchague moja, nikutendee hilo. 13. Basi Gadi akamwendea Daudi, akamweleza, akamwambia, Basi, miaka saba ya njaa ikujie katika nchi yako? Au miezi mitatu ukimbie mbele ya adui zako, huku wakikufuatia? Au siku tatu iwe tauni katika nchi yako? Fanya shauri sasa, ufikiri, ni jawabu gani nimrudishie yeye aliyenituma. 14. Naye Daudi akamwambia Gadi, Nimeingia katika mashaka sana; basi sasa na tuanguke katika mkono wa Bwana; kwa kuwa rehema zake ni nyingi; wala nisianguke katika mkono wa wanadamu. 15. Basi Bwana akawaletea Israeli tauni tangu asubuhi hata wakati ulioamriwa; nao wakafa watu toka Dani mpaka Beer-sheba sabini elfu. 16. Lakini huyo malaika aliponyosha mkono wake kuelekea Yerusalemu ili auharibu, Bwana akaghairi katika mabaya, akamwambia huyo malaika mwenye kuwaharibu watu, Yatosha, sasa ulegeze mkono wako. Naye yule malaika wa Bwana alikuwako karibu na kiwanja cha kupuria cha Arauna, Myebusi.17. Daudi, alipomwoma malaika aliyewapiga watu, akanena na Bwana, akasema, Tazama, ni mimi niliyekosa, ni mimi niliyepotoka; lakini kondoo hawa, wamefanya nini? Mkono wako na uwe juu yangu, na juu ya nyumba ya baba yangu.”

Baada ya tukio hili la kutisha la watu kupigwa kwa tauni, ambalo linaonekana kumuuma moyo sana Daudi, aliamua kumuomba Mungu na ingawa haiku wazi alikuwa anaombea nini lakini bila shaka alijiombea yeye na wakazi wa mji wa Yerusalem na hasa alikuwa anaomba kwa mji wa Yerusalem na maombi yake yalikuwa na uhakika kuwa Mungu hawezi kuipiga Yerusalem, kutokana na uzoefu wake Daudi anaonyesha mambo ya msingi makuu mawili

1.       Kuutafuta uwepo wa Mungu siku zote za masiha yetu Mstari wa 1-9  Katika Mistari hii Daudi alikuwa anaonyesha umuhimu wa kuwa na uhusiano usioonekana na Mungu “AKETIYE MAHALI PA SIRI PAKE ALIYE JUU ATAKAA KATIKA UVULI WA MWENYEZI” Daudi anasisitiza kuwwa na uhusiano usioonekana kati yetu na Mungu, Ukristo wetu sio tu ule unaoonekana, tunapoomba maombi ya kanisani kwa pamoja ni vema lakini uhusiano wetu na Mungu ni zaidi ya maombi ya kanisani, uko uhusiano wa siri kukaa katika uwepo wake  Mathayo 6:2.-4, 7-8.16-18.  Daudi anaonyesha kuwa mtu atakayedumisha uhusiano wa siri na Mungu na kukaa naye katika namna ambayo wengine wanaweza wasijue, Na kumtegemea Mungu, Mungu atakufanyia haya  Zaburi 91:3-9
·         Atakuokoa na mtego wa Mwindaji
·         Mungu atakufunika kwa mbawa zake  na utapata nkimbilio
·         Hutakuwa na hofu ya aina yoyote
·         Mapigo kama tauni na magonjwa ya kutisha  na vita hutaviogopa
·         Hata watu elfu na kumi elfu walianguka mapigo kwao hayatakukaribia wewe
·         Macho yako yataona mwisho wa wabaya

2.       Mabaya hayatakupata wewe.

Ni muhimu kufahamu kuwa Mabaya yanayozungumzwa hapa kama Pestilence (Magonjwa yasio na tiba), au plague (Mapigo ya hukumu) kama biblia nyingi za kiingereza zilivyoandikwa, Biblia ya kiebrania inatumia neno “NEGA ambalo maana yake ni KURUDIWA, au KUADHIBIWA au KUPUNGUKIWA NA NEEMA YA MUNGU, neno hili lina maana kuwa Mungu hatazuia majaribu yasitupate lakini, lakini Mungu hatatuadhibu, au anapotuadhibu hataacha tuangamiie katika mkono wake, atatutisha lakini hataacha tauni disaster zikaribie Hema yako, yaani amakazi yako hayatapigwa Daudi alikuwa anajua kuwa Mungu anaweza kupiga miji Mingine lakini ni vigumu kuruhusu Yerusalem kupigwa , haitakaribiwa ni makazi yake matakatifu, ukifanya masikani na Mungu, Mungu akifanya makazi kwako hakuna mabaya yatakayokupata, Mungu atatuma malaika zake wakulinde, Yeye ana Rehema nyingi hata anapotuadhi,

Mungu hatatuadhibu
Mungu hahatuondolea neema
Hatatupungukia
Hatoondoa rehema zake
Ikiwa tutaimarisha uhusiano wetu wa siri na yeye
Ikiwa tutautafuta uwepo wake, atatuhifadhi, hata wengine wakianguka ka maelfu yao sisi tutabaki salama
Ikiwa Mungu aliwaokoa watu wengi sana katia Biblia wasipatwe na mabaya kuna ushahidi wa
 kutosha kimaandiko kwamba Mungu hatakuacha upatwe na Mabaya 

Rev. Innocent Kamote

Mkuu wa Wajenzi mwenye hekima!

Jumatano, 26 Oktoba 2016

Kila amwaminiye Hatatahayarika!


Mstari wa msingi: 1Petro 2:6-8
 
6. Kwa kuwa imeandikwa katika maandiko Tazama, naweka katika Sayuni jiwe kuu la pembeni, teule, lenye heshima, Na kila amwaminiye hatatahayarika. 7. Basi, heshima hii ni kwenu ninyi mnaoamini. Bali kwao wasioamini, Jiwe walilolikataa waashi, Limekuwa jiwe kuu la pembeni.8. Tena, Jiwe la kujikwaza mguu, na mwamba wa kuangusha, Kwa maana hujikwaza kwa neno lile, wasiliamini, nao waliwekwa kusudi wapate hayo.”

 "Naye Kristo Yesu mwenyewe ni jiwe kuu la pembeni."

Tutajifunza somo hili kwa kuzingatia vipengele viwili muhimu vifuatavyo

·         Maana ya jiwe kuu la Pembeni
·         Kila amwaminiye Hatatahayarika

Utangulizi:

Leo katika Mistari hii kuna mambo ya msingi sana ya kujifunza ambayo tunayapata kutoka kwa Petro, kimsingi Petro mahali hapa alinukuu maandiko kwa kusudi la kuwatia moyo wote waliomuamini Yesu Kristo, na kulikubali neno lake, Petro anatuhakikishia kuwa hatutaaibika katika wakati huu wa sasa na hata wakati wa kuja kwake Bwana na wakati wa hukumu. Kila amwaminiye Hatatahayarika!

Jiwe kuu la Pembeni.

Nataka kwanza kuweka wazi maana ya Neno Jiwe kuu la Pembeni Yesu Kristo anaitwa jiwe kuu la Pembeni, katika taratibu za ujenzi za zamani jiwe hilo lilichongwa kwa umakini sana ili liwe limenyooka na lilitumika kutafuta unyoofu wa mawe au matofali mengine, jiwe hili kwa kawaida lilitumika kujengwa katika kona ya jingo na ndipo mawe au matofali mengine yangefuata, licha ya kuitwa jiwe kuu la Pembeni pia liliitwa Jiwe la Msingi jiwe hilo kwa mujibu wa masimulizi ya kale liliwekwa kwa vigelegele na shangwe na ndio ulikuwa msingi muhimu wa nyumba ulioshika jingo zima, Mara nyingi hasa jiwe hili la Msingi au la pembeni lilikuwa na Heshima zaidi lilipotumika kujenga Hekalu ambao kwa sasa unazungumzia kanisa au watu wa Mungu 

Waefeso 2:20-22 “20. Mmejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii, naye Kristo Yesu mwenyewe ni jiwe kuu la pembeni. 21. Katika yeye jengo lote linaungamanishwa vema na kukua hata liwe hekalu takatifu katika Bwana. 22. Katika yeye ninyi nanyi mnajengwa pamoja kuwa maskani ya Mungu katika Roho.”

Maandiko yanamtaja Yesu Kristo kuwa ndio jiwe kuu la Pembeni au jiwe la msingi, maandiko yanaonyesha kuwa wale wanaomuamini na kumtegemea watakuwa na heshima kuu lakini wasiomuamini na wanaomkataa watakumbwa na mwakwazo ya ajabu sana katika maisha yao, wataainbika katika ulimwengu huu na ule ujao

Biblia inapomtaja Yesu kama Jiwe katika sayuni inatabiri pia kuweko kwa watu watakaomkataa 

Zaburi 118: 22  Jiwe walilolikataa waashi Limekuwa jiwe kuu la pembeni.” Waashi wanaotajwa hapo ni wajenzi, Mafundi ujenzi Mason hili ni kundi la Makuhani wakuu, wazee na waandishi (waalimu wa torati) hawa ndio walikuwa na nafasi ya kwanza kulijenga Hekalu na kanisa kuanzia na jamii ya Wayahudi, lakini kupitia mafundisho yao hawakuwaelekeza watu kwa Yesu na walipinga kabisa mfumo mpya na msingi mpya wa Ujenzi wa Kanisa ambalo ni Yesu, Yesu kristo ni jiwe la kweli la Msingi wote wanaomkataa wataaibika, itakuwa bahati mbaya sana kwao kwani ni kama wameumbwa wapatwe na mabaya, Makunani wazee na waandishi ambao walitarajiwa kuwajenga watu na kuwaunga na Kristo na wamekataa itakuwa ni kama wale waangukao juu ya jiwe hilo ama wale ambao jiwe litawaangukia Mapema Mzee Simon alitambua unabii huu wa Isaya na Zaburi kuwa Yesu ndio jiwe lile na aliwaelekeza watu kwa kutoa habari zake

 Luka 2:34  Simeoni akawabariki, akamwambia Mariamu mama yake, Tazama, huyu amewekwa kwa kuanguka na kuinuka wengi walio katika Israeli, na kuwa ishara itakayonenewa.”

Simeon alikuwa ameelewa kuwa Yesu angekataliwa Israel nzima sawa na unabii wa Isaya na wenyeji wa Yerusalem wangemkataa masihi na kujiletea hukumu kubwa sana

Isaya 8:14-15 “14. Naye atakuwa ni mahali patakatifu; bali ni jiwe la kujikwaza na mwamba wa kujikwaa kwa nyumba za Israeli zote mbili, na mtego na tanzi kwa wenyeji wa Yerusalemu. 15. Na wengi watajikwaa juu yake, na kuanguka na kuvunjika, na kunaswa na kukamatwa.”

Mungu ampe neema kila mmoja wetu kutokuwa miongoni mwa wajenzi, waashi waliomkataa Yesu au watakao mkataa Yesu na kujiletea hukumu kubwa nay a aibu

Kila amwaminiye Hatatahayarika!

1Petro 2:6 “Kwa kuwa imeandikwa katika maandiko Tazama, naweka katika Sayuni jiwe kuu la pembeni, teule, lenye heshima, Na kila amwaminiye hatatahayarika.”

ni muhimu kufahamu kuwa Petro anaponukuu neno Kila amwaminiye hatatahayarika!, Neno hilo limetokana na na unabii wa Isaya katika kitabu cha nabii Isaya 28:16 Mstari huo unasomeka 

“16. kwa ajili ya hayo Bwana, MUNGU, asema hivi, Tazama, naweka jiwe katika Sayuni, liwe msingi, jiwe lililojaribiwa, jiwe la pembeni lenye thamani, msingi ulio imara; yeye aaminiye hatafanya haraka.”

Kuna lugha mbili hapo zinatumika  

1.       Na kila amwaminiye hatatahayarika - Petro
2.       yeye aaminiye hatafanya haraka – Isaya

Biblia zote zimetumia neno katika Isaya “He who believe shall not make HASTE” Neno la asili la kiebrania HASTE ni “NADAD” ambalo maana yake ni kutoupigwa vitani, kutokuchanganyikiwa, kutokimbia mbele ya adui zako, kutowapa kisogo adui zako, kutokuwaogopa, kutokuwa mkimbizi, kutokufutiliwa mbali, kutokuhukumiwa na kutokuaibika ndio kutokutahayarika

Petro anamthibitishia kila amwaminiye Yesu ambaye ni jiwe kuu la Pembeni hatakatiliwa mbali, hatapata aibu, hatakimbia vitani, atahishimika, kuna ushindi mkubwa kwa kila aliyemwamini na kumtegemea Yesu, kila mtu na amfanye Yesu kuwa tumaini lake aweze kuyafaidi mema ya nchi.

Na Rev. Innocent Kamote

Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima

Jumanne, 25 Oktoba 2016

Kuuona wema wa Bwana katika nchi ya walio hai!


 
Adniko la Msingi: Zaburi 27:13. “Naamini ya kuwa nitauona wema wa BWANA Katika nchi ya walio hai


Utangulizi:

Zaburi ya 27 ni wazi kabisa kuwa ni zaburi ya Daudi, Zaburi hii ina mambo mengi sana ya kutafakari, Muda hauwezi kutosha kutafakari mambo yote, lakini leo nataka tutafakari tumaini kuu la ajabu alilokuwa nalo Daudi, kuhusu ndoto yake na ahadi za Mungu kwake, Haikuwa wazi kabisa kuwa Daudi hapa alikuwa anapigana vita ya aina gani, au bwana alikuwa amempa ushindi wa namna gani ama bado adui walikuwa wakimtishia na ulifikia wakati akaogopa  lakini bado alisalia na tumaini moja tu kwamba yeye anaamini kuwa atauona wema wa Bwana katika nchi ya walio hai! Ni kitu gani kinampa Daudi moyo wa imani hii

1.       Mstari  1-3 Alikuwa na ujuzi kuwa Bwana ni Nuru yake. Kwamba hakuna giza mbele kama unamtumainia Mungu, hofu yote inaondoka na unaweza kuiona future ( kuwa na Maisha mazuri na ya furaha) hata kama kuna kila aina ya hila, wazushi, waongo, watenda mabaya, watesi, adui, majeshi ya maadui, hivi vyote haviwezi kumtisha Daudi kwa sababu Bwana ni Nuru yake, mtu asiye na Mungu yumo gizani, ataishi maisha ya hofu kuu sana kwa sababu.

·         Watenda mabaya, wenye dhambi, waovu, wicked or evil doer
·         Watesi, waonezi, wasengenyaji, wanyanyasaji
·         Adui, foes, enemies, wapinzani, wasiotaka ufanikiwe
·         Jeshi, wanaopigana nao kimwili na kiroho, kisaikolojia, kiakili na vyovyote vile

Daudi alisema hawaogopi hao kabisa kwa sababu Bwana ni ngome ya uzima wake, Huu ulikuwa ni uthibitisho ulio dhahiri kuwa Daudi alidumisha uhusiano wake na Mungu, mtu yeyote yule atakayedumisha uhusiano wake na Mungu hawezi kutembea gizani, hawawezi kupoteza tumaini hata kama wataogopa watajitia moyo, na Mungu kwa hakika atawapigania na kuwalinda hakuna adui anaweza kufanikiwa kwako kama ilivyokuwa kwa Daudi ndivyo itakavyokuwa kwa kila anayemtanguliza Mungu mbele

2.       Mstari 4-5 Daudi anaeleza sababu kubwa ya kumtegemea Mungu ni kwamba pia akipewa uhai na kulindwa na Mungu atautumia uhai huo kukaa nyumbani mwa Bwana, ana kiu na shauku ya kutaka kuendelea kumuabudu Mungu, ni kama anaweka Nadhiri kwa Mungu mradi Bwana atanisitiri siku ya Mabaya na kuniinua, basi katika maisha yangu nitamuabudu, nitamtafakari, hekaluni mwake nitamuimbia, Daudi aliongeza aina nyingine ya Mapito na maombi aliyotaka mungu amtendee lakini kubwa zaidi anahitimisha kwa imani kuwa

3.       Anaamini kuwa atauona wema wa Bwana katika nchi ya walio hai, katika eneo hili Daudi alimuomba Mungu Mstari 12, asimtie katika nia ya adui zake, nia ya adui zake ni kumuangusha ni kuona kuwa hafanikiwi, ni kutoa ushahidi wa uongo na maneno ya Jeuri sana, Lakini Daudi anaamini atauona wema wa Bwana katika inchi ya walio hai

Mstari 13 jambo gani kubwa tunajifunza, hapa Daudi alielewa wazi kuwa kuna maisha baada ya kufa, alijua kuna kuishi milele, alijua kuna kwenda Mbinguni, lakini hakufurahia kuishi kwa shida Duniani, hapa alimuamini Mungu kuwa hatamuacha afe bila kumuonyesha mema katika nchi ya walio hai yaani hapa Duniani,

Kuingia mbinguni sawa kupo, kula vizuri mbinguni sawa kupo, magari ya farasi mbinguni sawa yapo, maisha ya matanuzi huko mbinguni sawa yapo lakini Daudi aliomba auone wema wa Mungu hapa Duniani kwenye nchi ya walio hai, kuna nchi ya wafu sawa, lakini kabla ya kwenda huko je nisionje mema ? kuna kufaulu kule mbinguni sawa, lakini ndo nifeli na Duniani, kuna majumba mbiguni sawa lakini ndo niishi katika kijinyumba cha nyasi Duniani? Kuna magari ya farasi za moto mbinguni sawa lakini je hapa duniani nisiendeshe hata toyo?, kuna hali ya hewa nzuri Mbinguni sawa lakini ndio nisipigwe hata na kiyoyozi duniani Daudi alimuomba Mungu kwamba ni lazima ufikie wakati vita vimalizike, mapambano yaishe, awe na wakati wa starehe, afanye kazi ya kuabudu

ndugu ulivyopambana duniani inatosha sasa mwambie Mungu akufurahishe akuonyeshe wema wake sasa, lazima ufikie ndoto zako na kuepushwa na kila aina ya mabaya ya dunia hii na Mungu atakupa kustarehe Hatimaye daudi alistarehe

2Samuel 7:1-2 “1. Ikawa, mfalme alipokuwa akikaa katika nyumba yake, hapo Bwana alipomstarehesha, asiudhiwe na adui zake waliomzunguka pande zote, 2. mfalme akamwambia Nathani, nabii, Angalia sasa, mimi ninakaa katika nyumba ya mierezi, bali sanduku la Mungu linakaa ndani ya mapazia.

Uko wakati wa Mapambano lakini pia uko wakati wa kustarehe Mungu na akufanikishe katika vita vyako na pia akujaalie wakati wa Kustarehe kama ilivyokuwa kwa Daudi


Naamini ya kuwa nitauona wema wa BWANA Katika nchi ya walio hai
Rev. Innocent Kamote
Mkuu wa wajenzi mwenye Hekima!