Jumapili, 15 Aprili 2018

Livunjeni hekalu hili, nami katika siku tatu nitalisimamisha!

Yohana 2:19  Yesu akajibu, akawaambia, Livunjeni hekalu hili, nami katika siku tatu nitalisimamisha." 

John 2:19. “Destroy this temple . and I will raise it again in three days”

 
 Utangulizi.

Ni muhimu kufahamu kuwa moja ya matamko ya Yesu Kristo yaliyowahi kulete utata, mojawapo ni tamko hili “Livunjeni Hekalu hili nami katika siku tatu nitalisimamisha”, Tamko hili liliweza kutumiwa na maadui wa Yesu Kristo kama moja ya ushahidi mkubwa wa kumshitaki Yesu wakati wa kuhukumiwa kwake Marko 14:58Sisi tulimsikia akisema, Mimi nitalivunja hekalu hili lililofanyika kwa mikono, na katika siku tatu nitajenga jingine lisilofanyika kwa mikono.” Na Mathayo 26:59-61Basi wakuu wa makuhani na baraza yote wakatafuta ushuhuda wa uongo juu ya Yesu, wapate kumwua; wasiuone wangawa walitokea mashahidi wa uongo wengi. Hata baadaye wawili wakatokea, wakasema, Huyu alisema, Naweza kulivunja hekalu la Mungu, na kulijenga kwa siku tatu.” Unaweza kuona jinsi ambavyo matamshi haya yalivyoweza kutafasiriwa kwa utata na wale waliotafuta kumhukumu Yesu Kristo, usemi huu unaweza kubaki kuwa tata hata kwa jamii yetu leo kama hatutaweza kumsikiliza Mwalimu mkuu Roho Mtakatifu ili kwamba atusaidie kuyaelewa maandiko haya na kupata maana muhimu zilizokusudiwa, Ni kwa makusudi hayo basi leo tunachukua muda kujifunza kuhusu usemi huu wa Yesu “LIVUNJENI HEKALU HILI, NAMI KATIKA SIKU TATU NITALISIMAMISHA” usemi huu wenye nguvu Baba na autumie kumjenga kila mmoja wetu katika jina la Yesu Kristo amen. Tutajifunza somo hili kwa kuzingatia vipengele  viwili vifuatavyo:-

·         Maana ya Hekalu.
·         Livunjeni Hekalu hili nami katika siku tatu nitalisimamisha!

Maana ya Hekalu.

Ni muhimu kufahamu kuwa Jina Hekalu limetokana na jina la kiingereza cha zamani “HEKAHAL” ambalo maana yake ni “main building” au “Hall”, ambalo pia lilitafasiriwea kama neno “Temple” kwa kiingereza cha zamani, Katika lugha ya kiebrania neno Hekalu linatumika kama “BEIT YHWH” yaani nyumba ya Mungu au “BEIT HA ELOHIM” yaani nyumba ya Mungu, na neno nyumba yangu ni “BEIT” au BEITEKHA

Kwa kawaida  kwa mara ya kwanza neno hekalu lilitumika kumaanisha nyumba ya Mungu ambayo ilikuwa ni hema ya kukutania iliyokuwako Shilo  1Samuel 1:9Ndipo Hana akainuka, walipokwisha kula na kunywa huko Shilo. Naye Eli, kuhani, alikuwa akiketi kitini pake penye mwimo wa HEKALU la Bwana.”

Katika agano Jipya neno hekalu limekuwa na maana pana  zaidi na zenye tafasiri kadhaa kadhaa:-

1.       Hekalu linamaanisha mwili wa Yesu Kristo Yohana 2:19, 2:21
2.       Hekalu pia humaanisha mtu aliyemwamini Yesu Kristo 1Wakoritho 3:16-17
3.       Hekalu pia humaanisha Kanisa yaani watu waliomwamini Yesu Kristo Waefeso 2:21
4.       Lakini mbinguni pia kunaitwa hekalu Ufunuo 7:5
5.       Lakini yako pia majengo ya miungu mingine ambayo pia huitwa hekalu hapa duniani mfano ni lile hekalu na mungu mke Diana au Artremi Matendo 19:27.

Ni muhimu kufahamu hata hivyo kibiblia na kwa mujibu wa Imani ya kiyahudi na Kikristo kwa ujumla neno hekalu lilitumika zaidi kumaanisha nyumba ya Mungu iliyokuwako katika mlima Sayuni kwaajili ya kumuabudu Mungu, hili lilitwa Hekalu 1Falme 6:17, Nyumba ya Mungu 2Wafalme 11:10, Hekalu takatifu Zaburi 79:1, Nyumba ya Bwana 2Nyakati 23:5, 12, Nyumba ya Mungu wa Yakobo Isaya 2:3 Nyumba ya utukufu  Isaya 60:7, Nyumba ya sala Isaya 56:7, Mathayo 21:13 Nyumba ya sadaka 2Nyakati 7:12 Patakatifu 2Nyakati 36:17 Mlima wa nyumba ya Mungu Isaya 2:2 Patakatifu nyumba ya uzuri Isaya 64:11 Mlima mtakatifu Isaya 27:13 Mahali kwa Bwana 1Nyakati 29:1 Hema la ushuhuda 2Nyakati 24:6 Sayuni Zaburi 74:2, 84:7 na Yesu aliita Nyumba ya baba yangu Yohana 2:16.

Livunjeni Hekalu hili nami katika siku tatu nitalisimamisha!

Yohana 2:19-21.Yesu akajibu, akawaambia, Livunjeni hekalu hili, nami katika siku tatu nitalisimamisha. Basi Wayahudi wakasema, Hekalu hili lilijengwa katika muda wa miaka arobaini na sita, nawe utalisimamisha katika siku tatu? Lakini yeye alinena habari za hekalu la mwili wake.”

Kimsingi wakati Yesu alipokuwa akiyatamka maneno haya Wayahudi walifikiri kuwa Yesu alikuwa akizungumza juu ya Hekalu ambalo lilikuwa limekarabatiwa na Herode mnamo karne ya 19 Kabla ya Yesu, Hekalu hilo la kifahari ambalo wayahudi walikuwa wanajivunia lilikuwa limechukua muda wa miaka 46 hivi,  Yesu hakujisumbua kutoa ufafanuzi wa maana ya meneo haya, Wanafunzi wake tu ndio walioelewa kuwa Yesu alikuwa akizungumza juu ya mwili wake na juu ya uhai wake kwamba yeye ana uwezo wa kuutoa uhai wake na kuutwaa tena Yohana 10:17-18Ndiposa Baba anipenda, kwa sababu nautoa uhai wangu ili niutwae tena. Hakuna mtu aniondoleaye, bali mimi nautoa mwenyewe. Nami ninao uweza wa kuutoa, ninao na uweza wa kuutwaa tena. Agizo hilo nalilipokea kwa Baba yangu. Wayahudi walikuwa hawako tayari kumpokea Yesu na walikuwa tayari wamekwisha kupanga mpango wa kumwangamiza Yesu, Kwa hiyo Yesu alikuwa akizungumza habari ya mpango wao na kifo chake, hivyo usemi huu waoa hawakuuelewa lakini wanafunzi waliuelewa baadaye kuwa Yesu alikuwa anazungumza habari ya kusulubiwa kwake kufa na kufufuka, kwa hiyo Yesu alipofufuka siku ya tatu wanafunzi walishangaa neno la Mungu na unabii wa Yesu Kristo mwenyewe , hivyo walitambua kuwa kufa kwa Yesu Kristo halikuwa tukio la bahati mbaya bali ulikuwa ni mpango wa Mungu kwaajili ya uzima wa milele.

Usemi huu ulikuwa usemi wenye kuonyesha nguvu kubwa na uweza wa Yesu Kristo, kwamba yeye ni mweny nguvu na anazo funguo za mauti na za kuzimu yaani ana mamlaka yote hata leo Yesu bado analiangalia kanisa lake na hekalu lake ambao ni sisi wanadamu, kutokana na kazi za shetani katika maisha ya mwanadamu na kazi zake ulimwenguni pamoja na anguko la Mwanadamu,  kumekuweko na hali za kutokumcha Mungu, kuipenda dunia tamaa na kila aina ya dhambi  na vimekuwa ni matokeo makubwa ya kumomonyoka kwa uadilifu wa mwanadamu katika maisha yake  na kumekuwa ni mwanzo wa kaburi, Mwanadamu kwa asili ndani yake ameumbwa na Mungu kuwa Hekalu, Mioyo yetu iliumbwa na Mungu kwa kusudi la kuifanya kuwa nyumba ya ibada ya kwa Roho Mtakatifu, mioyo yetu imekusudiwa kuwa nyumba ya Mungu aliye hai, lakini kutokana na ubinafsi, dhambi na tamaa za dunia watu   na ibilisi wameharibu maisha yao matakatifu na kupungukiwa na utukufu wa Mungu, wameharibu nyumba ya Mungu kwa nyundo na mawe na mashoka wameweka chukizo la uharibifu mahali patakatifu, wamelinajisi hekalu, wameharibu dhamira zao na hazina hisia ya hofu ya Mungu kabisa, kila wanachokiwaza wanadamu, walichojaza mioyoni mwao, katika maamuzi yao na mapenzi yao uwepo wa Mungu umepewa nafasi ndogo sana au umenyimwa kabisa kuweko katika nafasi ya Moyo wa Binadamu

Ulimwengu umekuwa wa tofauti sana wanadamu wameharibika badala ya kuchagua mema wamechagua mabaya, maovu yanaonekana kuwa ni sifa na wema unaonekana kuwa ni ujinga Yesu alilijua hilo mapema inasikitisha kuwa watu walimchagua Baraba aliyekuwa muhaini na kumsulubisha Yesu aliyekuwa akiponya Magonjwa yao na kutoa muda wake akiwafundisha njia za Mungu kwa usahihi zaidi, Yesu alijua kuwa ni kwa kupitia kulinda heshima zao na tamaa zao na ubinafsi wao viongozi wa dini wana makusudi ya kumuua na hivyo kuleta uharibifu wa Mwili wake kama Hekalu la Roho Mtakatifu na shetani ameaharibu mioyo ya wanadamu ili kuleta uharibifu ndani yao ziko roho za uharibifu zimetumwa kukuharibia kila walichikifanya wanadamu katika dhamiri zao na mioyo yao ni uharibifu wa hekalu la Mungu.

Yesu akijua uweza na mamlaka alio nao alizungumza juu yamauti yake lakini pia anazungumza juu ya mauti yako na kwa ujasiri najua kuwa anao uwezo wa kurejesha tena, kile ambacho shetani ameharibu katika maisha yako yeye ana uwezo wa kukarabati ndani na Muda mfupi kama utampa maisha, yeye atafukuza wafanya biashara miungu na mapepo yanayoharibu maisha yako na atayahuisha tena kwa nguvu alizonazo, siku tatu inamaanisha kwa kazi yake aliyoifanya , kwa kusulubiwa na kufa na kufufuka inamaanisha ukweli kuwa alikufa kwa dhambi zetu na amefufukwa kwaajili ya haki Yesu ni wazi kuwa kwa kazi aliyoifanya msalabani inauwezo wa kumjenga na kumrejesha upya mwanadamu wa aina yoyotena kabila lolote na aliyeharibika kwa kiwangochopchote na mtu huyo akawa makazi ya roho mtakatifu wa Mungu, haijalishi sasa una miaka mingapi, haijalishi tatizo lako lina miaka mingapi Mungu anataka uamini kazi iliyofanyika msalabani kwamba ina nguvu za kipekee za kufanya kitu kipya katika maisha yako, Ndio maana Yesu Hakushughulika kuhesabu miaka ya hekalu kujengwa Yeye amesema livunje na ndani ya siku tatu atalisimamisha, Hekalu lililokuwa limejengwa kwa miaka 46 hata hivyo lilikuwa bado halijakamilika, Lakini kazi aliyoifanya yesu ni kamilifu kama ulimkubali yeye atalijenga hekalu tena atakamilisha mapungufu yako na atalijenga Hekalu lako bila nyundo kusikika 
 
1Wafalme 6:7 “Na nyumba ilipokuwa ikijengwa, ikajengwa kwa mawe yaliokwisha kuchongwa chimboni; wala nyundo, wala shoka, wala chombo cha chuma cho chote, sauti yake haikusikiwa ilipokuwa ikijengwa nyumba.”

Ni Yesu Kristo pekee ndiye mwenye uwezo wa kulijenga Hekalu lake bila kelele, wakati mwingine tumepiga nyundo, tumetumia shoka na vyombo vya chuma katika kuwajenga wanadamu Lakini Yesu anaweza kumjenga awaye yote bila Kelele, Leo atakujenga wewe pia bila kelele za wanadamu.

Na mkuu wa wajenzi mwenye Hekima 

Rev. Innocent Kamote.